Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _______________ MAJADILIANO YA BUNGE _________________ MKUTANO WA NANE Kikao cha Arobaini na Mbili – Tarehe 7 Agosti, 2012 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati Zifuatazo Ziliwasilishwa Mezani na:- WAZIRI WA MAMBO YA NJE NA USHIRIKIANO WA KIMATAIFA: Taarifa ya Mwaka na Hesabu za Kituo cha Kimataifa cha Mikutano cha Arusha kwa Mwaka 2010/2011 (The Annual Report and Accounts of Arusha International Conference Centre for the Year 2010/2011). NAIBU WAZIRI WA MAENDELEO YA MIFUGO NA UVUVI: Randama za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013. NAIBU WAZIRI WA KAZI NA AJIRA: Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kazi na Ajira kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013. MHE. JENISTA J. MHAGAMA - MWENYEKITI WA KAMATI YA MAENDELEO YA JAMII: Taarifa ya Mwenyekiti wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii, Kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ya Kazi na Ajira kwa Mwaka 2011/2012 pamoja na Maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2012/2013. MHE. CECILIA D. PARESSO - MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI KWA WIZARA YA KAZI NA AJIRA: Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani juu ya Wizara ya Kazi na Ajira Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2012/2013. MASWALI NA MAJIBU Na. 334 Posho kwa Wenyeviti wa Serikali ya Vijiji MHE. ABDUL JABIR MAROMBWA aliuliza:- Kumekuwa na kilio cha muda mrefu cha Wenyeviti wa Serikali za Vijiji kutopata posho zao za kila mwezi wakiwa ndio wasimamizi wakubwa wa miradi ya maendeleo katika vijiji vyao:- Je, Serikali ina mpango gani wa kuwapatia Wenyeviti hao posho yao ya kila mwezi? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Abdul Jabir Marombwa, Mbunge wa Kibiti, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, kwa kuzingatia majukumu makubwa ya Wenyeviti wa vijiji na Mitaa, Halmashauri zimekuwa zikilipa viwango vya posho ambavyo hutofautiana kati ya Halmashauri moja na nyingine. Viwango vya posho vinalipwa kutokana na mapato ya ndani ya Halmashauri na hivyo kutofautiana kati ya Halmashauri moja na nyingine. Ili kuboresha kiwango hiki Halmashauri zimesisitizwa kuhakikisha zinaimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani kila mwaka. Mheshimiwa Spika, Serikali katika mwaka 2012/2013 imerejesha ruzuku ya fidia ya vyanzo vya mapato vilivyofutwa baada ya kuonekana ni kero kwa kiasi cha shilingi bilioni 63.5. Kurejeshwa kwa ruzuku hii kutawezesha Halmashauri kumudu uendeshaji wa ofisi ikiwa ni pamoja na kulipa posho za Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji. Mpango wa Serikali ni kuimarisha ukusanyaji wa mapato ya ndani ya Halmashauri iil kuwezesha ulipaji wa posho kwa Wenyeviti wa Mitaa na Vijiji. MHE. ABDUL JABIR MAROMBWA: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa majibu ya Serikali. Lakini pamoja na majibu hayo nilikuwa na swali moja la nyongeza. Kwa kuwa Halmashauri nyingi nchini ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Rufiji uwezo wake wa kukusanya mapato na vyanzo vyake vya mapato ni duni sana. Je, Serikali haioni sasa kuwa kuna haja ya kuziangalia upya Halmashauri zile ambazo hazina uwezo ili iweze kutoa ruzuku iweze kuwapatia viongozi hawa wanaongoza vijiji vyetu? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Abdul J. Marombwa Mbunge wa Kibiti, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, hili tatizo analosema Mheshimiwa Mbunge ni kweli limekuwepo. Labda nieleze kwamba ni kwa nini lilijitokeza, mwaka jana na mwaka huu wa fedha uliopita, Serikali ilikuwa imeondoa hiki chanzo ambacho tumekisema hapa, kulikuwa kuna kitu tunakiita nuisance taxies tulifuta ile halafu baadaye Serikali ikaweka ruzuku pale. Lakini mwaka jana Waheshimiwa Wabunge walikumbuka hapa kwamba ruzuku ile ilipoondolewa ilibakia bilioni 10 tu na ndio iliyoleta matatizo hayo ambayo yanasababisha Mheshimiwa Marombwa azungumzie jambo hili. Nina hakika Wabunge wengine wote watakaosimama hapa watasemea jambo hilo. Lakini katika Bajeti hii tunayoizungumzia sasa tumepitisha hapa, tumeiomba Serikali irudishe kitu kinachoitwa the general purpose grant, hii ndio inayotumika kwa ajili ya kuendesha ofisi, kwa ajili ya mambo ya re-tooling, mambo ya capacity building na mambo mengine yanaingia mle ndani. Hii ni pamoja na hizi posho ambazo zinazungumzwa za Wenyeviti zinazosemwa hapa ambazo zinasaidia sasa kwenda kusaidia hizo Halmashauri ambazo Mheshimiwa Mbunge, anaziona wakati mwingine kwamba ziko hoi ndio maana yake, hii hela ya shilingi bilioni 65.5 ambayo mmempitishia Mheshimiwa Waziri Mkuu ndio inayokwenda kufanya kazi hiyo. (Makofi) Naelewa anachosema kwamba ni kweli Halmashauri hizi zinatofautiana lakini kilichosemwa hapa ni kwamba tuimarishe mapato yetu ya ndani na humu ndani msije mkasahau tumepitisha tena na maamuzi mengine makubwa na posho za madiwani zimepita na vitu vingine vya namna hiyo. Kwa hiyo, napenda kumwambia Mheshimiwa Marombwa tunashukuru kwamba unatukumbusha kuhusu wajibu wa hawa watu muhimu, wenyeviti wa vijiji wanafanyakazi nzuri hata kule kwako Mheshimiwa Spika, Njombe kule Wenyeviti wa vijiji na Mitaa wanakazi nzuri sana. Kwa hiyo, tuombe hii itakapokuja sasa muisimamie vizuri ili mhakikishe kwamba Wenyeviti wa Vijiji wanaweza wakapata hizo posho zao kama tulivyoeleza hapa. MHE. MICHAEL LEKULE LAIZER: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Kwa kuwa anachosema Naibu Waziri katika Halmashauri zetu hawana habari kwamba fedha za ruzuku zilizorudishwa zinapaswa kuwalipa wenyeviti wa vijiji. Je, Serikali sasa itaweka amri kwamba kila Halmashauri iwalipe Wenyeviti wa Vijiji? (Makofi) NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (TAMISEMI): Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Michael Lekule Laizer, Mbunge wa Longido na jirani yangu, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, hivi tunavyosema hapa ndio tunasema hivyo, ndio tunawaambia hivyo, ndivyo tulivyosema wakati Mheshimiwa Waziri Mkuu alipokuwa anapitisha Bajeti yake hapa alisema kwamba general purpose grant inarudishwa hapa kwa ajili ya kwenda kufanyakazi hiyo. Sasa nasema hivi sasa tunawaambia Halmashauri hela zinapokuja, hela hizi ni pamoja na kwenda kuwapa posho Wenyeviti wa Vijiji na Wenyeviti wa Mitaa. Kwa hiyo, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu nasema hapa mtu yeyote atakayekwenda kinyume na maelekezo yanayotoka hapa huyu ajue kwamba sisi tutashuka naye jumla jumla. Haiwezekani Bajeti imepitishwa na Waziri Mkuu anasema kwamba hii ni pamoja na kufanya kazi hiyo wala hututegemei kwamba wale wenyeviti wa vijiji ambao walikuwa wanadai ambao wanaonekana kwamba hawajalipwa tunaambiwa kwamba hawajalipwa no way. Tutafuatilia na Mheshimiwa Lekule Laizer pamoja na Wabunge wote tunaomba mtusaidie kuwaambia hela hizi zinapelekwa kule ni pamoja na kulipa posho za Wenyeviti wa Vijiji na Mitaa. (Makofi) SPIKA: Mheshimiwa Naibu Waziri circular ndio zinafanya kazi siyo maneno peke yake. MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru nilitaka kuuliza swali ambalo mwenzangu Mheshimiwa Lekule Laizer ameuliza, nakushukuru sana. (Makofi) Na. 335 Upungufu wa Walimu na Vifaa Shule za Nkasi Kusini MHE. DESDERIUS JOHN MIPATA aliuliza:- Wananchi wa Jimbo la Nkasi Kusini wameitikia wito wa ujenzi wa shule ya Sekondari kwa kila Kata lakini bado shule hizo zinakabiliwa na changamoto za upungufu wa walimu, vitabu vya Sayansi ya Jamii (Arts), madawati, ukosefu wa madawati ukosefu wa maabara na madarasa ya kidatu cha V na VI:- (a) Je, Serikali ina mpango gani wa kumaliza kabisa tatizo la ukosefu wa walimu na vitabu vya sayansi ya jamii (Arts)? (b) Je, Serikali itakubaliana na ushauri wa kupanua na kuziwezesha shule za Sekondari za Kate, Chala na Wapembe ili ziweze kupokea wanafunzi wa Kidato cha V na VI? (c) Je, ni lini tatizo la ukosefu wa maabara litatatuliwa katika shule za sekondari nchini? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (ELIMU) alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Desderius John Mipata, Mbunge wa Nkasi Kusini, lenye sehemu A, B, na C kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, ushirikiano wa wananchi, Serikali na wadau wa maendeleo katika kutekeleza Ilani ya Chama cha Mapinduzi ya kuwa na shule ya Sekondari mpaka ngazi ya Kata umeleta mafanikio ya ongezeko la shule za sekondari kutoka shule 1,745 (2005) hadi kufikia 4,367 (2012) ambazo kati ya hizo 3,337 ni shule za Sekondari ni Serikali na 1030 ni shule binafsi. Mafanikio haya yameenda sambamba na kuongezeka kwa mahitaji ya walimu, miundombinu na vifaa vya kufundishia na kujifunzia. Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi imeongeza idadi ya vyuo vya ualimu, vyuo vikuu na udahili katika kozi za ualimu pamoja na kuajiri walimu kadri wanavyofaulu. Mkakati huu umewezesha Serikali kuajiri na kuwapanga katika shule za sekondari walimu 9,226 (2010/2011) na walimu 12,188 (2011/2012). Serikali itaendelea kuajiri walimu na kuwapanga katika shule kadri wanavyohitimu na ifikapo mwaka 2014 upungufu utakuwa umekwishafika zaidi asilimia 90. Mheshimiwa Spika, kupitia utekelezaji wa mpango wa maendeleo ya elimu ya sekondari, Serikali imekuwa inatenga fedha za ruzuku ya uendeshaji (Capitation) katika shule za sekondari. Mwongozo wa matumizi ya fedha hizi unaelekezwa asilimia 50 kutumika katika ununuzi wa vitabu
Details
-
File Typepdf
-
Upload Time-
-
Content LanguagesEnglish
-
Upload UserAnonymous/Not logged-in
-
File Pages429 Page
-
File Size-