NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA ___________ MAJADILIANO YA BUNGE ____________ MKUTANO WA TATU Kikao cha Arobaini na Nne – Tarehe 16 Juni, 2016 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Naibu Spika (Mhe. Dkt. Tulia Ackson) Alisoma Dua NAIBU SPIKA: Katibu. (Hapa Waheshimiwa Wabunge wa Kambi Rasmi ya Upinzani Waliondoka Ukumbini) DKT. THOMAS D. KASHILILAH - KATIBU WA BUNGE: MASWALI KWA WAZIRI MKUU NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri Mkuu. (Makofi) Waheshimiwa Wabunge, nimeletewa orodha ya Waheshimiwa Wabunge walioomba kuuliza maswali kwa Waziri Mkuu leo. Tutaanza na Mheshimiwa George Malima Lubeleje. MHE. GEORGE M. LUBELEJE: Mheshimiwa Naibu Spika, nakushukuru kwa kunipa nafasi ili nimuulize Mheshimiwa Waziri Mkuu swali. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa kuwa barabara nyingi katika nchi yetu zimeharibika kutokana na mvua kubwa zilizopita kiasi cha kusababisha baadhi ya maeneo kukosa kabisa mawasiliano ya barabara na wananchi wanapata shida na magari yanapita kwa shida. Je, Serikali imeweka mkakati gani wa dharura kuhakikisha kwamba barabara hizi zinatengenezwa ili ziweze kupitika? Ahsante. NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri Mkuu majibu. 1 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Lubeleje, Mbunge wa Mpwapwa, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli huwa inajitokeza na hasa wakati wa msimu wa mvua barabara zetu kuharibika. Barabara hizi zinapoharibika kwa utaratibu ambao Serikali imejiwekea ni kuanzisha Mfuko wa Barabara ambao umepelekwa kwenye Halmashauri zetu za Wilaya ambako barabara nyingi za ngazi ya Wilaya zipo lakini barabara hizi ziko za ngazi ya mikoa na barabara kuu. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, Mfuko wa Barabara pamoja na TANROADS ambao ndiyo wanashughulikia matengenezo ya barabara hizi, yako maelekeo yametolewa kutenga fedha za kukarabati barabara zinazoharibika kwa dharura kama ambavyo Mheshimiwa Mbunge ameeleza. Kwa hiyo, mifuko hii uharibifu ukitokea kwenye maeneo hayo huwa inafanya kazi hiyo mara moja. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, jukumu la Serikali hapa ni kusisitiza mifuko hii kuendelea kukarabati barabara ambazo zinaharibika kwa dharura ili ziweze kurudishwa katika hali yake. Kwa kufanya hivyo itasaidia wananchi wa maeneo haya waweze kuendelea na shughuli zao kama kawaida. (Makofi) NAIBU SPIKA: Ahsante. Mheshimiwa Martha Moses Mlata. MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante. Naomba nimuulize swali Mheshimiwa Waziri Mkuu kwamba, nchi yetu ni moja kati ya nchi ambazo zina wagonjwa ambao magonjwa yao yamekuwa sugu na usugu huu unatokana na umaskini wa watu wetu kushindwa kugharamia maradhi hayo ambapo hupelekea vyombo vya habari, hususan TV kwenda kuwagundua kule walipo na kuwaweka hadharani na kuomba watu wawachangie ili waweze kupata matibabu. Suala hili naona kama ni aibu kwa Taifa letu. Je, Serikali haioni kwamba kuna umuhimu wa kuweka utaratibu wa kuwagundua watu hawa na kuwasaidia na Wizara ya Afya iweze kusimamia ili wapate matibabu? Ahsante. NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri Mkuu, majibu. WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, kwanza nikiri kwamba wako Watanzania wenzetu wanaopata matatizo makubwa ya kiafya na magonjwa sugu ambayo wakati mwingine inawezekana kwenye maeneo wanakoishi huduma hizi haziwezekani. Vilevile kwa kuwa Serikali ilikuwa na mpango ule wa kuchangia matibabu ya afya wakati mwingine hawana uwezo wa kuchangia. 2 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeandaa utaratibu ambao unatoa huduma bure kwa makundi; wako watoto wadogo, akina mama wajawazito, wazee lakini pia magonjwa kama kifua kikuu na kisukari. Haya ni makundi ambayo Serikali imeridhia matibabu yatolewe bure. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali inaweza kumhudumia Mtanzania ambaye amepata madhara makubwa inapoonekana hana uwezo kabisa na hasa kama ataripoti kwenye hospitali inayotibu magonjwa hayo. Serikali kupitia Wizara ya Afya, imeweka utaratibu huo na kwa hiyo, watu wanaendelea kutibiwa. Inawezekana pia Serikali hatuna uwezo mkubwa sana wa kutenga fedha za kuwatibu wagonjwa wenye magonjwa haya wote nchini lakini pale inapotokea shida maalum, Serikali na wakati mwingine hata wadau wanajitokeza pia katika kutoa msaada wa huduma kama hizi. Mheshimiwa Naibu Spika, Serikali pia imeandaa utaratibu ambapo Watanzania wanaweza kupata matibabu kwa gharama nafuu. Tumeanzisha ule Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF) lakini pia tuna Mfuko kwa ajili ya Watumishi (NHIF) ambapo pia ukichangia unaweza kutibiwa wewe na familia yako na wategemezi kwa bei nafuu. Kwa hiyo, hili jambo hata Serikali imeliona kwamba kuna Watanzania wengi wanapata madhara makubwa na kuchukua hatua. Mheshimiwa Naibu Spika, pia tunao wadau ambao wanajitokeza, ndiyo hao ambao Mheshimiwa Mbunge ameeleza pale ambapo wananchi wanapoamua kwenda kwenye TV. Viko vyombo vya habari vinasaidia kutuhabarisha Serikali kwamba mahali fulani kuna tatizo kubwa na Serikali au wadau hujitokeza kuweza kusaidia jambo hili. Mheshimiwa Naibu Spika, nitoe mfano, nami nataka nishukuru sana, Clouds FM juzi juzi hapa iligundua kwamba kuna kijana wetu anasoma Chuo Kikuu Mzumbe, maarufu kupitia Programu yao ya Kipepeo, walienda Mzumbe wakambaini yule kijana ana tatizo la macho na anahitaji kutibiwa nje ya nchi, wakahabarisha jamii na Serikali pia. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa nafasi hii, naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania maana ni miongoni mwa wadau waliojitokeza kumchangia binti yetu shilingi milioni 10 ili aweze kupata tiba. Clouds walifanya hivyo na wakafanikiwa na wameturejeshea mrejesho kwamba yule binti yetu amepata matibabu na sasa anaendelea kusoma pale Chuo Kikuu Mzumbe. (Makofi) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, kwa ujumla niseme tu, pamoja na mipango hii ya Serikali, bado Serikali hatujaweza kuwa na uwezo mkubwa sana wa kutibu watu wote lakini kupitia mipango hii tuliyoiweka, bado tumetengeneza mazingira ya unafuu wa kutibu watu wetu. Niendelee kuvisihi 3 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) vyombo vya habari viendelee kutusaidia kutuhabarisha wale Watanzania wenye matatizo makubwa ambao wako maeneo ambayo hayafikiwi ili tuweze kupata taarifa kwa ukaribu kama walivyofanya Clouds na wakati mwingine tunaona TBC na ITV wakienda kwa jirani. (Makofi) Mheshimiwa Naibu Spika, lakini kubwa zaidi nimeanza kuona pia hata Watanzania kupitia vipindi vyao, nimeona Aunt Flora sijui Flora TV akienda kwenye jamii na kutoa taarifa ya tatizo lililopo kwenye jamii ile halafu Watanzania wengine wanajitokeza lakini wakati mwingine na Serikali tukikumbushwa hilo tunakwenda kusaidiana. Kwa hiyo, jambo hili la tiba ni letu sote, Serikali pamoja na wadau. Tutaendelea kufanya hivyo ili kuwahudumia hawa ambao hawana uwezo. (Makofi) NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Martha Mlata, swali fupi. MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Naibu Spika, nashukuru sana. Namshukuru Waziri Mkuu kwa kweli kwa namna ambavyo ameweza kutoa maelezo na maelekezo na shukurani zake, nami napongeza vyombo vya habari kwa kazi wanayofanya. (Makofi) Mheshimiwa Naibu Spika, kwa sababu ni wananchi wachache wanaopata bahati ya kukutana na vyombo vya habari lakini jicho la Serikali kwa upande wa afya ni watumishi wetu wa afya tulionao kule. Je, Waziri Mkuu yuko tayari sasa kutoa maelekezo kwa watumishi wa afya walioko kule wawatambue na kuwabainisha watu wenye mateso kama haya na kuwapeleka Wizara ya Afya ili Serikali iweze kuona namna ya kuwasaidia? Ahsante. (Makofi) NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri Mkuu, majibu. WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, ni kweli na kwa bahati nzuri Waziri wa Afya yupo na moja kati ya sera yetu ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata tiba stahili. Kwa hiyo, ni rahisi pia kufikisha ujumbe huu kupitia Wizara yetu, kwa madaktari wetu pale ambapo wanafanya upembuzi wa magonjwa haya wakabaini ugonjwa huu kwa ngazi yao hawana uwezo nao, basi kwa sababu sasa tunaendelea na uboreshaji wa utoaji wa fedha kwenye Wizara zetu ili kuboresha afya, niahidi tu kwamba tutaendelea kuboresha bajeti zetu ili pia huduma kama hizi ziweze kutolewa sasa kwenye maeneo yote tukipata ushirikiano wa madaktari walioko kwenye maeneo yao. Ahsante. (Makofi) NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Oscar Rwegasira Mukasa. MHE. OSCAR R. MUKASA: Mheshimiwa Naibu Spika, ahsante sana kwa kunipa fursa ya kumuuliza swali Mheshimiwa Waziri Mkuu. 4 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) Mheshimiwa Naibu Spika, utafiti wa hali ya kipato na matumizi kwa ngazi ya kaya wa mwaka 2012 umebainisha Mikoa ya Kigoma, Geita, Kagera, Singida na Mwanza kuwa ni mikoa yenye hali ya umaskini wa kutupa kwa ngazi ya kaya. Kwa kuwa siyo wakati muafaka kwa wananchi wa mikoa hiyo kuendelea kubishana na takwimu hizi bali ni wakati wa kushirikiana na Serikali ili kuona namna gani tunaondokana na hali hii. Mheshimiwa Naibu Spika, Ibara ya 8(1)(b) ya Katiba inasema, “lengo kuu la Serikali itakuwa ni ustawi wa wananchi,” na hapa unaongelea ustawi wa wananchi karibu milioni 10. Kwa kuwa umaskini huu umejidhihiri kwenye mikoa ambayo kiasili ina fursa za uchumi, kwa mfano, pamba inayopatikana Geita na Mwanza, kahawa, tumbaku na mchikichi Kigoma na kahawa Kagera basi hiki ni kiashiria kwamba kama Taifa kuna mahali ama kisera, ama kimkakati, ama kimipango hatuendi sawa. Mheshimiwa Naibu Spika, kwa hiyo, naomba kusikia kutoka kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu, anawaambia nini wananchi wa mikoa hiyo mitano juu ya kuchukua hatua za dharura na za uzito unaostahili ili iondokane na hali hii ambayo inatutia aibu? Nashukuru. NAIBU SPIKA: Mheshimiwa Waziri Mkuu, majibu. WAZIRI MKUU: Mheshimiwa Naibu Spika, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge. Najua swali ni refu, limezunguka
Details
-
File Typepdf
-
Upload Time-
-
Content LanguagesEnglish
-
Upload UserAnonymous/Not logged-in
-
File Pages121 Page
-
File Size-