Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ____________ MAJADILIANO YA BUNGE ______________ MKUTANO WA NANE Kikao cha Ishirini na Moja – Tarehe 11 Julai, 2007 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Samuel J. Sitta) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA MIUNDOMBINU (MHE. DR. MILTON M. MAHANGA): Hotuba ya Bajeti ya Waziri wa Miundombinu kwa Mwaka wa Fedha 2007/2008 MHE. MOHAMED H. MISSANGA - MWENYEKITI WA KAMATI YA MIUNDOMBINU: Taarifa ya Kamati ya Miundombinu kuhusu Utekelezaji wa Wizara ya Miundombinu kwa Mwaka wa Fedha Uliopita Pamoja na Maoni ya Kamati kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka 2007/2008 MHE. BAKARI SHAMIS FAKI - MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI KWA WIZARA YA MIUNDOMBINU: Maoni ya Kambi ya Upinzani Kuhusu Utekelezaji wa Wizara ya Miundombinu kwa Mwaka wa Fedha Uliopita, Pamoja na Maoni ya Upinzani Kuhusu Makadirio ya Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka 2007/2008. MASWALI NA MAJIBU Na. 185 Zahanati ya Nyamilama Kuwa Kituo cha Afya 1 MHE. BUJIKU P. SAKILA aliuliza:- Kwa kuwa, Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2005 pamoja na mambo mengine mengi inalenga katika kuboresha huduma ya afya ili kupunguza vifo vya wananchi wa rika na jinsia zote kwa kuwasogezea huduma hiyo ikiwa bora karibu na makazi yao; na kwa kuwa, Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba imekusudia kuipandisha hadhi Zahanati ya Nyamilama kuwa, Kituo cha Afya ili wananchi wanaokizunguka hususan wakazi wa Tarafa ya Nyamilama waweze kupata huduma hiyo kwa karibu na kwa ubora zaidi:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kuiunga mkono Halmashauri hiyo kufikia azma yake hiyo kwa ufanisi na mapema zaidi? (b) Kwa kuifanya zahanati hiyo kuwa Kituo cha Afya. Je, Serikali itakuwa na mpango wa kuviwezesha vituo vya Mwamshimba na Nyamilama viweze kutoa huduma za upasuaji mdogo na kuongeza maji na damu kwa kuwa ni mahitaji ya watu wengi wanaovizunguka vituo hivyo? (c) Kwa kuwa, uwezo wa Halmashauri ya Kwimba kukamilisha zoezi la kuinua hadhi ya zahanati hiyo mapema ni mdogo iwapo msaada wa Serikali utachelewa? Je. Serikali haioni kuwa, itakuwa busara zaidi kutoa gari moja la wagonjwa wanaohitaji huduma ya haraka katika Hospitali ya Wilaya iliyoko Ngudu wakitokea katika vituo hivyo vya afya viwili? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Bujiku Phillip Sakila, Mbunge wa Kwimba, swali lake lenye sehemu a, b na c kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba, Serikali inalenga kuboresha huduma ya afya ili kupunguza vifo vya wananchi kwa kusogeza huduma bora karibu na makazi yao. Serikali itaunga mkono Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba katika mipango yake mbalimbali ya kuboresha huduma za afya. Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba imewahamasisha wananchi kujenga majengo ya ziada chini ya Mpango Maalum wa Kuboresha Afya ya Msingi, (MMAM) kwa kujenga kuta na kwamba Serikali itamalizia majengo hayo na kutoa dawa na watumishi. Uhamasishaji huo umefanyika mwezi Mei na Juni 2007. Aidha, Ofisi yangu kupitia mradi wa Ukarabati wa Vituo vya Afya na Zahanati uliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba shilingi 324,990,000/= kwa mwaka 2006/2007. Napenda kuishauri Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba ianze kwanza kuongeza majengo ya Zahanati ya Nyamilama ili Serikali ione uwezekano wa kusaidia. 2 Mheshimiwa Spika, Kituo cha Afya kinatakiwa kujengwa kwa kuzingatia vigezo vifuatavyo:- (a) Idadi ya watu watakaohudumiwa katika Kituo husika (catchment area) iwe kati ya watu 10,000 mpaka 50,000 (b) Wakazi wa eneo hilo waweze kupata huduma ndani ya kilomita 10 kutoka walipo hadi eneo la Kituo cha Afya (c) Kama kipo kikwazo cha Kijiografia kinachowafanya watu kupata huduma katika Kituo cha Afya kilicho karibu kwa sasa kama vile milima, mapori, mito isiyopitika na njia duni za usafiri (b) Mheshimiwa Spika, zahanati ya Nyamilama itakapopandishwa hadhi kuwa Kituo cha Afya, ikitoa huduma kamili zinazotolewa na Kituo cha Afya ikiwa ni pamoja na upasuaji mdogo. Huduma ya kuongeza damu katika Kituo cha Mwamashimba na Nyamilama inahitaji maandalizi makubwa. Hali ya fedha itakaporuhusu huduma hii inaweza kutolewa. Nawashauri wananchi kutumia huduma zilizopo katika Hospitali ya Wilaya ya Kwimba kwa sasa. (c) Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba ina Vituo vya Afya vitano (5) na ina gari moja la kubeba wagonjwa. Napenda kuishauri Halmashauri ya Wilaya ya Kwimba kuweka kwenye bajeti yake ya mwaka gharama za gari la kubebea wagonjwa. Serikali itaendelea kununua magari haya kwa awamu kulingana na uwezo wa kifedha. MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (TAMISEMI) nina swali la nyongeza. Kwa kuwa tatizo kubwa la vituo vya afya ni upungufu wa watumishi hasa Madaktari Wasaidizi kama alivyojibu Mheshimiwa Naibu Waziri. Kama tutakuwa na Madaktari Wasaidizi katika vituo vya afya nina hakika kwamba upasuaji mdogo utafanyika badala ya kutembea mwendo mrefu kwenda Hospitali za Wilaya. Je, hawa wataalamu wa afya wataongezwa lini katika vituo vya afya na zahanati ikiwemo Wilaya ya Mpwapwa? WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII: Mheshimiwa Spika, uhaba wa wafanyakazi na sio Ma-clinical officers peke yao ni mkubwa. Wafanyakazi tulionao katika vituo vyetu ni asilimia 32 tunaowahitaji. Kwa hiyo katika mpango mahsusi wa maendeleo ya afya ya msingi hili suala limefanyiwa mkakati na ningeomba Mheshimiwa Mbunge siku ya Jumanne tutatoa hotuba yetu ya bajeti haya masuala tutayaainisha vizuri zaidi. MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Katika jibu la msingi la Mheshimiwa Waziri amesema kwamba Wilaya ya Kwimba tumepatiwa zaidi 3 ya shilingi 300 milioni kwa ajili ya ukarabati wa zahanati na vituo vya afya. Ningependa kujua fedha hizo zimepelekwa lini kwa sababu mpaka leo najua fedha hizi hazijaenda ni lini fedha hizo zimepelekwa? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, fedha hizi za ukarabati wa vituo vya afya na zahanati zimepelekwa mwezi Juni, 2007 katika Wilaya 35 za Tanzania ikiwemo pamoja na Kwimba. Kinachongojewa sasa ni vituo vya afya gani viainishwe pamoja na zahanati gani ziainishwe ziletwe kwetu kwa ajili ya approval ili ukarabati huu uanze mara moja. Na. 186 Zahanati ya Bungu Kufanywa Kituo cha Afya MHE. PROF. IDRIS A. MTULIA( K.n.y. MHE. ABDUL J. MAROMBWA) aliuliza:- Kwa kuwa, Zahanati ya Bungu inawahudumia wagonjwa kati ya 150 na 250 kila siku; na kwa kuwa, Zahanati hiyo ipo katika barabara kuu iendayo Mikoa ya Kusini; na kwa kuwa, Kata hiyo ya Bungu ina wakazi zaidi ya 30,000:- (a) Je, Serikali haioni kuwa kuna haja ya kuifanya zahanati hiyo kuwa Kituo cha Afya? (b) Je, kama jambo hilo litakubaliwa, ujenzi wake utaanza lini? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdul Jabir Marombwa, Mbunge wa Kibiti, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, lengo la kupandisha hadhi ya Zahanati na kuwa Kituo cha Afya ni kuboresha zaidi huduma za afya kwa jamii katika eneo husika kulingana na Sera ya Afya ya Mwaka 1990 ambayo kwa sasa inapitiwa upya. Kama nilivyomaliza kujibu swali la 185 la Mheshimiwa Bujiku Sakila, Mbunge wa Kwimba, jambo la msingi ni kuzingatia vigezo vinavyotakiwa kuwa Kituo cha Afya. Vigezo hivyo kama nilivyosema ni pamoja na idadi ya watu, eneo husika (Catchment area) pamoja na sababu za Kijiografia. Mheshimiwa Spika, pamoja na vigezo tajwa hapo juu kupandishwa hadhi kwa zahanati kunategemea pia utayari wa wananchi wa eneo hilo kuchangia au kushiriki katika mkakati wa ujenzi wa kituo hicho. Kimsingi ili Zahanati iwe Kituo cha Afya ni 4 lazima iwe na jengo la wagonjwa wa nje kwa ajili ya huduma za kawaida, huduma kwa wajawazito na utawala. Pia ziwepo wodi mbili kwa ajili ya wanawake na wanaume, sehemu ya ufuaji, chumba cha maiti na tanuru la kuchomea taka. Kwa upande wa watumishi, Kituo cha Afya kinahitaji kuwa na watumishi wa kada mbalimbali wapatao 29. Mheshimiwa Spika, Zahanati ya Bungu inahudumia watu 29,869. Idadi hii ya watu inatosha kabisa kuanzishwa Kituo cha Afya kama taratibu za Msingi zinazopaswa kufuatwa zitazingatiwa. Kwa kuanzia kwenye vikao vya Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji pamoja na Mkoa. Mheshimiwa Spika, kulingana na sera ya kupeleka madaraka kwa wananchi, miradi yote ya maendeleo inapaswa kuanzishwa na walengwa wenyewe kupitia vikao halali vya maamuzi ya mipango ya maendeleo. Mkakati wa Serikali ni kuendelea kuwahamasisha wakazi wa Kata husika ili suala hili liweze kupewa kipaumbele. Naomba kumshauri Mheshimiwa Mbunge ashirikiane na wananchi katika eneo husika ili waweze kuwa na utayari katika kuchangia na kuhakikisha kuwa Zahanati hiyo inapandishwa hadhi na kuwa Kituo cha Afya kwa misingi na taratibu nilizozieleza hapo juu. MHE. PROF. IDRIS A. MTULIA: Mheshimiwa Spika, naomba kushukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Lakini ukiingia ndani ya hizi zahanati yako mambo mawili yamekuwa sasa ni ugonjwa mkubwa. La kwanza kuna upungufu mkubwa wa watumishi, la pili zahanati hizi mathalani Bungu yenyewe, Ikwiriri, Nyaminywili, Mkongo mpaka Mloka unaweza kwenda ukakosa hata panadol. Je, Serikali inawahakikishiaje wananchi wa Rufiji kwamba hizo dawa zitapatikana? WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII: Mheshimiwa Spika, ahsante. Suala la uhaba wa wafanyakazi nimelizungumza hivi punde kwamba si katika vituo vya afya au dispensary za Rufiji peke yake ni nchi nzima. Ndiyo maana tumeweka mkakati ambao tutauandikia na tutataka Waheshimiwa Wabunge watusaidie katika kutekeleza hilo. Kuhusu uhaba wa dawa ni kweli Bajeti haiwezi ikakidhi mahitaji, lakini mwaka hadi mwaka tunajaribu kuongeza kiasi cha dawa ambacho tunachopeleka katika vituo vyetu. Lakini ningependa pia sisi tusaidiane kwamba dawa zinaweza zikaisha mapema kuliko muda ambao tunatarajia kwa sababu ya matumizi mabaya. Kwa hiyo Kamati zetu za afya zikisimama kidete tunaweza tukapunguza suala hilo.
Details
-
File Typepdf
-
Upload Time-
-
Content LanguagesEnglish
-
Upload UserAnonymous/Not logged-in
-
File Pages131 Page
-
File Size-