HOTUBA YA SHUKRANI YA RAIS MPYA WA

JAMHURI YA MUUNGANO WA ,

MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE,

UWANJA WA TAIFA, DAR ES SALAAM,

21 DESEMBA 2005

Mwenyekiti wa na

Rais Mstaafu wa Awamu ya Tatu,

Mheshimiwa Benjamin William Mkapa;

Mtukufu Mfalme Letsie III wa Ufalme wa Lesotho;

Waheshimiwa Viongozi Wakuu wa Nchi;

Makamu wa Rais,

Mheshimiwa Dkt. ;

Rais wa Serikali ya Mapinduzi ,

Mheshimiwa Amani ;

Rais Mstaafu wa Awamu ya Pili,

Mheshimiwa ; Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mheshimiwa ;

Spika wa Baraza la Wawakilishi,

Mheshimiwa Pandu Ameir Kificho;

Jaji Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania,

Mheshimiwa Barnabas Samatta;

Jaji Mkuu wa Zanzibar,

Mheshimiwa Hamid Mahmoud Hamid;

Rais Mstaafu wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar,

Mheshimiwa Dkt Salmin Amour;

Waziri Kiongozi wa Zanzibar,

Mheshimiwa ;

Mawaziri Wakuu Wastaafu;

Wakuu wa Vyombo vya Ulinzi na Usalama;

Viongozi wa Serikali;

Viongozi wa Vyama vya Siasa;

Viongozi wa Dini; Wageni Waalikwa;

Ndugu Wananchi;

Mabibi na Mabwana:

Nimeelemewa na imani kubwa ambayo ninyi Watanzania wenzangu mmeionyesha kwangu, na kwa Chama changu, Chama Cha Mapinduzi (CCM). Kwa bahati mbaya, lugha yetu ina mapungufu. Haina neno la shukrani linaloweza kubeba ujumla wa hisia za shukrani nilizo nazo leo. Naomba kila mmoja wenu aridhike tu nikisema: Ahsanteni sana, tena sana.

Nitapata fursa ya kuelezea jinsi nitakavyojitahidi kutafsiri shukrani zangu kwa vitendo – kwa mipango na mikakati ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi – nitakapohutubia Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, tarehe 30 Desemba mwaka huu kule Dodoma. Leo, nimeomba fursa ndogo tu ya kutoa shukrani.

Shukrani za kwanza kabisa ni kwa Chama changu, CCM, kwa kunikabidhi usukani wa kuendesha utekelezaji wa sera zake. Maana, Chama Cha Mapinduzi kisingeridhika na uwezo wangu wa kutekeleza sera zake kisingenichagua niwe mgombea wake wa Urais miongoni mwa wenzangu wengi wenye uwezo ndani ya Chama chetu. Ninawashukuru wana-CCM wenzangu wote waliojitokeza pamoja nami kugombea kuteuliwa. Walitumia haki yao ya kidemokrasia ambayo inalindwa kwa dhati ndani ya Chama chetu, na uwezo wanao. Uwezo huo nitauhitaji sana wakati wa uongozi wangu, na ni matumaini yangu kuwa watakuwa tayari kunisaidia ili kwa pamoja tujenge Chama Cha Mapinduzi na tujenge nchi yetu na kuiendeleza.

Ni vigumu kuwataja viongozi wa CCM, na wana-CCM wenzangu, tulioshirikiana kufanya kampeni nchi nzima. Nawashukuru wote, kuanzia Mwenyekiti wa CCM, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa; Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Ali Mohamed Shein; Rais Mstaafu, Mzee Ali Hassan Mwinyi; Makamu Wenyeviti wa CCM, ndugu yangu Rais , na mzee wangu Mhe. John Samuel Malecela; Rais Mstaafu wa Zanzibar, Mhe. Dkt. Salmin Amour; Katibu Mkuu wa CCM, Mhe. ; Wenyeviti wote wa Mikoa na Wilaya na Makatibu wao; Wagombea Ubunge, Uwakilishi na Udiwani; marafiki zangu, wana- mtandao na wana-CCM wote.

Nyote nasema ahsanteni sana. Ujumbe wangu kwenu leo ni mfupi sana. Tumefanikiwa kuendelea kuidhibiti IKULU ya Tanzania kwa ridhaa ya Watanzania wenzetu. Sasa tuendelee kuwa kitu kimoja katika kuimarisha uongozi bora, na kutekeleza ahadi zetu kwa wananchi, na kwa dunia.

Kwenye kundi hili la shukrani siwezi kuisahau familia yangu – familia ya karibu, na familia ya mbali. Wamekuwa chemchem ya nguvu yangu, na nanga iliyonituliza kwenye dhoruba. Nakushukuru sana mke wangu, Salma. Ulinishangaza ulivyoibuka kuwa mwanasiasa na mtafuta kura mahiri. Ninawashukuru watoto wetu wote ambao hawakutetereka katika kunitia moyo na kunisaidia. Ahsanteni sana.

Shukrani za pili ni kwenu wananchi kwa kukubaliana na Chama Cha Mapinduzi kuwa Jakaya Mrisho Kikwete ametosha na anastahili kukabidhiwa usukani wa Serikali ya Awamu ya Nne. Kote nilikopita wakati wa kampeni wananchi walinisubiri, wakati mwingine kwenye jua kali, na hata nilipochelewa hawakuondoka; na nilipofika, walinisikiliza kwa makini na kunitia moyo. Watanzania wenzangu, ahsanteni sana. Ahadi yangu kwenu ni kuwa nitafanya kila lililo ndani ya uwezo wangu nitimize matarajio yenu katika kunichagua kwa kura nyingi kuliko nilivyokuwa nimetarajia.

Shukrani zangu za tatu ni kwa viongozi wakuu wa nchi rafiki, au wawakilishi wao, waliokubali mwaliko wa Rais anayeondoka madarakani kuja kushuhudia Tanzania ikibadili awamu za uongozi wa taifa, kwa mara nyingine, kwa amani na utulivu, baada ya uchaguzi huru na wa haki. Na hawakuja kushuhudia tu. Ninaamini wametuletea baraka kwa kuja kuungana nasi katika tukio hili la kitaifa, tukio la kihistoria. Ahsanteni sana wageni wetu wote kwa kuja.

Ninamshukuru Rais aondokaye madarakani, Mheshimiwa Benjamin William Mkapa, kwa busara zake, na kwa kuona mbali, pale aliponikabidhi uongozi wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa kwa miaka kumi, Wizara ambayo ni sura ya nchi yetu nje ya nchi. Na hakunikabidhi Wizara tu; alikuwa pia mwalimu wangu. Leo viongozi hawa waliokuja kutuunga mkono si wageni kwangu, na mimi si mgeni kwao. Ni mahali pazuri pa kuanzia kuongoza nchi. Ninayo maandalizi ya kutosha kutimiza azma ya Sera ya Mambo ya Nje ya taifa letu ya kudumisha mahusiano mazuri na ushirikiano na nchi zote zenye nia njema nasi, iwe ziko jirani au ziwe mbali nasi.

Juzi, wakati akiagana na Mabalozi wanaowakilisha nchi zao hapa Tanzania, Rais Mkapa aliwaeleza siri moja ya Watanzania, kwa kunukuu methali mojawapo ya Kiafrika isemayo: “Ukituona tuko juu kwa juu ni kwa vile tumesimama juu ya mabega ya viongozi miamba waliotutangulia.”

Watanzania hatubomoi yale yaliyojengwa na waliotutangulia, maana waliotutangulia ni miamba kweli kweli: Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere; Mzee Ali Hassan Mwinyi; na kaka yangu mpendwa, Benjamin William Mkapa. Nikiwa nimetanguliwa na miamba kama hii, nikiwa nimesimama juu ya mabega yao, kwa nini mimi Jakaya Mrisho Kikwete nisitembee kifua mbele, kwa kujiamini; na kuendeleza yote mema yanayotokana na uongozi thabiti wa miamba hawa walionitangulia?

Ndugu Wananchi,

Mmenikabidhi wajibu huu, ni wajibu mkubwa sana, lakini nitatembea kifua mbele, maana naongoza Tanzania: Nchi ya amani, nchi ya umoja, nchi ya mshikamano, nchi ya upendo na kicheko, nchi inayojiamini na kustahiki heshima.

Nilisema wakati wa kampeni, na leo baada ya kuapishwa narudia. Serikali ya Awamu ya Nne si ya kubeza au kupuuza yaliyoanzishwa na awamu za uongozi wa taifa zilizopita. Haturudi nyuma; tunaendelea mbele. Wanaotazamia mabadiliko ya ajabu ya sera na mwelekeo wamepotea. Serikali ya Awamu ya Nne ni ya kujenga juu ya yaliyofanywa na awamu zilizotangulia na kuendeleza yote mema kulingana na mahitaji ya dunia ya leo, yenye heri kwa taifa letu, na kwa dunia yetu, tena kwa kasi mpya, ari mpya na nguvu mpya. Na tushirikiane sote kuhakikisha kuwa hatimaye juhudi tutakazoziongoza zitaleta maisha bora kwa kila Mtanzania.

Kwa watani wetu kutoka vyama vingine vya siasa, ninazo shukrani kwa kutuchangamsha wakati wa kampeni. Lakini sasa uchaguzi umekwisha, na ninawaomba tushirikiane kuijenga nchi yetu. Ndugu zetu, kabila la Ashanti, kule Ghana, wana methali isemayo: “Watu wawili walio kwenye nyumba inayoungua hawaachi kuzima moto wakaanza kubishana.” Na sisi nchi yetu inakabiliwa na kazi kubwa ya kupambana na umaskini. Tusiache kupambana na umaskini tukaanza kubishana.

Shukrani zangu za mwisho ni kwa wote walioandaa shughuli hii, akiwemo Jaji Mkuu, na Kamati mbalimbali. Nayashukuru majeshi yetu yote kwa kutulinda, na kwa gwaride zuri ajabu. Umakini na umahiri wenu ni dhahiri. Mwenye macho haambiwi tazama. Naona fahari kukabidhiwa uongozi wa nchi, nikijua ninao watu hodari, na majeshi mahiri, kama tulivyoona leo. Ahsanteni sana.

Watanzania Wenzangu:

Kwa leo sina mengi zaidi ya kusema. Kama nilivyosema, nimeelemewa na imani yenu kwangu, na mengi nitayazungumza Bungeni na siku za usoni. Leo ni siku ya furaha; ni siku ya kushukuru; na zaidi ya yote shukrani zetu ni kwa Mwenyezi Mungu aliyeiepusha nchi yetu na dhoruba zinazowakuta wenzetu wengine barani Afrika na kwingineko. Tushukuru, na tuzidi kumwomba Mwenyezi Mungu atuongoze na kutujalia kila la kheri. Nawashukuru sana viongozi wa dini kwa dua zao leo hapa, na siku zote wakati wa uchaguzi. Mliombea uchaguzi wa amani, na Mwenyezi Mungu akasikia sala zenu. Tutaendelea kuhitaji dua zenu kipindi chote cha Awamu ya Nne.

Mungu Ibariki Afrika

Mungu Ibariki Tanzania

Ahsanteni sana kwa kunisikiliza.