Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA _________________ MAJADILIANO YA BUNGE _________________ MKUTANO WA NNE Kikao cha Arobaini – Tarehe 4 Agosti, 2011 (Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne S. Makinda) Alisoma Dua HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati ifuatayo iliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA KAZI NA AJIRA: Randama ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Kazi na Ajira kwa Mwaka wa Fedha 2011/2012. SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, kwa mujibu wa Kanuni ya 38, Waziri Mkuu anaweza kuulizwa maswali na Mbunge yeyote ambaye atazingatia masharti kuhusu maswali ya Bunge pamoja na mwongozo uliowekwa na Nyongeza ya 6 ya Kanuni hii. Maswali atakayoulizwa Waziri Mkuu, hayatakuwa na taarifa ya awali kama maswali yenyewe. Kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu kitakuwa ni Siku ya Alhamisi kwa dakika 30, lakini chini ya kifungu kidogo cha (4) kinasema, Waziri Mkuu anaweza kutumia kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu, kutoa taarifa au ufafanuzi kuhusu suala lolote linalohusiana na shughuli za Serikali na lenye maslahi kwa umma, kwa muda usiozidi dakika kumi ikifuatiwa na maswali kwa Wabunge kwa dakika 20 kuhusu taarifa yoyote na maswali mengine ya Serikali. Kwa hiyo, ninamuita Waziri Mkuu. WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Spika, ninaomba nikushukuru sana kwa kunipa fursa hii ili niweze kutoa taarifa fupi kwa mujibu wa Kanuni uliyoieleza sasa hivi. Taarifa hiyo ni matokeo ya mjadala wa Bajeti ya Uchukuzi, ambayo ilikuwa na mambo mengi. Nimeona nitumie fursa hii niweze kutoa ufafanuzi wa mambo yafuatayo:- Awali ya yote, ninapenda kutumia fursa hii kumshukuru sana Mheshimiwa Peter Serukamba, Mwenyekiti wa Kamati ya Miundombinu na Mheshimiwa Mhonga Said Ruhwanya, Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwa Wizara ya Uchukuzi na Waheshimiwa Wabunge wote, waliochangia kwa maandishi na kwa kuzungumza kwenye majadiliano ya Wizara hii ya Uchukuzi yanayoendelea hapa Bungeni. Michango yenu kwa kweli ni mizuri, ninawashukuruni sana kwa ujumla. (Makofi) Mheshimiwa Spika, nimeona nitoe maelezo haya, kwa sababu yaliyojitokeza ni mambo ambayo yameonesha uzito na sisi Serikalini tukaona pengine ni vizuri katika kujaribu kusaidia Bunge lako katika kuendeleza mjadala huu, tuyaweke bayana mambo fulani fulani. Mheshimiwa Spika, kwanza, ninataka kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba, Mheshimiwa Rais aliamua kuunda Wizara mbili kutokana na uzito wa majukumu yaliyokuwa katika Wizara hiyo moja na hii ilitokana kwa sehemu kubwa na mazingatio ya maoni yaliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge, ndani ya Bunge hili kwa nyakati tofauti. Kwa hiyo, uamuzi huo ulilenga kupunguza majukumu mengi yaliyokuwa yamebebwa na Wizara ya Miundombinu kabla ya kutenganishwa na kupata Wizara mbili ikiwemo hii ya Uchukuzi. Lengo la kuundwa kwa Wizara ni kuimarisha utekelezaji wa Miradi ya Sekta ya Uchukuzi ikiwemo ya 1 usafiri, reli, anga, maji pamoja na barabara kwa upande sasa wa Wizara ya Ujenzi na kabla ya kutenganishwa wote mtakumbukwa vipaumbele vilivyowekwa zaidi kwenye ujenzi wa barabara na madaraja. Kwa hiyo, wakati tukiendelea na majadiliano ya Wizara ya Uchukuzi, ninaomba niruhusu nitumie fursa hii kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote, kwa kupitisha makadirio ya Wizara ya Ujenzi, kwa sababu yamewezesha ujenzi wa barabara na madaraja kuendelea kwa kuzingatia ushauri wa Waheshimiwa Wabunge. (Makofi) Mheshimiwa Spika, Sekta ya Uchukuzi inahitaji uwekezaji wa mitaji mikubwa kwenye ujenzi wa reli, bandari na hata viwanja vya ndege. Vilevile uwekezaji kama huo unahitajika kwenye ununuzi na ukarabati wa ndege, injini za treni na mabehewa yake pamoja na mahitaji ya meli. Mahitaji hayo ni makubwa na ambayo Bajeti iliyotengwa haitoshelezi. Wizara hii kama ilivyo kwa Wizara zingine, inakabiliwa na ufinyu wa Bajeti. Hata hivyo, Serikali imekuwa siku zote inafanya kila jitihada kuhakikisha Wizara zinapata fedha za kutosheleza mahitaji. Kutokana na ufinyu wa Bajeti wa Wizara hii, jana, Serikali ililazimika kukutana na kuangalia uwezekano wa kuongeza bajeti ya Wizara ya Uchukuzi kutokana na vyanzo mbalimbali. Kukutana kwa Serikali ilikuwa ni muhimu ili kuweza kujadili michango mingi mizuri iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge ndani ya Bunge hili Tukufu, kwa mtazamo ambao unaweza ukaimarisha mijadala na kwa maana hiyo maslahi kwa Watanzania. (Makofi) Kwa hiyo, baada ya Kamati ya Miundombinu kupitia Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara kuishauri Serikali kuongeza bajeti hiyo kwa shilingi bilioni 95, jambo ambalo tuliliridhia na kulikubali, lakini hatukuweza kufikia kiwango hicho kama ilivyokuwa imeombwa. Kikao cha jana kimewezesha Serikali kufanikiwa kupata fedha hizo ambazo zitatumika kwenye maeneo matatu yafuatayo: Reli ya Kati, Kampuni ya Ndege Tanzania na Usafiri wa Majini yaani Meli katika Maziwa ya Victoria, Tanganyika na Nyasa. Kiasi hicho cha shilingi bilioni 95 ni kiasi ambacho Wizara ilikuwa imeji-commit au imejiahidi mbele ya Kamati kwamba, zikipatikana zitawezesha huduma za msingi katika maeneo hayo matatu kuweza kuendelea bila matatizo makubwa. (Makofi) Serikali inaamini kabisa kwamba, pamoja na nyongeza hiyo, bado bajeti hiyo haikidhi mahitaji yote yaliyopo kwa sasa. Hata hivyo, kwa kuzingatia kwamba, bajeti hii ni ya kwanza kwa Wizara tangu ilipoundwa Novemba, 2010 baada ya Uchaguzi Mkuu na kwa kuwa Sekta hii imepewa kipaumbele katika Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa miaka mitano, Serikali itahakikisha bajeti zijazo zinaipa Sekta hii kipaumbele. (Makofi) Mheshimiwa Spika, suala lingine lililoongelewa kwa hisia kali na Waheshimiwa Wabunge, wakati wa mjadala ni matatizo ya Shirika la Usafiri Dar es Salaam (UDA). Serikali imesikia kilio cha Waheshimiwa Wabunge, na kwa sasa imeshawaagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali, Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai na Taasisi ya Kudhibiti na Kupambana na Rushwa, kuanza uchunguzi mara moja ili kuiwezesha Kamati ya Bunge ya Mheshimiwa Peter Serukamba, iweze kutekeleza jukumu lake ipasavyo katika uchunguzi utakaofuatia. Ninataka kuliarifu Bunge lako kuwa, Serikali itatoa kila aina ya ushirikiano kwa Kamati hii kuhakikisha kwamba, jambo hili linashughulikiwa ipasavyo. (Makofi) Baada ya uchunguzi huo, Serikali itachukua hatua stahiki kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu, kwa wote watakaobainika kuhusika kulihujumu shirika hilo. (Makofi) Mheshimiwa Spika, Waheshimiwa Wabunge pia wamezungumzia suala linalohusu malipo ya pensheni kwa Wastaafu wa TAZARA kwa upande wa Tanzania, wanaodai kiasi cha shilingi bilioni 22. Suala hili liliamuliwa na Baraza la Mawaziri la TAZARA linalijumuisha Mawaziri husika kutoka nchi hizi mbili kwamba, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali kwa upande wa Tanzania na mwenye dhamana kama hiyo kwa upande wa Zambia, wafanye uhakiki wa madai haya kwa pande zote mbili. Wadhibiti hao wamewasilisha taarifa zao Serikalini kwa ajili ya kushughulikiwa. Kwa upande wa Tanzania na tayari Waraka wa Baraza la Mawaziri umeandaliwa na utajadiliwa hivi karibuni na hatua stahiki zitachukuliwa. Kwa hiyo, nilitaka nitumie nafasi hii kuwahakikishia Wafanyakazi wa TAZARA na Watanzania kwa ujumla kwamba, punde uamuzi huo wa Baraza utakapofanyika, hatua zote 2 zinazohusiana na malipo ya pensheni au mafao kwa wastaafu hao zitachukuliwa bila kuchelewa. (Makofi) Serikali imefanya kila linalowezekana ili kupata kiasi cha fedha kilichokuwa kimeombwa na Kamati ya Miundombinu pamoja na Serikali kukubali katika hali ngumu sana ya fedha tuliyonayo kama ilivyojitokeza kwenye majadiliano ya Bajeti ya Serikali katika Wizara mbalimbali zilizotangulia. Ninataka niwahakikishieni kuwa, Serikali ina nia ya dhati ya kuhakikisha Wizara zote zinapata Bajeti ya kutosheleza mahitaji yake. Tukumbuke kuwa mapato yetu bado ni madogo, tutaendelea kufanya kila liwezekanalo kuongeza mapato ya Serikali ili kuondokana na tatizo hili. Vilevile ninazitaka Wizara zote zitumie fedha walizotengewa kwa bajeti zao kwa malengo yaliyokusudiwa. (Makofi) Mheshimiwa Spika, utaratibu wa namna fedha hizi zitakavyowekwa katika bajeti, utatokana na ushauri nitakaokuwa nimepewa na ninadhani utawasilishwa katika nyakati tofauti hapa Bungeni, kwa ajili ya kuhakikisha kwamba imekuwa factored katika Bajeti. Mheshimiwa Spika, ufafanuzi wa masuala mengine yaliyochangiwa na Waheshimiwa Wabunge, utaendelea kutolewa na Waziri mwenye sekta pamoja na Naibu na Mawaziri wengine wanaohusika ili kuweza kuhitimisha hoja iliyo mbele yetu. Mheshimiwa Spika, baada ya kuyasema hayo, kwa muda uliobaki sasa nipo tayari kuendelea kujibu maswali ya Waheshimiwa Wabunge kama ulivyoelekeza. Ninakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii. (Makofi) MASWALI KWA WAZIRI MKUU SPIKA: Kama kawaida yetu, Kiongozi wa Kambi ya Upinzani yupo; Mheshimiwa Kiongozi wa Kambi ya Upinzani. MHE. FREEMAN A. MBOWE: Mheshimiwa Spika, ninakushukuru kwa kunipa nafasi ya kwanza kumwuliza Waziri Mkuu swali. Mheshimiwa Spika, pamoja na kumpongeza Waziri Mkuu, kwa kauli yake ya awali aliyoitoa hapa leo, kufuatia mjadala wa jana wa Bunge, ninapenda sasa kumwuliza swali moja la msingi ambalo linagusa maslahi ya Watanzania walio wengi sana kwa sasa. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa ni zaidi ya mwezi mmoja tangu Waziri wa Fedha aliposoma Bajeti katika Bunge hili la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Bajeti ambayo iliwapa Watanzania wengi matumaini ya kushusha bei ya mafuta ya petrol na diesel, lakini vile vile ilikusudia kupandisha bei ya mafuta ya taa; na kwa kuwa zimetolewa kauli mbalimbali zikiwemo kauli za EWURA, kauli za Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi, kauli ya Wizara ya Nishati na Madini na jana hatimaye EWURA waliweza kutoa bei elekezi ili itekelezwe na wafanyabiashara wanaofanya biashara ya mafuta; na
Details
-
File Typepdf
-
Upload Time-
-
Content LanguagesEnglish
-
Upload UserAnonymous/Not logged-in
-
File Pages155 Page
-
File Size-