NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA __________ MAJADILIANO YA BUNGE ___________ BUNGE LA KUMI NA MOJA MKUTANO WA KUMI NA TANO Kikao cha Ishirini na Moja – Tarehe 6 Mei, 2019 (Bunge lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Mwenyekiti (Mhe. Andrew J. Chenge) Alisoma Dua MWENYEKITI: Waheshimiwa tukae. Katibu. NDG. PAMELA PALLANGYO – KATIBU MEZANI: HATI ZA KUWASILISHA MEZANI Hati ifuatayo iliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Randama za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kwa mwaka wa fedha, 2018/2019. MWENYEKITI: Ahsante. Katibu. 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) NDG. PAMELA PALLANGYO – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU MWENYEKITI: Swali letu la kwanza leo linaulizwa na Mheshimiwa Ruth Mollel, Mbunge wa Viti Maalum na linaelekezwa Ofisi ya Rais, TAMISEMI. Na. 166 Athari za Mtambo wa Kuchoma Takataka za Hospitali na Dawa Zilizokwisha Muda – Mkuranga MHE. RUTH H. MOLLEL aliuliza:- Mtambo wa kuchoma takataka za hospitali na dawa zilizokwisha muda wake upo katika Kijiji cha Dundani Wilayani Mkuranga. Uchomaji unapofanyika moshi mzito huingia kwenye nyumba na maeneo ya wananchi wanaoishi karibu na mtambo huo na kuhatarisha afya zao:- Je, Serikali ina mkakati gani wa kunusuru afya na maisha ya wananchi wanaoishi karibu na mtambo huo? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE) alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Ruth Hiyob Mollel, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba upo mtambo wa kuchomea taka na dawa zilizokwisha muda wake uliojengwa na mwekezaji katika Kijiji cha Dundani, Wilaya ya Mkuranga. Hapo awali mtambo huo ulikuwa na kasoro za ujenzi ambapo Serikali ilimwagiza mwekezaji kuzirekebisha kwa ilani ya tarehe 18, Oktoba, 2017 yenye kumbu. Na. NEMC/HQ/EA/05/0702/VOL1/7 sambamba na 2 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) kusimamisha shughuli za mtambo mpaka kasoro zitakapokuwa zimerekebishwa. Mheshimiwa Mwenyekiti, marekebisho hayo yamefanyika na baada ya mamlaka zote, ikiwemo Serikali ya Kijiji cha Dundani kujiridhisha kwamba hakuna tena moshi unaoathiri mazingira, mtambo huo umeruhusiwa kuendelea na kazi na mpaka sasa hakuna taarifa yoyote iliyofika katika Ofisi ya Mkurugenzi Mtendaji, Wilaya ya Mkuranga kulalamikia shughuli za mtambo huo. MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Mollel. MHE. RUTH H. MOLLEL: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Waziri, pamoja na marekebisho ambayo yamefanyika, ni kwamba sasa ule moshi zamani ulikuwa unafika mbali, baada ya marekebisho ule moshi bado unatoka na bado unaathiri wananchi waliokuwa jirani, unasababisha watu kukohoa na harufu chafu kwa wananchi wanaozunguka lile eneo. Swali langu: Je, Serikali ilishafanya utafiti kwa sababu watu wanakohoa, tumejua ni madhara gani ya kiafya yanayosababishwa na moshi huo? Swali langu la pili; ni kwa nini sasa NEMC wasirudi tena kule Dundani na kuhakikisha kwamba ule moshi unatafutiwa namna ambayo itaudhibiti usiendelee kuchafua mazingira? MWENYEKITI: Ahsante. Majibu kwa maswali hayo Mheshimiwa Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Kandege. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. JOSEPHAT S. KANDEGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nikiri kwamba Mheshimiwa Ruth Mollel ni Diwani wa kata husika, kwa hiyo, yeye ni mdau katika eneo hilo. Kama ambavyo nimejibu katika jibu langu la msingi, kwamba mpaka sasa hivi hakuna taarifa ambayo imekuja Ofisi ya Mkurugenzi ikionesha kwamba kuna kasoro ambazo 3 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Serikali inatakiwa irekebishe, naomba Mheshimiwa Mbunge kwa kutumia vikao vyake alipeleke hili. Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kwa sababu sisi tunajali afya ya mwananchi kuliko jambo lingine lolote, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge, pamoja na swali lake la pili kwamba angetaka NEMC waende kwa mara ya pili kutazama; kwa sababu mtaji wetu kwa mwananchi ni kuhakikisha kwamba ana afya bora, basi naomba nimhakikishie kwamba Serikali kwa kupitia NEMC tutakwenda kuchunguza na tujiridhishe pasi na mashaka kwamba hakuna madhara ambayo yanatokana na kichomea taka hiki. MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Lubeleje. MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi ili niweze kuuliza swali moja la nyongeza. Kwa kuwa madawa yaliyokwisha muda wake (expired drugs) ni hatari sana katika maisha ya binadamu; na kwa kuwa baadhi ya maduka hayakaguliwi vizuri kuhakikisha kwamba madawa yaliyokwisha muda hayapo. Je, Mheshimiwa Waziri anasemaje kuhusu ukaguzi wa maduka yote ambayo yana madawa hayo yaliyokwisha muda wake? MWENYEKITI: Ahsante. Majibu kwa maswali hayo Mheshimiwa Naibu Waziri wa Afya, Mheshimiwa Ndugulile. NAIBU WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa taratibu zetu za afya, dawa zilizoisha muda au matumizi hazipaswi kutumika kwa matumizi ya binadamu. Mahospitali pamoja na wauzaji wa maduka binafsi wanatakiwa wazitenge tofauti na dawa ambazo zinaendelea kutumika ndani ya vituo vyetu vya kutolea huduma za afya lakini vilevile katika matumizi ya dawa za kuuzwa. 4 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna utaratibu maalum ambao umewekwa ambapo dawa na vifaa vya hospitali havichomwi tu kama takataka nyingine, vina utaratibu wake na utaratibu huu upo. Nitoe rai tu kuhakikisha kwamba mamlaka ambazo zinasimamia ikiwa ni pamoja na Mamlaka ya TFDA na Baraza la Famasia, basi wapite kuhakikisha kwamba wanatoa elimu hiyo na kuweka utaratibu mzuri wa uteketezaji wa hizi dawa ili zisije zikaingia katika mikono isiyo salama. MWENYEKITI: Ahsante. Waheshimiwa tunaendelea. Swali linalofuta linaulizwa na Mheshimiwa Vedastus Mathayo Manyinyi, Mbunge wa Musoma Mjini na linaelekezwa kwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Utumishi na Utawala Bora) Na. 167 Zoezi la Kuwaondoa Watumishi Wenye Vyeti Fake MHE. VEDASTUS M. MANYINYI aliuliza:- Serikali katika kuhakikisha inapata watumishi bora na wenye sifa iliamua kuwaondoa watumishi wasio na sifa pamoja na wenye vyeti feki, lakini zoezi hilo lilikumbwa na changamoto mbalimbali ambapo Afisa Utumishi aliwaondoa watumishi kwenye payroll bila sababu maalum na walipofuatilia Wizarani walirudishwa kazini:- (a) Je, kwa nini Serikali isiunde timu maalum ili ipite kila Halmashauri kupitia taarifa juu ya zoezi hili ili haki itendeke hasa kwa wale ambao hawana uwezo wa kwenda Wizarani? (b) Wapo watumishi ambao baada ya kuajiriwa kwa kutumia vyeti feki walijiendeleza kielimu zaidi ya Darasa la Saba na wameondolewa kwa kosa la udanganyifu wa vyeti: Je, Serikali haioni kuwa hao ni bora kuliko wale ambao hawakujiendeleza? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, MENEJIMENTI YA UTUMISHI WA UMMA NA UTAWALA BORA alijibu:- 5 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Vedastus Mathayo Manyinyi, Mbunge wa Musoma Mjini, lenye sehemu (a) na (b), kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kushirikiana na waajiri na Baraza la Mitihani la Taifa, Serikali iliendesha zoezi maalum la kuhakiki vyeti vya ufaulu mtihani wa Kidato cha Nne, Kidato cha Sita na Ualimu. Kupitia zoezi hilo, watumishi 15,189 walibainika kuwa na vyeti vya kugushi na kuondolewa kwenye orodha ya malipo ya mshahara (payroll). Hata hivyo, baada ya kupokea malalamiko kutoka kwa watumishi na vyanzo vingine kuhusu watumishi kuondolewa kimakosa au kwa uonevu katika orodha ya malipo ya mishahara, Serikali imekuwa ikifanya ufuatiliaji wa karibu ikiwa ni pamoja na kuunda timu za ufuatiliaji wa utekelezaji wa zoezi hili. Jumla ya watumishi 4,160 waliobainika kuondolewa kimakosa au kwa uonevu wamerejeshwa kazini. Kati ya watumishi waliorejeshwa kazini 3,057 ni Watendaji wa Vijiji/Mtaa na Kata. (b) Mheshimiwa Mwenyekiti, watumishi wanaojiendeleza zaidi ya Darasa la Saba wanafanya vizuri na Serikali inahimiza watumishi kujiendeleza kielimu. Hata hivyo, kwa mujibu wa Kanuni ile ya D.12 ya Kanuni za Kudumu katika Utumishi wa Umma za mwaka 2009, ni makosa kwa mtumishi kujipatia ajira kwa njia ya udanganyifu. Hivyo Serikali ilielekeza waajiri kuwaondoa kwenye orodha ya malipo ya mishahara Watumishi wa Umma wote walioajiriwa kabla ya tarehe 20, Mei, 2004 ambao katika kumbukumbu zao rasmi za kiutumishi walijaza taarifa za udanganyifu kwamba walifaulu mitihani ya Kidato cha Nne, lakini hawakuthibitisha taarifa zao kwa kuwasilisha vielelezo vya sifa hizo kama vile taarifa binafsi (personal records). Hivyo, pamoja na watumishi hao kujiendeleza kielimu, uamuzi wao wa kutoa taarifa za udanganyifu unawaondolea 6 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) sifa ya uaminifu na uadilifu kwa Serikali na hivyo wanakosa sifa za kuendelea kuwa Watumishi wa Umma. Ahsante. MWENYEKITI: Mheshimiwa Manyinyi. MHE. VEDASTUS M. MANYINYI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi ili niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Naibu Waziri, mkwe wangu, kwa majibu mazuri aliyoweza kunipatia, lakini (a) kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kati ya watumishi 15,000 walioondolewa waligundua kwamba watumishi 4,160 waliondolewa kimakosa. Hawa ni wale waliopata nafasi ya kuja Dodoma, Utumishi na kwenda Dar es Salaam kwenye Tume. Wale ambao hawakuwa na uwezo, tafsiri yake ni kwamba wamebaki huko. (Makofi) Sasa swali; ni lini sasa Serikali itaunda tume ambayo angalau itakwenda kila Halmashauri au Mkoani
Details
-
File Typepdf
-
Upload Time-
-
Content LanguagesEnglish
-
Upload UserAnonymous/Not logged-in
-
File Pages169 Page
-
File Size-