NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA __________ MAJADILIANO YA BUNGE ___________ MKUTANO WA KUMI NA TISA Kikao cha Ishirini na Tano – Tarehe 8 Mei, 2020 (Bunge Lilianza Saa Nane Mchana) D U A Naibu Spika (Mhe. Dkt. Tulia Ackson) Alisoma Dua NAIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tukae. Katibu. NDG. LAWRANCE MAKIGI - KATIBU MEZANI: HATI ZA KUWASILISHA MEZANI Hati Zifuatazo Ziliwasilishwa Mezani na:- NAIBU WAZIRI WA NISHATI: Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Nishati kwa mwaka wa fedha 2020/2021. MHE. USSI SALUM PONDEZA AMJADI (K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA KUDUMU YA BUNGE YA NISHATI NA MADINI): Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Nishati na Madini kuhusu utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ya Nishati Fungu 58 kwa mwaka wa fedha 2019/2020 pamoja na Maoni ya Kamati kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha 2020/2021. NAIBU SPIKA: Ahsante sana. Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni wa Wizara ya Nishati. Hayupo. Katibu. 1 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) NDG. LAWRANCE MAKIGI - KATIBU MEZANI MASWALI NA MAJIBU (Maswali yafuatayo yameulizwa na kujibiwa kwa njia ya mtandao) Na. 231 Uhaba wa Walimu – Mkoa wa Tanga MHE. OMARI A. KIGODA aliuliza:- Kutokana na uhaba wa walimu Mkoa wa Tanga umekuwa haufanyi vizuri katika matokeo ya ufaulu wa wanafunzi:- Je, kuna mkakati wowote wa Serikali wa kutatua changamoto hiyo? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Omari Abdallah Kigoda, Mbunge wa Handeni, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, Serikali imeendelea kuajiri Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari nchini ambapo kuanzia mwaka 2017 hadi 2019 jumla ya walimu 420 wameajiriwa na kupangwa katika Mkoa wa Tanga. Walimu 130 walikuwa wa Shule za Msingi na walimu 290 walikuwa wa Shule za Sekondari. Serikali itaendelea kuajiri Walimu wa Shule za Msingi na Sekondari nchini kwa kadri ya upatikanaji wa fedha. Na. 232 Kukamilisha Ujenzi Kituo cha Afya Mtii – Same MHE. NAGHENJWA L. KABOYOKA aliuliza:- 2 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Je, ni lini Serikali itakamilisha ujenzi wa Kituo cha Afya kinachojengwa Kata ya Mtii ambapo hakuna hata zahanati ya Serikali? WAZIRI WA NCHI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MITAA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Naghenjwa Livingstone Kaboyoka, Mbunge wa Same Magharibi, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, wananchi wa Kata ya Mtii kwa kushirikiana na Halmashauri na wadau wa maendeleo wamekamilisha ujenzi wa jengo moja lenye vyumba 14. Serikali inakamilisha taratibu za kuiombea zahanati hiyo ili ianze kutoa huduma. Serikali itaendelea kujenga vituo vya afya na zahanati kadri upatikanaji wa fedha utakavyoruhusu. Na. 233 Kufufua Viwanda Vilivyoko Mkoani Tanga MHE. SONIA J. MAGOGO aliuliza:- Je, Serikali ina mpango gani wa kufufua viwanda vilivyoko Mkoani Tanga ambavyo vilikuwa na tija kubwa sana kwa Taifa? WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA alijibu:- Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Sonia Jumaa Magogo, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, Mkoa wa Tanga ulikuwa na jumla ya viwanda 12 vilivyobinafsishwa wakati wa zoezi la ubinafsishaji vinavyojumuisha viwanda vya mbao, chai, sabuni na katani. 3 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Spika, mkakati wa jumla wa Serikali katika kushughulikia viwanda vilivyobinafsishwa ni kufanya ufuatiliaji na tathmini, kushauri wawekezaji kuhusu maboresho yanayopaswa kufanywa, kurejesha viwanda na kutafutia wawekezaji wengine wenye uwezo wa kuwekeza na kutafuta wawekezaji wapya. Mheshimiwa Spika, katika kutekeleza mkakati huo, Serikali ilifanya tathmini ya utendaji wa viwanda vilivyobinafsishwa ikiwemo viwanda katika Mkoa wa Tanga na kubainisha kuwa kuna jumla ya viwanda 12. Kati ya hivyo, viwanda viwili vinafanya kazi kwa ufanisi; viwanda sita vimerejeshwa Serikalini na viwanda vinne vinafanya kazi kwa kusuasua. Mheshimiwa Spika, katika viwanda sita vilivyorejeshwa Serikalini, Kiwanda cha Chai cha Mponde kuna mwekezaji aliyeonesha nia ya kukifufua. Aidha, Serikali itaendelea kutafuta wawekezaji watakaoweza kuwekeza katika viwanda vingine vilivyorejeshwa Serikalini na kuhamasisha wawekezaji wengine wanaoendesha viwanda vinavyozalisha chini ya uwezo uliosimikwa waongeze uzalishaji. Na. 234 Ujenzi wa Barabara ya Londo – Songea Km 113 MHE. JACQUELINE N. MSONGOZI aliuliza:- Je, ni lini Serikali itaanza ujenzi wa barabara ya Londo - Songea ambayo inaunganisha Mkoa wa Morogoro na Ruvuma yenye urefu wa kilometa 113 ambayo imekuwa ikiongelewa kwa muda mrefu sana na madaraja yalishajengwa na kilichobaki ni kuunganisha barabara hii? 4 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) WAZIRI WA UJENZI, UCHUKUZI NA MAWASILIANO alijibu:- Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Jacqueline Ngonyani Msongozi, Mbunge Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, barabara ya Londo – Songea (Lumecha) yenye urefu wa kilometa 124 ni sehemu ya barabara Kuu ya Kidatu – Ifakara – Malinyi – Kilosa kwa Mpepo – Londo – Lumecha (km 512) inayounganisha Mkoa wa Ruvuma na Morogoro kupitia Wilaya za Kilombero, Ulanga, Malinyi na Namtumbo. Mheshimiwa Spika, ili kutekeleza azma ya kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami, Serikali imefanya na kukamilisha kazi za upembuzi yakinifu na usanifu wa kina wa barabara yote. Mheshimiwa Spika, kazi ya ujenzi kwa kiwango cha lami imeendelea kutekelezwa kwa awamu ambapo ujenzi wa Daraja la Magufuli katika Mto Kilombero lenye urefu wa mita 384 na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 9.142 ulikamilika tarehe 30 Julai, 2017. Aidha, ujenzi wa barabara ya Kidatu – Ifakara (km 66.9) kwa kiwango cha lami unaendelea. Ujenzi wa sehemu iliyobaki ikiwemo Londo – Lumecha (km 124) kwa kiwango cha lami utaendelea kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha. Mheshimiwa Spika, kwa kutambua umuhimu wa sehemu ya barabara kutoka Londo – Songea (km 124) kiuchumi na kijamii, Serikali kupitia Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS) Mkoa wa Ruvuma, inaendelea kuifanyia matengenezo mbalimbali barabara hii kila mwaka ili iweze kupitika majira yote ya mwaka. Katika mwaka wa fedha 2019/2020, barabara hii imetengewa jumla ya Sh.1,068,795 kwa ajili ya matengenezo mbalimbali. 5 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Na. 235 Tatizo la Ardhi Kati ya Hifadhi na Wananchi – Wilaya ya Wanging’ombe MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza: - Je, ni lini Serikali itatatua tatizo la ardhi kati ya Hifadhi ya Mpanga – Kipengele na Vijiji vya Malangali, Wangomiko na Mpanga mpya katika Wilaya ya Wang’ing’ombe Mkoa wa Njombe? WAZIRI WA MALIASILI NA UTALII alijibu: - Mheshimiwa Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema Wiliam Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, Serikali inatambua uwepo wa vijiji vya Malangali, Wangomiko na Mpanga mpya ndani ya Pori la Akiba Mpanga -Kipengele kabla ya kuanzishwa kwake. Moja ya hatua iliyochukuliwa na Serikali katika kukabiliana na changamoto hiyo ni uthamini wa mali za wananchi na ulipaji fidia kwa mujibu wa sheria ili wahame. Mfano, mwaka 2007 wananchi 325 wa vijiji vya Ikovo, Usalimwani na Kigunga vya Wilaya ya Makete walilipwa jumla ya Sh.190,067,151. Mwaka 2012 wananchi 161 wa Kijiji cha Ikovo waliolalamika kupunjwa walilipwa jumla ya Sh.829,841,000. Aidha, mwaka 2018, Serikali ililipa fidia jumla ya Sh.837,071,100 kwa wananchi 308 wa Kitongoji cha Machimbo katika Kijiji cha Madabada, Wilayani Mbarali. Mheshimiwa Spika, ili kuondoa migogoro ya ardhi baina ya vijiji na hifadhi, likiwemo Pori la Akiba Mpanga- Kipengele, Serikali imekuwa ikiweka alama za kudumu (vigingi) zinazoonekana kuzunguka mipaka ya hifadhi. Aidha, jumla ya alama za kudumu (vigingi) 152 kati ya 494 zimewekwa kuzunguka mpaka wa Pori la Akiba Mpanga- Kipengele kwa ushirikiano na Serikali za mikoa, wilaya na vijiji husika. Zoezi hili linaenda sambamba na utoaji wa elimu kwa 6 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) wananchi kuhusu sheria na kanuni zinazosimamia maeneo ya hifadhi na umuhimu wa utekelezaji wa Mipango ya Matumizi ya Ardhi. Mheshimiwa Spika, utatuzi wa migogoro ya matumizi ya ardhi baina ya maeneo ya hifadhi na vijiji nchini, unafanyiwa kazi na Kamati ya Mawaziri wa Sekta nane ambazo ni wadau wa matumizi ya ardhi. Hivyo, Vijiji vya Malangali, Wangomiko na Mpanga mpya ni miongoni mwa vijiji vinavyofanyiwa kazi na Kamati hiyo ambapo utekelezaji wa zoezi la utatuzi wa migogoro katika maeneo hayo utaendelea kufanyika kwa kufuata uamuzi wa Baraza la Mawaziri. Utekelezaji huu ni shirikishi na utahusisha Serikali za mikoa na wilaya husika. Mheshimiwa Spika, Wizara inawaomba wananchi kuzingatia na kufuata Sheria za Uhifadhi wa Wanyamapori pamoja na kuacha kuvamia maeneo mapya na kuwa wavumilivu wakati Serikali ikifanyia kazi migogoro hiyo. Vilevile, halmashauri za wilaya zinakumbushwa kuandaa Mipango ya Matumizi ya Ardhi kwa vijiji vinavyopakana na maeneo ya hifadhi ili kupunguza migogoro kati ya wananchi na wahifadhi. Na. 236 Leseni Zilizotolewa na EWURA kwa Wazalisha Umeme Wadogo MHE. JUMA OTHMAN HIJA aliuliza:- Moja kati ya kazi za Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA) ni kutoa leseni za kufanya biashara ya umeme:- Je, ni leseni ngapi zimetolewa kwa Wazalishaji Wadogo (Small Power Producers) katika kipindi cha mwaka 2017 – 2018? WAZIRI WA NISHATI alijibu:- 7 NAKALA MTANDAO(ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Spika, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Juma Othman Hija, Mbunge wa Tumbatu, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, Wazalishaji Wadogo wa Umeme (Small Power Producers) ni wazalishaji wa umeme kuanzia kilowati (kW) 100 hadi Megawati (MW) 10. Kwa mujibu wa Sheria ya Umeme
Details
-
File Typepdf
-
Upload Time-
-
Content LanguagesEnglish
-
Upload UserAnonymous/Not logged-in
-
File Pages211 Page
-
File Size-