
Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru! Harith Ghassany [email protected] SOMA HAPA KWANZA Usambazaji wa kitabu hichi kwa mfumo wa Free Electronic Downloading unafanyika chini ya mkataba wa Creative Commons Attribution-NonCommercial-ShareAlike 3.0 ambao uko chini ya Sharia za nchi ya Marekani. Kwa mujibu wa Mkataba na Sharia hii, mtu anayekichukuwa kitabu hichi kupitia mfumo huu ana uhuru pia wa kukigawa, kukirudufu na kukisambaza chini ya masharti yafuatayo: • Kulitaja jina la mwandishi wa kitabu kwa njia isiyohalalisha matumizi binafsi ya kitabu • Kutokitumia kwa makusudi ya kibiashara wakati kinauzwa katika mfumo wa kitabu • Kutokubadilisha, kugeuza, au kuongeza chochote kwenye kitabu hichi Kwa maelezo zaidi, tafadhali tembelea: http://creativecommons.org/licenses/ by-nc-nd/3.0/us/ Kitabu hichi kinatolewa bure katika mfumo huu ili msomaji anufaike na baadaye naye akipendekeze kwa mwenzake ili hatimaye ujumbe wa kusimamisha amani uliomo kitabuni uwafikie walio wengi. Hata hivyo, mwandishi wa kitabu hiki anafahamu kwamba raha hasa ya kitabu ni kuwamo mikononi mwa msomaji, maana kitabu ni miongoni mwa vitu adhimu na vikongwe kabisa katika urathi wa mwanaadamu. Kwa hivyo, licha ya kutolewa fursa hii ya mfumo wa kukisoma bure kitabu hichi kupitia kwenye mtandao, ni matarajio ya mwandishi kuwa wako watakaopendelea wawe nacho mikononi na kukisoma kwa nafasi zao. Kwa vile walengwa wa mfumo huu wa Free Electronic Downloading ni Wazanzibari na Watanganyika wa kawaida, basi ipo haja kwa wale wenye uwezo, wakiwa ndani ama nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kutoa mchango wa kuvinunua vitabu ama kupitia mtandao wa kitabu, http://kwaherikwaheri.com, au moja kwa moja kutoka http://lulu.com na kuwafikishia walimu na wanafunzi walioko kwenye skuli na vyuo vya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Skuli, vyuo, maktaba, taasisi na watu binafsi wanaweza kumuandikia moja kwa moja mwandishi kupitia mtandao wa kitabu http://kwaherikwaheri.com ikiwa watahitaji kupata msaada wa wafadhili watakaojitokeza kusaidia. Wafadhili ambao hawatopenda majina yao kujulikana, wamuarifu mwandishi. Majina yao yatahifadhiwa na mwandishi anatanguliza shukrani za dhati kwa ukarimu wao. Mwandishi pia anatanguliza ombi na shukrani maalum kwa watakaoweza kusaidia kuviwezesha vituo vya mitandao vilivyopo Tanzania Zanzibar na Tanzania Bara kutoa muda maalum wa huduma za mtandao kwa bei nafuu kwa ajili ya wale watakaopenda kukisoma, kukichukua na ama kukihifadhi kitabu hiki kwenye vyombo vyao. Kuanzia hivi sasa, Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru! kimo machoni mwako. Fungua kurasa zake, zama na zamia kwenye bahari yake na ibuka na lulu zilizomo ndani yake. Mnakaribishwa nyote—walio karibu na walioko mbali. Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru! Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru! Zanzibar na Mapinduzi ya Afrabia Copyright 1431 Anno Hegirae / 2010 Anno Domini by Harith Ghassany Library of Congress Cataloging-in-Publication Data Mapinduzi ya Zanzibar, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Ukweli na Mapatano, Zanzibar na Oman, Afrabia, Masomo ya Afrabia. English translation of title: Goodbye Colonialism, Goodbye Freedom! Zanzibar and the Afrabia Revolution Keywords: Zanzibar Revolution, Union of the Republic of Tanzania, Truth and Reconciliation, Zanzibar and Oman, Afrabia Studies. Printed in the United States of America Na mtaujuwa ukweli na ukweli utawaweka huru. Biblia Yohane 8:32 Na sema: Ewe Mola wangu! Nipitishe kunako mlango wa ukweli na hishima, na nitowe kupitiya mlango wa ukweli na hishima. Na unipe nguvu kutoka kwako zenye ushindi zinisaidie. Qur’ani 17:80 Ujasiri mkubwa wa uongozi hufanywa na viongozi wenye kusukumwa na fikra zenye kuungwa mkono na nguvu na hisia za umoja wa kijamii katika kilele kipya cha kihistoria. Historia mpya ya kiutawala ilianza katika nchi ya Zanzibar na shujaa mwenye dhamana ya uongozi wa utawala, Rais Amani Abeid Karume, alipokutana na shujaa Maalim Seif Sharif Hamad, Ikulu ya Zanzibar, tarehe 5 Novemba 2009. Picha kutoka kwenye mtandao. Tabaruku Kwa wananchi wote wa Zanzibar, kwa Wazanzibari na marafiki wa Zanzibar popote pale walipo duniani, ili watoke katika kiza totoro cha upotoshaji wa historia ya Mapinduzi ya Zanzibar, mojawapo ya matukio makubwa kutendeka katika nchi yao, Afrika Mashariki na Kati, na kusudi waelekee kwenye mwangaza wa kudumu utakaoyaimarisha na kuyangarisha maridhiyano yao na kufunguwa kitabu kipya cha kujijuwa na kujitambuwa. Kwa Alhajj Rais Amani Abeid Karume kutokana na hikima, busara na ustahamilivu wa kibinaadamu na wa kisiasa anaouonyesha kwenye medani za Utawala wa leo Zanzibar, kuanzia kutochukuwa hatua ya kuyarejesha yaliyopita hadi kifo cha baba yake aliyekuwa Rais wa Kwanza wa Jamhuri ya Watu wa Zanzibar baada ya mapinduzi, na kwa kujitahidi kwake kupatanisha kambi zilizofarakana kwa nusu karne, ni ushahidi unaotosha wa dhamira ya kuelekeya kwenye Zanzibar Mpya inayotamaniwa na kila mwananchi wake na kila mpenda amani duniani. Ni majuzi tu ambapo katika historia ya nchi ya Zanzibar, Alhajj Rais Amani Abeid Karume na Alhajj Maalim Seif Sharif Hamad wameitekeleza ahadi waliyoitowa mbele ya ulimwengu ya kuyaweka maslahi ya nchi na utaifa wa Zanzibar mbele kuliko utashi wa kisiasa. Ahadi hiyo imepata baraka kamili za Baraza la Wawakilishi kutafuta suluhu ya kudumu itakayoungwa mkono na nguvu za wananchi wote ili kuumaliza mpasuko na mnaso wa kisiasa Zanzibar. Kwa ajili ya ndugu zetu wa iliyokuwa Tanganyika, leo Tanzania Bara, ili kiwafunguwe minyororo ya utumwa wa nafsi iliyowafanya wawaone ndugu zao wa Zanzibar kuwa ni mahasimu zao wanaopaswa kuendeleya kudhibitiwa kwa nguvu zote. Hii leo, Jamhuri ya Muungano wa Tanzania chini ya utawala wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, imepata Raisi ambaye anapopata nafasi hupenda kukumbusha namna viongozi wa Kizanzibari walivyompaliliya na leo hii ni mmoja kati ya Marais vijana wenye utawala mzuri na umaarufu barani Afrika. Furaha yangu ilifikiya kilele pale Rais Kikwete alipoizuru 1600 Pennsylvania viii Tabaruku Avenue, Washington DC, kama Rais wa Kiafrika wa kwanza kuonana na Rais Barrack Obama wa Marekani, ambaye mwenyewe ana asili ya jirani zetu wa Kenya. Inafahamika kuwa babu yake Rais Obama amewahi kuishi Zanzibar na kusoma ilimu ya dini ya Kiislam. Kwa ajili ya Wazanzibari na Watanganyika kwa ujumla wao ili kitabu hichi kiwawezeshe kuzibadilisha nafsi zao. Waweze kuona fursa za mapenzi na neema zilizopo kwao wao na kwa ndugu na majirani zao wa jadi, na kisha wafanye kazi kwa pamoja katika kujenga Muungano Mpya na uhusiano mkongwe baina ya Waafrika na Waarabu—Afrabia—utakaosimama juu ya ukweli na hivyo kuimaliza kabisa mitikisiko na misukosuko ya muda mrefu. Sina jengine la kuwatunukiya Watanzania Wazanzibari, Watanzania Bara, Waomani na Watanzania, Waafrika na Waarabu (Waafrabia) isipokuwa kitabu hichi ambacho ni tunda la fursa nyingi za ilimu ya bure ya msingi na ya sekondari niliyotunukiwa na Dola ya Zanzibar, pamoja na fursa za ilimu ya juu nilizotunukiwa na Dola ya Oman. Namshukuru Mungu Muweza kwa wema na ukarimu nnaotunukiwa katika maisha yangu na ya aila yangu na kufaidika nao kutoka Serikali ya Sultan Qaboos bin Said Al Said kiongozi ambaye anautambuwa na kuuhishimu wajibu wa Oman na taarikh zetu kwa Zanzibar. Sultan Qaboos bin Said Al Said anasifika duniani kwa kujitenga na mizozano na kwa siasa yake ya urafiki na kila nchi, na amekuwa tegemeo la kimataifa katika jitihada za kuleta mapatano ya kudumu katika migogoro mikubwa ya kimataifa na kwa kulinda amani duniani. Kwa unyenyekevu mkubwa nauomba uongozi na viongozi wetu adhiim wa pande mbili za Muungano na za uhusiyano mkongwe baina ya Waafrika na Waarabu—Afrabia, hadi raia kwa jumla, wake kwa waume, wakubwa kwa wadogo, vijana wa leo hadi Taifa letu la kesho, mkipokee kitabu chenu hichi kama ni kielelezo cha uzito wa nchi adhiim tuipendayo kwa dhati ya Zanzibar. Kwa wote hao, na kwa yote hayo natabaruku. Nawaomba tusome kwa pamoja kutoka historia ya Zanzibar ya nusu karne iliyopita juu ya umuhimu wa kuishi na kuongeza mapenzi baina ya watu wa Tanzania Zanzibar, Tanzania Bara, Oman na Khaleej, na Afrika Mashariki na Kati. Muhimu katika kufanikiwa katika kheri ni kujipa nguvu za kuweza kutazama mbele na kusamehe juu ya kuwepo uwezo wa kulipa kisasi. Tusiuwachiye uchungu wa mitihani iliyotukumba kuzigeuza shingo zetu kuangaliya nyuma tulikotoka. Yaliyopita si ndwele tugange yajayo. Yaliyomo Kutanabahisha xi Utangulizi xviii 1. Siri Nzito 1 2. Mirengo ya Kizalendo na Mapinduzi 11 3. Kwaheri Ukoloni, Kwaheri Uhuru! 31 4. Tupendane Waafrika 40 5. Sakura: Sadaka ya Tanganyika 54 6. Victor Mkello na Chama cha Wafanyakazi 73 7. Ali Muhsin na Nduguze 87 8. Musa bin Bek (Mozambique) na Zanzibar 99 9. John Okello – Kuibuka na Kuzama 120 10. Makomred na “Mungu wa Waafrika” 142 11. Katibu wa Midani ya Mapinduzi 154 12. Waafrika, Waarabu na Ukombozi wa Afrika 184 13. Misha Finsilber na Mapinduzi 216 14. Kuanguka kwa Ngome ya Kusini 224 x Yaliyomo 15. Fikra za Kuunda Shirikisho 242 16. Wagawe, Wasahaulishe, Watawale 249 17. Hayeshi Majuto Yao 259 18. Kosa la Mzee Nyerere 281 19. Kwaheri Ukoloni, Karibu Uhuru! 289 20. Mapinduzi Ndani na Nje 323 21. Nyumba ya Afrabia 348 Mapitio kwa Jumla 355 Viambatanisho 409 Marejeo 421 Faharisi 431 Shukurani 445 Mkusanyiko wa Picha 453 Mwandishi 497 Kutanabahisha Fikra na maelezo yaliyomo ndani ya kitabu hichi hazina uhusiano wa aina yoyote ile na Serikali, misimamo au sera za vyama vya siasa. Ni kitabu chenye kukusanya simulizi za wazee zenye kuungwa mkono na ushahidi kutoka nyaraka za kimataifa wenye kuufunuwa upotoshaji na kuukombowa utumwa wa kiakili ambao umekuwa ukitumika kwa nusu karne nzima
Details
-
File Typepdf
-
Upload Time-
-
Content LanguagesEnglish
-
Upload UserAnonymous/Not logged-in
-
File Pages485 Page
-
File Size-