Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Nje 2012/2013 Posted: Monday August 06, 2012 1:06 PM BT HOTUBA YA WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA MHESHIMIWA BERNARD KAMILLIUS MEMBE (MB.), AKIWASILISHA BUNGENI MAKADIRIO YA MAPATO NA MATUMIZI YA WIZARA YA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO W A KIMATAIFA KWA MWAKA WA FEDHA 2012/2013 UTANGULIZI 1. Mheshimiwa Spika, kufuatia taarifa iliyowasilishwa leo hapa Bungeni na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), naomba sasa kutoa hoja kwamba Bunge lako Tukufu lipokee, lijadili na kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa mwaka wa fedha 2012/2013. 2. Mheshimiwa Spika, awali ya yote napenda kutumia fursa hii kukupongeza wewe binafsi kwa kuliongoza kwa umahiri mkubwa Bunge hili la Bajeti la mwaka 2012/2013. Napenda pia kuwapongeza Mheshimiwa Job Ndugai (Mb.), Naibu Spika na Waheshimiwa Wenyeviti wanaokusaidia kuongoza Bunge hili kwa kazi nzuri wanayoifanya. 3. Mheshimiwa Spika, kwa namna ya pekee nachukua fursa hii kumpongeza Mheshimiwa Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa uongozi wake mahiri wa Serikali ya Awamu ya Nne. Chini ya uongozi wake Taifa letu limeendeleza utamaduni wetu wa kudumisha amani, utulivu na mshikamano. Nawaomba Watanzania wote tuendelee kudumisha hali hiyo ili kuimarisha umoja wetu ambao ni tunu isiyopatikana kwa bei yoyote. 4. Mheshimiwa Spika, niruhusu niungane na Waheshimiwa Wabunge wengine wote walionitangulia kuwapongeza kwa dhati kabisa Waheshimiwa Wabunge wapya, Mawaziri na Naibu Mawaziri walioteuliwa na Mheshimiwa Rais mwezi Mei 2012. Nawapongeza Wenyeviti na Makamu Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Bunge waliochaguliwa kipindi hiki kutokana na mabadiliko yaliyotokea kwenye nafasi mbalimbali humu Bungeni na ndani ya Serikali. Nampongeza pia Mheshimiwa Mussa Zungu Azzan, Mbunge wa Ilala, kwa kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge. 5. Mheshimiwa Spika, kwa njia ya kipekee kabisa, niruhusu niwapongeze Waheshimiwa Wabunge waliochaguliwa na Bunge lako Tukufu kuiwakilisha Tanzania kwenye Bunge la Afrika Mashariki. Wizara yangu kwa kuwa ndiyo inayosimamia masuala yote ya mambo ya nje, nawaahidi Waheshimiwa Wabunge ushirikiano wangu binafsi na ule wa Wizara nzima kwa kufanya kazi kwa karibu na kushirikiana na Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki. 6. Mheshimiwa Spika, naomba niwashukuru pia Mheshimiwa Mizengo Kayanza Peter Pinda (Mb.), Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania; Mheshimiwa William A. Mgimwa (Mb.), Waziri wa Fedha; pamoja na Mheshimiwa Stephen Masatu Wasira (Mb.), Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mahusiano na Uratibu kwa hotuba zao za kina ambazo zimetoa ufafanuzi na miongozo kwa masuala mbalimbali muhimu ya Taifa letu kwa mwaka wa fedha 2012/2013. Kwa ujumla wake, naomba kuwapongeza Waheshimiwa Mawaziri wote waliotangulia kuwasilisha bajeti zao kwa kazi nzuri walizozifanya. Hotuba zao zote zimefafanua kwa kina masuala ya uchumi, siasa na jamii yanayohusu nchi yetu na hivyo kuigusa pia Wizara yangu kwa njia moja au nyingine. 7. Mheshimiwa Spika, naomba nitumie fursa hii kutoa shukrani zangu za dhati na za uongozi mzima wa Wizara kwa Kamati ya Bunge ya kudumu ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama (NUU), chini ya uongozi madhubuti wa Mhe. Edward Ngoyai Lowassa (Mb.), Mwenyekiti wa Kamati kwa ushauri wao mzuri ambao wamekuwa wakiutoa mara kwa mara kwa Wizara yangu. Kamati hii imetoa mchango mkubwa sana katika kuiwezesha Wizara kukabiliana na changamoto zinazoikabili katika kutekeleza majukumu yake. Ninaamini ziara walizozifanya kwenye nchi mbalimbali kutembelea Balozi zetu zimewapa fursa ya kujionea wenyewe na kusikia kutoka kwa maafisa wetu changamoto mbalimbali zinazotukabili kama Wizara. Aidha, kwa ujumla, napenda kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote kwa michango yao wanayoitoa Bungeni katika kuishauri Serikali. 8. Mheshimiwa Spika, natoa shukrani na pongezi maalum kwa Mheshimiwa Mahadhi Juma Maalim (Mb), Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa ushirikiano anaonipa katika kutekeleza majukumu ya Wizara. Vilevile, nawapongeza na kuwashukuru Bwana John M. Haule, Katibu Mkuu, Mheshimiwa Balozi Rajabu H. Gamaha, Naibu Katibu Mkuu, Wakurugenzi, Mabalozi na wafanyakazi wote kwa msaada mkubwa wanaonipa katika kuiongoza Wizara hii. Pamoja na kukabiliwa na changamoto mbalimbali katika kutekeleza majukumu yao, nawashukuru kwa kazi nzuri na ya kizalendo ya kutetea maslahi ya Taifa letu. 9. Mheshimiwa Spika, shukrani za pekee ziwaendee wananchi na viongozi wa Mkoa wa Lindi, Wilaya ya Lindi na hasa wana-Mtama wote. Napenda pia nimshukuru mke wangu Mrs. Membe na watoto wangu kwa upendo na uvumilivu waliouonesha kwangu. 10. Mheshimiwa Spika, kabla ya kuanza kueleza kwa kina kuhusu hotuba yangu, niruhusu niungane na Viongozi wote, Wazanzibari na Watanzania kutoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki wote waliopoteza ndugu zao kwenye ajali ya meli ya MV Skagit iliyotokea Zanzibar. Kwa wale wote walioumia na wanaoendelea kujiuguza, namwomba Mwenyezi Mungu awape nguvu waweze kupona haraka. 11. Mheshimiwa Spika, vilevile, natoa salamu za pole kwa wale Wabunge wote waliopatwa na misiba ya wapendwa wao. Kwa wote, namwomba Mwenyezi Mungu awape faraja na azilaze Roho za Marehemu mahali pema peponi. Amina. TATHMINI YA HALI YA DUNIA KWA KIPINDI CHA 2011/2012 HALI YA DUNIA ULAYA NA MAREKANI 12. Mheshimiwa Spika, kwa ujumla, hali ya dunia kiuchumi, kisiasa na kijamii katika mwaka wa fedha 2011/2012 imekuwa ya mashaka makubwa na hivyo kuathiri utulivu katika nchi nyingi duniani. Hali hiyo imechochewa na mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi, kijamii na mabadiliko ya tabianchi katika maeneo mbalimbali duniani. 13. Mheshimiwa Spika, eneo la Ulaya limeathirika sana kiuchumi kutokana na madeni pamoja na mdororo wa uchumi ulioikumba dunia katika kipindi cha mwaka 2008. Hali hii pia iliathiri kwa kiasi kikubwa sarafu ya Euro, uchumi wa nchi zilizo katika ukanda wa sarafu hiyo ujulikanao kama “Eurozone” pamoja na nchi ambazo zinafanya biashara na nchi za Umoja wa Ulaya. Hali hiyo imechangia kwa kiwango kikubwa Viongozi katika baadhi ya nchi hizo kama vile; Ufaransa, Ugiriki, Italia, Hispania na Ireland kushindwa katika Chaguzi Kuu au kushinikizwa kujiuzulu. Kwa upande wa Marekani nayo ilikumbwa na misukosuko ya uchumi iliyosababishwa pia na mdororo wa uchumi wa mwaka 2008. Hata hivyo, uchumi wake umeanza kutengemaa baada ya mdororo huo. 14. Mheshimiwa Spika, kutokana na mdororo huo, nchi hizo zimelazimika kuchukua hatua kadhaa kunusuru uchumi wao ikiwa ni pamoja na kubana matumizi, kukopa zaidi ili kuwekeza katika sekta zenye kutoa ajira na kupunguza kutoa misaada kwa nchi zinazoendelea ikiwemo Tanzania kulingana na ahadi zao za awali. Kuna kila kiashiria kuwa uchumi wa Ulaya na Marekani hautapata utulivu kwa muda mrefu na hivyo uwezo wao wa kutoa misaada kupungua kadiri siku zinavyokwenda. Wizara na Balozi zetu za nje zinaendelea kufuatilia kwa makini hali ya uchumi inavyoendelea duniani na kuishauri Serikali kutekeleza mikakati ya kukabiliana na changamoto zitokanazo na hali hiyo ili kuimarisha uchumi wa Taifa letu na kuondokana na utegemezi. ASIA Mashariki ya Kati 15. Mheshimiwa Spika, eneo la Mashariki ya Kati bado liko katika hali ya tahadhari. Nchini Syria hali imeendelea kuwa tete kutokana na mapigano yanayoendelea nchini humo ambako waasi wanapigana dhidi ya Serikali ya Rais Bashar al – Assad tangu Januari mwaka 2011 na tayari wameshaingia kwenye Mji Mkuu wa Nchi hiyo. Umoja wa Mataifa na Jumuiya ya Nchi za Kiarabu (Arab League) zikiongozwa na Msuluhishi wa Mgogoro huo, Dkt. Kofi Annan wameshindwa hadi sasa kufanikisha kusitishwa kwa mapigano. Aidha, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limegawanyika ambapo wajumbe wa kudumu wenye kura ya turufu wametofautiana juu ya uamuzi wa kuchukua hatua za kijeshi dhidi ya Serikali ya Syria. Tanzania inaunga mkono jitihada za Msuluhishi Kofi Annan na kuwaomba wadau wote kutoingilia na kushinikiza matakwa yao nchini Syria na badala yake kumuunga mkono Msuluhishi ili kumaliza mgogoro huo kwa njia ya amani. 16. Mheshimiwa Spika, aidha, kuendelea kukua kwa uhasama baina ya Iran na nchi za Magharibi kunaleta changamoto ya ustawi wa amani katika ukanda huo. Uhasama huo unaletwa na hofu kuwa nchi ya Iran inarutubisha madini ya urani yanayotumika kutengeneza silaha za nyuklia. Tayari, Iran imewekewa vikwazo vya kiuchumi na Marekani ikishirikiana na nchi za Umoja wa Ulaya. Iran nayo imetishia kujibu mapigo kwa kufunga mlango wa Bahari ya Hormuz ambao hupitisha asilimia ishirini 20 ya mafuta yote ulimwenguni. Iwapo Iran itatekeleza uamuzi huo inaweza kuzusha vita ambayo italeta madhara makubwa kwa uchumi wa dunia. Hali hii ya mtafaruku baina ya Iran na nchi za Magharibi inaathiri pia mustakabali wa ukanda mzima wa Mashariki ya Kati kwa kuwa Iran ina ushawishi mkubwa kwenye siasa za nchi nyingine zenye machafuko kama vile Syria. Kuendelea kwa migogoro na machafuko katika ukanda wa Mashariki ya Kati kunaathiri kwa kiasi kikubwa uchumi wa dunia kwa sababu asilimia kubwa ya mafuta yanayotumika duniani hutoka katika ukanda huo. Pamoja na changamoto hizo, habari njema ni kwamba tayari Irani, Marekani, Nchi za Ulaya pamoja na wadau wengine wameshakubaliana kurejea kwenye meza ya mazungumzo na tayari mzunguko wa kwanza wa mazungumzo haya umeshafanyika. Imani yetu kama nchi ni kwamba wahusika wote kwenye mazungumzo hayo wataonesha utashi wa kweli wa kumaliza tatizo hilo kwa njia ya mazungumzo na si vinginevyo. Mashariki ya Mbali 17. Mheshimiwa Spika, kwa upande wa Mashariki ya Mbali hali ni tulivu ukiachilia majanga
Details
-
File Typepdf
-
Upload Time-
-
Content LanguagesEnglish
-
Upload UserAnonymous/Not logged-in
-
File Pages20 Page
-
File Size-