Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _______________ MAJADILIANO YA BUNGE _________________ MKUTANO WA NANE Kikao cha Thelathini na Tatu – Tarehe 26 Julai, 2012 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Anne S. Makinda) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati Zifuatazo Ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA NISHATI NA MADINI: Randama za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013. NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013. MHE. ABUU HAMOUD JUMAA (K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA VIWANDA NA BIASHARA): Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda na Biashara Kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka 2011/2012 Pamoja na Maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013. MHE. HIGHNESS SAMSON KIWIA - MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI WA WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA: Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani juu ya Wizara ya Viwanda na Biashara Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa Fedha, 2012/2013. MASWALI KWA WAZIRI MKUU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, maswali leo kwa Waziri Mkuu naona Kiongozi wa Kambi ya Upinzani hatumwoni. Kwa mujibu wa Kanuni zetu kama hayupo hawezi kuweko mbadala wake na kwa hiyo, nitaendelea na wale ambao walishaomba. MHE. ANNE K. MALECELA: Mheshimiwa Spika, kabla sijamwuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali, naomba tuwatakie heri Mama Anna Abdallah na Mama Makinda leo ni siku yao ya kuzaliwa, kwa hiyo happy birthday. (Makofi) Mheshimiwa Spika, baada ya hapo napenda kumwuliza Mheshimiwa Waziri Mkuu swali. Mheshimiwa Waziri Mkuu, kwa kuwa sisi wana Siasa hasa sisi tulioko humu ndani tuna uwezo mkubwa sana wa kuijenga nchi hii. Lakini pia tuna uwezo wa pili wa kuibomoa nchi hii na hata kuiingiza katika vita. Mheshimiwa Waziri Mkuu, siku za karibuni mmeanza tabia ambayo nilikuwa sijaiona muda wote tangu nimekuwa Mbunge katika kipindi changu cha tatu hiki Wabunge kuingia kwenye Majimbo ya wenzao na kuchukua hatua ya kuwakosoa kiutendaji na kutoa maneno yasiyoridhisha mbele ya wananchi kitu ambacho kimepelekea vurugu zikatokea mwishoni mwa wiki hata kuleta madhara. Je, Serikali inatoa tamko gani kwa sababu tabia hii ikiachiwa kuna siku tutaingia kwenye vita ya wenyewe kwa wenyewe? (Makofi) WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba nipongeze maana kama ni birthday yako nafikiri unastahili. (Makofi) SPIKA: Ahsante sana. WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijaribu kutoa maelezo kuhusu suala ambalo Mheshimiwa Anna Kilango Malecela, amejaribu kulieleza. Mimi nataka nikubali kwamba ni kweli ziko dalili za namna hiyo. Kwa bahati mbaya hata Jimboni kwangu yalinipata. (Makofi/Kicheko) Lakini mimi tafsiri yangu ilikuwa ni rahisi tu kwa sababu mambo haya yanategemea ukomavu wa mwanasiasa mwenyewe ambaye anakwenda kwenye eneo hilo. Maana wale waliokomaa wenye kuelewa dhamira ya Serikali ambao wanajua nia yetu hasa ni nini anajua wajibu wake anapokuwa katika maeneo haya ni kuzungumzia Sera za Chama chake, ama kusaidia kuweka sawa baadhi ya maeneo ambayo wanafikiri yanastahili kuboreshwa zaidi. Lakini sasa ukiwa na mwanasiasa ambaye kidogo hajafikia mahali pa kupevuka ni kweli ataanza kushughulikia individuals badala ya ku-deal na issues. (Makofi) Lakini mapema kabla hatujaja hapa Bungeni nilipata nafasi ya kuzungumza na msajili wa Vyama na nikamsihi sana kwamba asaidie vyama hivi vyote kwa kujaribu kukutana nao kimoja kimoja kujaribu kuwaelimisha juu ya ujenzi wa Demokrasia ya Vyama Vingi na maana yake hasa ni nini kwa sababu inaonekana bado wengi hatuelewi katika vuguvugu hili wajibu wetu hasa ni kitu gani. (Makofi) Mheshimiwa Spika, lakini wakati huo huo, Sheria ya Msajili wa Vyama ya Mwaka 1992 ambayo tulifanya Marekebisho hapa mwaka 2009 ukichukua na Kanuni zake za mwaka 2007 zinajieleza bayana kabisa, zimetoa maelezo mazuri sana namna Vyama vinavyopaswa kuendesha shughuli zake hasa nyakati hizi ambazo si za kampeni. Zimeeleza bayana kabisa. (Makofi) Lakini kizuri zaidi kwenye Sheria hizo na mimi naomba mzipitie msome kwa makini kama ni Chama ambacho kiko kwenye usajili wa muda Msajili wa Vyama anaweza akakifuta kwa matendo ambayo yanaashiria uvunjifu wa amani kwa maana ya matusi, kujaribu kudharauliana na kadhalika. Lakini hata Chama kilichoandikishwa kinaweza vile vile chini ya Sheria hiyo kufutwa endapo Msajili ataridhika na jambo hilo. (Makofi) Kwa hiyo, mimi nadhani nataka niwasihi viongozi wote kwa ujumla tuko hapa sisi wote ni watu wazima, tuko hapa kwa nia njema, tunataka kujenga nchi yetu vizuri, chonde chonde twende kwenye Majimbo tuzungumze masuala ya msingi ya Sera ya namna ya kutekeleza na kupeleka nchi hii mahali pazuri. Narudia tena unajua Mwanasiasa anayekaa anahangaika na individuals, watu hivi Pinda hiki, ujue na yeye vile vile ana tatizo kubwa sana katika upeo wake. (Makofi) Kwa hiyo, mimi nadhani kwa ufupi naweza nikalisema hivyo na kuwasihi wote tujaribu kufanya kazi hiyo kwa umakini mzuri kwa lengo la kujenga taifa letu na kwa heshima ya nchi yetu. (Makofi) MHE. MWIGULU LAMECK MCHEMBA MADELU: Mheshimiwa Waziri Mkuu, Serikali imeweka utaratibu mzuri sana kwa Waheshimiwa Wabunge, kwa kuanzisha Mfuko wa Jimbo, Mfuko wa Kuchochea Maendeleo. Lakini maendeleo hayo yanachochewa kwa kushirikiana na Madiwani. Lakini tofauti ni kwamba Madiwani wamekuwa wakichochea hayo maendeleo kwa kutumia posho zao wanazozipata. Je, Serikali haioni kuwa ni vyema kuwaangalizia utaratibu Madiwani wa kuwatengea fungu hata dogo tu linalolingana na Kata ili na wenyewe wanapoitwa kuchochea shughuli za maendeleo ambazo sote tunashuhudia wamekuwa wakisumbuliwa sana waweze kutumia mfuko huo tofauti na sasa wanavyotumia posho zao? (Makofi) WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwanza namshukuru sana Mheshimiwa Mwigulu Mchemba. Ni swali zuri lakini si rahisi sana kulijibu. Mimi ni Diwani vile vile wakinisikia na mimi nasema ovyo ovyo huko ni taabu vilevile. Lakini Sheria ile inachosema hapa ni nini kwa sababu ule mfuko ni wa Kuchochea Maendeleo katika Majimbo. Kuchochea maana yake nini hapa? Sheria inasema unapokuwa katika Jimbo lako miradi inayoendelea katika maeneo hayo. Unapofika mahali fulani na ukaombwa pengine msaada kumalizia mabati 40 au 50 Mfuko huu utakusaidia kuwezesha shule au zahanati hiyo kukamilisha ule mradi. Kwa maneno mengine ni fedha ambayo inakwenda kutoa mkusumo kwa wananchi katika maeneo yanayohusika. Si fedha ambayo unakuwa nayo unatembea unagawa kwa kila mtu unayemwona hapana. (Makofi) Kwa hiyo, basi kikubwa ninachokiona ni vizuri Waheshimiwa Wabunge ambao ndio Wenyeviti wa Mifuko ile na katika Sheria ile tumesema Madiwani, angalau wawili wawemo, tuhakikishe wale Madiwani, wawili wanakuwemo kwa sababu wanasaidia kuainisha baadhi ya miradi ambayo iko chini ya Kata fulani fulani kwa lengo la Mbunge kuweza kujua akipita pale asaidie namna gani. Sasa rai yake ni nzuri lakini kwa uwezo wa kibajeti tulionao leo pengine si rahisi sana. Lakini tunachoweza kuahidi tu mbele ya Bunge hili bado tutaendelea sisi kuboresha mafao/posho za Madiwani, ili kile kidogo kinapobanwa basi waweze kuchangia kwa kadri watakavyoona inafaa. (Makofi) MHE. MCH. PETER SIMON MSIGWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Nichukue fursa hii kabla sijauliza swali kuwatakia heri Waislam wote katika huu Mfungo wa Ramadhani katika Nguzo yao Muhimu. (Makofi) Mheshimiwa Waziri Mkuu swali langu, kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ambalo suala la Muungano ni suala la Katiba. Kila mtu anao uhuru wa kuabudu dini anayoitaka pasipokuingilia uhuru wa dini nyingine. Tarehe 20 Julai, 2012 Waziri wa Katiba wa Serikali ya Zanzibar alilihutubia Taifa la Zanzibar kupitia Televisheni na Radio akiwaambia watu wote wanaoishi Zanzibar na wanaoingia Zanzibar kuendana na Mfungo wa Ramadhani, akiamrisha kwamba Hotels zote na Restaurant zote zisiuze vyakula wakati wa asubuhi na mchana. Kama vile haitoshi alisema “watu wote wanaovaa nguo fupi hasa wanawake zinazoweza kuwatamanisha wanaume vyombo vya dola vichukue hatua” alisema vile vile “kwamba yeyote anayepatikana anakula chakula wakati wa mchana mamlaka ichukue hatua. (Makofi) Mheshimiwa Waziri Mkuu jambo hili ni hatari sana kwa Mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, jambo hili linadhalilisha Dini zingine. Naomba tuvumiliane nyie mkisema tunawavumilia. Jambo hili linatikisa uhuru wetu na Muungano wetu, ninaomba msimamo wa Serikali yako. (Makofi) WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, kwa bahati mbaya mimi sikusikiliza hiyo taarifa naomba kwanza niseme hilo. Lakini la pili sielewi hasa alisema nini naona ume-quote hivi. Kwa hiyo, sina hakika kama ndivyo ilivyokuwa au hapana. Lakini vyovyote vile itakavyokuwa kama unazungumza Serikali mbili iko Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na iko Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. Kauli imetoka kwa Kiongozi wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar. (Makofi) Ninachokifikiria hapa kwamba inawezekana kabisa kwa mazingira ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar wakati wa mwezi Mtukufu wa Ramadhani wameona hilo linaweza likasaidia kuwafanya wawe na mfungo mzuri. Kwa hiyo, mimi nadhani rai nzuri hapa ni kusema tuache waliendeleze kwa namna wanavyoona kwa mazingira yao inafaa. (Makofi) Lakini moja hili la uvaaji wa nguo fupi, nguo fupi nadhani tunakubaliana tu kwamba ni jambo ambalo si zuri halina staha. Linahitaji kwa kweli kusemwa na kila mtu, wala si jambo ambalo nasema linahatarisha Muungano hata kidogo, ni jambo tu ambalo linaeleweka tu.
Details
-
File Typepdf
-
Upload Time-
-
Content LanguagesEnglish
-
Upload UserAnonymous/Not logged-in
-
File Pages525 Page
-
File Size-