Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA ______________ MAJADILIANO YA BUNGE _____________ MKUTANO WA NNE Kikao cha Arobaini na Sita – Tarehe 13Agosti, 2011 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) DUA Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHA MEZANI Hati zifuatazo ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Randama za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa mwaka wa fedha 2011/2012. HOJA ZA SERIKALI Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2011/2012 - Wizara ya Nishati na Madini (Majadiliano yanaendelea) MICHANGO KWA MAANDISHI MHE. KISYERI W. CHAMBIRI: Mheshimiwa Spika, la kwanza, ni zaidi ya miaka kumi, umeme umepita katika maeneo ya Maweni, Majengo, Mukuyuni A, Mukuyuni B, Ari Halaa, Singu, Signo. Umeme huo ni wa msongo wa KV 33. Hakuna juhudi zozote zimefanywa kuwapatia wananchi umeme katika maeneo hayo. Nataka kufahamu lini wananchi wa maeneo hayo watapatiwa umeme? Mheshimiwa Spika, pili, katika bajeti ya TANESCO ya mwaka huu, fedha zimetengwa kupeleka umeme mtaa wa Muruki, Babati Mjini. Meneja wa Mkoa amekataa kupeleka umeme Muruki kwa kisingizio kuwa hakuna njia. Halmashauri ya Mji wameandika barua TANESCO na kuthibitisha njia ipo. Lini wananchi wa Muruki watapata umeme? Mheshimiwa Spika, tatu, ingawa tayari wameleta nguzo kwa ajili ya umeme Mamagha, Banga, Himiti, Haraa, hoja sasa ni muda mrefu sana, lini umeme utawekwa katika maeneo hayo? Mheshimiwa Spika, nne, muda mrefu sasa tumeomba umeme upelekwe Vijiji vya Imbilili, Mtuka, Malangi na Kiongozi. Lini maeneo hayo yatawekwa katika mpango na kupelekewa umeme? Mheshimiwa Spika, pamoja na hoja hizo hapo juu, nimeomba Meneja wa Mkoa atayarishe makisio ya maeneo hayo kupata umeme. Naomba ahimizwe kufanya kazi hiyo. MHE. SALEH A. PAMBA: Mheshimiwa Spika, napenda kumpongeza Waziri kwa hotuba nzuri yenye matumaini “kimipango” katika kutatua matatizo ya umeme. Miradi yote ya umeme aliyoitaja katika hotuba yake itachukua muda. Katika miaka mitatu ijayo, matatizo haya yatapungua. Kinachotakiwa kufanyika ni kuwa na timu ya ufuatiliaji wa miradi hiyo. Bajeti hii 1 ikipita, tunaanza mchakato wa bajeti mpya ya 2012/2013, inabidi Wizara ijipange katika kutekeleza miradi yake ambayo ni mingi na ya thamani kubwa. Mheshimiwa Spika, umeme wa maji, ili kuweza kutoa nafuu ya bei ya umeme, ni vema tukaendelea kutumia umeme wa maji ili ku-balance tariff kwa umeme wa gas na thermal lakini hili linahitaji TANESCO kusaidia katika kutunza vyanzo vya maji. Maji ni malighafi muhimu kwa TANESCO. Mheshimiwa Spika, kuhusu umeme vijijini. Asilimia 80 ya Watanzania wanaishi Vijijni ambapo uzalishaji unafanyika. Fedha zinazotengwa katika Rural Energy ni ndogo na kwa bajeti hiyo halitaweza kuleta umeme Vijijini kwa haraka. Katika bajeti ya mwakani, ni lazima REA ipatiwe bajeti ya kutosha ili kumaliza matatizo ya umeme Vijijini hasa kwa miradi ambayo mwaka huu haikutengewa fedha kama miradi ya Mkwaja – Mkalamo ya Wilaya Pangani. Hii itapunguza manung’uniko ya Waheshimiwa Wabunge ambapo mwaka huu hatukupata miradi hata mmoja. Mheshimiwa Spika, madini, hapa kuna tatizo hasa katika kuhakikisha kwamba wananchi wanafaidika na madini yao. Ni vyema kuhakikisha kwamba makampuni makubwa ya madini yanatekeleza corporate social responsibility kwa wananchi kama maji, shule na zahanati. Mheshimiwa Spika, Sheria, kwa vile nchi yetu imepata madini ya uranium, ni vyema kukawepo na Sheria kuhusu uchimbaji wa uranium ambapo ni madini mapya yanayotawaliwa Kimataifa. Ni vizuri tukajifunza toka nchi kama Namibia na Malawi ambao tayari wana sheria nzuri tu kuhusu uranium. Sheria hiyo iletwe haraka Bungeni. Mheshimiwa Spika, mafuta, ni lazima Sheria ya Mafuta ikaletwa hapa Bungeni. Nchi ya Saud Arabia na za Gulf zina Sheria Maalum ya Mafuta, si vizuri suala hili likabakia katika Sheria Mpya ya Madini. Sasa ni wakati wa kuwa na Sheria specific tusiwaachie TPDC peke kusimamia Sheria hii. MHE. FATUMA A. MIKIDADI: Mheshimiwa Spika, kwanza naunga mkono hoja kwa asilimia 100/100. Mheshimiwa Spika, nianze na Madini ya Chumvi. Madini ya Chumvi huchimbwa Mikoa 10 nchini Tanzania ambayo ni Lindi, Mtwara, Tanga, Pwani, Dodoma, Shinyanga, Singida, Mbeya, Dar es Salaam, Zanzibar na Ukanda wa Pwani. Chumvi ni madini hafifu sana katika madini yote nchini, hupata matatizo sana. Kwa hiyo, naiomba Serikali iangalie kwa jicho la huruma, wasiitoze tozo kama madini ya dhahabu au almasi. Madini ya chumvi yanakumbwa na matatizo 12 yafuatayo:- (1) Haina soko na ikipata soko haina bei, ni shilingi 1,200/= mpaka shilingi 1,500/= kwa kilo 50. (2) Serikali iliongeza mzigo mzito kwa wakulima kwa kuwataka wakulima hao waweke madini joto kwa faida ya wananchi. Serikali ilitumia madini ya chumvi kuweka Iodine (Madini Joto) ili wananchi wengi watumie Iodine kupitia chumvi baada ya kuona kuwa wanadamu wengi Tanzania wana upungufu wa Iodine mwilini, kuweka Madini Joto katika chumvi ni mzigo sana kwa mkulima. Tunaomba madini haya na mabomba yake yatolewe bure. Chumvi inaweza kuliwa bila madini joto, hili liangaliwe upya. Serikali itoe Madini Joto kwa wakulima wa chumvi. (3) Mzalishaji wa chumvi anatakiwa kodi ya Wizara ya Madini na Nishati kila mwaka. Anatakiwa alipe ushuru wa Maliasili kwa ajili ya mikoko ya shilingi 80,000/= kila mwaka kwa hekta 2.5 hata kama hatumii eneo lote alilopewa. (4) Anatakiwa alipe mrahaba wa asilimia tatu (3%) ya bei ya chumvi atakayouza. (5) Anatakiwa alipe ushuru wa shilingi 50,000/= kwa kila pakti ya kilo 50. 2 (6) Mkulima wa chumvi anatakiwa aweke Madini Joto ambayo huuzwa shilingi 30,000/= kwa kilo na huweka pakti 320 tu. Gharama hii huibeba mkulima kwa niaba ya wananchi wanaokula chumvi. (7) Kila mwaka anatakiwa afanye usajili kwa shilingi 200,000. (8) Anatakiwa awe na zana za kuchimbia madini. (9) Haijulikani ni wa Wizara ya Kilimo, Afya, Madini au Maliasili, wote wanadai kodi. Chambueni upya yupi ni yupi. Mheshimiwa Spika, katika suala la chumvi, tunaomba yafuatayo yatekelezwe:- (i) Serikali igawe bure Madini Joto kwa wakulima wa chumvi kwani zoezi la kuweka Madini Joto ni zoezi la Serikali baada ya kuona kuwa watu wengi hawana Madini Joto katika miili yao. Chumvi unaweza kula bila Madini Joto, hivyo zoezi la kula Madini Joto litapungua ila watu wanaweza kuumwa magonjwa 100 kwa kutokula madini joto. Kwa hiyo Madini Joto ni muhimu. (ii) Serikali iondoe baadhi ya tozo ya kila mwaka angalu itoze tozo mara moja tu. Angalieni suala la tozo. (iii) Wapewe pembejeo bure. (iv) Kuwe na Bodi ya Chumvi. (v) Tusaidiwe Kiwanda cha Kusaga Chumvi Lindi. Mheshimiwa Spika, kuna tatizo la soko ya zao hili la chumvi kwa sababu mwekezaji wa aliyenunua Kiwanda cha Karatasi Mgogolo ananunua chumvi kutoka nje badala ya kununua chumvi Tanzania. Zamani chumvi yote ilikuwa ikinunuliwa na Kiwanda cha Mgololo, sasa chumvi yote ipo tu haina soko. Chumvi za kula zinatoka Mombasa, tunataka aliyewekeza Mgololo anunue chumvi Tanzania pia tunataka soko la chumvi. Mheshimiwa Spika, madini ya gesi. Tutaka Vijiji vinavyopitisha bomba la gesi vipewe umeme. Vijiji hivyo ni Miteja, Njenga, Mkwanyule, Mpara, Nyamwage na Kilwa Kisiwani. Mheshimiwa Spika, madini. Katika Wilaya 93 zilizotajwa kuwa zina madini, Wilaya ya Ruangwa haikutajwa kama ina madini hivyo kutotambuliwa na Serikali. Kwa taarifa Ruangwa kuna madini ya Green Garnet, Green Tourmalines, Dhahabu, Blue Safaya, Marakati na rangi za kupaka nyumba. Kwa hiyo, Ruangwa pia wasaidiwe nyenzo za kufanyia, wapimiwe viwanja, wafanyiwe upembuzi na pia watambuliwe na Serikali. Mheshimiwa Spika, mwisho, naunga mkono hoja kwa 100/100. MHE. HAROUB MUHAMMED SHAMIS: Mheshimiwa Spika, awali ya yote, nashukuru Mwenyezi Mungu (S.W) kwa kunijalia Afya njema na kunipa uwezo wa kuchangia machache katika Wizara hii kwa maendeleo ya nchi yetu na watu wake. Mheshimiwa Spika, kumbukumbu sahihi zinaonyesha mgao wa umeme umeanza muda mrefu sana nchini toka mwaka 1992 mpaka sasa ni takriban miaka 20. Ni wazi kuwa Serikali haiko makini na haina dhamira ya kweli ya kutatua tatizo la nishati kwa ujumla wake. Mahitaji ya umeme nchini ni 1200 MW na vyanzo vyote 10 vinavyotegemewa kutoa umeme vinazalisha 818 MW tu na hata hizo 818 hazipatikani! Ni dhahiri kabisa Serikali haina dhamira ya dhati kumaliza tatizo la nishati ya umeme kwani miaka 20 ya tatizo hili ni mingi sana. Serikali haiko makini hata kidogo! Badala ya kuchukua hatua madhubuti kumaliza tatizo, Serikali inaingiza siasa na kulifanyia mzaha tatizo pale Waziri anapotoa kauli kuwa “umeme utakuwa historia kabla ya 2010”. Waziri au Serikali inatoa kauli hiyo kimzaha mzaha bila ya kusikiliza ushauri wa wataalam, kutokuwa na sera na nia njema ya kutatua tatizo na kutopanga bajeti ya kutosha/kutafuta mwekezaji makini. Badala yake 3 Taifa linabebeshwa mzigo wa umaskini zaidi kwa watu wake kutokana na mkataba mibovu ya uwekezaji katika nishati ya umeme kama ya DOWANS. Mheshimiwa Spika, pamoja na tafiti mbalimbali kuonyesha kuwa nchi yetu ina vyanzo vingi vya umeme vikiwemo vya maji kama Ruhudji -358 MW, Ruwakali - 222 MW, Stieglers Gorge- 1200 MW, Masigira - 118 MW, Mpanga - 114 MW, Kakumo-58 MW, Malagarasi-20 MW. Julmla ni 2085 MW. Mheshimiwa Spika, vyanzo vya umeme wa gesi. Mnazi Bay - 300 MW na Kinyerezi- 240 MW. Jumla 540 MW. Mheshimiwa Spika, vyanzo vya umeme wa makaa ya mawe. Mchuchuma - 600 MW na Kiwira - 400 MW. Jumla 1000 MW. Mheshimiwa Spika, pia kuna vyanzo vingi vya kuzalisha umeme wa upepo vikiwemo vya Singida na Makumbuko. Mheshimiwa Spika, Serikali haiko makini na haina dhamira, nia wala adhma ya dhati ya kutatua kero na adha ya nishati ya umeme ili kuwapunguzia umaskini wananchi wetu na kulifanya Taifa lisonge mbele kimaendeleo. Mheshimiwa Spika, kuhusu madini, wakati sasa umefika Serikali kubadilika, mikataba ya madini irekebishwe ili wananchi wanufaike na rasilimali zao walizojaliwa na Mwenyezi Mungu anayewapenda sana Watanzania. Majuto ni Mjukuu, tusisubiri kuja kujuta hapo badaye, watoto wetu watatuombea laana kutoka kwa Mwenyezi Mungu ikiwa hatutawatendea haki ya kupata manufaa ya madini yao. Mheshimiwa Spika, uchimbaji wa madini hasa dhahabu hapa nchini ni wa gharama nafuu zaidi ukilinganisha na nchi kama Angola lakini Angola pamoja na kuwa gharama ya uchimbaji ni kubwa, Serikali ya Angola inapata hadi 30% ya dhahabu inayochimbwa huko.
Details
-
File Typepdf
-
Upload Time-
-
Content LanguagesEnglish
-
Upload UserAnonymous/Not logged-in
-
File Pages174 Page
-
File Size-