NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA _____________ MAJADILIANO YA BUNGE __________ MKUTANO WA TANO Kikao cha Saba – Tarehe 8 Novemba, 2016 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Job Y. Ndugai) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa tukae. Tunaendelea na Mkutano wa Tano, Kikao cha Saba, lakini kabla hatujaendelea Waheshimiwa Wabunge, kama mlivyotangaziwa na Mheshimiwa Mwenyekiti, Mussa Azzan Zungu jana, kuhusiana na taarifa ya msiba. Tunaendelea kuomboleza msiba wa mpendwa wetu Marehemu Mzee Samuel John Sitta, Spika Mstaafu wa Bunge la Tisa. Msiba uliotokea jana huko Munich, Ujerumani. Mazishi ya Spika Mstaafu yako kwa mujibu wa Sheria ya Mazishi ya Viongozi ya 2006 ambapo Serikali ndiyo inayoratibu taratibu zote za mazishi hayo. Labda kwa ambao hawakumbuki vizuri niwakumbushe tu, kwamba mazishi ya viongozi yana-categories kubwa mbili; kuna mazishi ya kitaifa yanayowahusu viongozi wa juu , Rais, Makamu wa Rais, Waziri Mkuu Wastaafu au walioko madarakani na mazishi ya Kiserikali ni ambayo yanahusu Jaji Mkuu na Spika. Kwa hiyo, mazishi ya Mheshimiwa Sitta yatakuwa ni mazishi ya Kiserikali. Kwa hiyo, sisi Bunge tunaendelea kuwasiliana na wenzetu Serikalini kwa kuwa wao ndio waratibu wa mazishi hayo ya Kiserikali. Tutaendelea kupeana taarifa kuhusu taratibu za mazishi hayo na namna Bunge letu linavyoweza kushiriki katika kumuaga Marehemu mpendwa wetu. Jana Tume ya Utumishi wa Bunge iliketi na kuandaa mapendekezo ya namna ambavyo Bunge linaweza likashiriki katika ratiba nzima ya mazishi hayo ya Kiserikali; na tumetuma maafisa wetu Dar es Salaam kwenda kuungana na maafisa wengine wa Serikali walioko kule kuwa katika timu inayoratibu shughuli nzima ya mazishi. 1 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) Ofisi ya Bunge ilikuwa ikigharamia matibabu yake Marehemu kuanzia alipokuwa hospitali nchini India baadaye tukalazimika kumpeleka hospitali za Uingereza na mwishowe hospitali za nchini Ujerumani ambako mauti yamemkuta. Hivyo Ofisi ya Bunge ndiyo itakayogharamia usafirishaji wa mwili wake kutoka Ujerumani na kurejea hapa nchini. Mwili huo unatarajiwa kuondoka leo nchini Ujerumani kuja Tanzania na baada ya vikao ambavyo nimeshavielezea, vinavyoendelea hivi sasa ndani ya Serikali, tutajulishana namna bora ya ushiriki wetu. Waheshimiwa Wabunge, pamoja na mambo mengine niwakumbushe Waheshimiwa Wabunge kwamba tunao utaratibu ambapo Mbunge mwenzetu akifiwa tuna namna ambavyo huwa tunafanya ushiriki. Tukumbuke katika msiba huu Mama Margaret Sitta ambaye ni Mbunge mwenzetu amefiwa na mume wake. Kwa hiyo, ule ushiriki ambao huwa tunaufanya katika taratibu zetu sisi kama Wabunge pia tutafanya katika jambo hili. Lengo letu ni mwili huo pamoja na mambo mengine kuweza kuletwa hapa Bungeni Dodoma kabla Wabunge hatujaondoka ili Wabunge wote tuweze kupata fursa ya kumuaga Marehemu. Kama nilivyosema, tutaendelea kujulishana ratiba nyingine kadri tunavyozidi kupata habari na kadri tunavyoendelea na mipango ya mazishi. (Makofi) Niungane nanyi katika kumuombea mwenzetu ili Mwenyezi Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi. Amina. Katibu! RAMADHANI I. ABDALLAH – KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU SPIKA: Swali la kwanza tunaelekea Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu na linaulizwa na Mheshimiwa Neema Mgaya. Mheshimiwa Neema Mgaya. Na. 69 Tatizo la Ajira kwa Vijana Nchini MHE. NEEMA W. MGAYA aliuliza:- 2 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) Vijana wengi nchini wanakabiliwa na tatizo kubwa sana la ukosefu wa ajira. Je, Serikali imejipanga vipi kutatua tatizo hilo? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, AJIRA NA VIJANA: alijibu:- Mheshiwa Spika, kwa niaba wa Mheshimiwa Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Mheshimiwa Neema William Mgaya, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, kwa mujibu wa utafiti wa nguvukazi wa mwaka 2014, kiwango cha ukosefu wa ajira kwa vijana ni asilimia 11.7. Ili kukabiliana na tatizo hilo, Serikali imejipanga kutekeleza yafuatayo:- Mheshimiwa Spika, moja, ni kuendelea kutekeleza Mkakati wa Kitaifa wa Kukuza Ujuzi Nchini ambao umelenga kutoa mafunzo ya vitendo yatakayofanyika maeneo ya kazi. Aidha, ili kuwapa vijana wengi fursa za mafunzo Serikali imeanzisha programu maalum ya kutambua ujuzi uliopatikana kupitia mfumo usio rasmi na kuurasimisha kwa kutoa mafunzo ya muda mfupi kwa wale watakaobainika kuhitaji na kuwapa vyeti. Mheshimiwa Spika, ili kuthibitisha hilo kwa sasa Serikali inaendelea kufundisha vijana 400 katika kiwanda cha Took Garment Company Ltd. lengo ni kufundisha vijana 1000. Mafunzo mengine yataanza mwezi Novemba, 2016 katika kiwanda cha Mazava Fabrics, Morogoro pamoja na DIT Mwanza ambayo ni kwa ajili ya kutengeneza viatu na bidhaa za Ngozi. VETA nchi nzima watafundishwa vijana 4000. Serikali inaendelea kujadiliana na taasisi nyingine zikiwemo kiwanda cha Karanga Moshi na nyinginezo. Mheshimiwa Spika, pili, ni kuwezesha vijana kuwa wajasiriamali kwa kuwatambua vijana na mahitaji yao katika ngazi mbalimbali na kutoa mafunzo ya ujasiriamali kwa makundi mbalimbali ya vijana. Mheshimiwa Spika, tatu, ni kuhamasisha vijana wenye utaalamu mbalimbali kushiriki katika shughuli za kiuchumi kwa kuweka mazingira bora ya uwekezaji katika sekta zenye uwezo mkubwa wa kuzalisha ajira hususani kilimo na biashara. Aidha, Serikali itajikita zaidi kuhamasisha vijana na kuwawezesha kuwekeza kwenye viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ili kufikisha lengo la 3 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) asilimia 40 ya nguvu za kazi nchini kuwa katika sekta ya viwanda ifikapo mwaka 2020 kupitia Mpango wa Pili wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano. Mheshimiwa Spika, nne ni kuendelea kuimarisha Mfuko wa Maendeleo ya Vijana ambao kupitia mfuko huo vikundi vya vijana 6,076 vyenye wanachama 30,380 vimepata mikopo yenye masharti nafuu ya kiasi cha shilingi takribani bilioni moja na milioni mia sita kupitia kwenye SACCOS zao za Halmashauri za Wilaya ili ziweze kuwakopesha vijana mikopo ya masharti nafuu na hivyo vijana waweze kujiajiri. SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, mkiangalia ratiba ya siku ya leo imejaa kweli kweli kutokana na kutoendelea kwa shughuli hizi jana. Kwa hiyo, kwa kipindi hiki cha maswali watakouliza maswali ni wale wenye maswali ya msingi peke yao. (Makofi) MHE. NEEMA W. MGAYA: Mheshimiwa Spika, ninashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Lakini nina maswali mawili ya nyongeza. Mheshimiwa Spika, swali la kwanza, kwa kuwa tatizo la ajira ni kubwa na kwa kuwa tuna miradi mingi ya kilimo; kwa mfano kilimo cha chai kule Njombe, miwa Kilombero, kahawa, pamba kule Kanda ya Ziwa na katika miradi hii kuna fursa ya kuweka programu ya outgrowers. Mheshimiwa Spika, nilitaka kujua Serikali inatumia vipi hii fursa ya programu ya outgrowers kuwashirikisha vijana ili kuweza kutatua tatizo la ajira nchini? Mheshimiwa Spika, lakini vilevile tatizo hili la ajira nimekuwa nikilizungumzia mara kwa mara takribani miaka sita tangu nilipokuwa ndani ya Bunge hili, tangu nilipokuwa Mbunge wa Vijana. Nilitaka kujua, Serikali iniambie imeweza kutatua kwa kiasi gani tangu nianze kuzungumzia tatizo hili? SPIKA: Majibu ya maswali hayo Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mheshimiwa Antony Mavunde, na wewe mwenyewe ni kijana. NAIBU WAZIRI OFISI YA WAZIRI MKUU KAZI AJIRA NA VIJANA: Mheshimiwa Spika, swali la kwanza ameuliza namna gani Serikali tunaweza tukawashirikisha vijana kwenye fursa mbalimbali hasa za kwenye kilimo. Mheshimiwa Spika, tarehe 31 mwezi uliopita kupitia Wizara ya Kilimo pamoja na sisi Wizara chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu tumezindua mpango maalum wa kilimo ambao utawashirikisha vijana. Lengo lake ni kuwaweka 4 NAKALA YA MTANDAO (ONLINE DOCUMENT) vijana hawa katika makundi mbalimbali kutokana na mikoa yao waweze kushiriki katika kilimo cha nchi hii. Mheshimiwa Spika, katika mpango huu tunakwenda pia sambamba na mpango ambao upo chini ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji ambao ni mpango wanaouita ODOP (One District One Product) na lengo lake ni kufanya kitu kinachoitwa District branding ya kila sehemu kwa nchini nzima ambako shughuli za kilimo pamoja na shughuli nyingine za ujasiriamali zinafanyika. Kuwepo na kitu cha utambulisho katika Wilaya husika. Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimuondoe hofu Mheshimiwa Mbunge, kwamba Serikali inatambua kabisa kilimo biashara ni kati ya eneo ambalo linaweza likachukua vijana wengi kwa wakati mmoja, na tumeweka msisitizo mkubwa kuhakikisha kwamba makundi makubwa ya vijana yanapata fursa ya kuweza kushiriki katika uchumi wa nchi yao. Mheshimiwa Spika, lakini pili, katika swali lake ameuliza ni kwa kiwango gani sasa tumetatua changamoto hii. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba takwimu zinasema ukosefu wa ajira hasa kwa vijana nchini Tanzania umepungua kutoka asilimia 13.7 ya mwaka 2012 mpaka asilimia 11.7. Mheshimiwa Spika, lakini ukilinganisha Tanzania na nchi nyingine za jirani kwa maana ya Kenya na Uganda; tatizo la ukosefu wa ajira kwa Kenya ni takribani asilimia 17.3, kwa Tanzania tumekwenda mpaka asilimia 11.7. Mheshimiwa Spika, kwa hiyo ni dhahiri kwamba Serikali kupitia mipango yake mbalimbali imejaribu kutengeneza mazingira wezeshi kwa ajili ya vijana kutengeneza fursa mbalimbali na vijana wengi wameendelea kupata ajira. Mheshimiwa Spika, nimuondoe hofu kwamba tunayo mipango madhubuti ya kuendelea kusaidia kundi kubwa hili la vijana waweze kupata ajira na kuondoka katika adha hii ya ukosefu wa ajira. Na. 70 Ujenzi wa Barabara ya Kilometa 10 Ndani ya Mji wa Nzega MHE. HUSSEIN M. BASHE aliuliza:- Je, ni lini Serikali inakusidia kuanza utekelezaji wa ujenzi wa barabara ya kilometa 10 ndani ya Mji wa Nzega kama ambavyo Mheshimiwa Rais aliahidi wakati wa kampeni?
Details
-
File Typepdf
-
Upload Time-
-
Content LanguagesEnglish
-
Upload UserAnonymous/Not logged-in
-
File Pages249 Page
-
File Size-