NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ________ MAJADILIANO YA BUNGE _________ MKUTANO WA TATU Kikao cha Ishirini na Moja – Tarehe 3 Mei, 2021 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Job Y. Ndugai) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tukae. Tunaendelea na Mkutano wetu wa Tatu, Kikao cha Ishirini na Moja. Naomba niwasalimu kwa Jina la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. WABUNGE FULANI: Kazi iendelee! SPIKA: Katibu. NDG. PAMELA PALLANGYO – KATIBU MEZANI: HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati Zifuatazo Ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA ELIMU, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Randama za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa mwaka wa fedha 2021/2022. SPIKA: Ahsante Naibu Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Mheshimiwa Juma Omar Kipanga. Nakushukuru sana. 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi. NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2021/2022. SPIKA: Ahsante sana Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mheshimiwa Khamis Hamza Khamis. Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama,Kamati nyeti. Karibu Mheshimiwa kwa niaba ya Kamati. MHE. VINCENT P. MBOGO - MAKAMU MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA MAMBO YA NJE, ULINZI NA USALAMA: Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Mambo ya Nje, Ulinzi na Usalama kuhusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kwa mwaka wa fedha 2020/2021 pamoja na Maoni ya Kamati kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022. SPIKA: Ahsante sana Mwanakamati, Mheshimiwa Vincent Mbogo. Tunakushukuru sana kwa niaba ya Kamati. (Makofi) Katibu! NDG. PAMELA PALLANGYO – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU SPIKA: Maswali. Ofisi ya Rais, TAMISEMI, Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, Dar es Salaam. 2 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Na. 168 Kuimarisha Elimu ya Awali MHE. MARIAM N. KISANGI aliuliza:- Utaratibu wa watoto kuingia darasa la kwanza ni lazima awe amepitia shule za awali. Je, Serikali ina mpango gani wa kuimarisha madarasa ya elimu ya awali? SPIKA: Majibu ya swali hilo; mpango wa Serikali wa kuimarisha elimu ya awali. Swali la Kibunge, Mheshimiwa Naibu Waziri, TAMISEMI. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE) alijibu:- Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mariam Nassoro Kisangi, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, elimu ya awali ni muhimu katika kumwandaa na kumjengea msingi mwanafunzi wakati wote atakapokuwa anaendelea na masomo katika ngazi zote. Kwa kuzingatia suala hili, Serikali ilitoa maagizo kuwa kila shule ya msingi nchini iwe na darasa la awali ili kuwapokea wanafunzi walio na umri kati ya miaka minne hadi mitano ikiwa ni maandalizi ya kujiunga na darasa la kwanza. Mheshimiwa Spika, Serikali imeanda Mtaala wa Elimu ya Awali unaoendana na aina ya ujifunzaji unaotakiwa kwa watoto wa elimu ya awali. Mtaala huo umezingatia ujifunzaji kwa kutumia michezo. Hadi Februari 2021, walimu 70,712 wanaofundisha darasa la awali, la Kwanza na la Pili wamepatiwa mafunzo ya namna ya utumiaji wa mbinu sahihi za ufundishaji, ufaraguzi na utumiaji wa zana za kufundishia. 3 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Hatua hii imeimarisha ufundishaji na ujifunzaji katika madarasa ya awali nchini. Mheshimiwa, Serikali imezielekeza Halmashauri zote nchini kuhakikisha kuwa watoto wa Darasa la Awali, la Kwanza na la Pili wanapatiwa vyumba vya bora vya madarasa vinavyowawezesha kutengeneza mazingira bora ya kujifunzia kwa rika lao na kuhakikisha kuwa mtoto wa Darasa la Awali analindwa na kupata eneo zuri la kujifunzia kwa kucheza ndani na nje ya darasa. Hatua hii pia imehusisha kubadilisha madarasa haya kwa kuweka zana za ujifunzaji. Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuboresha miundombinu na kuwajengea uwezo walimu wanaofundisha Elimu ya Awali katika shule zote nchini kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. SPIKA: Sasa Mheshimiwa Naibu Waziri, Viswahili vingine vugumu; katika majibu yako unasema ufaraguzi. Sasa hapa taabu, unatuacha njiani. Mheshimiwa Mariam Kisangi, uliza swali lako. MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kunipa nafasi nami niweze kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri, ninayo maswali mawili ya nyongeza. Kwanza, kwa kuwa katika Mkoa wa Dar es Salaam wakati wa kuandikisha watoto kuingia darasa la kwanza kunakuwa na sharti la Watoto kwamba ni lazima waje na certificate ya kumaliza elimu ya awali; na changamoto hii imekuwa ni kubwa sana katika maeneo ya pembezoni mwa Mkoa wa Dar es Salaam katika shule kama za Mbande, Majimatitu, Charambe, Nzasa na maeneo mengi ya Mkoa wa Dar es Salaam:- Je, Serikali inatoa kauli gani sasa kuondoa changamoto hii kwa wananchi au wazazi ambao wanapeleka watoto wao kuwaandikisha darasa la kwanza? (Makofi) 4 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Spika, swali la pili. Kwa kuwa uwiano wa darasa la kwanza utakuta kuna mikondo minne au mitano ya lakini darasa la awali linakuwa moja tu, jambo ambalo ni changamoto kubwa kwa watoto wote ambao wanaanza darasa la kwanza kwenda kujiunga na elimu ya awali katika shule husika:- Je, Serikali imejipangaje sasa kuweka bajeti ya kutosha katika kuimarisha elimu ya awali katika shule zote za msingi? (Makofi) SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, mkiona swali lenyewe lilivyokuwa limeandikwa tu, ni sentensi moja; la Kibunge, lakini pia maswali ya nyongeza mazito kabisa. Hongera sana Mheshimiwa Mariam Kisangi. Majibu ya maswali hayo muhimu, Naibu Waziri, TAMISEMI, Mheshimiwa David Silinde, kwamba kuingia darasa la kwanza lazima mtu aje na cheti kutoka awali. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DAVID E. SILINDE): Mheshimiwa Spika, ahsante sana. Mheshimiwa Mbunge ameuliza swali hapa kwamba kumekuwa na sharti la certificate ya Elimu ya Awali; na anataka kufahamu Serikali inatoa kauli gani? Kwanza nieleze tu kabisa kwamba katika ngazi ya awali, Serikali haina utaratibu wa certificate. Hizo ni taratibu ambazo watu wamejitungia huko chini. Mara nyingi sana ni hizo shule za private zaidi ndiyo wamefanya hivyo, lakini huo utaratibu haupo. Mheshimiwa Spika, kauli ya Serikali ni moja tu; certificates zilizopo ni za darasa la saba, kidato cha nne, kidato cha sita na kuendelea, lakini kwa shule za awali certificate hakuna. Huo ni utaratibu ambao Serikali haiutambui. Kwa hiyo, hiyo ndiyo kauli ya Serikali. Mheshimiwa Spika, jambo la pili, uwiano wa wanafunzi, hususan darasa la kwanza na shule ya awali; na kwa sababu hiyo niseme tu kwamba kutokana na umuhimu 5 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) wa kuongeza wanafunzi katika shule za awali, ndiyo maana sasa hivi katika mipango yote ya Serikali ambayo tunayo, ikiwemo EP4R, Boost, Lens, RISE, miradi yote, tumehakikisha kabisa kwenye kila mradi tunaweka na component ya kujenga madarasa ya shule za awali ili kuhakikisha watoto wetu wanapata madarasa bora na tunaongeza madarasa ili watoto hao waweze kupata mazingira bora ya kujifunzia. Mheshimiwa Spika, ahsante sana. (Makofi) SPIKA: Mheshimiwa Waziri Ummy! Aah, majibu ya nyongeza, ahsante Mheshimiwa Waziri, nimekuona. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, namshukuru sana Mheshimiwa Naibu Waziri kwa majibu mazuri na vile vile nampongeza Mheshimiwa Mariam Kisangi. Nataka tu kuendelea kutoa tamko la kisera; ni marufuku shule kudai certificate ya awali kwa wanafunzi wanaoanza darasa la kwanza. Mheshimiwa Spika, ninachotaka kusema ni kwamba bado hatujafanya vizuri katika kuongeza access ya watoto kuanza elimu ya awali. Kwa hiyo, haileti mantiki kusema kila mtoto ili aanze Darasa la Kwanza awe na certificate ya awali. Tunawaahidi Waheshimiwa Wabunge kwenda kuweka nguvu za kuboresha watoto wetu hususan wa masikini kupata elimu ya awali, hususan katika maeneo ya vijijini. (Makofi) Mheshimiwa Spika, nimeona niweke hiyo; na wote ambao wanadai certificate ya elimu ya awali wajue kwamba wanatenda kinyume na maelekezo na miongozo ya Serikali. SPIKA: Kwa kweli jibu hili ni la kutia moyo sana. Ahsante sana Mheshimiwa Waziri, maana hii imekuwa shida sasa. Bado tuko katika Wizara hiyo hiyo ya TAMISEMI, Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhani, Mbunge wa Singida Kaskazini, kule Mtinko, Ilongero. (Kicheko/Makofi) 6 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Na. 169 Kumaliza Ujenzi wa Vituo vya Afya Kata za Makuro na Ngimu – Singida Kaskazini MHE. ABEID R. IGHONDO aliuliza:- Je, ni lini Serikali itamaliza ujenzi wa maboma ya vituo vya afya yaliyojengwa kwa nguvu za wananchi katika Kata za Makuro na Ngimu? SPIKA: Majibu ya swali la Singida Kaskazini, Naibu Waziri, TAMISEMI, Mheshimiwa Dkt. Dugange, tafadhali. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. DKT. FESTO J. DUGANGE) alijibu:- Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abeid Ighondo Ramadhani, Mbunge wa Jimbo la Singida Kaskazini, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, ili kuboresha huduma za afya katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida, katika mwaka wa fedha 2018/2019 Serikali iliipatia Halmashauri ya Wilaya ya Singida shilingi bilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa Hospitali ya Halmashauri. Katika mwaka wa fedha 2020/2021, hospitali hiyo imetengewa shilingi milioni 500 kwa ajili ya ujenzi wa wa wodi tatu na shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa vifaa tiba. Mheshimiwa Spika, katika mwaka wa fedha 2020/2021 Serikali imetenga shilingi milioni 150 kwa ajili ya kukamilisha maboma ya Zahanati Minyeye, Mnung’una na Msikii katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida. Aidha, katika mwaka wa fedha 2021/2022, Serikali imetenga shilingi milioni 250 kwa ajili ya kukamilisha maboma matano ya zahanati katika Halmashauri ya Wilaya ya Singida ili kuunga mkono jitihada zinazofanywa na wananchi katika kujenga na kuboresha miundombinu ya kutolea huduma za afya. 7 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Spika, Serikali itaendelea kuimarisha miundombinu ya huduma za afya katika Jimbo la Singida Kaskazini zikiwemo Kata za Makuro, Ngimu na nchini kote ili kuendelea kuboresha huduma za afya kwa wananchi.
Details
-
File Typepdf
-
Upload Time-
-
Content LanguagesEnglish
-
Upload UserAnonymous/Not logged-in
-
File Pages242 Page
-
File Size-