Nakala ya Mtandao (Online Document) BUNGE LA TANZANIA __________________ MAJADILIANO YA BUNGE __________________________ MKUTANO WA KUMI NA TANO Kikao cha Ishirini na Tatu – Tarehe 31 Mei, 2014 (Mkutano Ulianza Saa 3.00 Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Anne. S. Makinda) Alisoma Dua SPIKA: Waheshimiwa naomba tukae. Katibu tuendelee? HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI Hati Zifuatazo Ziliwasilishwa Mezani na:- WAZIRI WA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015. NAIBU WAZIRI WA MAJI: Hotuba ya Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015. MHE. HUSSEIN MUSSA MZEE K.n.y. MWENYEKITI WA KAMATI YA MIUNDOMBINU: 1 Nakala ya Mtandao (Online Document) Taarifa ya Kamati ya Bunge na Miundombinu Kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014 Pamoja na Maoni nya Kamati Kuhusu Makadirio na Matumizi ya Wizara hiyo, kwa Mwaka 2014/2015. MHE. PROF. PETER MAHAMUDU MSOLLA - MWENYEKITI WA KAMATI YA KILIMO, MIFUGO NA MAJI: Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji Kuhusu Utekelezaji wa Majukumu ya Wizara ya Maji kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014 na Maoni ya Kamati Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015. MHE. MUSSA HAJI KOMBO (K.n.y. MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI WA WIZARA YA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA): Taarifa ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015. MHE. MOSES J. MACHALI K.n.y. MSEMAJI MKUU WA KAMBI YA UPINZANI WA WIZARA YA MAJI: Taarifa ya Msemeji Mkuu wa Kambi ya Upinzani wa Wizara ya Maji Kuhusu Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara hiyo kwa Mwaka wa Fedha 2014/2015. SPIKA: Ahsante sana. Katibu tuendelee? HOJA ZA SERIKALI Makadirio ya Matumizi ya Serikali kwa Mwaka 2014/2015 - Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia SPIKA: Mheshimiwa Rajabu? Mheshimiwa Waziri, kidogo tu naomba ukae. 2 Nakala ya Mtandao (Online Document) MWONGOZO WA SPIKA MHE. RAJAB MBAROUK MOHAMMED: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba Mwongozo wako kwa kutumia Kanuni ya 68(7) ya Kanuni zetu za Bunge na kwa kuzingatia vilevile Kanuni ya 64(1)(a), lakini vilevile Kifungu kidogo cha (f). Mheshimiwa Spika, jana wakati Waziri wa Nishati na Madini, Mheshimiwa Profesa Muhongo, anahitimisha Hoja yake, alitoa shutuma kali dhidi ya Wabunge wa Kambi ya Upinzani ya kwamba, Wabunge wa Kambi ya Upinzani wako baadhi ambao wamehongwa na IPTL. Ushahidi anao na CD kupitia CCTV anayo. Kwa hiyo, hizi shutuma ni nzito na zinadhalilisha Kambi ya Upinzani na zinadhalilisha Wabunge wako. Tunaamini kwamba, Wabunge wa Kambi ya Upinzani wako clean kabisa na hawajihusishi na mambo hayo. (Makofi) Mheshimiwa Spika, tunakuomba Mwongozo Wako kwamba, kama kweli ushahidi anao na hiyo CD anayo basi aiwasilishe kwako. Ikiwezekana ichezwe hapa, ili waonekane au wajulikane wale ambao wamefanya udhalimu huo dhidi ya Wizara yake. Mheshimiwa Spika, naomba Mwongozo Wako. SPIKA: Kwamba, CD itachezwa hapa haiwezekani ndio maana tuna Kamati inaitwa Kamati ya Haki na Maadili ya Wabunge, ndio sababu hiyo. Lakini Mwongozo Wako tutaushughulikia wakati unaofaa. Mheshimiwa Mtoa Hoja? Wabunge wanavyopenda ubishani humu ndani, aah! Tuendelee na kazi. Mheshimiwa Mtoa Hoja? (Makof/Kicheko) WAZIRI WA MAWASILIANO, SAYANSI NA TEKNOLOJIA: Mheshimiwa Spika, kufuatia Taarifa iliyowasilishwa leo ndani ya Bunge lako na Kaimu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Miundombinu Kuhusu Wizara yangu, naomba kutoa Hoja kwamba, Bunge lako Tukufu likubali kupokea na kujadili Taarifa ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti wa Wizara ya Mawasiliano, Sayansi 3 Nakala ya Mtandao (Online Document) na Teknolojia kwa Mwaka wa Fedha 2013/2014 na Malengo ya Wizara katika Bajeti ya Mwaka wa Fedha 2014/2015. Aidha, naliomba Bunge lako Tukufu likubali kupitisha Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia Pamoja na Taasisi zake kwa Mwaka wa Fedha, 2014/2015. Mheshimiwa Spika, awali ya yote, napenda nitumie fursa hii kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema kwa kutujalia uhai na afya njema na kutuwezesha kukutana leo kushiriki katika Mkutano huu wa Bunge unaojadili Bajeti ya Serikali. Mheshimiwa Spika, niruhusu sasa niungane na Waheshimiwa Wabunge, Ndugu na marafiki katika kuwafariji na kuwapa pole familia, Ndugu, na wapiga kura wa Marehemu Mheshimiwa William Mgimwa aliyekuwa Mbunge wa Kalenga na Mheshimiwa Saidi Ramadhani Bwanamdogo, aliyekuwa Mbunge wa Chalinze. Napenda pia, kuungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu kutoa pole kwa familia na wewe mwenyewe Mheshimiwa Spika, Bunge lako Tukufu, Ndugu na marafiki wa marehemu. Mwenyezi Mungu aziweke roho za Marehemu mahali pema peponi, Amina. Mheshimiwa Spika, nachukua nafasi hii kuwapongeza Mheshimiwa Godfrey Mgimwa kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga na Mheshimiwa Ridhiwani Kikwete, kwa kuchaguliwa kuwa Mbunge wa Jimbo la Chalinze. Ushindi wao ni kielelezo tosha kuwa wananchi wana imani kubwa na Chama cha Mapinduzi (CCM) katika kuwaletea maendeleo. Mheshimiwa Spika, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia katika kipindi cha mwaka wa fedha 2013/2014 imetekeleza majukumu na mipango yake kwa kuzingatia Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Mwaka 2025, Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini Tanzania, Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2013/2014, Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano (2011/2012 – 2015/2016) na Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi ya mwaka 2010–2015. Aidha, katika kutekeleza majukumu yake, Wizara imezingatia Sera ya Taifa ya Teknolojia ya Nyuklia ya Mwaka 2013, Sera ya Taifa ya Bayoteknolojia ya mwaka 2010, Sera ya Taifa ya Utafiti na Maendeleo ya mwaka 2010, Sera ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia ya mwaka 1996, Sera ya Taifa ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya mwaka 2003, Sera ya Taifa ya Mawasiliano ya Simu ya mwaka 1997 na Sera ya Taifa ya Posta ya mwaka 2003. 4 Nakala ya Mtandao (Online Document) Mheshimiwa Spika, Mapitio ya Utekelezaji wa Mpango na Bajeti ya Mwaka 2013/2014. Mwaka wa fedha 2013/2014, Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia ilitengewa jumla ya Sh. 63,147,599,460. Kati ya fedha hizo, Sh. 27,218,364,000 zilitengwa kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida ambapo Sh. 20,212,187,000/= zilikuwa ni kwa ajili ya Mishahara na Sh. 7,006,177,000 zilikuwa ni kwa ajili ya Matumizi Mengineyo. Fedha za Maendeleo zilizoidhinishwa zilikuwa Sh. 35,929,235,460 ambapo fedha za ndani zilikuwa Sh. 30,295,482,000 na fedha za nje zilikuwa Sh. 5,633,753,460/=. Mheshimiwa Spika, majukumu yaliyotekelezwa na Wizara ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia pamoja na Taasisi zake katika kipindi cha mwaka 2013/2014 ni kama yafuatayo. Kwanza UTEKELEZAJI KATIKA SEKTA YA MAWASILIANO, Ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Mheshimiwa Spika, ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unatekelezwa kwa awamu tano ambapo awamu ya I na II zimekamilika na zinatumika tangu mwaka 2012 zikiwa na jumla ya kilomita 7,560. Kwa sasa Wizara ipo katika utekelezaji wa awamu ya III inayohusisha ujenzi wa vituo vitatu mahiri vya kutunza kumbukumbu (Internet Data Centres) vitakavyojegwa Dar es Salaam, Dodoma na Zanzibar. Pia, katika awamu hii utajengwa mtandao wa intaneti wa kasi (Internet Protocol/Multiprotocol Label Switching Network (IP/MPLS) pamoja na kuunganisha Unguja na Pemba katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Utekelezaji wa sehemu ya kwanza (I) ya awamu ya tatu (III) umeanza rasmi Desemba, 2013 ambapo hatua za ujenzi wa kituo mahiri cha kutunza kumbukumbu katika eneo la Kijitonyama, Dar es Salaam zimeanza. Mheshimiwa Spika, Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi Katika Ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Ujenzi wa Mikongo ya Mijini (Metro Networks). Wizara kwa kutambua umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi katika kutoa huduma za mawasiliano inatekeleza Awamu ya IV ya Ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa kushirikiana na makampuni ya simu Tigo, Airtel na Zantel. Awamu hii itagharimu jumla ya Dola za Kimarekani milioni 80 ambazo zitagharamiwa na makampuni hayo ambapo serikali itatoa ruhusa ya kutumia hifadhi ya njia (Right of Way). Umiliki wa mikongo ya mijini inayojengwa kwa utaratibu huu utakuwa ni wa serikali wakati makampuni hayo yatapewa sehemu ya mikongo hiyo kwa ajili ya matumizi yao binafsi. Aidha, utekelezaji katika Jiji la Dar es Salaam umekamilika ukiwa na jumla ya kilomita 91 zilizogharimu Dola za Kimarekani milioni sita. Hatua inayofuata ni utekelezaji katika Miji ya Morogoro, Arusha, Mwanza na Mbeya. 5 Nakala ya Mtandao (Online Document) Mheshimiwa Spika, Ujenzi wa Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika Njia ya Reli. Katika kuhakikisha kuwa Mkongo unafika katika maeneo mengi zaidi, serikali kwa kushirikiana na kampuni za simu (Airtel, Tigo na Zantel) wamekamilisha taratibu za kuanza ujenzi wa mkongo katika njia za reli kuanzia Dar es Salaam hadi Mwanza, Tabora hadi Kigoma na Dar es Salaam hadi Arusha. Mheshimiwa Spika, juhudi za Serikali katika Kupeleka huduma za TEHAMA kwa Watumiaji wa Mwisho. Serikali katika kuhakikisha kuwa inakuza matumizi ya TEHAMA nchini hususan katika kutumia Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano, inatekeleza yafuatayo. Kwanza, Uunganishwaji wa Vyuo vya Elimu ya Juu na Taasisi za Utafiti katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano. Mheshimiwa Spika, wizara inaratibu utekelezaji wa mradi wa kuunganisha Taasisi za Elimu ya Juu na Utafiti katika Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano unaofadhiliwa na Benki ya Dunia. Madhumuni ya mradi huu ni kuimarisha mfumo
Details
-
File Typepdf
-
Upload Time-
-
Content LanguagesEnglish
-
Upload UserAnonymous/Not logged-in
-
File Pages429 Page
-
File Size-