NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ___________ MAJADILIANO YA BUNGE ___________ MKUTANO WA TATU Kikao cha Saba – Tarehe 28 Aprili, 2016 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Job Y. Ndugai) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tukae. Waheshimiwa Wabunge, leo ni Kikao cha Saba cha Mkutano wetu wa Tatu. Napenda kuanza kwa kumshukuru sana Naibu Spika, Mheshimiwa Dkt. Tulia kwa kazi nzuri sana ambayo amekuwa akifanya hapa lakini pia Mwenyekiti Mheshimiwa Andrew Chenge na Mheshimiwa Najma Giga. Katibu. (Makofi) NDG. JOHN JOEL – KATIBU MEZANI: MASWALI KWA WAZIRI MKUU SPIKA: Mheshimiwa Waziri Mkuu, tunakukaribisha kwenye podium. Simwoni Kiongozi wa Upinzani Bungeni, kwa hiyo, swali la kwanza linaulizwa na Mheshimiwa Rashid Abdallah Shangazi, Mbunge wa Jimbo la Mlalo, uliza kwa kifupi iwezekanavyo. MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa kunipa nafasi. Katika Serikali ya Awamu… (Hapa microphone ilikuwa inakata sauti) SPIKA: Naona chombo hicho kina matatizo, ungewahi kingine cha karibu kwa haraka haraka. MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika… (Hapa microphone ilikuwa inakata sauti) 1 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) SPIKA: Jamani majirani jaribuni kuwasha huku mbele ili aje mbele huku. Zima hiyo. Sogea huku mbele kabisa, utumie microphone yoyote ile, sogea mbele siyo mstari huo, hama mstari huo, sogea mbele. MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Nne… (Hapa microphone ilikuwa inakata sauti) SPIKA: Kama haziongei zote itabidi tutumie hii ya Upinzani, wote tuje tuulizie hapa. Naomba uje utumie hii ya Upinzani hapa. (Makofi) MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika… (Hapa microphone ilikuwa inakata sauti) SPIKA: Hapana! Njoo tumia microphone hii hapa mbele tuokoe muda. (Makofi) MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, Serikali ya Awamu ya Nne iliendesha zoezi la Operesheni Tokomeza ambayo ilifanyika karibia nchi nzima. Hata hivyo, katika Wilaya ya Lushoto wakati wanaendesha zoezi hili walichukua silaha za wananchi ambao hawakukutwa na matatizo ya ujangili. Mpaka sasa hivi silaha hizo zinaendelea kushikiliwa katika Kituo cha Polisi cha Wilaya ya Same pamoja na Mkoa wa Kilimanjaro kwa ujumla. Je, ni lini wananchi hawa watarudishiwa silaha zao ili ziweze kuwasaidia katika kufukuza wanyama wakali? Ahsante. SPIKA: Kama utauliza la nyongeza usiwe mbali, Mheshimiwa Waziri Mkuu majibu. WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, nashukuru kwa swali hili la kwanza lililoulizwa na Mheshimiwa Shangazi, Mbunge wa Mlalo na naomba nilijibu kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, kwanza nikiri kwamba Serikali iliendesha zoezi la msako kwa wanaotumia silaha maarufu kama Operesheni Tokomeza na katika msako ule tulifanikiwa kukusanya silaha nyingi ambazo nyingine tulibaini zilikuwa hazimilikiwi kwa utaratibu kwa maana kwamba hazina vibali. Mheshimiwa Spika, nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge na wananchi wote ambao walikumbwa na tatizo hilo la kuchukuliwa silaha zao kwamba baada ya zoezi la uhakiki wa silaha hizo kukamilika linalofanywa na Jeshi la Polisi ili kujua uhalali wa umiliki wao na hata kama umiliki ulikuwa halali kujiridhisha pia kama hazikutumika kwa namna tofauti na matarajio ndipo sasa zitarudishwa kwa wamiliki kwa sababu wanamiliki kihalali na ni mali zao, kwa hiyo, watarudishiwa. 2 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Spika, nawakumbusha Wizara ya Maliasili na Utalii pamoja na mamlaka iliyohusika kukusanya silaha hizo wakamilishe haraka mchakato huo ili wananchi waweze kurudishiwa silaha zao ambazo wanamiliki kihalali, waendelee kuzitumia kihalali. (Makofi) SPIKA: Mheshimiwa Shangazi kama una swali la nyongeza wahi tena hapa hapa. MHE. RASHID A. SHANGAZI: Mheshimiwa Spika, nashukuru. Nina swali moja la nyongeza kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu. Pamoja na majibu yake mazuri lakini wananchi hawa ambao walikuwa wanazitumia silaha hizo kwa ajili ya kufukuza wanyama wakali wanashindwa kupata mavuno vile ambavyo wanastahili. Je, haoni kwamba ni muhimu zoezi hili likafanyika kwa haraka zaidi? SPIKA: Majibu Mheshimiwa Waziri Mkuu. Ahsante Mheshimiwa Abdallah Shangazi. WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba nijibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Shangazi kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, kama ambavyo nimesema liko tatizo la umiliki wa silaha nchini na kuwa kuna idadi kubwa ya wananchi wanaomiliki silaha isivyo halali. Ni kweli kwamba wananchi wale wanapata shida na wanyama kuharibu mazao yao, kwa hiyo, hawana uhakika wa kuvuna inavyostahili kwa sababu wanyama wanakula mazao hayo na silaha zile zilikuwa zinatumika kufukuza wanyama wale. Mheshimiwa Spika, hata hivyo, lazima Serikali ijiridhishe kama umiliki ule wa silaha ni halali na kama ni halali haikutumika kwenye matukio mengine? Kwa sababu sasa hivi kumetokea matukio mengi ya ujambazi wa kutumia silaha za moto na silaha hizi nyingine zinamilikiwa na watu kihalali, kwa hiyo, lazima tufanye utambuzi wa silaha hizi namna zinavyotumika. Tunawahakikishia tu wamiliki kwamba zoezi hili likikamilika, tutawarudishia silaha zao. Jukumu letu sasa ni kuziharakisha mamlaka husika zikamilishe zoezi hilo ili silaha zirudi kwa wamiliki halali. SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Waziri Mkuu. Tunaendelea na muuliza swali wa pili kwa siku ya leo, Mheshimiwa Mwita Mwikabe Waitara, Mbunge wa Jimbo la Ukonga, CHADEMA. MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi. Kwa niaba ya watu wa Ukonga, naomba nimtwange swali Mheshimiwa Waziri Mkuu. 3 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Spika, sasa hivi mvua zinaendelea kunyesha na kuna mafuriko karibu kila mahali ikiwepo na Mkoa wa Dar es Salaam na hasa Jimbo la Ukonga. Mheshimiwa Waziri Mkuu anaonaje akitoa maelekezo ya jumla kwa nchi nzima kwamba barabara za changarawe ambazo zinajengwa zipunguzwe ili zijengwe za lami hata kama ni lami nyepesi lakini kuwe na mitaro na karavati ili kupunguza mafuriko ambayo yanatokana na mvua kidogo kunyesha na maji kutapakaa sehemu zote? SPIKA: Sijui kama nimekupata vizuri, unaweza ukarudia swali lako vizuri? MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, naomba nirudie. Nimesema sasa hivi mvua zinaendelea kunyesha na kuna mafuriko kila kona ikiwepo Mkoa wa Dar es Salaam na hasa Jimbo la Ukonga. Sababu ya mafuriko haya, pamoja na kwamba kuna mabonde lakini barabara ni finyu sana, mitaro na makalavati hayapo, kwa hiyo, mvua ikinyesha maji yanatuama barabarani. Ni kwa nini Waziri Mkuu asitoe maelekezo kwamba kwa mtu yeyote ambaye anapewa ukandarasi wa kujenga barabara kwenye kiwango cha changarawe ahakikishe anaweka makaravati na mitaro ili mvua ikinyesha maji yaweze kutiririka kwenda kwenye sehemu yake ya kawaida? SPIKA: Ahsante sana kwa swali lako, Mheshimiwa Waziri Mkuu majibu. WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Waitara, Mbunge wa Ukonga, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, sehemu kubwa ya swali lake ni ushauri hasa kwa wataalam wetu wa ujenzi na miundombinu ya barabara na ushauri wake unatokana na uwepo wa mvua nyingi ambazo pia zinaendelea kwa sasa karibu nchi nzima. Sasa tunao watu wa mabondeni lakini pia hata wa maeneo ya juu kutokana na wingi wa maji yanaharibu na barabara. Mheshimiwa Mbunge ameomba tusisitize wataalam wetu kujenga mifereji kwenye barabara zote, kuweka madaraja madogo na makubwa kwa lengo la kufanya maji hayo yasipite juu. Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba ushauri huu tumeupokea na tutaendelea kusisitiza wataalam wetu kujenga mifereji mikubwa ya kupitisha maji mengi kwa wakati lakini pia madaraja pale ambako kuna dalili ya kupitisha maji. Kama ambavyo tangazo la watabiri wetu wa hali ya hewa walivyoeleza kwamba bado mvua nyingi zitakuja, pamoja na miundombinu iliyoko sasa lakini sehemu kubwa ya tahadhari ni wale ambao wako maeneo ya chini kwa maana ya mabondeni sasa waweze kuondoka wakae maeneo salama halafu baadaye tuweze kutekeleza ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na wale wengine sasa waweze 4 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) kuwa salama ili sasa tuweze kuendelea vizuri. Ushauri wake tumeuchukua. (Makofi) SPIKA: Ushauri wako umechukuliwa. Mheshimiwa Waitara. MHE. MWITA M. WAITARA: Mheshimiwa Spika, kwanza, namshukuru Waziri Mkuu kwa niaba ya Serikali kwa kukubali kupokea ushauri huo muhimu, lakini niulize swali dogo. Mheshimiwa Spika, kwa sababu maeneo ambayo yameathirika zaidi Dar es Salaam ni pamoja na Jimbo la Ukonga kama nilivyosema, barabara ya kutoka Banana – Kitunda – Kivule - Msongola hivi sasa ninapozungumza mawasiliano yamekatika. Barabara hii mwaka juzi ilitengewa shilingi milioni 537 na ilikuwa inaendelea kujengwa, lakini hivi ninavyozungumza sasa hivi hapa imekatika. Mheshimiwa Waziri Mkuu anaonaje akitoa maelekezo kwa hali ya dharura ili wahusika wachukue hatua ili wananchi wale waweze kupata namna ya kupita kuja mjini kupata huduma za kawaida za kijamii? Ahsante. SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, naomba msome vizuri zile kanuni zetu za maswali. Maswali ambayo yanauliza opinion ya Mheshimiwa Waziri Mkuu kwa kweli hayakubaliki, unaonaje, tunataka swali. Kwa hiyo, tunaendelea na swali la Mheshimiwa Zuberi Mohamed Kuchauka, Mbunge wa CUF. (Makofi) MHE. ZUBERI M. KUCHAUKA: Mheshimiwa Spika, ahsante sana kwa kuniona na kwa niaba ya wana Liwale na wananchi wote kwa ujumla, naomba niulize swali kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, Rais wa Awamu ya Tano wakati ule akihudumu kama Waziri wa Miundombinu aliwahi kusema kwenye Bunge hili Tukufu kwamba Sera yetu ya Kitaifa sasa hivi ni kuunganisha mikoa yetu yote ya Bara na Visiwani kwa barabara za lami. Ninachotaka kujua mpaka sasa hivi Serikali imefikia kiwango gani katika kutekeleza sera hiyo
Details
-
File Typepdf
-
Upload Time-
-
Content LanguagesEnglish
-
Upload UserAnonymous/Not logged-in
-
File Pages148 Page
-
File Size-