Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _______________ MAJADILIANO YA BUNGE _______________ MKUTANO WA KUMI Kikao cha Tisa – Tarehe 8 Februari, 2013 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Mwenyekiti (Mhe. Jenista J. Mhagama) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA FEDHA: Muhtasari wa Tamko la Sera ya Fedha, Mapitio ya Nusu Mwaka Februari, 2013 (Monetary Policy Statement – The Mid Year Review February, 2013). Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa ruhusa yako kabla sijawasilisha mezani taarifa niliyo nayo, naomba nitoe salaam za rambirambi na pole kwa waumini wote wa Kanisala Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Kati pamoja na familia ya Baba Askofu Thomas Laizer, kwa kifo kilichotokea jana cha Askofu wa Dayosisi hiyo. Tunamwomba Mwenyezi Mungu ailaze Roho yake mahali pema peponi. Amina. Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya salaam hizo, sasa naomba kwa niaba ya Waziri wa Nyumba na Maendeleo ya Makazi kuwasilisha mezani. Taarifa ya Mwaka na Hesabu zilizokaguliwa za Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa Mwaka ulioishia tarehe 30 Juni, 2011 (The Annual Report and Audited Accounts of the National Housing Corporation (NHC) Year ended 30th June, 2011). Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Naibu Waziri na tumepokea kwa masikitiko taarifa ya kifo hicho cha Askofu. Naomba sasa nimwite Mheshimiwa Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, nimemwona Mheshimiwa Naibu Waziri, tafadhali! NAIBU WAZIRI WA ELIMU NA MAFUNZO YA UFUNDI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, naomba kuwasilisha mezani. Taarifa ya Mwaka na Hesabu zilizokaguliwa za Mamlaka ya Elimu Tanzania kwa Mwaka 2010/2011 (The Annual Report and Audited Accounts of Tanzania Education Authority for the Year 2010/2011). Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha! MASWALI NA MAJIBU Na. 107 Biashara ya Dawa za Kulevya MHE. KIDAWA HAMID SALEH aliuliza:- UIimwengu mzima pamoja na Tanzania umekumbwa na janga kubwa la usafirishaji na utumiaji wa dawa za kulevya. (a) Je, ni nchi zipi zinazoongoza kwa kufanya biashara hii mbaya? (b) Je, ni wanawake wangapi wa Kitanzania wamekamatwa katika nchi mbalimbali na hapa nchini kwa kufanya biashara hiyo? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, URATIBU NA BUNGE alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Kidawa Hamid Saleh, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Mwenyekiti, dawa za kulevya zinazozalishwa na kutumiwa kwa wingi duniani ni Bangi ikifuatiwa na Heroin na Cocaine. Nchi zinazoongoza kwa kufanya biashara ya dawa hizi ni kama ifuatavyo:- - Bangi – Marekani; - Heroine – Afghanistan; na - Cocaine - Brazil. (b) Mheshimiwa Mwenyekiti, kati ya mwaka 2010 hadi 2012 jumla ya wanawake wa Kitanzania 17 walikamatwa wakijihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya. Kati yao wanawake 14 walikamatwa hapa nchini na watatu walikamatwa Brazil. MHE. KIDAWA HAMID SALEH: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Nina maswali mawili madogo ya nyongeza. (i) Kwa kuwa, katika Bunge la Bajeti lililopita tulielezwa kuwa kuna mkakati wa pamoja wa nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki za kupambana na tatizo hili. Je, ni nini mafanikio ya utekelezaji wa mkakati huo? (ii) Naomba Serikali ikawaeleza Watanzania ni nchi zipi ambazo zimeweka adhabu ya kifo katika nchi zao wakati wanapowakamata wahalifu wa aina hiii? Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, URATIBU NA BUNGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu maswali mawili ya Mheshimiwa Kidawa Hamid Saleh, Mbunge wa Viti Maalum, ya nyongeza mawili kama ifuatavyo:- Wakati wa Bajeti tulisisitiza tukasema kwamba Serikali imeunda kikosi maalum yaani Task Force ndani ya nchi ambacho kinajumuisha idara mbalimbali za Ulinzi na Usalama ambazo ndiyo zimeweka nguvu mpya katika udhibiti wa dawa za kulevya na ndiyo maana utakuta baada ya kuweka kikosi hicho ukamataji umekuwa wa nguvu sana na umekuwa mkubwa sana ukilinganisha na miaka ya nyuma. Kwa mfano, mwaka 2011 kiasi cha Bangi kilichokamatwa ni tani 17,000 na mwaka 2012 kilo 48,000 ukilinganisha na miaka ya nyuma kama mwaka 2010 ambapo ilikuwa 4,000 na hii ni kwa sababu ya ushirikiano uliowekwa pamoja na kikosi hiki maalum cha Task Force. Hata Heroine mwaka 2011 baadaya kuanzisha kikosi hiki cha kupambana na madawa ya kulevya kinaunganisha nguvu kubwa, kilo 2,655 zilikamatwa mwaka 2011 ukilinganisha na miaka ya nyuma kama mwaka 2008 ambapo kilo tatu tu zilikamatwa wakati kila idara ikifanya kivyake. Kwa hiyo, hapa nilichosema ni kwamba nguvu kubwa imewekwa ndani ya nchi kwa ushirikiano mkubwa wa pamoja ambao Mheshimiwa Rais aliagiza kwa kuundwa kikosi maalum ambacho kitakuwa na washiriki katika vikosi vyote na sehemu zote za ulinzi na usalama. Lakini kama ulivyosema tuna ushirikiano wa pamoja wa East Africa ambao unatumika katika kupashana habari na kuangalia biashara hii inavyofanywa hasa sehemu za mipaka ambao umeleta mafanikio katika siku hizi za karibuni. Kuhusu swali la pili la kwamba ni nchi gani inatoa adhabu ya kifo. Naomba niseme kwa sasa jibu hilo sina lakini najua zipo nchi kama China, nchi hiyo jambo kama hili ni moja kwa moja unakwenda. Hiyo nina uhakika nayo! Lakini vile vile na baadhi ya nchi za Kiarabu kama Saudi Arabia. Sasa ukitaka niorodheshe zaidi ya hizo nipe muda, lakini najua angalau nchi hizo zinatoa adhabu ya kifo. MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, tunaendelea na swali linalofuata sijaona tena mtu aliyesimama. Kwa hiyo, tutaendelea na swali linalofuata ingawa nilikuwa nimemwona Mheshimiwa Richard Ndassa, sasa sioni kama anasimama tena. Mheshimiwa Richard Ndassa, utaratibu ni kwamba lazima usimame kwa mujibu wa Kanuni na jicho la Spika likuone, lakini ukikaa hawezi kujua kama unataka kuzungumza. MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa jicho lako kuniona. Naomba nimwulize Mheshimiwa Waziri kwamba mbali na Mkoa wa Iringa unaojulikana kwa ulimaji wa Bangi ambao wanasema kwamba wao ni mboga kwao, ni mkoa gani mwingine unaoongoza kwa kulima Bangi? (Kicheko) MWENYEKITI: Ahsante sana, lakini sijui umeuliza swali hilo kwa sababu wewe unatoka Mkoa wa Iringa, lakini tunaomba Waziri ajibu! WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, SERA, URATIBU NA BUNGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kumjibu Mheshimiwa Richard Ndassa swali lake la nyongeza kama ifuatavyo:- Sijui kama ana mfano wa watu wanaofanana na Bangi watu wa Iringa huyu, lakini Iringa siyo Mkoa unaoongoza kwa kulima Bangi katika nchi hii. Mkoa wa Iringa siyo unaoongoza, Mkoa unaoongoza ni Mkoa wa Mara. Kwa hiyo, huo ndiyo Mkoa unaoongoza na hata ukiniambia nitoe takwimu hapa za Bangi tuliyoiteketekeza na kuikamata kwa kiasi kikubwa ni Mkoa huo wanaotoka akina Mheshimiwa Vincent Nyerere yaani Mkoa wa Mara. (Makofi/Kicheko) MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri, nadhani tutahitaji kujua hiyo taarifa rasmi ya hiyo mikoa inayoongoza ili tujiridhishe vizuri ndani ya Bunge. Waheshimiwa Wabunge, tunaendelea na swali linalofuata na linakwenda Ofisi ya Waziri Mkuu na litaulizwa na Mheshimiwa Amina Abdulla Amour, Mbunge wa Viti Maalum. Na. 108 Utegemezi wa Wawekezaji Kutoka Nje MHE. AMINA ABDULLA AMOUR aliuliza:- Dhana ya kutegemea Wawekezaji kutoka Nje ni dhana potofu:- (a) Je, Serikali inasemaje kuhusu dhana hiyo? (b) Je, Serikali itaacha lini kutegemea Wawekezaji kutoka nje? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU, UWEKEZAJI NA UWEZESHAJI alijibu:- Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Amina Abdulla Amour, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kwa pamoja kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Mwenyekiti, dhana ya kutegemea wawekezaji kutoka nje siyo dhana potofu. Hii ni kutokana na ukweli kwamba mafanikio ya kiuchumi ya nchi nyingi zilizoendelea na zinazoendelea duniani yanatokana na jitihada za makusudi za kuhamasisha na kuvutia uwekezaji kutoka nje ya nchi hizo. Lengo la kuvutia uwekezaji kutoka nje ni kupata manufaa yatokanayo na uwekezaji huo ikiwa ni pamoja na upatikanaji wa mitaji, ujuzi na teknolojia mpya na ya kisasa, kuongeza fursa za ajira, fursa za masoko nje ya nchi kwa bidhaa na huduma zinazozalishwa nchini, idadi ya watalii kutoka nje, mapato ya fedha za kigeni, mapato ya Serikali kutokana na makusanyo ya kodi na kuongeza kasi ya kukua kwa uchumi wa nchi. Suala la msingi ni kuhakikisha kwamba, kama nchi tunapata manufaa yanayotarajiwa kutokana na uwekezaji kutoka nje. Hata hivyo, uwekezaji kutoka nje hautazuia wala kuondoa umuhimu na faida za uwekezaji wa ndani. Tunahitaji kuongeza kiwango cha mitaji kutoka nje ili kujenga uwezo wa wananchi wetu wa kumiliki na kuendesha miradi na uchumi wao. (b) Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itaendelea kuweka mazingira wezeshi ya kufanya biashara na kuwekeza nchini ili kuvutia uwekezaji wa ndani na kutoka nje ya nchi. Hii ni kutokana na ukweli kwamba kiwango cha kuweka akiba kama sehemu ya Pato la Taifa hapa Tanzania ni cha chini sana na hakiwezi kukidhi mahitaji yetu ya uwekezaji. Pia uwezo wetu wa kukopa mitaji ni mdogo, hivyo, tunayo sababuya msingi ya kuvutia mitaji kutoka nje. Serikali itaendelea kuhamasisha na kuvutia uwekezaji kutoka nje na ndani ili kujenga uchumi wenye misingi imara na endelevu ambayo itawezesha Tanzania kuwa nchi ya uchumi wa kati kama dira yetu ya taifa ya 2025 inavyotuelekeza. (Makofi) MHE. AMINA ABDULLA AMOUR:
Details
-
File Typepdf
-
Upload Time-
-
Content LanguagesEnglish
-
Upload UserAnonymous/Not logged-in
-
File Pages196 Page
-
File Size-