NAKALA YA MTANDAO – (ONLINE DOCUMENT) BUNGE LA TANZANIA __________ MAJADILIANO YA BUNGE _________________ MKUTANO WA SITA ___________ Kikao cha Tisa – Tarehe 9 Februari, 2017 (Bunge Lilianza Saa Tatu Asubuhi) D U A Spika (Mhe. Dkt. Tulia Ackson) Alisoma Dua SPIKA: Naomba tukae. Waheshimiwa Wabunge, tunaendelea na Mkutano wetu wa Sita, leo ni Kikao cha Tisa. Katibu. NDG. RAMADHANI ISSA ABDALLAH - KATIBU MEZANI: HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI SPIKA: Waziri wa Fedha na Mipango. WAZIRI WA FEDHA NA MIPANGO:- Muhtasari wa Tamko la Sera ya Fedha, Mapitio ya Nusu Mwaka 2016/2017 (Monetary Policy Statement The Mid-Year Review 2016/2017). SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Dkt. Mpango, Waziri wa Fedha. Naomba nimwite Mheshimiwa Waziri wa Maji na Umwagiliaji. Anakuja Mheshimiwa Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji. NAIBU WAZIRI WA MAJI NA UMWAGILIAJI: Taarifa ya Mwaka ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji kwa Mwaka wa Fedha unaoishia tarehe 30 Juni, 2016 (The Annual Report of Energy and Water Utilities Regulatory Authority for the Financial Year ended 30th June, 2016). 1 NAKALA YA MTANDAO – (ONLINE DOCUMENT) SPIKA: Ahsante sana Eng. Isack Kamwelwe, Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji. Karibu sana Mheshimiwa. (Makofi) MWENYEKITI WA KAMATI YA BUNGE YA KILIMO, MIFUGO NA MAJI: Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Kilimo, Mifugo na Maji kwa kipindi cha kuanzia mwezi Januari, 2016 hadi Januari 2017. SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa. Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii. (Makofi) MWENYEKITI WA KAMATI YA BUNGE YA ARDHI, MALIASILI NA UTALII: Taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Ardhi, Maliasili na Utalii kwa kipindi cha kuanzia Januari 2016 hadi Januari 2017. SPIKA: Katibu. NDG. RAMADHANI A. ISSA - KATIBU MEZANI: MASWALI NA MAJIBU SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tutaanza na Ofisi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu. Swali linaulizwa na Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo, Viti Maalum. Na. 95 Umuhimu wa Kuanzisha Benki ya Vijana MHE. HALIMA A. BULEMBO aliuliza:- Serikali imeanzisha Benki ya Wanawake na Benki ya Kilimo na kwa sasa asilimia kubwa ya Watanzania ni vijana:- (a) Je, ni lini Serikali itaona umuhimu na kuanzisha Benki ya Vijana? (b) Je, kwa nini Serikali isianzishe dhamana kwa vijana kukopa? (c) Je, Serikali haioni umuhimu wa kujenga mfumo madhubuti wa Hifadhi ya Jamii ili vijana waweze kujiwekea akiba ya uzeeni, kupata Bima ya Afya na kupata mikopo ya kuendesha biashara zao? 2 NAKALA YA MTANDAO – (ONLINE DOCUMENT) NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, KAZI, VIJANA NA AJIRA alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Halima Abdallah Bulembo, Mbunge wa Viti Maalum, lenye vipengele (a), (b na (c). kama ifuatavyo:- (a) Mheshimiwa Spika, Serikali inalipa umuhimu sana suala la kuanzisha Benki ya Vijana nchini ili kuwawezesha vijana kupata huduma za mikopo yenye masharti nafuu. Kwa hatua za awali, Serikali imeona ni muhimu kwanza kuwajengea vijana tabia ya kuweka akiba na kukopa kwa kuanzisha SACCOS za vijana katika kila Halmashauri ili baadaye ziweze kuwekeza hisa katika Benki itakayoanzishwa. Hatua hii itawezesha Benki ya Vijana itakapoanzishwa kumilikiwa na vijana wenyewe. (b) Mheshimiwa Spika, suala la Serikali kuanzisha dhamana kwa vijana kwa ajili ya kukopa ni la msingi. Tunakubaliana na ushauri wa Mheshimiwa Mbunge na tutaufanyia kazi. Aidha, utaratibu utategemea uwezo wa kifedha wa Mfuko wa Maendeleo ya Vijana na ubainishaji muhimu wa nani apewe dhamana ya Serikali kwa lengo la kuwanufaisha vijana wote. (c) Mheshimiwa Spika, Mifuko ya Hifadhi ya Jamii imeweka utaratibu wa mwanachama kujiunga katika mfuko wa uchangiaji wa hiari pamoja na kujiunga na Bima ya Afya. Serikali kwa kushirikiana na mifuko hiyo imekuwa ikiwahamasisha vijana kupitia mafunzo, mikutano na makongamano mbalimbali ili waweze kutumia fursa hiyo kwa ajili ya ustawi wa maisha yao. SPIKA: Mheshimiwa Halima, naona wamekosea jina hapa, naona hujabadilisha jina sawasawa. (Kicheko) Mheshimiwa Halima, swali la nyongeza. (Kicheko/Makofi) MHE. HALIMA A. BULEMBO: Mheshimiwa Spika, nakushukuru. Naomba niulize swali moja dogo la nyongeza. Pamoja na majibu mazuri ya Naibu Waziri, changamoto kubwa katika kuanzisha Benki za Maendeleo ni mtaji. Hivi sasa nchini kwetu tumejiwekea utaratibu kwamba kila Halmashauri hutenga 5% kwa ajili ya vijana. Bajeti ya mwaka huu katika Serikali za Mitaa imekusanya takriban shilingi bilioni 600 ambapo katika ile 5% ya vijana ni sawasawa na shilingi bilioni 30. Iwapo fedha hizi zitatumiwa vizuri, tunaweza kuanzisha Benki ya Vijana zenye matawi katika kila Halmashauri na tukiweza katika hili, tutaweza kutatua suala zima la mikopo kwa vijana. 3 NAKALA YA MTANDAO – (ONLINE DOCUMENT) Je, Serikali haioni ni vyema sasa, Halmashauri zote nchini kuwa wanahisa wa Benki za Vijana na kutumia fedha hizi kama mtaji wa kuanzisha benki hii? (Makofi) SPIKA: Ahsante sana Mheshimiwa Halima. Majibu ya swali hilo Mheshimiwa Naibu Waziri, Anthony Mavunde, Ofisi ya Waziri Mkuu. NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU (KAZI, VIJANA NA AJIRA): Mheshimiwa Spika, nataka tu nianze kwanza kwa kumpongeza sana Mheshimiwa Mbunge kwa kazi kubwa anayoifanya ya kuwafuatilia vijana wa nchi hii na amekuwa mstari wa mbele kuhakikisha kwamba vijana wengi wanapata fursa ya mitaji na mikopo. Mheshimwa Spika, katika swali lake la msingi, ni kweli kwamba umekuwepo utaratibu wa utengaji wa 5% za mapato ya ndani kwa kila Halmashauri ambao lengo lake kubwa ni fedha hizi kwenda kuwafikia vijana. Kama nilivyosema kwenye majibu yangu ya msingi, lengo kubwa la uanzishwaji wa benki hii ni kutaka ije imilikiwe baadaye na vijana kupitia SACCOS za kila Halmashauri. Mheshimiwa Spika, kwa hiyo, hatua ya kwanza ambayo Serikali tuliianza ni kwamba mwaka 2014/2015 alitafutwa mtaalam kwa ajili ya kufanya upembuzi yakinifu na baadaye sasa Serikali tukaanza kuchukua hatua; mojawapo ni kuhakikisha kwamba kila Halmashauri nchi nzima inaanzisha SACCOS ya vijana ili baadaye SACCOS hizo za vijana ndiyo zije zimiliki hisa katika hii benki. Mheshimiwa Spika, kwa hiyo nimwondoe hofu tu Mheshimiwa Bulembo kwamba tukikamilisha uanzishwaji wa SACCOS katika Halmashauri, kazi itakayofuata sasa itakuwa ni namna ya kuutafuta huo mtaji na wazo alilolitoa ni wazo jema. Kama Serikali, tunalichukua, tutaona namna ya kuweza kulifanyia kazi. SPIKA: Waheshimiwa Wabunge, tuendelee na swali linalofuata, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha. (Makofi) Na. 96 Uhitaji wa Vifaa vya Maabara za Sekondari Serengeti MHE. MARWA R. CHACHA aliuliza:- Ujenzi wa Maabara za Shule za Sekondari Wilaya ya Serengeti umeshakamilika kwa kiwango kikubwa lakini maabara hizo zimebaki kuwa makazi ya popo:- 4 NAKALA YA MTANDAO – (ONLINE DOCUMENT) Je, ni lini Serikali italeta vifaa vya maabara kama ilivyoahidi? NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA alijibu:- Mheshimiwa Spika, kwa niaba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, TAMISEMI, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Marwa Ryoba Chacha, Mbunge wa Serengeti, kama ifuatavyo:- Mheshimiwa Spika, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti ina mahitaji ya vyumba vya maabara 63. Zilizokamilika ni 22 na zinatumika; maabara 29 zimekamilika lakini hazina vifaa na vyumba vya maabara 12 viko katika hatua mbalimbali za ujenzi. Mheshimiwa Spika, Serikali imetenga shilingi bilioni 16 kupitia mradi wa P4R kwa ajili ya ununuzi wa vifaa vya maabara zote zilizokamilika nchi nzima. Vifaa hivyo vinatarajiwa kupatikana kabla ya mwisho wa mwaka wa fedha 2016/2017. SPIKA: Mheshimiwa marwa, swali la nyongeza, nilikuona. MHE. MARWA R. CHACHA: Mheshimiwa Spika, ahsante. Kwanza nichukue nafasi hii kuwapongeza sana wananchi wa Jimbo la Serengeti kwa kujitahidi kukamilisha vyumba vya maabara kwa asilimia 81. Mheshimiwa Spika, kwa kuwa wamekamilisha kwa asilimia 81, Mheshimiwa Naibu Waziri uko hapa na umekuja pale Jimbo la Serengeti na umeona hali ilivyo; kwa kuwa wananchi hawa wamejitahidi kwa hali hii. Je, Serikali kupitia hizi fedha za P4R mko tayari kukamilisha hivi vyumba 12 ambayo ni sawa na asilimia 19? (Makofi) Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili; kwa kuwa ujenzi wa maabara ulipaswa pia kuendana na upungufu wa vyumba vya madarasa: Je, kupitia hizi pesa za P4R, mko tayari kupeleka sehemu ya fedha hizi kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa? Mheshimiwa Spika, ahsante. (Makofi) SPIKA: Majibu ya swali hilo Mheshimiwa Naibu Waziri, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mheshimiwa Selemani Said Jafo. NAIBU WAZIRI, OFISI YA RAIS, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA: Mheshimiwa Spika, kwanza naomba niwapongeze kwa kazi kubwa 5 NAKALA YA MTANDAO – (ONLINE DOCUMENT) waliyoifanya; na kama kuna deficit ya vyumba 12, niseme kwamba Serikali tutashirikiana, siyo na watu wa Serengeti peke yake, isipokuwa jukumu letu kubwa ni kuhakikisha tunapata maabara katika kila sekondari zetu zilizokamilika. Ndiyo maana Mheshimiwa Mbunge nilikwambia hiyo juhudi iendelee, lakini Serikali na sisi tutatia nguvu yetu kuhakikisha maeneo yote yale ya Serengeti yanapata maabara kama tulivyokusudia. Mheshimiwa Spika, ndiyo maana nimezungumza hapa kwamba tumetenga karibu shilingi bilioni 16. Lengo ni kwamba zile maabara ambazo wananchi wamejitolea kwa nguvu kubwa kuzijenga, lazima ziwe na hivyo vifaa. Kuanzia mwezi Machi mpaka mwisho wa mwaka hapa tutajikuta tumekamilisha suala zima la maabara siyo Serengeti, lakini katika maeneo mbalimbali. Mheshimiwa Spika, suala zima la ujenzi wa vyumba vya madarasa, ni kweli. Tuna changamoto ya vyumba vya madarasa katika maeneo mbalimbali ikiwepo kwako Serengeti,
Details
-
File Typepdf
-
Upload Time-
-
Content LanguagesEnglish
-
Upload UserAnonymous/Not logged-in
-
File Pages193 Page
-
File Size-