Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _________________ MAJADILIANO YA BUNGE ____________ MKUTANO WA KUMI NA SITA Kikao cha Thelathini na Saba – Tarehe 24 Julai, 2009 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua MASWALI NA MAJIBU Na. 272 Halmashauri ya Wilaya ya Dodoma Kukabidhiwa Jengo lake MHE. JENISTA J. MHAGAMA (K.n.y. MHE. FELISTER A. BURA) aliuliza:- Kwa kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma inatumia majengo ya iliyokuwa Shule ya Sekondari ya Aga-Khan kama Ofisi zake:- Je, ni lini Halmashauri itakabidhiwa jengo lake linalotumiwa na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ? WAZIRI WA MIUNDOMBINU alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza kabisa, napenda kuchukua fursa hii, kutoa shukrani nyingi sana kwako wewe mwenyewe binafsi na kwa Waheshimiwa Wabunge wenye taaluma ya afya, ambao wamemhudumia Naibu Waziri, Mheshimiwa Hezekiah Chibulunje, wakati alipopata matatizo hapa Bungeni. Natoa shukrani nyingi sana pia kwa Wabunge wote, ambao wamekwenda kumpa pole na kumwombea dua ili aweze kupona mapema. Mheshimiwa Naibu Waziri, sasa hivi anaendelea vizuri, yuko katika mapumziko na Mungu akijalia, tutakuwa naye hivi karibuni. Mheshimiwa Naibu Spika, ninakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kuwa, eneo lenye majengo yanayotumiwa na baadhi ya Wizara za Serikali hapa Dodoma ni mali ya Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, kwa mujibu wa Hati Miliki Na. 12814 iliyotolewa tarehe 2 Desemba, 1958. Eneo hilo ambalo lilijulikana kama Town Hall Plot, majengo 1 yake yalianza kutumiwa na Wizara za Serikali kwa nyakati mbalimbali kutokea mwaka 1973, baada ya kuvunjwa kwa Serikali za Mitaa na yameendelea kutumiwa na Wizara za Serikali hata baada ya kuanzishwa tena Mamlaka za Serikali za Mitaa. Hivi sasa majengo hayo mali ya Manispaa ya Dodoma pamoja na jengo jipya lililojengwa kwenye eneo hilo na iliyokuwa Wizara ya Ushirika na Masoko, yanatumiwa kama Ofisi za muda za Idara ya Ushirika, iliyoko chini ya Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika; Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko; Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana; Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inatambua haki ya Kisheria, ambayo Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma inayo juu ya Miliki ya majengo hayo, pamoja na hali ya kutokuwa na ofisi zake za kufanyia kazi. Pia kwa kuzingatia kuwa, kwa muda mrefu Wizara za Serikali zimekuwa zikiyatumia majengo hayo, pamoja na kuongeza jengo jipya kwenye eneo hilo, Wizara yangu itaandaa mazungumzo kati ya Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma na Wizara za Serikali zinazohusika ili kupata utaratibu wa namna ya kupata usuluhisho wa tatizo hili. MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri wa Miundombinu, naomba kuuliza maswali mawili madogo ya nyongeza :- Kwa kuwa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma imeshateseka kwa muda mrefu sana kwa kukosa ofisi ; na kwa kuwa ofisi wanayotumia ni jengo la iliyokuwa Sekondari ya Aga- Khan; na kwa kuwa jengo lile siyo lao hawawezi kuongeza chumba hata kimoja na baadhi ya ofisi wanatumia vyumba vilivyokuwa vyoo, ambavyo hakuna madirisha hakuna nini:- (i) Je, serikali haioni kwamba inawatesa Watumishi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ? (ii) Ni lini Serikali itazungumza na Halmashauri na kutenga fedha kwa ajili ya kujenga Ofisi ya Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma ? WAZIRI WA MIUNDOMBINU: Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Felister Bura, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, moja ni kwamba, Serikali inatambua tatizo ambalo Wafanyakazi wa Halmashauri ya Dodoma wanalipata, kwa kutokuwa na majengo yao na hasa baada ya kuwa tumekiri kwamba, wana eneo ambalo kwa haki kabisa ni la kwao, ambalo walilipata mwaka 1998; na pale kwenye Plot ile Town Hall bado ina kibao chake kile kwamba, jengo lile limezinduliwa Julai, mwaka 1959 na Sir Richard Turnbull, ambaye alikuwa Gavana wakati ule. Tunatambua tatizo ambalo lipo na tutashughulikia haraka iwezekanavyo, usuluhishi wa kupata Plot hii au majengo yale ambayo yalikuwa ya Halmashauri ili waweze kurudishiwa na tukishafanikiwa hilo, maana yake ni kwamba, sasa hatutakuwa na tatizo la kutenga pesa kwa ajili ya ujenzi wa Ofisi mpya. 2 MHE. JENISTA J. MHAGAMA: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa Wizara ya Miundombinu imekuwa ikifanya kazi ya kujenga majengo na kuyauza na kukusanya pesa na kujenga mengine; na kwa kuwa Halmashauri zetu nyingi katika nchi yetu ya Tanzania kwa kweli hazina ofisi nzuri zinazopendeza ukilinganisha na hadhi ya Halmashauri katika nchi yetu ikiwemo Halmashauri ya Wilaya ya Songea:- Je, Mheshimiwa Waziri sasa yuko tayari katika ule mpango wa kujenga, kuuza na kupokea pesa, baadhi ya pesa wanazozipata baada ya kuuza majengo haya wanaweza sasa kutengeneza programu rasmi ya kujenga ofisi kwa ajili ya Halmashauri zetu ikiwepo Halmashauri ya Wilaya ya Songea ? WAZIRI WA MIUNDOMBINU: Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mhagama kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali kupitia TBA, inatenga pesa kila mwaka kwa ajili ya mpango wake mahususi wa kuwajengea nyumba watumishi wa Umma. Imetenga pesa mwaka uliopita na imetenga tena katika mwaka huu wa fedha, lakini katika Halmashauri za Wilaya mbalimbali, ujenzi huu unaweza ukafanywa pia na TBA kama Mkandarasi, lakini kwa kutumia pesa ambazo wenyewe Halmashauri wamezitenga kwa ajili ya ujenzi huo. Wizara ya Miundombinu kupitia TBA, itakuwa tayari kufanya kazi hiyo kama ambavyo imetimiza kazi hiyo maeneo mbalimbali, kwa mfano, katika Mkoa wa Manyara na katika Halmashauri za Mkoa wa Manyara. Na 273 Ujenzi wa Daraja la Kigamboni MHE. SAVELINA S. MWIJAGE (K.n.y. MHE. ANIA S. CHAUREMBO) aliuliza:- Kwa kuwa Serikali ina mpango wa kujenga Daraja la kusaidia uvukaji eneo la Kigamboni Wilaya ya Temeke; na kwa kuwa wananchi wanategemea sana utekelezaji wa ujenzi kuanza mara moja:- (a) Je, Serikali inasema nini kuhusu kuanza kwa ujenzi huo? (b) Je, ujenzi huo utagharimu kiasi gani cha fedha? WAZIRI WA MIUNDOMBINU alijibu:- 3 Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Ania Saidi Chaurembo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli Serikali ina mpango wa kujenga Daraja la Kigamboni ili kupata ufumbuzi wa kudumu wa usafiri wa Wananchi wa eneo la Kigamboni Wilaya ya Temeke. Kwa kuwa ujenzi wa Daraja kubwa la Kigamboni unahitaji fedha nyingi kuliko uwezo wa Serikali, Serikali imeamua kufungua milango na kukaribisha Wawekezaji kutoka Sekta Binafsi ili kuwekeza katika ujenzi na uendeshaji wa Mradi huu kwa kushirikiana na Shirika la Taifa la Hifadhi ya Jamii (NSSF). Mheshimiwa Naibu Spika, mchakato wa kumtafuta mbia kutoka Sekta Binafsi chini ya utaratibu wa Public Private Partnership (PPP), umeshaanza kwa kuorodhesha (shortlisting) makampuni yaliyoonesha nia ya kuwekeza katika Mradi huu. Aidha, NSSF inaendelea kuandaa nyaraka za zabuni za kumpata Mshauri (Transaction Advisor), atakayesaidia NSSF kuandaa nyaraka za zabuni ya kumpata mbia toka Sekta Binafsi. Gharama za ujenzi wa daraja hili zitajulikana baada ya zoezi la kumpata Mkandarasi wa kujenga Daraja hili kukamilika. MHE. SAVELINA S. MWIJAGE: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana. Kwa kuwa, matatizo ya Daraja la Kigamboni ni sawasawa na matatizo ya Daraja la Bujugo na Kashalo:- Je, ni lini Serikali itawaonea huruma watu wa Kashalo na kuwasaidia angalau kivuko au daraja ili waache kutumbukia mara kwa mara kwenye Mto ule? NAIBU SPIKA: Mheshimiwa, wala siyo sawasawa; Kigamboni ni bahari na Kashalo ni mto tu. Haya Mheshimiwa Waziri majibu. (Kicheko) WAZIRI WA MIUNDOMBINU: Mheshimiwa Naibu Spika, ningependa kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Savelina Mwijage kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, ni bahati mbaya sana sikumbuki kwa ukamilifu, ratiba ambayo tumeiweka kwa ajili ya eneo hilo la Bujugo, lakini namuahidi kwamba, tukimaliza session hii, nitampatia majibu kwa maandishi. Na 274 Tatizo la Uratibu kwenye Mifuko ya Jamii MHE. AZIZA S. ALLY aliuliza:- 4 Kwa kuwa Mifuko ya Jamii Tanzania inakabiliwa na tatizo la uratibu; na kuwa kuwa haki ya mafao ya Wafanyakazi wa Tanzania zinatofautiana sana kutokana na Mifuko hiyo kuundwa kwa Sheria tofauti na kuwa kwenye Wizara tofauti na hivyo kusababisha mafao ya Wastaafu kutofautiana:- (a) Je, Serikali haioni kuwa Mifuko hiyo kuwa na Sheria tofauti ni tatizo kubwa? (b) Je, Serikali inasema nini kuhusu kuleta Sheria Bungeni ili Mifuko hiyo iwe na Sheria moja ili mafao ya wafanyakazi yasitofautiane kati ya wale wa Serikali Kuu na za Mitaa na wale wa Mashirika ya Umma? WAZIRI WA KAZI, AJIRA NA MAENDELEO YA VIJANA alijibu:- Mheshimiwa Naibu Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Aziza Sleyum Ally, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, Tanzania ina Mifuko sita ya Hifadhi ya Jamii. Mifuko hiyo imeundwa kwa Sheria za Bunge na ipo katika Wizara tofauti kama ifuatavyo: NSSF upo chini ya Wizara ya Kazi, Ajira na Maendeleo ya Vijana; PPF upo chini ya Wizara ya Fedha; PSPF upo chini ya Wizara ya Fedha; LAPF upo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Serikali za Mitaa; GEPF upo chini ya Wizara ya Fedha; na NHIF upo chini ya Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii. Mheshimiwa Naibu Spika, utaratibu wa kila Mfuko kuwa na Sheria yake, umesababishwa pamoja na mambo mengine, mafao yanayotolewa na Mifuko hiyo kutofautiana. Baada ya Serikali kubaini tatizo hili, hatua za kutafuta ufumbuzi wake zimeanza kuchukuliwa. Hatua hizo ni pamoja na kuandaliwa kwa Sera ya Taifa ya Hifadhi ya Jamii ya Mwaka 2003. Sera hiyo pamoja na mambo mengine, inabainisha matatizo na changamoto zinazoikabili Sekta ya Hifadhi ya Jamii na utaratibu wa kutafuta ufumbuzi wake. Aidha, kutungwa kwa Sheria ya Mamlaka ya Udhibiti na Usimamizi wa Hifadhi ya Jamii Na. 8 ya Mwaka 2008 ni sehemu ya utekelezaji wa Sera hiyo. Sheria hiyo inampa uwezo Mdhibiti na Msimamizi wa Hifadhi ya Jamii, kuboresha na kusimamia suala zima la mafao ya Mifuko. Sheria mpya inaelekeza Mifuko yote kurekebisha Sheria zake ili ziendane na Sheria ya Usimamizi na Udhibiti wa Hifadhi ya Jamii.
Details
-
File Typepdf
-
Upload Time-
-
Content LanguagesEnglish
-
Upload UserAnonymous/Not logged-in
-
File Pages213 Page
-
File Size-