Hii ni Nakala ya Mtandao (Online Document)

BUNGE LA ______

MAJADILIANO YA BUNGE ______

MKUTANO WA NNE

Kikao cha Arobaini na Tatu - Tarehe 10 Agosti, 2011

(Mkutano Ulianza Saa Tatu Asubuhi)

D U A

Mwenyekiti ( Mhe. George B. Simbachawene) Alisoma Dua

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, huu ni Mkutano wa Nne, Kikao cha arobaini na tatu na leo ni tarehe 10 Agosti, 2011.(Makofi)

HATI ZILIZOWASILISHWA MEZANI

Hati ifuatayo iliwasilishwa Mezani na:-

NAIBU WAZIRI WA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA MICHEZO: Randama za Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo kwa mwaka wa fedha, 2011/2012.

MASWALI NA MAJIBU

Na. 392

Ukosefu wa Maji safi na salama Kondoa

MHE. MOZA A. SAIDY aliuliza:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa maji umekuwa ni kero kubwa katika sehemu nyingi hapa nchini:-

Je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha miradi ya maji safi na salama Wilayahi Kondoa ambako kuna ukame mkubwa wa maji? NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MAJALIWA K. MAJALIWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri Mkuu naomba kujibu swali la Moza Abeid Saidy, Mbunge wa Viti Maalum kuwa kwa kuzingatia kero kubwa ya maji wanayopata wananchi wa Wilaya ya Kondoa, Serikali inatekeleza mipango mbalimbali ya maji ili kuondoa kero hizo kama ifuatavyo:-

Kwanza kupitia programu ya maendeleo ya sekta ya maji, Serikali inajenga miradi ya maji ya visima virefu, mtiririko, mabwawa na uvunaji wa maji ya mvua katika vijiji na taasisi mbalimbali ambapo katika mwaka 2010/2011 ziliidhinishwa shilingi bilioni 2.4 kwa kazi hizo. Hadi mwezi Juni, 2011 Serikali ilishatoa shilingi milioni 622. Halmashauri ya Wilaya ya Kondoa imepanga kutumia fedha hizo kwa ajili ya kuendelea kutekeleza miradi ya maji ambayo utekelezaji wake ulianza na unaendelea. (Makofi)

Pili, kupitia mradi wa Belgium Fund for Food Security (BFFS) ulioanza kutekelezwa mwaka 2007 na ambao unatarajiwa kukamilika mwaka 2013, Halmashauri katika mwaka 2010/2011 imepanga kujenga miradi ya maji ya visima virefu katika vijiji tisa, kujenga mradi wa maji mtiririko katika kitongoji cha Maidiwi, kujenga visima vifupi katika vijiji vya Mlua na Itiso, kujenga mradi wa uvunaji maji katika shule ya msingi Msera na Isongolo na kujenga malambo mawili katika vijiji vya Ombiri na Manantu. (Makofi)

Tatu, Mamlaka ya Hifadhi ya TANAPA ambayo imesaini mkataba wa ujenzi wa kisima kirefu katika kijiji cha Chubi ambapo wananchi 1,210 wananufaika. Aidha, Halmashauri ya Wilaya inatarajia kujenga, kukarabati pamoja na kupanua miradi mbalimbali ya maji katika vijiji zaidi ya 80. (Makofi)

Nne, kupitia wadau wa maendeleo kama Bwana Mustafa Jaffer Sabodo wa Lindi anayeishi Dar es Salaam kwa mahusiano mazuri na Mheshimiwa naye pia amekuwa akichangia katika sekta ya maji Wilayani Kondoa ambapo amegharamia uchimbaji wa visima kumi katika vijiji vya Chemba, Ombiri, Iyoli, Jenjeluse, Mapango, Jangalo, Kinkima, Itolwa, Mlongia na Kitongoji cha Chang’ombe katika kijiji cha Kingale ambapo wanavijiji 36,068 watanufaika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuzingatia maelezo hayo ni dhahiri kwamba Serikali inachukua juhudi za dhati kutatua tatizo la maji katika maeneo yenye ukame mkubwa katika Wilaya ya Kondoa. (Makofi)

MHE. MOZA A. SAIDY: Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Waziri. Napenda kumuuliza Mheshimiwa Naibu Waziri maswali mawili ya nyongeza. Kwa mujibu wa jibu la Serikali, kwa kuwa kuna maendeleo ya programu ya maji. Naomba Mheshimiwa Waziri atutajie ni vijiji vingapi vitakavyonufaika na maji hayo na ni lini vitapata maji hayo ya visima virefu, mradi wa mtiririko wa mradi wa maji na mabwawa? (Makofi)

Pili, kwa kuwa mwaka 2000 katika Kata ya Kinyesi kulichimbwa kisima cha maji, maji yale ambayo hayana manufaa kwa wananchi ambayo si matumizi ya maji salama. Kwa kuwa maji yale wanadamu wakinywa ni ya uchungu na wanyama wanapoyanywa maji yale wanavimba matumbo na hufa. Je, Wizara itawasaidiaje wananchi wa eneo lile kubaini kwamba chanzo ni kisima au ni mkondo wa maji yenyewe? (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MAJALIWA K. MAJALIWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, kama ambavyo nimeeleza kwenye jibu la msingi kwamba programu hizi ambazo nimezitaja hapa ambazo Serikali inaendelea miradi yake na kila mwaka tumeweza kutenga fedha na nimeeleza kwamba kufikia mwaka 2013 miradi hii itaweza kukamilika na wananchi wanaweza kupata manufaa ya maji hayo. (Makofi)

Swali la pili ambalo unataka kujua madhara yanayopatikana kwa maji yale yanayotokea kwenye mto na athari ambazo wanazipata binadamu na wanyama, suala hili ni la kitaalamu, tutakachofanya ni kwamba tutawasiliana na Mkurugenzi na Mkemia pale kwa maana Idara ya Afya kuona athari zinazoweza kujitokeza kwenye eneo hilo lakini pia tuone namna ambavyo tunaweza tukazuia matumizi ya maji hayo kama itathibitika kwamba yana matatizo hayo. Ahsante sana. (Makofi)

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja dogo la nyongeza.

Pamoja na majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Serikali ipo tayari kufufua maporomoko ya Ntomoko ambayo yalikuwa yanasaidia vijiji 17 kupata maji katika Wilaya ya Kondoa na maporomoko hayo hayajafanyiwa ukarabati kwa muda mrefu, hivyo wananchi wa vijiji vile hawapati maji safi na salama? Je, Serikali ipo tayari kurekebisha miundombinu ya maporomoko yale?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MAJALIWA K. MAJALIWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nikuhakikishie kwamba Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na kwa kuwa inatambua uwepo wa Halmashauri zetu za Wilaya nchini ambazo zinatekeleza miradi mbalimbali ya maji, napenda kukuhakikishia kwamba kama maporomoko ya Ntomoko ni miongoni mwa maeneo ambayo Wilaya ya Kondoa imeyapa kipaumbele kwa ajili ya kupata maji na kwa kuwa natambua Wilaya ya Kondoa kuwepo kwa mito mingi sana ambayo inatiririsha maji, tunaweza tukafanya utafiti wa kina wa kuona namna ambavyo tunaweza kuhuisha tena maporomoko hayo ya Ntomoko ili yaweze kutoa maji mengi. (Makofi)

Na. 393

Tatizo la Maji Masasi na Nanyumbu

MHE. KURUTHUM J. MCHUCHULI (K.N.Y. MHE. CLARA D. MWATUKA) aliuliza:-

Katika Wilaya ya Masasi na Nanyumbu kuna tatizo kubwa la maji hivyo kusababisha wanawake kutafuta maji mbali sana na huuzwa kwa bei ya shilingi 1,000/= kwa kila ndoo?

Je, Serikali ina mpango gani wa haraka wa kuondoa tatizo hilo?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MAJALIWA K. MAJALIWA) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Clara Diana Mwatuka, Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Mtwara kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Halmashauri ya Wilaya ya Masasi kuanzia mwaka 2007 – 2009 ilitekeleza miradi yenye kuleta matokeo ya haraka (quick wins) ambapo katika Wilaya hii jumla ya visima 13 vilikarabatiwa na visima saba vilichimbwa na jumla ya shilingi milioni 88.9 zilitumika. Miradi hii ilileta mafanikio makubwa ambapo idadi ya wakazi wanaopata maji safi na salama iliongezeka kutoka 12,177 hadi 40,410 sawa na asilimia 26.1 ya wakazi wote. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia programu ya maji safi na usafi wa mazingira vijijini (RWSSP) utekelezaji wa mradi wa vijiji kumi vya Sengenya, Ulanga, Lukula, Ndwika, Holola, Mara, Ndechela, Nandembo, Chivirikiti na Chipuputa unaendelea ambapo tayari visima 16 vimechimbwa na kazi ya ujenzi wa visima hivyo itaanza mara baada ya kazi ya usanifu wa miradi hiyo kukamilika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka 2011/2012 Halmashauri ya Wilaya ya Masasi imeidhinishiwa shilingi milioni 913 kwa ajili ya kuendelea na utekelezaji wa miradi ya vijiji kumi vilivyochaguliwa ili kuondoa tatizo la maji katika Wilaya ya Masasi. Aidha, Halmashauri katika Bajeti yake imetenga shilingi milioni 500 kwa ajili ya ununuzi wa mtambo wa kuchimba visima vya maji ili kuchimba visima vingi zaidi ndani ya Wilaya hiyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mikakati ya kuboresha huduma ya maji katika Wilaya ya Nanyumbu, Wilaya mpya, ni pamoja na kukarabati visima vilivyopo, kuchimba visima vipya kupitia wahisani mbalimbali wakiwemo Kanisa la Anglikani na JICA, kujenga pamoja na kukarabati mitandao ya maji na kutafuta vyanzo mbadala vya maji, ikiwa ni pamoja na kuendeleza teknolojia ya uvunaji wa maji ya mvua katika mapaa ya majengo yaliyojengwa kwa kutumia bati.

MHE. KURUTHUM J. MCHUCHULI: Ahsante sana Mheshimiwa Mwenyekiti kwa kunipa nafasi niulize maswali mawili madogo ya nyongeza.

Kwa kuwa katika jibu la msingi Mheshimiwa Naibu Waziri ametuonyesha kwamba kuna pesa zilizotengwa kwa ajili ya kuendeleza miradi ya maji katika Wilaya ya Masasi na Nanyumbu ambazo ni shilingi miliioni 913 ambazo naamini kwamba hazitoshelezi. Je, Serikali haioni sasa umuhimu wa kuongeza pesa zaidi ili kutekeleza miradi hii kwa haraka ili ikamilike na wananchi wa Nanyumbu na Masasi wasiendelee kuteseka kwa adha ya kutokupatikana kwa maji? (Makofi)

Swali la pili, kwa kuwa tatizo la maji lililopo Masasi na Nanyumbu linafanana na tatizo la maji lililopo Wilaya ya Rufiji hususani katika Tarafa ya Ikwiriri na Tarafa ya Kibiti, je, Mheshimiwa Naibu Waziri anawaeleza nini wakazi wa Tarafa ya Ikwiriri na Kibiti katika suala la upatikanaji wa maji safi na salama?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MAJALIWA K. MAJALIWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu pale TAMISEMI tunacho kitengo kinachoshughulikia masuala ya maji katika Halmashauri zetu na kitengo kile kinapata feedback (mrejesho) kutoka Halmashauri na mahitaji yake na kwa hiyo, hutenga Bajeti kwa ajili ya kuunga mkono mahitaji ya Wilaya husika. Lakini bado katika kila Halmashauri yenyewe huwa inatenga fedha kulingana na umuhimu na mahitaji ya wakati huo ya maji na kuweza kutoa huduma hiyo kama ambavyo imeelezwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, fedha ambayo nimeitaja hapa ni ile ambayo Serikali iliweza ku- support Halmashauri kwa ajili ya kuboresha miradi ya maji mbalimbali. Kwa hiyo, Halmashauri ya Masasi hata Nanyumbu Wilaya mpya nayo inaweza kutenga fedha zake ili kuweza kuboresha sekta hiyo na kama kutaonekana kwamba kuna mahitaji ya ziada basi watujulishe TAMISEMI kitengo kinachoshughulikia na usambazaji wa maji kwenye Halmashauri zetu zinaweza kufanya kazi hiyo na ninakuhakikishia kwamba tupo tayari kuongeza huduma hiyo ili wananchi wengi waweze kunufaika. (Makofi)

Swali la pili la Mheshimiwa Mchuchuli ametaka kujua Serikali ina mpango gani kule Ikwiriri kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikuhakikishie kwamba Wilaya ya Rufiji ni miongoni mwa Wilaya ambazo zina chanzo kikubwa sana kupitia Mto Rufiji na hilo Serikali inatambua. Kwa utaratibu ule ule wa TAMISEMI kupeleke fedha zile ambazo zimekadiriwa na Halmashauri kupitia kwa watalaam kwa maana ya Afisa Mipango iko tayari kupeleka. Lakini bado Halmashauri yenyewe iweke kipaumbele mahitaji ya maji ya Ikwiriri na maeneo mengine ili pia wananchi wa Rufiji waweze kupata maji ya kutosha. Ahsante sana. (Makofi)

MHE. MARIAM R. KASEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi ya kuuliza swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa tatizo la maji Masasi wenzetu wa Red Cross waliliona ni tatizo kubwa na walianza kuchimba bwawa katika Kijiji cha Mihima, bwawa ambalo halikukamilika kwa sababu muda wao ulikuwa umeisha na Serikali haikuchukua hatua yoyote ya kumalizia lile bwawa. Je, Serikali inaweza ikatenga fedha kwa haraka wakaenda kumalizia bwawa lile kwa sababu fedha za wafadhili zilishatumika katika kuondoa tatizo la maji kwenye vijiji hivyo?

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MAJALIWA K. MAJALIWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Mbunge ametaka kujua jitihada zilizofanywa na Red Cross za kuchimba bwawa ambazo pia bwawa lile inaonekana halikupata mwendelezo ili kuweza kutoa huduma. Ninachoweza kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge ni kwamba leo hii baada ya kikao hiki nitafanya mawasiliano na Mkurugenzi kujua kwamba bwawa hilo sasa lina hali gani na je, Halmashauri kwanza ina mpango upi na sasa kama wanahitaji mahitaji yoyote kama ambavyo nimeeleza kwenye majibu yangu ya msingi ya awali na nyongeza kwamba Halmashauri inapoona itakuwa na mzigo mkubwa inapaswa kutoa taarifa TAMISEMI ili na sisi tuweze kuweka kiwango cha fedha cha kusaidia kuboresha bwawa hilo ikiwemo na hili ambalo lilianzilishwa na wadau wetu Red Cross. (Makofi)

MHE. JENISTA J. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kuniona na ninalo swali moja dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Waziri wakati anajibu swali la msingi alilithibitishia Bunge kwamba TAMISEMI wanakuwa na fungu la kusaidia Halmashauri ambazo Bajeti za maji ndani ya Halmashauri hizo zinakuwa ni kidogo na zinashindwa kutosheleza mahitaji na kwa kuwa katika Kata ya Mkongotema wananchi wangu wa kijiji cha Mkongotema walikuwa na matumaini makubwa ya mradi wa maji wa Benki ya Dunia na walikwishakamilisha vigezo vyote mpaka wakandarasi walishamaliza kazi zote. Lakini Serikali ilitoa tamko kwamba haijapokea fedha za kutekeleza mradi huo na Halmashauri iliomba ombi rasmi TAMISEMI kwa ajili ya mradi huo. (Makofi)

Je, Mheshimiwa Waziri anakubaliana na mimi kwamba katika fungu hilo sasa kuna umuhimu wa kuwapa fedha ya maji wananchi wa kijiji changu cha Mkongotema kwani fedha zote zilizotengwa zilishindwa kupelekwa na Benki ya Dunia na Serikali pia, sasa njia pekee ni kupitia Mfuko huo wa TAMISEMI? (Makofi)

NAIBU WAZIRI, OFISI YA WAZIRI MKUU, TAWALA ZA MIKOA NA SERIKALI ZA MITAA (MHE. MAJALIWA K. MAJALIWA): Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la mradi wa maji Mkongotema unaoshughulikiwa na World Bank kama uliweza kuendelea na mchakato wa kukamilisha miradi na ukakwama mwishoni ilikuwa ni wajibu wa Afisa Mipango kuwasiliana na Ofisi ya TAMISEMI.

Lakini kwa sababu tayari limeletwa hapa kama ni tatizo tutawasiliana na Maafisa wetu pale TAMISEMI waweze kuwasiliana na Afisa Mipango kule Halmashauri ya Wilaya ya Songea ili kuona tatizo hili limefikia ukubwa wa kiasi gani ili tuone sasa kama Halmashauri ile ilishaleta mpango huo ndani ya TAMISEMI kuona kama inaweza kupata priority ya kuwekewa fedha kwa ajili ya kuboresha mradi huo. Ahsante sana. (Makofi)

Na. 394

Uboreshaji wa Barabara - Kwimba

MHE. RICHARD M. NDASSA (K.N.Y. MHE. MANSOOR S. HIRAN) alijibu:-

Rais wa Jamhuri ya Muungano wakati wa ziara yake ya Kampeni Wilayani Kwimba tarehe 25/10/2010 aliahidi kuboresha barabara za Wilaya hiyo kwa kiwango cha lami:-

Je, Serikali inasema nini juu ya utekelezaji wa ahadi hiyo kwa kuboresha barabara kwa kiwango cha lami kutoka Magu Mjini kupitia Ngudu hadi Hungumalwa?

NAIBU WAZIRI WA UJENZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Mansoor Shanif Hiran, Mbunge wa Kwimba, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inatambua umuhimu wa barabara ya kutoka Magu Mjini kupitia Ngudu hadi Hungumalwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo, kutokana na ufinyu wa Bajeti kwa sasa, Serikali kupitia Wakala wa Barabara (TANROADS) itaendelea kuifanyia matengenezo barabara hiyo kwa kiwango cha changarawe ili iweze kupitika kwa urahisi majira yote ya mwaka. Wizara itaangalia uwezekano wa kujenga barabara hii kwa kiwango cha lami hali ya fedha itakaporuhusu.

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na majibu ya Mheshimiwa Naibu Waziri, naomba nimuulize swali moja dogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, amesema kwamba mpaka hapo hali ya fedha itakaporuhusu, ni lini hali ya fedha itaruhusu? Na isiporuhusu itakuwaje? (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa , kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaposema hali ya pesa itakaporuhusu tuna maana ya ujenzi wa hiyo barabara kwa 100% kuweza kuimalizia. Sio kwamba, tumekaa tu hiyo barabara haijajengwa, hapana! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, barabara kutoka Magu kuja Ngudu hadi Jojiro, tumeifanyia kazi sana tangu Mheshimiwa Rais atoe ahadi yake kwenye kipindi chake cha kwanza. Kwanza tumeiingiza kwenye Mpango wa Benki ya Dunia pamoja na Serikali wa Performance Management and Maintainance Program (PMM) kuanzia mwaka 2008 mpaka leo, kwa hiyo imekuwa well maintained. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, na sio hivyo tu, kipande cha barabara ambacho muuliza swali la msingi alitaka kuelewa pia kutoka Ngudu kwenda Nyamilama hadi Hungulamwa, kipande hicho ni mwaka jana tu Wizara imeweza kuipandisha hiyo barabara hadhi kutoka barabara ya Wilaya kuwa barabara ya Mkoa. Kwa hiyo, sasa hivi kutoka Magu mpaka Hungulamwa, kilomita zote 77 sasa ziko chini ya maintainance ya TANROADS na tayari tumeshaanza ujenzi angalau wa kilomita moja mwaka jana, kutokea Ngudu kuelekea Magu. Na mwaka huu vilevile tumetoa pesa ya kuendelea na ujenzi kidogo kidogo mpaka tutakapopata pesa ya kutosha. (Makofi)

MHE. MURTAZA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana. Ningependa nimuulize Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ya Rais ilikuwa ni kujenga kipande cha kilomita mbili kutoka eneo la kwa Mkocho mpaka Kivinje. Barabara hii ni kero kubwa sana kwa wakazi wote wa Wilaya ya Kilwa, kwa sababu wazazi wanajifungua njiani kutokana na hali ya corogations zilizopo kwenye barabara hiyo. Ni nini ahadi ya Serikali kutekeleza mpango huu kwa haraka? Sio miaka mitano. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA UJENZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Ujenzi, napenda kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Mangungu, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipande cha barabara anachokiulizia ambacho kipo mbali kabisa na swali la msingi kutoka kwa Mkocho kwenda Kivinje, ni kipande kifupi tu ambacho mimi ninaamini Waheshimiwa Wabunge, tukishirikiana pamoja na Halmashauri zetu na vilevile Mameneja wetu wa TANROADS katika Mikoa, ni kutumia ubunifu mara nyingine kuweza kujenga hizi barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitoe tu mfano kwamba, kilomita moja ya barabara inaweza kugharimu zaidi hata ya shilingi bilioni moja, lakini vilevile kwa lami nyepesi inaweza kugharimu hata kwa shilingi 150,000/=, 160,000/= ukajenga barabara kilomita moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, ningemuomba Mheshimiwa Mbunge, tushirikiane, tukae chini, tuangalie Bajeti yake katika Wilaya, tuangalie namna ya kujenga hicho kipande cha kilomita mbili tu. Hakihitaji kwa kweli msaada wa Wizara katika kuweza kukitatua. (Makofi)

Na. 395

Mgawanyo wa Askari Polisi kwenye Maeneo mbalimbali ya Kazi

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE aliuliza:-

Wilaya ya Chamwino yenye majimbo mawili na Tarafa tano imepewa jumla ya askari polisi 100 na Jimbo la Mtera lenye Tarafa tatu, wamepewa askari watano tu katika Kituo cha Polisi Mvumi:-

Je, Serikali haioni kuwa askari polisi watano hawatoshi kuwalinda wananchi kwenye hizo Tarafa tatu na vijiji 62?

Je, Serikali inachukua hatua gani za kukomesha wimbi kubwa la ujambazi na mauaji kwenye Kata za Handali na Manela?

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Livingstone Lusinde, Mbunge wa Mtera, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakubaliana kabisa na Mheshimiwa Mbunge kwamba askari watano waliopo katika kituo kidogo cha Mvumi hawatoshi kuwahudumia wananchi wa Jimbo zima la Mtera. Lakini tatizo hili la uchache wa askari lipo nchini kote kutokana na ufinyu wa Bajeti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, askari waliopo katika vituo vidogo vya polisi kama hicho cha Mvumi, hawafanyi kazi peke yao, kwani huongezewa nguvu kutoka vituo vikubwa pale linapotokea tatizo la uhalifu. Aidha, Jeshi la Polisi linafanya kazi kwa kushirikiana na wananchi na wadau wengine kupitia mpango wa Ulinzi Shirikishi/Polisi Jamii. Hata hivyo, Serikali inajitahidi kuongeza idadi ya askari kadri hali inavyoruhusu ili kufikia lengo la Kimataifa la wastani wa askari mmoja kwa kila raia 450 hadi 500. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge na Bunge lako Tukufu kwamba takwimu zetu zinaonesha kwamba hali ya uhalifu katika Kata hizo ni ya chini ikilinganishwa na sehemu nyingine za mkoa wa Dodoma na Tanzania kwa ujumla. Hata hivyo, Wizara yangu italifikiria ombi lake la kuongezewa askari ili tuweze kupambana na vitendo vya ujambazi katika Kata za Handali na Manela. (Makofi)

MHE. LIVINGSTONE J. LUSINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la kwanza, kwa kuwa hata hicho Kituo chenyewe cha Polisi kilichopo Mvumi ni gofu tu ambalo askari wamehamia, sio kituo hasa kilichojengwa. Waziri atakubali kuongozana na mimi kwenda kukagua na kujionea mwenyewe kwa macho hali waliyonayo askari ambao wanaishi pale ili kuweza kushirikiana na mimi walau kuboresha tujenge kituo hicho kimoja pale? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, Waziri yupo tayari kuwapa hata usafiri, ili waweze kufika kwenye baadhi ya maeneo kwa urahisi zaidi na kuwahi sehemu zenye matukio ya ujambazi? Ahsante. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Livingstone Lusinde, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza, nipo tayari kwenda katika eneo na kuhusu swali la pili, niseme kwamba, Bajeti yetu imeshapita na katika Bajeti yetu kipindi hiki ambacho tunacho hatuna, hatukuweka kwa sababu ya ufinyu wa Bajeti kwamba tunaweza kununua vyombo vya usafiri lakini kwa kuwa tulikuwa tumeshazungumza na hali tunaielewa nataka kumhakikishia kwamba tutajitahidi kuona angalau labda tunaweza tukapata pikipiki moja ya kuweza kumsaidia katika kituo hicho. (Makofi)

MHE. CHIKU A. ABWAO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona na kuniruhusu kuuliza swali dogo la nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ni majibu ya kawaida kwa Serikali kusema kwamba kuna upungufu wa askari pale inapotokea maswali ya kuuliza ama kuhitaji ongezeko la askari katika maeneo kadha wa kadha, na kwa kuwa Serikali mara nyingi imekuwa ikizuwia mikutano ya hadhara na wakati huo huo kama ikiamuliwa kufanyika hiyo mikutano askari huwa wanakuja wengi sana. Je, kipaumbele cha askari katika kazi zake ni kipi na kuzuwia maandamano na mikutano ya hadhara au kulinda usalama wa mali na raia? (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Chiku Abwao kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu askari, wala sio maneno kwamba ni majibu ya kawaida ambayo Serikali inatoa hapa Bungeni, ni ukweli kwamba standard za Kimataifa wanahitajika askari mmoja kwa wananchi 450 mpaka 500. Lakini kwa Tanzania, ni askari mmoja kwa raia 1500. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mikutano ya hadhara na kuhusu maandamano. Mkutano wa hadhara unapoombwa kibali kikatolewa ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba mikutano yote inakwenda salama na niseme tuna mfano mzuri kabisa, matokeo yanayotokea Uingereza leo, kwa wale ambao mnafuatilia, ni kielelezo tosha kwamba Serikali yoyote iliyo madarakani inawajibu wa kuhakikisha kwamba amani ndani ya Taifa inakuwepo. (Makofi)

MHE. RAJAB MBAROUK MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa sababu, suala la Mtera linafanana fanana kabisa na suala la Mji wa Chakechake, na kwa kuzingatia kwamba Mji wa Chakechake, ndio Mji ambao unapokea wageni wengi wa Kitaifa na Kimataifa katika Kisiwa cha Pemba. Je, Mheshimiwa Waziri, ana mkakati gani wa makusudi wa kuongeza ulinzi katika Mji huu wa Chakechake?

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu swali la nyongeza ya Mheshimiwa Rajab Mbarouk Mohammed, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli hili ni swali jipya. Lakini katika mkakati mzima tulionao wa kuhakikisha kwamba usalama wa raia na mali zao vinakuwa vipo katika hali ambayo ni ya kuridhisha. Tunao huo utaratibu kwa Taifa lote na ikiwemo Chakechake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, isipokuwa tu nimpe uhakika kwamba Mheshimiwa Waziri, atafanya ziara kama nilivyotaja jana, kuna maeneo atakwenda kule Pemba. Nafikiri hata maeneo kama haya atakwenda kutizama mwenyewe na kutokana na hilo tutatizama ni hatua gani tunaweza tukachukua Mheshimiwa Mbunge. (Makofi)

Na. 396

Hali ya Gereza la Isanga

MHE. DKT. DAVID M. MALLOLE aliuliza:-

Wafungwa katika Gereza la Isanga wanatumia ndoo (mitondoo) kujisadia haja kubwa na ndogo licha ya kwamba kuna shida kubwa ya maji hali inayoweza kusababisha magonjwa ya mlipuko kama vile kipindupindu ndani na nje ya Gereza:- Je, ni lini Serikali itajenga vyoo vya kisasa ndani ya Gereza hilo ili wafungwa waweze kutumia vyoo badala ya ndoo wanapojisaidia?

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Dkt. David Mciwa Mallole, Mbunge wa Dodoma Mjini, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inao mpango wa muda mrefu wa kukarabati na kuboresha miundombinu yote ya Jeshi la Magereza yakiwemo Magereza yenye ulinzi mkali (Central Prisons). Magereza hayo ni pamoja na Isanga, Ukonga, Segerea, Keko, Butimba, Uyui, Lilungu, Lindi, Arusha, Maweni, Karanga na Ruanda. Katika utekelezaji wa mpango huo, tayari ukarabati unaendelea kufanyika katika Magareza ya Maweni, Butimba, Uyui, Karanga, Lilungu na Isanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Gereza la Isanga ni miongoni mwa Magereza yaliyokarabatiwa kwa sehemu kubwa na eneo lililobaki ni la mfumo wa majitaka sehemu ya wafungwa maalum ambalo nalo pia lipo katika hatua za mchakato wa kufanyiwa kazi. Tutaendelea kukarabati miundombinu kwenye Magareza yaliyobaki kadri uwezo wa fedha utakavyoruhusu. (Makofi)

MHE. DKT. DAVID M. MALLOLE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante, ninaomba kuuliza maswali mawili tu ya nyongeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mpango wa kukarabati na kuboresha miundombinu yote katika Magereza yetu ni mpango wa muda mrefu, na kwa vile sehemu kubwa ya wafungwa waliopo katika Gereza la Isanga ni mahabusu. Je, Serikali ina mkakati gani wa kuharakisha kesi zetu zilizoko Mahakamani ili mahabusu ambao wataonekana hawana hatia, waweze kuachiwa huru na kwa hivyo, Magereza waweze kupata nafasi kidogo ya kuweza kupumua? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, swali la pili, katika mkakati huu wa muda mrefu wa kuboresha miundombinu yetu, Mheshimiwa Waziri anaweza akasema kwa uhakika ni nyumba ngapi za askari wetu wa Magereza ya Isanga, zinaweza kuwa zinaboreshwa mwaka hadi mwaka angalau kuanzia sasa mpaka kufikia mwaka 2015? Kwa vile, askari wetu wapo katika hali mbaya sana katika nyumba zao. Ahsante sana. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Dokta Mallole, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la kwanza, sasa hivi Wizara yangu na Wizara ya Katiba na Sheria, tupo katika mazungumzo ambayo yamekuwa yanaendelea kuona kwamba hatua zinachukuliwa ili kesi ziwe zinasikilizwa kwa haraka na watu ambao wapo mahabusu ambao kwa mfano itakuwa ushahidi haukukamilika ama utachukua muda, basi twende kwa mujibu wa sheria lakini kwa shabaha ya kuona kwamba tunapunguza idadi ya mahabusu ambao wanakuwa katika Magereza lakini tukizingatia utaratibu wa Sheria. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu swali lake la pili, siwezi nikampa kwa uhakika kwamba ni nyumba ngapi zitafanyiwa kazi. Isipokuwa nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa kuwa hili Gereza lipo hapa na sisi bado tupo hapa, tulikuwa tuna azma ya kwenda katika magereza ya hapa maeneo ya jirani tuweze kutizama na kutathmini wenyewe ili kama tutazungumza ni hatua gani zitachukuliwa ziwe ni hatua za uhakika. (Makofi)

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Naomba kutoa majibu ya nyongeza nikiongezea majibu mazuri ya Naibu Waziri, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli tunashirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani kuhakikisha kwamba mrundikano wa kesi unapungua kwa kiasi kikubwa, na katika Bajeti yetu ya mwaka huu, kipaumbele namba moja ni kumaliza kesi zote na viporo vyote vya nyuma. Kwa hiyo, nawaomba Waheshimiwa Wabunge, muwe na subira, wakati wa Bajeti yangu tutaeleza ni mkakati gani na fedha kiasi gani zimetengwa kwa ajili ya kupunguza mrundikano wa kesi. (Makofi)

MHE. MOHAMED HABIB JUMA MNYAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Kwa kuwa tatizo hili la kujisaidia kwenye ndoo au kwa jina maarufu mtondoo sio tatizo la Gereza la Isanga tu, lakini ni tatizo la Magereza yote Tanzania pamoja na Vyuo vya Mafunzo, na si suala hilo tu, pamoja na unyanyasaji mwingine unaotokezea katika Magereza ya watuhumiwa au wafungwa kuvuliwa nguo zote wakati wanapelekwa Mahakamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je, Mheshimiwa Waziri sasa kwa kuwa tatizo hili linakwenda kinyume na maadili ya kibinadamu. Upo tayari kupata uhakika iundwe Tume kupitia Magereza yote halafu kukomesha suala hili moja kwa moja Tanzania? (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA MAMBO YA NDANI YA NCHI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, nilipokuwa nikijibu swali la Dokta Mallole, kuhusu Gereza la Isanga, ukilitazama swali lake anasema kwamba kwa ujumla wake Gereza zima wanatumia ndoo, lakini si kweli. Katika Gereza la Isanga ni sehemu moja tu na hiyo sehemu ni ya wafungwa wa kunyongwa, lakini sehemu nyingine vipo vyoo ambavyo tumetengeneza, vinakuwa havitoshi, lakini bado jitihada zinafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pia magereza mengine zipo jitihada zinafanyika, vipo vyoo vinatengenezwa, ingawa havitoshi! Na kutotosha kwenyewe sio kwa sababu Serikali haina nia wala Serikali haiwapendi Watanzania wake, lakini tatizo kubwa ambalo tumekuwanalo ni tatizo la uhaba wa fedha. Lakini tumekuwa na programu ambayo mwaka hadi mwaka Bajeti inavyoruhusu tumekuwa tunafanya maboresho na kuhakikisha kwamba hiyo inafanyika. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini kuhusu suala la pili au suala hilo hilo la kusema kwambatuunde Tume ya kuweza kuchunguza, mimi nimwambie Mheshimiwa Mbunge kwamba hatujafika huko, na hili tunaweza tukalizungumza kwa sababu ni kitu ambacho kimo mikononi mwetu, kimo katika uwezo wetu, tatizo kubwa tulilonalo sio kwamba ni kitu kinafanyika kwa makusudi. Kinafanyika kwa sababu ya uwezo mdogo wa fedha tuliokuwanao lakini kwa kadri Bajeti inavyoruhusu ndivyo tunavyokwenda tunafanya maboresho. (Makofi)

Kwa hiyo, nikujibu Mheshimiwa Mbunge kule hatujafika, wafungwa tunaamini kwamba ni binadamu na haki zao zipo palepale, kwa sababu wamekuwa wafungwa, lakini isipokuwa ni hali halisi ambayo tumekuwa tunayo ya kifedha ambayo jinsi inavyoruhusu ndivyo jitihada zinavyofanyika kuhakikisha kwamba tunawatengenezea vyoo vya kisasa.

Na. 397

Matumizi ya Maji yatokanayo na Kuyeyuka kwa Theluji Juu na Mlima Kilimanjaro

MHE. JOSEPH R. SELASINI aliuliza:-

Theluji inayoyeyuka juu ya Mlima Kilimanjaro imetengeneza mito chini ya ardhi (underground rivers) na maji yake yote yanaibukia nchi jirani ya Kenya:-

Serikali ina mpango gani wa kufanya utafiti wa maji hayo hatimaye kutoboa mito hiyo ili maji yake yaweze kuwanufaisha wananchi wa Rombo wanaokabiliwa na matatizo makubwa ya maji?

Je, kwa nini Serikali isifanye malambo kuzuia maji ya mito mingine ya msimu ambayo nayo hupeleka maji nchini Kenya?

WAZIRI WA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA (K.N.Y. WAZIRI WA MAJI) alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Maji, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Joseph Selasini, Mbunge wa Rombo lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara yangu kupitia Bodi ya Maji ya Bonde la Pangani inaendelea na taratibu za kumwajiri mtalaam mshauri atakayeandaa Mpango wa Pamoja wa Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji wa Bonde la Pangani (Integrated Water Resources Management and Development Plan – IWRMD). Taratibu za manunuzi zimekamilika na sasa Wizara ipo kwenye majadiliano (negotiations) na mtalaam mshauri huyo ili kutia saini mkataba. Mpango huo utajumuisha utafiti wa hali maji katika mfumo mzima wa Mlima Kilimanjaro pamoja na maji shirikishi ya Ziwa Chala na Jipe. Utafiti huo pia utawezesha kujua uhusiano uliopo kati ya theluji/barafu ya Mlima Kilimanjaro na maji yanayotoka katika chemichemi zinazozunguka mlima huo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maji yanayotiririka kutoka Mlima Kilimanjaro na chemichemi zake ni maji shirikishi, hivyo utekelezaji wa miradi ya maji huhusisha majadiliano ya pamoja baina ya nchi husika. (Makofi) Mwaka 2010 Wizara ilituma watalaam Wilayani Rombo kuona uwezekano wa matumizi ya mito ya msimu katika kuvuna maji. Taarifa ya watalaam hao ilionyesha upo uwezekano wa kujenga malambo kwa ajili ya kukusanya maji ya mito hasa wakati wa mvua. Lakini hata hivyo, taarifa ilielekeza kuangalia namna ya udhibiti wa mawe yanayotoka mlimani na upotevu wa maji ardhini. Taarifa kamili itapatikana baada ya kukamilika kwa Mpango wa Pamoja wa Usimamizi na Uendelezaji wa Rasilimali za Maji wa Bonde la Pangani. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwanda wa chini Wilayani Rombo hupata mvua kidogo, Wizara yangu kupitia Bodi ya Maji ya Bonde la Pangani inaendelea kutafuta vyanzo vingine vya maji kwa ajili ya maeneo hayo. Mwezi Mei, 2011, Wizara ilimwajiri Mkandarasi Maji (Tech Engineering Ltd.) kwa ajili ya kuchimba visima virefu 15 katika uwanda huo. Mkandarasi tayari yupo eneo la mradi tangu tarehe 2/8/2011 kwa ajili ya uchimbaji visima hivyo. Jumla ya shilingi milioni 360 zimetengwa kwenye Bajeti ya mwaka 2011/2012 ili kutekeleza mradi huo. (Makofi)

MHE. JOSEPH R. SELASINI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza ninaishukuru sana Serikali kwa kutambua tatizo la maji katika Jimbo la Rombo na kwa mikakati ambayo imeanza kuchukuliwa. Pamoja na hayo nina maswali mawili ya nyongeza. (Makofi)

Kwa kuwa maji yatokanayo na theluji na chemichemi za Mlima Kilimanjaro yaliyotengeneza underground rivers ambazo maji yake sasa yanatumika katika nchi jirani ya Kenya hasa maeneo ya Loitokitoki, Chumvini na Taveta; na kwa kuwa wananchi wa Rombo ambao wapo jirani na maeneo hayo huvuka na kwenda kuchota hayo maji, je, Serikali haioni kwamba umefika wakati kuyatumia maji hayo wakati tukiendelea kusubiri huo utafiti kama wenzetu wanavyofanya? (Makofi)

Kwa kuwa utafiti umeonyesha kwamba malambo yanaweza yakachimbwa katika maeneo mbalimbali ya ukanda wa chini, lakini kinachosubiriwa ni utafiti wa namna ya kudhibiti mawe kutoka mlimani, pamoja na maji yanapotea ardhini. Je, Serikali inaweza ikawaambia wananchi wa Rombo ni lini utafiti huu utakamilika ili kuwapa matumaini ya kupatikana kwa maji na kutatua tatizo hili haraka iwezekanavyo? (Makofi)

WAZIRI WA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA (K.N.Y. WAZIRI WA MAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumshukuru Mheshimiwa Joseph Selasini kwa maswali yake ambayo nitayajibu kwa pamoja kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba theluji inapoyeyuka mlimani Kilimanjaro, maji yake yanatokea pande za Tanzania, hata kule Mwanga katika vijiji vyangu vya Kileo maji hayo yanatoka kule, pamoja na upande wa pili wa nchi ya Kenya. (Makofi)

Katika jibu la msingi tumeeleza kwamba Serikali imekamilisha utafiti ambao umeonyesha kwamba tunaweza kufunga malambo hayo, tunangojea taratibu zote zikamilike ili tuweze kukabiliana na tatizo hili. Lakini tunapongoja tatizo hili likamilike, ningependa kutoa taarifa kupitia Bunge lako Tukufu kwamba katika mradi wa maji na utunzaji wa mazingira, Serikali hivi sasa itachimba visima virefu katika vijiji tisa ambavyo vitasaidia kukabiliana na tatizo hili. Pamoja na visima hivyo virefu Serikali inajiandaa kuchimba lambo kubwa ambalo litazuia maji kwa ajili ya kunywa kwa binadamu na litatoa nafasi kwa mifungo kujengewa mahali pa kunywea maji. (Makofi)

MHE. LEKULE M. LAIZER: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi niulize swali moja la nyongeza, kwa kuwa maji haya haya ya Mlima Kilimanjaro ndiyo yanakuja kwenye Bwawa Jipe na maji ya kutoka Bwawa Jipe yanakuja Bwawa la Nyumba ya Mungu. Je, Serikali haioni kwamba Jipe imejaa magugu maji na kuona kwamba magugu maji hayo yanasababisha Nyumba ya Mungu kuisha maji na kuweka hasara katika wananchi wanaozunguka mabwawa hayo mawili? Je, Serikali itachukua hatua gani kuliokoa Bwawa Jipe lisiishe kwa ajili ya hayo magugu maji? (Makofi)

WAZIRI WA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA (K.K.Y. WAZIRI WA MAJI): Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru sana Mheshimiwa Lekule Lazer kwa kuuliza swali hili, ni kweli kwamba Ziwa Jipe lina magugu mengi yanayosababishwa na gugu la asili linaloitwa Taifa Domengelisisi, gugu hili limeenea sana katika Ziwa Jipe na ni mmoja wa miradi ambayo inashughulikiwa kati ya nchi zetu mbili yaani trans boundary project na hofu aliyoeleza Mheshimiwa Lekule Laizer ni hofu ambayo wote tunayo kwamba magugu haya kwa kuwa yanatoa maua na mbegu, mbegu zile zinasambazwa kwa upepo, mbegu hizo zinaweza kuelea kwenye maji na kupelekwa katika Bwawa la Nyumba ya Mungu, hivi sasa hakuna hatari kubwa kwenye Bwawa la Nyumba ya Mungu kwa sababu magugu hayo hayajaota kwa wingi katika eneo lile. Lakini tatizo kubwa lipo katika Ziwa Jipe na Serikali inaendelea kulifanyia utafiti kuona ni jinsi gani tunaweza kukabiliana nalo, kwa sababu ni gugu kubwa na lina mizizi mirefu na kukabiliana kwake ni kugumu kidogo kuliko magugu yale ambayo awali yaliota katika Ziwa victoria. (Makofi)

Na. 398

Wimbi la Wahitimu wa Vyuo Vikuu

MHE. PHILIPA G. MTURANO aliuliza:-

Kumekuwepo na wimbi kubwa la wahitimu wa Vyuo Vikuu hapa nchini na kupelekea uhitaji mkubwa wa ajira kwa vijana hawa:-

Je, Serikali ina mikakati gani ya muda mfupi na mrefu ya kukabiliana na wahitimu hawa ambao wengi wao huonekana mitaani bila shughuli maalum za kufanya?

Je, Serikali itakinusuru vipi kizazi hicho ambao wengi wao kihistoria wanatokea familia za vijijini maskini na ambazo hazikopesheki?

Je, Serikali itakuwa tayari kuwalipia madeni ya ada au kusamehe wasirejeshe mikopo waliyokopeshwa na Bodi ya Mikopo kwa kuwa hawana mahali pa kupata fedha?

NAIBU WAZIRI WA KAZI NA AJIRA alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kazi na Ajira, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Philipa Gofrey Mturano, Mbunge wa Viti Maalum lenye sehemu (a), (b) na (c) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kukabiliana na wahitimu wengi wa Vyuo Vikuu kuingia katika soko la ajira Serikali ina mikakati ifuatayo:-

(i) Kuendeleza kuboresha sekta ya elimu na mafunzo ili iweze kutoa wahitimu wenye taaluma zinazoendana na mahitaji ya soko la ajira na hivyo kufanya wahitimu wengi kuwa na ujuzi unaohitajika kwenye soko la ajira. Sambamba na hili Serikali imeendelea kuboresha mitaala kwa kuhimiza Vyuo Vikuu kuingiza masomo ya ujasiriamali;

(ii) Kuendeleza kuboresha mazingira ya uwekezaji kwenye sekta zenye uwezo wa kutoa ajira zaidi ili kuvuta wawekezaji wa ndani na nje ya nchi kuwekeza kwenye sekta mbalimbali na hivyo kufanya vijana wengi wanaohitimu elimu ya juu waweze kuajiriwa;

(iii) Kwa kupitia Wakala wa Huduma za Ajira yaani Tanzania Employment Services Agency, - TaESA, Tanzania imeendelea kuwaunganisha watafuta kazi na waajiri; na

(iv) Pia Serikali inaandaa programu ya kukuza ajira kwa vijana kwa mwaka 2011 - 2015 ambayo inalenga katika kuwapatia vijana fursa ya ajira za kuajiriwa na kujiajiri wenyewe. Programu hii inalenga katika kuwajengea vijana uwezo wa stadi mbalimbali pamoja na upatikanaji wa mikopo nafuu na nyenzo za kufanyia kazi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumhakikishia Mheshimiwa Mbunge kuwa Serikali ina nia njema ya kuwawezesha vijana waliohitimu ngazi mbalimbali za elimu waweze kujiajiri na kuajiriwa, kulingana na taaluma kwa kupitia mikakati iliyowekwa hapo na Serikali. Mikakati yote inawalenga vijana waliopo vijijini na mijini.

Pia Serikali kwa sasa haiwezi kulipia madeni ya ada au kuwasamehe wahitimu waliokopeshwa na bodi ya mikopo ya elimu ya juu kwa vile utaratibu uliowekwa unazingatia pia shida na uwezo wa familia walikotoka wahitimu. Ni busara kuendelea kuwahimiza vijana wahitimu kutimiza masharti ya mikopo ya mikataba waliyokubaliana bodi hiyo ili utaratibu huu uweze kuwa endelevu na kuwanufaisha vijana wengine waliopo vyuoni. (Makofi)

MHE. PHILIPA G. MTURANO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru, naomba nimuulize Waziri, kuna vijana ambao kwa kukosa ada wameshindwa kumaliza Vyuo Vikuu, sijui hawa Serikali inasemaje?

NAIBU WAZIRI WA KAZI NA AJIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Kazi na Ajira naomba kujibu swali la nyongeza la Mheshimiwa Philipa Geofrey Mturano, kama ifuatavyo:-

Swali hili ni jipya kidogo, lakini ninachoweza kusema kwamba Bodi ya Mikopo imejiandaa kuwakopesha vijana wote wenye sifa za kukopesheka na wale ambao hawana sifa za kukopesheka maana wanajilipia ada wenyewe. Sasa kama wanakuwa wanashindwa ni jukumu la wazazi wao kuweza kuwasaidia kulipia ada hiyo ya Vyuo Vikuu. (Makofi)

Na. 399

Ardhi ya Kijiji cha Ronsoti Kuchukuliwa na JWTZ

MHE. ESTHER N. MATIKO aliuliza:-

Wananchi wa Kijiji cha Ronsoti wamenyang’anywa ardhi yao na JWTZ, ardhi ambayo walimilikishwa kisheria mwaka 1976, kwa hali hiyo wananchi wamefukuzwa kwenye maeneo yao na hawatakiwi kuonekana kabisa kwenye maeneo hayo jambo linalowafanya sasa wakose eneo la kufanyia shughuli zao za kila siku za kukimu maisha yao:-

Je, kwa nini Serikali haichukui hatua ya kuwapa wananchi hao eneo mbadala au kuondoka wanajeshi hao?

Je, Serikali inatoa tamko gani juu ya ardhi ya Watanzania kumilikishwa Wakenya katika Kijiji cha Nyabirongo, Kata ya Susuni sehemu ya Matongo licha ya shughuli za wananchi kufuatilia haki zao juu ya eneo hilo bila mafanikio?

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kujibu swali la Mheshimiwa Esther Matiko, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kulijulisha Bunge lako Tukufu kuwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania halikuwahi kunyang’anya wananchi wa Kijiji cha Ronsoti ardhi bali Serikali ilitwaa sehemu ya ardhi ya kijiji hicho kwa ajili ya matumizi ya jeshi kutokana na umuhimu wa eneo hilo kuisalama yaani strategic importance. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ardhi hiyo ilikabidhiwa Jeshi la Wananchi wa Tanzania, Kikosi Maalum cha 76 ambacho hapo awali kilikuwa kwenye Kijiji cha Nyandoro, kwa ajili ya kuimarisha ulinzi wa mipaka ya nchi yetu. Kufuatia hatua hiyo, wananchi waliokuwa wakitumia eneo hilo kwa shughuli mbalimbali walidai Serikali iwalipe fidia. Serikali ilishughulikia madai hayo kuanzia mwaka 2007 kwa kukutanisha pande zilizohusika na kimsingi makubaliano yamefikiwa kuwa Jeshi libakie eneo hilo na kwamba ifanyike tathimini ya ardhi na mali isiyohamishika iliyokuwa ikimilikiwa na wananchi katika eneo hilo ili walipwe fidia na kuhamia maeneo mengine. Mwaka 2009/2010 Wizara yangu kwa kushirikiana na Halmashauri ya Wilaya ya Tarime, ilikamilisha upimaji wa mipaka ya vijiji vyote 39 ikiwemo Kijiji cha Ronsoti na eneo linalotumiwa na Jeshi la Wananchi lilipimwa na kuwekewa mipaka. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mwaka wa fedha wa 2011/2012 Serikali itafanya uthamini wa mali za wananchi hao wa Ronsoti ili walipwe fidia kwa mujibu wa Sheria ya Ardhi Namba 4 ya mwaka 1999 na Sheria ya Utwaaji Ardhi Na. 47 ya mwaka 1967. Aidha, wananchi hao watapewa ardhi mbadala kwa ajili ya makazi na shughuli za kiuchumi na kijamii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo, hakuna sehemu yoyote ya ardhi katika Kijiji cha Nyabiongo, Kata ya Susuni, iliyomilikishwa kwa raia wa kigeni wakiwemo wa Kenya. Wizara yangu kwa kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, inafuatilia taarifa alizotoa Mheshimiwa Mbunge juu ya kuwepo wageni waliojitwalia ardhi kwenye Wilaya za Tarime na Rorya ili ikithibika kuwa kweli wachukuliwe hatua za kisheria.

Hata hivyo, imebainika kwamba marekebisho yaliyofanywa kwenye Sheria ya Ardhi Na. 4 ya mwaka 1999 ambayo yaliruhusu wageni kumiliki ardhi yamekuwa na athari mbaya kwa maslahi ya Taifa. Ili kurekebisha kasoro hii hivi sasa Wizara yangu inaandaa marekebisho ya Sheria za Ardhi pamoja na kuhusisha Sera ya Ardhi ya mwaka 1995 ili kuziba mianya yote kwa lengo la kulinda maslahi ya Taifa katika ardhi ambapo mahitaji yake yanazidi kuongezeka siku hadi siku.

Naomba Bunge lako Tukufu likubali kutuunga mkono mabadiliko hayo yatakapowasilishwa katika Bunge hili Tukufu. Aidha, uongozi wa Wilaya ya Tarime, umetanabaishwa kuhakikisha kuwa hakuna mgeni atayemilikishwa ardhi kinyume isipokuwa wale watakaosajiliwa na kupangiwa ardhi iliyotengwa kwa ajili ya uwekezaji kupitia kituo cha uwekezaji TIC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia Bunge lako Tukufu narudia kuwakumbusha Wakurugenzi wote wa Wilaya na Miji nchini pamoja na Maafisa wa Ardhi kulinda ardhi ya Taifa letu kwa kuzingatia sheria za nchi wakati wa kufikiria maombi yoyote ya kumilikishwa ardhi. (Makofi)

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru nina maswali mawili ya nyongeza. Kwa kuwa Serikali imetwaa eneo lile na takribani miaka mitano sasa, wananchi wale wamezuiwa wasifanye shughuli zozote za maendeleo ikiwepo hata kuvuna mazao yao ya kudumu. Je, Serikali hii ya , haioni kwamba ni thabiti sasa ifanye juhudi zote kwa haraka mno kuwalipa fidia stahiki wananchi hawa na kuwapeleka kwenye maeneo mbadala haraka iwezekanavyo?

Kwa kuwa uwepo wa wanajeshi wamechang’anyikana na wananchi kumepelekea matendo mengine maovu kutendeka kama ubakaji wa wanafunzi wa shule za misingi, je, haioni hiki kitu ni kibaya sana na kinahitaji waraka wa aina yake kuwahamisha wananchi hawa haraka sana iwezekanavyo?

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

Naomba nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba fidia stahiki zitatolewa kwa wananchi na zoezi hilo kama itakavyokuwa katika maeneo mengine mengi ambapo wananchi wanasubiri fidia tutalishughulikia na ninatoa wito kwa wadau wahusika katika kesi hii ni Wizara ya Ulinzi kwamba fidia zipatikane na sasa hivi ninarekebisha fidia zenyewe kwa sababu viwango vingine vilionekana kama vilikuwa chini kwa hiyo, vilikuwa kero na kuleta migogoro. Kwa hiyo, suala hilo kwa kweli linashughulikiwa na Serikali na sina wasiwasi kwamba litatekelezwa haraka iwezekanavyo. (Makofi)

Kuhusu vitendo vya ubakaji ambavyo nimevisikia ni kweli tunamshukuru Mheshimiwa Mbunge kwa kutuletea taarifa hizo na ninaamini wenzangu katika Wizara husika kwamba hili litachunguzwa kwa sababu kwa vyovyote vile lazima Jeshi litakuwa na majirani. Kwa hiyo, nadhani tatizo hapa siyo kwamba lipo karibu ila ni tabia kama ni kweli litashughulikiwa. (Makofi)

MWENYEKITI: Jamani, mtakubaliana na mimi kwamba jibu lilikuwa refu na kwa hiyo swali hili muda wake umekwisha na umepitiliza. Sasa swali letu linalofuatia linakwenda Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii na linaulizwa na Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha.

Na. 400

Uboreshaji wa Hospitali Nchini

MHE. MARYAM S. MSABAHA aliuliza:-

Watanzania wengi wanaosumbuliwa na magonjwa ya shinikizo la damu, kisukari na saratani ya damu wamekuwa wakienda India kupata matibabu;

Je, Serikali ina mikakati gani ya kuboresha Hospitali zetu za Muhimbili, Bugando, KCMC na ile ya Rufaa Mbeya ili Watanzania wengi hasa wale wa Vijijini ambao hawana uwezo wa kwenda kutibiwa nje waweze kupata huduma hizo kikamilifu?

Je, Serikali ina mpango gani wa kuwarudisha nchini madaktari wengi wanaosomeshwa nje na kukatalia huko?

NAIBU WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha, Mbunge wa Viti Maalum, lenye sehemu (a) na (b) kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imekuwa ikifanya jitihada za kuziwezesha Hospitali zetu zinazotoa huduma za ubingwa wa juu (super specialised services) ili kuweza kutoa huduma ambazo kwa sasa zinapatikana nje ya nchi. Mpaka sasa huduma za upasuaji mkubwa wa moyo, kuweka viungo bandia vya nyonga na goti, uchunguzi kwa kutumia mashine ya MRI, zimekwishaanzishwa hapa nchini. Aidha, huduma za kusafisha damu kwa wagonjwa wenye matatizo ya figo, upasuaji ubongo, baadhi ya saratani, meno na huduma za dharura zimeboreshwa kwenye hospitali zetu hizo kubwa.

Vilevile Serikali imeendelea kupanua huduma ambazo zilikuwa zinapatikana katika hospitali katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili tu na sasa zinapatikana katika hospitali nyingine kwa mfano huduma kwa wagonjwa wenye saratani sasa wanaweza kuhudumiwa katika Hospitali ya Bugando juhudi za kupanua huduma hizo zinaendelea. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, madaktari wanaosomeshwa na Serikali ndani na nje ya nchi wanawajibika kufanya kazi katika vituo ambavyo Serikali itawapangia baada ya kumaliza mafunzo. Kabla ya kupata udhamini wa kulipiwa ada ya mafunzo wanatakiwa kuweka saini makubaliano yanayowataka kurudi na kufanya kazi katika vituo watakavyopangiwa na Serikali. Aidha, Serikali ina mpango wa kuboresha mazingira ya kazi pamoja na kuweka vivutio kwa madaktari (incentive scheme) na watumishi wengine katika sekta ya afya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mkakati wa kuboresha mazingira ya kazi na kuweka kwa incentive scheme pamoja na uzalendo wao, baadhi ya Madaktari Bingwa wameanza kurudi na kusaidiana na Serikali kuanzisha huduma ambzo zilikuwa zinapatikana nje ya nchi kama upasuaji mkubwa wa moyo kwa watoto wachanga. Mfano wa kuigwa ni Profesa Mahalu wa Hospitali ya Rufaa ya Bugando ambaye juzi mimi pamoja na yeye tumezindua huduma ya kupasua moyo yaani Open Heart Surgery kwa watoto wachanga wenye kilo chini ya 10. (Makofi)

MHE. MARYAM S. MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Nashukuru kwa majibu mazuri ya Mheshimiwa Naibu Waziri. Napenda kumuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwa kuwa Madaktari Bingwa wamekuwa wakifanya kazi katika mazingira magumu, je, Serikali ina mpango gani kuhakikisha madaktari hao wanapewa mishahara ya kutosha na kuwajengea nyumba ili waipende kazi yao?

Pili, kwa kuwa dawa hizi zinauzwa ghali na wagonjwa wa saratani hawana pesa za kununulia hasa wa vijijini, je, Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha wagonjwa hao wanapatiwa dawa hizo kwa bei nafuu na kwa gharama nafuu?

NAIBU WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Maryam Msabaha, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba mpaka sasa hivi Madaktari Bingwa pamoja na wataalamu wote na wafanyakazi wote wa sekta ya afya wanahitaji kuendelea kupewa motisha zaidi. Lakini kwa sababu Serikali nia inayo lakini tunasema kwamba rasilimali au resources ndiyo imekuwa changamoto, naomba kusema kwamba pale ambapo Madaktari Bingwa wanaweza wakatumia facilities zilizopo kufanya kazi ya ziada baada ya saa za kazi wanaruhusiwa mfano ni katika Hospitali ya Rufaa ya Muhimbili ambapo tuna zile huduma za fast track ambazo zaidi ya 60% ya mapato wanalipwa kila mwisho wa mwezi Madaktari Bingwa ambao wanaona wagonjwa kwenye hospitali zile. (Makofi)

La pili, kuhusu dawa za saratani ni kweli kwamba Serikali inajitahidi sana kununua dawa kwa ajili ya matibabu ya saratani pamoja na kuhakikisha kwamba tiba ya mionzi inakuwepo. Lakini tatizo ni kwamba hatuna resources za kutosha, pale ambapo panakuwa na upungufu kidogo dawa hazijawasili kwa muda na zimekwisha ndiyo wagonjwa wanashauriwa waende wakanunue.

Lakini naomba nikuhakikishie kwamba si wagonjwa wengi wanakwenda kununua dawa kwa sababu tunahakikisha kwamba kila wakati dawa zinakuwepo Ocean Road Hospital na kwa sasa hivi dawa zitakuwepo Bugando na baada ya muda dawa zitakuwepo pia kwenye Hospitali ya KCMC pia. (Makofi)

MWENYEKITI: Nilikuona Mheshimiwa Vullu na baadaye Dkt. Kigwangalla.

MHE. ZAYNABU M. VULLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi hii ili niulize swali moja la nyongeza.

Kwa kuwa tatizo la kisukari, pressure na saratani limekuwa ni tatizo gumu hapa nchini na kwa kuwa alijitokeza Mganga au Mchungaji wa Loliondo Samunge, watu wengi walikwenda kupata kikombe kwa babu; na kwa kuwa mpaka sasa hivi Serikali haijatoa tamko rasmi kujua kikombe kile kiliweza kutibu watu wangapi? Je, Serikali inaweza ikatupa taarifa kwamba ni watu wangapi walipona na wangapi walikufa? Na kama ile dawa ilikuwa inafaa je kuna mkakati gani wa kuiendeleza ili Serikali isipate hasara kwa sababu kikombe kimoja tu mtu anapona?

NAIBU WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Zaynabu M. Vullu, Mbunge wa Viti Maalum, kutoka Pwani swali lake la nyongeza kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli alijitokeza Mchungaji wa Samunge akawa anatoa kikombe kwa ajili ya kutibu maradhi ambayo ni sugu na kwa sababu maradhi sugu mengi yanatokana na matatizo tunayoyaita Psychosomatic Diseases ambayo hayana origin ya ki- psychology kwa hiyo yanakuwa mengi, hayawezi kutibika katika hospitali zetu bila kufanyiwa counselling. (Makofi)

Sasa walijitokeza Watanzania wengi lakini sisi kama Serikali hatukuwa na mtu ambaye alikuwa anahesabu wale watu. Sasa mimi labda nimueleze Mheshimiwa Mbunge kwamba kwa sababu anataka kufahamu idadi, mimi naomba anipe time nikawasiliane na Mkuu wa Mkoa wa Arusha tutapata idadi ya watu waliokwenda kule. Tutafuatilia wale ambao walikuwa wanakwenda kwenye clinic zetu za diabetes na saratani kwamba ni wangapi wanarudi kutibiwa na ni wangapi hawajarudi ili tuweze a rough picture kwamba ni wangapi wamefariki.

Lakini naomba niseme kwamba ubora au efficacy ya ile dawa bado tunafuatilia kupitia Shirika letu la NIMRI. Waheshimiwa Wabunge niliwaambia kwamba na mara nyingi nimeshajibu kwamba tutakapopata majibu ya ufuatiliaji wetu tutakuja kutoa tamko hapa Bungeni. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba uvumilivu. (Makofi)

MWENYEKITI: Tuanze na humu humu kuna watu waliokwenda kwa maana hiyo tuanze na utafiti humu humu. (Kicheko)

Mheshimiwa Dkt. Kigwangalla!

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesikitishwa sana na majibu ya Mheshimiwa Waziri kwa maana hayana ukweli ndani yake kwa sababu mazingira wanayofanya kazi Madaktari Bingwa hapa Tanzania ni duni sana na badala ya kuwavutia wengine waliopo nje kurudi ndani, waliopo ndani sasa hivi wamekuwa wakiondoka na mojawapo ya matatizo ambayo Mheshimiwa Waziri ameyaongelea hapa ni tatizo la makazi kwamba wanawapatia nyumba na wanawapa pesa za nyumba lakini ukweli ni kwamba mwaka jana mwezi wa kumi kuna waraka umetoka ambao umeondoa posho za nyumba na umeondoa posho ya makazi na Madaktari wengi wamekasirika.

Je, Mheshimiwa Waziri yupo tayari kubadilisha kauli yake na kutuambia ukweli sasa hivi hapa?

NAIBU WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Mbunge ambaye ni Daktari mwenzangu kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali sasa hivi inajitahidi sana kubadilisha mazingira ya kufanya kazi kwa Madaktari Bingwa na ndiyo sababu wengine wameanza kurudi na mfano hai ambao nimeutoa, lakini pia nitakwenda kukusanya majina ya wote waliorudi ni Profesa Mahalu ambaye alikuwa ni Bingwa wa Open Heart Surgery kwa ajili ya magonjwa ya watoto wachanga, amerudi. Sasa hivi anavyosema kwamba hatutoi incentives kwa ajili ya nyumba, naomba nisema kwamba madaktari wanapata posho zao kama inavyostahili ila ni kwamba hatujaweza kuwapa kiwango ambacho kinastahili ila tunajitahidi jinsi ambavyo Serikali inaendelea kuwa na ahueni ya kuweza kuwa na Bajeti ya kutosha. (Makofi)

MWENYEKITI: Mniruhusu tumalizie swali la mwisho kwa sababu tulichelewa kuwasilisha hati. Swali letu litaulizwa na Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar.

Na. 401

Upatikanaji wa Dawa – ARV kwa Wagonjwa

MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR aliuliza:-

Katika kuadhimisha siku ya UKIMWI duniani mnamo tarehe 01/12/2010 pamoja na mambo mengine, waathirika wa UKIMWI wamelalamika kwamba kumekuwepo na uhaba wa kupata dawa zao za ARV kwa sababu dawa hizo pia zinatumiwa na wafugaji kurutubishia mifugo yao na kuwasababishia usumbufu mkubwa kuzipatia dawa hizo.

Je, Serikali inalizungumziaje suala hilo na kujibu kilio cha wagonjwa hao?

NAIBU WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII alijibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa niaba ya Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, naomba kujibu swali la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum, kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, habari za kwamba kuna baadhi ya wafugaji wa Mkoa wa Mbeya wanaotumia dawa za kupunguza makali ya UKIMWI (ARVs) kwa ajili ya kurutubisha mifugo yao ziliripotiwa kwa mara ya kwanza na Gazeti la Mtanzania Toleo Na. 4990 la tarehe 11 Januari, 2010. (Makofi) Kufuatia taarifa hiyo, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mbeya na Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa nyakati tofauti ziliunda Kamati maalum kwa ajili ya kuchunguza ukweli wa suala hili. Uchunguzi huu ulifanywa kwenye vituo vitano vyenye wagonjwa wengi Mjini Mbeya ambapo ulihusisha kuwahoji wagonjwa 104 kati ya wagonjwa 500 wanaotumia ARVs, wafanyakazi katika vituo vya kutolea huduma na familia za wafugaji na baadhi ya waandishi wa habari wa Mkoa wa Mbeya. Vilevile timu ya uchunguzi ilifanya uchunguzi wa kumbukumbu za utunzaji wa ARVs kwenye Bohari za Dawa za Hospitali na vituo vilivyoidhinishwa kutoa huduma za dawa za ARVs kwa wagonjwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuliarifu Bunge lako Tukufu kwamba uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa taarifa kwamba wafugaji wa Mkoa wa Mbeya wanatumia vidonge vya kupunguza makali ya UKIMWI (ARVs) kwa ajili ya kurutubisha mifugo yao siyo za kweli. Aidha, naomba ifahamike kuwa dhana potofu kuamini kuwa ARVs zinanenepesha na kwamba zinaweza kutumika kunenepesha mifugo kwa kuwa ushahidi wa kisayansi unaonyesha kuwa dawa hizi hazina tabia hiyo. Hata hivyo, Serikali inaendelea kufuatilia ili kuhakikisha kuwa dawa zote ikiwa ni pamoja na ARVs zinatumiwa kwa matumizi yanayokubalika na si vinginevyo. Yoyote atakayebainika kutumia dawa yoyote kinyume na matumizi yake halisi, hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali, itaendelea kuhakikisha kuwa wagonjwa wote wanaostahili kupata dawa za kupunguza makali ya UKIMWI (ARVs) wanaendelea kuzipata kama kawaida na bila usumbufu wowote kwa kuhakikisha kuwa vituo vyote vilivyosajiliwa kwa ajili ya huduma hiyo, vinakuwa na dawa za kutosha kwa wakati wote. (Makofi)

MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi ya kuuliza maswali mawili ya nyongeza.

Kwanza napenda kuweka sawa kwamba mimi sikuulizia Mbeya, nimeuliza waathirika may be wa Tanzania nzima wanalalamikia hili lakini yeye kajibu Mbeya. (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Serikali katika majibu yake inasema kwamba taarifa zilizotolewa na Gazeti la Mtanzania siyo za kweli. Sasa kama siyo za kweli Serikali ilimchukulia hatua gani Mwandishi huyo wa Gazeti la Mtanzania kwa sababu aliipotosha jamii kwa sababu kila mtu aliisikia hiyo taarifa na inasemwa kila sehemu.

La pili, je, kama siyo kweli hilo tatizo mbona Serikali haikukanusha kipindi hicho ambapo taarifa zilitolewa kupitia vyombo vya habari ikiwemo na televisheni hata mimi mwenyewe niliona siku ya kuadhimisha siku ya UKIMWI duniani ya tarehe hiyo, niliona kwa macho yangu. Mbona Serikali haikukanusha inakuja kukanusha leo hapa Bungeni baada ya mimi kuuliza swali?

NAIBU WAZIRI WA AFYA NA USTAWI WA JAMII: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujibu maswali mawili ya nyongeza ya Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, Mbunge wa Viti Maalum kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli kwamba baada ya kufuatilia ilionekana kwamba ilikuwa ni kitambo kidogo ambayo na mimi sina kumbukumbu yake lakini ilionekana kwamba huyo mwandishi alikuwa siyo sahihi kwa sababu iliripotiwa mara ya kwanza kutoka Mbeya na ndiyo sababu tuliona kwamba tufanye uchunguzi kule Mbeya na ninakumbuka kwamba suala hili lilitolewa ufafanuzi nafikiri kupitia kwa Katibu Mkuu wa Wizara. Mheshimiwa Mbunge mimi nakuomba nitawasiliana na wewe baada ya kupata ile press release kama ilifanya hivyo. (Makofi)

Suala la kufuatilia watu wanaotoa taarifa za uongo katika Mkoa iliachiwa kwa Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa sasa kama amechukua hatua au hakuchukua hatua ni suala la kufuatilia na nitakupa taarifa. (Makofi)

La pili, mbona Serikali haikukanusha? Mimi naomba niseme kwamba hili suala lilipojitokeza Serikali ya Mkoa husika ndiyo ilikuwa na majukumu ya kukanusha na ninaomba nikuhakikishie kwamba ninakumbuka pamoja na kwamba sipo kwenye Wizara hii lakini ninakumbuka kuona kulikuwepo na mamlaka iliyokanusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa kama hawakukanusha basi naomba niseme leo kwamba natangazia Taifa hili kwamba hiyo ilikuwa ni uongo na kwamba dawa za ARVs haziwezi kunenepesha mifugo, ni taarifa potofu ni kama ilivyokuwa inaambiwa kwenye dawa za uzazi wa majra, ili uweze kunenepesha mfugo kwa dawa za uzazi wa majira au ARVs ni lazima utumie aina nyingi sana za dawa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba niseme kwamba hilo Serikali inasema kwamba ni uongo, nimechukua fursa hii leo kusema hilo kama halikufanyika kwa wakati muafaka.

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, muda wetu wa maswali umekwisha na mtaona kwa kweli inakuwa taabu kweli hapa kutoa nafasi kwa waulizaji wengi zaidi kwa sababu majibu bado yanakuwa marefu sana na bado maswali pia yanakuwa marefu sana. Tuendelee kufanya mazoezi ya kuuliza maswali mafupi na Waheshimiwa Mawaziri kujibu kwa kifupi. (Makofi)

Matangazo nitaanza na wageni, kuna wageni wa kutoka APNC Tanzania ambao ni Dkt. Hussein Sinda, Mhadhiri Mwandamizi Chuo Kikuu cha Dodoma lakini pia amefuatana na Dkt. Anthonyi Seppo yeye anatoka Parliamentary Centre of Canada na Ndugu Daniel Batdam Katibu Mkuu APNC Canada Kanda ya Afrika na Ndugu Phabris Fifons naye ndiye anaongoza Sekretarieti ya kutoka APNAC Ghana. (Makofi)

Lakini kuna wageni wengine waliofika kwa ajili ya shughuli za mafunzo. Tuna wanafunzi 70 kutoka Shule ya Sekondari ya Jamhuri Dodoma, wanafunzi sabini! Karibuni sana, tunawaombea mjitahidi na masomo na ninyi mnayo haki ya kuja kuingia humu ndani siku moja. (Makofi)

Pia wapo viongozi sita kutoka madhehebu mbalimbali ya Kikristo wanaojishughulisha na uelimishaji wa vijana kuhusu madhara ya dawa za kulevya. Sijui wako wapi? Naona labda wamekosa nafasi. Wapo pia wanafunzi 22 kutoka Chuo cha Biashara (CBE) Dodoma. Kutoka CBE Dodoma! Naona wapo basement.

Wapo wanafunzi 37 na walimu watano kutoka shule ya msingi ya mazoezi Kigurunyembe, Morogoro. Eeh, karibuni sana kutoka Kigurunyembe, Morogoro. Karibuni sana Dodoma na karibu mjifunze shughuli zetu. Wapo pia wanafunzi 40 wa Jumuiya ya Kiislamu ya Chuo cha Serikali za Mitaa, Hombolo, Dodoma wakiongozwa na Ndugu Abbas Yusufu. Pia wanatoa shukrani kwa Waheshimiwa Wabunge waliowachangia pesa ya futari kwa mwezi huu mtukufu wa Ramadhani. Wapo wapi hao? Nadhani wamekosa nafasi. Aah, wapo basement, karibuni sana! (Makofi)

Pia wapo wageni wa Mheshimiwa Livingstone Lusinde, Mbunge wa Mtera ambao ni wanachama sita wa Umoja wa Wanamvumi wanaoishi Dar es Salaam. Eeh, wale pale! Karibuni sana! Karibuni sana! Mheshimiwa Mbunge wenu anatufurahisha sana hapa, anafanyakazi nzuri sana. (Makofi)

Wapo wageni wa Mheshimiwa Mkiwa Kimwanga, ambaye ni Mwenyekiti wa BMU kutoka Mwanza ambaye ni Bwana Toyo Jackson Msiba. Karibu sana! Karibu sana!(Makofi)

Yupo pia mgeni wa Mheshimiwa Rachel Mashishanga, Bwana Paulo Robert, karibu sana! Yupo mgeni wa Mheshimiwa Susan Lyimo, Ndugu Mariam Mongi, Katibu wa Kamati ya Msukumo BAWACHA, Kinondoni. (Makofi)

Pia wapo wageni wa Mheshimiwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, wametoka Halmashauri ya Wilaya ya Singida wakiongozwa na Mwenyekiti, Mheshimiwa Celestine Yunde. Wapo pia na wasaidizi wanne wa Naibu Waziri, Mheshimiwa . Karibuni sana! Karibu sana Waheshimiwa Madiwani kutoka Singida. Karibuni sana! (Makofi)

Pia kuna wanafunzi kumi wakiongozwa na Bwana Ali Patrick, hawa ni wageni wa Mheshimiwa Esther Matiko. Naona wapo basement, karibuni sana! (Makofi)

Sasa matangazo ya kazi, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Huduma za Jamii Mheshimiwa Margaret Sitta anawatangazia Wajumbe wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Huduma za Jamii kuwa kutakuwa na kikao kifupi leo tarehe 10 Agosti, saa 5.00 asabuhi katika Ukumbi wa Pius Msekwa. Lakini mara nyingi tumekubaliana vikao vianze saa 7.00 mchana, sina hakika kama kuna kibali cha Spika katika jambo hili. Kama kipo ni kwa muda huo na kama hakipo muda wetu ni ule ule wa saa 7.00 mchana. (Makofi)

Mheshimiwa , Mwenyekiti wa Kamati ya Katiba, Sheria na Utawala anawatangazia Wajumbe wa Kamati hiyo kwamba kutakuwa na kikao leo tarehe 10 Agosti, 2011 mara baada ya kuahirisha Kikao cha Bunge, saa 7.15 mchana, chumba namba 227. (Makofi)

Pia Mheshimiwa , Mwenyekiti wa Kamati ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, anawatangazia Wajumbe wake kuwa kutakuwa na kikao leo tarehe 10 Agosti, 2011 mara baada ya kuahirisha kikao cha Bunge saa 7.15 mchana katika chumba namba 231. (Makofi) Mheshimiwa Sylvester Massele Mabumba, Makamu Mwenyekiti wa Kamati wa Sheria Ndogo, anawatangazia Wajumbe kwamba kutakuwa na kikao saa 7.15 mchana katika chumba namba 219. (Makofi)

Kaimu Katibu wa Bunge, Ndugu John Joel anatangaza hapa kwamba leo tarehe 10 Agosti, 2011 saa 7.20 mchana, Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP) angetoa maelezo ya ziada kwa Wabunge juu ya kampeni ya kushawishi utii wa sheria bila kushurutishwa ili kudumisha amani, usalama na utulivu nchini. Kutokana na sababu zisizozuilika shughuli hiyo haitafanyika leo na badala yake IGP atakutana na Wabunge siku ya Jumapili, tarehe 14 Agosti, 2011 kuanzia saa 4.30 asubuhi katika Ukumbi wa Pius Msekwa. Saa 4.30 asubuhi, siku ya Jumapili, tarehe 14 Agosti, 2011 ni semina muhimu sana ili tuweze kujua utii wa sheria bila kushurutishwa. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, hayo ndiyo matangazo yetu. Tunaendelea Katibu!

MWONGOZO WA SPIKA

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwongozo wa Spika!

MWENYEKITI: Mwongozo wa Spika! Nimemuona Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar na Mheshimiwa Dkt. . Haya Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar.

MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mwongozo wako. Natumia Kanuni ya 68(7).

MWENYEKITI: Mmh!

MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: “Hali kadhalika, Mbunge anaweza kusimama wakati wowote ambapo hakuna Mbunge mwingine anayesema na kuomba Mwongozo wa Spika kuhusu jambo ambalo limetokea Bungeni mapema, ili Spika atoe ufafanuzi kama jambo hilo linaruhusiwa au haliruhusiwi kwa mujibu wa Kanuni na taratibu za Bunge na majibu ya Spika yatatolewa papo hapo au baadaye, kadri atakavyoona inafaa.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mwongozo wako kwa kuwa katika kipindi cha Maswali na Majibu, Mheshimiwa Esther Matiko, alisema wanajeshi wanapochanganyika na wananchi, wanabaka watoto wa shule na Mheshimiwa Waziri hakusita, akamsifia ahsante sana na akasema kweli. Alivyomjibu kuwa ni kweli na amempongeza muuliza swali. Naomba Mwongozo wako kuwa Bunge hili linapenda kujua kama hii ndiyo kauli ya Serikali hapa Bungeni kuwa wanajeshi wanabaka watoto wa shule? (Makofi)

MWENYEKITI: Mmh! Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla.

MHE. DKT. HAMISI A. KIGWANGALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kwa mujibu wa Kanuni ya 68(7) naomba Mwongozo wako kuhusiana na maamuzi ya kiti kwa hoja zinazowasilishwa Bungeni kutaka kujadili suala la dharura kwa mujibu wa Kanuni ya 47 na 48. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, utakumbuka wiki iliyopita mimi na wenzangu ambao tunatokea mikoa ya wakulima wa pamba tuliwasilisha hoja ya dharura kutaka suala la bei ya pamba lijadiliwe na Bunge lako Tukufu, lakini bahati mbaya sana tukaambiwa kwamba lile halikuwa jambo la dharura, jambo la dharura ni vita peke yake. Lakini katika hali ya kushangaza jana suala la mafuta ambayo pengine yanawagusa watu wengi muhimu tukiwemo na sisi Wabunge, kwa sababu tuna magari, limejadiliwa hapa kama jambo la dharura sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ningeonelea kwamba kujadili suala la bei ya pamba na mustakabali wa kilimo cha pamba nchini, lingekuwa ni jambo la dharura zaidi kwa sababu linagusa zaidi ya asilimia 40 ya Watanzania. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hali ya kusikitisha tuliambiwa kwamba sisi hatuwezi kujadili hoja yetu ya jambo la dharura kuhusiana na bei ya pamba, badala yake jana imetolewa fursa hiyo. Naomba Mwongozo wako kama Kanuni hii inasema ukweli au inasema uongo na ninaomba Mwongozo wako ili niweze kuambiwa ni kwa nini, ni criteria zipi zinatumika kuamua kwamba jambo fulani ni la dharura na jambo lingine si la dharura. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante!

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge nimeombwa ...

MBUNGE FULANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, Taarifa!MWENYEKITI: Ngoja tumalize kwanza na maneno haya halafu tunafungua sehemu nyingine. Tumalize kwanza na haya mawili, maana ukiweka Mwongozo ukachanganya na Taarifa, itakuja na taarifa sasa utashindwa kutambua kwamba umetokea wapi.

Kuhusiana na suala la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, hili tutalitolea Mwongozo wake baadaye. Lakini suala la Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla. Kwanza hoja hii ilikwishafungwa kwa sababu ilianza na kumalizika kwa utaratibu wa ambavyo ilimalizika. Kwa hiyo, kuianzisha tena si utaratibu mzuri sana wa uendeshaji wa shughuli za Bunge. Kwa faida tu ya wengine lakini pia wakulima wa pamba, tunazo Kanuni zetu ambazo zinatoa sifa za kitu kinapokuwa cha dharura. Nakumbuka Mwongozo huu niliutoa mimi mwenyewe na katika maneno yangu pamoja na kwamba sikumbuki Hansard vizuri, nilisema jambo hili Mheshimiwa Waziri Mkuu alikwishalisema. (Makofi)

Kwa hivyo, ukiiangalia Kanuni hasa ile ya 48(3)(c) inasema kwamba jambo hilo; “hakutatokea fursa ya kulijadili siku za karibuni kwa njia ya kawaida ya kushughulikia mambo ya Bunge.”

Lakini pia ukisoma na zile nyingine zote Mheshimiwa Dkt. Hamisi Kigwangalla, hakuna hata mara moja ambapo Bunge lilipuuza jambo ulilolileta, ila tuliliangalia na kuona kwamba lilipata fursa ya kujibiwa na Serikali na kwa hakika hatuhitaji majibu ya Serikali zaidi na maelezo mengi yalitolewa. Lakini kabla ya wewe kulisema, Mheshimiwa Waziri Mkuu alikwishalitolea majibu kwenye swali lililoulizwa katika Kipindi cha Maswali kwa Waziri Mkuu katika siku za nyuma yake. (Makofi)

Kwa hiyo, mimi naamini udharura wa jambo ni pale ambapo linapata sifa za Kanuni ya 47 na 48 kwa uzima wake. Sasa tafsiri hii pengine inaweza ikawa inaleta shida lakini kwa mujibu wa jambo lenyewe, lilikwishatolewa majibu yake na Mheshimiwa uliridhika, labda tu pengine zimekuja hisia mpya, lakini mimi nadhani hakika jambo hili lilitendewa haki na mjadala wa jambo hili umezungumzwa sana humu Bungeni na Serikali ili-respond katika jambo hili. (Makofi)

Mheshimiwa Mbunge, nakuomba uridhike na majibu haya, lakini kama kuna hoja nyingine inayohusiana na masuala ya pamba unaweza kuileta kwa njia nyingine. (Makofi) Waheshimiwa Wabunge hili lingine la Mheshimiwa Faida Mohamed Bakar, nilisema nitalitolea Mwongozo baadaye, lakini kwa kuwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, ameniomba alitolee ufafanuzi jambo hili, mimi kwa kutumia nafasi niliyonayo namruhusu afanye hivyo. Mheshimiwa Waziri! (Makofi)

WAZIRI WA ARDHI, NYUMBA NA MAENDELEO YA MAKAZI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante!

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nifafanue kwamba taarifa hii imetolewa hapa Bungeni kwamba inawezekana vitendo kama hivyo vimetokea na nilipojibu nilisema bayana kwamba tunashukuru kwa taarifa hiyo ya wasiwasi, lakini kwamba tutaifanyia kazi kama ni kweli Serikali itachukua hatua husika, ilibidi tufanye tafakari kabla hatujachukua msimamo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru! (Makofi)

MWENYEKITI: Pamoja na maelezo hayo, mimi nayachukulia kama ni maelezo ya ziada tu ya kuweka ufafanuzi wa jambo lenyewe, lakini kiti kinalichukua na kwamba kitaliletea Mwongozo wake kwa jambo hilo maalum. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge tunaendelea. Katibu!

HOJA ZA SERIKALI

Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka 2011/2012

(Majadiliano yanaendelea)

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, tunaendelea na uchangiaji wa hoja ya Waziri wa Viwanda na Biashara na mchangiaji wetu wa kwanza asubuhi hii atakuwa ni Mheshimiwa Muhammad Amour Chomboh, akifuatiwa na Mheshimiwa . Mheshimiwa Muhammad Amour Chomboh! Hayupo!

MHE. DEOGRATIAS A. NTUKAMAZINA: Mwongozo! Mbona nilitangazwa kwamba nitaanza mimi Deogratius Ntukamazina, Mbunge wa Ngara?

MWENYEKITI: Mheshimiwa upo kwenye…,

Kwanza nilikuwa sijakuruhusu na tulikwishakubaliana hapa kwamba tusiwashe microphone mpaka umeitwa. Sasa labda kwa kukufahamisha tu baada ya Mheshimiwa Luhaga Mpina, unayefuatia ni Mheshimiwa Deogratias Ntukamazina. (Kicheko)

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii ili na mimi niweze kuchangia hii hoja ya Viwanda na Biashara. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza leo suala la ujenzi wa viwanda nchini wakati wazalishaji wa mazao ya kilimo hapa nchini wameshakata tamaa. Wazalishaji wa mazao ya kilimo wameshakata tamaa na wameamua kuondoka katika sekta hiyo ya uzalishaji wa mazao ya kilimo. Wameamua kufanya hivyo kutokana na changamoto nyingi zinazokuwa zikijitokeza. Kwanza ni mabadiliko ya hali ya hewa ambayo yanapelekea mazao yao kukauka mara kwa mara kutokana na ukosefu wa mvua.

Tatizo lingine ni kukosa soko la uhakika la mazao yao na Serikali imeshindwa kwa kipindi kirefu kutafuta soko zuri kwa ajili ya mazao ya wananchi hao wanayoyazalisha. Matokeo yake sasa wananchi walio wengi wameamua kuondoka katika sekta ya kilimo na kuanza shughuli zingine. Sasa tunazungumzia ujenzi wa viwanda, viwanda ambavyo mwisho wa siku vitakosa raw materials kwa sababu wananchi sasa hawazalishi tena.

Leo hii nikitolea mfano mazao yetu ya biashara, pamba, kahawa, pareto, chai na korosho toka mwaka 1977 uzalishaji wa pamba ulikuwa tani 195,000 lakini mpaka mwaka 2010, uzalishaji wetu wa pamba ni tani 265,000. Kwa hiyo, utakuta kwamba uzalishaji wetu ni ule ule wa toka miaka ile. Hatujaongeza uzalishaji mpaka sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunafanyaje katika mazingira hayo? Tumeshindwa kuwapa wananchi wetu motisha ili waweze kulima kwa sababu tunawapa bei ya kugalaliza na tumeshindwa kuwatafutia soko zuri kwa ajili ya mazao yao.

Sasa hivi tunalo tatizo kubwa, wananchi wanataka soko la zao la pamba. Shinyanga, Mwanza, Tabora, Mara na maeneo mengine ya wananchi ambao wanalima pamba, zao la pamba limekosa soko. Wananchi wanalima na kuuza kwa bei ya kutupa, wala Serikali haijajihusisha kujua kwamba kulima kilo moja ya pamba inagharimu shilingi ngapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini inajua mapema kuhusu wanunuzi kwamba wakinunua kwa shilingi 1,100/= wanapata hasara. Sasa wananchi tunawafanya hivyo, huku tunazungumza suala la Kilimo Kwanza? Hatuwezi kuzungumzia suala la Kilimo Kwanza kama wakulima wenyewe hatuwapi motisha waende wakalime. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu isimamie wakulima waweze kupata bei hiyo hiyo ya shilingi 1,100/= kwa kilo ya pamba kuliko ilivyo sasa hivi ambapo bei imeshuka na kuwa shilingi 800/= kwa kilo ambayo ni hasara kubwa. Serikali inaweza hilo na kwa njia za haraka Serikali inaweza kufanya yafuatayo:-

Kwanza ili kuhakikisha kwamba wakulima wa pamba wanapata bei ya shilingi 1,100/= kwa kilo, kama nilivyosema siku ile kama kweli wanunuzi wa pamba yetu, soko la dunia limeshuka kiasi kwamba wao ni lazima wanunue kwa shilingi 800/= kwa kilo. Mimi ninavyozungumza nina experience kubwa na soko la zao la pamba kwamba kila inapofika mwezi wa kumi na moja na uzuri wake, soko hili linaisha mwezi wa tatu. (Makofi)

Kwa hiyo, wanachoweza kukifanya kama Serikali ni kuwapa dhamana hawa, kuwapa insurance ili waweze kununua pamba. Wakiwapa insurance watakuwa na uwezo wa kuongezea ule ukomo wa kukopa, watakapowaongezea ukomo wa kukopa maana yake ni kwamba wanaweza kununua pamba sasa hivi kwa shilingi 1,100/= na wakaiweka stoo mpaka hata mwezi wa kumi na moja ndiyo wana- release. (Makofi)

Lakini wanunuzi wetu kwa sababu ni wadogo na mtaji ni mdogo na dhamana zao ni ndogo hawawezi kununua pamba wakaiweka stoo, wanachotaka wao ni kununua leo, kesho wanauza marobota wanapata fedha tena wananunua kesho. Sasa Serikali ikifanya tu hilo jukumu la kuwadhamini wakapata insurance ambayo itatugharimu, sio fedha nyingi wakanunua pamba hiyo na kuiweka stoo baadaye watai-release na watapata faida lakini bado wakulima wetu watakuwa wamenunuliwa kwa bei iliyo nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo la wananchi wetu wanaofuga, ufugaji hapa nchini imekuwa tatizo. Kwa muda mrefu wananchi wetu hawapati bei nzuri ya mifugo yao. Ng’ombe wanauzwa kwa bei ya kutupa na niiambie Serikali kwamba Mungu alileta zawadi kwa nchi maskini kwa kuwaletea mifugo kama ng’ombe. Ukichinja ng’ombe huna cha kutupa, ngozi inakwenda kwenye viwanda, ng’ombe anakwenda kulima akirudi unakamua maziwa, unamla huku anatembea, samadi ile inatumika kama mbolea, ng’ombe unamla huku anatembea, lakini Serikali tunazungumza kwamba tuna mipango yetu mizuri, tunasema tunataka tuzifungulie fursa tulizonazo ili ziwezeshe kukuza uchumi, wafugaji wetu hawa tumeshindwa kuhakikisha kwamba wanapata soko zuri kwa ajili ya mifugo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nikuambie kwamba minada yangu ya kule Jimboni Kisesa, minada ya Itinje, Senani, Tindabuligi na mingine wanauza pale Maswa wananchi wa Jimbo la Kisesa. Ng’ombe wa kawaida anauzwa sh. 290,000/= akifika Pugu Dar es Salaam anauzwa sh. 451,000/= tofauti ya sh. 161,000/=. Ng’ombe mkubwa ananunuliwa katika minada hiyo niliyoitaja kwa sh. 380,000/=, akifika Pugu anauzwa kwa sh. 608,000/= tofauti ya sh. 228,000/=. Anayenufaika ni mlanguzi na sio huyu mkulima aliyehangaika kumchunga huyo ng’ombe kwa zaidi ya miaka mitano akimpa malisho, maji na hifadhi na sisi tuko hapa tunatunga sheria. Serikali ifanye kila linalowezekana kuhakikisha kwamba viwanda sasa vinajengwa haraka. Kuna ushahidi kwamba kule kwa walio na viwanda ushahidi wa kitakwimu, kwanza niwashukuru sana gazeti la The Guardian, kila wakati wamekuwa wakituletea takwimu ya jinsi ya masoko ya mifugo yanavyokwenda, ni uzalendo wa hali ya juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ushahidi pale popote palipo na viwanda bei ya ng’ombe ni kubwa. Masoko ya Kongwa, Arusha, Dar es Salaam ndio wanaotoa bei kubwa ya mifugo, lakini Shinyanga wazalishaji wa ng’ombe karibu kila mtoto anayezaliwa ana ng’ombe mmoja kwa wastani wa wananchi wanaoishi Shinyanga, Kiwanda cha Shinyanga kilishashindikana. Niiombe Serikali ifanye haraka sana. Sasa hivi kuna wananchi wa kawaida wazawa wanaokiendeleza Kiwanda cha Shinyanga, lakini wazawa hawa wanahitaji kuungwa mkono na Serikali. NDC tunayoizungumza leo hii ichukue jukumu la kuingia ubia na wawekezaji pamoja na wakulima hatujaiwezesha vya kutosha. Hawa wawekezaji wa Mkoa wa Shinyanga wanahitaji support ya NDC, wanahitaji support ya wawekezaji wengine wa kuja kuwa-join ili kuhakikisha kwamba Kiwanda cha Nyama Shinyanga kimejengwa na kimekamilika na kimeanza kutoa huduma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha Nguo Shinyanga ahadi kubwa kabisa ya Mheshimiwa Rais na Waziri wa Viwanda na Biashara na Waziri wa Kilimo. Ahadi kubwa ya Mheshimiwa Rais ni Kiwanda cha Nguo Shinyanga na Kiwanda cha Nyama Shinyanga. Simamieni basi mhakikishe kwamba viwanda hivi vimejengwa ili viweze kuongeza thamani ya mazao yanayozalishwa huko Shinyanga, thamani ya pamba inayozalishwa Shinyanga. Hata hili tatizo tunalolalamika leo kuhusu suala la pamba litakuwa limetatulika kama Kiwanda kitakuwa kimejengwa, tutauza wenyewe pale, tutatengeneza nyuzi sisi wenyewe, tutatengeneza nguo sisi wenyewe. Mawaziri msikwepe jukumu la kusimamia bei ya pamba ni la Serikali, msije mkasema kwamba jukumu la kusimamia bei ya pamba ni la watu binafsi. Serikali iwalinde wananchi wake vinginevyo tutakosa wazalishaji. Sasa Waziri kusema kwamba suala la price it’s none of the Government concern. Hii hapana Serikali iwalinde wananchi wake kwa kuwapa bei nzuri za pamba na mazao mengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulijipanga vizuri katika Mpango wetu wa Miaka Mitano. Tuna mambo ambayo tumeyaainisha mle, lakini tunachotakiwa sasa ni umakini wa kutekeleza mambo hayo tuliyoyaainisha katika mpango wetu huu wa miaka mitano. Nilikuwa nazungumzia hapa suala la NDC, NDC kuipa jukumu kubwa la kuingia ubia na wawekezaji au kuingia ubia na wakulima au na wananchi wengine wanaotaka kuwekeza katika nchi yetu, sio suala la mzaha, waliomba shilingi bilioni 24.35, tumeweza kuwapa shilingi bilioni 7.06, sasa bado tunatakiwa kuhakikisha kwamba tunatafuta fedha za kutosha kuhakikisha kwamba hawa NDC wanatuwakilisha vizuri katika suala zima la kuingia ubia na wawekezaji mbalimbali, kwa maana ya kutekeleza dhamira yetu ya PPP kikamilifu. Lakini tukienda hivi tutaendelea kujipanga, tutaishia kujipanga hatutaingia kwenye utekelezaji, tuweke fedha za kutosha. Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imefanya vizuri, Waziri hapa alikuwa anazungumza Viwanda vya Ngozi. Viwanda vya Ngozi nimeona ule ukurasa wa Waziri aliouzungumza kila mahali amesema tu kwamba kuna wawekezaji mbalimbali waliojipanga kuja kuwekeza Viwanda vya Ngozi nchini. Lakini wote wamejipanga tu hakuna hata mmoja aliyekuja kuwekeza. Nimesoma ujenzi wa Viwanda vya Ngozi, Viwanda vya Ngozi vinajengwa kwenye maeneo ambako hakuna ngozi. Wananchi kule Mkoa wa Shinyanga wanazilalia zile ngozi hazina wanunuzi halafu wanunuzi wanalalamika eti wamekosa ngozi nchini, wananchi wanalalia ngozi kule hawana mahali pa kuzipeleka, jenga Kiwanda mahali ambapo raw material inapatikana. Leo Mkoa wa Mwanza hakuna, Tabora hakuna, Shinyanga hakuna, Mara hakuna, halafu wewe unalalamika ngozi hakuna, wakati watu wanalalia hawajui wazipeleke wapi? Maziwa watu wanamwaga hawajui wayapeleke wapi, hakuna wa kuwekeza viwanda hivyo. Leo Serikali inalalamika kwa kufuga ng’ombe wengi, Serikali yenyewe inalalamikiwaje kwa kushindwa kujenga viwanda nchini toka uhuru. Tuwatendeeni haki wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina. Sasa nitamwita Mheshimiwa Deogratias Ntukamazina atafuatiwa na Mheshimiwa Richard Ndassa na Mheshimiwa Naomi Mwakyoma Kaihula ajiandae.

MHE. DEOGRATIAS A. NTUKAMAZINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipa nafasi hii na mimi naomba kwa niaba ya wananchi wa Ngara niweze kuchangia mawazo na labda kuishauri Wizara ya Viwanda na Biashara kwa sababu sekta hii ya Viwanda na Biashara ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kumshukuru Mheshimiwa Rais Dokta Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na ile Tume yake ambayo katika Mpango wa Miaka Mitano wa kwanza wamesisitiza sana kurudisha Viwanda Mama kuwa na basic industries. Hatuwezi kuendelea bila ya kuwa na basic industries. Kwa hiyo, naishauri Wizara hii ifuate ushauri huo na ihakikishe kwamba tunarudisha vile viwanda ambavyo ni muhimu sana. Lazima tuwe na industrial base yetu turudishe viwanda vyetu ambavyo vilifilisika au viliharibika. Turudishe viwanda vya Textiles. Tulikuwa na viwanda vizuri sana vya Nguo, Viwanda vya URAFIKI, MUTEX, MWATEX, SUNGURATEX, KILTEX, POLYTEX. Viwanda hivyo kama vingeendelea kuwepo akinamama wa Tanzania wasingekuwa wanahangaika kwenda Uchina, Dubai kutafuta nguo na nguzo wanazoleta ni hafifu. Turudishe Kiwanda cha Kuzalisha Zana za Kilimo (UFI). UFI ilikuwa inazalisha zana za kilimo na kama UFI ingeendelea kilimo chetu kingekuwa kimepiga hatua kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mchina aliyekinunua Kiwanda cha UFI aliacha kutengeneza zana za kilimo anatengeneza mabomba ya chuma. Sio vibaya kwa sababu mabomba ya chuma hayo nasikia yanapeleka maji kutoka Victoria kwenda Shinyanga, lakini tuanzishe tena Kiwanda cha Kuzalisha Zana za Kilimo ili kuboresha kilimo chetu. Tuwe na viwanda vya chuma. Tulikuwa na Tanga Steel Rolling Mills, Kiwanda hicho kilikuwa kinatengeza vyuma imara na nondo imara. Sasa hivi nasikia nondo zinatengenezwa Kariakoo, nondo hafifu sana. Siku hizi watu wanaojenga nyumba wana matatizo sana na nondo hizi. Kwa hiyo turudishe na tunao mradi wa Mchuchuma, mradi wa Liganga, kwa hiyo, hatuna shida ya chuma turudishe Viwanda vya Chuma. Kwa kifupi nasisitiza kwamba industrial base ndio itatusaidia katika kufikia lengo letu la kuwa nchi ya uchumi wa kati (Medium Income Economy). Nchi unazoziona za China, nchi za Tiger economise za Singapore, Malaysia, South Korea, Taiwan zimefika mahali zilipo kwa sababu ya viwanda, kwa sababu ya kuuza nje mazao ambayo yamezalishwa katika viwanda vyake. Ulaya ilikuwa maskini sana mpaka mwaka 1750 walipoanza industrial revolution wakaanzisha viwanda, ndio Europe sasa inawika kwa sababu ya viwanda. Kwa hiyo, turudishe viwanda vyetu iwe ndio msingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hayo, kabla sijakwenda kuiangalia Wizara hii kwa macho ya Ngara, naomba nizungumzie TBS. TBS ina kazi kubwa sana. Naiomba Wizara iisaidie TBS, kwa sababu inaweka viwango vya uzalishaji, lakini pia inamlinda mlaji. Sasa ukienda Kariakoo kuna viwanda vingi vinatengeneza vyakula fake, vinatengeneza juice fake, wanaagiza vitu vya ajabu, maisha yetu yako katika hatari. Naomba Wizara isaidie suala la TBS ipatiwe uwezo ili iweze kuweka viwango na iweze kufuatilia hawa wafanyabiashara ambao hawana business ethics, hawajali maisha yetu, wanatengeneza vitu vya ajabu na wanaagiza vitu vya ajabu. Lakini nasoma majukumu ya TIRDO na yale ya Tume ya Ushindani, Taasisi hizo mbili nazo zina kazi za kuangalia na kumlinda mlaji. Kwa hiyo, Taasisi hizo tatu zisaidiane ili kulinda usalama wa afya ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niache kwanza mawazo ya ujumla niende kwenye upande wa Ngara. Wizara hii ya Viwanda na Biashara ni muhimu sana kwa Wilaya ya Ngara. Wilaya ya Ngara watu wanasema ni maskini kwa sababu tunaposema kipato cha mtu wastani wa Taifa ni kama sh. 700,000/=, sisi kwetu Ngara ni sh. 240,000/=. Kwa hiyo bado tuko nyuma, lakini Ngara sio maskini, Ngara ina soko kubwa la Rwanda na Burundi. Tukifanya biashara na Rwanda na Burundi tutasonga mbele. Rwanda na Burundi ni nchi ndogo sana, lakini zina watu milioni 19. Rwanda peke yake ina watu milioni 11 na Burundi ina watu milioni nane, tukifanya biashara na hizi nchi tutaweza kupiga hatua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nianze na SIDO. SIDO ilianza mwaka 1973. SIDO ilianza kama Shirika la Kuanzisha na Kuendeleza Viwanda lakini SIDO hiyo haijafika Ngara. Mwaka huu nilikwenda Bukoba kikazi nikatembelea Ofisi za SIDO, nikamkuta Meneja nikamwuliza naomba tafadhali uje Ngara uweze kutoa elimu ya ujasiriamali kuhusu kuanzisha viwanda vidogo. Jibu nililopata lilini-put off kwa Kiswahili sina tafsiri ya put off. Lakini aliniambia Mheshimiwa Ntukamazina hatuna nauli ya kwenda Ngara na hatuna posho ya kujikimu, labda umpigie simu Director General wetu Dar es Salaam Bwana Laizer atuwezeshe kwenda Ngara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa hilo ni jambo la ajabu wa sababu SIDO ninayoijua ambaye ilianza mwaka 1973 ilikuwa inaendelea vizuri, ilikuwa ina wafadhili. Sasa baada ya jibu hilo la Bukoba nililoambiwa na Meneja wa Bukoba nilifanya utafiti wangu mwenyewe nikakuta kwamba SIDO is under funded, SIDO ilikuwa na utaratibu wa kuwakopesha wajasiriamali vifaa vya kufanyia kazi kwa njia ya hire purchase, utaratibu huo haupo. Sasa naiomba Wizara iiangalie SIDO kama ni Shirika muhimu sana. Viwanda Vidogo pamoja na Mradi wa MKURABITA pamoja na SACCOS, VICOBA naviona kwamba ndio ukombozi wa wanyonge wa Ngara na sehemu mbalimbali. Kwa hiyo, naiomba Wizara iisaidie sana SIDO iweze kuja Ngara na sehemu mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuhusu Ngara na Wizara hii, sisi tuko mpakani kama nilivyosema tunapakana na nchi ya Burundi na Rwanda na Congo haiko mbali, hilo ni soko kubwa sana, naomba tuanze rasmi au Serikali iruhusu biashara ya mpakani. Nilishazungumza na Mheshimiwa Waziri Mkuu akaniambia alishaunda Tume ya Kumshauri Kuanzisha Biashara ya Mpakani na bahati nzuri Waziri Mkuu alishafika Ngara akaona jinsi Ngara ilivyo well situated, ilivyo well placed ikipakana na hizo nchi mbili za Burundi na Rwanda zenye watu milioni 19. Kwa hiyo, naomba tuachane na huu mtindo wa kuwa na biashara kupitia njia za panya. Turuhusu biashara ya mpakani Karagwe, Kigoma ili tuweze kusaidia hizi nchi. Hizi nchi ni ndogo sana hazina ardhi lakini zina market kubwa sana, watu ni wengi sana. Ngara tuna hekta 300,000 ambazo ni arable land, lakini tunalima, sasa hivi hekta 50,000. Katika Kilimo Kwanza tunaweza tukaongeza kilimo na tukiruhusiwa kuuza katika hizi nchi watu watapata motisha na tutaweza kufanya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine kuhusu Wizara hii pamoja na Ngara ni kuanzisha Masoko ya Kimataifa kwa sababu ya market kubwa sana ya Rwanda, Burundi pamoja na Congo. Kuna soko la Kabanga ambalo limesharuhusiwa, lakini kuna sehemu zingine za Murusagamba na Bugarama ambapo tunaweza kuanzisha hayo masoko. Kwa hiyo, hiyo nayo ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ambalo linahusu Wizara hii ni mgodi wa Kabanga Nickel. Kabanga Nickel ni mgodi wa pili katika ukubwa duniani baada ya ule wa Canada. Ukisaidiwa na Wizara mbalimbali, kwa mfano karibu wanaanza kujenga mgodi, wanasubiri enviromental impact assessment wakishaanza wataajiri watu 5,000. Lakini pia kama nilivyosema tunaanzisha Viwanda vya Chuma, kazi kubwa ya nickel ni kuchanganywa na chuma ili kuzalisha chuma cha pua (iron steel) na hiyo tutaihitaji sana tutakapokuwa na viwanda vyetu vya chuma. Kabanga Nickel inazihusu Wizara mbalimbali na nimekuwa nikizungumza na Wizara mbalimbali kwa mfano, tunahitaji barabara ya lami ambayo leo nilitaka kumwuliza swali Naibu Waziri wa Ujenzi kutoka Munzani kupita Rulenge kwenda Murugalama barabara hiyo itaweza kutumiwa na Kabanga Nickel kwa ajili ya kubeba mizigo, lakini pia nimeshazungumza na Waziri wa Uchukuzi kuhusu reli ya Isaka, Keza, Rwanda-Burundi ambayo itasaidia kubeba mizigo ya Kabanga Nickel.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Wizara ya Nishati na Madini ni muhimu sana kwa mgodi huu ambao ni muhimu sana kwa Taifa, mgodi huu utakapoanza kazi utahitaji umeme wa megawati 30. Mradi wa Rusumo ambao ni nchi tatu zinashirikiana na nilikuwa nimeambiwa unaweza kuwa tayari mwaka 2013, utakuwa unatoa megawati 20 kwa kila hizo tatu. Kwa hiyo, hautoshi kwa mgodi huu wa Kabanga Nickel itabidi TANESCO iwezeshwe waweze kuwapatia megawati 30. Kwa hiyo, Wizara ya Viwanda na Biashara ni muhimu sana kwenye Wilaya yetu ambayo iko mpakani ina soko kubwa za hizi nchi mbili au nchi tatu tukiweka na Congo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niungane na Waheshimiwa Wabunge waliochangia jana kuhusu kurudisha Tume ya Bei. Tume ya Bei ilikuwa imeanzishwa mwaka 1973. Niliwahi kuwa Katibu wa Scope nasimamia Mashirika yote ya Umma 425. Sasa kwa nini ilivunjwa? Ilivunjwa kama Mashirika mengine yalivyofilisika tukaanzisha Privatisation. Yote ni sera za mtu aliyekuwa anaitwa Ronald Reagan pamoja na dada yake Margareth Thutcher, Waziri Mkuu wa Uingereza walipoingia madarakani late Seventeen’s pamoja na early eighties wao ndio walibadilisha kabisa kwamba Public Sector is ineffective, is inefficient, wakati sio kweli. Kuna wakati ambapo Rais wa Benki ya Dunia alikuwa anaitwa McNamara alimsifu Baba wa Taifa Nyerere na Public Sector yake akasema: “It was a success story”.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sehemu zote duniani hata India, Brazil zote zilikuwa na Public Sector. Lakini hao Conservatives wawili walipoingia madarakani Reagan na Margareth Thatcher ndio walioua Mashirika yetu wale vijana ambao mko wadogo hamjui historia. Hao ndio walioua Mashirika yetu na wakasema tuanzishe Privatization. Sasa Tume ya Bei nayo ikaingia kwenye mkumbo huo ikafa. Lakini tukumbuke kwamba sisi lengo letu au dira yetu ile 2025 tumesema ni People Centred Development. Kama ni People Centred Development Serikali haiwezi ku-abdicate responsibility ya Macro Economic Management. Responsibility ya kuhakikisha kwamba wananchi hawadhulumiwi na wafanyabiashara. Sasa hii Market economy waliyokuwa wanaisifu Margareth Thutcher na Reagan imewaaibisha kuanzia mwaka 2007. Wameaibika sana hawa watu baada ya hii Global Financial Crunch waliona kwamba hizi ni market failures. Baada ya mortgage kushindikana kwenye Housing na wenyewe wameona kwamba market economy is not the most efficient. Kwa hiyo, turudishe Tume ya Bei iweze kusaidia ku-regulate without stifling. Sasa Kiswahili sikijui. Ku-regulate without stifling the Private Sector ili wananchi wetu waweze kulindwa, walaji wetu waweze kulindwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na mambo mengi kama nitapata nafasi nyingine.

MWENYEKITI: Tutakuomba siku moja uje utoe semina juu ya jambo hilo. Hiyo ndiyo michango ya watu wenye uzoefu mkubwa katika Taifa na ni vizuri kuwatumia. Nakushukuru sana kwa mchango mzuri. (Makofi)

MHE. RICHARD M. NDASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa nafasi hii ya asubuhi nami nichangie hoja iliyoko mbele yetu. Lakini, la kwanza, naiomba Serikali, bahati nzuri Waziri wa Maafa yupo ndani humu pamoja na Waziri wa Kilimo. Mlitupatia barua tarehe 11 Julai, kutupa taarifa ya chakula. Lakini mpaka jana chakula cha njaa kilikuwa hakijafika. Kwimba iligawiwa tani 2589.1, tani 258 kilikuwa ni cha bure. Lakini, pia Mheshimiwa Waziri Mkuu alituambia tutapewa na pesa za kusafirishia hiki chakula, lakini mpaka jana pesa hizo zilikuwa hazijafika Benki. Naiomba sana Serikali, kwa sababu hii ni ahadi na wananchi wa Wilaya ya Kwimba wana njaa. Kwa hiyo, naomba chakula hicho kipelekwe haraka ili kusudi wananchi wetu waweze kupata chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, juzi ilikuwa Siku ya Nane Nane, Sikukuu ya Wakulima Tanzania. Wananchi wengi waliweza kusherehekea. Lakini, Nane Nane hiyo kwa wakulima wa pamba wa Mwanza, wakulima wa pamba wa Shinyanga, Mara na Kagera, wamesherehekea Nane Nane kwa kukopwa mazao yao. Mbali na kuuziwa shilingi 1,100/= bei ya awali, elekezi, wamekopwa. Lakini mbali na kukopwa, pesa hiyo hawajalipwa hizo shilingi 800/=.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi tunaotoka kwa wakulima wa zao la pamba siyo kwamba tunasema hivi hivi tu, hapana, iko shida kweli kweli. Unakopa, lakini bei ni ya chini. Una shida ya chakula, una shida ya kulipa kitu fulani, lakini unakopwa. Lakini, Serikali tunapoiomba, itoe basi angalau tamko. Tunao Wakuu wa Wilaya, tunao Wakuu wa Mikoa, hivi kuwaambia tu kule jamani ee, sasa hivi wakulima wa zao la pamba, wamelima pamba yao, tunaomba wasikopwe, nalo ni shida! Lakini tukumbuke zao la pamba linalimwa na Mikoa 13 Tanzania, Wilaya 42, si chini ya wananchi milioni 14 wa nchi hii. Tukichukulia zao hili hivi hivi, kwa kweli tutakuwa hatuwatendei haki wananchi hawa milioni 14. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la pamba siyo sawa na korosho, maana naona kuna utaratibu hapo wa kujumuisha mazao. Zao la pamba haliliwi, siyo sawa na korosho. Korosho ukiitoa tu kule unaweza ukaila. Pamba huwezi ukaila. Kahawa unaweza ukaila, lakini pamba huwezi ukaila. Sasa tusijumuishe mazao as if kwamba pamba ni sawa sawa na korosho, hapana! Pamba ni zao lingine tofauti kabisa! Naishauri sana Serikali iwe makini. Lakini tunaposema hapa, mnaona kama vile, nafikiri hawa…kwa sababu…, hapana! Wakulima wetu wa zao la pamba wa Mikoa hiyo wanapata shida kweli kweli. Toeni basi tamko hapa na ningeomba sana ikiwezekana leo kama mnaweza mkaenda mkakaa kule, mkaja humu ndani, mkasema kwamba bei ya sasa iwe shilingi 800/=. Sijui Serikali nayo imekuwa Wakala wa Bodi ya Pamba, sijui. Lakini labda inawezekana imekuwa Wakala kwa sababu Serikali inakuja humu inatangaza bei, lakini hapo hapo inasema sisi hatutangazi bei. Naomba sana, narudia, narudia kwa uchungu kabisa, naomba Serikali itamke, itoe tamko kwa Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya kwamba kuanzia sasa wakulima wa zao la pamba wasikopwe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili ni kuhusu Kilimo Kwanza; Bila viwanda hakuna kilimo kwanza, kilimo kwanza bila masoko hakuna, kilimo kwanza bila bei yenye uhakika hakuna kilimo kwanza kwa sababu mtu anapolima anategemea bei yenye uhakika, masoko yenye uhakika. Lakini unapolima lazima uwe unategemea viwanda. Nakumbuka wakati Mheshimiwa Rais anafungua Nane Nane alisema, sasa ni wakati muafaka wa kusindika mazao yetu. Niiombe Serikali, niko hapo hapo kwenye zao la pamba, nitacheza hapo hapo, siendi mbali, mfanye utaratibu mzuri wa kuanzisha viwanda vya nyuzi, tusipige longolongo, tuamue. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, alikuwepo, Mheshimiwa Rais alipokwenda kuzindua kiwanda (ginnery) tarehe 27/07/2007, ginnery inayoitwa Sagala Ginnery Limited, alitoa ahadi kwamba tutoke sasa kwenye kutengeneza marobota, twende kwenye kutengeneza nyuzi pamba. Mtu huyu amekuwa akileta maombi siku nyingi, Waziri wa Viwanda na Biashara unafahamu. Tukipata viwanda vya nyuzi viwili, viwili tu kwa kuanzia, pamba yetu itapata soko, itapata sehemu ya kupeleka, wananchi wetu bei itapanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalishaji kwa Mikoa yetu hauzidi marobota 700,000. Kila kiwanda cha nyuzi kikichukua marobota 200,000, marobota 300,000 ndiyo tutapeleka nje, hivi tunasita nini Serikali? Mwekezaji huyu tayari eneo analo, tatizo ni Serikali kutoa guarantee. Angekuwa ni Mhindi, guarantee ingetoka, angekuwa ni Mzungu, guatantee ingetoka, lakini kwa sababu ni mtu mweusi anazungushwa kushoto na kulia, mbele na nyuma, mwishowe atakata tamaa. Serikali itoe guarantee ili kusudi Tanzania tuwe na kiwanda cha nyuzi, tuwaokoe wakulima wetu wa zao la pamba. Kwa kuanzia, tunaweza kusema hebu tuanze na huyu aliyeonyesha nia, mzawa, Mtanzania, vinginevyo, pamba yetu itaendelea kudidimia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali tupunguze urasimu, maana mtu huyu mara anaambiwa nenda Uwezeshaji, nenda Ikulu, nenda Wizara ya Viwanda, nenda huko. Hebu tufike mahali tuamue, tukwamue zao la pamba. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali, nafikiri kuna kujichanganya. Nawaheshimu sana Mawaziri, inawezekana Serikali nayo kwa sababu inaongozwa na watu, labda kuna kupitiwa. Serikali ilitoa tamko hapa kuhusu suala zima la mizani. Suala la mizani ambalo lilitolewa GN na Waziri aliyekuwepo wa Viwanda, katika maelezo yake Waziri Mama Nagu alisema: “Aidha, katika kuhakikisha wafanyabiashara wanatumia vipimo sahihi, ili kumlinda mlaji, Wizara kupitia Tangazo la Serikali (Government Notes No.233) la tarehe 3 Julai, 2009, ilipiga marufuku matumizi ya mizani ya aina ya Steel Yard baada ya kubainika kuwa mizani hiyo ni rahisi kuchezewa na hivyo kuwaibia wakulima hasa wakati wa ununuzi wa pamba. Utekelezaji wa Sheria ya kupiga marufuku mizani ya aina hiyo utaanza kutekelezwa msimu wa ununuzi wa pamba 2011/2012” ambao ndio unaoendelea huu. Sasa hapa inawezekana ni kuchanganya tu. Sheria hii au Government Notes hii haijabadilishwa mpaka leo. Lakini Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika alipokwenda Mwanza, hakutekeleza, hakusimamia Waraka huu. Nashauri Serikali mbadilishe Waraka huu kwa sababu mizani ya Yard Steel bado inatumika badala ya digital. Kwa sababu ilisahau, basi ibadilishe ili kuhalalisha mizani. Jioni wakati Waziri ana-wind up, naomba anijulishe kama tumefikia wapi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la mizani, niwaombe sana watu wa mizani, wananchi wetu bado wanaendelea kuibiwa kupitia mizani hii. Sasa, unapunjwa bei, unakopwa, halafu mzani nao unakuibia. Hivi huyu mkulima wa zao la pamba kweli tunamtakia haki? Sijui, Serikali sijui inatetea nini, visingizio vingi tu. Hivi hawa wakulima wa zao la pamba, Serikali yao imewakosea nini? Mzani huu, kila siku unatetewa tu mzani! 2009/2010 kwenye bajeti ya Waziri wa Viwanda ilitamkwa mzani, 2011/2012 utatamkwa mzani huo huo, Waziri anatoka hapa anakwenda kusema mzani huu huu uendelee kutumika. Tumechoka kunyonywa na mzani huo! Serikali lazima ichukue maamuzi, wafanyabiashara hawa wana mambo yao. Kama unataka tuendelee kuibiwa, sawa, lakini siku ya siku wakulima wa zao la pamba watakapocharuka, sijui nisemeje, ngoja niishie hapo! (Kicheko/Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, kwa sisi Wakristo tuna ile sala ya kuungama:- “nakuungamia Mungu Mwenyezi……” Unakwendaaa……. “Nimekosa mno kwa mawazo, kwa maneno, kwa vitendo na kwa kutotimiza wajibu”. Serikali timizeni wajibu wenu, fanyeni kazi kwa vitendo ili haya malalamiko tunayolalamika humu yaweze kutoka. Yatosha. Naunga mkono hoja. (Makofi)

MHE. NAOMI M. KAIHULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana pamoja na Wabunge mnaonisikiliza. Napenda nimshukuru Mwenyezi Mungu kwa kunipa nafasi hii na afya njema kuweza kuzungumza na Bunge lako Tukufu. Sifa na utukufu vimrudie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ningependa kujadili kidogo katika hii Wizara ya Viwanda na Biashara ambayo mimi mwenyewe ni mmojawapo katika Kamati yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninayo kama mambo matatu hivi ambayo nitayazungumza. Jambo la kwanza, naomba nianze kwa kusema, suala la bajeti ni suala la kupanga. Kama tulivyokwishakwambiwa na tulivyozoezwa na tulivyokuzwa kwamba kupanga ni kuchagua, ndiyo maana kukawa na vipaumbele, mara tukasema kilimo kwanza na vitu vinavyofuatia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini naomba kwamba Waheshimiwa Wabunge wote, sisi kama Wabunge, unajua tuna jina moja la ukoo ambalo ni Wabunge, ambao tunakotoka huko wananchi wanasema hivi hawa Wabunge walikuwa wanafanya nini huko ndani? Kwa hiyo, hapa hatukwepi, hawasemi Mbunge wa CHADEMA, hawasemi Mbunge wa NCCR wala wa CCM, wanasema tu Wabunge kwa sababu tunakuwa hatujaandikwa majina juu ya vipaji vyetu. Kwa hiyo, tunapofanya maamuzi wakati huu, tufanye maamuzi ya kama Wabunge sawa na mtoto wako kwenye ukoo akikosa watamsema kwa jina lako: “Aah, mtoto wa fulani bwana ana tabia mbaya”. Sasa sisi tufanye kazi ya viapo tulivyoapa na Mungu atusaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ya Viwanda na Biashara, kwa kweli ni Wizara mojawapo ambayo ni nyeti, ingeweza kuchukua hata namba moja katika kipaumbele kwa sababu inagusa, yaani ni take off ya vitu vingi ambavyo viko katika mpango wa miaka mitano wa maendeleo wa kukuza uchumi. Kwa sababu tunajua kabisa kwa ukweli kwa uhalisia kwamba bila uchumi ambao ni imara hakuna maendeleo. Kwa hiyo, hapa hatuwezi kuzungumza vitu vya maneno maneno tu, tunazungumza vitu vya uhakika na vya hasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kwanza niunge mkono hotuba na mapendekezo yaliyotamkwa na Kamati ya Kudumu ya Viwanda na Biashara. Mapendekezo yake yaliyotolewa mle yazingatiwe kwa umuhimu sana wakati huu. Pia bahati nzuri safari hii hata hotuba ya Upinzani pia iliweza kutambua mambo yale yale ambayo pia yalikuwa yamewekwa kule. Kwa bahati nzuri hata Wizara yenyewe iliyaona haya mambo lakini ikazidiwa katika kupangiwa bajeti. Kutokana na hivyo, napenda niseme hivi, siwezi kuunga mkono hii bajeti kama ilivyo kwa sasa hivi kwa sababu gani? Kwa sababu mambo makubwa ambayo kweli ndiyo ya bajeti ya kupanga kwa vipaumbele hayajazingatiwa. Kwa hiyo, naomba tu tuitendee haki nchi hii na wananchi wa Tanzania kwa kufanya kitu kilicho sahihi, nacho ni hiki, kwamba, tuwarudishe hawa Viwanda na Biashara siyo kwa kuwa tunawachukia, kwa kweli hatuwachukii, wamefanya bidii sana, ila tuwarudishe kwa wenzao wakawasaidie kupanga upya, kuongeza. Safari hii sisi kama Bunge tunafanya kazi yetu kama Bunge kwa sababu tunaletewa hapa siyo ku-rubber stamp. Tunaletewa na sisi tuone jinsi gani ambavyo kitu hiki kinaweza kikafanya kazi, kikatupa heshima kwa wananchi tunaowasimamia. Kwa hiyo, turudishe hii bajeti wakaongezwe kwenye mambo muhimu ambayo tumeyatambua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, hatuelewi kwa nini NDC inashindwa kuwezeshwa. NDC iliomba bilioni 46, ikapewa bilioni saba. Jamani! Sasa hapa inakuwa kichekesho kwa kweli! Katika kupanga, kuweka vipaumbele ndani ya hiyo bajeti, NDC kama ingetendewa kama ilivyosema, ingeweza kufanya maajabu ya jambo mojawapo ambalo linatusumbua sana nalo ni suala la umeme. Kwa hiyo, NDC yenyewe inasema kwa sababu katika miradi yake ile mitatu ya Mchuchuma, Liganga na kule Ngaka, katika mpangilio mahsusi pamoja na ubia na wenzake, ingeweza kuzalisha umeme MW600 katika muda mfupi, siyo mrefu. Hii siyo tena ile ya kwamba tulikwenda kuazima vitu, ahaa, hii ingekuwa ya kudumu na ingekuwa ni kitu ambacho sisi Watanzania wenyewe tunakimiliki, kinakwenda kutegua kitendawili cha umeme usiotaka kupatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, katika hizo bilioni 46 ingeweza kufanya mpangilio wa kuweza kuunganisha msongo wa umeme pamoja na wabia wale wa Sweden kama walivyofanya. NDC ni watu wetu, sasa tunashindwa nini? Naomba sana NDC wapewe hizo bilioni zao hata zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda nizungumzie juu ya SIDO, jamani nyie Serikali ya CCM mnatekeleza Kilimo Kwanza, lakini nashangaa mnashindwa nini kuona uhusiano uliopo kati ya SIDO, Kilimo Kwanza na Miradi ya NDC? Kwamba SIDO inatoa ajira, SIDO inataka kutapakaa Tanzania nzima, SIDO inataka iwe na mitaa mpaka huko vijijini ili watu wabaki huko vijijini. Ukiunganisha kazi ya SIDO na mkiwawezesha na wenyewe waliomba bilioni 11 tu nyie mnawapa shilingi bilioni moja. Hivi kweli jamani? Hivi mnasema kweli au mnatutania? Ngoja niwaambieni nyie Serikali ya CCM. Serikali ya CCM nyie ni ndugu zetu, Serikali ya CCM tumewaweka mstari wa mbele vitani, sasa kama nyie ni askari wa mstari wa mbele mnakwenda kufanya vitu vya mchezo mchezo kwa nini? Mtu anaomba shilingi bilioni 11 na anakwambia vitu vizuri kabisa na nyie si ndiyo mmeapa kwamba mnataka kuondoa tatizo la ajira. Tatizo la ajira ambalo straight away linaondolewa kwa kuiwezesha SIDO. Iwezesheni SIDO iondoe tatizo sio kwa maneno. Sasa hivi sio wakati wa maneno, sasa hivi ni wakati wa vitendo, tendeni. Ipeni SIDO shilingi bilioni 11 ifanye kazi, ipeni hela NDC katika miradi yake ambayo ifanye kazi shilingi bilioni 46, sio nyingi ukizijumlisha ni kama 50 au 60. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, fanyeni hivyo kwa sababu naamini tukiwarudisha mtapata pesa tu. Kwa sababu hapa tumekulia katika dini, wana wa Israeli walipokuwa wanatoka utumwani na walipofika Bahari ya Shamu wakaanza kumlalamikia Musa, naye Musa akaanza kumlalamikia Mungu, Mungu akamwambia Musa, una tatizo gani? Una nini humo mkononi? Musa ana fimbo. Fimbo ikafanya maajabu na sisi ndivyo ilivyokuwa. Sasa kwa nini hamtaki kutumia fimbo mliyonayo? Tunayo NDC wako tayari watafanya, SIDO imeweka miundombinu, kwa nini tunashindwa kuvitumia hivi vitu jamani! Jamani tumerogwa? Naomba sana waombezi wote Watanzania wanaoliombea Bunge hili na wanaiombea nchi hii watuombee. Kama tumefunikwa na pepo la kutoelewa litoke. Naomba sana waombezi msikome kuomba katika dini zote kwa sababu huu ni ufumbuzi tuwarudishe hawa jamaa waende zao wakapange wapewe pesa na zitapatikana. Mnakumbuka kuna pesa kule Wizara ya Ujenzi. Nashangaa wenyewe walipata mpaka za ziada zipo zipo tu, kama vile ambavyo waliwagawia kidogo ndugu zetu wa Uchukuzi bado zimebaki kule. Bunge hili ndilo ambalo linaweza likaweka taratibu ya jinsi ya kuwagawia. Kwa sababu hii ni take off.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ngoja niwaambie ndugu zangu. Bahati nzuri ni Mwanaharakati lakini pia ni Mwalimu. Hili suala la NDC na SIDO tunasema ni hitaji mkakati, strategic need. Ni suala la mkakati kwa sababu gani. Ukitumia na kuwawezesha hawa watawawezesha na wengine. Ukimwezesha NDC hasa kwenye mpango wa chuma kikaja na umeme ukaja, unawezesha viwanda, unawezesha kilimo, unawezesha ajira, unawezesha maendeleo, maendelo in the new sense ya development. Naomba sana tuwarudishe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu na mwisho nimezungumzia NDC, nimezungumzia SIDO nataka nizungumzie sasa biashara ya viwanda vyetu. Nimesoma, wamesema wameshafanya kazi nzuri tu ya kufanya tathmini na ufuatiliaji na bahati nzuri wakaweza, wakavitenga viwanda vingine hivi vilifanikiwa na hivi havikufanikiwa, sawa sijui kama hiyo ripoti yao ya tathmini walituletea. Kama hawajatuletea watuletee, lakini ninachotaka kuzungumza ni hili tatizo la Serikali na hili tatizo lisipoondoka, nawaambieni Wabunge, tusipoliondoa hili tatizo la Serikali, tukakaa kuilinda Serikali ya CCM, tukalinda uzembe mchelea mwana kulia, hulia nani? Tutalia, mimi sitaki kulia. Kwa hiyo, lazima katika Serikali wanaposhughulika na wafanyabiashara, wafanyabiashara wasiwaweke mifukoni. Serikali nyie mmewekwa mfukoni, sijui kwa nini? Au kuna wafanyabiashara ndani yenu mnapopanga mambo wamo wanaowafanya hivi na hivi? Sikiliza vile viwanda mtu anapofanya vurugu ni kazi ya Serikali. You are state power na ndiyo maana tumeweka madaraka na mamlaka kwa Rais. Ngoja niwaambie mifano tunayo, Mungu amrehemu Baba wa Taifa, Marehemu Julius Nyerere. Kama mtu ameishinda Serikali yeye anamwambia kwa mamlaka yake kwa faida ya nchi na kwa mamlaka aliyopewa anamweka ndani na kumpuzisha huko. Ni mhujumu ili nchi ipone. Sasa nashangaa nyie mmekaa hapo wako wafanyabiashara tunaona. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaambia hii Bajeti ni ya kwanza, Bajeti ijayo sisi tunawafanyia mkakati na bahati nzuri mna upinzani ambao ni strong this time. We are not going to joke with you. Hakikisheni kwamba matatizo yale ambayo yapo ya watu ambao wanataka kuwaweka mfukoni kama ilivyotokea katika mafuta, humo humo ndani watu hawataki kufanya mnavyoagiza kwa mfano sukari. Kwa nini sukari mpaka sasa bei inapanda juu badala ya kushuka? Serikali mnaweza kutuambia, halafu nyie mkae hapa, jamani Wabunge ndugu zangu tuna heshima nyingi. Mimi ni Mwalimu wa muda mrefu siwezi kupoteza heshima yangu wakati niko Bungeni. Tunapaswa tulinde heshima zetu, kila mmoja wetu ana heshima, tuzilinde. Serikali mliagiza kupitia kwa Waziri Mkuu akatamka kwamba, bei ya sukari ishuke, lakini mpaka leo bado inapanda? Sasa na viwanda ni hivyo hivyo, tunataka tujue Zana za Kilimo Mbeya imefikia wapi? Kiwanda cha UFI kimefikia wapi na viwanda vingine vilivyokufa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsanteni sana, naomba mengine mje nitawaeleza. Mbarikiwe. (Makofi)

MHE. ISMAIL A. RAGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Awali ya yote kwanza napenda kuwapongeza wale wote wanaofunga Mwezi huu Mtukufu wa Ramadhani na kuwatakia kheri na baraka ili Mwenyezi Mungu awajaalie. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii naunga mkono Wizara hii hasa nikinukuu ukurasa wa 38 wa Hotuba ya Waziri aliposema: “Wizara kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika imefanya utafiti kuwezesha kupata soko la tumbaku ya Tanzania nchini China, Uturuki na Iran”. Jambo hili kwa kweli napenda kuipongeza Serikali yangu kwa kazi nzuri ambayo imeanza kuifanya. Lakini kubwa kuliko yote ningependa kuchukua nafasi hii kuipongeza Serikali pamoja na Chama changu cha Ushirika hasa Mwenyekiti wangu ambaye ni Mbunge wa Mpanda anayeshughulikia masuala ya tumbaku, Mheshimiwa Selemani Kakoso kwa kusimama kidete na kuhakikisha kwamba tumbaku yote ambayo tumelima mwaka huu ambayo inafika takriban kilo milioni 120 Serikali imekubali kununua yote, I mean wale wanunuzi wa tumbaku. Nawapa hongera sana.

Mheshimimiwa Mwenyekiti, ndugu zangu tumbaku kwa kule Tabora ni uti wa mgongo. Sasa hivi viwanda ambavyo tunategemea vinavyosindika tumbaku viko Morogoro. Uwezo wake wa kusindika tumbaku pale Morogoro ni kilo milioni 80 tu basi. Mwaka jana ilibidi zaidi ya kilo 16 milioni ziende Malawi kusindikwa. Kwa maana hiyo basi, viwanda hivyo vya tumbaku ambavyo viko Morogoro vimezidiwa uwezo kutokana na uwezo wa kulima tumbaku. Ukizingatia Mkoa wa Tabora ndiyo unaolima tumbaku kwa asilimia 63.5, ni wakati muafaka kwa vigezo hivyo kufikiria sasa kuweka kiwanda kingine cha tumbaku pale Tabora kwa kushirikiana na Vyama vya Ushirika. Bila kufanya hivyo kwa kweli tutakuwa hatuwatendei haki wananchi wa Mkoa wa Tabora. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, bahati mbaya yupo, sipendi kumtaja jina lake. Yuko mama mmoja anatumiwa sana na NGO kuvuruga soko letu la tumbaku kule nje. Anakwenda kwenye vijiji na Serikali inamwangalia, anatafuta wale wakulima wadogo kabisa ambao wana matatizo anapiga picha na kupeleka nje kusema hayo ndiyo maisha ya wakulima wa tumbaku. Si kweli hata kidogo. Namwomba aje Tabora aone wakulima wa tumbaku wanavyoendesha pikipiki, magari na baiskeli kwa raha mstarehe na nyumba nzuri za kisasa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, njia ya kuwaokoa wananchi wa Tabora ni kuhakikisha kwamba sasa tunapata Kiwanda cha Tumbaku. Pale Igunga, napenda kuongelea juu ya Manonga ginnery, kiwanda hiki hakifanyi kazi tangu mwaka 1992, mpaka sasa ni takriban miaka kumi. Kiwanda hiki ni muhimu sana kwa wakulima wa pamba kwa sababu ginnery yenyewe ni kubwa mno, lakini nimesoma hapa kwenye Hotuba ya Mheshimiwa Waziri ukurasa wa 13 juu ya Benki ya TIB: “Kuimarisha kifedha Benki ya Rasilimali Tanzania ili kiwe chombo madhubuti cha kuchochea mapinduzi ya viwanda nchini kwa kutoa mikopo ya muda mrefu na riba nafuu kwa wawekezaji wakubwa, wa kati na wadogo nchini kote.” Kiwanda hiki kina milikiwa na Chama cha Ushirika cha Nzega na Igunga. Hivi Serikali inashindwa nini kusaidia wakapata mkopo halafu kiwanda hiki kikaanza kufanya kazi. Nitamwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuwa ana-windup akubaliane nami nimpeleke Igunga pale Manonga akaone uzuri wa kiwanda hicho, mpaka leo wananchi wanakiangalia vizuri ili aweze kuwasaidia hawa ndugu zangu wa Igunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora Wallah! tuna matatizo mengi. Lakini Serikali yetu naamini safari hii ni Serikali sikivu na hasa kwa sababu inaongozwa kwa Chama cha Mapinduzi, tulikuwa na kiwanda kizuri sana cha Asali pale Kipalapala, tukiuza asali nje kwa jina la Queens Honey. Sasa fikiria jina la Queens Honey inapewa asali ya Tabora, lakini sasa kiwanda hicho kimekufa wala hatujui hatma yake itakuaje. Kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri aangalie suala hili atatusaidia vipi ili ndugu zangu wa Kipalapala Wamishionari ambao kwa kweli walifanya kazi kubwa sana kuwashawishi wananchi kuweza kushikamana na kuzalisha asali hii. Tulikuwa na kiwanda cha maziwa pale kinaitwa Nyamwezi Creameries, tulikuwa tunapata maziwa, tunapata pale na sisi wenyeji wa Tabora tunaita Mbowoto yaliyoganda barabara yana cream safi, fresh milk unapata batter, unapata jibini si ndiyo cheese hiyo? Lakini sasa hivi viwanda vyote hivi vimekufa. Tena cha kusikitisha wakati nasoma Shule ya Msingi Urambo Extend School kulikuwa na kiwanda pale cha Tanganyika Parkers cha kusindika embe kwenye kopo na chenyewe kikang’olewa kikapelekwa Dar es Salaam. Yaani tunaonewa Tabora jamani, sijui mnatutaka nini? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nakuja kwenye jambo ambalo namwomba Mheshimiwa Waziri atulize masikio yake vizuri. Kwanza nimewasikia Waheshimiwa wa Kanda ya Ziwa ndugu zangu wanaolima pamba ambao wanataka kiwanda cha nyuzi. Tabora sisi tuna kiwanda cha nyuzi, lakini kimefungwa tangu tarehe 25/11/2010 mpaka leo hakizalishi, kisa tulikosa malighafi. Wafanyakazi walikuwa 350 na walikuwa wanafanya kwa shift tatu saa moja asubuhi mpaka saa tisa, saa tisa mpaka saa tano usiku, saa tano usiku mpaka saa moja ya asubuhi. Kiwanda kile kilikuwa kinafanya kazi masaa 24 na nyuzi zile zilikuwa na ubora wa hali yake. Zilikuwa zinasafirishwa kwenda Colombia, Uturuki, Ujerumani, India, Mauritius na nchi nyingine. Lakini sijui kaingia mdudu gani pale kile kiwanda kimefungwa, hatima yake hatujui.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitamwomba Mheshimiwa Waziri atakapokuja kutoa maelezo hapa basi ajaribu kuwaeleza wananchi wa Tabora angalau basi hata hiki kiwanda chetu kimoja kufanya kazi. Sasa cha kuchekesha, kiwanda hiki kilivyokuwa kinakufa, kilifika mahali kikawa na wafanyakazi 74, kikaendelea kikabaki na wafanyakazi 11. Sasa hakina mfanyakazi hata mmoja na kimefungwa kabisa na hatujui kitafunguliwa lini. Baya zaidi wafanyakazi hawa 350 wamedhulumiwa pesa zao za PPF, wamekatwa mishahara yao lakini mpaka leo mimi Mbunge wao wote huu nimejaribu kuongea na PPF, Mkuu wa Kanda ya Mwanza nimeshindwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali wajaribu kuona suala hili watatusaidiaje? Kwa sababu kuwanyima watu haki zao hasa baada ya kukatwa pesa zao, hii ni dhambi kubwa sana. Sidhani kama Mungu atawasamehe na mimi nasema katika kipindi hiki cha Mwezi wa Ramadhan hao watu wanaodhulumu watu Wallah Subhanah Wataala, naomba uwaangamize kabisa. Haiwezekani mfanyakazi anakatwa hela na PPF, halafu leo halipwi pesa yake maana yake nini? Naamini kabisa tunayo Serikali sikivu na nina imani kabisa Mheshimiwa Waziri hasa kwa jinsi ninavyokuamini kwa kufuatilia majambo ni hodari. Nilipokuja ofisini kwako kukupigia kelele juu ya soko la tumbaku hukuchelewa kumtuma Naibu Waziri kwenda Iran, hukuchelewa kututuma mimi pamoja na viongozi wengine kwenda kwenye Ubalozi wa China. Kwa hiyo, inaonekana kwamba wewe ni mfanyakazi mzuri pamoja na wenzako na nisimsahau Katibu Mkuu wako ambaye ni mama shupavu pale anasimamia mambo vizuri sana. Pamoja na Kamati ya Bunge inafanya kazi nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naunga mkono bajeti hii mia kwa mia. (Makofi)

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi na mimi niweze kuchangia kwenye Bajeti hii ya Wizara ya Viwanda na Biashara, na kabla sijaendelea na mimi naungana na Mheshimiwa Ndassa kama alivyosema tatizo la njaa, nashukuru sana Serikali kwa kutusaidia tani 1500, lakini nataka kuwaambia kwamba hatujapata mpaka sasa hivi, naomba sana Serikali ifanye haraka. Tatizo la pili ni kwamba accessment iliyofanywa kwenye Jimbo la Solwa wamekosea, Waziri mwenye kitengo hiki nilipenda kuongea na wewe jana na juzi lakini hukuwa na muda na mimi, wamekosea. Solwa ni critical area ambalo tatizo la njaa lipo, lakini tumepata chakula kidogo na kuna maeneo wamepewa chakula kingi wakati hawakuhitaji, ndiyo maana nimesema wamekosea. Lakini naiomba Serikali ifikirie kwa mara ya pili na kuona ni namna gani inaweza kutuongezea chakula.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaanza na suala la EPZ, kama kuna eneo ambalo linaiondoa nchi mahali ambapo inatamani kufika kwenye maendeleo bora ni eneo la EPZ, (export processing Zone). Maeneo mengi na nchi nyingi duniani kuna nchi sasa hivi 120 zipo kwenye mfumo wa EPZ na wamepiga hatua kubwa sana, nchi nyingi duniani zikiwemo za far east, Thailand, Malyasia, China, hapo zilipofikia ni kutokana na mfumo wa EPZ.

Mheshimiwa Mwenyekiti, EPZ maana yake ni mfumo ambao unalenga na unaridhisha wawekezaji wa ndani na wa nje kuja kuwekeza kwenye mfumo ambao utawasaidia wao kuwekeza kirahisi na waweze kuzalisha ama viwanda, manufacturing au sekta yoyote ya huduma kwa ajili ya ku-export. Lengo kubwa ni ku-promote export kwa ajili ya kupata fedha za nje, kwa ajili ya kupata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, EPZ yetu Tanzania sasa hivi ina makampuni 44, asilimia 44 ni ya Watanzania na asilimia 41 ni wageni na asilimia 15 ni joint venture baina ya Tanzania, angalia ni namna gani Watanzania walivyokuwa na mwamko sasa hivi na hata ukienda TIC ukitazama statistic pale Watanzania ndiyo wamezidi foreigner kwa maana ya kuwekeza katika mifumo yote miwili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo ambalo litaikuza nchi ni EPZ kwa maana inatafsiri sasa uchumi bora katika nchi kwa maana ya kununua malighafi au mazao yaliyolimwa na Watanzania kama vile Pamba na kadhalika. Leo EPZ waliomba bilioni 73 lakini pesa waliyopata ni kidogo sana, hatuko serious, sitaki kusema kwamba Wizara hii hatuiungi mkono, tutaiunga mkono, lakini naiomba Serikali ioneshe commitment katika review ya bajeti yake Disemba kama alivyoahidi Waziri Mkuu iseme kwamba tutaisaidia ili iweze kuondokana na matatizo yake na iweze kutekeleza miradi na programu yake vizuri kama ambavyo tumejipanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la pamba ambalo lipo katika Mkoa wa Shinyanga na maeneo mengine yote ya mazao ya biashara, majibu yake yapo EPZ. EPZ ni eneo pekee ambalo linaitoa nchi pale ilipo kufika kwenye maeneo ambayo tayari inapendeza. Sasa hivi makampuni 44 ambayo yamewekeza kwenye EPZ capital yake ni dola milioni mia sita na hamsini ajira iliyotokea mpaka sasa hivi ni elfu kumi na tatu na mia tano na imeanzishwa mwaka 2006, angalia ni namna gani EPZ ilivyopiga hatua kwa muda mchache tu, hivi tukiwa na miaka kumi hadi kumi na tano, nchi kama Kenya EPZ yao wana miaka 20, lakini hatua walizofikia ni nzuri, si nzuri sana kama vile ambavyo sisi tutakavyopiga hatua nzuri kwa sababu nchi yetu ina amani, ina rasilimali na ina vitu vingi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naiomba sana Serikali iwekeze na itoe fedha za kutosha kwenye Wizara ya Viwanda na Biashara katika kitengo cha EPZ. Hatutakuwa na maana wala uchumi wa Tanzania hautakuwa na maana nzuri, katika suala zima la Mpango wa Maendeleo wa Miaka Mitano kama hatutazami eneo hili la EPZ, sina shaka na umeme Serikali itafanya vizuri, sina shaka na maeneo mengine Serikali inashughulikia vizuri, lakini tusipowekeza vizuri kwenye EPZ hakuna maendeleo, tutabaki kuongea tu hapa uchumi utabaki hivi hivi na hakuna maeneo ambayo tunaweza tukajivunia sisi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Makamu Mkurugenzi wa World Bank, Justin alikuja hapa, alifurahishwa sana na jinsi ambavyo EPZ inafanya kazi, nami nampongeza sana Mheshimiwa Dokta Meru amefanya kazi nzuri sana, mpaka ameandikiwa barua na Makamu Mkurugenzi wa World Bank kwamba kazi umefanya vizuri, keep it up sisi tupo na wewe. Kuandikiwa barua na Mkurungenzi kama huyu siyo kazi ndogo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu mwingine ili sasa Watanzania waweze ku-peak vizuri, naishauri sana Serikali kupitia TIB iweze kupanga mwongozo mwingine ili Watanzania wenye kuonesha nia ya kuwekeza kwenye viwanda ambavyo kwa kweli ndiyo vitakavyoitoa nchi yetu hapa kwenda mbele kuwa na masharti nafuu kwenye benki yetu ya TIB, Watanzania waweze kupata mkopo, wafanye biashara, waingie kwenye sekta ya viwanda ili nchi yetu iweze kutoka vizuri kupitia mfumo huu wa EPZ.

Mheshimiwa Mwenyekiti kuhusu SIDO, SIDO ni eneo ambalo linaweza likaajiri Watanzania wengi sana, bilioni moja, siwezi nikasema chochote ndiyo maana nikasema Serikali ioneshe commitment, EPZ ioneshe commitment, SIDO ioneshe commitment pamoja na NDC ambayo litaiongelea sasa hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, SIDO ni eneo ambalo linatoa mafunzo mazuri sana kwa Watanzania, wanakuwa wajasiriamali wadogo wadogo, pale ndipo wanapoanzia, anakwenda anakua na mwishowe anaingia kwenye mfumo wa EPZ na baadaye anakuwa ni mfanyabiashara mkubwa mno. Nchi nyingi hatua hizi ambazo programu za Serikali tumezipanga sasa hivi ndizo zilizowafanya nchi kama Thailand, China ziendelee. Nchi hizi jeuri yao yote ni kwenye mifumo hii yote miwili katika nchi zao. Naomba SIDO, naomba wafikiriwe fedha walizoomba bilioni 11 wamepewa bilioni moja, naomba sasa bilioni kumi hii Serikali ioneshe commitment.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Dodoma tuliwahi kwenda kwenye uzinduzi wa suala la Wajasiriamali waliofundishwa namna ya kutengeneza bidhaa za ngozi, nilifurahishwa kweli, Wizara ilipokuwa inaikabidhi SIDO eneo ambalo vijana wetu wanafundishwa, wanakuwa na ujuzi wa kutengeneza mikanda, wanakuwa na ujuzi wa kutengeneza viatu, kupitia rasilimali zetu za ngozi walifundishwa wengi na inapendeza sana lakini naomba sasa ili SIDO iweze kupanuka nchini ni vizuri waweze kupata fedha za kutosha. Shinyanga tuna ngozi za kutosha na namwomba sana Mkurugenzi wa SIDO afikirie kufanya zoezi hili katika Mkoa wa Shinyanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Solwa, Kata ya Didia, MVIWATA walikuja pale na wakaahidi kujenga soko kubwa sana la mazao kwenye Kata ya Didia. Wamejenga hapa Kibaigwa na sasa hivi nadhani wanajenga soko kubwa sana la mpunga pale Mbarali. Mpaka sasa hivi imesimama, namwomba Waziri wakati anakuja kuhitimisha hoja yake hapa hili soko atueleze hatua zake zimefikia wapi, kwa sababu tunahitaji sana soko hili, ndiyo majawabu ya masoko yetu, ndiyo majawabu ya mazao wanayolima wakulima ili waweze kupata bei nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu NDC, hakuna eneo zuri ambalo Tanzania inaweza ikaondokana na tatizo la umeme kama NDC. NDC wana-program nzuri sana, wameonesha kabisa namna ya quick wins kupata umeme haraka na wa muda mrefu. Lakini inashangaza sana, naungana na Mheshimiwa Kayombo na wenzangu pia hapa kwamba NDC ndiyo eneo ambalo Serikali na yenyewe ioneshe juhudi. Kwa sababu tatizo ambalo tutaondoka nalo sasa hivi hapa, Wizara ya Nishati itakuwa tarehe 13, eneo kubwa na umeme wa uhakika ambao unaweza kupatikana ni NDC peke yake, jenereta hizo ambazo tunanunua ni umeme wa dharura tu na muhimu kuwa nao, lakini NDC wanachotaka sasa hivi ni msongo wa kutoka Ngaka kwenda Songea ambao ni milioni 46.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naona ni kengele ya kwanza.

MWENYEKITI: Ni kengele ya kwanza.

MHE. AHMED A. SALUM: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la ngozi, tulikaa na wadau wa ngozi kwa maana kwamba viwanda vya ngozi walitueleza masikitiko mengi tuliwasikiliza sana na nasema kwa jinsi ambavyo statistics zilizofanywa Tanzania Tanneries Association kuna haja kubwa sana ya kuingilia suala hili kati. Mimi na Kamati yetu tumeunda Kamati Ndogo kufuatilia hili suala, naamini kabisa viwanda vya ngozi watulie sisi kama Kamati Ndogo ya Wizara ya Viwanda tuingilie kati ili tuone tutafanyaje kutatua tatizo la ngozi ili wapate raw material ya kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la bar codes, sisi tulikuwa hatuna bar code, hii ni namba ambayo kila mzalishaji wa bidhaa anapewa inayoelezea information na maelezo kamili ya mazao haya yanazalishwa nchi gani. Namshukuru sana Waziri wa Viwanda amefanya kazi kubwa sana hii, sasa hivi Tanzania bidhaa zitakuwa zinajulika kwamba ni za Tanzania hata Tanzanite ambayo ilikuwa inachukuliwa kupelekwa Kenya na kupata bar code za Kenya na kujulikana kwamba zinatoka Kenya kwa sababu ya Bar code tu. Sasa hivi nina imani kabisa kwa kuwa bar code zinafanyika hapa zitapata namba hapa hapa na bidhaa zetu zitajulikana zinatoka Tanzania hongera sana. Waziri wa Viwanda namshukuru sana, amefanya kazi kubwa, sisi tupo na wewe tutakusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu suala la pamba, tatizo la pamba linalojitokeza kwanza naomba kusema kwamba, kuna makampuni sasa hivi yamenunua kwa deni, kwenye Kata ya Usule, kuna makampuni yamenunua kwa deni, SHIRECU wamenunua, Jambo wamenunua kwa deni na mpaka sasa hivi hawajalipwa, nimejaribu kufuatilia, wananiambia hawana fedha, wanangoja fedha za mkopo kutoka TIB na benki zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ingilie suala hili, suala la kuokoa zao la pamba ambalo linaajiri zaidi ya watu milioni kumi na nne, naomba nitoe ushauri kwa Serikali yetu. Kwanza, hakuna eneo lingine ambalo tungeweza kuokoa zao hili ni kutoa insurance kwa wanunuzi wa pamba wa Tanzania ili wanunue pamba ile wai-stock na wasiiuze mpaka mwezi wa pili, kwa sababu trend inavyokwenda bei ya pamba itapanda tu. Ikipanda bei mwezi wa pili wauze na warudishe fedha Serikalini. India pamba waliyonayo sasa hivi siyo pamba wanayolima wenyewe, wanainunua Tanzania, Sudan na nchi zingine za Afrika, wana-stock ile pamba wakisubiri bei ipande halafu ndiyo wanawauzia China.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali ifanye mazungumzo na Serikali ya China wanunuzi wa pamba wa China waje Tanzania direct ili kuondoa huu ujanja ujanja unaofanywa na baadhi ya wafanyabiashara. Pamba ya India inaonekana ni ya India wakati inanunuliwa katika nchi zingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wa tatu ni kuwa na viwanda. Urafiki inaanza kufa, toeni kiwanda cha Urafiki pale, ongeeni na China tununue share ile, ili kiwanda cha Urafiki kihamie Shinyanga, inafanya nini hapo Dar es Salaam hamna! Hivi Dar es Salaam kuna pamba pale? Dar es Salaam kuna msongamano wa magari tu. Hamisheni Kiwanda cha Urafiki kije Shinyanga ndiyo soko kubwa la uhakika na wengine wote ambao wanataka kuwekeza Waziri wa Viwanda na Waziri Mkuu mnapokwenda nje tuleteeni wawekezaji wa viwanda vya nguo. Watanzania kama wapo sasa hivi wajitokeze tufanye organisation wawekeze katika suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakuna eneo lingine zaidi ya kuwa na viwanda vya nguo ama viwanda vya nyuzi kwenye Mkoa wetu wa Shinyanga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, makampuni yanayonunua pamba sasa hivi yamechaguliwa machache, naiomba Serikali sasa hivi huu ukiritimba ndiyo uliofikisha pale bei ya pamba, lakini kama makampuni mengi yangeruhusiwa, competetion ingekuwepo, hata bei ingepanda zaidi ya mia nane ya sasa hivi. Lakini sasa hivi kuna makampuni machache tu yameteuliwa, kwa hiyo, yakikaa ndiyo hayo hayo waliyofanya kwenye mafuta na suala la pamba ndiyo hivyo hivyo, hivi wakikaa wakafanya cartel, mna haja gani ya kuwazuia? Tulete tena hoja ya dharura tuongee tena, inakuwa kazi Serikali inaposhindwa kufanya, tupitie Bunge na kuishinikiza Serikali ifanye kazi yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja, haya niliyoyaongea, wakati Waziri ana- wind up namwomba sana aeleze vizuri ili tuone tutafanyaje. Nakushukuru sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana, sasa nitamwita Mheshimiwa Opulukwa simuoni, nitamuita Mheshimiwa Mabumba atafuatiwa na Mheshimiwa Mnyaa.

MHE. SYLVESTER MASSELLE MABUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa nafasi hii nami niweze kuchangia hoja iliyopo mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, napenda kumpongeza Waziri, Naibu Waziri na watendaji wa Wizara hii kwa hotuba nzuri ambayo wametuletea. Napenda kuzungumza yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, sekta hii ya viwanda na biashara ni muhimu sana katika maendeleo ya nchi yetu, tukilifahamu hili napenda niishauri Serikali kwamba ili Tanzania iweze kuendelea tunahitaji uwekezaji mkubwa katika viwanda na biashara. Sekta ya viwanda ndiyo mkombozi wa Tanzania kwa njia ya kuweka ajira ambazo zitawawezesha watu wetu kupata vipato lakini wakati huo huo kuweza kulipa kodi Serikalini na kuongeza mapato ya Serikali yetu ili Serikali nayo iweze kutoa huduma kwa watu wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ili tufanikishe kuwa na viwanda vya uhakika, tunahitaji nishati ya umeme wa uhakika. Pasipo umeme sekta ya viwanda haiwezi kufanikiwa. Naomba Serikali ihakikishe kwamba shida ya umeme tunaiondosha baada ya miaka hamsini tusiseme tena habari ya umeme kama ni tatizo katika maendeleo ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niipongeze Serikali kwa nia yake ya kutaka kuwa na one stop service ambayo itasaidia kuondosha urasimu. Kuna urasimu mkubwa sana Mwekezaji anapotaka kuwekeza hapa Tanzania inabidi afuate mzunguko mrefu matokeo yake wanakimbilia nchi za jirani ambazo hazina urasimu kama nchi ya Rwanda. Tuondoshe urasimu ili tuwe na wawekezaji ambao wataweza kuwekeza hapa Tanzania. Tunahitaji wawekezaji waadilifu, wawekezaji ambao kweli watakuwa na mapenzi mema na nchi yetu. Ili tuweze kuwatambua, tunaomba Serikali kwa ujumla wake ikitumia pia vyombo vyake vya dola kuwatambua hawa wanaokuja kuwekeza Tanzania. Kwa sababu wengine wana matatizo kule wanakoondoka katika nchi zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuepuka kuwa na wawekezaji wababaishaji, tunaomba Serikali itumie vyombo vyake vya dola kuwatambua ili mwisho wa siku azma ya kuwa na wawekezaji ambao watasaidia kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi yetu tuweze kuwapata.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali inahitaji pia kuhakikisha kwamba sekta ya viwanda na biashara inashirikiana kwa karibu na Wizara kama ya Kilimo na Chakula kwa sababu Wizara ya Kilimo ndiyo mzalishaji wa malighafi katika viwanda. Tunahitaji kuwa na viwanda ambavyo vita- process mazao ya wakulima. Tumechoka kuuza vitu ambavyo ni ghafi, ambavyo havipati bei nzuri matokeo yake tunanufaisha Mataifa makubwa na sisi tunaendelea kuwa maskini zaidi. Naomba sasa nchi yetu iuze bidhaa ambazo ni refined, processed katika eneo la kilimo kwenye uvuvi, mifugo na kadhalika. Tuna ngo’ombe wa kutosha tukiweza kusindika mazao ya mifugo, Serikali yetu itaweza kupata fedha nyingi za kigeni na hivyo kuweza kusimamia maendeleo ya nchi yetu. Tunahitaji fedha za kigeni kutokana na sekta ya viwanda ambayo itatusaidia kuuza vitu ambavyo vimeongezwa thamani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie kuhusu benki ya rasilimali TIB. Ili TIB iweze kufanya kazi yake vizuri, naishauri Serikali iongeze mtaji katika benki hii na benki hii pia ilenge katika kusaidia wazalendo. Wazalendo wana uchungu na maendeleo ya nchi yetu, tuweke mtaji wa kutosha ili kipaumbele kiwe ni kuwakopesha wawekezaji wazalendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna manufaa ya kuwasaidia wawekezaji wazalendo kwa sababu kwanza wao wataajiri Watanzania wenzao, tofauti na ilivyo wawekezaji wa nje ambao wanakuja na watu wao, kwa hiyo Watanzania wanakosa ajira kutokana na hali hiyo kwamba wawekezaji wa nje wanaajiri watu kutoka nje ya Tanzania. Lengo la Tanzania ni kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata ajira ya kutosha na hivyo tunapotekeleza dira ya 2025 kwamba ifikapo mwaka huo Tanzania iwe nchi yenye kipato cha kati hatuwezi kufikia hapo kama Watanzania wataendelea kuwa wao ni wasindikizaji katika shughuli za uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia niseme kwamba tunahitaji sasa Tanzania ambayo inakuwa ni nchi ya viwanda, viwanda vidogo vidogo. Kwa hiyo, migodi ya chuma kule Mchuchuma na Liganga, naomba Serikali itafute wawekezaji waadilifu ili tuepuke ile aibu ambayo sasa hivi tunayo kwenye madini ya dhahabu, almasi, gesi na kadhalika tumekosea kwenye Mikataba yetu. Sasa Mwenyezi Mungu kwa vile ametujalia kuwa na migodi hii ya chuma basi tuwe na wawekezaji ambao mwisho wa siku Serikali yetu itanufaika. Tunaomba Wizara hii ishirikiane na Wizara ya Uwekezaji kuhakikisha kwamba viwanda vya chuma ambavyo vitaanzishwa Tanzania viwe na wawekezaji waadilifu ambao watalipa kodi nzuri Serikalini na ambao wataajiri Watanzania na ambapo pia watawezesha uchumi wa nchi hii kweli kukua kama dira yetu ya 2025 inavyoelekeza kuwa na uchumi wa kati. Haiwezekani mpaka leo tunaitwa nchi maskini, lakini ukiangalia tuna rasilimali nyingi sana. Sasa rasilimali hizi tuzitumie kwa manufaa ya watu wetu na manufaa ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapozungumza habari ya viwanda basi tujielekeze katika viwanda vidogo vidogo. Viwanda vidogo vinahitaji uwekezaji ambao ni wa kati, unahitaji teknolojia rahisi. Lakini vile vile ni rahisi kuvi-manage. Pia vinaweza kuendeshwa na Watanzania. Kwa hiyo, naomba Shirika la SIDO liwezeshwe. SIDO iwezeshwe ili kusaidia wazalendo, SIDO isaidiwe ili kuhakikisha kwamba sasa tunaingia katika nchi yenye viwanda vidogo vidogo, viwanda ambavyo mali ghafi iko ndani ya nchi yetu. Mfano tukihitaji kutengeneza furniture hatuhitaji mbao kutoka nje, nchi yetu ina misitu ya kutosha. Naomba Serikali ipige marufuku kuagiza samani kutoka nje ya Tanzania. Tukifanya hivyo tutawalinda hawa wenye viwanda vidogo walio ndani ya nchi yetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiwekeza katika Shirika la SIDO tukaliwezesha naamini hata hii kero ya kuwa na Wamachinga ambao wamekata tamaa itapungua. Tunahitaji vijana wetu waweze kujiajiri kupitia utaratibu wa viwanda vidogo vidogo vya SIDO. Lakini SIDO haiwezi kufanikiwa kama haijapewa mtaji wa kuwezesha kufanikisha azma yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie maeneo ya uzalishaji EPZ na SEZ, EPZ haziwezi kufanikiwa kama hatujaweka miundombinu inayotakiwa. Moja, ni kuwa maeneo yale yawe na industrial sheds ukiwekeza katika ujenzi wa industrial sheds ambazo viwanda vile vinaweza vikafanya uzalishaji mzuri na tutaweza kufanikiwa. Naomba Serikali yetu ihakikishe kwamba katika maeneo ya EPZ panakuwepo na umeme wa uhakika. Katika maeneo haya pia yawe na miundombinu ya barabara ya uhakika kwa sababu haiwezekani ukaliteua eneo kuwa ni eneo la EPZ, halafu lisiwe na supporting infrastructure za kuvutia wawekezaji, lazima miundombinu muhimu inayotakiwa katika maeneo haya Serikali iweke. Haiwezekani mwekezaji aje aweke miundombinu hii ni sisi tuwekeze ili kuvutia wawekezaji inakuwa ni rahisi wao kuja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwa sababu tuna raw material nyingi mfano, wakulima wa pamba, kahawa, katani, korosho hizi ni raw material ambazo sekta hii ya viwanda ingeweza kutilia mkazo sana. Leo hii tunapiga kelele hapa bei ya pamba imeshuka sh. 800/= badala ya sh. 1,100/= ni kwa sababu hatuna viwanda hivi. Lakini tungekuwa na viwanda hivi basi tungeweza kuwa na uhakika wa wanunuzi. Wakulima wanatekeleza wajibu wao kwa sababu hakuna mjomba wa kuwasaidia sisi wana siasa tunapoomba Serikali, Serikali itege sikio na isikie vizuri. Tunawavunja moyo watu wetu, tunapowakatisha tamaa wakulima hawa wakimbilie wapi? Tunaomba sana wakulima wa pamba, korosho na kadhalika Serikali kupitia viwanda na biashara na masoko Serikali isimamie, ihakikishe hasa kwamba masoko yanatafutwa ya kutosha ya uhakika ili wananchi waweze kuuza mazao yao ambayo wameitikia wito wa Serikali kuibadili nchi yetu kuwa nchi ya kipato cha kati. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia nizungumzie kero ambayo inanisumbua sana kwamba nchi yetu imegeuzwa kuwa ni eneo la kuuza bidhaa feki. Kwa nini nchi yetu imeachia wafanyabiashara ambao wanakwenda kuleta bidhaa ambazo ni feki? Niwaite ni wezi kwa sababu Watanzania wanatumia fedha zao kununua vitu ambavyo si vya ubora unaostahiki kwani baada ya muda mfupi vinaharibika lakini huwezi kuvirudisha ulikovinunua. Naomba sana Tanzania Bureau of Standards wafanye kazi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama wameshindwa basi tuanze utaratibu wa kuwajibika, asisubiri mtu kufukuzwa aondoke mwenyewe, kwa sababu sasa hivi ni aibu kubwa kwamba tunaletewa vitu vibovu sana nchi hii. Simu, television na kadhalika ni mbovu hata matrekta kwa mfano power tillers, nazo ni mbovu kati ya vitu ni vibovu kwa sababu kama ni kitu ambacho unauziwa lakini hata spear hazina, maana yake ni nini? Maana yake huyu aliyenunua Mtanzania mnyonge unamkatisha tama, unamrudisha nyuma katika maendeleo yake. Sasa naomba Mamlaka ambazo tumezipatia majukumu hayo wakishindwa waondoke. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii. Ahsante sana. (Makofi)

MHE. MOHAMED HABIB JUMA MNYAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kunipatia nafasi hii ili nitoe mchango wangu katika Bajeti ya Wizara hii ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vema bora tuanze kwa kuiangalia bajeti ya Wizara hii mwaka juzi ilikuwaje, mwaka jana na mwaka huu. Tukiangalia sehemu hizo tu basi tutaanza kupata hii picha ya bajeti ya mwaka huu ikoje. Mwaka 2009/2010, Wizara hii ilipangiwa bilioni 55.7 mwaka 2010/2011 ilipangiwa bilioni 64.2, hapo ni dhahiri kutoka mwaka 2009 kwenda mwaka jana kulikuwa na ongezeko tayari la bajeti asilimia 13. Lakini mwaka huu 2011/2012, imepangiwa bilioni 57 tayari kuna upungufu wa asilimia 11.3. Kwa hiyo, ukiangalia sehemu tatu hizo tu ukilinganisha bajeti ya mwaka juzi na mwaka jana na mwaka huu tayari unaweza kupata ile picha halisi. Kwa hiyo, tusitegemee makubwa kwa bajeti ya mwaka huu ikiwa kuna upungufu wa fedha hili la mwanzo linaonekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini mara nyingi katika hii bajeti huwa tunaangalia mambo ya maendeleo. Yawe matumizi ya kawaida, mishahara, nini, ni vitu vya kawaida ambavyo vinahitajika kwa wafanyakazi. Lakini tunatazama kimaendeleo, sasa kwa kimaendeleo bajeti ya mwaka huu imepangiwa bilioni 27.67 fedha ya ndani, kuna asilimia 59.2, fedha ya nje asilimia 40.8 ambayo kwa kawaida huwa haipatikani yote. Kwa kulinganisha na fedha za maendeleo za bajeti ya mwaka jana tayari kuna upungufu wa asilimia 18. Hili ni tatizo kwamba mipango yetu kwa maendeleo badala ya kukua mwaka hadi mwaka inapungua na siyo mipango inapungua au bajeti zinapungua kwamba tumepiga hatua kubwa kimaendeleo, hapana, hatujapiga hatua kimaendeleo, halafu na bajeti yenyewe inapungua. Hili ni tatizo kubwa na kasoro hii tuione na ni jambo ambalo linahitaji kufanyiwa marekebisho ikiwezekana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika bajeti hii jambo linalosikitisha zaidi kwamba sisi tunapiga makelele, tunahitaji maendeleo na hakuna maendeleo ya nchi yoyote duniani yanayoweza kupatikana kwa kuita wawekezaji wengi tu kila siku katika kila sekta. Maendeleo ya nchi yoyote duniani yanapatikana kwa ukuaji wa biashara na viwanda. Wewe ita wawekezaji wa kila aina lakini watahamisha fedha watapeleka nchi za kwao na sisi hapa tutaendelea ku -mark time. Lakini ikiwa tunataka maendeleo ya kweli ni kukua kibiashara na viwanda. Sasa hili la biashara na viwanda linatuvunja moyo. Mwalimu Nyerere alianzisha NDC kwa malengo maalum na alijua tuna chuma, tuna madini, tuna makaa, tuna kila kitu. Ni kitendo kinachosikitisha kwamba lile lengo la kuanzishwa NDC sasa hivi tunaliacha mkono. Hatuitumii NDC kama tulivyopaswa tuitumie NDC. Walitolewa wataalam nchi hii kwa ajili ya kuja kutusaidia kuhusu viwanda na chuma tulichonacho Tanzania. Wakatolewa watalaam wakasomea metallurgy sijui kama tangu mwaka huo wa Mwalimu wametolewa watalaam wengine kusomea mambo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini la kusikitisha NDC katika hiyo hiyo wakhal minal khalil, wameomba bilioni 24 wanapewa bilioni saba. Sasa hicho ni kichekesho. Lakini kuna miradi kama minne mikubwa NDC hao hao wanatakiwa waiendeleze miradi hiyo mradi mmoja/miwili mikubwa hiyo ya aibu ambayo miaka 20 iliyopita tunaimba chuma cha liganga na mkaa wa mawe wa mchuchuma na bado wamepewa NDC. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka 20 iliyopita bado tunasema Liganga na mpaka leo hakuna kilichoendelea. Lakini la ajabu zaidi kwamba wawekezaji walikuweko miaka mingi sana wa kuja kuwekeza hiki chuma na mkaa wa mawe Serikali hii kwa sababu ya ukiritimba wake kwa sababu ya kutotoa maamuzi kwa sababu nyingine ambazo wanazijua Serikali, Makampuni yote hayo hayakupata kuja kuwekeza, miaka imepita. Hivi leo tayari ndio tunavuta pumzi kuna kampuni ya Kichina. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuitahadharisha Serikali ya CCM kwamba kweli Wachina wanatusaidia lakini nataka mtambue au tujue kama nchi, kama Taifa ikiwa miradi yote reli tutegemee Mchina, chuma cha Liganga, tutegemee Mchina, kila kitu tutegemee Mchina, angalieni matokeo ya baadaye Mchina huyu atakapokuja kukosa mahali na nini matokeo yake? Duniani hakuna wawekezaji wengine wowote au ndio hatuelewani na hao wawekezaji wengine wa nchi zote isipokuwa Mchina tu, kila kitu Mchina, Mkaa wa Kiwila, Mchina; Reli, Mchina; Liganga, Mchina; Barabara, Mchina. Sasa ninachotahadharisha kama nchi lazima tuangalieni na hizi athari kwa sababu inaweza ikatokea siku tukatofautiana lakini ile tofauti ikatuathiri kama Taifa kama leo tunavyopiga makelele kwa wawekezaji wa mafuta basi itakuja kutokea kwa wawekezaji wa Kichina. Kwa hiyo, kama Taifa tuwe waangalifu na kama wawekezaji tunawahitaji lakini tutafute direction tofauti tusitegemee mahali pamoja tu. Mchina huyo atumiwe na nchi zote za Afrika, Angola, sijui wapi, haiwezekani! Ni lazima tutafute mahali pa kujikwamua. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la huu mradi wa magadi, mradi huu kama ni baraka za Serikali kwa NDC zilipatikana tangu mwaka 1996 ulipotoka Waraka wa Baraza la Mawaziri, ukaleta mgogoro kuhusu mambo ya Flamingo lakini migogoro mingine tutambue kwamba inasababishwa aidha na nchi nyingine kwa sababu leo nchi ikiwa inasafirisha, inazalisha magadi kwa wingi na inasafirisha nchi za nje. Ziko nchi hazifurahi, watatuletea sababu za environment, watatuletea sababu za flamingo, watatuletea sababu za kila aina. Lakini wako tayari wa-export, sisi tuagize kutoka kwao, sisi kuzalisha ni ngumu. Sasa tujiulize je, hii NDC imewezeshwa vya kutosha na nini kilitokea mpaka hiyo kampuni ya Tata Chemicals ikajitoa mwezi Machi 2009 ambayo ilikuwa ni ubia mzuri wa kuweza kuzalisha haya magadi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiacha eneo hilo, tuje eneo la viwanda. Kuna jambo moja linatusikitisha sana na Watanzania hawa wanashangaa sana kwamba kila siku viwanda vyetu gharama zinapanda. Kwa hiyo, bidhaa za viwandani hatujaona siku angalau bei zikashuka kwa faida iliyopatikana au kwa unafuu wa viwanda ilivyopata. Mheshimiwa Waziri nategemea unajua kwamba katika viwanda hivi mnavyosimamia kuna viwanda 35 tayari vimeshaunganishwa na mfumo wa gas ambayo inapatikana hapa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni mategemeo yetu na viwanda vingi vinavyotumia boilers badala ya kukata kuni na nini, sasa hivi wanatumia gas. Sasa inakuwaje hizi bidhaa zisishuke bei wakati viwanda hivi tayari vimepata saving ya takriban kuanzia mwaka 2004, gas ilipoanza kuzalishwa mpaka kufikia Juni, 2011 tayari hivi viwanda kwa ujumla wake wame-serve kiasi cha dola bilioni 2.87. Hii ni saving imepatikana kwa viwanda. Mwananchi wa kawaida huku chini ambaye ananunua hizo bidhaa za viwandani kama ni mabati, saruji au ni kitu gani, mbona hakuna unafuu wa bei au tutaweka regulatory katika kila kitu? Kuna EWURA kwa ajili ya Maji na Nishati, sasa regulatory wa bidhaa ni nani? Basi atafutwe na regulatory wa bidhaa ili aangalie baina ya huyu mtumiaji mwananchi na hawa wenye viwanda. Inakuaje bei hizi hazishuki, siku zote bei iwe zinapaa tu na wao wanapata punguzo na wanapata faida wanapata saving lakini kwa wananchi bei hazipungui?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri akija hapa atujibu na swali hili limeshaulizwa katika Bunge hili kiasi cha mara tatu au nne, Serikali bado mpaka leo inashindwa kutoa jibu sahihi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii bahati nzuri inaongozwa na vijana, wote vijana wabichi, damu zinachemka, wang’ara lakini hawako aggressive kibiashara, leo mkisikia China anafanyabiashara kubwa sana duniani kwa sababu ya incentive anayotoa kwa wananchi wake. Leo wafanyabiashara wetu sijui wanajengewa jumba gani pale, Wamachinga, hakuna njia yoyote ya kuwasaidia hawa wafanyabiashara wetu wakatoa bidhaa waka-export, wakatuma nchi za nje. Leo China kule kwa taarifa yenu Mchina yoyote anaposafirisha kontena moja mbali na faida anayopata na Serikali ina fungu lake linamwekea kila mwaka huyu amesafirisha makontena mangapi aliyopeleka Tanzania, Ghana, South Africa, Nigeria ile faida unayopata Serikali nayo imekuwekea package yake kila mwaka inakulipa kwa bidhaa ulizosafirisha. Hawa wafanyabiashara wa Tanzania mmewapa incentive gani mpaka leo? (Makofi)

Kuna kitu gani wamepewa? Kuwajengea lile jumba pale wakakusanyike pale na mifuko na mikoba yao basi? Haiwezekani! Kwa hiyo, ni lazima wawe aggressive, hatuwezi kuendelea kibiashara kama hawajawa aggressive. Ni lazima kuwe na Vitengo vya Espionage ili kujua watu wanafanya nini duniani. Haiwezekani wawe wamelala tu. Mawaziri ni vijana, ndio tunaowategemea, naomba wawe aggressive katika biashara, wajuwe mambo ya kufanya, wasome watu wanafanya nini duniani. Ni lazima kuwe na Vitengo vya Espionage. Leo miaka 40 ya Uhuru ndiyo tumeweza kuwa na Barcode, hawaoni aibu? Mpaka leo ilikuwa hatujajua Tanzania tunahitaji kuwa na Barcode katika biashara, ina maana wanajua leo?

(Hapa kengele ililia kuashiria kwisha kwa muda wa mzungumzaji)

MWENYEKITI: Ahsante Mheshimiwa, muda wako umekwisha.

MHE. MOHAMED HABIB JUMA MNYAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante lakini nafikiri watakubaliana nami hawa Mawaziri vijana. Ahsante. (Makofi)

MHE. CAPT. JOHN D. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru na mimi kupata nafasi. Kwanza, niwapongeze Waislamu wote waliofunga, leo chungu cha 10. Inshallah Mwenyezi Mungu atawajalia wamalize, halafu tusherehekee Idd Elftri vizuri. (Makofi)

Pili, niishukuru Serikali jana kupitia EWURA na Wizara, kwa tamko ambalo Bunge ililitoa kwa Serikali kuhusiana na suala la mafuta maana hivi ninavyosema ingawa nafikiri ita- manoeuvre, kule kwetu Mbinga, Vijiji kama Kingirikiti, Mbamba-Bay, Lituhi, leo hii petroli ni shilingi 6,000/= na hawajui ni lini mambo haya yatarudi kwenye hali ya kawaida. Kwa hiyo, niishukuru Serikali lakini zile saa 24 karibu zinakaribia, nategemea leo hii Serikali itatoa tamko lingine la kuwafanya watu waone kwamba wana Serikali yao thabiti. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nirudi kwenye Wizara hii, mradi wa Mungaka, hapa mmesema mradi wa Ngaka siyo Ngaka, sehemu ile inaitwa Mungaka. Kwa hiyo, ule mradi wale wawekezaji wako pale karibu miaka minne sasa, tunasema kwamba ooh tutatafuta wawekezaji wakipatikana tutafanya nao mpango lakini kwa mradi wa Mungaka wawekezaji wako pale, tayari wameshasema wanaweza kutoa megawatt 400, sasa mnataka wawekezaji gani kuliko hawa? Wako pale, umeme uko pale, ni suala la Serikali kutoa fedha na kupeleka huko Mufindi na umeme upo, sio tatizo tena katika Taifa letu. Naomba sana NDC wapewe uwezo ili mradi huu wa Mungaka uweze kufanya kazi yake vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo nina mchango mdogo sana lakini nataka nizungumzie biashara ya Tanzania, Malawi na Msumbiji. Tunapoimarisha Mtwara Corridor maana yake unaimarisha bandari ya Mtwara, maana yake unaimarisha bandari ya Mbamba-Bay ili i- correspond na bandari ya Mkata Bay ili mazao yakitoka Mtwara-Mbamba-Bay yaende Mkatabay yaende kwenye SADC countries. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini ukiangalia uchumi wa watu hawa ni duni. Tunaambiwa kwamba tunafanya kazi ya kusaidia uhai wa viwanda vya ndani. Kuna tatizo la sukari kule. Tatizo kubwa sana na tukihubiri sisi ni sukari. Tunaambiwa kwamba Watanzania walio kule mpakani, Mtwara, Newala, Tunduru, Songea, wapate sukari ya kutoka Tanzania ambayo ni shilingi 3,000/= lakini sukari ya Malawi tu pale ng’ambo kilomita 40, pale mdomoni tu ni shilingi 1,500/= mpaka 1,900/= lakini wakifanya biashara hii Watanzania, wale watu wa Mapato wanachukua sukari wanaizamisha kwenye maji ya Ziwa Nyasa, hiyo ni haki gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunalinda viwanda vya nani? Hivi Kiwanda cha Kilombero cha Mtanzania gani? Kiwanda cha Mtibwa Sugar cha Mtanzania gani hasa? Watanzania wale wanaweza kupata sukari ileile maana walewale waliowekeza Kilimanjaro, waliowekeza Kilombero ndiyo walewale wanazalisha Malawi sukari. Sasa unazuia sukari ya Malawi isije Tanzania kwa sababu ya kulinda viwanda vya ndani wakati gharama yake ni kubwa mara mbili ya ile ya kule. Naomba mturuhusu, hawa akina Murji wafanyabiashara, waende kule Malawi wachukue sukari walete Ukanda ule na sisi tu-enjoy hiyo raha ambayo watu wa Dar es Salaam, watu wa wapi wana-enjoy, sisi ni maskini wa kila kitu, hata kunywa chai ni maskini, why? (Makofi/Kicheko)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri leo atoe kauli hapa kwamba wale watu wataruhusiwa kufanya biashara. Tangu wakati wa Mheshimiwa Dkt. nimesema, Mheshimiwa Dkt. Nagu alifika kule akatuahidi watafanya hivyo labda kwa sababu tu walimtoa mapema lakini ameingia mwingine naomba aendeleze kile ambacho Mheshimiwa Dkt. Nangu alikwishafanya. Leteni watu wafanye biashara, waende Malawi, Mbamba-Bay wakachukue sukari. Sukari iko nyingi lakini Watanzania wale wananyanyaswa, sukari yao inazamishwa kwenye Ziwa. Hiki ni kitu gani? Huu ni uhuru gani? Sisi watu wa mpakani kule tunafaidi nini? Kwa nini msituite Wamalawi basi? Wale ni Watanzania, Watanzania gani ambao tunataka sukari kwa shilingi 1,500/= hamtaki mnataka tule sukari ya shilingi 3,000/=. Hii maana yake nini? Tunalinda viwanda vya ndani, viwanda gani hivi? Naomba Waziri akisimama hapa atuambie biashara ya sukari, wao wanakuja, Wamalawi hawajui kula wali, wanakula ugali wale, siku hizi tunawafundisha kula wali, wanachukua mchele wetu wanapeleka kule wanafanyabiashara lakini sisi hatufanyi nao biashara kwa sababu gani? Kwa hiyo, Waziri akisimama hapa leo jioni aseme kwamba kuanzia sasa biashara hiyo ni huria, tufanye biashara na wale watu wa Malawi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, halafu tunasema tunafanya biashara ya samaki. Hakuna samaki watamu duniani kote kama wa Ziwa Nyasa. Ni watamu mno. Muulize Mheshimiwa Waziri Mkuu anajua, ni watamu kuliko samaki wowote katika dunia hii.

MBUNGE FULANI: Zanzibar wapo!

MHE. CAPT. JOHN D. KOMBA: Zanzibar kuna samaki gani, kuna samaki wa chumvi tu lakini nazungumzia samaki wa maji baridi, samaki mbasa, kuna samaki mbufu, kuna samaki tilapia, wote ni watamu lakini hakuna masoko ya kuhifadhi samaki. Kwa hiyo na hili suala liko chini ya Wizara hii, naomba tujengeeni masoko ya kuhifadhi samaki wale. Jenga soko Mbamba-Bay, Liuli, Kiagara, Lituhi na maeneo yote ya Ziwa ili samaki wale wavuliwe na wanapendwa kila mahali. Hakuna mtu asiyependa dagaa wa Nyasa hapa, ni watamu kama nini lakini hatuna soko la kuhifadhi samaki wale.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho EPZ. Mimi ni mkazi wa Songea pia pamoja na kwamba ni mkazi wa Mbinga, yako maeneo ambayo EPZ imechukua kule Songea, Ruiko, Msindo, Lilambo, Kwajumbe Idi, Ruwawazi, miaka minne iliyopita, watu wale wamekaa, hawajengi nyumba, hawalimi mazao, hawafidiwi, wako tu. Walikuwa matajiri sasa maskini kisa ni EPZ. Hii ni haki kweli? Kwa hiyo, kama tumeshindwa kupata pesa kwa sasa waruhusiwe kutumia maeneo yale. Wamekaa tu wanasubiri Serikali, lini itakuja kuwafidia, lini EPZ hiyo itaanza? Naomba sana watu hawa wafikiriwe ama sivyo tutakataa, kama mradi huo huko mbele zaidi waruhusiwe kufanya biashara zao za kilimo, ujenzi ili waweze kukidhi mahitaji yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo sina mengi, kwa hayo machache nashukuru sana. Naunga mkono hoja. Ahsante sana. (Makofi)

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia hoja hii ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nitoe taarifa halafu niendelee na mchango wangu. Jimbo langu la Nyang’hwale kwa kweli lina njaa kubwa sana. Vyakula ambavyo tuliahidiwa vya gharama nafuu kwa kilo moja shilingi 50 havijafika na vya shilingi 350 upatikanaji wake pale kwenye Ghala la Taifa Shinyanga pamekuwa na ukiritimba wa hali ya juu. Meneja yule anawanyanyasa Wakala wangu kutoka Jimbo la Nyang’hwale hawajapata chakula tangu tumeahidiwa tani 300 mpaka leo hazijatoka, tumepewa kama tani 100 na kitu tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa ya pili, wakulima wa pamba wa Nyang’hwale wamenipigia simu wanasema wananyanyaswa na makampuni ambayo yananunua pamba. Soko la pamba lilivyofunguliwa waliuza pamba yao kwa bei ya shilingi 1,100 na wakapewa risiti za mkopo leo hii wanaenda kudai pesa zao wanalazimishwa walipwe kwa bei ya shilingi 800/=. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri leo jioni atoe tamko kwa hayo makampuni waliokopa pamba kwa kipindi cha mwanzo kwa shilingi 1,100/= kwa nini wanawanyanyasa wakulima hawa kwa kuwalazimisha bei ya shilingi 800/=?

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya taarifa hiyo, napenda ni-declare interest kwamba mimi ni mjasiriamali. Mchango wangu wa kwanza nitazungumzia kuhusu leseni za wafanyabiashara wa kati. Hizi leseni za wafanyabiashara wa kati zimekuwa zikitolewa sijui kwa utaratibu gani? Naomba leo tueleweshwe kwa sababu tumeona wafanyabiashara wa kigeni wanafanyabiashara ndogondogo na za kati hususani Kariakoo.

Mheshimimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara wa Kichina wamejaa pale Kariakoo. Sasa naomba tuambiwe wale ni wawekezaji wakubwa ama ni wafanyabiashara wa spare za pikipiki, magari, maduka ya kuuza vifaa vya ujenzi na kadhalika mpaka kuna Wachina wengine wanaendesha daladala, wanapiga debe, wamefungua mpaka mama ntilie pale Buguruni na mwingine yuko Kinondoni. Sasa tunataka tuelezwe hizi leseni ni vipi? Mtanzania atafanya biashara gani kama wanatoa leseni kama njugu kwa wafanyabiashara wa kigeni? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maisha bora kwa Mtanzania kwa mtindo huu hayatakuwa bora. Leo tunasema Serikali ni sikivu, inahurumia wananchi wake, si kweli kwa sababu leo Watanzania kazi ambazo wanaweza kuzifanya zimekuwa zinafanywa na wageni! Mgeni akifika leo, ni ndani ya wiki moja ama mbili mtaona ameshafungua duka lakini kwa Mtanzania ukitaka kufungua duka utazungushwa zaidi ya miezi miwili, tunaomba Waziri leo hapa atupe maelezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara alisimama Kariakoo na kuongea na wafanyabiashara mwanzoni mwa mwaka. Akatoa ahadi kwa wafanyabiashara kwa kauli yake yeye mwenyewe, akatoa siku 90 akiwaahidi wafanyabiashara wa Kitanzania kwamba hawa wafanyabiashara wageni hususan Wachina, biashara hizo watakuwa wamezifunga lakini tangu kauli hiyo itolewe zaidi ya maduka 300 yameshafunguliwa Kariakoo na sehemu zingine. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunashangaa wafanyabiashara wa kigeni kwa nini bidhaa zao zinakuwa na bei ya chini sana. Serikali ijaribu kuangalia je, inakusanya kodi zake sawasawa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mfanyabiashara wa spare, nitatoa mfano kidogo. Kipuri hichohicho nakinunua China kwa dola moja, unalipa fright…

MWENYEKITI: Samahani Mheshimiwa, umesema tu ni mjasiriamali, ungetusaidia kama ungesema unafanya biashara gani.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Sawa! Mimi ni mfanyabiashara, naleta vipuri na pikipiki.

MWENYEKITI: Hapo sasa sawa endelea.

MHE. HUSSEIN NASSOR AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, spare hiyo unainunua dola moja China, unailipia fright, unakuja kulipa ushuru, unauza labda dola moja na nusu, huyohuyo Mchina anakuja anauza dola moja. Je, hiyo spare ameileta kwa miujiza gani kama siyo ukwepaji kodi? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyohuyo Mchina anakuuzia dola moja huko China, wewe unasafirisha unakuja kuuza dola moja na nusu yeye anauza dola moja. Je, wewe Mtanzania utatoka pale ulipo? Sera hii ya utoaji wa leseni, naomba jioni tuelezwe utaratibu ukoje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nina wasiwasi kwamba vipuri ama vitu ambavyo tunatumia Watanzania kwa nini viuzwe kwa bei ya chini? Viwango vyake inawezekana viko chini. Nitatoa mfano. Leo kuna mipira ambayo imeingizwa nchini, ni mibovu, mipira hiyo inasababisha ajali kwa Watanzania, nguvu kazi nyingi inapotea, bei yake ni chini. Sisi tunaoleta mipira mizuri na tunauza kwa bei nzuri tunakuwa hatuuzi. Kwa hiyo, tunaomba Shirika la Viwango lijaribu kuvipima vitu ambavyo tunatumia. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba leo Mheshimiwa Waziri hapo atutamkie kuhusu suala la usumbufu ambao sisi wafanyabiashara tunafanyiwa na TRA. TRA imekuwa ikitusumbua sana hasa wafanyabiashara wazawa. Sijui kuna nini hapa katikati. Ukipita mitaani, utakuta wamening’iniza tai zao kwenye maduka ya wazawa lakini pita kwenye maduka ya wageni, hawapo! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Mheshimiwa Waziri atuambie utaratibu wa hizi mashine za risiti. Kuna baadhi ya maduka makubwa hawana hizo mashine na kuna baadhi ya maduka ya wageni hawana pia lakini wazawa wanasumbuliwa sana kwa ajili ya mashine hizo. Sasa namwomba atuambie zina utaratibu gani? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri ajaribu kuangalia kwa undani zaidi maana tunaandaa bomu ambalo wakati wowote litalipuka. Iwapo Watanzania tuna uwezo wa kuzifanya kazi ndogondogo za kuweza kutupatia kipato chetu, leseni zinatolewa kwa wageni, sisi Watanzania tufanye nini? Tunaomba leo Waziri atoe tamko na mimi nasema kwamba nimo kwenye Chama cha Wafanyabiashara (CHAWASAPI), niko tayari kuongea na wenzangu iwapo hatutapata majibu ya maana leo hapa na sisi tufunge maduka, tuache kutoa huduma ndani ya wiki moja. Tunasema leo atuambie ni kwa nini leseni zinatolewa kama njugu kwa wafanyabiashara wa kigeni. (Makofi)

Mheshimiwa Waziri, napenda nizungumzie kadhia ambayo ilijitokeza Mwanza…

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge, unaa-address Mwenyekiti, siyo Waziri.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Samahani. Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nizungumzie tatizo ambalo lilijitokeza Mwanza. Wafanyabiashara walipata hasara kubwa sana, maduka yao yalivunjwa, mali zao ziliibiwa. Ninavyosikia kuna baadhi ya watu walipoteza maisha na wengine mpaka sasa hivi wanauguza majeraha ya risasi. Serikali ituambie wafanyabiashara hawa ambao walipata hasara kutokana na hiyo kadhia, mpaka sasa hivi imewachukulia hatua gani wale watu ambao walianzisha virugu hiyo kwa sababu wanajulikana. Nimekwenda kutembelea baadhi ya maduka, vioo vimevunjwa na mali zimeibiwa. Sasa Serikali ituambie kama sisi wafanyabiashara hatuna haki, basi tuelezwe kwa sababu vurugu hizi zimeanzishwa na watu fulani ambao wanajulikana. Ni hatua gani ambayo imechukuliwa? Sisi ni watu ambao tunaipenda Serikali, tuna ushirikiano mzuri na Serikali lakini inaonekana baadhi ya sehemu tunakuwa hatutendewi haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, naomba jioni leo Mheshimiwa Waziri lazima atueleze utaratibu wa wafanyabiashara wa kigeni, ni kwa nini wamehozi sehemu mbalimbali ya biashara ambazo tunaweza kuzifanya sisi wenyewe Watanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, siungi mkono hoja. Ahsante. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Amar. Sasa nitamwita Mheshimiwa Mussa Kombo na Mheshimiwa Deo Filipukunjombe ajiandaye.

MHE. MUSSA HAJI KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kunipa nafasi hii. Mie sina maneno mengi sana isipokuwa nitatoa ushauri kidogo tu kwa Mheshimiwa Waziri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vyetu vingi sana havizalishi kwa sababu ya kukosa umeme na suala hili ni la msingi sana. Nafikiri kitu kizuri ni Wizara hii kukaa na Wizara ya Nishati na kulizungumzia suala hili la distribution ya umeme. Hivi viwanda vingekuwa vinapewa privilege maalum wakati umeme ukikatwa kwenye majumba ya wananchi ili viweze kuzalisha na wapate circuit ambayo itakuwa ni kwa ajili ya viwanda tu. Sio wakati wananchi wanakatiwa umeme, basi na viwanda vinakatiwa umeme, itakuwa ni matatizo ya kila siku, viwanda havitazalisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyomsikia Mheshimiwa Mnyaa hapa akizungumzia kwamba, kuna viwanda 35 ambavyo vinaweza kutumia gesi lakini pia kuna viwanda ambavyo vina uwezo wa kutoa umeme vyenyewe, kwa mfano kiwanda cha Wazo Hill. Tutoe elimu ya kuvifanya viwanda hivi badala ya kuwa na standby generator za diesel, waweke standby generators za gesi sasa kwa sababu uwezo huo tunao, ambao unaweza ukatusaidia sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni uchomaji wa bidhaa chakavu au hizi bidhaa zilizokuwa hazina thamani, ambazo haziko katika standard, zinazokamatwa na TBS. Bidhaa hizi nyingine ni za vifaa vya electronics, nyingine ni computers; vifaa hivi vinachomwa wazi, vinaleta matatizo ya kuharibu mazingira! Zinaleta radioactive, sumu mbaya! Napenda kusema ni bora au ni jambo la busara kuondoa maumivu haya ambayo tunayo pajengwe mahali maalum ambapo uteketezaji huo utakuwa unafanyika. Hawa Fair Tribunal wanaweza wakatusaidia utaratibu mzuri kama ule wa vifaa vya hospitalini vinapochomwa haviwezi kuwa-affect wananchi, haviwezi kuharibu mazingira lakini leo tunachoma madude haya nje! Yanaletwa pale yanaoneshwa tena kwa fahari kwenye TV! Ni hatari sana kwa maisha yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho. Sisi Watanzania tunasafirisha vitu vingi sana kutoka nje, lakini bahati mbaya sana hatuna elimu ya packaging, vifungasho vya vitu vile. Kwa mfano, tunasafirisha korosho na mambo mengine lakini hakionekani! Wengine wanavitumia vikaonekana kama ni vitu vilivyozalishwa Kenya au nchi nyingine jirani! Mimi nafikiri Wizara hii badala ya kuonesha kwenye maonesho tu, ilikuwa inatakiwa pia muwafunze hawa wazalishaji na wasafirishaji wa vitu vyetu kutoka nje. Utaalamu huu wakisaidiana na TBS, utatusaidia kuweka heshima yetu nje kama tunazalisha lakini kwa utaratibu huu ambao wenzetu wengi hapa wanazungumzia magari yanakuja hapa, yanachukua matunda kupeleka Kenya, sijui wapi na nini, haionekani kama matunda yale ni ya Tanzania. Likifika Kenya, siku ya pili liko Uingereza, liko nchi mbalimbali, ile thamani ya kuonekana kama sisi tunazalisha vitu vizuri kama vile, haipatikani!

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuondoe sasa siasa nyingi katika uchumi, uchumi uendeshe siasa. Hili suala la Wamachinga ambalo linaonekana ni uadui na Serikali za Miji au Halmashauri au City, nafikiri tunahitaji Wizara hii kukaa pamoja na Halmashauri hizi wakatafuta njia nzuri ya kusaidia ili kufanya hawa Wamachinga wasionekane kama ni mbwa wa mji. Wengine wanawasikitikia watoto waliokuwa wanatembea mitaani! Sasa hawa Wamachinga tutafika mahali tutawaona ni kama wale watoto wa mitaani. Unamkuta Mmachinga anauza kitu chake, wakati mwingine cha shilingi 50,000/= na ndio mtaji wake wote wa kuendesha maisha yake. Anakuja kukamatwa na Mgambo, vitu vile vinachukuliwa na virungu vya Mgambo alivyofundishwa na Jeshi la Mgambo anajihisi anarudi kulekule mwanzo, hana maendeleo yoyote! Matokeo yake anakuchomoleeni nyie sasa kwenye mifuko yenu. Anawabaka, tunasema watu hawa wabaya! Tujaribu kutafuta Sera ya kuweza kuwaweka hawa nao katika maisha mazuri. Haiwezekani ikawa kuna Sera tu ya watu ambao wanakaa kwenye majokofu mazuri na nini hawa tukawadharau! Wanasaidia hawa Wamachinga society ya Watanzania katika maisha yao kwa vitu vyao rahisi. Sasa ikiwa kitu anachouza Mmachinga hakiko kwenye standard, lile sio kosa la Mmachinga! Lile ni kosa la Serikali na TBS lakini Mmachinga akiuza kitu kile ukinunua kwa bei rahisi, unajisaidia na wewe maisha yako ambapo uwezo wako wewe mwenyewe wa maisha yako ni shilingi 1,500/= kama dola moja. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutizame umuhimu wao hawa! Tutizame umuhimu wa wananchi wetu wanaweza vipi kusaidiwa kuondoka katika ugumu huu wa maisha uliopo sasa. Nafikiri tutizame pia heshima ya Mtanzania; tusimheshimu yule ambaye ana gari kubwa peke yake! Tuwaheshimuni na wale ambao suruali zao zikivaliwa unaona kila kitu nje! Tuwaheshimu kama ni Watanzania wenzetu, tutafute njia za kuwaondoa katika matatizo ndio tutaweza kwenda katika Sera zetu nzuri na kuendesha nchi yetu bila ya ubaguzi wa kipato. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na wenzangu kusema kwamba wale wote ambao wanafunga kama mimi Sheikh, Mungu atujalie na kutupa Baraka kubwa. Nakushukuru. (Makofi/Kicheko)

MHE. DEO H. FILIKUNJOMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana kwa kunipa fursa hii. Kwanza utaniwia radhi, sauti yangu leo imekaa ndivyo sivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeisoma vizuri, nimeisikiliza vema hotuba ya Waziri wetu wa Viwanda na Biashara. Kimsingi, kuhusu Barcode, mimi niseme kwa niaba ya Wabunge wenzangu na mimi mwenyewe hatuna shaka nayo. GS1 ni jambo jema, ni mpango mzuri, lakini mpango mzuri hasa kwa sababu utaratibiwa na kuendeshwa na wataalamu waliobobea, mashirika tunayafahamu, chini ya uangalizi wa Serikali. Kwa hiyo, endeleeni na tunaamini kabisa mpango huu pia utawasaidia wafanyabisahara na wakulima wale ambao wapo kule Ludewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu ukaguzi wa bidhaa kabla hazijaingizwa hapa nchini, hapo napenda kutia shaka kidogo. Niseme naipongeza Serikali kwa sababu imechelewa kuitekeleza Sheria ya Viwango, Namba 2 ya mwaka 2009. Sheria imekuwa makini kwenye hili. Naipongeza Serikali kwa sababu, Sheria hii tumeitelekeza, Sheria hii tungeifanyia kazi, leo tungepata madhara makubwa sana! Tungepata madhara makubwa kwa sababu, zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii tumesema tukishapitisha Sheria hii kwamba vitu vikaguliwe nje kabla havijaja hapa! Tulipitisha Sheria moja tu kwamba, magari yakaguliwe kabla hayajaja hapa nchini, lakini kwa Sheria hii, TBS wameshindwa kuisimamia vyema! Magari yanayokuja Tanzania leo hayakaguliwi, yanakuja magari mabovu, yanakuja magari yameharibika, TBS wameshindwa kufanya kazi! Sasa kama wameshindwa kusimamia jambo moja tu, sidhani kama wanaweza kusimamia bidhaa zote! Kwa hiyo, kwa hili mimi naona Serikali imefanya busara kutokuitekeleza Sheria. Serikali iwe makini sana na TBS. TBS sio waaminifu. TBS hawatendi kazi ipasavyo na naomba sana wawajibike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi ni nchi gani duniani ambayo imeendelea bila viwanda? Tuna nchi gani hapa duniani ambayo imeendelea kwa kilimo? Kupanga ni kuchagua, nyie mnasema kila siku lakini kwa hakika hapa tumepanga kurudi nyuma na sio kwenda mbele. Hakuna nchi yoyote duniani ambayo imeendelea bila viwanda lakini sisi Wizara yetu ya Viwanda tumeitelekeza, tumeiweka pembeni, tumeacha kuona huu ni mhimili, mhimili wetu tumeweka katika kitu kingine, mhimili wetu ni Kilimo Kwanza. Kilimo Kwanza hakiwezi kwenda bila viwanda! Kilimo Kwanza hakiwezi kufanikiwa bila masoko! Wananchi wanaolima kule Ludewa leo wanataka uhakika wa soko la mahindi ndipo watafanikiwa lakini pia tukiwa na viwanda, kilimo chetu kitakuwa ni kilimo bora zaidi kuliko kilimo hiki cha sasa hivi. Kwa hiyo, kwa upande fulani ukitizama vizuri sana, umaskini wetu tumeamua kuutengeneza sisi wenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tizama nishati ya umeme! Inasikitisha sana kuona kwamba leo hii baada ya miaka 50 ya Uhuru tumekaa tunalaumu TANESCO lakini ukweli ni kwamba sisi wenyewe Serikali yetu imeshindwa kuwajibika ipasavyo. Serikali yetu imepanga na sisi wenyewe tumeamua kuwagawia giza Watanzania badala ya kuwapatia umeme! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi tunavyozungumza, vijana huko saluni zimefungwa, mazao hayaendi, viwanda vya maziwa vinasimama, sisi kwa kisingizio cha kwamba Shirika letu la TANESCO tulikuwa tumeli-specify lakini tunakuwa wepesi sana wa kutoa sababu kwa nini tumeshindwa, tunashindwa kujenga sababu za kwa nini tumeshindwa kwenda mbele! Tunabaki kulaumu NDC kila siku, tutalaumiana humu ndani, lakini ukweli ni kwamba, Serikali yetu imetutendea dhambi Watanzania kwa sababu Serikali haitimizi na kutekeleza wajibu wake ipasavyo. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumezungumza kila siku na mie nawashukuru Waheshimiwa Wabunge wote tunazungumza hili kwa umoja, kuhusu makaa ya mawe ya Ngaka, Kiwira pamoja na Mchuchuma. Maeneo haya peke yake yanaweza kuzalisha Megawatt zisizopungua 1,600 kwa wakati mmoja. Leo Mwenyezi Mungu anatushangaa na Ulimwengu unatushangaa, tunalalamika na umeme wa maji! Takwimu na tafiti zinaonesha kuwa nchi zote duniani ambazo zimeendelea zinatumia umeme wa makaa ya mawe. Makaa ya mawe tunayo, kila kitu tunacho, tunalalamika na giza! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii kule Liganga na Mchuchuma, tunasema Mwekezaji amepatikana na mazungumzo yanaendelea! Mwaka mzima si neno, tutasubiri, NDC wanazungumza na Wizara yake lakini Serikali imejiandaa vipi kwa mradi ule mkubwa wa Liganga na Mchuchuma? Kuna Mwekezaji mdogo tayari ameanza kufanya kazi kwa mazingira magumu sana! Miundombinu bado ni mibovu. Hakuna mazingira wezeshi ambayo yapo tayari kwa ajili ya kupokea mradi huu! Barabara hakuna! Hakuna uwanja wa ndege! Umeme huu ukizalishwa, utabebwa kwa msongo upi? Kwa hiyo, naitaka sana Serikali ianze kujiandaa. Iende sambamba na hayo inayoyasema. Ianze kuyafanyia kazi kwa vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukitizama kwa umakini sana, tatizo la umeme leo ni tatizo la kutengenezwa kwa maslahi binafsi na ya wachache! Kwa maslahi ya watendaji wetu ambao wako Serikalini! Wamesahau kabisa maslahi ya umma, wamesahau kabisa dhamana ambayo tumewapatia! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Serikali ilivalie njuga suala hili, Wizara zote ziungane zifanye kazi kwa pamoja. Wizara ya Viwanda na Biashara ni Wizara mtambuka kwenye baadhi ya maeneo inategemea Wizara nyingine. Naomba sana Mheshimiwa Waziri Mkuu, Wizara zishirikiane, Serikali ifanye kazi kwa umoja, tutaweza kufanikiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nasema tatizo hili ni la kutengenezwa kwa sababu zifuatazo. Wakati Wizara ya Viwanda na Biashara inatujia hapa leo na kusema kwamba ina mpango mkakati kwa ajili ya Liganga na Mchuchuma, mimi nina barua hapa imesainiwa na Bwana David Jairo, akiwa Katibu Mkuu wakati huo. Katibu Mkuu huyu, ambaye Wizara yake yeye inapaswa kupokea mradi wa umeme, David Jairo, anaandika barua kwamba Mradi wa Liganga na Mchuchuma usimame kwanza! (Makofi)

(Hapa Barua husika ilioneshwa Bungeni)

MHE. DEO H. FILIKUNJOMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni barua ya tarehe 21 Machi, 2011. Mtumishi huyu, mtumishi wa Serikali, ni Katibu Mkuu ambaye Wizara yake ingenufaika na mradi wa umeme lakini yeye anasema mradi huu usimame kwanza! Sijui kwa maslahi gani? Ndipo hapo inapofika mahali tunaona na sisi kwamba, Watendaji wetu wanafanya kazi kwa maslahi binafsi zaidi, wamesahau kabisa dhamana ambayo tumewatuma! Wamesahau tija! Wamesahau kabisa Watanzania! Kuna watu wachache wananufaika na mgawo wa giza! Ushahidi mmojawapo ni huyu bwana! Haiwezekani Watanzania tunalalamika na umeme lakini Mtendaji Mkuu, Katibu Mkuu wa Wizara, anaandika barua ya kusimamisha mradi huo! (Makofi)

Mheshimiwa Waziri Mkuu, naomba sana utuonee huruma wananchi wa Ludewa…

MWENYEKITI: Una-address Mwenyekiti.

MHE. DEO H. FILIKUNJOMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakuomba sana, wananchi wa Ludewa wako tayari kuitumia rasilimali ile kwa manufaa ya Watanzania wote. Wananchi wa Ngaka wako tayari, wananchi wa Kiwira wako tayari. Haiwezekani tunakaa kwenye giza, tunagawana giza badala ya kugawa mwanga. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengine ni mambo ya ajabu sana! Shirika la NDC tunawalaumu bure tu. NDC hawana matatizo! NDC wameomba USD milioni 46 tu ambayo ni fedha kidogo sana kwa ajili ya kujenga msongo wa umeme. Kupanga ni kuchagua, sisi tumepanga kutokuwapa hizi pesa lakini Serikali hiihii ya kwetu ilikuwa nyepesi sana na kila siku ilisisitiza kwamba iko tayari kulipa shilingi bilioni 94 za DOWANS ambazo hatukupanga na hazikuwemo kwenye bajeti! Pesa za DOWANS shilingi bilioni 94 mlisema tutalipa na tuko tayari lakini shilingi bilioni 46 kwa ajili ya umeme wa Watanzania, mnasema hizi pesa hakuna! Ndugu zangu, hebu naomba Serikali iwe na huruma kwa Watanzania, hebu muwakumbuke waliowatuma, tuwakumbuke waliotupatia dhamana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, haiwezekani fidia ya DOWANS mnasema tutalipa, wakati hizi fedha hazikuwepo kwenye bajeti na sijui mngezitoa wapi lakini fedha ambazo wanaomba NDC, ambazo ni kidogo tu, hamtaki kuzitenga! Hamtaki kuwapatia, hamtaki Watanzania nao wanufaike na umeme! Hamtaki wananchi wa Ludewa nao waweze kunufaika na ule mradi wa kule Ludewa! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupanga ni kuchagua nimekubali kabisa. Leo hii mradi wa vitambulisho umetengewa shilingi bilioni 300, mimi sina shaka, natambua umuhimu wake lakini shilingi bilioni 300 na shilingi bilioni 40 kwa ajili ya umeme, Mtanzania kipi leo ni cha msingi kwake? Mtanzania wa kawaida leo anataka kitambulisho au anataka umeme? Kwa nini, tusianze na haya madogomadogo ya msingi ambayo Watanzania wanayahitaji na kuyatarajia kutoka kwetu? Shilingi bilioni 200, wapewe kidogo hawa wenzetu, shilingi bilioni 100 zije kwenye umeme huku, tufanye yote yaende kwa pamoja. Tumepanga kutokwenda mbele tumepanga kusimama hapohapo. Kupanga ni kuchagua, naomba tuwasaidie Watanzania, tuwakumbuke wenzetu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda na Biashara ni Wizara muhimu sana, ni Wizara inayotegemea Wizara nyingine. Kwa hiyo, naomba sana, nasihi sana, naisihi sana Serikali yetu iwe makini kwenye kupanga kwa sababu kupanga ni kuchangua, tupange mambo yenye maslahi kwa Taifa. Tupange mambo yenye maslahi kwa wana Ludewa. Wananchi wa Ludewa leo wanataka soko la uhakika, mwananchi wa Ludewa leo hataki power tiller, ukimhakikishia soko la mahindi lipo atalima mpaka utakimbia mwenyewe. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo Ludewa unashangaa mahindi tunayo, mengine yanaoza kwa sababu wa kununua hakuna lakini Serikali inaleta mahindi mengine tena ya msaada Ludewa, hapo unashangaa, tumepanga kufanya kitu gani na tunafikiria kitu gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa Ziwa Nyasa wapate soko la samaki, soko la samaki lijengwe Manda, Lupingu na Makonde pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukifanya namna hiyo, naamini kabisa wananchi wetu watatuunga mkono, tusifanye mambo haya kama Bwana David Jairo anayefikiria mambo yake binafsi. Mimi naamini Waheshimiwa Mawaziri wametusikia, twende mbele, tushikamane, tuiunge mkono, tuisaidie sana Wizara yetu ya Viwanda na Biashara. Ahsante sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Nakushukuru sana.

MWONGOZO WA SPIKA

MBUNGE FULANI: Mwongozo wa Spika!

MWENYEKITI: Hapana ili kutenda haki kuna mtu mmoja hapa ameumia sana Mheshimiwa Mangungu upo, nakupa dakika kumi tu unaweza ukatoa ujumbe wako.

MHE. MURTAZA A. MANGUNGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa sikuwa na uchungu sana lakini nilikuwa na machungu mengi. Nikushukuru kwa kunipa nafasi japo kwa uchache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijaanza kutoa mchango wangu katika hotuba hii ya bajeti, lazima kwa mujibu wa Kanuni ya 61 na-declare interest mimi ni mmoja kati ya wafanyabiashara ambao tunaagiza bidhaa kutoka nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna tatizo kubwa la umeme hivi sasa. Sisi wafanyabiashara tunaelewa nini athari ya umeme. Nimeipitia na kuiangalia vizuri sana hotuba ya bajeti ya Waziri wa Viwanda na Biashara, sijaona hata eneo moja ambalo Serikali imeweza kufikiria japo kutoa dhamana kwa wafanyabiashara ambao sasa hivi wanashindwa kurudisha mikopo yao katika mabenki. Mimi nadhani hili liangaliwe kwa mtazamo mpana na Serikali iangalie kama vile ambavyo inaweza kudhamini wakulima na watu wa nyanja nyingine, basi wafanyabiashara nao wanashindwa kurejesha mikopo yao kama inavyotakiwa kutoka katika benki ambazo wamekopa, tuangalie na tutoe dhamana, utaratibu huu upo na nchi zote zinafanya pale ambapo crisis inatokea, siyo sababu ambazo zimesababishwa na wao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo la pili ambalo nataka nilizungumzie ni kuhusu suala la bei ya bidhaa, bei ya bidhaa inapanda na hakuna chombo ambacho kinasimamia bei za bidhaa. Bidhaa zote mimi nakubali ziingie katika mfumo wa soko huria lakini bidhaa muhimu ambazo zinawaumiza wananchi wa kawaida lazima ziwekewe mfumo wa kudhibitiwa bei. Kwa kuwa nilikuwa najua nitachangia katika hotuba ya bajeti hii ya Wizara ya Viwanda na Biashara, nimefanya research nyingi sana katika nchi tofauti duniani, hakuna nchi hata mmoja ambayo imeacha uhuru wa wafanyabiashara kuamua bei ya kila kitu, hakuna na kama ipo mimi niko tayari leo Waziri atakapotoa maelezo nakubali kupewa adhabu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa soko huria duniani umeanzishwa na Marekani lakini Mawaziri wote wanafahamu, Marekani kuna kitu kinaitwa Price Control, lazima utoe bei ya ukomo, kuwe na ceiling, mtu ikasema kitu hiki mimi nauza bei hii, wananchi wanaumia na hawana mahali pa kukimbilia, Serikali hiihii ndiyo ambayo inatakiwa iwasimamie wananchi. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nikupe mfano mmoja, mwezi wa tano na wa sita, bei ya chakula ilikuwa ni kali sana, Serikali ikaamua ikubaliane na wafanyabiashara kuwauzia vyakula kutoka katika Ghala la Taifa. Bei ya mahindi wamenunua kwa shilingi 300 lakini bei ya unga inauzwa shilingi 950, kweli Serikali mnaliangalia hili au mnasema tu kwamba inakwenda kwa kufuatana na soko? Gharama ya kusaga unga kweli inafika shilingi 650? Huu ni uonevu, lazima tuweke vitu hivi kwa mpangilio na mwenendo ambao unatakiwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naamini kabisa leo hii tunazungumzia suala la bei ya chakula, jana tumezungumzia tatizo la mafuta, sasa hivi Serikali muelewe kabisa ni lazima tuweke mechanism nzuri ya kusimamia bei ya bidhaa, haiwezekani vika-flow all over na vinginevyo basi Serikali, mashirika yetu tulikuwa na NDL, tulikuwa na NMC, yarudie tena kuzalisha vyakula, kama tunasema ushindani wa bei, basi wasishindane wafanyabiashara peke yao, lazima washindane na chombo kingine ambacho kinaweza kuuza bidhaa kufuatana na maslahi ya wananchi. Kwa nini tuliua NDL na NMC, sisi wote tumekua tukiwa tunajua kwamba mikate, ngano, sukari, mchele, tunanunua NMC au NDL, kwa nini tumeyaua? Hili ni tatizo nililolizungumza jana, kufuata zile policy support instrument, IMF na World Bank, hawajui maisha yetu Watanzania, kama ninyi hamna ndugu maskini, sisi tuna ndugu maskini. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wabunge wengi hapa katika michango yao wamezungumzia sana tatizo la viwanda. Sisi tuna mazao mengine ambayo tunayazalisha, mazao haya hayawezi yakapata soko la uhakika kama hayana mwendelezo. Nimeangalia katika vitabu hivi vya bajeti, SIDO wamepewa pesa kidogo sana. Kwa nini hatuwaongezei mtaji SIDO ikaweza kuongeza viwanda vidogovidogo tukasindika mazao yetu? Kweli tunajua kwamba kuna mgao wa umeme, kuna giza lakini hata hili nalo tuwamulikie tochi mlione, hamlioni hili? (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo mengi ambayo yamepewa viwanda yameshindwa kufanikisha, lakini sisi watu wa Mikoa ya Kusini hasa Lindi, Mtwara na Ruvuma hatujawahi kupewa viwanda. Tupeni sisi tunaweza kuviendesha. Hawa walioshindwa, wameshindwa wao sisi hatujashindwa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, la mwisho kabisa, najua muda ambao umenipa ni mfupi lakini nitazungumzia masuala mawili kwa haraka sana. Kwanza, BRELA wajitahidi kueneza hizi huduma zao katika maeneo yote ya Wilaya. Haiwezekani leo mtu yeyote ambaye anataka kujisajili kibiashara lazima afike Dar es Salaam, hili tuangalie lakini kuna mgogoro ambao umekuwa ukiendelea, nadhani ipo haja sasa ya BRELA kutoa elimu ya kutosha kwa wananchi kuelewa nini maana ya biashara. Kuna tatizo la GS1, limezungumzwa kwenye vyombo vya habari, lakini kwa nini isitolewe elimu ya patient law kwenye sheria zetu za biashara kwamba mtu akishabuni mradi wake aende akausajili, elimu hiyo hapa haitolewi, lakini sheria zetu zina-accommodate.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lingine nataka nizungumzie suala la stakabadhi ghalani, tumelizungumza hapa lakini sheria hii iangaliwe, sikatai sheria kuwepo, lakini wananchi hawajaelimishwa vya kutosha jinsi gani ambavyo wanaweza kunufaika na stakabadhi ghalani, hasa wananchi wa Lindi na Wilaya ya Kilwa. Tuliangalie vizuri na tutoe mwongozo ambao unatosha na stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa na mengine lakini naomba nikushukuru na kwa hayo yote naunga mkono hoja hii kama masahihisho hayo yatafanyika, nashukuru sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana Mheshimiwa Mangungu. Wakati natoa matangazo baada ya maswali, nilisahau tangazo moja na lenyewe ni la matokeo ya michezo iliyofanyika siku ya Jumamosi, tarehe 9 Agosti, 2001. Kulikuwa kuna mashindano kati ya timu ya Bunge ya Mpira wa Miguu na Mpira wa Mikono. Kwa Mpira wa Miguu, timu ya Bunge ilishinda goli moja bila dhidi ya British Council na kwa Mpira wa Mikono, Bunge walishinda magoli 19 dhidi ya Veterani ambao walipata magoli kumi. Nimeambiwa mchezaji hapa ambaye alikuwa ni nyota wa mchezo siku hiyo alikuwa ni golikipa Mheshimiwa Jenista Muhagama. (Makofi)

Mheshimiwa Mnyika nilikuona.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mwongozo wako kwa mujibu wa Kanuni ya Bunge, Kanuni ya 68(7) kuhusu jambo ambalo limetokea mapema hapa. Waheshimiwa Wabunge kwenye michango yao ya siku ya leo wengi wamezungumza kuhusu suala la umeme na wengine wamezungumza kuhusu makaa ya mawe na masuala yanayohusiana na chuma na katika michango yao wamerejea suala la bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini ambayo wameitaja kwamba itasomwa tarehe 13. Katika hoja nyingi zilizojitokeza hapa ni kwamba kuna miradi ambayo iko chini Wizara ya Viwanda na Biashara hususan ya Mchuchuma, Liganga, Ngaka na mengineyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mwongozo wako kwenye jambo moja kwamba tarehe 18 Julai, Waziri Mkuu alipotoa hoja ya kuahirisha mjadala wa bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini, aliliahidi Bunge kwamba Serikali itaandaa Mpango wa Dharura wa Umeme, pamoja na yale masuala mengine na aliahidi kwamba Serikali itafanya hivyo kwa kuzishirikisha Kamati za Bunge. Sasa katika jambo lililo mbele yetu Kamati zinazohusika hasa kwa karibu ni Kamati ya Fedha na Uchumi, kwa maana ya uchumi na kwa maana ya bajeti nyongeza ya fedha; Kamati ya Nishati ya Madini, ambayo mimi ni mjumbe na Kamati ya Viwanda na Biashara kwa maana ya NDC na miradi hii iliyokuwa inataka pesa. Kwa taarifa nilizonazo mpaka hivi sasa zikiwa zimebakia siku chache sana kwa bajeti kusomwa Bungeni, hakuna Kamati yoyote kati ya hizi Kamati tatu ambayo Serikali imeshakwenda kuwasilisha ule Mpango wa Dharura na masuala mengine ya kurekebisha hii bajeti ya Wizara iliyoko mbele yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mwongozo wako ili tuweze kupata maelezo ya Serikali kwa nini mpaka sasa Kamati hizi hazijahusishwa lakini Mwongozo wako vilevile kwenye suala mahsusi kwamba tarehe 13, tunakwenda kufanya kitu gani. Kinachoelekea mpaka hivi sasa ni kwamba Serikali itakwenda kutoa maelezo tarehe 13 na kuwasilisha Mpango wa Dharura na baadaye Bunge litakwenda kupitisha. Nataka Mwongozo wako kama Kamati hizi tatu zitahusishwa ili mambo mengine hata haya yaliyojitokeza hapa ya NDC ikiwemo masuala ya maelekezo ya Jairo lakini vilevile kuna taarifa kutoka ndani ya Serikali kwamba kampuni hii ambayo tumeelezwa hapa ya Sichuan itatekeleza ule mradi imesema kwamba haina pesa kwa ukamilifu wake kama ilivyoahidi kwenye mkataba, sasa haya ni mambo ambayo tungeyajadili kwenye Kamati kama yangekuja kwenye Kamati mapema na tungeweza kuishauri na kuisimamia Serikali kama wajibu wa Bunge. Naomba Mwongozo wako Mheshimiwa Mwenyekiti juu ya suala hili.

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, ni kweli kwamba maelezo ya Mheshimiwa Mnyika ndivyo ambavyo tumekuwa tukienda toka tulipoahirisha bajeti ya Wizara ya Nishati na Madini. Kwanza katika ile sehemu ya kwanza ya Mwongozo aliouomba, amesema ametaka kujua jinsi ambavyo Wabunge wametajataja sana miradi ya umeme, ni kwa sababu iko connected na masuala ya viwanda zaidi na ukizungumza viwanda unazungumza pia biashara. Kwa hiyo, iko connected ilikuwa si vibaya kugusagusa hilo suala la umeme kwa kiasi ambacho wengi wameweza kugusa.

Pia hiyo ikamfanya Mheshimiwa Mbunge akumbuke kwamba sasa tunakwenda tarehe 13 na leo ni tarehe 10 lakini yale ambayo yalisemwa hayajafanyika. Mimi nadhani bado tuna muda wa siku hizi mbili, tatu tujaribu kuona mawasiliano haya yatakuwaje. Sipendi niseme jambo hili la kulisemea baadaye kwa sababu ni dhahiri kwamba kama itakuwa katika hayo majadiliano kati ya Kamati hizo na Serikali yasiporidhisha basi tunajua utaratibu gani utakaoendelea. Kwa hiyo, mimi niseme tu kwamba tusubiri katika muda huo wa siku mbili, tatu tuone hali hiyo itakuwaje.

Nimemuona Mheshimiwa Waziri wa Nchi, Mheshimiwa Lukuvi, kwa maelezo ya nyongeza.

WAZIRI WA NCHI, OFISI YA WAZIRI MKUU (SERA, URATIBU NA BUNGE): Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba tu nimtoe wasiwasi Mbunge wa Ubungo kwa Mwongozo aliouomba kwa kusema mambo mawili. La kwanza, miradi hii inayotajwa na Mheshimiwa Filikunjombe na mingine yote ya Mchuchuma inatekelezwa na NDC ambayo kiusimamizi, kisera iko ndani ya Wizara ya Viwanda na Biashara. Kwa hiyo, Wabunge hawajakosea kuzungumzia miradi hii kwa sababu inasimamiwa na Wizara ya Viwanda na Serikali ni moja, whether huyu amepewa Biashara na Viwanda, maamuzi atakayoyatoa Waziri wa Viwanda jioni ni maamuzi ya Serikali. Kwa hiyo, si lazima asimame Ngeleja hapa ili aseme mambo ya umeme, huyu Waziri ana majibu na atatoa majibu kuhusiana na miradi yote hii. (Makofi)

La pili, Mheshimiwa Waziri Mkuu siku ile alisema tutakuja kutoa Mpango wa Dharura, hii miradi ya Ngaka si Mipango ya Dharura, hii mnaijua sana hatutaki orodha, tulichoahirisha hapa mlitaka tulete Mpango wa Dharura wa kuikwamua hii nchi katika janga hili la umeme kwa muda mfupi iwezekanavyo na Serikali inajiandaa kwa hilo. Nataka nimhakikishie Mheshimiwa Mnyika, ahadi ya Mheshimiwa Waziri Mkuu ya kuitaarifu na kukutana, Waziri atafanya kazi hiyo kabla ya tarehe 13, hilo halitakiukwa, tutafanya. Waziri atawasilisha kwa utaratibu wake Mipango ya Dharura ambayo Serikali imeridhika kwamba inaweza kukwamua tatizo hilo la umeme kwa muda mfupi. (Makofi)

MWENYEKITI: Kwa maelezo hayo nadhani Mheshimiwa Mnyika umeridhika, tusubiri tu katika hizi siku mbili tatu nini kitafanyika, naamini na wao wamesikia ili tuweze kwenda pamoja siku ya tarehe 13.

Basi jioni tutakapoingia tutaanza moja kwa moja na majumuisho ambapo wataanza Mawaziri kwa kadri watakavyokuwa wamepangiana na baadaye tutaenda kwenye Kamati ya Matumizi. Basi nasitisha shughuli za Bunge hadi saa 10.00 jioni.

MICHANGO KWA MAANDISHI

MHE. JITU V. SONI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kwanza kumshukuru Mwenyezi Mungu, na pili wananchi wa nchi wa Jimbo la Babati Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt.Jakayaa Mrisho Kikwete, pamoja na Mheshimiwa Mizengo Kayanda Peter Pinda, kwa kazi kubwa na yenye malengo ya kumsaidia kila Mtanzania kuwa na maisha bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia napenda kumpongeza Mheshimwa Chami - Waziri wa Viwanda na Biashara pamoja na Naibu Waziri, Mheshimiwa Lazaro Nyalandu kwa jitihada yao pamoja na team nzima ya Wizara kuboresha Sekta ya Viwanda na kuboresha mazingira ya biashara nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa ushauri katika Wizara hii ya Viwanda na Biashara ili kuboresha mazingira zaidi kufanya kazi na pawe na win situation kwa upande zote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuishauri Serikali kuharakisha Kitengo cha BRELA iende Mikoani haraka na pia wapokee forms za Annual returns ya Limited companies Mkoani. Ni kero kubwa kutumia Dar es Salaam hiyo returns na malipo yake. Makampuni mengi hulipa fine kwa ajili ya ucheleshwaji wa uwasilishaji wa ripoti ya mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia kuandikisha na kutoa certificates/extracts/na BRELA ngazi ya Taifa tu inachelewesha kusajili makampuni na business names. Nashauri zile ofisi za BRELA Mkoani zianze mapema ili Mtanzania mwenye uwezo mdogo pia aweze kusajili jina la biashara pamoja na kampuni jirani na alipo yeye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia usajili wa brand name, elimu juu ya kusajili brand au jina au product kwa umma utolewe. Wengi wa Watanzania hawajui usajili huu na kupokonywa na wajanja wanaojua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali Kuu pamoja na Serikali ya Mitaa iangalie upya Maafisa Biashara – Mkoani na Wilayani. Kwa sasa kufanya kazi ya kuandika leseni za biashara na kukaa maofisini wengi wao hawajui hata namna ya kuandikisha makampuni, business names, kusajili product, jina au brand. Hawana namna yoyote ya ushauri kwenye kukuza biashara, kuleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi, kibiashara katika Mkoa na Wilaya. Pia ukitaka ushauri na data kuhusu Mkoa au Wilaya kwa biashara tofauti ndani ya eneo lao hawajui. Wangepata mafunzo ya namna ya kuendeleza biashara ndani ya eneo lao. Wawe na data kamili ya fursa za biashara ndani ya eneo lao, wawe na data kamili kutuma ngazi ya juu ili uwepo uhalisia wa biashara na fursa zilizopo Mkoani na Wilayani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iangalie namna ya kudhibiti bidhaa ambazo hazina ubora, bidhaa ambayo Watanzania wananunua kwa bei ya juu na bidhaa kuharibika haraka na muda mfupi, (Taasisi) wadhibiti waliopo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara hawana namna na nyenzo za kufanya kazi, wanabaki Dar es Salaam. Pia Sheria ya Kuuza Bidhaa Feki na yenye ubora wa chini. Ingerekebishwa, waagizaji wangeshitakiwa chini ya (Economic Sabotage) uhujumu uchumi.

Spare ya Magari na Matrekta, spare za machine mbalimbali, vifaa vya ujenzi, bidhaa ya madawa, vipodozi, vyakula vyote vinaletwa chini ya viwango. Mfano mzuri ni kufuli. Kufuli huleta hasara kwa Watanzania wengi sana kuanzia wanafunzi hadi wazazi wafanyabiashara, wakulima na wengine. Kufuli nyingi kwa asilimia 85 ikiwemo ya Solex, Tri-Circle, YALE na nyinginezo ni feki. Ufunguo mmoja wa kufuli ya aina moja hufungua kufuli nyingine. Tunanunua kufuli yenye brand name kwa bei ya juu, lakini funguo zinafunguliana. Naomba Wizara ifanyie kazi suala la kufuli na pia bidhaa nyingine, Tanzania isiwe dumping ground.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nashauri Wizara hii ndiyo iwe kiunganishi kati ya Wizara zote, nyingine wawe coordinators. Mara nyingi coordination kati ya Wizara na Wizara haipo. Mfano, ni kiwanda cha Pamba (guinery) Mkoani Manyara ya Hanang Cotton Mills Wilayani Babati, ina tatizo. Leo miaka mitatu haina umeme. Kiwanda kipo tayari kufanya kazi, pamba imenunuliwa, lakini Wizara ya Viwanda, Kilimo, Chakula na Ushirika bado hawajafuatilia. Ni Wizara ya Nishati na Madini ndiyo imejaribu lakini Wizara ya Viwanda na Biashara, Kilimo, Chakula na Ushirika, Kazi na Ajira, Fedha zote zinazohusika ili Serikali ipate mapato, ajira kwa wananchi, soko la zao la pamba kwa wakulima na mapato kwa TANESCO pia. Serikali ni moja na Wizara ambazo zingeshirikiana naamini tungepata maendeleo kwa haraka na manufaa kwa wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri Serikali iangalie namna ya kuwezesha Watanzania kuanzisha viwanda vidogo na kati kwa kuwezeshwa kiutaalam na kuwawezesha kupata mikopo kutoka taasisi ya kifedha. Taasisi nyingi hawako tayari kukopesha wakulima na wafanyabiashara wanaotaka kuanzisha miradi ya viwanda vya kusindika mazao ya kilimo. Pia Wizara iwe (co- ordinator) kiunganishi kati ya wafanyabiashara na Taasisi za Fedha na Wizara nyingine ili tupate mafanikio na muda wa kukamilisha mradi ufanikiwe. Tukiwa na viwanda vidogo na vya kati vingi, nchi itapata mapato, ajira itaongezeka, mazao ya wakulima yatapata soko na kadhalika. Pia ni muhimu Serikali iangalie namna ya kuanzisha viwanda vya zana za kilimo, mfano, vya vifaa vya umwagiliaji, mbolea, pampu za kupigia dawa na nyinginezo. Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali kwa kuanzisha bar-code yetu ya Tanzania na itatupa fursa, mali na bidhaa ya Tanzania kujulikana na kwa ubora wake. Tunashauri Serikali ifanye bidii ili elimu juu ya bar-code itolewe kwa wananchi wengi na wafanyabiashara wengi kuijua na faida yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo kubwa, tunaomba Wizara ya Viwanda na Biashara itatue ni double licencing, na ada ya (regulatory bodies). Wakala mbalimbali na wadhibiti ambao hawafanyi kazi kwa pamoja kama team, kila wakala au mdhibiti anakuja kwa wakati wake na sheria na kanuni inayomruhusu, inampotezea muda mwenye kiwanda na management ya viwanda na pia gharama yote huwa inabebwa na mwenye viwanda. Mfano, katika viwanda vya maziwa, toka muda wa kuanza kufanya hadi kufikia uzalishaji, ni wakala 17 wanahusika. Sasa wangefanya kazi kama team moja, gharama ingepungua na muda wa management kutumika katika mahojiano na kumtembeza katika kiwanda badala ya siku 17 ingekuwa siku moja au mbili.

Pia mara nyingi kazi zinazofanywa na hizo regulatory bodies ni duplication. Wangeweza kufanya kazi pamoja kwa kushirikiana ili kupunguza adha na gharama. Pia gharama hizi hupelekea bidhaa zinazozalishwa hapa nchini kuwa na bei ya juu na kushindwa katika soko la ndani na nje katika ushindani wa biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, gharama ya uzalishaji maziwa Tanzania ni kubwa kuliko nchi za jirani na nyingine. Pia ni tatizo katika viwanda vingi nchini. Wizara na Serikali waangalie namna ya kupunguza gharama za regulatory bodies na waweze kushirikiana ili kuleta ufanisi, one stop counter au one stop regulatory body ambayo itakuwa na waatalam wa sekta zote na tuweze kushindana katika masoko ya ndani na nje. Pia suala la double licencing liangaliwe upya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba Wizara ya Viwanda na Biashara itume waatalam wake pamoja na Waziri kutembelea Babati Vijijini ili waone fursa zizopo za kukuza viwanda vidogo kati na kubwa Wilayani Babati Vijijini, na watushauri jinsi ya kusonga mbele na Babati Vijijini iwe moja ya sehemu yenye viwanda nchini, pia kuangalia namna ya kukuza biashara mbalimbali Wilayani Babati. Fursa zipo (potential), nia ipo na uwezo upo. Tunaomba ushauri na uwezeshaji

MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda na Biashara kimsingi ndiyo roho ya uchumi wa Taifa lolote duniani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chimbuko halisi la mapinduzi ya viwanda na biashara katika Mataifa ya nchi za Ulaya hasa yale mapinduzi ya viwanda ni nchini Uingereza katika karne ya kumi na tisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushauri wangu sasa kwa Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara ni kwamba, Taifa letu limejaaliwa kuwa na raslimali zenye mwelekeo wa kuleta mapinduzi ya kiviwanda na biashara nchini Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uwepo wa makaa ya mawe huko Mchuchuma na Mlima wa chuma huko Liganga, mapinduzi yako na mzizi wake katika eneo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Mataifa yote yanayopiga hatua za kiuchumi na kiviwanda ulimwenguni yakiwemo Uchina, Urusi hata nchi ya Kiafrika ambayo ni Afrika Kusini, wana mpango wa kudumu wa kutumia makaa ya mawe katika uzalishaji wa nguvu za umeme kwa ajili ya mapinduzi ya sekta ya kiviwanda na uchumi kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwetu Tanzania kuwepo kwa madini ya chuma huko Liganga na makaa ya mawe Mchuchuma ambayo kimsingi yana uhusiano wa moja kwa moja na uzalishaji au uchenjuaji wa chuma ghafi wakati huo huo makaa ya mawe yana manufaa ya kuzalisha nguvu za umeme, Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara nyingine kwa niaba ya Serikali zichangie kikamilifu na kutoa fedha za kutosha na kuwekeza kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC), ili kuwa na nafasi na ushawishi kwenye ubia na mwenezaji Sichuan Hongda Corporation Limited. Mheshimiwa Mwenyekiti, hebu Watanzania tuone umuhimu katika kuwekeza katika jambo hili ambalo lina masilahi makubwa kwa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kupitia mradi huu wa uchimbaji chuma, tutapata chuma cha pua (steel) ambacho chaweza kuwa kichocheo cha kuanzisha viwanda mama, kutengeneza reli na mataruma kwa kuliwezesha Shirika la Reli nchini kutandaza reli karibu nchi nzima na hivyo kurahisisha shughuli za uchukuzi nchini na maghati ya bandari zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwepo kwa chuma cha kutosha nchini kutarahisisha pia shughuli za ujenzi wa madaraja, ghati katika bandari mbali mbali nchini Tanzania. Ziada ya chuma pia inaweza kuuzwa nchi za nje na kukuza uchumi wa nchi hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuwepo kwa mkakati kabambe wa kuendeleza mradi wa Mchuchuma, makaa ya mawe pamoja na chuma Liganga, unapashwa kupewa kipaumbele cha kipekee. Tanzania pia inayo gesi ina madini ya uranum, yote haya yanaweza kuwa na mchango mkubwa katika suala la biashara kwa kuuza nchi za nje na ziada pia inaweza kuwekezwa katika uzalishaji wa umeme na umeme huo ziada inaweza kuuzwa nchi za jirani zenye mahitaji ya umeme na hivyo kuchangia katika kuliingiza Taifa fedha za kigeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania yenye mapinduzi ya viwanda itategemea sana hatua Serikali yetu itakazozichukua tangu sasa na siku za baadaye.

MHE. MWANAMRISHO T. ABAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hoja hii ya Wizara ya Biashara na Viwanda nitachangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa uwezeshaji wananchi kiuchumi, kwanza haujawafikia wananchi hasa wale wa vijijini. Baadhi yao mfuko huu wa mikopo, hawajapata mikopo eti wanaambiwa hawataweza kulipa kwa wakati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watendaji katika Halmashauri zetu ndio wanawapa masharti magumu wananchi, tofauti na malengo yenyewe yalivyo ya kumwezesha mwananchi kiuchumi na lazima upunguze masharti ya mikopo hasa kwa wale wa vijijini kama kweli ndio malengo yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi isiyo na viwanda huwa masikini na wananchi wake pia huwa masikini kwa sababu ajira hamna, kwani viwanda ndiyo msingi wa uboreshaji wa ajira hasa kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zamani kulikuwepo na kiwanda cha Bora ambacho kilikuwa kinatengeneza viatu na tukawa tunavaa viatu vyetu vinavyotengenezwa na nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanini Serikali haifufui kiwanda hiki? Kama ngozi nchini zipo, kwani ng’ombe tunao na ajira zitapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuliwepo viwanda vya SIDO, hata Zanzibar shirika hilo lilikuwepo, viwanda hivyo vilikuwa vinazalisha nguo, masufuria na vitu vingine na Serikali ilikuwa inapata mapato. Sasa kwani viwanda hivi vyote vilibinafsishwaje? Serikali ilikuwa haina uwezo wa kuviendeleza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mara nyingi Zanzibar huwa mnaiweka nyuma katika maendeleo. Zanzibar ni nchi ina Mikoa mitano, Unguja mitatu na Pemba miwili. Sasa katika hotuba ya Waziri wa Viwanda na Biashara ukurusa wa 149 (218)(d), amesema kuhusu kuimarisha Ofisi ya Zanzibar ili iweze kusaidia juhudi za kukuza Sekta ya Biashara Visiwani ni sawa. Lakini naomba, hiyo Ofisi iwe na matawi yake katika kila Wilaya zote kwani kuna Sekta ya Uvuvi Vijijini na uzalishaji wa Mwani. Hawa mnawasaidiaje? Kuna vikundi vya ushirika wa mifugo na mimea ya matunda, miti ya mbao, yaani mivinge. Hawa nao mnawasaidiaje? Kwani mara nyingi huwa mikopo haiwafikii na yote huishia Mijini kwenye wajanja na ndio maana nikashauri hiyo Ofisi iwe na matawi katika Wilaya ili wananchi wafaidike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ushauri wangu ni kwamba, kwanza Wizara ifufue viwanda vyote vilivyopo nchini na pia Wizara iweke mkakati wa kila kipindi cha bajeti, ijenge kiwanda kipya kimoja na ijenge viwanda katika kila Mkoa kulingana na mazao au nishati au malighafi iliyopo katika Mikoa yetu ya Tanzania kwa kupima miradi ya SIDO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wasalaam.

MHE. MARYAM S. MSABAHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami nachukua fursa hii kuchangia hotuba ya Waziri wa Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na viwanda vingi sana hapa Tanzania, lakini kuna baadhi ya viwanda vingi vimekufa na hata hivyo vilivyobaki havizalishi vya kutosha kutokana na tatizo kubwa la nishati ya umeme. Kutokana na tatizo hili la umeme, linapelekea Serikali kukosa pato la Taifa na pia kukosekana kwa ajira nyingi na za uhakika kwa vijana. Napenda kumwuliza Mheshimiwa Waziri, ni viwanda vingapi vinavyofanya kazi na kuingizia Serikali pato la Taifa na pia ni viwanda vingapi vimekufa na Serikali ina mpango gani kuvifufua viwanda hivi vilivyokufa kwa mfano MUTEX kilichopo Musoma, MWATEX kilichopo Mwanza na vinginevyo? Naomba Waziri anipatie majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Shirika la SIDO limesaidia sana wananchi wakiwemo akina mama wengi, wamepata mafunzo ya usindikaji wa vyakula: Je, Serikali haioni sasa kuna umuhimu wa kuwawezesha SIDO ili waweze kutoa mafunzo zaidi hasa kwa wajasiriamali wengi waliopo vijijini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kuna Mikoa mingi hapa Tanzania katika msimu wa matunda, matunda mengi huwa yanaharibika kwa kukosa soko la uhakika: Je, Serikali ina mikakati gani kuhakikisha inawajengea wakulima hawa wa matunda viwanda vidogo vidogo vya usindikaji wa matunda? Endapo Serikali itajenga viwanda hivi, wakulima wengi watanufaika na matunda yao yanayoozea mashambani na vijana wengi watajipatia ajira katika viwanda hivyo na pia itachangia kuongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kuna baadhi ya viwanda vya wawekezaji vimekuwa vikiwanyanyasa wafanyakazi na kuwapa kipaumbele wageni kuliko wazawa: Je, Serikali haioni sasa milango inayofunguka mbele ya wawekezaji wageni haifunguki mbele ya wawekezaji wazawa? Naishauri Serikali, masharti ya wawekezaji wa kigeni yawe sawa na masharti ya wawekezaji wazawa ili kuwapa kipaumble wazawa wa hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya saruji vimekuwa vikizalisha saruji, lakini saruji hii upatikanaji wake kwa wananchi umekuwa ni wa taabu na saruji hii imekuwa ikiuzwa kwa bei ya juu. Lakini ukiangalia saruji inayozalishwa nje, imekuwa ikipatikanika kwa bei nafuu. Tatizo hili la saruji kuuzwa kwa bei ya ghali inawafanya Watanzania walio masikini na waishio vijijini washindwe kumudu kununua saruji na kutoweza kujenga nyumba za kisasa. Nilikuwa namwomba Waziri aniambie ni kwa nini saruji ya kutoka nchi za nje inapatikanika kwa bei nafuu kuliko saruji yetu inayozalishwa hapa nchini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uhaba wa sukari, imepelekea kupanda kwa bei ya sukari. Serikali haioni kwamba umefika wakati muafaka kwa wafanyabiashara wadogo wa sukari wanaochukua sukari kutoka nchi za jirani kama Malawi wakaachiwa kufanya biashara hii bila kufukuzana na TRA? Ukiangalia kama Mkoa wa Mbeya, kiasi kikubwa cha sukari wanayotumia inatoka Malawi na hii ni kwa sababu ya uhaba wa uzalishaji wa sukari hapa Tanzania. Nilikuwa naishauri Serikali kama haitaki Watanzania kutumia sukari inayotoka nchi za wenzetu, basi Serikali ihakikishe kwamba viwanda vyote vinavyozalisha sukari hapa Tanzania viboreshwe ili viwe na uimara wa kuzalisha sukari kwa kiasi kikubwa na Watanzania waweze kutumia sukari yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitaunga mkono hoja endapo nitapatiwa majibu kwa haya yote niliyoyachangia kwa maandishi hapo juu.

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Waziri, Naibu wake, na watendaji wote wa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kuandaa hotuba na kuileta hapa Bungeni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi zote zilizoendelea duniani viwanda ndivyo vilivyoweza kuinua uchumi wa nchi na pato la wananchi hao. Kwa hapa kwetu suala la viwanda bado hatujaweza kulipa kipaumbele kwa kutambua umuhimu wake. Hili linajionyesha wazi kwenye bajeti iliyopangwa kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bajeti iliyopangwa haiwezi kutekeleza mipango mizuri iliyoainishwa hata nusu, ndiyo maana kila mwaka Wabunge wanasema/kutoa maombi yale yale. Ahadi zinatolewa hazitekelezeki. Leo ni miaka kumi tunajadili chuma cha Liganga na Mchuchuma kupata vyuma na makaa ya mawe kwa nishati. Utekelezaji uko wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulikuwa na viwanda vingi maeneo mbalimbali na viwanda vile vilijengwa kimikakati kutegemeana na upatikanaji wa materials kwenye maeneo hayo. Viwanda vyote vimebinafsishwa pamoja na mashirika ya umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, waliobinafsishiwa viwanda vingi wanashindwa kuviendeleza na hivyo vimekufa na wengine wamebadilisha matumizi ya viwanda hivyo na kuanzisha shughuli nyingine. Mfano, TAWICO Arusha, kiwanda pekee cha kuchakata Nyara za Serikali na kutengeneza bidhaa zake kama ngozi, kwato, pembe za wanyamapori. Leo pale ni sehemu ya kuunganisha bodi za magari. Serikali imenyamaza kimya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda cha kutengeneza zana za kilimo, Mbeya, leo kinatengeneza bia. Viwanda vingine vimefanywa ni karakana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wawekezaji hawa wamekiuka mikataba yao, kwa nini Serikali imeendelea kunyamaza kimya? Tunashindwa kusimamia mikataba hii muhimu huku vijana wetu wanaranda kwa kukosa kazi mijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itoe maelezo, nini hatma ya viwanda ambavyo tangu vibinafsishwe mpaka leo havijawahi kufanya kazi na ni hatua gani zimechukuliwa kwa wale waliouza mashine zote viwandani kama vyuma chakavu na hivyo kuua kabisa viwanda hivyo, mfano Kiwanda cha Nyuzi Tabora, Misitu Handeni na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu imeonyesha udhaifu mkubwa sana kulinda viwanda vyetu vya ndani kwa kuruhusu biashara huria kwa kila kitu bila utaratibu wala kuangalia athari zake kwa soko la ndani. Ni tatizo. Sisi tumekuwa ni soko zuri kwa bidhaa za nchi za jirani wakati bidhaa zetu hazina wanunuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, miaka 1990 – 2003 Kiwanda cha Urafiki kilikuwa kinafanya kazi nzuri sana na kwa wakati ule Best Khanga, best kitenge, Afrika Mashariki zilipatikana Tanzania kutoka Kiwanda cha Urafiki. Kwa kushindwa kulinda soko letu leo kanga ya Urafiki haina nguvu haina soko. Zipo khanga za Kichina Kariakoo zinauzwa hadi Sh. 2,000/= kwa doti. Nani anunue khanga ya Urafiki kwa Sh. 5,000/=?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna viwanda vya plastics hapa ndani ya nchi, lakini ukienda sokoni, plastics nyingi zimejaa kutoka Kenya tena weak kuliko za kwetu. Tunaendeleza viwanda vya Kenya, vya kwetu vimeendelea kudorora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha Serikali kuruhusu uingizaji wa vitu vidogo kama tooth picks, cotton buds na kadhalika, inaonyesha kwa jinsi ambavyo tumeshindwa kusimamia hata viwanda vidogo na kutoa ajira kwa vijana wetu. Ni utaalamu gani unahitajika kutengeneza tooth picks? Hii ni aibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bidhaa feki, bado hatujawa na utendaji mzuri wa TFDA, TBS na Fair Competition. Wanakuwa wapi mpaka bidhaa zinaingia madukani/masokoni? Mwaka 2010/2011 Tume imekamata na kuteketeza bidhaa za Shilingi milioni 824.7. Je, ni ngapi ambazo ziliwafikia walaji kabla ya wao kuteketeza hizo chache? Je, ni athari kiasi gani na risks kwa walionunua bidhaa hizo kwa maisha yao na familia zao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nchi tuamke. Watendaji fanyeni kazi. Kuna nyaya za umeme/na vifaa vingine vya umeme feki, kuna tairi za magari feki, madawa kwenye pharmacy feki na vyakula madukani feki. Ni kwa kiasi gani tunahatarisha maisha ya Watanzania? Leo magonjwa ya Kansa yameongezeka mpaka kwa watoto. Je, siyo bidhaa, vyakula feki tunavyoruhusu kuingizwa Tanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imetamka hapa Bungeni kwamba samani zote za ofisi za Serikali zitanunuliwa ndani ya nchi kwa material/mbao zetu. Mbona bado wanaagiza fanicha nje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali ifufue kiwanda cha mbao cha Tabora (Tabora Forest) kiweze kutumia neema ya mbao tulizonazo Tabora kutengeneza fanicha quality, tutoe ajira kwa vijana wa Tabora na kuendelea uchumi wa Mkoa na Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumeshauri mara ngapi kuhusu viwanda vya maziwa na kutengeneza juisi za matunda? Tulitegemea angalau kwa bajeti hii ionyeshe viwanda vya matunda kwa Mikoa yenye matunda, yaani Tabora, Tanga/Muheza na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wajibu wa Serikali kuwalinda wajasiriamali wa ndani ya nchi kwa kutambua mchango wao kwa uchumi wa Taifa na maendeleo kwa ujumla. Mheshimiwa Mwenyekiti, Katibu Mkuu wa Wizara hii ya Viwanda na Biashara anatuhumiwa kwa kuwapora wajasiriamali mradi kuanzisha mfumo wa utambuzi wa bidhaa (Bar Code).

Mheshimiwa Mwenyekiti, wajasiriamali wa Kampuni ya GIS Tanzania Ltd walitoa wazo hilo na wakaleta maombi kuomba kusajiliwa kwa mradi huo. Katibu Mkuu aliwaomba wamwachie yeye jina hilo asajili. Walipokataa alitumia nafasi yake ya utendaji mkuu wa Wizara kusajili kampuni ya GIS National Limited.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huu ni ubinafsi wa hali ya juu, haukubaliki na inashangaza Mtendaji Mkuu awe na maslahi binafsi kwenye suala hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunawakatisha tamaa wajasiriamali na tunaonyesha udhaifu mkubwa kwa watendaji wa Serikali. Serikali itoe maelezo juu ya tuhuma hizi nzito.

MHE. RAMADHAANI H. SALEH: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichukue nafasi hii kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kutufikisha katika Bunge hili tukiwa katika hali ya uzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nichukue nafasi hii kumshukuru Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri ambayo imejaa matumaini kwa Watanzania ambao wana hamu ya maendeleo ya nchi yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie hotuba hii kwa kujikita upande wa viwanda. Tanzania ina tatizo kubwa la viwanda, tatizo hilo linapelekea hata hali ya uchumi kuwa siyo nzuri. Viwanda ndiyo njia pekee ambayo inaweza kuinua uchumi wa nchi yetu. Bila kuwa na viwanda, uchumi wetu hautakua, hata tatizo la ajira nchini halitaondoka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri aniambie, ni lini ataanza kuvifufua viwanda hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima wetu Watanzania, asilimia kubwa wanategemea kuuza mazao yao katika viwanda na kwa sasa bado Serikali haijajipanga vizuri katika eneo hilo. Ndio kusema kwamba uchumi wa wananchi ambao wanategemea kilimo, maisha yao yanakuwa hatarini kwa kukosa sehemu ya kuuzia mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi ambazo zimeendelea, kama nchi ya China wamepiga hatua kwa sababu ya viwanda. Naomba nijikite zaidi upande wa biashara. Biashara katika nchi yetu, vile vile bado haijashughulikiwa vizuri. Kumekuwa na wafanyabiashara wababaishaji, wafanyabiashara hao wamekuwa wakituletea bidhaa ambazo zimepitwa na muda, na nyingi kati ya hizo haziko katika kiwango kinachotakiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri atakapofanya majumuisho, naomba atuambie ni lini wafanyabiashara hao watachukuliwa hatua ambayo inafaa, hata baadhi ya maradhi ambayo wananchi wanapata katika nchi yetu, ni baadhi ya vyakula vya makopo ambavyo vimepitwa na muda kuuzwa katika maduka nchi bila kuangaliawa tarehe ya kumaliza muda wake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namwomba Mheshimiwa Waziri awatupie macho hawa (TBS) ambao ndio wenye dhamana ya viwango nchini, kwani hata madawa ya Kichina yamezagaa nchini, na yenyewe ndiyo yanayotukatishia maisha yetu Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri, hatua kali juu ya wanaohatarisha maisha yetu Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.

MHE. MARIAM S. MFAKI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Waziri wa Viwanda na Biashara, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wa Wizara kwa kuandaa hotuba hii ya Wizara. Baada ya utangulizi huo, naomba kuchangia yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mauzo ya biashara mbalimbali zikiwemo vipuli vya magari, mashine, vinakuwepo vipuli vyenye ubora na vile ambavyo havina ubora ambavyo kwa watu wengi havitofautiani sana na wakati mwingine ananunua bila kujua. Naomba Serikali itoe maekelezo, vifaa hivi viwekwe kwa ubora wao na viwe wazi na maduka yafunguliwe kufuatana na ubora wa vyombo hivyo ili wasiwachanganye wanunuzi, wafanyabiashara waeleze kweli, wasiwadanganye wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi wameitika wito wa kuanzishwa viwanda vidogo vidogo kama vile vya kukamua mafuta ya alizeti, kusaga unga na kadhalika. Tunaomba sasa Serikali ituwezeshe kupata masoko ya ndani na nje ya nchi. Vile vile tunaomba Serikali itutafutie mafunzo ya kusindika nyanya, mapera, embe na mboga mbalimbali. Ni lini Serikali itaendesha mafunzo hayo kwa wanawake wa Mkoa wa Dodoma ambao wengi ni wajasiliamali? Hilo ni muhimu sana ili biashara zao ziwe na tija kwa manufaa yao na familia zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Vituo vya SIDO vinafanya kazi nzuri sana ya kufundisha wajasiriamali na kuwakopesha. Tunaomba SIDO iboreshe kwa kuongezwa fedha ili ifundishe watu wengi na wawakopeshe waweze kujiajiri. Kwa kufanya hivyo, tutapunguza umasikini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Maonyesho ya bidhaa katika sherehe za wakulima, Nane Nane ni muhimu sana na wananchi wanajifunza sana. Baada ya kuona na kugawa zawadi na kutawanyika, Serikali inakaa kimya, wananchi wanakaa kimya, mpaka tena nanenane nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua, Serikali imeweka utaratibu gani wa kuhakisha maonyesho haya wananchi wanafaidikaje kupata maoni yao? Vinginevyo, maonyesho yataonekana ni kuja kusherehekea tu, basi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja mia kwa mia.

MHE. CONCHESTA L. RWAMLAZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie hoja hii kwanza kwa kuongelea bajeti yenyewe. Bajeti hii ni ndogo na tafsiri yake ni kwamba Serikali haina dhamira ya kufufua viwanda na hata kutekeleza miradi mikubwa ambayo baadaye ingepelekea nchi hii kuendelea kiviwanda. Nchi zilizoendelea msingi mkubwa ni viwanda, lakini pia ni msingi wa mapato ya Serikali.

Wabunge wengi wakisimamia wanaomba kutengenezewa miundombinu katika majimbo yao mfano, maji, barabara na kadhalika. Lakini mbinu za kuongeza mapato je? Viwanda ni sululuhisho, ajira kubwa hutolewa na viwanda P.A.Y.E. ya uhakika, lakini walipa kodi hutambuliwa kwa urahisi. Wizara imeweka bidii kufanya tathmini ya viwanda vilivyobinafsishwa na kufa na vingine kuendelea. Tunaomba Serikali ichukue hatua za haraka kuvirejesha viwanda vilivyoshindwa katika mikono ya wazawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa mjadala EPZA ili maeneo haya yaweze kufanikiwa, Serikali itoe fedha za kulipa fidia kwa wananchi waliotwaliwa maeneo yao. Serikali iandae mpango wa kuwapatia watu makazi (settlement) ili wanapopata fidia wawe tayari na sehemu za kuishi. Kwa kuwa mara nyingi fedha hizi zinakuwa kidogo, wajengewe nyumba bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba SIDO wapewe uwezo wa kifedha ili watimize malengo yao ya kuandaa maeneo katika kila Wilaya ili kusaidia vijana wetu waweze kujiajiri. SIDO ni mtambuka, zana zinatengenezwa chini yake, zinanunuliwa na Watanzania walio wengi wa hali ya chini na ndiyo wanaojenga uchumi wa nchi. Serikali iongeze fedha kwa SIDO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri Mkuu alitoa bei elekezi ya kununua sukari hapa nchini kwa bei ya Sh. 1,700/=. Hivi sasa katika Mkoa wa Kagera, sukari inauzwa kwa kati ya Sh. 3,000/= mpaka Sh. 2,500/=. Je, kilichotokea ni nini? Serikali itoe majibu na tamko juu ya bei ya sukari nchini.

MHE. ALBERT O. NTABALIBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami naungana na Waheshimiwa Wabunge wengine kupongeza Wizara na Mheshimiwa Dkt. Cyril A. Achami na Naibu wake - Mheshimiwa Nyalandu kwa hotuba nzuri na ya kina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia Wizara hii kwa mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Masoko ya mipakani ni moja ya hatua katika kuboresha biashara. Katika jibu la Waziri alijibu kwamba Jimbo la Manyovu – Kasulu, katika Kijiji cha Mnanila, soko hilo litajengwa. Naomba niishukuru Wizara na Waziri, kwani wananchi wamepongeza sana hatua hiyo kwani ni ukombozi thabiti wa kuendesha biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunayo kero kubwa ya uuzaji/biashara ya mifugo hasa minada. Jimbo la Manyovu linao mnada wa Tarafa ya Muyama ambao ulikuwa unasaidia wafugaji kupata mahali pa kuuzia mazao ya mifugo ambao umefungwa na hivyo kuleta kero kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwako ni kuwasiliana na Mkurugenzi wa Wilaya ya Kasulu/Afisa Biashara, kuamuru kufungua mnada huo, kwani pia umekuwa kikwazo cha kukubalika kwa chama tawala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bidhaa/ubora, naishauri Serikali kuwa wakali kwani wauzaji wanaweza kukueleza kwamba hii ni original na hii ni feki. Naomba tabia hii ikomeshwe, kwani inaonyesha Wizara haidhibiti ubora wa bidhaa zake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wa kawaida wanataka Wizara ifanye yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wanataka Urahisi wa kupata leseni za biashara, motisha ya ufanyaji biashara hasa ya uuzaji nje, kutoa vizuizi njiani na kuepusha kusumbuliwa na askari wetu, kutenga maeneo ya kufanyia biashara ndani ya Halmashauri zetu, kupunguza biashara barabarani hasa Dar es Salaam, bei ya vitu kutokuwa kubwa, Wizara ijitangaze, ijulikane kwa watu wadogo, muda wa kuchukua bidhaa bandarini, kutambua biashara za mama ntilie na mitumba. Punguzeni kutoa leseni kwa wageni ambao kazi zinafanywa na wazawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, nawaamini kabisa na ninawatakia kazi njema. Mungu awape hekima na Watanzania wajue vijana mnatuwakilisha.

MHE. JOHN P. LWANJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua Serikali ina msimamo gani kuhusu juhudi nilizofanya za kutafuta wawekezaji wa Kiwanda cha Saruji Itigi. Maombi yamekuwepo toka enzi za Mheshimiwa Bazil Mramba, Mheshimiwa Mary Nagu na sasa Mheshimiwa na Naibu Waziri - Mheshimiwa Lazaro Nyalandu. Itigi inajulikana, iko katikati ya nchi na ina miundombinu yote pamoja na malighafi ya jas na kadhalika. Ni rahisi kusambaza saruji kwa bei nafuu sana kutoka Itigi kwenda Kanda za Magharibi, Kati na Ziwa kwa reli na barabara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kujua, utafiti wa malighafi ya chokaa katika mbuga za Ughwandi na Wambere umefikia wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Mawaziri wa Wizara hii watatembelea Itigi kuona uchimbaji wa jas Kiwanda cha Chaki, Kiwanda cha alizeti na viwanda vidogo vidogo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasilisha.

MHE. NAOMI A. M. KAIHULA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie suala la maendeleo ya viwanda na biashara. Hakuna maendeleo ya kweli bila viwanda. Tanzania hii ya sasa inapaswa kuimarisha viwanda vya msingi vile vya mkakati. Mfano, viwanda vya uzalishaji wa zana za kilimo, kiwanda cha UFI na kile cha zana za kilimo Mbeya, hivi vilikuwa vinazalisha vifaa vya kilimo kwa ajili ya wananchi waliokuwa wanahitaji zaidi. Hivi ni kwa nini hatuzalishi vifaa vyetu tunawaacha wananchi wetu kuagiza vitu vyenye bei kubwa toka nje? Tufufue viwanda vyetu watu wapate nafuu ya bei na vifaa bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutathamini viwanda vyote vilivyoanzishwa wakati wa Baba wa Taifa ambavyo kusema ukweli vilikuwa vimepangwa kimkakati na vilitawanyika Tanzania pote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mwalimu J. K. Nyerere alikuwa anaona mbali sana kwa wakati. Lakini Serikali yetu haioni lazima tutambue kuwa World Bank (WB) na IMF hawa wanafanya maamuzi kwa faida ya nchi zilizoendelea ambazo nia yao ni kutugeuza sisi kuwa ‘Masoko’ yao hivyo wanafanya ujanja ujanja kutuchelewesha kujitegemea? Hivyo, wanapitia mlango wa nyuma kwa kutuletea mikataba mibovu msfano kutushauri kujitoa katika uzalishaji )production) na kurudi kwenye service. Je huoni kuwa hapa kuna hila tu. Serikali haya haiyaoni?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inapaswa kuwa na “Intelligence”. Lazima vijana wetu wasomi wa mambo mbalimbali wafundishwe “ujasusi wa kiuchumi”. Hawa wapelekwe nchi mbalimbali wakafanye kazi kwa ajili ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali pia inapaswa kuwa makini zaidi katika utekelezaji wa majukumu yake, mojawapo la msingi ni kuhakikisha kuwa “wana-enforce the law”. Hii ndiyo kazi yao kuu katika utekelezaji wa sheria. Ni muhimu wakajichunguza ndani yao iwapo wote wana lengo moja, kwani ilivyosasa Serikali imejichanganya sana hadi kufikia kuzidiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imepewa chombo cha dola ili kuisaidia kutekeleza sheria. Mfano mzuri ni wafanyabiashara wa mafuta, sukari na kadhalika wanaelekea kuwa wako juu ya Serikali hadi Serikali inashindwa kuwa na uamuzi wa jinsi ya kuwadhibiti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hayo hapo juu yanawezekana iwapo Serikali itakuwa mwaminifu kwa wananchi na siyo kwa Chama chao kama ilivyo sasa kila wakati kulindana na kupongezana hata kwa mambo yasiyokuwa na tija kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

MHE. HAROUB MOHAMED SHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali kabisa namshukuru Mwenyezi Mungu (S.W.) kwa rehema, neema na ihsani zake nyingi kwangu. Ni wajibu kutamka neno la Shukrani, Alhamdulillah.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Viwanda na Biashara ni jambo kubwa, zuri na muhimu sana siyo tu kwa maendeleo ya nchi yoyote, bali pia kwa heshima na ustaarabu wa maendeleo hayo na nchi husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu iko nyuma sana katika sekta hii ya viwanda, na biashara pia. Wakati siyo umefika sasa, bali umepita kwa Serikali kuweka mkazo wa dhati katika kuinua viwanda na biashara kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vyetu vingi vina hali duni sana, ni wajibu wa Serikali kuratibu uboreshwaji wake. Vile ambavyo vina hali nzuri ni vichache.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili dhana ya kutaka kulipeleka Taifa katika uchumi wa kati, ni wajibu wa Serikali kusimamia kwa vitendo, nia safi na uwajibikaji wa kweli katika sekta ya viwanda na pia biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umasikini wa watu wetu hauwezi kuondoka kwa kuweka mipango na mikakati bila ya usimamizi wa dhati ya utekelezaji wake. Serikali ifanye wajibu wake ili mazao ya wakulima yaongezewe thamani kwa kusindikwa viwandani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lipo tatizo kwenye viwanda vyetu la kuomba nembo ya TBS na kisha kuzalisha bidhaa za chini ya viwango, na hivyo kushindwa ushindani wa soko la ubora, “Quality standards”. Hali hii haitusaidii! Serikali ipo, lakini pamoja na kuwa inasikia, lakini haioni! Balaa zaidi ni kwenye viwanda vya dawa, hasa za watoto. Wanakoroga sukari na ladha tu bila ya “medicinal contents” zinazostahili kuwemo kwenye dawa husika!

Mheshimiwa Mwenyekiti, dawa hasa za maji, “Liquid medicine” mara nyingi zinakuwa na uchafu. Kabla sijakuwa Mbunge, nilinunua dawa ya kikohozi ya motto. Nilipofika nyumbani nikaitikisa ili nimnyweshe mtoto, nikakuta vigae vya chupa kwenye dawa hiyo! Niliipeleka TDFA, pamoja na juhudi hiyo niliyoifanya, hakuna faida iliyopatikana kwani nilijibiwa bila ya aibu, “wanaohusika wametoka, njoo kesho. Hiyo ndiyo hali ya Serikali sikivu! Je, macho, inaona?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na bidhaa nyingi zinazozalishwa na viwanda vyetu kuwa na viwango vya chini, pia zinakuwa ghali ukilinganisha na za nje. Tatizo ni nini? Wenye viwanda wanapewa msamaha wa kodi wa “malighafi”, mishahara wanayowalipa wafanyakazi wao ni duni sana. Kwa kigezo gani bidhaa zao zinakuwa ghali?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili nchi iweze kusonga mbele ni lazima sekta ya biashara ikue. Kukua kwa biashara ni pamoja na nchi kusafirisha bidhaa zake za viwandani nje ya nchi. Hii itasaidia kuinua uchumi na kutuliza mfumuko wa bei. Serikali lazima ilisimamie hilo. Viwanda vizalishe bidhaa bora zinazokidhi ushindani katika soko, lakini pia ziwe na bei muafaka zinazoweza kushindana na bidhaa zilizo bora zinazotoka nchi jirani ya Kenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa biashara unahitaji kuboreshwa na Serikali iweke mazingira mazuri ya ushindani baina ya wafanyabiashara, Serikali itangaze bidhaa zetu nje ya nchi hasa kupitia Balozi zetu na maonyesho ya nje. Wafanyabiashara wa kati na wadogo wapewe vipaumbele vya kuwezeshwa ili wakue. Misamaha ya kodi kwa wafanyabiashara wakubwa iangaliwe ili kuwe na “Real Fair Competition” baina yao na wafanyabiashara wa kati na wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la bidhaa feki “counter feit goods” linazidi kukua nchini. Hii inaonekana kama kuna mwanya (loop hole) au kuna mtandao maalum wa wafanyabiashara wakubwa ambao wana mahali pa kuegemea na hivyo wao hawaguswi. Badala yake wanakaliwa rohoni wafanyabiashara wa kati na wadogo tu.

Mheshsimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuwasilisha mchango wangu. Naomba uzingatiwe kwa faida ya nchi yetu.

MHE. ELIZABETH N. BATENGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wote kwa kuandaa na kuwasilisha hotuba nzuri yenye maelezo ya kina.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivi kumetokea nini kinachofanya sukari ipande sana? Inashangaza sukari kuuzwa zaidi ya Sh. 2,000/= Mjini Bukoba kilometa 80 toka Kiwanda cha Kagera Sugar. Naomba maelezo ni kwa nini bei inazidi kupanda licha ya Serikali kutamka bei isizidi Sh. 1,700/=.

Mheshimiwa Mwenyekiti, soko huria ni mfumo ulioanzishwa baada ya Serikali kujitoa katika biashara. Mfumo wa soko huria unapaswa kusimamiwa na Serikali ili wafanyabiashara wasijipangie bei kiholela hasa wanaponunua mazao ya wananchi. Nashauri kwamba Serikali iwe na chombo cha kudhibiti bei kwa ajili ya bidhaa mbalimbali na pia mazao ya wakulima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei za bidhaa zinatofautiana na Mkoa hadi Mkoa, Wilaya na zinapofika vijijini huwa bei inakuwa kubwa sana. Je, haiwezekani bei zikalingana sehemu nyingi kama ilivyokuwa kwa bia na soda?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mikoa ya Kanda ya Ziwa inaumia sana kutokana na bei kubwa ya vifaa vya ujenzi, maana vyote husafirishwa toka Dar es Salaam kwa kutumia malori. Serikali ina mpango gani wa kuleta mwekezaji wa kujenga kiwanda cha saruji ili wananchi wa maeneo hayo nao wapate ahueni ya bei, lakini pia vijana wapate ajira? Haifai kulundika viwanda vyote Dar es Salaam, Morogoro Arusha na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. SHAFFIN A. SUMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naunga mkono hoja. Lakini kuna masuala ambayo Serikali inahitaji kujipanga vizuri zaidi na kuweza kuleta ufanisi zaidi katika mwaka huu wa fedha. Fedha zilizoombwa na Wizara ni kiasi kidogo sana ukilinganisha na hali halisi ya mahitaji ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili tuweze kuzalisha ajira kwa wingi ni bora “SIDO” iwezeshwe kwa kupewa fedha za kutosha. SIDO ina uwezo wa kuandaa vijana wetu kuweza kukabiliana na ushindani wa kibiashara unaotegemewa kuwepo hapo baadaye.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tabora una uwezo wa kuendelea kupanda maembe mengi sana, lakini hata sasa kipindi cha msimu wa maembe tunakuwa na maembe mengi sana na hatuna pa kupeleka, hakuna hata kiwanda kimoja cha kusindika maembe. Hali hii inasikitisha sana. Serikali itusaidie tupate wawekezaji wa kusindika matunda yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora inaongoza kwa kuwa na asali nzuri lakini kwa hukosa soko la uhakika. Wananchi wengi wanajishughulisha na kulima tumbaku jambo ambalo sasa linaathiri ubora wa asali kwani nyuki wengi wanakwisha lakini pia nyuki zilizobaki zinanyonya kutoka kwenye miche ya tumbaku ambapo asali inayopatikana inakosa ubora wake wa awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itusaidie kuokoa uvunaji wa asali na kuendelea kuhimiza utunzaji na uvunaji wa asali, lakini pia Serikali itusaidie kufufua kiwanda cha asali cha Kipalapala. Mkoa wa Tabora tuna kiwanda kimoja cha nyuzi, lakini tangu kibinafsishwe, utendaji umekuwa ukipungua mwaka hadi mwaka na sasa kimefungwa. Naomba Serikali iingilie kati na kutusaidia kiwanda hiki kiweze kufanya kazi ili Wanatabora wanufaike na ajira lakini pia pamba iweze kupata soko la uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tabora inazalisha tumbaku nyingi kuliko Mikoa yote ya Tanzania inayolima tumbaku, lakini jambo la kusikitisha ni kwamba hatuna kiwanda cha tumbaku wakati eneo tunalo, mali ghafi tunayo na raslimali watu wapo. Ni kwa nini tukose kiwanda cha tumbaku?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itupe majibu na mpango mzuri wa kuiendeleza Mkoa wa Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuwasilisha.

MHE. SALUM K. BARWANY: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kwa kuchangia katika eneo la soko la bidhaa za biashara katika masoko ya nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna miaka 50 leo Serikali haijawaandaa Watanzania kama wafanyabiashara wa bidhaa zetu kwa masoko ya nje. Bado tunategemea wageni kuuza mazao yetu huko nje, bado Watanzania ni middle men katika sekta hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kipindi chote tumeshindwda kuingia katika mashirika ya Kimataifa katika kuuza bidhaa zenye ubora katika masoko ya nje na tumeshindwa kuingia katika ushindani wa kiuchumi duniani. Ni muhimu kwa sasa kutoa elimu kwa wananchi kwa jumla kuhakikisha bidhaa zetu zina ubora unaohitajika Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mali nyingi za wakulima (bidhaa) zake hupelekwa katika masoko yakiwa ghafi na hupelekea wakulima hao kupata bei ya chini wanapopeleka bidhaa zao hizo sokoni. Hatuwezi kuboresha katika maana ya uboreshaji bidhaa zetu kama bado hatujawa na viwanda, yaani Processing Industries kwa bidhaa ya wakulima?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni vyema tuhakikishe kila zao la biashara tuanze na kiwanda angalau kwa asilimia 20 ya zao hilo la biashara lile Processed pale pale kwenye zao husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tufungue mjadala wa Kitaifa juu ya stakabadhi ghalani, kwani kwa sasa wakulima wengi wana malalamiko juu ya mfumo huo, lakini inaonekana ni Serikali tu inaona ina maslahi juu ya mfumo huo, lakini bado wakulima wana malalamiko juu ya makato makubwa wanayokatwa. Katika makato makubwa zaidi ya 30% ya bei ya bidhaa hizo hutozwa tozo hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wakulima waulizwe, watoe maoni yao juu ya stakabadhi ghalani kwamba tangu mfumo huu uanzishwe, wakulima wanauonaje? Una maslahi kwao au unawanufaisha wachache?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu soko la korosho, tulipopata uhuru mwaka 1961 tulikuwa na tani 140,000 wakati tukiwa na watu 12,000,000. Lakini leo idadi ya Watanzania zaidi ya milioni 40 bado zao hilo halijaongezeka zaidi ya kupungua tani zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni wakati muafaka sasa Serikali ianzishe utaratibu wa kushughulikia soko la korosho ikiwa Processed kupitia viwanda vilivyopo Kusini ili tuondokane na kuuza korosho ghafi.

MHE. ZAYNABU M. VULLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda nimshukusru Mwenyezi Mungu kwa kutufikisha hapa leo na pia nawatakia kheri Waislam wote wanaofunga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wake wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kuunga mkono hoja na pia kuipongeza hotuba ya Mheshimiwa Waziri japo nina maoni/mapendekezo yangu kidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Mheshimiwa Waziri, amezungumzia suala kukuza biashara, uuzaji mazao nje ya nchi na pia kuendeleza biashara ya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Pwani una uwezo wa kuzalisha mazao ya matunda mbalimbali ambayo wakati wa msimu huwa mengi mpaka yanaoza. Je, Serikali ina mkakati gani katika kuwakomboa wakulima hao angalau hata kwa kuwaletea viwanda vidogo vidogo chini ya SIDO? Naomba majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nini mkakati wa kuendeleza viwanda mbalimbali ambavyo hapo awali tulikuwa navyo, lakini sasa vingi vyake vimekufa? Viwanda vyetu vinasaidia kununua mali ghafi za hapa nchini na pia hutoa ajira kwa wananchi. Naomba nielezwe, nini mpango wa kuongeza au kurejesha viwanda hivyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipatiwe majibu. Naunga mkono hoja.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda niwapongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu, wadau wote wa Sekta ya Viwanda na Biashara kwa kazi nzuri waliyoifanya ya kuandaa hotuba nzuri yenye mambo mazuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja. Pamoja na hotuba nzuri, lakini bado tuna changamoto nyingi ambazo Serikali inatakiwa ipambane nazo. Kwa upande wangu, nitachangia katika maeneo yafuatayo:-

(a) Maendeleo ya Viwanda;

(b) Maendeleo ya Biashara;

(c) Matatizo ya ukosefu wa masoko; na

(d) Wingi wa wageni wanaofanya biashara katika Jiji la Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ya viwanda ni mazuri sana. Natambua kuwa Serikali imejipanga vizuri katika kufufua hata viwanda ambavyo vilishakufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ni makubwa na hasa katika Jiji la Dar es Salaam. Tatizo ni miundombinu pamoja na juhudi za Serikali katika kuanzisha viwanda vingi ambavyo vitasaidia kuongeza ajira kwa wananchi wetu na kuinua uchumi wetu lakini tatizo ni umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kutoa maeneo ya viwanda Kigamboni, Mbagala, Tuangoma, Bunju, Tegeta na hata maeneo ya kawaida kubadilishwa matumizi kutoka biashara kwenda viwanda vidogo. Lakini pamoja na yote, bado kuna viwanda vikubwa ambavyo tulikuwa tunavitegemea vianze kwa haraka, lakini mpaka sasa bado vinasuasua. Mfano, Dar es Salaam Cement – Mbagala, kuna nini kinachosababisha kiwanda hiki kisimalize ujenzi na kuanza kazi na badala yake watu wanaagiza cement kutoka nje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipatiwe majibu ya kiwanda hiki. Pia kuna mlundikano wa viwanda ambavyo sidhani kama ni rasmi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna Wachina wanajaza machupa ya maji na wanafanya kazi zao usiku. Naomba Wizara iangalie maeneo ya Mbagala Zakhem Industry Area ivikague viwanda hivyo kama vina ukweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama kuna mpango wa kufufua viwanda, basi tuangalie na kiwanda cha UFI Ubungo. Kwa kuwa mpango wa Serikali ni kilimo kwanza kiwanda hiki kitatusaidia katika kuunda zana za kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wilaya ya Ilala eneo la TAZARA kuna viwanda vya Bhakresa. Je, Halmashauri ya Wilaya ya Ilala inafaidika kimapato au ni ajira tu ambao wanapata wananchi? Lakini ajira inatolewa kwa wananchi wote Tanzania, siyo kwa wananchi wa Ilala tu. Pia Wilaya ya Kinondoni kuna Kiwanda cha Urafiki cha zamani ambacho sasa kinamilikiwa na Wachina. Nataka nijue wananchi na Halmashauri wana-benefit vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara inisaidie kujua nini kinaendelea Matshusta Electrical Company, ALAF Tanzania Ltd, National Steel Company, Sub-Scania? Mbona makampuni haya hayaeleweki kwa wananchi? Yapo au yamekufa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima nikubali maendeleo ya kibiashara yapo na ni makubwa sana. Naipongeza Serikali yangu kwa kutoa elimu ya ujasiriamali. Kwa kweli wananchi wanajitahidi kufanya biashara kuanzia zile ndogo ndogo na kati na mpaka zile biashara kubwa. Tatizo ni mitaji, Bank siyo rafiki wa maskini, ni rafiki wa tajiri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wengi wanafanya biashara lakini hawana dhamana za kuweka Bank. Hali hiyo inasababisha wafanyabiashara ndogo ndogo wasikue kutokana na ufinyu wa mitaji. Zile Bank ambazo zinasaidia wananchi hao, zinatoa riba kubwa sana. Naomba Serikali yangu sikivu ya CCM iangalie tatizo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara iwajengee uwezo na kutoa bajeti nzuri kwa maafisa biashara, kwani wanafanya kazi kubwa ya kuhamasisha wananchi wafanye biashara na kutoa elimu ya biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Hotuba ni nzuri, tatizo ni ufinyu wa bajeti.

MHE. MUSSA HASSAN MUSSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote ningependa kuchukua fursa hii adhimu kumpongeza Mheshimiwa Waziri na Mheshimiwa Naibu Waziri kwa umahiri wao mkubwa katika kuendesha Wizara hii muhimu sana kwa letu Taifa hili

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kutambua kwamba ujasiri na uwezo huo umetokana na watendaji wao, hivyo sina budi pia kuwapongeza Watendaji wote kutoka Wakurugenzi hadi Maafisa Waandamizi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika pongezi zangu, nilisema kwamba Wizara hii ni muhimu sana kwa vile inawagusa wananchi walio wengi katika ujumla wa wa kazi wa nchi hii hata kama kuna tabaka ya wafanyabishara wa juu, kati na wa chini (wajasiriamali).

Mheshimiwa Mwenyekiti, miongoni mwa majukumu ya Wizara hii pia ni kuulinda mtaji na pia kuhakikisha kwamba wazawa nao wanafaidi na raslimali ambazo zimo katika nchi yao. Mchango mkubwa katika hotuba hii ni kuiomba Wizara hii kuhakikisha kwamba jitihada zote zinafanyika ili kuwawezesha wafanyabiashara ndogo ndogo kwanza kuwaelimisha na hatimaye kuweza kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, hatua ya mwanzo ni kuelimisha na hatua ya pili ndiyo kuiwezesha na siyo vinginevyo. Kupiga vita bidhaa feki kutoka nje. Hili ni eneo ambalo lina madhara mengi kama uchunguzi unafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa eneo la chakula, inaweza kuathiri afya ya walaji na kuwaletea madhara katika maisha yao. Vifaa vya umeme vinaweza kuleta hasara kubwa kwa kuleta (short) na kuunguza aidha, nyumba au sehemu zao za biashara lakini mwisho wa siku ni kuliingizia hasara Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tukiacha kuzungumzia bidhaa, ni vyema pia mkazingatia suala zima la wafanyabiashara wenyewe. Je, tunahitaji kutoa leseni kwa wafanyabiashara wageni kwa hizi biashara ndogo ndogo? Kufanya hivyo ni kuwavunja moyo wafanyabiashara wazalendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunaelewa kuridhia mkataba wa (free movement of people) na Common Market kabla, ni busara kubwa kufanya tathmini ya ndani kabisa kuona faida na hasara kisha tujipange ili kuona tunapiga hatua na haturudi nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Ahsante.

MHE. MARY P. CHATANDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri, Naibu Waziri na Watendaji wa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kuandaa bajeti ambayo ameiwasilisha kwa umahiri mkubwa ingawaje bajeti iliyotengewa haitoshelezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Tanga unatoa matunda mengi sana yakiwemo machungwa, embe, nanasi na kadhalika, lakini matunda hayo yanakosa kiwanda cha kusindika. Je, Serikali haioni ipo haja ya kuusaidia Mkoa huo, kwa kuwatafutia wawekezaji binafsi ili kuokoa matunda kuoza kwa kukosa soko/kiwanda? Pamoja na mpango mzuri wa Serikali wa kuanzisha soko kuu la Kimataifa la Ununuzi wa Matunda litakalojengwa Segera, lakini bado kuwepo kwa kiwanda cha kusindika kitasaidia ajira kwa wanawake na vijana na makundi hayo yatakuwa yamejiwezesha kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, Serikali ifanye jitihada ya kufufua viwanda vya nguo kama vile MUTEX, URAFIKI na kadhalika, kwani tunayo pamba nyingi ambayo inatosheleza. Hii itasaidia kupunguza kupeleka fedha nje ya nchi na kuinua uchumi wetu sambamba na kuongeza ajira kwa vijana na wanawake.

MHE. ENG. STELLA M. MANYANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, napenda kumpongeza Mheshimiwa Dkt. Cyril Chami na Naibu wake, Mheshimiwa Lazaro Nyarandu kwa jitihada kubwa wanayofanya katika kuona Wizara ya Viwanda na Biashara inafanikiwa katika malengo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nimpongeze Bibiye Joyce Mapunjo - Katibu Mkuu wa Wizara pamoja na Naibu wake kwa kazi nzuri. Aidha, nawapongeza Wakurugenzi wote wa Taasisi zilizopo chini ya Wizara hii kwa kutekeleza majukumu yao vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda na Biashara ndiyo yenye jukumu la kutimiza azma ya Tanzania ya kuifanya kuwa ni nchi yenye viwanda vya kati (semi industrialization) na kufikia uchumi wa kati. Wizara hii ndiyo yenye mashirika mengi ya uwezeshaji (BDS) na hivyo kuwajengea mazingira mazuri ya biashara wananchi wa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini cha kushangaza, bajeti inayotengwa kwa ajili ya Wizara hii ni ndogo sana. FCC wamefikia hata kushindwa kulipia bili zao za umeme na maji, hiyo fair competition tutaipataje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la kusikitisha zaidi, kamati yetu imegundua kuwa Wabunge wengi wanaoifahamu Kamati hii kwa ujumla tu, na hivyo kushindwa kuichangia ipasavyo. Kamati ilishauri Wizara itoe Semina kwa Wabunge wote. Jambo hilo halikufanyika, badala yake maamuzi yakabadilishwa na kuja na semina kwa Kamati tu ambao tayari wanafahamu mengi kuhusu Wizara hii. Kubadilisha maamuzi ya Kamati ni kutokuitendea haki na mwanzo wa kupuuza maagizo ya Kamati. Jambo hilo sikubaliani nalo. Hata hivyo, bado nashauri semina itolewe kwa Wabunge juu ya NDC, EPZA, SIDO na CARMATEC awamu ya kwanza, na kuendelea na mashirika mengine, ili kujitangaza na kuelimisha juu ya kazi za Wizara. Elimisheni juu ya GSI.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kutambua umuhimu was haraka wa kuwekeza katika NDC, kuendeleza maeneo huru ya EPZA, ikiwemo fidia, mitaa ya biashara ya SIDO na kuendeleza teknolojia ya trecta CARMATEC, kwa mwaka huu wa fedha 2011/2012, Serikali itoe kauli juu ya nia yake tuliyoelezwa kwa mdomo juu ya kutoa angalau Shilingi bilioni 50 tu kwa ajili ya kuwezesha hayo mashirika manne.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, kuwe na malengo madhubuti ya kuendeleza mashirika yaliyobaki katika mwaka wa fedha 2011/2012.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TIRDO wakopeshwe ili kutumia viwanja vyake vizuri au waingie ubia na BRELA ili wajenge majengo ya kusaidia Wizara na Taasisi zake. Mapato ya leseni yarejeshwe mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutengwa maeneo maalum ya biashara kwa vijana, na Serikali iwaanzishie Benki kwa ajili ya mitaji na uangalizi wa Serikali.

MHE. DEO H. FILIKUNJOMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana Wizara ya Viwanda na Biashara itoe kipaumbele kwenye uendelezaji wa miradi ya Liganga na Mchuchuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii process ya kumpata huyu mwekezaji toka China, Sichuan Hongda: je, haiwezi kuwa fast tracked kwa manufaa ya Wanaludewa na Watanzania wote?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

MHE. ALIKO N. KIBONA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara kwa bajeti ambayo kwa vyovyote walijiridhisha kabla ya kuileta Bungeni ili ijadiliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maoni yangu na ushauri wangu ni kwamba Wizara na Serikali kwa ujumla, viwanda vyetu vya nyama, nguo na vingine vingi, mkakati wa kuvifufua uanze; Wizara ipewe bajeti (fedha) ya kutosha ili iweze kutekeleza majukumu yake; viwanda vidogo vidogo (SIDO), nchi hii itaendelea kuwa na soko kwa bidhaa za wenzetu nchi za nje zikiwemo bidhaa hafifu (mbovu).

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri kwamba tuanze sasa mawazo ya kuliwezesha Shirika la Kuendeleza Viwanda na lile la Maendeleo ya Taifa. Vijana wetu watapata ufundi wa kuzalisha bidhaa mbalimbali na kukuza ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwira Coal Mine, pale pana wafanyakazi wanalipwa kwa muda mrefu na hawazalishi umeme. NDC, ipewe nafasi ya kuendeleza Mgodi wa Kiwira ili umeme uanze kuzalishwa.

MHE. HUSSEIN MUSSA MZEE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni muhimu kwa Wizara kuweka viwanda vingi vyenye hali ya juu ambavyo vitasaidia kwa upatikanaji wa kazi kwa vijana wetu ambao ni wengi, vitasaidia upatikanaji wa fedha za kigeni ili kukuza uchumi wa Taifa letu, lakini viwanda vitakavyojengwa viwe vile vinavyopata mali ghafi inayotoka nchini mwetu ili kuwapatia soko Watanzania ili kukuza vipato vyao, kuipa mwelekeo mzuri, kauli yetu ya Kilimo Kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ikishirikiana na Serikali Kuu, kushughulikia uingizaji wa vifaa visivyo na kiwango, maana kumekuwa na wimbi kubwa la uingizaji wa vifaa vya electroniki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara kwa kutenga maeneo maalum kwa ajili ya wafanyabiashara wadogo wadogo (Machinga), kwa kuwekea maeneo ya biashara ni moja, lakini wapatiwe pia njia ya kufanya biashara zao kwa utulivu, wapatiwe mikopo ya kukuza biashara hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara iko haja ya kuanzisha viwanda vya matunda ambayo yanapatikana nchini kwetu, viwanda vya nyama na samaki ili kukuza uchumi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umefika wakati kuwajali wasanii wetu ili wapate tija kwenye biashara yao na kupatikana mapato ya Taifa. Kwa hivyo, COSOTA washirikiane na wataalam kufanya udhibiti kwa kuwapatia hati miliki na kuwapatia stika, ili wanufaike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwakilisha.

MHE. GREGORY G. TEU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lini Serikali kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara, sitawekeza kwa kuyaruhusu makampuni yenye uwezo wa kuwekeza katika kutengeneza/kuunda magari mapya (manufacture) hapa nchini kama wanavyofanya wenzetu wa Afrika Kusini na hata India. Maeneo makubwa yenye nafasi ya kutosha kuwawezesha wawekezaji wa aina hii, tunayo. Uwekezaji wa aina hii utasaidia nchi yetu kuongeza “Foreign Reserve.”

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile utengenezaji/uundaji wa magari mapya hapa nchini utasaidia kuondokana na uagizaji wa magari yaliyotumika (used), ili kupunguza hatima ya uchafuzi na uharibifu wa mazingira.

MHE. MOZA A. SAIDY: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mwenyezi Mungu kwa kuniwezesha kufika kwenye Bunge hili Tukufu. Nichangie machache kwenye Wizara hii:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa biashara ni maendeleo, uhai mkubwa, biashara hudumisha uhai, ni biashara, hivyo ni wajibu wa Serikali kuwawezesha wajasiriamali wadogo wadogo kupata ujuzi, taasisi za mikopo na Benki zote zitoe mikopo nai wafanyabiashara wa Tanzania wafanikiwe kwa tija kubwa. Ni wajibu wa Serikali kuweka mazingira mazuri ya wazawa na kuwashindanisha katika biashara husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2010 kiwango cha uzalishaji viwandani kilishuka kutokana na kushuka kwa sekta ya umeme na gesi. Sekta ya umeme na gesi ni muhimu sana katika shughuli za viwanda hasa katika kuchangia ukuaji wa uchumi, kwa sababu mahitaji ya umeme yamekuwa yakiongezeka kwa MW 70 kila mwaka. Kutokana na hali hii ya kupungua kwa ukuaji wa umeme, imedidimiza sana uzalishaji wa viwandani na kupelekea wananchi kukosa ajira/kuachishwa kazi, uzalishaji kupungua, mapato ya Serikali kupungua (makusanyo ya kodi) na kupungua kwa wawekezaji kwenye sekta ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mamlaka ya mapato Tanzania ilinukuliwa ikisema kuwa kuendelea kwa mgao wa umeme tokea mwanzo mwa Januari, 2011 unaweza kukosesha mapato Serikali ya zaidi ya shilingi bilioni 840.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na hayo, mchango wa Serikali ya viwanda katika pato la Taifa bado mdogo sana. Hali hii inatokana na Serikali kutokuwa makini kutumia fursa ya viwanda kama mkombozi wa ajira kwa vijana wasiopungua laki saba ambao humaliza Shule za Sekondari, Vyuo vya Ufundi na Vyuo Vikuu kila mwaka na kukaa bila ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna viwanda vilivyopo Tanzania visivyopungua 12, na tunayo makampuni yanayofanya vizuri katika sekta ya viwanda, navyo ni 11 ambavyo ni Tanga Cement Company Ltd., Mbeya Cement Company Ltd., Tanzania Distillers Company Ltd., 21St Century Textile Mills Ltd., S.S. ALAF, Yol Gases Ltd., Fast African Cable (T) Ltd., Dar Brew (T) Ltd., Nampande Tanzania Ltd., TTC (Tanzania Cigarete Company) Ltd., TBL (Tanzania Brewersies) Ltd.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sambamba na viwanda, biashara nayo ni sehemu muhimu katika kuviendeleza hivyo. Soko la bidhaa ni lazima liwe pana ili kuvi-boost viwanda vizalishe kwa wingi, lakini soko kwenye viwanda bado ni duni sana kutokana na sababu mbalimbali kama ughali wa biashara kutokana na kodi ya Serikali, bidhaa nyingi za Tanzania kutokuwa na ubora unaohitajika kama nchi nyingine za SADC au EAC, wigo wa ushindani katika soko la Kimataifa, kasumba ya Watanzania kupenda zaidi vya nje ya nchi kuliko bidhaa za ndani. Ujuzi wa wafanyakazi viwandani bado ni mdogo, hakuna ubunifu kwenye kutengeneza bidhaa, matokeo yake viwanda vingi bidhaa zake ni za kufanana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nitoe mapendekezo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapinduzi yoyote ya viwanda lazima yaanzie kwenye programu ya viwanda vidogo (SIDO) kwa sababu kwa kupitia SIDO ndiyo tunaweza kujenga msingi imara wa viwanda kuanzia bidhaa. Kwa mwaka huu wa fedha SIDO wanatengewa Shilingi bilioni 1.7 ili kuendeleza Sekta ya Viwanda vidogo vidogo. Kama tutakuwa makini SIDO inaweza kuwa kichocheo kizuri katika mapinduzi ya viwanda tunayokusudia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri mapendekezo yatekelezwe. MHE. RAJAB M. MOHAMMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ubinafsishwaji wa Kiwanda cha nguo cha Urafiki kilichopo Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali yetu kupitia Urafiki na mkopo kutoka Serikali ya China katika mwaka 1966 – 1967 iliweza kujenga kiwanda hiki ikiwa na lengo kuu la kujenga uchumi wa nchi yetu kwa kutumia raslimali ambayo mali ghafi yake (pamba) inazalishwa hapa nchini, na kubwa zaidi ni kuwapatia ajira wananchi wake na kuwapatia soko la uhakika wakulima wetu wa pamba nchini. Kiwanda kiliweza kufanya kazi vizuri na kutoa bidhaa bora katika ukanda mzima wa Afrika Mashariki na hata nje ya Afrika.

Baada ya mtikisiko wa mabadiliko ya kiuchumi duniani, kiwanda hiki kilibinafsishwa na Serikali yetu kuingia ubia na Wachina ambapo Serikali ilichukua asilimia 49 ya share na China ilimiliki asilimia 51.

Mwaka 1995 – 1996 ukarabati mkubwa ulifanyika katika kiwanda hiki na uzalishaji uliongezeka, pamoja na wabia hao ambapo Serikali ilipatiwa mkopo mwingine na Serikali ya China wa dola za kimarekani milioni 27 kwa ajili ya ununuzi wa mitambo mipya na ya kisasa. Kwa bahati mbaya mitambo iliyoagizwa na kufungwa haikuwa na ubora uliohitajika na ilikwishatumika (mikuukuu). Kutokana na ubadhirifu huo, kiwanda kilisuasua kiuzalishaji na kuanza kupunguza wafanyakazi na kutoa taarifa ya upatikanaji hasara katika uzalishaji.

Kutokana na hali hiyo, migogoro baina ya wabia na wafanyakazi ilijitokeza hadi kuilazimisha Mahakama kuamrisha Mwajiri kuwalipa wafanyakazi stahili zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mbali na hayo, wadau hawa waling’oa mitambo (Mill No.II) na kuuzwa kama ni vyuma vichakavu ambapo haieleweki ni kiasi gani mashine hizi ziliuzwa.

Vilevile kutokana na ubia huo, Menejimenti nzima ambayo inaongozwa na wabia hao, haionyeshi dhamira ya dhati ya kukiendeleza kiwanda hicho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na hali hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri wakati atakapokuja kufanya majumuisho ya bajeti yake, anipatie ufafanuzi ufuatao:-

(a) Mkopo wa dola za kimarekani milioni 27 ulitumikaje? Je, ni kiasi gani kimeshalipwa kwa Serikali ya China?

(b) Je, ni lini kiwanda hiki kimefanyiwa ukaguzi wa kimahesabu?

(c) Ni nini matumaini ya Serikali kwa manufaa ya wananchi juu ya kiwanda hiki?

MHE. MARGARET S. SITTA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni soko kubwa sana la India kutokana na nguo nyingi sana za aina ya ‘dira’ zinazoingizwa nchini na kuvaliwa sana na wanawake wa Tanzania na mimi mwenyewe nikiwemo. Kitambaa kinachotumika ni hafifu kwa kuwa ni chepesi sana: Je, Serikali haiwezi kuhamasisha wenye viwanda vya nguo nchini kutengeneza aina hiyo ya nguo hapa nchini na kuzifanya imara zaidi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la ngozi ni muhimu sana na taarifa nilizonazo, tulianza sisi nchini kutengeneza bidhaa za ngozi kabla ya Ethiopia. Je, ni kweli Ethiopia wanatengeneza bidhaa nyingi zaidi ya Tanzania na kama ni kweli, kwanini, ambapo tulianza na tuna ngozi nyingi?

MHE. DEOGRATIAS A. NTUKAMAZINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni muhimu sana kwa sababu ikiwa na viwanda mama (basic industries) tutaongeza thamani ya bidhaa zetu. Tutauza Finished goods. Turudishe kiwanda cha kuzalisha zana za kilimo ili tuboreshe kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya chuma ni muhimu sana. Nickel itakayozalishwa na mgodi wa Kabanga itasaidia kupata chuma cha pua (iron steel). Miradi ya Mchuchuma na Liganga ni muhimu sana, Wizara iiwezeshe NDC tupate creadible wawekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara iiwezeshe TBS iweze kuweka viwango vya uzalishaji, na hasa ilinde afya ya walaji. Sasa hivi tuna vyakula ambavyo ni Substance au contaminated, hivyo hivyo juices, dawa ya mbu, dawa ya meno. Nondo zinazozalishwa Kariakoo ni dhaifu sana, siyo kama zile zilizokuwa zinazalishwa kwenye kiwanda cha Tanga Steel Rolling Mills.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TIRDO na Tume ya Ushindani ziwezeshwe ili pamoja na TBS ziwalinde walaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara iwe makini katika biashara ya bilateral, kuna biashara ya AGOA; tukiwa na viwanda vyetu vya nguo, ngozi tunaweza tukaitumia fursa ya AGOA tukauza zaidi Marekani. Tuwe proactive na biashara ya kanda – EAC, SADC na COMESA. Hili ni soko kubwa sana tukichangamkia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Multilateral Trade with European Countries ni soko zuri. Mheshimiwa Mwenyekiti, tukatae nchi yetu isiwe dumping place ya bidhaa hafifu kutoka nchi za Far East. Nondo zinazotoka nchi hizo ni hafifu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, BRELA ifanye kazi yake vizuri, wachuuzi wa Kichina, Wakorea walioko Kariakoo na sehemu nyingine wanaofanya biashara ndogo ndogo ambazo zingefanywa na Watanzania wamepewa leseni na nani? Siyo BRELA?

Mheshimiwa Mwenyekiti, turudishe Tume ya Bei. Nchi ambayo inawathamini wananchi wake na ni masikini haiwezi kuacha kazi yake ya kuwalinda walaji wake dhidi ya wafanyabiashara ambao hawana Ethics. Haiwezi ku-abdicate responsibility yake ya macro-economic management market forces siyo perfect. Hatujafika stage ya development ya kuachia the invisible hand ya Adam Smith bila regulation yoyote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuache mtindo wa kutowaamini mameneja wetu wazalendo. Tuwajenge, tuwahamasishe, tuwawezeshe kwa kuwawakea mazingira mazuri ya kazi ikiwa ni pamoja na maslahi mazuri, wataweza. Tujifunze kutokana na mameneja feki wa – NETGROUP SOLUTION kutoka South Africa to manage TANESCO, Management ya RITES kutoka India ku- manage reli yetu, mameneja wetu wapewe management training kwenye vyuo vyetu ikiwa ni pamoja na Uongozi Institute.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Ngara inahitaji msaada wa Wizara hii. Per capital income ya wananchi wa Ngara ni Sh. 170,000/=, Sh. 240,000/= wakati wastani wa kipato Kitaifa ni Sh .700,000/= kwa mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, SIDO itawasaidia sana vijana wetu wanaotaka kujiajiri kwa kuanzisha viwanda vidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iruhusu biashara ya mpakani – cross boarder trade. Ngara inapakana na nchi za Rwanda na Burundi zenye watu wapatao milioni 19. Hili ni soko kubwa sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri/Naibu Waziri na Mkurugenzi wa EPZ mwone jinsi Ngara ilivyo well situated kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mgodi wa Kabanga Nickel ni muhimu sana kwa uchumi wetu. Nickel inatoa chuma cha pua (Iron Steel). Serikali ita-support kwa mgodi huu kuwapatia umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba reli ya Isaka – Keza – Burundi – Rwanda ijengwe, itasaidia kubeba mizigo ya Nickel kuleta Dar es Salaam ili ipelekwe Canada kwa ajili ya kuyeyusha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, soko la Kimataifa kuwepo Ngara.

MHE. PEREIRA AME SILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kwa kukushukuru kwa kunipa nafasi ya kuchangia kwenye hoja hii ya Wizara ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niIshukuru sana Wizara kwa hotuba nzuri na inayotoa matumaini. Pamoja na pongezi hizo, naomba nichangie katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ya viwanda. Maendeleo ya nchi nyingi husaidiwa sana na kuwepo kwa viwanda. Faida kubwa ni kusarifu mazao ya ndani na hivyo kusaidia sekta kama ya kilimo (misitu, mifugo, uvuvi na kadhalika). Aidha, viwanda ni muhimu katika kuwapatia wananchi hasa vijana ajira za kuendeleza maisha yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya viwanda vyetu na uendeshaji havijatusaidia sana kimaendeleo kwa vile bado bidhaa zetu zinaendelea kuuzwa nje zikiwa ghafi na hivyo kuhamisha ajira pia. Wakati umefika kwa Wizara kuweka kipaumbele katika kuchakata mazao kabla ya kuuza nje na hata ndani ili tuweze kupata faida za ziada za uzalishaji wa misingi. Kwa sasa na hususan baada ya kuzindua Kilimo Kwanza usarifu wa mazao ya kilimo ni lazima vinginevyo ongezeko la uzalishaji wa mazao litashindwa kupata soko na hivyo kuwavunja moyo wakulima na kuacha kuongeza uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ubora wa bidhaa sokoni. Soko la Tanzania hivi sasa limevamiwa na bidhaa hafifu na ambazo hazina ubora. Hii ni changamoto kubwa kwa uendelezaji wa viwanda, afya za watumiaji na mazingira. Bei ndogo za bidhaa hizi ikijumuisha na uwezo mdogo wa wananchi wa kununua, hufanya soko la bidhaa hizi kuwa kubwa na kuhamasisha waingizaji wa bidhaa hizi. Wizara haina budi kulitambua tatizo hili pamoja na madhara yake na kuchukua hatua za kufaa. Bidhaa hafifu pamoja na urahisi wake zinawatia hasara wananchi na hivyo kuifanya kazi ya kuondoa umaskini kuwa ngumu zaidi. Hatua za dhati zichukuliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ndani ya EAC. Jumuiya ya Afrika Mashariki imeingia mikataba mingi ya utengamano ikiwemo Itifaki ya Umoja wa Forodha na Soko la Pamoja. Aidha, hivi sasa majadiliano ya Umoja wa Sarafu yanaendelea. Pamoja na hatua kubwa Jumuiya hii iliyozifikia, inasikitisha sana kuona utekelezaji wa Instruments za awali zinatekelezwa kwa kusuasua sana. Kwa mfano utekelezaji wa Umoja wa Forodha unakwamishwa na wingi wa NTB na ni wazi kwamba bado faida za hatua za utengamano hazijaleta tija halisi. Mara nyingi imeonekana kuwa bidhaa za Tanzania ndio zinapata vikwazo pengine kuliko bidhaa za nchi nyingine hasa Kenya. Nashauri jambo hili lizungumzwe kwa lengo la kulimaliza vinginevyo hakutakuwa na haja ya kuendelea kwa majadiliano ya hatua nyingine za utengamano wakati makubaliano ya awali hayatekelezwi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, urasimishaji wa sekta isiyo rasmi. Tanzania ni moja kati ya nchi yenye sekta isiyo rasmi kubwa sana na hata ukusanyaji wa mapato huathiriwa kwa kiasi kikubwa. Nashauri Wizara ya Viwanda na Biashara na wadau wengine ikiwemo Wizara ya Fedha na Wizara ya Uwekezaji zijipange kwa pamoja ili kwa upande mmoja, kuboresha ujasiriamali na kwa upande wa pili kurasimisha biashara zao ili wachangie kwa kulipa kodi stahiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. AUGUSTINO M. MASELE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja ya Waziri. Hata hivyo, nitoe ushauri kwamba juhudi zaidi ziwekwe katika kujenga mazingira ya ushirikiano maalum kabisa na Wizara zingine ikiwemo Wizara ya Fedha, Uchukuzi na Ujenzi pamoja na Nishati na Madini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Viwanda na Biashara ni injini ya ukuaji wa uchumi wa nchi yetu. Itakumbukwa kuwa nchi karibu zote zilizoendelea duniani zimezingatia na zitaendelea kuitegemea Sekta ya Viwanda na Biashara. Kuanzia Mapinduzi ya Viwanda nchini Uingereza na nchi za Ulaya iliyokuwa katika Karne ya Kumi na Tisa hali hiyo haitakuwa tofauti na hapa kwetu kwa sekta hii. Nchi yetu imejaliwa kuwa na rasilimali zote ambazo zimeyafanya Mataifa yaliyoendelea kufikia hatua yalipo sasa. Tanzania ina Bandari nzuri, ina ardhi yenye rutuba yenye kuweza kuzalisha mazao ya biashara na chakula, nishati na madini hasa makaa ya mawe, dhahabu, urani, Tanzanite na mito yenye maporomoko yenye kuweza kuzalisha umeme wa kutosha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kufuatia kupitishwa kwa Sheria ya Public and Private Partnership, niiombe Wizara itilie maanani uwezeshwaji wa wazawa wa nchi hii utakaowawezesha Watanzania waweze kushirikishwa katika kumiliki rasilimali za nchi hii kwa kushirikiana na wageni. Kwa upande wa Wizara ya Viwanda na Biashara kuchukua nafasi ya kumiliki viwanda mbalimbali nchini badala ya kuachia wageni tu ndio wawe wamiliki wa viwanda na kupewa misaada ya kifedha kupitia taasisi za umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaimani kubwa kuwa kwa sasa nchi yetu imefikia hatua nzuri ya kuwa na wasomi kutoka Vyuo Vikuu mbambali vya hapa nchini na nje ya nchi, tofauti na hapo awali nchi yetu ilipopata Uhuru wake na matokeo yake viwanda vingi vilianzishwa na vingi vilikufa, kwa sasa hali ni bora zaidi. Sasa ni wakati kwa Wizara kuchukua nafasi yake katika usimamizi wa shughuli za uendeshaji wa Bandari ya Dar es Salaam pamoja na miundombinu ya uchukuzi kwa ufanisi wa shughuli za Viwanda na Biashara pamoja na Mashirika ya Bima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la ushirikishwaji wa wafanyabiashara wa ndani na nje ya nchi yetu ili kuboresha na kukuza uchumi wa nchi kiwe kipaumbele nambari wani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuendelea na mpango wa uhamasishaji wa wawekezaji na kutoa kipaumbele kwa viwanda vinavyoongeza thamani ya mazao ya kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuliwezesha Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) ambalo limekusudia kutekeleza Miradi ya Makaa ya Mawe ya Mchuchuma na Ngaka na chuma cha Liganga. Miradi hii mikubwa ni chachu ya maendeleo ya uzalishaji wa viwanda vikubwa na vidogo kutokana na upatikanaji wa nishati ya umeme wa uhakika kutokana na makaa ya mawe, upatikanaji wa mali ghafi ya chuma ambayo ni bidhaa inayoweza kuuzwa hata nchi za nje na kuliingizia Taifa pato na kukuza uchumi. Katika hili Serikali ichukue maamuzi magumu ya kuipa fedha zaidi NDC ili iweze kuwa na nguvu ya kimaamuzi na utekelezaji pindi Shirika hili litakapoingia ubia na mwekezaji kutoka nchini Uchina.

MHE. HAJI KHATIB KAI: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehma kwa kuniwezesha kuamka salama siku ya leo na nikiwa na afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nichangie kwa maandishi kwenye hotuba ya bajeti ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda niungane na hotuba ya Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani kwa kutoa masikitiko makubwa wakati tunajiandaa kutimiza miaka 50 ya Uhuru wa nchi yetu, Sekta ya Viwanda na Biashara imeathirika sana kutokana na kukosekana kwa nishati ya umeme wa uhakika nchini mwetu na kusababisha viwanda vingi kufungwa na kukosekana kwa ajira nchini jambo ambalo linarudisha nyuma Taifa letu. Wizara ya Viwanda na Biashara ni Wizara moja muhimu sana katika nchi yoyote ile kwani ndio inayosimamia maendeleo ya uchumi wa nchi, ikiwa ni pamoja na Viwanda na Biashara. Viwanda na Biashara ni uti wa mgongo wa nchi yetu kwani pia ndio inayosimamia uwekezaji na kulipatia tija Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la kusikitisha ndani ya nchi hii kuna urasimu na Serikali imekuwa ikinyamaza kimya sijui kwa nini. Kwa nini nasema hivyo? Nasema hivyo kwa sababu kwenye hotuba ya Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda na Biashara amesema kuhusu taarifa za urasimu ilizozipata juu ya uanzishwaji wa mradi wa umeme uliopo Mkoani Singida. Kamati imekusudia kumwita Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO ili atoe sababu za msingi kwa nini hadi leo hajasaini Mkataba wa mradi huu. Hivi suala kama hili mtu mmoja analifanya na Serikali inanyamaza, je, ni kweli Serikali ina juhudi za makusudi za kuondoa tatizo la umeme na kuviwezesha viwanda kufanya kazi na kusababisha ajira kwa vijana walio wengi ambao hawana kazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho wa mwaka wa fedha 2010/2011, Wizara iliidhinishiwa na Bunge kiasi cha shilingi bilioni 64,260,500. Kati ya fedha hizo shilingi bilioni 31,542,839,000 ni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na shilingi bilioni 32,717,666,500 ni kwa ajili ya matumizi ya maendeleo. Ni jambo la kushangaza sana kwamba bajeti iliyopita ya mwaka wa fedha 2010/2011, imekuwa kubwa kuliko bajeti ya Wizara hii ya mwaka wa fedha 2011/2012, kulikoni? Bajeti ambayo imepungua hadi kufikia shilingi bilioni 27,676,129,000/=, kwa hali hii Serikali haionyeshi nia ya dhati kuiwezesha Wizara hii ya Viwanda na Biashara kufanya kazi zake kwa ufanisi pamoja na kuongeza mapato kwa Taifa hili. Mwisho naomba ufafanuzi kwa hili.

MHE. KHATIB SAID HAJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii na mimi kuwa mmoja wa wachangiaji katika bajeti ya Wizara hii ya Viwanda na Biashara. Ni Wizara muhimu sana katika maendeleo ya Taifa letu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda katika nchi yoyote ndio nguzo na mhimili muhimu sana kwa maendeleo ya Taifa. Hivyo ni wajibu wetu kama Taifa kuweka mkazo maalum katika sekta ya viwanda. Kutokana na mwonekano ulio wazi ni kwamba maendeleo ya viwanda katika Taifa letu bado tuko chini sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja katika matatizo makubwa yanayoikabili Sekta ya Viwanda ni ukosefu wa umeme wa uhakika katika nchi yetu. Jambo hili si tu kwamba linawavunja moyo wawekezaji wa nje wenye nia ya kuja kuwekeza katika viwanda bali pia linasababisha viwanda vichache vilivyopo vizalishe chini ya kiwango na hata kupelekea viwanda vingi kufungwa kabisa. Suala hili ni zito na sisi kama Taifa hatuna budi kulipa uzito stahiki ili tuweze kupiga hatua mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutoa mapendekezo mawili muhimu ya kutatua tatizo hili sugu la umeme linalotukabili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa Mchuchuma na Liganga. Mradi huu ni jibu lililo wazi katika tatizo hili la umeme. Shirika la NDC litakapowezeshwa ni uhakika kwamba kwa kiasi kikubwa tatizo hili litapungua kwa kiasi kikubwa na kama sio kumalizika kabisa. Hivyo ni jukumu la Serikali kulipa uwezo wa kutosha Shirika hili ili liweze kuendeleza mradi huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mradi wa umeme wa upepo Singida. Mradi wa umeme wa kutumia upepo wa Singida ni chanzo kingine muhimu cha umeme wa uhakika. Kwa mujibu wa tafiti za kitaalamu zinaonyesha unafuu mkubwa wa umeme huo pindi utakapokamilika. Hivyo, ni jukumu la Serikali kama vile inavyoonekana dhamira ya kweli kwenye maandishi basi ikamilishe kwa vitendo miradi hii na kuwezesha Sekta ya Viwanda iweze kuimarika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kueleza hofu na mashaka yangu juu ya utendaji wa TBS. Taasisi hii ndio yenye Mamlaka ya Ukaguzi wa Bidhaa zote ziingiazo na zitengenezwazo ndani ya nchi yetu. La kusikitisha ni kuongezeka kwa bidhaa zisizo na viwango, mbovu na zisizostahiki kuingizwa katika soko la nchi yetu. Mfano mdogo tu hivi sasa katika Mji wa Dodoma kuna wingi wa Bulb kutoka China ambazo ni mbovu ambazo hazifai kwani ukinunua hata bulb 10 huwezi kupata hata mbili (2) zitakazotumika kwa usiku mmoja tu. Hivyo, ni wajibu wa Taasisi hiyo kufuatilia kwa makini zaidi uingiaji wa bidhaa hapa nchini.

MHE. AMOS G. MAKALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie hoja ya Wizara ya Viwanda na Biashara katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kujenga Kiwanda cha mbadala cha Sukari Mtibwa. Kutokana na matatizo yaliopo sasa kwa wakulima wa miwa na wafanyakazi wa Kiwanda cha Mtibwa kuhusiana na bei ndogo ya miwa, ucheleweshaji wa malipo kwa wakulima, ucheleweshaji wa mishahara na malipo kwa wastaafu waliokuwa wafanyakazi wa Kiwanda cha Mtibwa, ni dhahiri matatizo haya yanasababishwa na uwepo wa kiwanda kimoja kinachotumia Sheria ya kutoruhusu kiwanda mbadala ndani ya km 80. Mheshimiwa Waziri atoe tamko, hii sheria ni kandamizi kwa wakulima, hairuhusu ushindani. Katika kitabu cha hotuba inaonyesha Serikali haijauza nje sukari kutokana na uzalishaji mdogo kuliko mahitaji. Naomba Serikali itafakari upya Sheria hii kwani haitoi ushindani wa kibiashara zaidi inakandamiza wakulima, Sheria hii haifai kuendelea kuwepo kwa sababu zifuatazo:-

1. Haitoi ushindani, mnunuzi ndiye anayepanga bei na mkulima hana soko mbadala, badala yake wakulima wanaendelea kuuza miwa kwa bei ndogo tofauti na viwanda vingine kama Kilombero.

2. Sheria hii ilitungwa wakati wa uchumi hodhi kulinda viwanda vya Serikali hivyo katika soko huru haitoi ushindani.

3. Kuongezeka kwa mahitaji ya sukari katika uzalishaji. Takwimu zinaonyesha uzalishaji wa sukari umepungua, mahitaji ni makubwa kuliko uzalishaji, hii imethibitishwa na kupanda bei ya sukari, hotuba ya hali ya uchumi na hotuba ya Waziri imeonyesha ukurasa wa 58 kuwa uhaba wa sukari ulipelekea Serikali kutoa vibali vya waagizaji sukari kuagiza nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo, kwa maelezo haya, naomba Serikali itoe tamko kuhusu hoja ya kuruhusu wawekezaji wengine kujenga kiwanda mbadala katika Tarafa ya Turiani. Bila kutolea ufafanuzi suala hili sitaunga mkono hoja hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.

MHE. DKT. MARY M. NAGU: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru na kuwapongeza Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu pamoja na Watendaji wote wa Wizara ya Viwanda na Biashara, kwa kazi nzuri wanazofanya na kuendeleza yale yote tuliyoaanzisha wakati nilipokuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara itembelee Wilaya yangu ili kuona rasilimali ya Maziwa yaliyo na chumvi na magadi ili kuona uwezekano wa kuanzisha Kiwanda cha Kemikali kama Nitrate inayotumika kwa wingi katika machimbo ya madini. Nitawashukuru sana kama rasilimali hii ikibadilishwa kuwa fursa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Hanang ni Wilaya ya Kilimo na Mifugo. Nitakuwa tayari kushirikiana na Waziri na Naibu Waziri kuona viwanda vya kuongeza thamani kwa mazao ya kilimo na mifugo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuna Ziwa Bosotu lenye samaki wengi. Ziwa hili likipata Mwekezaji mmoja wa kusindika samaki itakuwa imewapatia vijana wavuvi ajira ya kuvua samaki lakini wakati huohuo kuongeza thamani ya samaki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawatakia mafanikio mema katika kupitisha bajeti ya Wizara ili maombi yangu nayo yapate kutekelezwa.

MHE. SULEIMAN NASSIB OMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Kiwanda cha Sukari Mtibwa. Nilipata nafasi ya kutembelea eneo hili kwa matembezi binafsi. Wafanyakazi wa Kiwanda na wananchi wanakilalamikia sana kiwanda hiki. Baadhi ya malalamiko yao ni bei ndogo za miwa ukilinganisha na bei za viwanda vingine, malipo yanacheleweshwa kwa zaidi ya miezi minne (4) toka miwa inapouzwa kiwandani, malipo madogo ya mishahara, stahiki za wastaafu hadi leo hazijalipwa na migogoro baina ya kiwanda na wanavijiji wanaoishi karibu ya kiwanda. Hili ni tatizo kubwa sana. Serikali bado haijatoa kipaumbele katika kutatua mgogoro huu. Tumekalia bomu. Kama hatua za haraka hazikuchuliwa kutatua matatizo yaliyotajwa hapo juu yanaweza kutokea maafa makubwa. Naomba Waziri wa Biashara na Viwanda achukue hatua za haraka kutatua migogoro hiyo. Zaidi ya hivyo, wakulima wengi wameanza kuacha kulima zao la miwa na wameanza kupanda mazao mengine, kutokana na mgogoro huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la sukari. Hivi sasa kunaonesha kuna tatizo la sukari. Katika mwezi huu wa Ramadhan, matumizi ya sukari ni makubwa. Hivyo ingekuwa vizuri Waziri akaeleza kuhusu uzalishaji wa sukari. Pia hakutaja uzalishaji wa hivi sasa wa sukari katika viwanda vilivyopo nchini na kama uzalishaji huo unatosheleza mahitaji ya sukari nchini. Namwomba Waziri atoe maelezo katika majumuisho yake.

MHE. ABUU H. JUMAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu, mwingi wa rehema, kwa kuniwezesha kupata fursa hii kuweza kuchangia bajeti ya Wizara ya Viwanda, Biashara na Masoko ya mwaka 2011/2012.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Pia napenda kuishukuru Serikali ya Chama cha Mapinduzi kwa sera zake nzuri za kuhakikisha Sekta za Viwanda, Biashara na Masoko inatoa mchango mkubwa katika kuandaa uchumi wa nchi yetu kuweza kuhimili katika mfumo wa ushindani katika masoko ya kitaifa, kikanda na kimataifa katika mfumo wa sasa wa utandawazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, mazingira mazuri watakayojengewa wananchi katika Sekta hii yatakuwa kichocheo cha wananchi kuongeza bidii katika shughuli za uzalishaji ambazo ni ukulima, ufugaji, uvuvi na biashara. Ongezeko la uchumi wa Taifa litaweka mazingira mazuri ya uwekezaji, kuongeza ajira na kuongeza uwezo wa kubadili mali ghafi (raw materials) zetu kuwa na thamani zaidi (finished goods) kwa faida zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuipongeza Serikali kwa kutambua kwamba uwezo wa wananchi wa kuwa na viwanda vikubwa si rahisi kutokana na uwezo mdogo wa mitaji na rasilimali zinazohitajika kuwekeza katika sekta hii. Juhudi kubwa na mikakati inayofanywa ya kuendeleza wajasiriamali, viwanda vidogovidogo mijini na vijijini na biashara ndogo imewanufaisha wananchi kwa kuongeza ujuzi na kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada kubwa ya Serikali ya kuendeleza Sekta ya Viwanda na Biashara na Masoko, bado kuna matatizo mengi ambayo yanaikabili sekta hii ambayo mengi yako nje ya uwezo wetu kama kuporomoka kwa thamani ya pesa yetu katika soko la dunia, gharama kubwa ya mali ghafi na vipuri toka nje, kupanda kwa bei za mafuta na bidhaa za petroli, nishati, umeme usio na uhakika na miundombinu duni ya kusafirisha mazao na malighafi kutoka vijijini, hii ni pamoja na kusuasua kwa usafirishaji wa reli. Changamoto zote hizo zinafanya bidhaa zetu kuwa na bei kubwa hivyo kuumiza sana wananchi. Nashauri Serikali iweke mikakati ya kushirikisha wadau wote kutafuta mbinu za kuwezesha kutatua matatizo hayo ya msingi ili viwanda vyetu viweze kuzalisha na wananchi wapate unafuu wa bei.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uwezo mdogo wa uzalishaji katika viwanda vyetu, wafanyabiashara wamechukua mwanya huo kuweza kuingiza bidhaa duni ambazo zinaongeza kumuumiza mwananchi. Uwezo mdogo wa kipato unamlazimisha mwananchi atafute bidhaa zenye unafuu wa bei bila kufikiria madhara yake. Kwa unyonge huu, wananchi wengi wameunguliwa nyumba zao, magari na vifaa vya nyumbani kama Majokofu na Luninga. Nashukuru Serikali kuweka ukaguzi wa viwango vya bidhaa zinazoingizwa hapa nchini lakini kuna haja ya kufanya utafiti na kufahamu mianya na njia nyingi za panya zinazotumika kuingiza bidhaa hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni jambo linalofahamika kwamba uwekezaji katika sekta hii ya viwanda unafungua mianya ya kuongeza uchumi wa nchi kwa maana rasilimali za ndani ikiwa ni mali ghafi za hapa nchini zinatumika kwa hiyo wananchi ambao wengi ni wakulima na wafugaji wanapata pesa za mazao yao na idadi ya wananchi/vijana wanaoajiriwa katika sekta hii huongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna viwanda vingi vya Serikali ambavyo vilibinafsishwa na kupewa wawekezaji ambao Serikali ilifikiri wangeweza kuviendeleza badala yake kuna wawekezaji ambao wamebadili mfumo wa uzalishaji au wamefunga viwanda vile bila kufanya chochote. Mfano mzuri ni Kiwanda cha Tanganyika Packers kilichopo Kawe Mjini Dar es Salaam. Kiwanda hiki kilikuwa na soko la kununua mifugo kutoka kwa wananchi na kusindika nyama. Nyama hii iliweza kuuzwa nje ya nchi na kupata fedha za kigeni. Kiwanda hiki pia kilikuwa kimetoa ajira kwa wananchi ambao walikuwa na kipato cha kuaminika hivyo kilipunguza umaskini kwa wananchi kwa kiasi kikubwa. Serikali iangalie namna ya kurudisha viwanda hivi na kuwapa wawekezaji wenye uwezo na moyo wa kuendeleza nchi hii ili viendelee kuzalisha na kuongeza pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ina wataalamu wengi ambao kama Serikali kwa makusudi kabisa ikawawezesha na kuwapa ushirikiano, wanaweza kutumia ujuzi wao na uzoefu wao kuanzisha viwanda na kuacha dhana ya kutegemea bidhaa za kutoka nje kama vipuri, nguo, zana za kilimo, madawa ya wanyama, mazao na binadamu na bidhaa nyingi nyingine kwa matumizi ya kawaida ya wananchi. Bidhaa nyingi zinauzwa nje, zinazotengenezwa na viwanda vya hapa nchini ni zile zinazotegemea sanaa za mikono, viungo, madini na mali ghafi. Uwiano wa pesa tunazopata kwa kuuza bidhaa katika soko la nje ni kidogo sana ukilinganisha na bidhaa tunazonunua. Hii inaonyesha kwamba hatujajizatiti na kujipanga vizuri katika ushindani wa biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maeneo huru ya uzalishaji wa bidhaa za kuuza nje (Export Processing Zone – EPZ) ni mkakati mzuri uliowekwa kupata wawekezaji watakaojikita katika kuzalisha bidhaa za kuuza nchi za nje. Serikali iwe makini katika kuhakikisha wananchi wanashirikishwa kikamilifu katika mpango huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iweke mikakati ya kuwapa wananchi nyenzo katika Sekta ya Madini, Ardhi na dhamana za leseni za biashara na kushawishi wawekezaji waungane na wafanyabiashara wa ndani. Sheria pia iwatake wawekezaji watoe ajira kwa wananchi na asilimia kubwa ya wafanyakazi katika viwanda hivyo wawe ni wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Jimbo la Kibaha Vijijini hatuna viwanda vingi, kwa hali hiyo ajira kwa vijana wetu ni ndoto. Kiwanda kilichopo ni Ranchi ya Ruvu nayo haina uwezo wa kuajiri vijana wengi. Uchumi wa wananchi wa Jimbo hili unategemea kilimo cha mboga na matunda ya aina mbalimbali, ufugaji na uvuvi. Jimbo lina ardhi ambayo inaweza kutumiwa na wawekezaji ambao wana uwezo wa kujenga viwanda vya kusindika mazao haya ili kuongeza thamani ya bei ya mazao haya na kukuza pato la wananchi. Baada ya kuelezea hali halisi ya uchumi wa Jimbo la Kibaha Vijijini, natumaini katika bajeti hii, Serikali itaweka mipango ya kutekeleza ahadi ya Mheshimiwa Rais aliyoitoa wakati wa kampeni kubwa alipotembelea katika Jimbo la Kibaha Vijijini. Ahadi hiyo alitoa kwamba Serikali itajenga Kiwanda cha Kusindika Nyanya zinazolimwa katika Jimbo lile na Majimbo ya jirani katika Kata ya Ruvu. Kiwanda hiki kitaongeza thamani na bei ya zao la nyanya kwani baada ya kusindikwa zinaweza kupata soko la ndani na nje ya nchi na kuondoa umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na ahadi hiyo, wananchi wa Jimbo la Kibaha Vijijini wanaiomba Serikali ijenge Chuo cha Ufundi katika Kata ya Kwala au Magindu ili kuweka mazingira yatakayowezesha kuwa na fani za kuanzisha viwanda vidogovidogo vitakavyotumia rasililimali zilizopo. Naomba katika mipango ya Serikali ya kutoa elimu ya ujasiriamali, ratiba ijumuishe wananchi wa Jimbo la Kibaha Vijijini ili nao waweze kufanikiwa kupata mafunzo ya ufundi, mbinu za ushindani katika biashara na mawasiliano ili kupata uwezo wa kushiriki kikamilifu katika sekta hii na kuharakisha maendeleo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, soko la mazao yanayolimwa katika Jimbo la Kibaha Vijijini pia ni tatizo. Wananchi wa Jimbo la Kibaha Vijijini wanayo ari sana ya kufanya shughuli za kuwapa tija na kuwakwamua katika umaskini. Wananchi hawa wamejitahidi kufanya shughuli za ujasiriamali kwa uwezo walio nao na hasa wanawake na vijana ambao wanajitahidi kutumia ujuzi wa asili kutengeneza bidhaa za mikono, kulima mazao ya mbogamboga, matunda na samaki wanaopatikana Mto Ruvu. Soko lao kwa uzoefu wanapanga bidhaa zao kando ya barabara kuu ili kuwauzia abiria wanaosafiri kwa kutumia barabara hiyo. Mfumo huu wa biashara ni wa kienyeji mno, naomba Serikali kwa huruma ya kusaidia wananchi wale ambao uwezo wao ni mdogo kuboresha na kujenga Soko la Mlandizi ili mazao haya yaweze kukusanywa kwa urahisi kuwavutia wafanyabiashara kufika na kununua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa uvuvi, naipongezea sana Serikali kwa kuwa makini katika kuzuia ujangili unaofanyika wa uvuvi haramu katika Maziwa, Mito na Bahari ambao zilikuwa zinaathiri sana upatikanaji wa mazao ya uvuvi. Pamoja na kwamba samaki wanapatikana katika nchi yetu lakini wana bei kubwa kiasi kwamba si wananchi wengi wanaweza kununua na kula samaki labda walioko katika maeneo ya uvuvi. Hii inachangiwa na kutokuwepo na uwezo wa wavuvi wetu kununua zana za kisasa za kuvua pamoja na njia za kuhifadhia samaki kwa muda mrefu. Nashauri Serikali ingechukua hatua za kuona kwamba samaki ni chakula bora na hawana madhara kwa afya hivyo kama Sekta ya Uvuvi ikiimarishwa kwa kuwezesha wavuvi kupata elimu ya kuvua, mitaji ya kununulia vifaa bora vya kuvua na kuhifadhi samaki, samaki watapatikana kwa wingi na wataweza kuuzwa katika soko la nje na la ndani na kwa wingi wa upatikanaji wa samaki hawa, wananchi wataweza kununua kwa bei nafuu. Kwa kuwa samaki ni lishe bora, ulaji wake kwa wingi utasaida kuboresha afya za wananchi kuwa katika hali nzuri na matumizi ya taasisi za afya yatapungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema awali, Jimbo la Kibaha Vijijini lina mifugo mingi na pia kuna samaki wengi wa aina ya Kambale wanaopatikana katika Mto Ruvu. Serikali inaweza kuwasaidia wananchi wa Jimbo hili hasa wale walio kandokando ya Mto Ruvu, kuwajengea Chuo au Taasisi ya Utafiti wa Kutotoa Vifaranga vya Samaki aina ya Kambale na kuwafundisha wananchi jinsi ya kufuga samaki kwa kuwaelekeza kuchimba/kujenga mabwawa ya kufugia samaki. Kwa kuwa uwezo wa wananchi wa Jimbo la Kibaha Vijijini ni mdogo, Serikali ingeweza kuunga mkono juhudi za wananchi wale kwa kuwajengea Kiwanda cha Kusindika/Hifadhi Samaki ili waweze kunufaika kwa vijana kupata ajira na kuondoa umaskini uliopo kwa jamii hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. MOSHI S. KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana kuchangia katika bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara. Nijikite sana na viwanda vidogo vidogo – SIDO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, SIDO ni eneo pekee iwapo likiboreshwa naamini Watanzania wengi hasa wa Mikoani na Wilayani na Vijijini wanaweza wakanufaika sana. Kumekuwa na tatizo la kutokupata fedha za kuendesha Shirika hili la SIDO ambalo ni muhimu sana katika maendeleo ya wananchi hasa wa vijijini. Naishauri Wizara ihakikishe wanatenga fedha za kutosha ili kuweza kunusuru Shirika hili ambalo kimsingi ndilo linaloweza kutatua matatizo hasa ya kuweza kusindika matunda katika maeneo ya vijijini ambako kuna matunda yanayoharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ujenzi wa Kiwanda cha Tumbaku. Naiomba sana Serikali iweze kuweka juhudi binafsi za kunusuru sekta ya zao la Tumbaku ambayo inakumbwa sana na tatizo la ukosefu wa soko. Ili kunusuru na kuwasaidia wakulima wa Tumbaku nchini, ni vema Serikali kupitia Wizara ya Viwanda iwasaidie wakulima hawa wa Tumbaku nchini waweze kumiliki Kiwanda chao cha Tumbaku ambacho kitawasaidia kusindika Tumbaku zao na pindi soko linapokuwa limepata mtikisiko kama uliojitokeza mwaka huu, basi wanaweza wakatumia fursa ya kuhifadhi Tumbaku iliyosindikwa na kuifanya Tumbaku hiyo iweze kusubiri soko wakati mtikisiko unapoisha. Kwa sasa viwanda vilivyopo vinamilikiwa na wafanyabiashara, yaani Makampuni yanayonunua Tumbaku na ndio yanayomiliki viwanda, jambo ambalo linaifanya sekta hii iwe ngumu sana katika kupata soko zuri. Naiomba sana Serikali iweze kulichukulia uzito mkubwa sana wa kuwasaidia wakulima hawa wa zao la Tumbaku nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu masoko, naishauri Wizara ihakikishe inatafuta masoko ya mazao ya Tumbaku, Pamba, Korosho ambayo yamepata mtikisiko wa kushuka bei. Wizara ikiongeza jitihada za kutafuta masoko nje ya nchi, itawasaidia sana wakulima wanaozalisha mazao hayo katika kanda mbalimbali hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni eneo la usindikaji wa maziwa na mazao yote yatokanayo na mifugo. Eneo hili halijaangaliwa kwa kina na Wizara kwani nchi yetu ina idadi kubwa ya mifugo lakini cha ajabu hata Kiwanda cha Viatu hatuna. Naishauri Serikali ielekeze nguvu kuwasaidia wafugaji ambao naamini tukiwajengea viwanda vidogovidogo katika maeneo yao hasa vya usindikaji wa maziwa, wafugaji wanaweza wakatoa mchango mkubwa wa pato la Taifa pamoja na kuwanufaisha wao na kuwa na maisha bora kuliko jamii yoyote hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, soko huria, naomba sana liangaliwe kwani uhuru uliopo hauwasaidii Watanzania bali unatoa mwanya kwa watu wa nje ya nchi, jambo ambalo ni hatari sana kwa Watanzania. Naiomba Serikali ichambue shughuli za kibiashara ambazo zinaweza kufanywa na wananchi, wazawa wapewe nafasi kubwa kuliko ilivyo sasa wageni wanapewa nafasi ambazo hawazifanyii kazi ipasavyo. Mifano ipo kama kuuzwa kwa Kiwanda cha Viatu Morogoro, matokeo yake Mwekezaji hakukiendeleza bali amekitelekeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataunga mkono hoja pale patakapokuwa pametolewa maelezo ya ziada ya Mheshimiwa Waziri.

MHE. MENDRAD L. KIGOLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Viwanda na Biashara ni nguzo ya kuimarisha uchumi wa nchi yetu ya Tanzania. Bila viwanda basi uchumi wetu hauwezi kukua na kuwawezesha watu kuwa na maisha bora. Changamoto ambazo zinaikabili Wizara hii, ni tatizo la umeme, tatizo la reli, tatizo la gharama kubwa za uzalishaji mali na uendeshaji wa biashara na tatizo la kuwa na mitaji midogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa ipo Dira ya Taifa ya Maendeleo ya Uchumi wa Viwanda vya Kati ifikapo mwaka 2025, Serikali inatakiwa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa shughuli za viwanda, biashara na masoko. Pia kusimamia kikamilifu mikakati ya viwanda, biashara na masoko ili kufikia malengo yaliyowekwa ili kuhakikisha uzalishaji mali unakuwepo na kuimarisha masoko ya ndani na nje.

MHE. DKT. ABDALLAH O. KIGODA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Waheshimiwa Mawaziri kama “Seasoned Economists” naelewa wazi wanajua kuwa nchi yoyote haiwezi kuendelea bila ya “Investiment Drive”. Wizara ya Viwanda ndio hasa inayohitaji kuvutia uwekezaji mkubwa ili sekta hii i-sustain sekta nyingine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uwekezaji wa kutia moyo kupitia SEZ, nadhani inabidi wawe more aggressive. Waondoe milima ya urasimu na tatizo la kutokutoa maamuzi ili kuvutia wawekezaji na hapohapo kupunguza coasts of doing business na adage ya Kilimo Kwanza, maendeleo ya viwanda kupitia uwekezaji is paramount.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ambalo limekuwa shelved kwa muda mrefu ni lile la uanzishwaji wa soko la Kimataifa Segera. A lot of promotion needs to be done, especially in the wake of public private partnership. Value addition ya soko hili itakuwa kubwa kwa uchumi wa nchi pamoja na a little bit of agro-processing.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawatakia kila la kheri katika utekelezaji na uendeshaji wa Wizara hii key.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. HUSSEIN N. AMAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri atoe ufafanuzi kuhusu utoaji wa leseni kwa wageni toka nje kufanya biashara za kati na ndogondogo kama uuzaji wa vipuri vya pikipiki na magari, viatu, nguo, vifaa vya umeme na ujenzi, mama lishe na daladala.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hawa wafanyabiashara wengi wanakwepa kulipa kodi kwa sababu zifuatazo:-

1. Wanauza bidhaa kwa bei ya chini sana ukilinganisha na bei za nchini mwao. Je, bidhaa hizo zinaletwa na nini toka nchini mwao? Je, hawalipi kodi za Serikali?

2. Bidhaa zao hazikidhi ubora, je, Serikali haioni kuwa wazawa hawatafanya tena biashara hapo baadaye na kutengeneza bomu la watu watakaokuwa hawana kazi tena?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri atoe tamko kuwa Serikali imeshindwa kusimamia Sheria zake na kuacha wananchi wakiteseka. Mfano bei ya sukari sokoni inauzwa Shilingi 2,200 - 2,500/= wakati Serikali ilitangaza bei ya sukari ni shilingi 1700/=, je, kuna nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mfano mwingine ni bei ya nishati ya mafuta ya dizeli, petroli na mafuta ya taa, bei ya mafuta ya taa ilipanda mapema sana lakini dizeli na petroli kuna nini mbona haishuki, je, Serikali haioni hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Waziri atoe ufafanuzi wa kina kwa Watanzania wafanyabiashara ni kwa nini TRA inawasumbua sana wazawa kuliko wageni. Pia atoe takwimu ya wafanyabiashara wageni ambao wametozwa faini kwa ajili ya kukwepa kulipa kodi pia kwa Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri awatangazie wafanyabiashara kuwa kauli yake aliyoitoa mwanzoni mwa mwaka huu eneo la Kariakoo Dar es Salaam ya kuwa anatoa siku 90 kwa wafanyabiashara wa kigeni kuwa watakuwa wamefunga biashara zao. Je, ni kwa nini hadi leo hawajafunga na maduka ya wageni kuongezeka kwa kasi zaidi Jijini Dar es Salaam?

MHE. MARTHA J. UMBULLA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nimpongeze sana Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dkt. Cyril Chami, Naibu wake Mheshimiwa Lazaro Nyalandu na Katibu Mkuu wa Wizara hii kwa hotuba nzuri na ya kina. Hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba huchangia kama ifuatavyo:-

(a) Je, Kiwanda cha General Tyre ufufuaji wake umefikia wapi? Ni nini kauli ya Serikali kuhusu kiwanda hiki muhimu?

(b) Kwa kuwa Mkoa wa Manyara una Ng’ombe, Mbuzi na Kondoo wengi kulinganisha na Mkoa wa Arusha ambako kuna Kiwanda cha Nyama, je, ni lini Serikali itaanzisha Kiwanda cha Nyama Mkoani Manyara, Babati hii siyo tu itawasaidia Wanamanyara kupata ajira, bali pia itapunguza kusafirisha ng’ombe kwa shida mpaka Arusha na kuongeza pato la Taifa.

(c) Kwa kuwa kuna wageni wengi sana walioajiriwa kuongoza viwanda mbalimbali hapa nchini na ambao wanawaajiri watu kutoka nje ya nchi yetu na kuacha wazawa/Watanzania hata zile kada za chini ambazo hazihitaji taaluma. Je, Serikali imeshaliona hili? TANALEC Arusha, Hoteli za Kitalii na kadhalika na kadhalika) ina mkakati gani wa haraka kuhusu tatizo hili kubwa?

(d) Je, Serikali ina mkakati gani ya kupeleka elimu ya kuboresha uzalishaji wa mazao ili kuongeza thamani ya mazao yatakayokidhi ushindani wa Soko la Kimataifa? Hii ni kwa sababu ajira kubwa Tanzania (+80%) iko katika Sekta ya Kilimo ambako wakulima walio wengi hawana elimu ya kuboresha ama kuongeza thamani kwa mali ghafi ya viwanda vyetu nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. HAWA A. GHASIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri wa Viwanda na Biashara, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu wake kwa kazi nzuri inayofanyika katika kuendeleza Sekta ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kufahamu ni kwa vipi Wizara ya Viwanda na Biashara inasaidia Sekta ya Viwanda katika Mkoa wa Mtwara, hasa Viwanda vya Mbolea na Saruji ambavyo Mtwara ina fursa kubwa sana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kufahamu ni lini eneo la EPZA la Mtwara litaanza kuendelezwa?

Mheshmiwa Spika, Mkoa wa Mtwara umebahatika kuwa na gesi ya kutosha na pia kuna suala la utafutaji wa mafuta ambao unaendelea. Je, Wizara imejipangaje katika kupokea na kuendeleza viwanda vinavyofanana na fursa iliyopo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawaomba Waziri na Naibu wake na Katibu Mkuu na Wasaidizi wake kutembelea Mkoa wa Mtwara ili kujionea wenyewe fursa zilizopo na kuziweka katika vipaumbele vya Kitaifa badala ya kutembelea Mkoa huo kupitia misafara ya viongozi wa Kitaifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. GODFREY W. ZAMBI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia hotuba ya Wizara kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha kuona kwamba Viwanda vingi vya Nguo nchini havifanyi kazi au vimekufa kabisa. Viwanda kama vile Mbeya Textile Mills, Mwanza Textile, Musoma, Arusha na kadhalika, havizalishi bidhaa za nguo kama ilivyotarajiwa. Matokeo yake ni kwamba Pamba nyingi inayozalishwa nchini inakosa soko na wakulima wetu wanahangaika sana kuuza Pamba yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunazungumza sana kujenga viwanda ili kuongeza thamani ya mazao ili kupata bei nzuri, sasa inashangaza kuona kwamba Viwanda vya Ngano na vile vya Kuchambua Pamba vinasuasua/vinakufa. Nataka kujua katika hali hiyo, tunaongezaje thamani ya Pamba yetu? Je, kweli iko dhamira ya dhati ya kujenga viwanda imara vya nguo nchini? Je, si aibu kwa nchi yetu kuuza Pamba yetu nje ya nchi ambako nguo na bidhaa nyingine hutengenezwa na baadaye kuuza kwetu tena kwa bei kubwa sana? Ni hatua gani huchukuliwa kwa wawekezaji waliouziwa Viwanda vya Nguo kisha wakabadilisha matumizi yake?

Mheshimiwa Mwenyekiti, inasikitisha pia kuona kwamba Viwanda vya Nyama vilivyokuwa vinamilikiwa na Serikali kama vile Tanganyika Packers – Dar es Salaam, Tanganyika Packers – Mbalizi, Mbeya vilikufa kienyeji sana. Kiwanda cha Tanganyika Packers – Mbalizi, Mbeya ambacho kilijengwa miaka ya 1970s kimsingi hakijawahi kufanya kazi. Nataka kujua hivi kulikuwa na maana gani kujenga kiwanda hicho kwa pesa za walipa kodi wa nchi hii na kisha kukitekeleza? Je, sasa Serikali ina mpango gani wa kukiendeleza kiwanda hicho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Viwanda vya Zana za Kilimo, Viwanda vya Ubungo Farm Implement (UFI) na Zana za Kilimo, Mbeya – (ZZK) vilikuwa muhimu sana katika maendeleo ya kilimo nchini. Hata hivyo, viwanda hivyo havipo tena! Inasikitisha sana maana kila kitu kizuri kinakufa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika moja ya ziara zake Mkoani Mbeya mwaka 2008/2009, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete aliagiza Kiwanda cha Zana za Kilimo Mbeya kufufuliwa. Nataka kujua utekelezaji wa agizo la Mheshimiwa Rais limefikia wapi? Je, Serikali kupitia Wizara hii ina mpango gani kuhakikisha kwamba Viwanda vya Zana za Kilimo vinajengwa nchini? Hivi sasa majembe ya mkono na yale ya kukokotwa na wanyamakazi, yana bei sana. Naiomba Serikali isimamie bei ya zana hizo ili mkulima aweze kuvipata kwa bei nafuu. Tukumbuke bila mpango madhubuti wa Zana za Kilimo, itakuwa ndoto kufanikisha mpango/dhana ya Kilimo Kwanza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba SIDO iwezeshwe zaidi kifedha ili iweze kutekeleza mipango yake vizuri. SIDO iwezeshwe kuajiri wataalam wenye ujuzi zaidi. Nasema hivyo kwa sababu wataalam wenye ujuzi zaidi hawapendi kujiunga na SIDO kwa sababu mishahara na mazingira ya kazi haviridhishi! Hii ni changamoto ambayo ni lazima ipatiwe majibu kama kweli tunataka SIDO ifanikiwe. Kwa mfano mashine za kukoboa Kahawa zinazotengenezwa na SIDO zina ubora wa chini sana ukilinganisha na zile zinazotengenezwa Kenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei ya vifaa vya ujenzi. Pamoja na ukweli kwamba vifaa vingi vya ujenzi vinapatikana hapa nchini lakini bei zake ziko juu sana. Kwa mfano, bei ya saruji ni kati ya shilingi 14,000/= na 25,000/= nchini kote, bei hiyo ni kwa mfuko mmoja. Leo tuna viwanda vitatu vya saruji nchini na kwa taarifa ya Waziri uzalishaji wake umekuwa unaongezeka mwaka hadi mwaka. Najiuliza kama hali ndiyo hiyo, kwa nini bei ziendelee kupanda? Kama bei ya Bati, Nondo, Misumari na kadhalika vyote vikiwa na bei juu, huyu Mtanzania maskini atajenga nyumba nzuri kweli?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Wizara isimamie vizuri eneo hili ili wafanyabiashara wasijipatie faida kubwa kwa kumuumiza mwananchi vinginevyo hakutakuwa na maana ya kuwepo viwanda nchini mwetu.

Mheshmiwa Spika, naunga mkono hoja, nawasilisha.

MHE. MHONGA S. RUHWANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yoyote ili iendelee kwenye Sekta ya Kilimo lazima iwe na viwanda vya kutosha ili malighafi inayotokana na kilimo ipate soko. Tuwekeze kwenye viwanda vya kusindika nyama, matunda na mazao mengine ya kilimo kwani mazao mengi yamekuwa yakiharibika au kuuzwa kwa bei ya kutupa kwa kukosa mahali pa uhakika pa kuuzia bidhaa zao. Kilimo Kwanza bila viwanda hakiwezekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zaidi ya miaka mitano Wabunge tumekuwa tukishauri Serikali kufufua Viwanda vya Tanganyika Packers, Machine Tools Moshi, General Tyre, ZZK Mbeya, Kiwanda cha Nyama Shinyanga na vingine vingi. Hivi Serikali haisikii? Kwa nini haifanyi kazi yenye tija ili kufufua viwanda hivyo na vingine vingi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, najua vingi vimebinafsishwa lakini ni wajibu wa Serikali kabla ya kuwekeana mikataba na wawekezaji kuwepo kifungu ambacho kila Mwekezaji atakayechukua kiwanda halafu asikiendeleze baada ya mwaka kiwanda hicho kirudi mikononi mwa Serikali ili kumudu hali mbaya ya uuwaji wa viwanda ulipo sasa. Ajira zinakosekana, masoko yanayotokana na mazao ya mifugo na kilimo yanakosekana. Hivyo ni wajibu wa Serikali kuona umuhimu huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haonyeshi juhudi za makusudi za kuiwezesha Wizara hii iweze kufanya kazi yake ipasavyo. Hili inadhihirishwa na ufinyu wa bajeti. Wizara iliomba shilingi bilioni 114.1 lakini imepewa pungufu shilingi bilioni 74.13 badala yake shilingi bilioni 39.97 ndizo zilizotolewa. Je, ni kweli Serikali iko makini na ina lengo la kutimiza shughuli zake? Vilevile katika bajeti hiyo shilingi milioni 175.9 zimetengwa kwa ajili ya posho, vipaumbele vya Wizara ni vipi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kigoma tunalo eneo la uwekezaji la biashara, Kigoma Special Economic Zone. Eneo lipo lakini halijaendelezwa, mara ya mwisho Kigoma SEZ ilitengewa shilingi milioni 500. Je, Serikali ina mpango gani wa kuendeleza eneo hili muhimu la uwekezaji?

MHE. SUSAN L. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ya Viwanda na Biashara ni Wizara muhimu sana kama ingekuwa na mipango inayotekelezeka. Wizara ambayo ingeweza kuinua uchumi wa nchi na kutokomeza umaskini kwa Watanzania wa Mijini na Vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, leo hii pamoja na ubinafishaji uliofanywa na unaoendelea kufanywa, kwa Watanzania walio wengi hawajafaidi ubinafsishaji wa viwanda vingi nchini hasa ukizingatia viwanda vingi vilivyobinafsishwa havifanyi kazi zilizokuwa zinafanya awali ama vimebadilishwa matumizi kuwa maghala na vingine hata kufugia mbuzi na vingine vinavyofanya kazi, vimekuwa mateso kwa Watanzania wanaofanya kazi kwa kuvunja mikataba iliyowekwa baina yao na Serikali na wafanyakazi hao, pia kutoa ujira mdogo. Kubadili matumizi kwa viwanda hivyo vilivyobinafsishwa kumeleta umaskini wa kipato kwa Watanzania kwa kupoteza ajira. Yote hayo yanafanyika Serikali ipo inaona sawa, iko kimya ili mradi wao wameshaweka kibindoni pesa za mauzo hayo ya hisa/viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kubadili matumizi ya viwanda hivyo si tu kupoteza ajira za wafanyakazi, Watanzania wamepata anguko la kukosa soko la bidhaa/malighafi zilizokuwa zinatumiwa na viwanda hivyo. Serikali hii pamoja na kuelewa watu wengi wamekosa ajira, haikuwaandalia Watanzania kazi mbadala kwa kutoa elimu ya kutosha, kujenga viwanda vidogovidogo vya kutosha kulingana na ukubwa wa tatizo. Matokeo imebaki ikilaumu eti Watanzania ni wavivu, wazururaji wakati Serikali haijaweka mipango madhubuti ya kuwapatia ajira. Sanasana kuacha nguvu kazi hasa vijana kupotea na kutumia madawa ya kulevya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niitake Serikali ieleze kabla ya ubinafsishaji tulikuwa na viwanda vingapi vilivyokuwa vinafanya kazi kwa kila Mkoa itoe orodha. Baada ya ubinafsishwaji tuna viwanda vipi na vingapi vitajwe kwa majina kila Mkoa ambavyo havifanyi kazi na sababu na Serikali imechukua hatua gani? Iwaambie Watanzania, kitendo cha Serikali kukaa kimya bila taarifa kwa Watanzania ni dharau na uvunjifu wa maadili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na Watanzania kukosa ajira, Serikali imeshindwa kuwawekea mazingira mazuri ya kufanya shughuli za kilimo na kuwasogezea huduma ya viwanda vidogo kulingana na ongezeko la watu nchini, wasomi na kadhalika. Serikali inasema sana na mipango ya vitabuni bila kutoa elimu ya kuwaandaa Watanzania wajiajiri. Hakuna vitendo vya kutosha kwa Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inatia uchungu kuona wageni kutoka nchi za nje wananeemeka na kuwaacha Watanzania wanahangaika. Miaka 50 ya Uhuru, viwanda vyote tumeuza, hii ni hatari kwa usalama wa nchi. Mtuambie Watanzania waende wapi? Wakija Mijini kujitafutia riziki wanapigwa, wakibaki Vijijini huduma hakuna, hayo hayavumiliki, Serikali iseme itawawezesha vipi Watanzania maskini wajitegemee?

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara imekuwa gumzo. Leo Mtanzania miaka Hamsini ya Uhuru ameandaliwa afanye biashara ndogo za ubuyu, za mkononi lakini mgeni kutoka nje atanyenyekewa, atadhaminiwa mtaji ili apate kunyanyasa Watanzania. Serikali iwaambie Watanzania faida ya kuwa na Wizara hii inayoshughulikia Viwanda na Biashara. Ni mategemeo yangu kuwa Wizara hii ingemkomboa Mtanzania wa Mjini na Kijijini kwa kuweka mpango kwa vitendo, kwa kusogeza viwanda vya mazao yanayozalishwa kila Mkoa yawe ya mifugo na nafaka ili mkulima apate soko na mfanyabiashara apate bidhaa za viwandani auze wote kwa pamoja waongeze kipato na waongeze pato la Taifa. Serikali haioni hayo, haifanyi maamuzi sahihi, kwa mtindo wa kuandika sana bila vitendo, mmefanya Watanzania kutoelewa umuhimu wa Wizara hii, Wizara inabaki kujali wageni zaidi, watendaji waende vijijini wakatoe elimu, watu waelewe maeneo ambayo wao wanaweza kufaidika kutokana na mipango na jinsi wanavyoweza kutumia fursa zilizopo kwenye Wizara hii kujiunga, kuanzisha viwanda, kufanya biashara na kujikwamua kiuchumi. Wizara iende ikatoe elimu shule za sekondari na vyuoni kuwaandaa Watanzania wajiajiri. Watanzania wamechoka kusikia matamko bila vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nahitaji majibu, ahsante.

MHE. DKT. MARY M. MWANJELWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza naomba nichukue fursa hii kuipongeza Wizara hii kupitia Waziri wa Viwanda na Biashara, Naibu Waziri pamoja na Katibu Mkuu na timu nzima ya Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda na Biashara ndiyo inayoangaliwa kiuchumi duniani kote. Kupitia biashara ndipo na nchi itakapoweza kukusanya kodi hence pato la Taifa kuongezeka

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la utambuzi wa bidhaa zetu (originality) ni zuri sana, naipongeza Serikali katika hatua hii lakini ni mchakato gani uliotumika kwa kupata Kampuni itakayoshughulikia suala hili (Barcodes)? Serikali itoe maelezo ya kina kwa sababu kumekuwa na malalamishi mengi kuwa kuna sura ya harufu ya rushwa na upendeleo, toka kwa wadau mbalimbali. Aidha, wananchi pia ningeshauri wapewe elimu ya kutosha juu matumizi ya mfumo huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii Kiserikali ndio inatakiwa itoe mkakati wa kimasoko (marketing) ndani na nje ya nchi ukiondoa mwekezaji. Itoe maelezo imejipanga vipi katika kuifanya nchi marketing, maelezo ya ukurasa wa 147 hotuba ya Mheshimiwa Waziri hayatoshelezi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini biashara ndogondogo hazikui? Je, Serikali ina mkakati gani katika kuwaendeleza wafanyabiashara hawa wadogowadogo? Ianzishe benki ya walala hoi ambayo pia masharti yake yawe nafuu sana na bidhaa zao wanazouza zipewe kipaumbele kununuliwa ili kuwawezesha zaidi kimasoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kwa nini viwanda vyetu uzalishaji wake unazidi kudidimia na bidhaa zizalishwazo zinakosa soko? Kwa nini kuna gharama kubwa ya uendeshaji wa viwanda (high cost of doing business)? Kwa nini bado miundombinu kama ya umeme, maji, reli, mawasiliano bado ni mibovu tu? Hali hii itasaidiaje kusonga mbele kwa viwanda vyetu?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini kumekuwepo na migomo ya mara kwa mara viwandani kwa wafanyakazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini kumekuwepo na mahusiano mabaya kati ya Public Sector na Private Sector? Tukumbuke kuwa sera ya PPP (Private Partnership Programme) ni muhimu sana katika kusukuma gurudumu la maendeleo kwa haraka na ufanisi zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye suala la Shirikisho la Afrika Mashariki, kama Tanzania, Serikali inasemaje, imejiandaa vipi kwenye suala la masoko, biashara na viwanda? Tukumbuke tumekuwa kwenye Custom Union, Common Market, Common Currency na Federation sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja lakini nipatiwe majibu ya kina na makini.

MHE. SAID A. ARFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, najaribu kutafakari kama Serikali hii ina dhamira ya kweli ya kutekeleza maneno, mahubiri na maandiko mazuri yanayoonyesha kwamba tunataka kusonga mbele kama Taifa wakati utekelezaji wake haupo, kama upo hauridhishi na kukatisha tamaa kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumekuwa tukisikia miaka nenda miaka rudi mradi wa Mchuchuma na Liganga hadi sasa hakuna jambo lililofanyika na tukaweza kujivunia, tatizo ni nni? Tumerogwa? Hapana tatizo, hatuna umakini katika kupanga na hasa utekelezaji. Serikali sasa iongeze mtaji kwa NDC ili miradi iliyopo chini ya NDC iweze kutekelezwa. Tumechoka na hadithi za Liganga na Mchuchuma kila siku. Nchi hii tunashindwa kuamua tufanye nini wakati tupo gizani na tuna mrundikano mkubwa wa mamilioni ya tani ya makaa ya mawe na tunakosa umeme. Serikali sasa iamue kuwekeza katika miradi ya kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika nchi yetu katika maeneo mengi tunazalisha matunda, yanayofika sokoni ni kidogo zaidi kuliko yale yanayoharibika na kuoza mashambani kwa kuwa hatuna mpango madhubuti wa kuthibiti hali hii kwa kujenga viwanda vdogovidogo katika maeneo yenye Maembe kule Mpanda, Machungwa au Mananasi katika maeneo mengine wakati Serikali kwa makusudi inalipunguzia Shirika la SIDO uwezo wa kifedha mwaka hadi mwaka, ni kweli tunayo dhamira na utashi wa kubadili hali hii kama tunavyohubiri na kuandikwa vema katika Ilani ambayo kila leo inatajwa na kusifiwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie na hali ya mafuta na umuhimu wa kuwa na Tume ya Bei. Nadhani sasa tujifunze hasara za kupokea mifumo inayoletwa bila kutafakari kwa kina na kukubali kuwa na soko huria (soko holela), Serikali inashindwa kulisimamia sasa hilo soko holela. Kama tumeridhia bei itapangwa na soko, inakuja leo tunataka kusimamia soko? Tulikubali wenyewe basi tuwe wapole tu hata inapofikia leo wafanyabiashara wanaitunishia misuli Serikali huo ndio mfumo wa soko huria ambao tulikubali wenyewe. Ni vema sasa Serikali ikaangalie upya umuhimu wa Tume ya Bei kama ilivyokuwa hapo nyuma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Stakabadhi Ghalani na Masoko, nitapenda kupata maelezo ni vigezo vipi vinatumika ili kuweza kusajili kijiji A au B kuwa na maghala na mfumo wa Stakabadhi Ghalani na ni kwa nini mfumo huu unaendeshwa kibaguzi? Unakuta Vijiji kadhaa katika Mkoa vina utaratibu huo wakati Vijiji vingine havina utaratibu huo. Eneo moja katika Wilaya wanaweka mpunga au mahindi ghalani eneo lingine katika Wilaya hiyohiyo hawana. Naomba maelezo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho Maghala. Jukumu la ujenzi wa Maghala ni la Serikali na Taasisi zake kamwe lisiwe ni mzigo kwa wananchi ambao leo wanachangia ujenzi wa Madarasa, Zahanati, Vituo vya Polisi, Ofisi za Watendaji, Kata/Vijiji na kadha wa kadha, orodha ni ndefu ya mzigo wa michango au uchangiaji katika maendeleo. Bila kuwa na maghala hata kama Kilimo Kwanza kitafikia malengo yanayokusudiwa, mazao mengi yataharibika kama tutakuwa hatuna maghala. Tujiandae sasa. Tulijenga maghala tukayauza, mimi nashindwa kuelewa kabisa mipango ya nchi hii. Tuanze tena, tujenge maghala lakini kwa bajeti inayopewa Wizara hii itabakia kuwa ndoto.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana.

MHE. HERBERT J. MNTANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza sana Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Naibu Waziri kwa ari mpya wanayoonyesha kusaidia Sekta ya Viwanda nchini na mkakati katika bajeti ndogo ya 2011/2012.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu mkakati mpya wa kufufua viwanda vya nguo. Mtikisiko unaoendelea sasa kuhusu bei ya Pamba kushuka, ni ishara inayohitaji mkakati wa kufufua upya viwanda vya nguo vilivyokuwepo kama vile Kiltex – Arusha, Mwatex – Mwanza, Mutex – Musoma na Sunguratex – Dar es Salaam. Hii itasaidia kuboresha bei ya malighafi ya Pamba na kuongeza ajira. Hivyohivyo kurejesha viwanda na maghala ya Korosho Mtwara na Lindi, Pwani na Dar es Salaam.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivvyo, Serikali lazima itambue kwamba ili wawekezaji wa viwanda wajitokeze Tanzania ni lazima mambo yafuatayo yatekelezwe:-

1. Ardhi ya uwekezaji ipatikane bila urasimu.

2. Uwepo wa barabara kwa ajili ya kufikisha malighafi viwandani na kuondoa bidhaa viwandani kwa gharama nafuu.

3. Maji kwa uzalishaji na matumizi ya wafanyakazi wengi wanaofanya kazi eneo moja. 4. Umeme kwa uendeshaji wa mashine za uzalishaji na mwanga kwa matumizi ya utendaji na usalama wa wafanyakazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bila ushirikiano wa Sekta hizo kwa pamoja na kuwezeshwa mafanikio hayatakuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa miaka mingi NDC imepewa majukumu makubwa lakini haiwezeshwi! Kuipa NDC jukumu la kuungana na NSSF katika kujenga mradi wa umeme Mchuchuma au Liganga na au kuwezesha NDC na NSSF kuwekeza na kufufua kiwanda cha Matairi Arusha bila kuiwezesha NDC ni ndoto ambayo utekelezaji wake hautakamilika kwa vitendo. Serikali ina tamko gani juu ya kuiwezesha NDC katika bajeti hii ya mwaka 2011/2012?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuboresha Vyuo vya Biashara (CBE). Majengo ya vyuo vya CBE Dar es Salaam na CBE Dodoma yanahitaji ukarabari na kupewa muono wa kisasa hasa baada ya CBE kuongezewa uwezo wa kutoa Diploma za Juu (sawa na degree) pia baada ya kuongeza udahili, mkakati uwepo wa kuongeza mabweni na kujenga hosteli hasa hapa Dodoma ambapo nafasi za viwanja bado zipo. Je upo mkakati gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, usimamizi wa biashara kati ya Tanzania na Kenya, Wilaya ya Muheza inazalisha machungwa ambapo wastani wa asilimia 40 yanasafirishwa kwenda Kenya. Hata hivyo, wafanyabiashara kutoka Kenya wanaingia Tanzania na kununua machungwa kwa fedha za Tanzania. Hii ina maana wanabadilisha fedha nchini Kenya na kuacha fedha zao kwao na kununua fedha za Tanzania hukohuko Kenya, je, huu ndio mfumo mzuri wa biashara kwa nchi zetu kabla ya kukamilisha mfumo wa soko huria? Hivi Wizara ya Viwanda na Biashara inaweza kutoa takwimu za mauzo ya machungwa yanayopita mipaka ya Horohoro na Namanga kutoka Tanzania kwenda Kenya? Mheshimiwa Mwenyekiti, uwekezaji katika Shamba la Mpira Kihuhwi, Muheza na madai ya wafanyakazi. Kwanza, naipongeza Wizara ya Viwanda na Biashara kwa msimamo thabiti juu ya uendelezaji, uwekezaji na kusaidia wafanyakazi wa Shamba la Mpira Kihuhwi, Muheza kufuatilia madai ya mafao yao kwa Mwekezaji aliyewatoroka. Kimsingi, naamini Wizara hii kupitia Msimamizi Mkuu NDC, inatambua wajibu wa kusaidia mhimili mwingine wa Taifa (Mahakama) kuheshimiwa kwa utekelezaji wa maamuzi yake kwa hukumu iliyotolewa kwa kuwapa haki wafanyakazi kulipwa haki zao. Kwa kuwa Serikali (mhimili mwingine) ndio ulioingia mkataba wa ukodishaji wa shamba hilo na mwekezaji basi Serikali lazima iwajibike katika utekelezaji wa hukumu hasa baada ya Mwekezaji kutoroka nchini. Ni matarajio yangu na wafanyakazi wa Kihuhwi Rubber Planntion, Muheza watapata msaada wa malipo yao mapema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa kuwa Shamba la Kihuhwi halikuwa linaendelezwa kwa miaka mingi hasa kwa kupanda miti mipya, wananchi waliotelekezwa wametumia sehemu ya ardhi tupu kupanda mazao ya kudumu na kujenga nyumba. Ushauri wangu kwa Serikali, utaratibu wa kuthamini mazao ya kudumu na nyumba za wananchi hao ufanywe kwa ushirikishwaji ili kujenga fursa nzuri za uwekezaji wa baadaye kati ya Mwekezaji na wananchi waliopo maneneo hayo hasa Kijiji cha Maskati na Msowelo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, wananchi na sisi viongozi wao tunapenda kufahamu Mwekezaji mpya ni nani na ana mkakati gani wa dhati wa kuendeleza Shamba hilo la Mpira Kihuhwi. Je, ana uzoefu katika zao la mpira na soko la biashara ya zao la mpira? Ni ni vema tukapata maelezo hayo muhimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. ANNAMARYSTELLA J. MALLAC: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi hii ili niweze kuchangia katika Wizara hii ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo tulilonalo katika Tanzania yetu hii ni maneno matupu ya kutamanisha na mipango mizuri lakini isiyowagusa wananchi kwa faida ya maendeleo yao. Viwanda hivi haviwagusi wananchi maskini ambao ndiyo wanaoteseka katika nchi hii. Viwe viwanda vidogovidogo au vikubwa, tunapoviongelea hapa, tunawaongelea wamiliki wenye pesa, matajiri na siyo maskini. Ningefurahi sana kama Serikali ingeweza kuanzisha viwanda vidogovidogo kupitia Halmashauri zetu na kuweza kuwaajiri wananchi maskini na wasio na mitaji. Suala hili linahitaji ubunifu kwani linawezekana na linaweza kuinua kipato cha Watanzania wengi na kuingizia pato Serikali. Ili kuinua uchumi wa wananchi wasiyojiweza Serikali inaweza kuanzisha viwanda vidogovidogo kama vifuatavyo hapa chini, viwanda vya kutengeza sabuni na nguo za batiki, viwanda vya ufinyanzi, viwanda wa ushonaji na viwanda vya usindikaji wa vyakula na kadhalika. Kutokana na ukosefu wa ubunifu na urasimu wa baadhi ya vingozi, ndiyo tunashindwa kufanya vitu vya maendeleo kwa manufaa ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunapoongelea viwanda vikubwa hatuangalii tunawasaidia vipi wananchi wasiojiweza kwa athari na faida zake mfano Serikali inakuwa haitambui Watanzania wake wanalipwa kiasi gani kutoka kwa Wawekezaji au mwenye kiwanda na kama inajua ufuatiliaji wake unakuwa hakuna. Hapa ndipo tunapowatesa wananchi na kutoonyesha ushirikiano. Namwomba Mheshimiwa Waziri aliangalie suala hili na kulifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, the same kwenye biashara, wanaohangaika ni wafanyabishara wadogowadogo kama Wamachinga. Sasa katika plan za Miji Wizara inatakiwa kuangalia misingi ya biashara kwa wafanyabiashara wadogo ambao wananyanyasika katika nchi yao kama Wamachinga ambao hufukuzwa bila kuandaliwa sehemu za kupeleka biashara zao na kama wanaandaliwa basi kibiashara hazifai na kiusafi kwa maana ya ukosefu wa choo na maji, huduma hizo zinakuwa hazijakamilika. Ukiangalia kibiashara hapo kunakuwa hakuna haki ila mara nyingi ubabe ndiyo hutumika. Namwomba Waziri kupitia Wizara hii angalie sana migogoro hii ambayo imekuwa kero kubwa kwa wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, maendeleo ya vijana. Vijana ndiyo nguvukazi kwa Taifa lakini leo hii vijana wanasaidiwa kwa maneno matupu. Mimi nasimamia upande wa Mikoani kwa sababu ndiko kwenye athari za wazi zinazoonekana. Vijana wa Wilayani na Mikoani wapo nyuma na hawapewi kipaumbele chochote katika maendeleo yao. Utakuta Serikali inapotoa agizo, vijana wanafuata, lakini utekelezaji ndiyo tatizo. Mfano kuna mikopo ya vijana waliojiunga pamoja hupewa na wapofuata utaratibu kwa Afisa Maendeleo ya Vijana kwa pesa zinazotengwa na Wizara na pia kwa kila asilimia tano ya bajeti ya Halmashauri lakini vijana hata wafanye hivyo hakuna utekelezaji na wanapokosa kuajiriwa kwa kukosa mitaji ndiyo mwanzo wa kufanya maovu kama uvutaji bangi, ubakaji na mengine mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi kwa Wizara, tunaomba mabadiliko. Mimi kama mama, naona uchungu kuona vijana wanapotea na kukosa mwelekeo. Naomba Wizara iangalie sana vijana, pia ihakikishe inatoa semina kwa Maafisa Maendeleo ya Vijana ili wawe karibu na vijana katika kuhakikisha wanapata mabadiliko kimaisha. Vijana wanahitaji mitaji kiuchumi, kielimu na mengineyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namalizia kwa kumuuliza Waziri, vijana ndiyo kundi linaloteseka na maisha magumu Wilayani na Mikoani, je, wakijiweka katika vikundi na kuanzisha biashara, Serikali haiwezi kuwahamishia tena sehemu nyingine zisizo na vyoo wala maji kama walivyofanyiwa wafanyabiashara wauza mitumba wa Wilaya ya Mpanda na kuwapotezea mwelekeo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sana vijana waokolewe katika mazingira magumu ya ajira waliyonayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasilisha.

MHE. ALI K. SEIF: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri, ukurasa wa nane, Wizara ina nia ya kuimarisha ushiriki binafsi katika Soko la Ushindani, msimamo huo ni sawa lakini duniani kote watu binafsi wanapatiwa mikopo ya kuendesha shughuli za biashara. Hapa kwetu fursa hiyo ya mikopo hasa kwa watu binafsi, wazawa ni tatizo kubwa na wakati mwingine watu binafsi wageni ndio wanathaminiwa na vyombo vya fedha. Kimsingi huo, wafanyabiashara binafsi wa Tanzania siku zote watashindwa kushiriki kikamilifu katika soko la wafanyabishara binafsi wa kigeni, je, Serikali ina mpango gani kuhusu suala hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 12 wa hotuba ya Waziri wamesema Wizara imekusudia kuimarisha Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB). Benki hii itakapoimarika kimtaji na kuweza kuwakopesha wahusika itakuwa ni mkombozi mkubwa. Lugha ya kuimarisha tu peke yake bila ya mikakati ya kuimarisha hatutofika mahali. Je, Serikali ina mpango na mkakati gani wa kuimarisha Benki hiyo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukurasa wa 13, aya ya 24, Mwekezaji katika mradi wa Makaa ya Mawe, chuma cha Liganga na viwanda vya kemikali amepatikana ambaye ni Kampuni ya Sichuan Hongda Co-operation ya China. Tahadhari yangu juu ya mkataba wa mradi huo, Tanzania ina uzoefu wa kuingia mikataba mibovu, yaliyotokea hapo nyuma yasije yakatokezea sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika hotuba ya Waziri, ukurasa 15, Wizara imesema ina nia ya kuimarisha uzalishaji mali viwandani kwa kuvifufua na kuviendeleza kwa teknolojia ya kisasa viwanda vyote ambavyo viliuzwa huko nyuma na kutelekezwa. Ni wazo zuri sana hilo lakini ukisoma aya ya 27, 28 na 29 huoni ni kwa mkakati gani nia ya hapo juu (kifungu ‘f’ ukurasa 15) itafikiwa. Kwanza, mimi naona hayo ni maneno tu matamu lakini yasiyo na mkakati uliodhihirishwa kwenye kitabu cha Wizara. Kama Serikali ina mikakati ya kufikia huko kwa viwanda vilivyotelekezwa, ninaomba niambiwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wazo la kutoa motisha au vivutio vya uwekezaji kwenye viwanda vya nguo, ngozi na kadhalika (ukurusa 17 kifungu ‘g’) ni mzuri lakini vivutio vyote hivyo isije ikafika hatua ya sisi tukapoteza zaidi kama hali iliyoko kwenye migodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Msasani kuna Taasisi inayohusiana na Maendeleo ya Viwanda (TIRDO). Je, Taasisi hii imefanikiwa vipi katika kuendeleza viwanda wakati huu wa biashara huria? Je, Taasisi hii ina uhusiano gani na SIDO (Shirika la Viwanda Vidogo)?

MHE. RITTA E. KABATI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kumpongeza Waziri wa Wizara hii, Mheshimiwa Dkt. Cyril A. Chami (Mb), Naibu Waziri, Mheshimiwa Lazaro Nyalandu (Mb), Katibu Mkuu Bibi Joyce Mapunjo na Watendaji wote wa Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa SIDO. Naomba niipongeze SIDO kwa kazi kubwa wanayoifanya kwa uanzishwaji wa viwanda vidogovidogo ambavyo vimeweza kuinua hali ya uchumi hapa nchini angalau kwa kiasi fulani lakini bado haijaweza kuwasaidia sana vijana wetu. Napenda kutoa ushauri wangu kama ifuatavyo, SIDO wawe na ushirikiano wa moja kwa moja na Vyuo vyetu vya VETA. Naamini kabisa ushirikiano wao ungeweza kuwasaidia vijana wetu wengi sana mara wamalizapo mafunzo kuweza kujiajiri kwa kuwa na vitendea kazi na ubora wa kazi zao wangepata masoko ya uhakika kwa uuzaji wa bidhaa zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na maonyesho mengi sana yanayofanyika sehemu mbalimbali hapa nchini ambayo huandaliwa na Shirika la SIDO na tumeshuhudia ubunifu mbalimbali. Je, wale wabunifu wa vitu mbalimbali Serikali inawasaidiaje? Ifike mahali wale wabunifu wetu wanaogundua mashine, mitambo wafahamike rasmi na Serikali hii kwa kutangazwa na kusaidiwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ajira katika viwanda hapa nchini. Wizara hii zamani ilikuwa ndio mkombozi wa ajira hapa nchini tofauti na sasa Wizara hii imeruhusu raia wa kigeni kufungua viwanda mbalimbali au kufungua magereji hapa nchini hali ambayo imesababisha wananchi walio wazawa wa nchi hii kushindwa kuendelea na biashara zao. Imefika sehemu hata biashara ndogondogo kama ice cream, pipi, maua na kadhalika kufanya na wenzetu wageni. Naomba jambo hili lichukuliwe kwa umuhimu wake. Siamini kama sisi Watanzania tukienda katika nchi za wenzetu tunaweza kupata kibali kirahisi cha kuendesha au kufanya biashara ndogo kama hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vingi sasa hapa nchini vimefungwa tatizo hasa ni nini? Ningependa kupatiwa majibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. DKT. FENELLA E. MUKANGARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika utendaji wa Wizara, naomba yafuatayo yaangaliwe kwa karibu na ikiwezekana yafanyiwe kazi kwa mujibu wa sheria.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Nishati na Madini kuhakikisha TPDC na Kampuni chini yake ianze mapema iwezekanavyo kufanya biashara ya mafuta.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, BP shares zake zinunuliwe na Serikali au wadau/wananchi na iendelee kufanya biashara ya mafuta kama kampuni, yaliyojitokeza siku za karibuni kuhusu mafuta ni maono tosha ya umuhimu wa kusimamia kwa karibu suala la mafuta na umeme. Inaonekana mifumo ya usimamizi na uwajibishaji wa watendaji husika na wafanyabishara bado ni dhaifu. Hivyo basi tunataka maslahi ya nchi pia yazingatiwe sio ya wafanyabiashara tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, ni kwa kiasi gani maeneo yaliyotengwa kwa programu za EPZ na SES katika Mikoa yote 17 iliyotajwa katika hotuba ya bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara yamezingatia utoaji fursa kwa vijana. Kwa mfano kuhakikisha utoaji wa nafasi za makusudi za kumiliki fursa na rasilimali mbalimbali kwa vijana zinazingatiwa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, pamoja na kwamba utoaji kipaumbele katika kusimamia na kukaribisha ufufuaji wa viwanda vilivyobinafsishwa ni muhimu, muhimu zaidi ni kuhakikisha kuna mpango maalum wa kufufua nyanja zote za viwanda na biashara zinazoendana na uwezo wa kutoa nafasi ya kuwahusisha vijana wetu katika kazi mbalimbali za viwanda zitokanazo na kilimo, uvuvi, madini (packaging na processing) hata habari (hardware and software) hata kama ni assembling. Ni muhimu kuwe na utekelezaji wa dhati wa kutengeneza enabling environment yaku-engage vijana wetu katika kazi mbalimbali. Mfano masuala ya Packaging/branding etc, vijana wapate nafasi ya kubuni designs packing mbalimbali za bidhaa zetuna viwanda na VETA zibebe huo mtazamo katika mitaala yao, lakini wakiwa pia na mwingiliano wa karibu na Wizara ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, sehemu zilizotengwa kwa EPZ zitayarishwe kwa dhati kisheria ili maamuzi na wawekezaji wakiwa tayari wasikwame kwa sheria au kanuni zetu zilizopo za Wizara ya Ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, naomba uwezekano wa kubadili saa za kufanya biashara maduka ya Miji mikubwa yafunguliwe muda wote, saa mbili na nusu au saa tatu mpaka saa mbili au saa tatu usiku, saa za maduka kufunguliwa zisiendane na saa za maofisini (flexibility iwepo).

MHE. REGIA E. MTEMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Morogoro ulitengwa kuwa Mkoa wa Viwanda. Bahati nzuri kuna viwanda kadhaa vilivyoanzishwa lakini vingi vya viwanda hivyo hivi sasa vimefungwa na vingine havifanyi kazi kwa ufanisi. Napendekeza Serikali ivifufue viwanda hivi kwa kutumia mpango wa PPP ili kufikia lengo lake la awali la kuufanya Mkoa wa Morogoro kuwa Mkoa wa Viwanda. Vijana wengi wanategemea ajira kupitia viwanda hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya sukari Mtibwa na Kilombero viangaliwe upya ili vizalishe sukari kwa bei ambayo ni reasonable kwa wakazi wanaoishi maeneo ya viwanda hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile viwanda hivi viangaliwe upya ili kuwasaidia wakulima wa miwa kupata faida katika kilimo chao. Mfumo wa DRD unalalamikiwa sana na wakulima hawa. Wakulima wa miwa washirikishwe katika upimaji wa viwango vya sukari kwenye miwa yao wanayopeleka kwenye viwanda hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha Zana za Kilimo, MTM cha Mang’ula Kilombera kifanyiwe uchunguzi wa kina kwani inasemekana kuna ufisadi katika kiwanda hiki. Napendekeza, Wizara kwa kushirikiana na CAG wafanye uchunguzi pamoja na ukaguzi maalum.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha KPL (Kilombero Plantation Limited) kinalalamikiwa na wananchi wanaoishi kwenye maeneo yanayozunguka kiwanda hicho kuwa wameharibiwa mazao yao hivyo wanahitaji compasation kwa mazao yao.

MHE. REBECCA M. MNGODO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kutoa mchango wangu kuhusu hotuba ya Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Dkt. Cyril A. Chami (Mb), alipowakilisha Bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2011/2012.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wajasiriamali walio wengi hapa nchini hawana taarifa za kutosha kuhusu namna ya kupata masoko ya bidhaa zao hasa nje ya nchi. Napendekeza ziwepo njia rahisi za kuwapa taarifa wajasiriamali wetu ili wajue jinsi ya kuyafikia masoko ya bidhaa zao hasa kwa nchi za nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia mafunzo ambayo yametolewa kwa wajasiriamali 38,583 mwaka 2010/2011, nashauri mafunzo yatolewe kwa kutumia vyombo vya habari, kwa mfano Radioni. Kigharamiwe kipindi cha redio cha elimu kwa wajasiriamali ili kusudi wafikiwe wajasiriamali wengi zaidi kwa wakati mmoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la ubora wa viwango vya bidhaa zinazoingia nchini linazidi kukomaa. Ni kwa nini TBS haikagui bidhaa kabla hazijaingia sokoni? Mara nyingi tumeona bidhaa zikiteketezwa kwa moto kwa kugundulika kwamba zimeingia sokoni kinyemela bila kuwa na viwango vya ubora unaotakiwa. Walaji na watumiaji wengi wa bidhaa zinazotoka nje ya nchi ambazo hazina ubora wameathirika kwa kulipa gharama kama vile ya mali yenye viwango vya juu vya ubora. Napendekeza kwamba ukaguzi ufanyike mapema kabla ya bidhaa kumfikia mlaji ili kuepuka usumbufu unaojitokeza kwa walaji na watumiaji wa bidhaa zilizo chini ya bora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa haya machache, naomba kuwasilisha hoja.

MHE. KABWE Z. ZITTO: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa mujibu wa Mpango wa Maendeleo wa Taifa 2011/2012 – 2015/2016, sekta ya viwanda (manufacturing) inatakiwa ifike lengo la kuchangia 23% ya GDP. Mpango umeainisha vikwazo vya maendeleo ya viwanda ikiwemo umeme, mitaji na low linkages.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pendekezo kubwa la Mpango wa Maendeleo ni viwanda vya bidhaa za kilimo (Agroprocessing). Kama tunataka tupate ukuaji wa kasi wa sekta ya viwanda, first things is Agroprocessing. Hii inaendana kabisa na concept ya Rural Growth ambayo ninaipendekeza kila siku hapa Bungeni. Agroprocessing industries itapelekea viwanda vingine kukua (backward linkages), kukuza sekta ya huduma na hivyo kukuza uchumi kwa ujumla. Mapendekezo ya hotuba zote zijazo yawe yanafanya reference kwa Mpango wa Maendeleo. Hotuba ieleze utekelezaji wa Mpango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mchuchuma/Liganga. Miradi hii miwili ni miradi ambayo sina haja ya kueleza umuhimu wake. Mpaka sasa mkataba kati ya Sichuan Hongda na NDC haujasainiwa. Taifa zima limeaminishwa kuwa mradi utatekelezwa lakini ukweli ni kwamba miezi sita imepita hakuna maendeleo ya uhakika ambayo yamefanyika, inasikitisha sana mradi huu kuchelewa. Hii ni complex project, NDC must do vigoruous PR kuhusu mradi huu. Kamati yangu ya POAC imewapa NDC nguvu zote za kisiasa lakini ukimya unatisha. Huu mradi wa chuma, makaa, umeme na reli unapaswa kulindwa na kila Mtanzania. Wizara iandae safari ya Mawaziri wote kwenda Ludewa. Rais aombwe afanye cabinet meeting moja kule. We must rule the ration behind this project. Sichuan Hongda wasukumwe kukamilisha lakini tuwe na full back position. Hatupaswi kuchelewa. Nakosa maneno ya kueleza kuhusu mradi huu. Ninachotaka ni kuupa umuhimu wake. Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu watoe kipaumbele. Tusipoteze mradi huu. NDC pia watengeneze brochure nzuri na five minutes DVD on this project. DVD zigawiwe kwa Wabunge na Wahariri wa Vyombo vya Habari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Magadi Soda, huu ni mradi mwingine wa kimkakati. Mradi huu umepigwa vita sana na watu hata Wabunge. Serikali imekaa kimya. Tafadhali mradi huu uendelee. Mradi huu uelezwe vizuri kwa umma. Wafanyeni Watanzania wajivunie miradi hii. Make us proud of our resources. This is done through paper PR – mradi huu uendelee haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, General Tyre East Afrika Limited, NDC na NSSF wapewe kiwanda hiki haraka waunde SPV, waite tenda ya kupata strategic investor. Hili lifanywe haraka sana. NDC isimamie mashamba/NSSF manufacturing. NSSF wapo tayari hata leo iwapo Serikali itaamua. Zabuni ya kupata strategic investor itangazwe kabla ya mkutano ujao wa Bunge. Lazima ionekane tunafanya mambo, tuache maneno, tuonyeshe vitendo. GTEAL ifufuke haraka iwezekavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawatakia kila la kheri.

MHE. HAMAD ALI HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze na kusema kwamba viwanda ni sehemu moja ambapo tungeweza kuokoa idadi kubwa sana ya vijana katika kuwapatia ajira kwani viwanda hivi vikifanya kazi sawasawa na kwa kuwa vitakuwa vinafanya shughuli zao hapa nchini maana yake ni kuwa vijana na watu wetu ndio watakaofanya kazi katika viwanda hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo linalosikitisha ni kuona kwamba viwanda vyetu vinakufa badala ya kuimarika. Tuna viwanda vingi ambayo vimekufa na vingine viko taabani na vinaelekea kufa, hii inatokana na nini? Hili jambo limeshamiri hapa kwetu peke tofauti na nchi wa wenzetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vingi hapa kwetu ambavyo vimekufa na ambavyo vinakua vingi vyao ni vile ambavyo vimekodishwa kwa wageni na wengi wao ni wale wa kutoka India. Kama vile kwamba wanakampeni maalum ya kuhakikisha kwamba wanaua viwanda tubaki kuendelea kuagiza bidhaa toka katika mataifa yao. Unaweza ukashangaa ni vipi viwanda wamepewa vinafanya kazi lakini leo vipo ambavyo hata vyuma vya mitambo vimeuzwa kama chuma chakavu, inasikitisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mataifa mengi yalioendelea hutumia utaratibu wa kuanzisha viwanda vidogo SIDO kwa kuamini ni mahali ambapo vijana na watu wengi wanaweza kuwaelekeza huko ili na wao waweze kujipatia uwezo wa namna ya kumudu maisha yao, hasa ukizingatia Serikali kuu haina uwezo wa kuwaajiri watu wote. Hivyo basi, maeneo kama hayo ndio mbadala wa Serikali kuona kwamba, inawawezesha wananchi wake kuweza kukabiliana na maisha yao ya kila siku. Lengo la Serikali la kuanzisha Sera ya Viwanda ni kuwasaidia wananchi wetu lakini kama vile lengo hili halikuwa ndio hoja ya kuanzisha viwanda au kama vile ilikuwa ni hoja ya muda mfupi na ikifikia muda fulani jambo hili iwe ni basi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuanzia Serikali kuu na watu wote tunafaa tuanze utamaduni sasa wa kujali bidhaa (fanicha) za hapa nchini na tuachane na fanicha za kutoka nje, kufanya hivyo ni kumdumaza Mtanzania. Kuacha kutumia fanicha za hapa nchini kwetu maana yake ni kumdumaza Mtanzania kiuchumi, kuuwa utaalam wa watu wetu kwa wale wanaotengeneza fanicha hapa nchini na kukamilisha ile dhana yangu ya kuuliwa viwanda vyetu ili tuendelee kuagiza bidhaa toka kwao (wawekezaji tunaowapa viwanda) na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migogoro iliyopo katika baadhi ya viwanda hapa nchini bado ni mwelekeo uleule wa kuelekea kule kwa kukiuwa kiwanda na kuwaacha watu bila kazi na baadaye tuendelee kuagiza kila kitu kutoka nje na Tanzania tuendelee kuwa ombaomba kila siku na wao waendelee kuonekana kuwa ni nchi zilizoendelea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha. Ahsante.

MHE. VICTOR K. MWAMBALASWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ndogondogo. Kumeanza kujitokeza mtindo wa raia wa nchi zingine kuingia nchini mwetu kama wawekezaji lakini badala ya kuwekeza wanaanza kufanya biashara ndogondogo kama kuuza maduka na hata mama lishe. Hali ni hatari sana ikiachwa iendelee Watanzania watakuwa wageni nchini mwao. Naiomba sana Wizara ihakikishe biashara ndogo zinafanywa na Watanzania tu na wanaokuja kuwekeza wawekeze kwenye biashara kubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali ya umeme nchini. Sasa hivi nchi yetu ina uhaba sana wa umeme. Wakati huohuo nchi yetu imebahatika kuwa na mkaa wa mawe mwingi sana. Naiomba Serikali kupitia Wizara hii ifanye kila iwezalo ili kutumia potential hii kubwa ya mkaa wa mawe ili kuzalisha umeme mwingi wa kutosha nchini na akiba ya kuuza nchi jirani. Jambo hili lifanywe kwa dharura. Sheria ya PPP imetungwa na kanuni zake tayari zimetoka kwenye gazeti la Serikali. Wizara inaweza kutumia sheria hii kuwatumia wafanyabiahsara kuzalisha umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. JASSON RWEIKIZA: Mheshimiwa Mwenyekiti, bei ya sukari. Hali inatisha, bei imepanda sana tena kiholela, kwa nini? Nina taarifa kuwa bei inapangwa kufuatana na nguvu ya soko. Nina taarifa pia kuwa waangalizi wa biashara ya sukari ni Bodi ya Sukari. Wadau wanasema kuwa Bodi hii imejaa wala rushwa, ndio maana hawadhibiti bei na wanatoa vibali vya kuagiza sukari kutoka nje kwa watu wachache ambao pia ndio walewale wenye viwanda. Hali hii haileti ushindani bali inachochea ukiritimba (monopoly), kwa hiyo hawa watu wanapanga bei watakayo. Mheshimiwa Mwenyekiti, Kampuni ya NICOL. Wanahisa hawajapata gawio tangu mwaka 2005 ilipoanzishwa. Wahusika ni walewale kina Idd Simba. Hawa wanajiita wazawa. Kampuni hii imeondolewa katika soko la hisa (DSE). Ni matapeli. Serikali kupitia Wizara hii isimamie maslahi ya wanahisa wa NICOL.

MHE. DIANA M. CHILOLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kutumia nafasi hii kwa njia ya maandishi kuwapongeza Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Dkt. Cyril Chami, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Lazaro Nyalandu, Katibu Mkuu pamoja na watendaji wote walioshiriki kuandaa Bajeti hii nzuri yenye lengo la kuinua uchumi wa nchi kupitia viwanda na biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile napenda kuipongeza Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara kwani imetambua kazi nzuri inayofanywa na Wizara pamoja na hotuba ya Bajeti ya Wizara hii. Nina imani ushauri uliotolewa na Kamati utazingatiwa na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninapenda kuikumbusha ahadi ya Serikali iliyotolewa tangu miaka mitatu iliyopita na aliyekuwa Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Dkt. Mary Nagu kuwa Serikali itatuletea mwekezaji ambaye atajenga kiwanda cha kusafisha mafuta mkoani Singida. Ninasikitika kusema kuwa mpaka sasa bado hakuna mwekezaji yeyote aliyepelekwa na Serikali kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta ya alizeti ili yaweze kufikia kiwango cha kuingia kwenye soko la Kimataifa, je, ni lini mwekezaji ataletwa? Nasubiri majibu ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kiwanda cha ngozi cha Sepuka, napongeza juhudi za Halmashauri ya Wilaya ya Singida pamoja na wananchi kwa kujenga kiwanda cha kuwamba ngozi nilichokitaja hapo juu. Ni ukweli usiofichika kiwanda hiki kinafanya kazi nzuri sana za kuwamba ngozi vizuri pamoja na kutengeneza vitu mbalimbali mfano viatu, mikanda ya suruali, mikoba na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba wataalam wenye taaluma zaidi waletwe ili kuja kuwapa taaluma zaidi wataalam waliopo kwa lengo la kuongeza uzalishaji wa kiwanda. Ninaomba vifaa viongezwe ili kuboresha uzalishaji zaidi. Pia ninaomba kama haitawezekana kupeleka wataalam basi wataalam wetu wapelekwe kozi ili kupata ujuzi zaidi kwa lengo la kukuza uzalishaji wa kiwanda hicho. Ninaomba Serikali iwatafutie soko la bidhaa zinazozalishwa kwenye kiwanda hicho ili tuachane na tabia ya kusubiri wiki ya Nanenane au wiki ya Sabasaba kila mwaka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda cha maziwa Sepuka katika Kijiji cha Mmsungua, Halmashauri ya Singida, napenda kuipongeza Halmashauri ya Singida kwa kujenga Kiwanda cha maziwa fresh kwa kushirikiana na wananchi ili kusaidia wafanyabiashara wa maziwa kupata kiwanda cha kutengeneza maziwa fresh pamoja na kuhifadhi kitaalam yasiyoharibika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninaomba Serikali ikiboreshe kiwanda hiki ili sasa kiweze kusindika maziwa na kuyauza kama viwanda vya Mara na Tanga. Ninasubiri maelezo ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wataalam wa kiwanda hiki cha maziwa wapewe taaluma zaidi.Ninaomba Serikali kuongeza vifaa katika kiwanda hiki cha maziwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ukweli usiopingika kuwa asali inayopatikana Mkoa wa Singida ni ya kiwango cha juu Afrika nzima, ni sababu zipi asali hii inakosa soko? Ninaomba Serikali kusaidia kupatikana soko la asali ya Singida ili wazalishaji wa asali waweze kupata moyo wa kuzalisha zaidi? Nasubiri majibu ya Serikali tafadhali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kushuka kwa bei ya zao la pamba nchini, napenda kuieleza Serikali kuwa kati ya Mikoa inayolima zao la pamba ni pamoja na Mkoa wa Singida. Ni bahati mbaya sana kila mwaka uzalishaji wa zao la pamba Mkoani Singida unazidi kushuka tatizo linalosababisha wakulima wa zao la pamba kupunguza juhudi za kulima zao la pamba ni pamoja na bei kushuka kila mwaka. Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuiomba Serikali kuangalia uwezekano wa kufidia shilingi mia nne zinazopungua ili wakulima wapate faida kutoka shilingi 700 hadi shilingi 1,100. Hii itawatia moyo sana wakulima wa zao la pamba nchini kote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Meneja wa SIDO Mkoa wa Singida kwa juhudi zake kubwa za kuwasaidia wajasiriamali wa Mkoa wa Singida kwa kuwapa semina mbalimbali za kujifunza mambo mbalimbali ya uzalishaji kwa kutafuta wahisani mwenyewe. Vilevile ambavyo anajitahidi kusafirisha wajasiriamali kwenye maonyesho mbalimbali Dar es Salaam na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, SIDO ya Singida inafanya kazi kubwa sana hivyo naomba aongezewe fedha ili aweze kusaidia zaidi wajasiriamali wa Singida wakiwemo wanawake na vijana kwa kutoa mafunzo mbalimbali pamoja na kuwakopesha ili waweze kuendesha miradi yao kwa lengo la kuinua vipato vya familia. SIDO imekuwa karibu sana na wananchi. Vilevile iweze kununua bidhaa mbalimbali za wajasiriamali mfano Visonzo na kwenda kuuza kwenye masoko ya Kitaifa na Kimataifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumaliza kwa kuunga mkono hoja nikiwa na imani Mheshimiwa Dkt. Chami na Mheshimiwa Nyalandu watajibu hoja zangu ili nisiwasumbue kwenye vifungu. Mungu awatie nguvu, afya na mshikamano ili waweze kutekeleza majukumu yao vema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wajasiriamali wengi hususani wanawake wanafanya kazi kubwa sana ya kutengeneza bidhaa mbalimbali za kuuza ili kupata fedha za kuinua vipato vyao kwa lengo la kuondokana na umaskini na kwa kuwa wajasiriamali hawa hushindwa kwenda kushiriki kwenye maonyesho mbalimbali mfano Sabasaba Dar es Salaam, Nanenane Dodoma ninaiomba Serikali kuwawezesha wajasiriamli hawa nauli pamoja na posho ya kujikimu kama anavyofanya mke wa Rais Mstaafu Mama Anna Mkapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii itasaidia sana kutangaza vipaji na kazi nzuri zinazofanywa na wajasiriamali wakiwemo wa Mkoa wa Singida. Naomba nipatiwe majibu na Waziri au Naibu Waziri wakati anajibu michango ya wabunge.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la wageni kutokupewa leseni za kufanya biashara ndogo ndogo, napenda kuungana na Wabunge wenzangu waliochangia hoja ya kuitaka Serikali kuacha utaratibu wa kuwapa leseni wageni kutoka nchi mbalimbali mfano Wachina kufanya biashara ndogo ndogo kwani wanawanyima fursa Watanzania wanaofanya biashara hizo kwani wanavunjika moyo na kuendelea kudidimia kiuchumi. Ninasubiri maelezo ya Serikali inapotoa majibu kutambua mchango wangu pamoja na maoni yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu kujenga kiwanda cha kusindika nyama na machinjio ya kisasa, napenda kuikumbusha Serikali kuwa kati ya mikoa inayofuga mifugo mingi ni pamoja na Mkoa wa Singida kwani ni mkoa wa nne. Hivyo ninaishauri Serikali kutafuta mwekezaji wa kujenga kiwanda cha kusindika nyama za kopo na kadhalika pamoja na kujenga machinjio ya kisasa ili kuwasaidia wafugaji kupunguza mifugo yao pia kuacha kusumbuka na kazi ngumu ya kusafirisha mifugo inayonunuliwa kwenye minada. Ninasubiri maelezo ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, narudia tena kuunga mkono hoja na kuwatakia kazi njema nikizingatia Katibu Mkuu wa Wizara hii ni mama.

MHE. AGNESS E. HOKORORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri wa Viwanda na Biashara kwa hotuba nzuri yenye matumaini kwa Watanzania. Napenda kuchangia hotuba hiyo kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, uharakishwaji wa ujenzi wa Kiwanda cha Mbolea Mtwara, naomba Serikali suala hili lipewe kipaumbele ili kuweza kuondoa nchi yetu katika kutegemea pekee mbolea ya Minjingu ambayo hata hivyo haitoshelezi mahitaji ya Watanzania. Malalamiko ya pembejeo hii yamekuwa mengi, ni dhahiri kuwa haitoshi. Kwa kuwa sasa upatikanaji wa gesi ya Mnazibay ni kwa uhakika malighafi ya uzalishaji ya mbolea hiyo utakuwepo bila mashaka, ni vema Serikali ikachukua hatua za haraka za kuharakisha ujenzi wa kiwanda ili tatizo la mbolea ya Minjingu ambayo pia haitumiki katika aina zote za udongo kutokana na suala la PH na acidity.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la uboreshaji wa bidhaa ili kuongeza bei badala ya kuuza bidhaa ghafi, Serikali ione namna ya kuimarisha viwanda vya korosho na kuwezesha ubanguaji wa korosho badala ya kuuza koroshi ghafi. Mkoa wa Mtwara unaongoza katika uzalishaji wa korosho hata hivyo ilivyo sasa korosho inauzwa kwa shilingi 1,600/= kwa kilo ikiwa mbichi ambapo ingebanguliwa ingeweza kuuzwa shilingi 35,000/= kwa kilo. Tanzania tunauza korosho ghafi kwa thamani ndogo sana badala ya Tanzania kuuza korosho iliyobanguliwa ambapo pia thamani yake itakuwa imepanda. Serikali ina mpango gani wa kuhakikisha viwanda vya korosho vya Mtwara vinasimamiwa na Serikali badala ilivyo sasa kuna viwanda vya watu binafsi/wawekezaji ambapo pia hawawezi kununua korosho yote.

Aidha, viwanda vya kubangua Korosho vya Tandahimba vinavyomilikiwa na wanaushirika/kikundi ambavyo pia zana zake ni ndogo sana na za kizamani mfano wanatumia mashine ya mguu ya kubangua, Serikali ina mpango gani wa kuwaongezea nguvu wakulima hawa hasa wanaushirika walioanzisha pale Kitame – Tandahimba?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali kupitia Wizara hii inahakikishaje viwanda vinavyobangua korosho Mkoani Mtwara wanapata bidhaa bora? Mamlaka zinazosimamia Usalama Mahali pa Kazi (OSHA) hawafanyi kazi zao vizuri kama nilivyohoji katika Wizara ya Kazi na Ajira, kwa namna hiyo viwanda vyetu vitawezaje kuzalisha bidhaa bora? Wafanyakazi wake watawezaje kufanya kazi katika viwanda hivyo bila wao kupata athari za kiafya? Katika viwanda vya kubangua korosho hakuna vitendea kazi kabisa, pamoja na kwamba viwanda hivi si vya Serikali lakini ni jukumu la Serikali kuhakikisha viwanda vilivyopo vinalinda walaji na wafanyakazi kwa ujumla ili bidhaa inayotolewa iwe bora pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sasa katika viwanda vya korosho Mtwara wanabangua korosho hawana gloves, hawana musks na wanabangua kwa mikono wakiwa wamepaka mafuta mkononi kizamani sana na hata wale wanaochemsha korosho hawana hata cha kufunika usoni na ikumbukwe kuwa moshi wa mafuta ya korosho huwezi kuuvumilia kwa dakika kadhaa kwa kuwa unapalia sana, kiafya pia sio sahihi lazima kutakuwa na madhara kiafya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.

MHE. DKT. LUCY S. NKYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Watendaji wote wa Wizara ya Viwanda na Biashara kwa hotuba nzuri. Ninawatakia utekelezaji mzuri na wenye mafanikio wa Bajeti ya 2011/2012. Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nitoe rai zifuatazo kwa nia ya kuboresha. Napenda kumtaarifu Mheshimiwa Waziri na Naibu Waziri kwamba wakulima wa Wilaya ya Morogoro Vijijini wanazalisha viungo vingi sana aina ya karafuu, abdalasin (cinamon), hiliki na tangawizi. Tunaomba tutafutiwe soko la uhakika na lenye neema zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba kusaidiwa kusindika matunda hususani mananasi, machungwa na embe, ikiwezekana Shirika la SIDO lisaidie kutoa mafunzo pamoja na kukopesha vitendea kazi kama solar dryers kwa ajili ya kukausha matunda na mbogamboga.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwanda pekee cha kusindika matunda katika eneo la Mkambarani kimefungwa. Kama huyo mwekezaji ameshindwa basi auze ili vijana wapate ajira na wakulima waweze kuuza matunda yao. Tunaomba Wizara iangalie uwezekano wa kuanzisha Special Economic Zone katika Wilaya ya Morogoro Vijijini ili na sisi vijana wetu wapate ajira na Halmashauri ipate kuongeza mapato yake.

Kwenye uwanda wa tambarare wananchi wanalima pamba nyingi, mpunga na mahindi. Kwanza soko la mazao haya siyo nzuri, tunaomba Wizara kupitia vyombo husika itusaidie kutafuta wawekezaji wa kusindika mazao haya. Hatua hii itasaidia kuhamasisha uzalishaji zaidi.

Naomba Wizara iwaelekeze/kuhamasisha wasindikaji wa maziwa kuanzisha vituo vya ununuzi wa maziwa kwa wafugaji wa Tarafa ya Ngerengere na Mvuha. Maziwa ni mengi sana yanayoharibika kwa kukosa soko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba SIDO iangalie namna ya kuwasaidia vijana wanaomaliza sekondari na vyuoni ili waweze kujiajiri wenyewe kwa kutumia rasilimali zilizopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. RUKIA KASSIM AHMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nimpongeze Waziri wa Viwanda, Biashara na Masoko pamoja na Naibu Waziri wake kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi napenda nizungumzie kuhusu ubora wa bidhaa zinazotengenezwa hapa kwetu Tanzania. Bidhaa hizi zinakuwa chini ya viwango na pia zinakuwa ghali sana kuliko hata zile zinazotoka nje ya nchi, hivyo basi nashauri Serikali ifanye utaratibu wa kuangalia hizi bidhaa zinazotengenezwa na viwanda hapa nchini kwetu. Ni sababu gani zinazosababisha kuwa ghali kiasi hiki kwa mfano saruji, inayotengenezwa Tanzania ni ghali zaidi kuliko inayokuja kutoka Oman. Saruji ya Oman ina ubora zaidi kuliko inayotengenezwa hapa kwetu Tanzania, ni vyema Serikali ikaangalia tatizo ni lipi linayosababisha hali hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia Serikali iweke viwanda vya kusindika vyakula kwa mfano maziwa, nyama, samaki, matunda na hata ngozi. Hali hii itapelekea wakulima wetu kupata masoko ya kuuzia mazao yao na wataondokana na umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna baadhi ya viwanda vinatumia kemikali katika kufanya shughuli zao, maji yanayotiririka katika viwanda hivi basi yanaleta madhara kwa binadamu. Naiomba Serikali iliangalie sana suala hili kwani maji haya yanafika katika mabonde yaliyo karibu na viwanda hivi na watu wetu wanalima mboga mboga ambazo zinaweza zikaleta madhara kwa binadamu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naishauri Serikali kuwa viwanda vijengwe kando kidogo na maeneo wanayoishi watu ili moshi unaotoka katika viwanda hivi unaoweza kaleta madhara kwa binadamu usiwafikie.

MHE. EUSTACE O. KATAGIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri na Naibu wake na watendaji wote kwa kuandaa Bajeti nzuri na kuwakilisha vizuri. Nawapongeza kwa uendeshaji na utendaji mzuri katika Wizara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu bidhaa zetu wenyewe, wananchi wahamasishwe kupenda na kuthamini bidhaa zetu zinazozalishwa hapa nchini ili soko na bidhaa zetu lianze hapa nchini. Bidhaa zisizo halisi (fake), tunashukuru jitihada ambazo tayari zinafanywa, lakini bado jitihada zaidi zinatakiwa kushughulikia suala hili. Tatizo hili pia linaruhusu unfair competition kwa bidhaa zetu hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wafanyabiashara wa nje, kuna tatizo la watu kutoka nje ambao wanafanya biashara hapa nchini bila uhalali wa kufanya hivyo. Tunataka hatua zichukuliwe ili hizi biashara wafanye Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. KOMBO KHAMIS KOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kusema kwamba Wizara ya Viwanda na Biashara ni miongoni mwa Wizara inayotegemewa sana na Watanzania katika nyanja zifuatazo:-

(i) Kutoa ajira kwa vijana wa Tanzania; na

(ii) Uzalishaji kwa maendeleo ya Taifa

Mheshimiwa Mwenyekiti, kiwango cha fedha kilichotajwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa ajili ya maendeleo ambazo ni kwa ajili ya mwaka wa fedha 2011/2012 na ambacho ni kiasi cha shilingi 27,676,129,000/= kiasi ambacho kimetajwa kwamba ni pamoja na Taasisi zake hakitoshi na kwamba hakuna maendeleo yoyote yatakayotokana na mapinduzi ya miradi ila ni kuendelea kudorora kwa uchumi wa nchi pamoja na kuwakosesha vijana ajira kutokana na kukosekana kwa miundombinu ya kuwaendeleza vijana katika kuwapatia ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kima cha shilingi 30,052,589,000/= kwa ajili ya Matumizi ya Kawaida na kuendeleza sekta ya viwanda, viwanda vidogo na biashara ndogo, biashara na masoko kiasi hicho hakiwezi pia kuleta mapinduzi ya viwanda, viwanda vidogo vidogo, biashara ndogo ndogo biashara na masoko kutokana na upana wa sekta ya viwanda biashara na masoko. Vilevile kima hicho kamwe hakitoweza kuwapatia vijana wa Kitanzania katika kuwapatia ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina wajibu wa kuhakikisha kwamba Watanzania wanapewa upendeleo katika sekta ya viwanda, viwanda vidogo, biashara ndogo ndogo ili waweze kupata ajira zitakazowaendeleza kupata riziki halali na kuwapa uwezo wa kuzishughulikia familia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizungumzia suala zima la masoko linatokana na wazalishaji wa mashambani, mazao ya biashara kama vile korosho, kahawa, chai na pamba hawapatiwi pembejeo na kwa wale ambao wanaendeleza kilimo hicho wanavunjwa moyo na bei zinazotolewa na wanunuzi na Serikali kuunga mkono matakwa ya wanunuzi wa mazao hayo ya wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ina wajibu wa kuhakikisha kwamba wakulima na wafugaji wanaendelezwa ili biashara zao ziweze kuwapatia tija. Wananchi wana mifugo ya kutosha bei ya nyama ktika nchi ya Congo ni mara tano zaidi ya bei ya Dar es Salaam kwa nini wananchi wasipewe fursa ya kusafirisha mifugo yao nje ya nchi ili waweze kujipatiia maendeleo endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali isikubali kabisa kuingia ubia na Mashirika na Taasisi ambazo hazina malengo ya kuwaendeleza wananchi katika kuwaletea maendeleo na hatimaye wanatumia mbinu katika kuwakandamiza wananchi wa Tanzania katika kuwakosesha maendeleo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mlahaka uliopo baina ya Serikali na wakulima upo karibu kimaneno zaidi kuliko kivitendo, ni wajibu wa Serikali kuhakikisha kwamba imerejesha mahusiano yake ya karibu zaidi kwa wakulima kivitendo kuliko maneno ili iweze kuwaendeleza na kuzalisha kwa wingi lakini pia kuwapatia masoko ya kuuzia biashara zao na ambazo zitakuwa na tija.

MHE. SAID MUSSA ZUBEIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimpongeze Waziri na Naibu Waziri pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa umahiri wao wa kuandaa na hatimaye kuiwasilisha Bungeni Bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Bajeti ni nzuri na inakidhi haja ila makosa madogo madogo ya kibinadamu hayaachi nami acha nijielekeze huko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania hivi sasa tuna tatizo kubwa la umeme na kwa kiasi kikubwa suluhu ipo kwenye Wizara hii kwa hivyo naiomba Serikali itafute shilingi bilioni166 kwa ajili ya miradi ya Ngaka na Mchuchuma ambapo ikifanikiwa itawezesha upatikanaji wa MW 600 ambapo umeme huu utakuwa na uhakika zaidi na rahisi zaidi na kama fedha hakuna basi Serikali ifanye mazungumzo na NSSF ili waingie ubia na itakuwa fahari zaidi kwani hii Taasisi ni ya kwetu wenyewe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna mradi wa umeme wa upepo hapa mimi ndio nashangaa kabisa, huu mradi pesa tayari zipo kutoka Exim Bank ya China, kibali cha Serikali kutoka Hazina tayari watu wa NDC wanakwenda na kurudi TANESCO kila siku ili waonane na viongozi kwa marekebisho ya mwisho ili mradi uanze. Wala hauhitaji pesa la kushangaza mashirikiano hayapo kutoka TANESCO je, huko TANESCO kuna kiasi gani? Toka Mei hadi leo hii jambo halijakamilika na huu ndio umeme wa bei rahisi kulikoni hata huu tunaotumia, mimi naona bado tunahitajika kuchunguza watendaji wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa SIDO kuwa na mkakati wa makusudi wa kuviinua na kutoa mtaji wa kutosha ili tuweze kuinua ujuzi na ajira kwa vijana. Naishauri Serikali kupitia Wizara hii iyape kipaumbele maeneo mawili haya kwa hivi sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Serikali kwa uanzishaji wa bar codes hii itawakomboa wafanyabiashara na nchi yetu kutambulika kibiashara Kimataifa na mategemeo yangu sasa idadi ya mauzo ya nje yataongezeka kwani sasa hatupitii Afrika Kusini wala Kenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante.

MHE. FAIDA MOHAMED BAKAR: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa kazi nzuri anayoifanya kwa kushirikiana na Mheshimiwa Naibu Waziri wake, kwa kweli Wizara hii imepata Mawaziri watendaji. Naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia hoja hii kwanza kuhusu ufujaji wa viwanda. Kwa kuwa maendeleo ya nchi yoyote (Taifa lolote) yanapatikana kutokana na viwanda, kwa sababu ya malighafi iliyonayo, ni vyema kutumia malighafi tulizonazo kama ngozi, matunda, madini, pamba, katani na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutengeneza vifaa (mali) tofauti hapa nchini kuliko kuuza malighafi hizo kwanda nje ya nchi. Hii inasababisha mauzo hayo yawe na mapato madogo sana na nchi kukosa mapato ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ikifufua na kuboresha viwanda mbalimbali wananchi watapata ajira katika nchi yao kuliko sasa wanavyopata taabu ya kuhangaika kutafuta ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naishauri Serikali iweze kufungua viwanda vilivyokufa na kuanzisha viwanda vingine vipya ili nchi yetu ipate mapato ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja.

MHE. ABDUL J. MAROMBWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nianze kuchangia hotuba hii katika eneo la viwanda vidogo vidogo ambavyo viko chini ya SIDO. Kwa muda mrefu nchi yetu inauza bidhaa zake nyingi zikiwa ni ghafi (row). Hali hii husababisha bidhaa nyingi kuuzwa kwa bei ndogo na kuwafanya wakulima wasinufaike na mazao wanayoyalima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Rufiji ni miongoni mwa Wilaya ambazo zinalima mazao mengi kwa kuwa ardhi yake ina rutuba ya kutosha. Miongoni mwa mazao hayo ni korosho. Tunaishukuru sana Serikali kwa kuanzisha mpango wa stakabadhi ghalani ambao kwa kiasi fulani umesaidia kupandisha bei ya zao hili. Pamoja na wakulima wa korosho kwa kiasi wananufaika, lakini bado kuna hasara kubwa sana inayotokana na zao hili kuuzwa likiwa ghafi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namuomba Waziri alielekeze Shirika la Viwanda Vidogo Vidogo liende kuendesha mafunzo ya kubangua korosho katika Kata za Bungu, Mjawa, Kibiti, Mlanzi Ruaruke, Dimani na kadhalika ili kupitia vyama vyake vya ushirika vya msingi viweze kuhamasika kununua viwanda vidogo vidogo. Vyama hivi vimejipanga vizuri ila tatizo lililopo ni kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu namna ya uendeshaji wa viwanda vidogo vidogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine ni masoko kwa wakulima wa mazao mbalimbali. Ni vizuri sana kwa Serikali kwenda katika maeneo ya vijijini wakishirikiana na watendaji wa Halmashauri kuwatafutia wakulima masoko kwa mazao yao wanayoyalima. Kwa upande wa Wilaya Rufiji matunda mengi ambayo yanalimwa hayana masoko ya uhakika hasa mananasi, maembe na kadhalika kwa kufanya hivyo wakulima watahamasika na hatimaye kuongeza uzalishaji wa mazao wanayoyalima. Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu Kiwanda cha Sukari, Mtibwa kwa muda mrefu wakulima wengi wa miwa (outgrowers) wanaozunguka kiwanda hiki, kwa kiasi kikubwa hawanufaiki na mazao wanayoyalima kutokana na mmiliki wa kiwanda hiki kutowajali wakulima hawa. Mmiliki huyu ambaye amepewa kiwanda hiki na Serikali kwa asilimia mia moja haonyeshi nia yoyote ya kutaka kukiendeleza kiwanda na badala yake uzalishaji unazidi kupungua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa hakuna utaratibu wowote wa kuvuna miwa kwa mwaka huu 2011. Je, Serikali inatoa tamko gani kwa wakulima hawa ambao wengi wamekopa pesa benki hasa CRDB na wanatakiwa warejeshe kwa wakati? Je, kiwanda kitaanza uzalishaji wa sukari lini? Je, kwa nini Serikali isiwe na hisa katika kiwanda hiki ili wakulima nao waweze kupata mahali pa kusemea? Kwa sasa wakulima hao hawana sauti yoyote kwa kiwanda hiki ambacho kilikuwa mali ya Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala lingine ni kuhusu kiwanda cha kusindika nyama cha Ruvu. Kiwanda hiki kilipoanza kujengwa kiliwekewa jiwe la msingi na Rais Jakaya Mrisho Kikwete. Ahadi iliyotolewa na Mheshimiwa Waziri wa Mifugo wakati huo ni kuwa kiwanda kingeweza kuanza kazi muda mfupi sana. Jambo la kushangaza ni kuwa hadi sasa hakuna jambo lolote linaloendelea kwenye kiwanda hiki na hata kama kinaendelea kujengwa speed inayoenda nayo ni ndogo sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali/Waziri leo alithibitishie Bunge hili ni lini ujenzi huu utakamilika na ni lini kiwanda hiki kitaanza kazi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. JENISTA J. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa kwa muda mrefu Wizara imekuwa ikiwapa matumaini wananchi wa Jimbo la Peramiho kuhusu ujenzi wa Soko la Kimataifa mpakani mwa Songea na Msumbiji, tunaomba msaada wa utekelezaji wa hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la sukari ni sugu, Jimbo la Peramiho wameanza kilimo cha miwa ya sukari, ninaomba muongozo wa Serikali katika kusaidia uanzishaji wa viwanda vidogo ili kupunguza tatizo hili. Kuacha Halmashauri kufanya haya yote hawawezi kwa kuwa hupewa ukomo wa Bajeti na mahitaji ni mengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. MHE. GOSBERT B. BLANDES: Mheshimiwa Mwenyekiti, niruhusu nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na watendaji wote wa Wizara hii kwa kazi nzuri wanayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, SIDO inafanya kazi nzuri kwa Taifa hili lakini wanakwamishwa na ufinyu wa Bajeti. Fedha iliyotengwa kwa ajili ya SIDO safari hii ni kidogo sana na haziwezi kuisaidia kufanya kazi zilizokusudiwa. Serikali iongeze fedha katika Bajeti hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile SIDO Kagera imedorora kiasi kwamba ni kama haipo. Tatizo ni lilelile la uhaba wa fedha. Ni lini SIDO Kagera itaamka kwa manufaa ya wananchi wa Kagera ikiwemo Wilaya za Karagwe, Ngara, Biharamulo, Bukoba Vijijini, Muleba, Nkenge, Chato na Bukoba Vijijini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu inasifika kwa ufugaji wa ng’ombe, mbuzi, kondoo, nguruwe, kuku, sungura na bata na ni ya tatu Afrika nzima. Ajabu hatuna kiwanda cha kusindika nyama nchi nzima. Hii ni aibu wa Taifa hili changa. Ni hujuma kwa wafugaji wote nchini. Mifugo yetu tangu tupate Uhuru hadi leo tunauza kwa minada yaani bei ya kukadiria badala ya kuuza kwa kilo. Utaratibu huu unawapunja wafugaji na kuwanufaisha wanunuzi. Wizara ianzishe haraka sana ununuzi wa kutumia vipimo vya kilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ni lini itaamua kuwajali wafugaji wetu? Hata viwanda vya maziwa, wafugaji hapa nchini wanamwaga maziwa kwa sababu hatuna soko. Serikali ianzishe Kampuni ya Maziwa ya Taifa la baadaye iuze hisa za Kampuni hiyo kwa wazawa hata wageni. Serikali imelala usingizi katika suala zima la mazao ya mifugo. Serikali iamke leo siyo kesho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahadi ya Serikali kujenga kiwanda cha nyama Kyaka – Kagera inatekelezwa lini? Hii ni ahadi ya siku nyingi tangu Bunge lililopita. Serikali ifanye kila linalowezekana kiwanda hiki kianze kazi haraka iwezekanavyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu soko la AGOA, sisi Wabunge tunataka tujue orodha ya vitu vyote vinavyouzwa katika soko la AGOA ili tuwasaidie, tuwaelimishe wananchi tunaowaongoza na Wabunge wote tuelimishwe vizuri ili tuwe walimu wa wananchi wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, bei ya Kahawa Mkoani Kagera hasa Wilaya ya Karagwe ipo chini ni kati ya shilingi 800 hadi 1,000/=, nchi jirani ya Uganda wananunua Kahawa hii toka Tanzania kwa shilingi 3,000/= hadi 5,000/=. Je, Serikali inalisemea vipi tatizo hili? Wakulima wetu wanaibiwa na wanunuzi wa Kahawa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la ndizi linazaliwa hapa nchini hasa Karagwe, Mbeya, Kilimanjaro na Arusha. Sisi wananchi wa Karagwe tutafutiwe masoko ya Kimataifa ya kuuza ndizi zetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania inauza kinywaji cha Konyagi Kenya na Kampuni ya Azam inauza unga Kenya, nazipongeza kampuni hizi. Kenya inaingiza bidhaa hapa nchini zaidi ya 300. Tatizo ni nini? Serikali isaidie.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. PHILIPO A. MULUGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi natoka Chunya Jimbo la Songwe, sehemu iliyo na kilimo na uvuvi katika Ziwa Rukwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upande wa kilimo, wakulima wanalima alizeti, karanga, ufuta na mahindi lakini hakuna soko, Serikali haijawatafutia soko la kudumu na badala yake wanauza rejareja na kulanguliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vijana wa Jimbo la Songwe wanavua samaki Ziwa Rukwa, wanatoa samaki wengi ila hawana soko la uhakika, je, Serikali haioni haja ya kujenga kiwanda cha kusindika samaki na nyama kwa vile Chunya kuna zao la ng’ombe sana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itoe ufafanuzi wa zao la pamba kutolimwa katika Wilaya ya Chunya kwani tangu mwaka 1997 Serikali ilipotangaza stop ya kulima pamba Bonde la Songwe Wilayani Chunya mpaka leo wananchi wanauliza msimamo wa Serikali kuhusu stop ya kutolima pamba, kukiwa na visingizio eti kuna mdudu wa zao la pamba wakati zao hilo linalimwa nchini Malawi takribani kilomita 200. Je, huyo mdudu mbona Malawi hayupo?

Je, Serikali ni lini itarudia tena kutafiti mdudu huyu ili warudishe zao la pamba kwa wakulima wa Chunya?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. BALOZI SEIF ALI IDD: Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na malalamiko mengi miongoni mwa wananchi kuhusu Wachina wanaofanya biashara za Kimachinga pale Kariakoo, biashara ambazo zingeweza kufanywa na Watanzania wenyewe. Kumekuwa na mapendekezo kwamba Wachina hao wasihamishwe kufanya biashara za aina hiyo au wanyimwe leseni. Bila shaka Serikali inalitafakari suala hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na tafakari hiyo ya Serikali na hatua ambayo inafikiria kuchukua, ningependa kutoa tahadhari kwamba suala hili lichukuliwe kwa busara kubwa. Ningependa ieleweke kwamba kule China, Jiji la Guanzhan wapo Watanzania wengi wanaofanya kazi ambazo zinaweza kufanywa na Wachina wenyewe, kazi hizo hizo za Kimachinga pamoja na kazi za mama lishe na Serikali ya China haijawabugudhi Watanzania hawa na wananchi wengine kutoka nchi za Kiafrika. Wanafanya kazi zao kwa njia ya amani na wanaendesha maisha yao vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, na hatua ambayo Serikali inakusudia kuchukulikwa dhidi ya Wachina hao, lazima hatua hizo zichukuliwe kwa uangalifu maana hatua kama hizo zitaweza kuchukuliwa na Serikali ya China dhidi ya Watanzania. Kama Serikali itaamua kuwafukuza na Watanzania, nao watafukuzwa kama kuwanyima leseni na Watanzania wafanyiwa hivyo hivyo. Hatma ya hatua zote hizo ni kuzorotesha uhusiano baina ya nchi zetu mbili, uhusiano ambao umekuwa mzuri miaka nenda miaka rudi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naisihi sana Serikali yetu ichukue tahadhari kubwa katika suala hili. Kitu ambacho tunaweza kukifanya kama itakuwa ni lazima ni kuzuia influx ya Wachina kuingia nchini kwa kuzingatia population ya China.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. SELEMANI S. JAFO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza Wizara kuja na mikakati ya kukuza uchumi wa nchi yetu kwa kutumia biashara na masoko.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara kufanya yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha KIBRICO na STAMICO vilivyopo Wilayani Kisarawe vimebinafsishwa. Kwa bahati mbaya mitambo yote imehamishwa na viwanda havifanyi kazi tena. Hii inasikitisha sana. Naiomba Serikali ivirejeshe viwanda hivi Serikalini na kuviboresha ili viweze kuleta ajira kwa vijana wanaoishi Kisarawe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Kisarawe ipo karibu sana na Jiji kuu la biashara yaani Dar es Salaam. Pia Kisarawe kunazalishwa matunda mengi sana aina ya machungwa, mafenesi na maembe. Naiomba Wizara iangalie uwezekano na kuleta viwanda vya kutengeneza juice ili matunda yanayozalishwa Kisarawe yapate soko la uhakika na kukuza ajira kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho napenda kuipongeza Wizara kwa kazi nzuri inayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.

MHE. SALOME D. MWAMBU: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nichangie Wizara ya Viwanda kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, mapinduzi ya viwanda yanategemea mapinduzi ya kilimo. Ili tuweze kutimiza azma ya Kilimo Kwanza lazima tuanzishe viwanda vya kutosha na kukarabati viwanda vyote vilivyotelekezwa mfano, Sungura Textile, Urafiki, Kilitextile, UFI na Zana za Kilimo Mbeya (ZZK).

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la SIDO lipewe fedha za kutosha ili lifanye kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi hii ili iweze kupata maendeleo ni lazima NDC iwezeshwe na ipewe fedha za kutosha.

MHE. YUSSUF HAJI KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, naanza kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kuniwezesha kuwepo ndani ya ukumbi huu wa Bunge nikiwa na uhai na uzima wa afya njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nichangie katika Wizara hii kuhusu wafanyabiashara wadogo wadogo. Wafanyabiashara wadogo wadogo ni wengi sana ndani ya nchi yetu ambao wanajitahidi sana kujinasua katika wimbi la umaskini na kujitafutia riziki ya halali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, changamoto wanazokumbana nazo ni nyingi sana. Kwanza mtaji mdogo, masoko, elimu ya biashara na usumbufu wa mgambo. Nashauri Serikali iwawezeshe wafanyabiashara wadogo wadogo kwa kupatiwa mitaji mizuri kwa biashara. Serikali ikopeshe wafanyabiashara wadogo kwa mikopo yenye riba nafuu na ambayo wanaweza kupata bila masharti magumu. Pia wapewe elimu ya biashara ili wafanye biashara kwa ufanisi mkubwa na wafanye biashara endelevu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jambo lingine wanasumbuliwa na askari wa mgambo hasa Wamachinga, wananyang’anywa bidhaa zao ovyo ovyo. Sasa hii humsaidii mfanyabiashara isipokuwa anadhalilika na ni hatari sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nazungumzia kuhusu viwanda ndani ya nchi yetu wakulima wanazalisha matunda mengi ambayo ni ya msimu, hayakai muda mrefu matunda ambayo yakikaa muda tu yanaharibika. Bahati mbaya hatuna kiwanda chochote cha kusindika matunda, mfano wa matunda ambayo tunayo ni mananasi, nyanya, machungwa na mengi mengineyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali iangalie kwa makini sana kuanzisha viwanda vidogo na vikubwa vya kusindika matunda. Tukifanya hivyo, vijana watapata ajira, tutauza nchi jirani tutapata pesa za kigeni na nchi itakuza pato lake kuliko kuacha matunda yakaoza bure bure.

Kuhusu Shirika la Ndege (ATC) ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania ni hasara kwa Taifa letu. Wafanyabiashara wengi wa nchi jirani wanatumia usafiri wa treni kuunganisha mizigo kutoka Bandari ya Dar es Salaam kupeleka katika nchi zao mfano, Rwanda, Burundi, Uganda na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokufanya kazi kwa ufanisi reli kumesababisha wafanyabiashara wa ndani na nje kukosa usafiri wenye uwezo wa kubeba mizigo kwa wingi na kwa bei nafuu. Tatizo hili limekosesha Taifa pato na kama haitoshi Watanzania wengi wamekosa ajira. Umakini unahitajika pamoja na usimamizi mzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vilevile kuhusu usafiri wa ndege kama unakuwa mzuri basi wafanyabiashara wanakuwa na nafasi nzuri kufanya biashara zao tena kwa muda muafaka. Ukosefu wa Shirika letu la Ndege kufanya kazi kwa ufanisi ni kupoteza ushindani wa biashara na pia Serikali kukosa mapato. Ni jukumu la Serikali kusoma mabadiliko ya wakati na kusimamiwa vizuri mashirika yote muhimu. Ahsante.

MHE. EUGEN E. MWAIPOSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchaniga kwa maandishi niliyotaja hoja ya Wizara ya Viwanda na Biashara, kwanza kwa kumpongeza Waziri, watendaji wote wa Wizara na Serikali kwa kutuletea Bajeti nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uzuri wa hoja/Bajeti naomba kwa niaba na uwakilishi wa wananchi wa jimbo la Ukonga nichangie kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uwezeshaji wa wafanyabiashara ndogo ndogo, Serikali imekuwa kila wakati inaonyesha dhamira ya dhati ya kuwawezesha wafanyabiashara wadogo wadogo, lakini ipo haja sasa ya kuhakikisha jambo hili linafanikiwa. Kwanza naishauri Serikali kuwawezesha wafanyabiashara hawa kuanza biashara kabla ya kulipa kodi. Katika utaratibu wa kuwakadiria wafanyabiashara kodi na kulipa kabla ya kufanya biashara inawadumaza na kuwakosesha fursa kutokana na mitaji yao midogo waliyonayo, uwepo utaratibu wa kuwaruhusu kuanza biashara baada ya kupata usajili na kufuatiliwa ili kulipa kodi baada ya kuonekana kama kweli kuna faida katika biashara hiyo. Hili linawezekana maana hata wawekezaji wanapewa muda kabla ya kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, upatikanaji wa usajili wa jina la biashara na leseni ya biashara. BRELA inafanya kazi nzuri ila naishauri kuhakikisha inakuwa na mtandao nchi nzima ili kuweza kutoa huduma ya usajili katika nchi nzima tofauti na ilivyo sasa kuwa ni lazima mtu aje hadi Dar es Salaam. Pia naishauri Serikali irudishe shughuli za utoaji wa leseni kwa BRELA ili kuondoa ukiritimba na usumbufu kwa wahitaji wa leseni hizo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wakati wa kuleta mrejesho Waziri anipatie majibu ya mambo hayo pamoja na matumizi mabaya ya eneo la Banana - Ukonga lililokuwa Hachari ya kutotolea vifaranga na kutolewa kwa mwekezaji kwa ajili ya shughuli hiyo na mpaka sasa eneo hilo limegeuzwa la kukodishwa watu kwa ajili ya baa ambazo ni zaidi ya baa 20 zilizopo katika eneo hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasilisha.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda na Biashara ni mhimili muhimu wa uchumi wa Taifa na kuboresha maisha ya wananchi. Matatizo ya uchumi katika Taifa letu ikiwemo mfumuko wa bei yanachangiwa na kupungua kwa uzalishaji katika nchi yetu ambapo tunagawiwa kuwa Taifa la wachuuzi. Uchumi wetu unakua kwa sekta chache hususan madini, utalii na mawasiliano ambazo zinachangia ukuaji wa uchumi mpana bila kuondoa umaskini wa kipato wa wananchi walio wengi. Viwanda na Biashara ni viungo muhimu vya kubadili hali hiyo kwa kuchangia pia muunganiko na nyuma na mbele (backward & forward linkage) na sekta nyingine ikiwemo kilimo. Hivyo, siungi mkono Bajeti hii mpaka Serikali ikubali kuongeza Bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara kutoka shilingi bilioni 57 mpaka kiwango kisichopungua jumla ya shilingi bilioni 114. Serikali izingatie kwamba viwanda ni kati ya vipaumbele vitano vya nchi yetu kwa mujibu wa Mpango wa Taifa wa miaka mitano ambapo kipengele A.1.1.2 kiwango kinachohitajika kwa viwanda pekee bila kuunganisha sekta zingine ni zaidi ya shilingi bilioni 300.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inapaswa kuweka mkazo katika kufufua viwanda na kuimarisha uzalishaji. Wabunge tupatiwe nakala ya tathmini ya mwaka 2007/2008 ya viwanda ambayo imeeleza bayana ukiukwaji wa mikataba ya ubinafsishaji ili Bunge liweze kuisimamia Serikali kuchukua hatua za haraka wakati uchambuzi wa kikosi kazi kilichoundwa mwezi Juni ukiendelea katika majumuisho Waziri atoe kauli kuhusu hatua ya viwanda vifuatavyo vilivyomo Jimbo la Ubungo ambavyo ubinafsishaji holela umesababisha uzalishaji udidimie na kupungua ajira hususani kwa vijana. Kiwanda cha Nguo cha Urafiki (naunga mkono maelezo ya Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani uk.10 na 11). Kiwanda cha Zana za Kilimo Ubungo (UFI) ambayo sasa imebadili jina na hata aina ya uzalishaji.

Pia mali zimeporwa ikiwemo kiwanja cha michezo cha Ubungo Shooting Stars, Kiwanda cha Ubungo Maziwa, Kiwanda cha Ubungo Garments na viwanda vingine nilivyovitaja kwenye swali langu la msingi kwa Wizara na mapendekezo yangu ya hatua za kuchukuliwa. Ukiangalia vigezo vya ufanisi wa viwanda kwa kutazama suala la kuongeza ajira kati ya mwaka 2006 mpaka 2010 wastani wa ongezeko la ajira kwa mwaka ni ajira 4,000 tu (uchambuzi wangu kuhusu takwimu za hali ya uchumi). Mpango wa Taifa unaelekeza wastani wa ajira 20,000 kwa mwaka, hivyo ufanisi wa Serikali kwa sasa ni 20% tu. Hii ni aibu miaka 50 baada ya Uhuru na ni bomu la wakati kutokana na ukosefu wa ajira kwa vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nyongeza ya Bajeti kwa Wizara ya Viwanda na Biashara ielekezwe katika kuongeza ruzuku kwenye Taasisi, Mashirika na Wakala kwa kuzingatia ufanisi (performance based allocation) hususani katika vifungu vifuatavyo; 1001 (Kasma 270300), 1003 (kasma 270700 na 270800), 2001 (kasma 270300), 2002 (kasma 270800), 4002 (kasma 270600). Ufanisi huu unahitajika pia kwa miradi ya maendeleo Vol. IV fungu 44 Kifungu 1003 (kasma 4920, 4933, 6260), kifungu 2002 (kasma 4938) na kifungu 4002 (kasma 4901). Nyongeza na ufanisi huo kwa mwaka 2011/2012, Wizara izingatie mahitaji katika Jimbo la Ubungo na Taifa kwa ujumla.

Mheshimiwa Mwenyekiti, EPZA iongezewe fedha kwa ajili ya fidia kwa wananchi na ukamilishaji wa Benjamin Mkapa SEZ ikiwemo ujenzi wa mfumo wa maji taka kama ulivyoelezwa kwenye mpango wa Taifa wa miaka mitano A.1.1.2 (uk. 112) pamoja na marekebisho niliyoyapendekeza wakati wa majadiliano ya mpango huo. SIDO iongezewe fedha kujenga mitaa ya viwanda vidogo ikiwemo katika Manispaa ya Kinondoni kuongeza ajira kwa vijana. NDC iongezewe fedha ya mchango wake kwenye uwekezaji, Serikali itoe kauli kuhusu taarifa kwamba Kampuni ya Sichuan Hongda C.L ya China kuwa haina fedha za kutosha. FCC, TBS, TFDA ili kuongeza nguvu katika udhibiti wa ubora wa bidhaa.

MHE. MARIAM N. KISANGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukosefu wa masoko kwa bidhaa za Watanzania ni tatizo. Watanzania tunalima matunda na hususani Mkoa wa Dar es Salaam tuna matikiti maji, bamia, nyanya chungu na mboga za aina nyingi lakini cha kushangaza tunasikia masoko kama Mlimani Shoprite na Shoprite ya Kamata wanaagiza mboga na matunda kutoka South Africa. Kama ni kweli sasa hawa Watanzania wakauzie wapi? Lakini pia hata samaki, Serikali inaagiza samaki toka nje. Hawa samaki wa Tanzania wanaenda wapi au tukauzie wapi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niishauri Serikali yangu kuwa tuangalie sana suala la masoko ya ndani kwa bidhaa zote. Hali si nzuri ukiuliza unaambiwa ni package yetu. Je, kweli tatizo ndio hilo? Lakini kama haitoshi katika migodi yetu ikiwemo ya Barrick wanaagiza vitu kama maji, maziwa, nyama, mboga za majani na matunda, uniform na marapurapu vyote vinatoka nje. Je, kwa mtindo huo soko la ndani si wanasaidia kuliua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali yangu sasa niishauri washirikiane na Wizara ya Nishati na Madini kuwabana wawekezaji. Naomba kama mikoa ya Nyanda za Juu wanashindwa kufanya hivyo basi ije mkoa wa Dar es Salaam badala ya Nairobi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli nikiwa kama Mbunge wa Mkoa wa Dar es Salaam ninayo masikitiko makubwa kwa kuingiliwa na wageni na hasa Wachina na Wakenya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wachina wamezagaa Kariakoo na sasa wamehamia Mwenge, Kawe, Mbagala, Buguruni, Tabata, Temeke na Keko. Inashangaza Wachina hawa wanakuja kufanya nini mitaani. Jibu wanafanya biashara ndogo ndogo ambazo zilikuwa zifanywe na Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada zinazofanywa na Wizara kupambana na hali hiyo bado tuongeze bidii ya kulinda masoko yetu na tutoe elimu kwa wananchi ya kuwatolea taarifa wageni hao. Ni ngumu Wizara kujua matatizo ya vitongojini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa nachangia juu ya Taasisi/Wakala zilizo chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wakala wa Vipimo wanafanya kazi kubwa na nzito kwa kuwahakikishia wananchi wanapata huduma ya usahihi na kipimo timilifu. Wakala wa Vipimo wana kazi kubwa ya kuzunguka Tanzania nzima. Lakini mara nyingi wanakuwa Dar es Salaam kutokana na ufinyu wa Bajeti. Naomba Wizara iwasaidie Wakala huu kuwajengea uwezo wa kifedha waweze kufanya kazi zao vizuri. Pia Wakala nao waongeze ubunifu wa miradi ambayo itawasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Wakala wawe kama zamani ikague na mizani midogo midogo ya nyama, samaki na vyakula kwa ujumla watu wanaibiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, TBS isaidiwe pia ifanye kazi yake vizuri na kupata maendeleo. Naiomba Wizara ikae na Wizara ya Nishati na Madini kazi za EWURA zifanywe na TBS. Kwa nini tunapeleka sampuli nje badala ya kujengea uwezo makampuni yetu. Kama tatizo ni maabara basi Serikali ijenge maabara ya kutosha. Fedha nyingi ya Tanzania inaenda katika Makampuni ya kigeni. Naiomba Serikali yangu sikivu ya CCM izingatie ushauri huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, SIDO ni rafiki wa wafanyabiashara wadogo na hasa wanawake. Tuangalie Shirika hili kwa maendeleo zaidi na nilitegemea leo nione mkakati wa SIDO. SIDO leo tungetakiwa iongeze matawi Kinondoni na Temeke nayo itusaidie hata kutoa elimu kwa vijana wetu wanaomaliza sekondari waweze kujitegemea. Serikali iangalie SIDO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, NDC nayo imeelekea kufa kwa kutojengewa uwezo na Serikali. Nafikiri NDC inataka kusaidia Serikali katika masuala ya umeme. Sasa Serikali yetu iwajengee uwezo wa kifedha Shirika hili tupate nafuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nitakuwa sijatenda haki Wilaya yangu ya Temeke nisipoisemea Sabasaba. Hawa wanafanya kazi nzuri, mradi huu unalipa sana, lakini bado tuzidi kubuni maonesho mengine makubwa badala ya kufanya mara moja kwa mwaka. Pia Serikali iangalie hayo mapato ya Sabasaba yasaidie kufanya maendeleo ya Sabasaba zaidi na kuboresha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishauri sasa kwa kuwa mji unakua tununue maeneo mengine Kinondoni na Ilala na Kigamboni, pia tuandae viwanja vya maonesho madogo madogo badala ya maonesho kama ya Syria kupeleka fedha Diamond Hall bado zije kwa TanTrade.

Pia sasa TanTrade itusaidie katika shughuli za maendeleo Wilaya ya Temeke na hasa maendeleo ya wanawake. Tunashukuru mmetupa elimu ya ujasiriamali sasa itusaidie vitendea kazi. Temeke ndio walinzi wa mradi huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nishukuru kwa kutupa ukumbi pale tunapokuwa na semina. Tunawaombea Taasisi hii ipate maendeleo. Japo yapo maendeleo makubwa miaka mitatu hii ukilinganisha na nyuma, majengo ni safi na yanapendeza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mheshimiwa Waziri, Mheshimiwa Waziri wangu mdogo kijana mchapakazi, Katibu Mkuu wetu mama mwenzetu. Tunajali na kuheshimu kazi zako. Hongereni sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja na napongeza Wizara kwa jitihada zake. Ahsante sana.

MHE: AZZA H. HAMAD: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kupata nafasi hii ya kuchangia kwa maandishi katika Wizara hii. Nimpongeze Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote kwa uandaaji wa Bajeti hii kwa kutoutambua Mkoa wa Shinyanga hata sehemu moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Shinyanga tuna mifugo ya kutosha lakini cha kushangaza Shinyanga hakuna kiwanda cha maziwa, hakuna kiwanda cha ngozi, hakuna kiwanda cha nyama. Ni kwa nini Serikali imeshindwa kuutambua mkoa huu na kupeleka viwanda hivi maeneo ambayo hayana mifugo? Hii inasikitisha sana kwani tunaishia kuwaambia wafugaji wapunguze mifugo wakati Serikali haijawasaidia chochote, hatuwatendei haki wafugaji hawa naomba wahusika mkae na mtubu kwa imani zenu na mtambue kama Mkoa huu hamjautendea haki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili ni ahadi ya Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho Kikwete alipotembelea Mkoa wa Shinyanga alisema tunatakiwa kutoka kwenye marobota ya pamba na kuwa na kiwanda cha nguo lakini sijaona popote kwenye hotuba hii, hivi kweli tunaendeleaje kumshawishi mkulima wa pamba aendelee kulima pamba wakati soko la uhakika la zao hili halipo? Tunatambua kabisa pamba hailiwi sasa tunawasaidiaje wakulima hawa ambao kwa mwaka huu kuna njaa kubwa katika Mkoa wa Shinyanga na bei ya pamba imeshuka, soko hakuna, sasa wananchi hawa mnataka waishi maisha ya namna gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itambue kwa dhati haiwatendei haki wakulima wa pamba na wanunuzi wetu wa pamba wa ndani, kwa sababu ndiyo zao kubwa la biashara tunalolitegemea lakini Serikali inalitambua hili ila haitaki tu kulitatua imebaki ni mipango tu ambayo haitekelezeki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho nimalizie kwa kusema siungi mkono hoja mpaka pale Mheshimiwa Waziri leo jioni atakapokuwa anajibu aniambie mipango mizuri, mikakati, tathmini na vinginevyo vitakwisha lini kwa Kiwanda cha Nyama cha Shinyanga na Kiwanda cha Nguo cha Shinyanga ili kupata soko la uhakika la zao la pamba. Nashukuru sana naomba majibu kwa wakulima wa pamba na wafugaji wanaohangaika kwa muda mrefu sasa.

MHE. DKT. BINILITH S. MAHENGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza napenda kuipongeza Serikali kwa kupata wawekezaji katika miradi wa Mchuchuma utakaofua umeme wa MW 600 na kuunganisha MW 300 na Gridi ya Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeangalia kwa makini sana hotuba ya Mheshimiwa Waziri, lakini cha kusikitisha hakuna mkakati wowote wa kujenga viwanda ili kuongeza thamani ya mazao yanayolimwa humu humu nchini. Mazao ambayo yanalimwa na Watanzania wengi hapa nchini ni pamoja na pamba, pareto, tumbaku, chai, kahawa na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sababu kubwa ya kuyumba kwa masoko ya mazao ya pamba, tumbaku duniani ni kutokana na kukosa viwanda vya ndani ya nchi, tunategemea mno masoko ya nje. Masoko makubwa yanaweza kupatikana humu nchini kama Serikali itajielekeza katika kujenga viwanda vya kusindika haya mazao humu humu nchini. Ajira zitaongezeka zaidi kuliko ilivyo sasa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Serikali itoe maelezo kwa nini wakati wote inaahidi kwamba suluhu ya soko la mazao haya ni kuwa na viwanda vya ndani lakini hakuna mkakati wowote wa ujenzi wa viwanda vya mazao mathalani pareto, pamba na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasilisha.

MHE. DKT. WILLIAM A. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri yeye binafsi pamoja na Naibu Waziri kwa kazi yenu nzuri hapo Wizarani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa sasa ni wakati wa kuchukua maamuzi ya kuwawezesha wazalendo kuchukua biashara kubwa pamoja na kuwawezesha wazalendo kuanzisha viwanda vikubwa ili nchi iweze kuingia katika uchumi kati.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Wizara kuweka kipaumbele kuwezesha elimu biashara ya Kimataifa, sasa ni wakati wa kuweka kipaumbele katika kuweka mkakati wa elimu ya biashara Kimataifa (International Trade) kwa wajasiriamali makini katika Tanzania. Mpango huu unaweza kuwa katika semina kila mkoa zenye kulenga skills za uhusiano kibiashara Kimataifa.

MHE. JUMA OTHMAN ALI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Waziri kwa hotuba yake. Naiomba Serikali iwashawishi wawekezaji kwa kuweka viwanda vya maziwa katika Jiji la Dar es Salaam kwa sababu maziwa ni muhimu sana kwa matumizi ya kila siku, hii pia itawapa wafugaji wetu kupata soko lenye uhakika pia ajira kwa vijana wetu zitaongezeka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba viwanda vya ngozi kama SIDO viboreshwe kwa mikoa yote ambayo ina wafugaji wengi pia wapate soko lenye uhakika, pia wajasiriamali wataongezeka, na ajira zitapatikana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Wizara iwashawishi wawekezaji kwa kuweka kiwanda cha kusindika samaki kwa sababu samaki ni chakula muhimu sana pia ukizingatia upatikanaji wake ni wa msimu na uvuvi ni moja ya rasilimali katika nchi yetu hii itawapa moyo wavuvi wetu kwa kuwa na uhakika wa kipato chao pia vijana wetu wataelekea huko na kuweza kujiajiri wenyewe pia itasaidia kutoagiza samaki wa makopo toka nje. Kwa kuwa kule Zanzibar hasa Kisiwa cha Tumbatu kuna samaki wengi sana hii itapunguza umaskini kwa kuwa kutakuwa na soko lenye uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. MKIWA A. KIMWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami napenda kuchangia hoja hii iliyoko mbele yetu, kwani ni hoja muhimu sana, kwa kuwa kila kitu kinagusa biashara na pia viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ni muhimu huwezi kusema viwanda na biashara, bila kuzungumzia kazi na ajira, hivi ni vitu vinavyoenda sambamba kabisa na hakukua na haja ya kuwepo na Wizara ya Kazi na Ajira, ingekuwa Viwanda, Biashara Kazi na Ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika viwanda wafanyakazi ndio wazalishaji wa bidhaa ambazo ndio huleta biashara hapo mwisho wa kazi iliyofanyika. Tunapogusa viwanda lazima tuguse pia wazalishaji, wazalishaji hao ambao hutaabika, kufanya kazi katika viwanda hivyo bila vifaa stahiki na wengine huwa vibarua hata miaka kumi, ndani ya viwanda hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vyote ambavyo vimekufa mna mpango gani kujenga viwanda vipya na kufufua viwanda vya zamani? Hebu tazama Kiwanda cha Mbolea Tanga, kimekufa, sababu zinazotolewa ni finyu. Kiwanda cha Foma Tanga, nani kakitafuna maana mnunuzi alihamisha mpaka mitambo, ina maana Wazigua na Wasambaa pamoja na Wadigo hawahitaji kazi? Na kama sheria inaridhia kuhamisha mitambo, baada ya kukinunua, ni vema tukarekebisha sheria hiyo na tuamue mwekezaji anapoamua kuwekeza Tanga halafu ahamishe mitambo na kupeleka mahali pengine.

Mheshimiwa Mwenyekiti, MUTEX nayo haina mwelekeo, vijana zaidi ya 3,000 wamepoteza ajira. Vioski vya maziwa vya Kyagata na Makongoro pia vimekufa. Vioski hivi vilikuwa vinapeleka katika Kiwanda cha Maziwa ya Mara.

Kiwanda cha Nguo Mwanza (MWATEX) nacho hoi, hatujui ni nini kinachofanyika hapo, kilichojaa ni malalamiko ya wafanyakazi ni bora sasa tukafuatilia viwanda hivi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha Ngozi Mwanza, Kiwanda hiki kilifungwa kwa sababu ya kumwaga maji taka ndani ya Ziwa Victoria. Majibu haya niliyasikia hapa tarehe 8 mwezi wa nne, wakati akijibu swali ndani ya Bunge hili. Sasa ni wakati muafaka wa kukifufua kiwanda hicho, kwani mabwawa ya maji taka yapo hata nusu kilometa haifiki na waweze elekeza bomba zao kwenye mabwawa hayo, cha muhimu Kiwanda kifunguliwe na vijana wetu waweze kupata ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni imani yangu kuwa Serikali hii haifanyi kazi kama timu. Hivi sasa Jiji la Mwanza wanapima viwanja ambapo palikuwa na mashamba ya watu, shamba moja likipimwa linaweza kutoa viwanja zaidi ya vinne. Mtu huyu anapewa kiwanja kimoja tu, hivi eneo alilokuwa akilima akapata mazao ya kula na kuuza, leo hii hawana wakifanyacho, hawalimi wala hawauzi, ni bora sasa Wizara hii ikafanya mpango wa makusudi wa kuwajengea kiwanda cha juisi ya embe, huko kunavunwa embe nyingi sana, ili vijana hawa waweze kupata ajira baada ya kuchukuliwa ardhi za wazazi wao ambao ndio kilimo kilikuwa kiwanda chao. Ahsante.

MHE. AMINA ANDREW CLEMENT: Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Serikali iwashawishi wawekezaji wajenge viwanda vya kusindika samaki kwa sababu hapa kwetu samaki wanavuliwa wengi lakini kwa msimu, kama kutakuwa na viwanda hasa Dar es Salaam upatikanaji wa samaki utakuwa rahisi hata samaki wengine wataletwa kutoka Zanzibar kwa sababu ni karibu, pia itasaidia kupata ajira ya vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa pamba ni kilimo katika nchi yetu washawishi kiwanda kinachotengeza kanga pia watengeze madira kwa sababu kanga inayotengezwa hapa nchini ni bora kuliko madira yanayotoka India, pia itapunguza kuagiza madira mabovu na badala yake kupatikana hapa kwa sababu kina mama wengi wanapenda kuvaa dira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya ngozi viboreshwe kwa kuwa ngozi ipo nyingi hapa nchini kwetu, hii itawarahisishia wafugaji kuuza kwa urahisi pia kupata ajira vijana wetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Ahsante. MHE. ASHA MSHIMBA JECHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii kwa asilimia mia moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naungana na Waheshimiwa Wabunge wenzangu waliosema Bajeti hii ni ndogo mno, hasa ukizingatia Wizara hii ni mtambuka. Ipo mipango mingi ya kipaumbele kwa nchi yetu katika Wizara hii. Mfano, kuwaendeleza wajasiriamali wadogo kuwa wa kati kwa kusanifu mazao yao ili kuuza ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suluhisho la hayo ni viwanda vidogo vidogo, masoko na kuwaweza kifedha na utaalamu wananchi kupitia vikundi, SACCOS, Ushirika na kadhalika ili waweze kuzalisha kwa malengo, kipato chao kiongezeke na uchumi kijumla wa nchi uweze kukua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo zile taasisi zilizo chini ya Wizara hii ni lazima Serikali iziwezeshe ili ziweze kutoa ujuzi na vitendea kazi kwa kuwafuatilia na kuwa karibu na wajasiriamali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la mwani linaendelea kulimwa katika Ukanda wa Bahari, lakini hadi sasa wakulima hawajapata suluhisho la kilimo hicho, kwani matajiri au mawakala wao ndio wanaotoa vifaa na bei baada ya mavuno ni lazima kuuza kwao. Je, hadi sasa Serikali inawaambiaje wakulima wa mwani kuhusu bei bora ili na wao waweze kukuza kipato chao?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa mwani ni zao linalouzwa nje ya nchi, kuna utafiti wowote uliofanyika, angalau kujua kwenye masoko ya nje bei ikoje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja hii, ahsante.

MHE. ABIA M. NYABAKARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, napongeza Wizara na viongozi wake. Mchango wangu utakuwa juu ya masoko ya mahindi mkoani Rukwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Wizara ya Viwanda na Biashara iandae Kitengo cha Biashara kinachoshughulikia masoko ya mahindi kupeleka nje, mwananchi auze kwa Serikali, Serikali itafute masoko tutapata faida kubwa sana badala ya wajanja wachache kunufaika na biashara hiyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Asante.

MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda na biashara ni sekta nyeti sana ya kuendeleza uchumi wa nchi yetu. Kwa bahati mbaya sana Wizara hii imepata Bajeti ndogo isiyotufikisha popote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, NDC ni Shirika ambalo lina wataalam wazuri na lilifanya kazi kubwa sana lakini NDC hii imeomba siku nyingi fedha kwa ajili ya kuendesha miradi ya makaa ya mawe, Mchuchuma, Liganga na Ngaka ili wazalishe umeme. Wote tunajua umuhimu wa umeme kwa nchi yetu na tunajua ni jinsi gani kutokana na mabadiliko ya tabia nchi kuwa cha umeme wa maji (hydro electric power) si cha kuaminika tena. Hivyo suluhu, letu ni makaa ya mawe. Kwa kweli fedha waliyotengewa ni ndogo sana, waongezewe ili waweze kufanya kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sera ya uwekezaji ni nzuri lakini imepelekea baadhi ya viwanda vyetu kufa kabisa. Pamoja na utetezi wa Serikali kwamba wanafuatilia na vitafufuliwa, mfano Tanzania General Tyre Arusha, Kilimanjaro Machine Tools na kadhalika, viwanda vingine vimebadilishwa uzalishaji. Mfano kile cha pembejeo za kilimo UFI sasa hivi ni godown na vingine vingi, lakini Kiwanda cha Urafiki ambacho kilikuwa kinazalisha sana uzalishaji umepungua. Kibaya zaidi baadhi ya mashine zimeuzwa kama vyuma chakavu. Lakini pia wafanyakazi wa Kitanzania wamekuwa wakinyanyaswa hasa kwa upande wa mishahara na nafasi za uongozi yaani menejimenti.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi nyingi zimeendelea kupitia viwanda. Nchi zote za Ulaya na Mashariki ya mbali ziliendelea baada ya kutoka kwenye kilimo na kwenda kwenye viwanda kama Industrial Revolution. Hivyo ni vyema pawe na mkakati mzuri wa kuboresha na kufufua viwanda vyetu. Viwanda vyote ambavyo vilibinafsishwa na havizalishi basi virudishwe mikononi mwa Serikali ili vizalishe. Hii pia itasaidia sana ajira kwa Watanzania wengi waliopo vijiweni huku wakiwa na elimu na ujuzi. Tunahitaji Tanzania yenye viwanda na kuepuka aibu ya kuwa na rasilimali, malighafi na viwanda visivyofanya kazi.

MHE. MUSA KHAMIS SILIMA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na Katibu Mkuu wa Wizara kwa kazi yao nzuri wanayofanya kwa wananchi/Watanzania. Kazi zenu ni nzuri sana tatizo letu ni ukosefu wa fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na kukosa kwenu fedha basi jitahidini kwa kidogo mlichonacho mkitumie vizuri Mungu atawasaidia maendeleo yatapatikana tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaomba Serikali sasa iwasaidie NDC katika suala zima la umeme kwani maendeleo ya viwanda hayawezi kupatikana bila umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, matatizo ya umeme yanasababisha hata wawekezaji waogope kuja kuwekeza Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja asilimia mia moja.

MHE. SALIM HEMED KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Waziri wa Viwanda na Biashara, Naibu Waziri na watendaji wake wote kwa kazi nzuri iliyofanywa mwaka uliopita katika kukuza viwanda na biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na juhudi za Wizara bado Serikali inatoa Bajeti ndogo kwa Wizara hii kiasi kwamba malengo mengi muhimu hayawezi kutekelezwa kwa ukamilifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ubora wa bidhaa. Tuna matatizo ya kupokea bidhaa zisizo na viwango. Kwa mfano bidhaa za umeme, bidhaa za ujenzi na kadhalika. Jambo hili lina athiri sana, jamii katika suala zima la uchumi wao. Miongoni mwa nchi zinazolalamikiwa kwa bidhaa zisizo na ubora ni China. Ni kwa nini bidhaa za Kichina hapa Tanzania hazina viwango lakini bidhaa za Kichina katika nchi nyingine ni za viwango.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wafanyabiashara wa ndani wanakuza utaalamu wa kazi zao na hivyo kufanyakazi kwa mazoea tu. Naomba Serikali ihimize suala la utaalam ili wafanyabiashara wasifilisike.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu wafanyabiashara wa nje, waliopo hata nchini wanafanya biashara nzuri lakini Serikali ingeweka vigezo ni biashara gani wageni wanapaswa kufanya na biashara gani hawapaswi kufanya. Hali ilivyo sasa ni vurugu tupu, wapo wafanya biashara wa nje wanauza pilipili, binzari pale Kariakoo biashara ambayo ingefanywa na Watanzania wajasiriamali tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la kusindika bidhaa za kilimo, moja ya majukumu makubwa kabisa ya Wizara hii ni kushawishi ujenzi wa viwanda vitakavyosindika mazao ya kilimo, ili tuuze nje mazao yaliyosindikwa na kuyaongezea thamani ili kukuza mapato ya Watanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni aibu kuona wakati wa msimu, embe zinaoza, machungwa yanaoza, mananasi yanaoza, kwa kuwa hakuna viwanda vya kusindika mazao hayo. Lakini baadhi ya viwanda vilivyobinafsishwa kwa mfano viwanda vya korosho havitumiwi kwa kubangulia korosho. Lakini ili viwanda vyote hivyo vifanye kazi zao vizuri lazima pawe na umeme wa uhakika jambo ambalo pia ni tatizo. Kwa ufupi sekta ya viwanda kama ingefanya kazi vizuri, ingekuza biashara kwa kuuza bidhaa zilizosindikwa na hivyo kukuza uchumi wa nchi yetu. Tuuze nje bidhaa nyingi zaidi kuliko sisi kuagiza bidhaa nyingi nje. Hili linawezekana na Serikali ifanye wajibu wake.

MHE. AMINA M. MWIDAU: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa naomba nichukue nafasi hii kumpongeza Mheshimiwa Waziri kwa hotuba yake nzuri na kuwa yote aliyoyaeleza kwenye hotuba yake yatatekelezwa, basi nchi yetu itaanza kuwa na viwanda angalau.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nichangie kama ifuatavyo:-

Kiwango cha ukuaji wa shughuli za kiuchumi za uzalishaji bidhaa za viwandani, mwaka 2009 kilikuwa 8.0% na mwaka 2010 7.9%. Mwaka 2010 kiwango kilishuka kutokana na kushuka kwa sekta ya umeme na gesi. Kushuka huku kwa kiwango kilikuwepo pia kwa miaka ya nyuma. Mfano mwaka 2007 ukuaji wa sekta ya umeme na gesi ulishuka toka 10.9% mpaka kufikia 5.4 kwa mwaka 2009. Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii ni muhimu sana katika kuchangia ukuaji wa uchumi na mahitaji ya umeme yamekuwa yakiongezeka kila mwaka kwa wastani wa MW 70 kwa mwaka. Hali hii ya kupungua kwa ukuaji wa umeme unadidimiza mahitaji ya umeme viwandani kwa kiasi kikubwa na kupelekea wananchi kukosa ajira kwa kusimamishwa kazi viwandani, uzalishaji wa bidhaa kupungua au kusimama kabisa, mapato ya Serikali (kodi) kwenye viwanda kupungua, kupungua kwa wawekezaji kwenye sekta ya viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, madhara ya ukosefu wa umeme kwenye uchumi wa Taifa ni mkubwa sana hasa kwa nchi inayojitahidi kujikwamua kwa kupitia viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kweli tatizo sugu sasa hivi katika viwanda vyetu ni ukosefu wa umeme. Mamkala ya Mapato Tanzania ilinukuliwa ikisema kuwa mgao wa umeme unaotokea viwandani toka mwanzoni mwa mwaka huu unaweza kuikosesha mapato Serikali ya zaidi ya shilingi bilioni 840.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba Mheshimiwa Waziri kwa mujibu wa Hali ya Uchumi wa Taifa katika mwaka 2010 uzalishaji wa kamba (kwa sekta ya viwanda) ndio pekee ulipungua kutoka tani 7,913 mwaka 2009 hadi tani 5,548 mwaka 2010 sawa na upungufu wa 29.9%.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini pamoja na kukua kwa bidhaa nyingine viwandani (uzalishaji) lakini bado mchango wa viwanda katika Pato la Taifa (GDP) ni mdogo sana 2% tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali lazima izingatie kwamba idadi ya watu milioni 43 kwa Tanzania haiendani na ujenzi wa viwanda kwa nchi zote zilizopiga hatua kwenye mapinduzi ya viwanda duniani basi idadi ya watu na ujenzi wa viwanda huwa yanakwenda kwa pamoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba sasa nizungumzie Tanga. Kwa kweli miaka ya nyuma ya 1970 hadi 1990 Tanga ulikuwa mji wa viwanda, lakini cha kusikitisha hii leo hakuna hata kiwanda kimoja cha maana ukiachia Kiwanda cah Saruji. Viwanda vikubwa vilivyokufa ni mbolea, chuma, foma, uzalishaji wa katani ndio kabisa uliuwa viwanda Tanga na ilikuwa inachukua idadi kubwa ya watu (ajira).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kinachonisikitisha kwenye Bajeti ya Wizara sijaona sehemu Tanga inatajwa katika kufufuliwa viwanda hivyo halafu ndio kujengwe viwanda vipya na ukizingatia Mheshimiwa Rais ameahidi kuirudisha Tanga kuwa mji wa viwanda zaidi ya ulivyokuwa hapo awali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namwomba Mheshimiwa Waziri alifanyie kazi hilo kwani Tanga sasa hivi hakuna ajira kabisa, hali za vijana ni mbaya sana, viwanda vilivyopo ni vidogo na vya Wahindi havitoi ajira kubwa na wananyanyasa sana vijana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mzunguko wa pesa ni mdogo sana Tanga na watu wengi kwa vile hawana ajira wanashindwa kutofautisha weekend na weekdays.

MHE. FATUMA A. MIKIDADI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hongera kwa Bajeti nzuri. Napenda kutoa pongezi kwa viwanda vya chumvi. Tanzania tuna chumvi karibu mikoa tisa, lakini wanaosindika chumvi ni wachache tu na hakuna viwanda vya kutosha vya chumvi. Tunanunua chumvi ya unga toka Kenya. Serikali iweke mazingira mazuri ili wawekezaji wa kusindika chumvi waje Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, chumvi hiyo hiyo, haina soko kwa sababu mwekezaji aliyekuwa ananunua chumvi Kiwanda cha Mgololo sasa ameacha na mwekezaji aliyekuja sasa katika Kiwanda cha Mgololo ananunua chumvi ya nje. Why? Kwa nini ananunua nje wakati chumvi ipo Lindi, Mtwara, Dar es Salaam, Bagamoyo, Tanga, Zanzibar, Kigoma, Pwani na kadhalika. Tunaomba jibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, zao la chumvi halina Wizara, kwani ni idara nyingi wanataka kodi, ardhi wanatoza ushuru (kodi), viwanda wanatoza ushuru (kodi), Halmashauri wanatoza ushuru (kodi) na watu wa madini wanatoza ushuru (kodi).

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo kwanza tunaomba ushuru upunguzwe, pili tunataka iwekwe katika Wizara moja badala ya kuwa na Wizara zote nne nilizozitaja hapo juu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka soko la chumvi, hivi sasa chumvi ya mwaka 2009 – 2011 ipo ndani Lindi, haijauzwa tusaidieni soko la chumvi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, SIDO, EPZ, TIRDO NDC na TBS waongezewe pesa kwa manufaa ya wananchi. Pesa waliopata haitoshi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vipimo vya rula vya kupimia pamba vimepitwa na wakati. Wawe na vipimo bora. Viwanda vya Korosho Mkoa wa Lindi vya Lindi Mjini, Nachingwea, Mtama sasa vimekufa tangu vimebinafsishwa kwa nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono bajeti.

MHE. LUHAGA J. MPINA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mahitaji ya soko la nyama ndani na nje ni tani na kilo ngapi? Je, nchi inakidhi mahitaji ya soko la nyama katika soko la dunia? Je, kuna changamoto gani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inafanya jitihada gani kuhakikisha kuwa kuna soko la uhakika la zao la pamba, kama ilivyofanya kwenye tumbaku?

Mheshimiwa Mwenyekiti, taasisi kama Tanzania Agricultural Market Development Trust (TAG MARK) Agricultural Marketing Forum (AMF), Tanzania Cotton Board (TCB) zinafanya nini kuhakikisha kuwa bei nzuri ya mazao nchini inapatikana?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa nini Shirika na NDC mpaka sasa halijaonesha nia ya kuanzisha kiwanda cha nguo na nyama Mkoani Shinyanga, licha ya changamoto zilizopo katika upatikanaji na bei ya uhakika ya pamba na mifugo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kitendo cha wakulima kususia kilimo ni tatizo kwa Taifa linalotegemea kilimo ambapo ni zaidi ya Watanzania 75% wanategemea kilimo, sehemu kubwa ya export inategemea kilimo, ajira, mapato ya Serikali, na malighafi katika viwanda vya ndani, chakula na biashara. Je, Serikali/Wizara inafahamu hali hii tete inayolikabili Taifa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waziri atanihakikishia kuwa kuanzia kesho bei ya pamba itakuwa shilingi 1,100/= kama ilivyokuwa awali?

MHE. JAMES D. LEMBELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa dhati kabisa napenda kuanza mchango wangu kwa ufupi sana kusema ninaunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninajua kutokana na ufinyu wa Bajeti ya Wizara hii mwaka huu, Wizara itakuwa/itakumbana na changamoto nyingi katika kutekeleza majukumu yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina jambo moja ninaomba ufafanuzi kuhusu Kiwanda cha Nyama cha Shinyanga, kiliuzwa kwa mwekezaji mzawa mwaka 2007 mwezi wa saba. Kuanzia mwaka huo, wawekezaji hao wamekuwa katika mkakati wa kupata fedha za kuanza uzalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hata hivyo pamoja na jitihada hizo, wanakumbana na vikwazo vingi. Mara CHC inataka kukichukua kiwanda, mara uongozi wa Mkoa unapeleka wawekezaji wengine kwenye kiwanda ambacho kwa sasa sio mali ya Serikali ili mradi tu kuwakatisha tamaa Watanzania wenzao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, taarifa za uhakika nilizonazo wawekezaji hawa wapo mbioni kama sio katika kipindi cha miezi mitatu basi minne watakuwa wamekamilisha zoezi la kupata pesa na vielelezo vipo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka ufafanuzi ni kwamba kwa nini baadhi ya watendaji katika vyombo vilivyopewa dhamana ya kubinafsisha mashirika ya Serikali wanawanyanyasa wawekezaji hawa badala ya kushughulikia watu walionunua mashirika miaka kumi na zaidi na hawajaendeleza mashirika hayo wanasakama watu (wazalendo) ambao wamenunua mashirika miaka minne iliyopita? Ninataka kujua kama hao maafisa wa CHC katika suala la kiwanda cha nyama Shinyanga wanataka kukirejesha kiwanda hicho Serikalini kwa manufaa ya nani?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. BENEDICT N. OLE NANGORO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nawapongeza Waziri, Naibu Waziri, Katibu Mkuu na Naibu pamoja na wataalam kwa hotuba nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda strategic kama vile sementi, vyuma na vyakula vipewe kipaumbele ili vifanikiwe katika uzalishaji na ushindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya zamani vya nguo, matrekta, ngozi na kadhalika vifufuliwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya kujengwa vizingatie maeneo muhimu kimkakati kwa mfano, eneo la umeme, uchukuzi na usafiri ili vifaa vya msingi vipatikane.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mipango ilenge ujenzi wa viwanda vya shughuli mbalimbali – katika agroecological zones zinazozalisha malighafi zitakiwazo na viwanda hivyo.

MHE. MOHAMED H. MISSANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Nampongeza Mheshimiwa Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Cyril Chami na Naibu wake, Mheshimiwa Lazaro Nyalandu kwa hotuba nzuri ya bajeti ya Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya jambo la kusikitisha ni Tanzania kugeuzwa kuwa dampo la bidhaa feki na bandia na Serikali inashindwa kuchukua hatua thabiti za kukabiliana na tatizo la bidhaa feki na bandia. Suala hili ni kero kubwa kwani wananchi wananunua bidhaa hizo lakini hawapati thamani ya fedha yao (no value for money). Hivyo, wananchi wanaumizwa bila sababu za msingi. Naitaka Serikali kuchukua hatua thabiti za kukabiliana na tatizo hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa muda mrefu kiwanda cha Matairi (General Tyre) Arusha hakifanyi kazi na kimesababisha matairi mabovu kuingizwa nchini jambo ambalo linasababisha ajali nyingi barabarani na wananchi wengi kupoteza maisha. Matairi mabovu au feki yana mchango mkubwa katika ajali za barabarani. Nashauri Serikali kufufua Kiwanda cha Matairi cha General Tyre kupitia wafadhili au wawekezaji wa ndani na nje, NSSF wameonyesha nia ya kuwekeza katika kiwanda hiki.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimboni kwangu Kijiji cha Msungua Kata ya Sebuka kuna Kiwanda kidogo cha Ngozi pamoja na Maziwa. Wanakijiji hicho wanatengeneza viatu vizuri sana ambavyo Waziri Mkuu Mheshimiwa Pinda ni shahidi kwani alitembelea kijiji hicho na alifurahishwa sana. Aidha, katika maonesho ya nane nane mwaka huu hapa Dodoma, Waziri Mkuu Mheshimiwa Pinda alikwenda katika banda la Halmashauri ya Wilaya ya Singida na kukagua maendeleo ya kiwanda hicho. Naomba Wizara isaidie kiwanda hiki kwa mambo mawili; kuwatafutia soko na kuwaongezea utaalam. Jeshi la Magereza linaweza kuombwa kununua viatu hivyo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Singida tuna Viwanda vya Mafuta ya Alizeti vinafanya vizuri. Naomba tusaidiwe ili pawe na double refine ya mafuta ya Alizeti badala ya kupelekwa Kenya.

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Tanzania ni nchi ya tatu katika Bara la Afrika kuwa na mifugo mingi cha ajabu Tanzania ni nchi yenye viwanda vichache vinavyosindika mazao yatokanayo na mifugo. Hatuna viwanda vya kusindika maziwa, nyama, ngozi na kadhalika. Hii inaonesha jinsi tusivyoweza kupita hatua katika uzalishaji viwandani bali tunarudi nyuma. Wafugaji wetu hawajaweza kunufaika na mifugo yao kutokana na kukosa soko la uhakika wa mazao yatokanayo na mifugo yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na wafugaji kukosa viwanda kutokana na mazao ya mifugo yao kadhalika wakulima hawanufaiki na mazao yao kutokana na kukosa soko la uhakika kwa mazao yao. Matunda na mbogamboga zinaoza ovyo kwa wakulima, Serikali iiwezeshe SIDO kwa fedha za kutosha ili wakulima wadogo wadogo wawezeshwe na SIDO kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya kusindika mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulibinafsisha viwanda ili kuongeza uzalishaji. Taarifa ya Waziri imesema kuwa viwanda 17 havizalishi. Taarifa ya Waziri haijasema iwapo wamiliki hao wamekwisha nyang’anywa viwanda hivyo. Naomba maelezo katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi waliotoa maeneo yao kwa ajili ya uwekezaji (EPZA) walipwe fidia kuondoa lawama kwa Serikali yao. Ni zaidi ya miaka mitano sasa wananchi hao hawawezi kufanya jambo lolote la maendeleo kwa sababu hawajalipwa fidia na hawawezi kuhama wala kufanya jambo lolote la maendeleo katika maeneo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi ni mmoja wa Wabunge waliotembelea Mradi wa Liganga na Mchuchuma pia na Ngaka. Ni utajiri mkubwa uliopo pale, nahisi watumishi wa Wizara hii hawajawahi kutembelea maeneo hayo ndiyo maana maamuzi yanasuasua na hawajali Wabunge wanapochangia kwa uchungu. Majibu yao ni ya mezani kwa sababu hawaendi “site” kuona hali halisi. NDC iwezeshwe ili miradi hiyo ya kuzalisha umeme kwa kutumia makaa ya mawe na pia uzalishaji wa chuma uanze mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatizo la kupanda kwa bei ya sukari ni kubwa mno. Kwanini Serikali isitoe leseni kwa wafanyabiashara wengi kuagiza sukari? Pamoja na kulinda viwanda vya ndani lakini ukiritimba kwa waagizaji sukari walio wachache wanawauza sana wananchi wetu. Tunajua jinsi wanavyokubaliana kuficha sukari ili bei ipande ndiyo waruhusu sukari yao kuingia sokoni. Naomba Serikali kufuatilia jambo hiki kwa ukaribu zaidi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. IGNAS A. MALOCHA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sekta hii ni muhimu sana katika kuinua uchumi kwa jamii ya Watanzania ili jambo hili muhimu lifanikiwe haina budi kujikita katika maeneo ya uzalishaji yaani maeneo ya vijiji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, yapo maeneo ambayo mwanzo Serikali ilihamasisha wananchi kwa kuanzisha viwanda vidogo vya kusindika mazao yanayozalishwa kama vile karanga, alizeti na ufuta lakini hadi sasa yanaonekana Majengo hayo yamechakaa bila kufanya kazi baadhi ya maeneo hayo ni Laela, Mji Mdogo wa Mtowiza Makao Makuu ya Tarafa ya Mtowiza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Shirika la SIDO limepwa fedha kidogo ukilinganisha na umuhimu wake. Hivyo, Serikali inatakiwa iongeze fedha katika Shirika la SIDO ili kuliwezesha kufanya kazi zake vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, elimu ya teknolojia inayotolewa na SIDO isambazwe nchi nzima kwa wakulima ili wakulima waweze kutumia elimu hiyo. Kwa kusindia mazao yao na kujipatia faida nzuri kwa kuuza bidhaa iliyosindikwa badala ya kuuza mazao halisi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ushirikiano wa Wizara ya Viwanda na Biashara na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika. Ili kuleta ufanisi katika Wizara hii ya Viwanda na Biashara lazima ishirikiane na Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao ya biashara. Lazima Serikali iimarishe mazao ya biashara kutoka katika Mikoa mbalimbali kadri ardhi na hali ya hewa inavyoruhusu ustawi wa mazao hayo ili kurahisisha utafutaji wa soko la mazao hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naunga mkono hoja.

MHE. DKT. MAUA A. DAFTARI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nampongeza Waziri na Viongozi wote wa Wizara hii kwa juhudi zao za kuendesha Wizara. Naomba nichangie katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanzani kuhusu Viwanda. Kazi kubwa imefanyika katika kutafuta wawekezaji wa kuwekeza katika ujenzi wa viwanda. Ili kilimo kiweze kuleta tija kwa nchi na wananchi lazima kuweko na linkages baina ya viwanda na mazao yanayozalishwa. Umuhimu wa kuwa na viwanda vya kubangua korosho, kusaga maganda ya korosho na kuwa na viwanda vya kutumia mabaki hayo kutengeneza mafuta na chakula cha mifugo. Kwa kufanya hivyo, tutakuwa tunalipa bei zao la korosho na kuongeza ajira.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mazao ya buni, katani, karanga, tangawizi nao yachukue mfano huo huo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya vifaa vya kilimo vilivyokufa vifufuliwe na vipya vijengwe, si lazima kutengeneza majembe ya mkono tu lakini, pia mashine ya kupandia mbuga, matrekta ya aina zote na majembe yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vya chuma tutafute wawekezaji ili wawekeze katika eneo hili.

Viwanda vidogo vidogo vya kusaidia wananchi kuzalisha ni vema SIDO au binafsi au kwa ubia wasambaze mabawa yao mikoani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umuhimu wa kuwa na kiwanda cha kuyeyusha udongo unaotokana na uchimbaji wa dhahabu.

Uwezekano wa kuwa na viwanda vya kutengeneza nyavu, mashine za boti kwa kutumia wawekezaji au kuingia nao ubia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu biashara. Nakerwa sana na Tanzania kufanywa Dampo la Sub-standard goods zinazoletwa toka Asia. Wenzetu wa Marekani wanapiga marufuku bidhaa za chakula zinazotokana na chochote na maziwa yanayotokana na nchi fulani ambayo ilishukiwa kuweka malarine kwenye utengenezaji wa maziwa yapo hata mayari artificial tutafika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia nakerwa na kuona wageni wamejaa Kariakoo wakiuza viatu na maua. Je, tuna hakika maua yao yanatengenezwa kwa tumia vitu gani. Je, mbona nchini kwao hawaruhusu watu toka nje kufanya kazi wanazoweza kuzifanya wao. Wageni sasa wanamiliki lodge na hoteli za kima cha chini. Wananunua viwanda halafu wanavigeuza ma- godown nasi tupo tunaangalia tu. Kwa nini Tanzania inageuza a dumping place kwa substandard furniture na textile toka Asia?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Viwanda vya Kanga zinazotengenezwa hapa nchini ni za hali ya chini, nyepesi, zimepunguzwa urefu na upana na thinness na vitenge pia! Wenzetu wanapiga marufuku mazao ya baharini toka Japan kuepuka mionzi, sisi sasa tunaagiza samaki toka Japan wakati tukijua uchafuzi wa bahari Japan na mionzi, tunajiandaa kweli? Wazawa wapewe nafasi wawezeshwe, wasibandikiwe kodi na tax exemption wakapewa wageni tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migodi ya dhahabu, almasi na madini mengine sasa isitolewe kibali bila wazawa nao kuwa wamiliki wa hisa 50% kama wanavyofanya wenzetu.

MHE. MARIAM R. KASEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, nachukua nafasi hii kuchangia hotuba ya Waziri wa Viwanda na Biashara kwa maandishi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mkoa wa Mtwara ni miongoni mwa Mkoa mmojawapo katika nchi yetu na ni mkoa ambao wananchi wake wamekuwa wakishiriki kikamilifu katika uzalishaji mali kwa ajili ya kujiondolea umaskini na kuchangia katika pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na jitihada kubwa za wananchi hawa kuanzisha vikundi vya kiuchumi, SACCOS, viwanda vidogo vidogo vya usindikaji na ubanguaji Korosho na kadhalika lakini Mheshimiwa Mwenyekiti, bado Wizara hii haijatambua kabisa shughuli za wananchi hawa wa Mkoa wa Mtwara hasa katika Jimbo langu la Masasi.

Masasi kuna vikundi vya akinamama vya ubanguaji korosho, kuna Vyama vya Ushirika ambavyo sasa wapo katika maandalizi ya mwisho ya kuandaa ubanguaji korosho, tuna maandalizi ya kuwaangalia Halmashauri zetu juu ya kuanzisha ubanguaji korosho, tuna vikundi vya VICOBA ambavyo hivi sasa wameungana na kuanzisha ushirika wao lakini hadi hivi sasa Wizara hii hatujaona jitihada zozote za kuunga mkono jitihada hizi za wananchi ambao wana kiu kubwa ya kuondokana na umaskini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Masasi kama Wizara ingekuwa na jitihada za makusudi za kuweka viwanda vidogo vidogo kwa mfano vya kutengeneza juisi ya Mabibo, wine ya mabibo, juisi za maembe, usindikaji wa nyanya, akinamama na vijana wangeweza kupata ajira na kupunguza uzururaji .

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa ni SIDO peke yake ndiyo imeonesha jitihada za kuwasaidia wananchi, hivyo tunalishukuru shirika hili. Viwanda Vidogo vidogo vinaweza kuleta maendeleo kwa wananchi wetu hivyo basi kupitia Wizara hii ni maombi yafuatayo kwa wananchi wa Jimbo langu la Masasi kama ifuatavyo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, naiomba Wizara iwezeshe vikundi vya ubanguaji korosho na elimu ya biashara na mitaji ili kuendeleza ubanguaji katika njia bora na kuuza bidhaa zao zikiwa na vifungashio vya kisasa ili bidhaa ziingie katika soko zikiwa na ubora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ifanye jitihada za kutafuta wawekezaji, au Serikali iwawezeshe akinamama na vijana kuanzisha viwanda vidogo vidogo vya usindikaji wa bidhaa mbalimbali hasa vya juice na wine na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali isimamie mfumuko wa bei za bidhaa mbalimbali zinazotoka viwandani ili kuwawezesha walaji au watumiaji wa bidhaa hizo kumudu gharama hizo kama vile kupanda kwa bei ya sukari, bidhaa za ujenzi kama bati, saruji na kadhalika. Pia mafuta ya taa kwani watumiaji wakubwa ni wananchi waliopo vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naunga mkono hoja kwa asilimia mia moja. Ahsante sana.

MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na viwanda vingi Tanzania baada ya kupata uhuru lakini viwanda vingi vimefungwa kwa mfano, Kiwanda cha Tembo cha Mbao kilichoko Mkumbara, Korogwe vijijini kimefungwa wakati kilihudumia Mikoa ya Tanga Kilimanjaro, Arusha na Pwani. Kimefungwa na mmiliki wake hajulikani na wafanyakazi hawajui watalipwa lini. Je, Serikali ina mpango gani wa kuamsha kiwanda hiki kwa kuwa viwanda vingi vimebinafsishwa kati ya hivyo vingi vimekufa, lini vitaamshwa? Kumekuwepo na biashara nyingi lakini zinafanywa karibu na vituo vya mafuta kama hoteli za kulala wageni, je, hii haileti maafa kwa wananchi na ni kwa usalama huwa inakuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti, wananchi wameamua kutaka kujengwa Kiwanda cha Chai kwenye msitu wa Sakare kwenye Tarafa ya Bungu, Korogwe vijijini. Je, Serikali itawasaidiaje wananchi hawa kwa msaada wa kupata kiwanda hicho? Leseni za biashara hizi zinapotolewa wahusika wanaangalia sehemu za biashara?

MHE. CAPT. JOHN D. KOMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, pongezi kwa Wizara ikiwa pamoja na Waziri na Naibu wake. Pamoja na pongezi hizo naona kuna matatizo katika maeneo yafuatayo:-

Kwanza, Mradi wa Ngaka – Mbinga ambao ungeweza kutoa MW 400, naomba Serikali isiwe na kigugumizi. Itoe pesa ili mtandao wa umeme kutoka Ngaka hadi Mufindi uweze kusafirisha umeme ulio kwenye grid ya Taifa.

Pili, Serikali isikubali pendekezo la wawekezaji la kuchimba makaa ya mawe na kupeleka viwandani Kyela na Dar es Salaam ukiacha wananchi wa maeneo hayo kuendelea na umaskini wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara kati ya Malawi na Tanzania, kama Serikali inaamua kuimarisha bandari ya Mtwara na Mbambabay ili kuimarisha biashara kati ya Malawi na Tanzania, biashara hiyo ni kwa faida ya nani na nani watashirikishwa kwenye biashara hiyo? Nasema hivyo kwa sababu hadi sasa wananchi waishio mwambao wa Ziwa Nyasa hawaruhusiwi kufanya biashara mbalimbali na Malawi ikiwa ni pamoja na biashara ya sukari. Bado biashara hiyo ni ya magendo tu kwa nini isiwe rasmi.

MHE. HAJI JUMA SEREWEJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa kuniruhusu kuchangia hoja hii. Kwa niaba ya wananchi wangu wa Jimbo langu la Mwanakwerekwe, naunga mkono hoja hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Waziri wa Wizara hii na Naibu wake pamoja na watendaji wote wa Wizara hii kwa mipango mizuri ya Wizara hii. Lakini kupanga mipango ni rahisi sana lakini kuitekeleza ni vigumu, kwa hiyo, namwomba Mheshimiwa Waziri asimamie vizuri sana ili kazi itekelezwe vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na kazi za Wizara hii ilivyokuwa humu nchini, basi ni wazi kuwa fedha walizozipata Wizara hii ni kidogo sana katika kutekeleza mipango ya kazi za Wizara kwa sababu nchi inaendelea kwa viwanda na nchi inaendelea kwa biashara. Kwa hiyo, naiomba Serikali izidishe fungu la fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naipongeza sana Wizara kwa kuweza kuifikisha pazuri nchi yetu kwa kujiunga na kuanzisha G 51 nchini na kupata kuanzisha nembo za mistari za utambuzi wa bidhaa zetu (bar codes) jambo ambao litafanya bidhaa za nchi yetu kutambulikana kikamilifu na kuondokana kuzipa umaarufu nchi ambazo tulikuwa tunachukua nembo hizo. Naiomba Wizara iharakishe alama hizo zianze kufanya kazi haraka.

Mheshimiwa Mwenyekiti, NDC ni chombo cha umma kinachomilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa chombo ni vizuri kikawezeshwa kifedha ili kifanye kazi zake vizuri hapa nchini. Kwa hiyo, naomba kizidishwe fungu na kifanye kazi zake vizuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yoyote inaendelea kwa viwanda na hata vijana wetu watapata ajira kwa wingi sana na sasa hivi viwanda vingi vimekufa kabisa. Naiomba Serikali ichukue juhudi kusimamia viwanda hivyo ili vifanye kazi na vile vilivyobinafsishwa basi waliopewa viwanda hivyo wasimamiwe vizuri ili viwanda hivyo vifanye kazi vizuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, EPZ imeletwa kwa lengo zuri la kukuza viwanda, kuuza mauzo ya nje, kuongeza ajira, kukuza teknolojia, kuunganisha bidhaa zetu na masoko ya nje Kimataifa na kuhamasisha usindikaji wa mazao yetu. Ukitazama mambo haya kama yatafanyika na kufanikiwa vizuri, basi nchi itapiga hatua kubwa ya maendeleo. Lakini mambo haya yote ili kufanikishwa yanahitaji fedha. Kwa hiyo, wapeni fedha ili wafanikishe vizuri na nchi yetu iondokane na umaskini. Bila fedha tutakuwa kila siku tunazungumza hayo hayo bila kupata mafaniko yoyote yale na yote haya yamebebwa na Wizara ya Biashara, Masoko na Viwanda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni Wizara muhimu sana lakini fungu la bajeti ni dogo, dogo, dogo, tena dogo. Naiomba Serikali izidishe fungu kwenye Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante na narudia tena kuunga mkono hoja hii.

MHE. ESTHER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwa na malalamiko karibu nchi nzima, katika maeneo ya mradi wa EPZ hasa wananchi wanapopisha mradi wa EPZ kwa kuacha maeneo yao kwa makubaliano ya kulipwa fidia lakini mbali na wananchi kupisha maeneo yao kwa ajili ya mradi huo, mbali na tathmini kufanyika, lakini wengi wanalalamika kutolipwa fidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, moja ya eneo lenye malalamiko ni eneo la Tairo Wilayani Bunda. Tathmini ilifanyika tangu mwaka 2007 watu zaidi ya 402 wamepisha maeneo yao kwa ajili ya mradi wa EPZ, lakini mpaka sasa bado hawajalipwa, watu 228 bado hajalipwa huu ni mwaka wa nne. Tangu tathmini ifanyike ni miaka minne sasa, watu wanashindwa kuendeleza maeneo yao. Je, Serikali imetenga kiasi gani cha fedha katika bajeti ya mwaka huu ili kuwalipa wahanga wa EPZ

Kwa kuwa wamefanya tathmini muda mrefu watu wameshindwa kuendeleza makazi yao, tangu mwaka 2007, je, Serikali itatumia utaratibu gani ili haki itendeke? Je watafanya tathmini upya ili malipo yeendane na gharama halisi za maisha na ujenzi ya sasa?

MHE. DKT. CHARLES J. TIZEBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, natoa pongezi kwa Wizara na hasa Waziri na Naibu Waziri wake kwa kazi nzuri na hotuba nzuri.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia katika mambo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ifanye kazi kwa karibu sana na Wizara za Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Wizara ya Kazi na Ajira ili kubaini mahitaji mahususi ya viwanda vidogo vidogo ambavyo vinaweza kujengwa katika maeneo yasiyo na viwanda vikubwa. Mkakati wa namna hii wa pamoja utawezesha Serikali kuelekeza nguvu zake za mafunzo, vifaa na mitaji katika maeneo ambayo yanazo rasilimali na malighafi kwa ajili ya uzalishaji.

MHE. SYLVESTER M. MABUMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kumpongeza Mheshimiwa Waziri, Naibu Waziri na watendaji wote wa Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nizungumzie umuhimu wa Sekta ya Viwanda na Biashara kwa maendeleo ya nchi yetu. Nashauri Wizara hii iwe na ushirikiano wa karibu na Wizara ya Kilimo na Chakula. Pia nashauri iwe na mpango endelevu pamoja na mambo mengi, ijenge viwanda vya kusindika mazao ya wakulima (agro-processing plants) ili kuongeza thamani ya mazao hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kufanikisha azma hii naiomba Serikali yetu iondoshe urasimu unaowavunja moyo wawekezaji wa ndani na nje ya nchi wanapotaka kuwekeza. Hapa Tanzania upu mzunguko mrefu hadi mwekezaji kuweza kupata kibali cha kuwekeza ukilinganisha na nchi kama Rwanda ambayo imeondoa mambo ya urasimu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, niipongeze Serikali kwa vile Mheshimiwa Waziri ameeleza katika hotuba yake kwamba wanatarajia kuanzisha One Stop Services kwa wawekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili Sekta ya Viwanda iweze kufanikiwa hapa nchini ni lazima Serikali ihakikishe pamekuwepo umeme wa uhakika. Hivyo, nashauri kadhia ya ukosefu wa umeme iondoshwe hapa nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda nizungumzie Benki ya Rasilimali TIB, benki hii ipewe mtaji wa kutosha ili iweze kuwasaidia wawekezaji wazalendo wapate kuwekeza na hivyo kuchangia wigo wa ajira na kuchangia ukuaji wa uchumi wa nchi hii. Viwanda vya wazalendo visaidiwe kwa sababu wao wana uchungu na maendeleo ya nchi yetu. Nashauri watendaji katika benki hii wakishindwa kutimiza wajibu wao wawajibike kwa manufaa ya umma.

Mheshimiwa Mwenyekiti, migodi ya chuma ya Mchuchuma na Liganga itumike katika kuibadili nchi yetu ili iwe nchi ya viwanda. Hata hivyo, naomba kutanabaisha kwamba tusirudie makosa tuliyoyafanya kwenye sekta ya madini ya dhahabu, almasi, gesi na mengineyo ambayo mikataba tuliyoingia na wawekezaji haina manufaa na nchi yetu. Nashauri tutafute wawekezaji waadilifu ili Tanzania na watu wake wapate manufaa stahiki. Naomba sana chuma ya Liganga na Mchuchuma kisaidie maendeleo ya viwanda hapa Tanzania kwa kuwa na wawekezaji ambao siyo wababaishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu iwekeze kwenye viwanda vidogo vidogo ambayo vinahitaji mitaji midogo, teknolojia rahisi lakini pia vinatoa ajira kwa wananchi wengi. Viwanda hivi vitasaidia maendeleo ya Tanzania. SIDO nashauri iwezeshwe na iwasaidie wananchi kuanzisha viwanda vidogovidogo. Serikali ipige marufuku uagizaji wa furniture kutoka nje ili kuvisaidia viwanda vya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo lingine ni maeneo ya uwekezaji EPZ na SEZ. Ili maeneo hayo yaweze kukuza uzalishaji, nashauri Serikali iweke miundombinu yote muhimu inayohitajika ili kuvutia wawekezaji kwenye maeneo hayo. Umeme wa uhakika, barabara, industirial sheds vyote ni muhimu sana. Nia hii njema ya Serikali lazima itekelezwe kwa vitendo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile biashara za matunda, mbogamboga, maua na kadhalika zimeonesha kuwa na masoko ya uhakika huko Amerika, Ulaya na Asia, naishauri Serikali yetu ifufue Shirika la Ndege la Tanzania ili lisaidie kusafirisha mazao haya kwenda kwenye masoko. Biashara hii inachangia pato la Taifa kwa kuingiza fedha za kigeni za uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naomba nizungumzie uwepo wa bidhaa feki zisizo na ubora ambazo zimekithiri sana hapa nchini. Naomba mamlaka husika TBS, FDA na kadhalika kama zimeshindwa kudhibiti uingizaji wa bidhaa hizo zivunjwe na Serikali ilete mswada ili Bunge litunge sheria kali itakayodhibiti bidhaa feki hapa Tanzania.

MHE. NYAMBARI C. M. NYANGWINE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchukua nafasi hii kumpongeza Waziri na Wizara hii Mheshimiwa Dkt. Cyril A. Chami pamoja na Naibu Waziri wake Mheshimiwa Lazaro S. Nyalandu kwa juhudi zao wanazozionesha katika kuongoza Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia hoja hii kwa kuuliza maswali yafuatayo:-

(a) Je ni lini Nembo za Mistari (Bar codes) zitaanza rasmi kutumika hapa Tanzania?

(b) Kwa nini wafanyakazi katika viwanda vya wageni hususan Wahindi na Waarabu hunyanyaswa? Je, Wizara inalifahamu hilo? Je, ni hatua zipi zimechukuliwa?

(c) Serikali ina mpango gani wa kuufanya ukanda wa Sirari – Tarime, Wilaya ya Tarime kuwa ukanda maalum wa Kibiashara?

(d) Je, Serikali ina mkakati gani wa kuanzisha viwanda hapa nchini?

(e) Ni kwa nini biashara nyeti hapa nchini zimeshikwa na wageni?

(f) Je, Wizara imejiandaaje kujenga masoko ya kisasa yenye hadhi katika mipaka ya nchi yetu hususan eneo la Sirari, Wilayani Tarime?

(g) Je, Serikali inakabilianaje na tatizo la bidhaa bandia hapa nchini?

(h) Wizara inasaidiaje wafanyabiashara wadogo wadogo wanaokwenda China, Dubai na Turkish kwa kuwaongezea mitaji isiyokuwa na riba?

(i) Je, Serikali inalinda vipi masoko ya wakulima hapa nchini?

(j) Kwa nini Bandari ya Dar es Salaam inawanyanyasa wafanyabishara wazalendo kwa kuwacheleweshea mizigo yao bandarini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja.

MHE. MARTHA M. MLATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kupata nafasi hii ili kuongea niliyonayo kwa njia ya maandishi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nianze kwa kuipongeza Wizara kwa hatua nzuri ambayo imefikia hasa kwa uimarishaji wa Viwanda na kufufua vilivyosahaulika. Pia uzalishaji hapa nchini umeongezeka na ni kwa ubora unaokidhi. Pamoja na hayo, naiomba Wizara itupie macho viwanda vidogo vidogo hasa Mkoani kwangu, zao la Alizeti limekuwa ni mkombozi kwa wakulima wa zao hilo kwani wanakamua mafuta kupitia viwanda vidogo, tatizo kubwa ni namna ya kupata kiwanda kikubwa ambacho kitaweza ku-double refu. Ili ubora uweze kukidhi soko la ndani na nje, kipo kiwanda pale Singida tunachoona ndio Mkombozi, lakini nacho hakiwezi ku-double refu. Naiomba Wizara ikatembelee viwanda hivyo na hata kile kikubwa na kuona namna gani watatoa msaada.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba kutoa ushauri wa namna ya kupunguza msongamano wa vitu feki kutoka nchi za nje hasa China, kwani wamegeuza nchi yetu ni dampo au ni ya kujifunzia. Mfano, furniture zote toka chini ni geresha ya finishing tu, ukinunua leo kesho kiti kinavunjika. Hivyo, naomba uwekwe utaratibu wa kwamba wanaotaka kuuza furniture zote zinazotumia mbao, waje waweke kiwanda hapa watengeneze, tutanunua!

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa naomba niendelee na wimbo wangu usiokwisha, kwani tangu 2006 nimekuwa naimba wimbo wa COSOTA hadi wenzangu sasa huniita dada wa COSOTA au mama COSOTA. Kweli inauma sana, sasa leo siimbi ila nalia na nitaendelea kulia, mnadai kuwa kuandamana ni kitu kibaya, lakini nitashawishi wasanii wote nchini. Kwanza nyimbo za CD, DVD, TAPE na kazi zote za sanaa, machapisho na kadhalika kwanza visitumiwe. Pili, tupige hodi Wizarani ili Waziri atuongoze mpaka kwa Mtendaji wa COSOTA tupate majibu ya kwa nini tangu COSOTA ianzishwe, bado hatujawa na mafanikio katika kazi zetu za sanaa na hali tunazalisha na zinatumika, why?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2007, mkutano Mkuu wa COSOTA ulifanyika na kuteua au kuchagua wajumbe wa Bodi, lakini Mheshimiwa Waziri alikwama kuteua Mwenyekiti wa Bodi na hivyo Bodi hiyo haikufanya kazi mambo yakawa varuvaru. Nilipoona hali inakuwa mbaya 2008, nikamuuliza Waziri kulikoni? Ikawa kimya, 2009 Bunge la bajeti, nikamwuliza tena wapi! Yaani hadi tunafikia ukingoni mwa kumaliza Bunge, Waziri akaamua kuteua Bodi nyingine tena sio ile iliyochaguliwa na wanachama. Ukweli hii imeathiri sana utendaji kazi wa COSOTA kwa mengi, CEO wa COSOTA, kwanza hajawahi kuthibitishwa toka alipoajiriwa kwani hapakuwa na bodi. Pamoja na hayo, mwaka 2007 iliyokuwepo ilipanga kuanza taratibu za kurekebisha mfumo wa COSOTA, kupanga utekelezaji wa kifaa cha kuzuia wizi wa kazi za sanaa na kurekebisha mfumo wa utendaji wa COSOTA yote yale yalikwamishwa na Waziri alipoacha kutumia Bodi hiyo kwa kuteua Mwenyekiti. Kwa kweli nasikitika sana kwani kwanza, hata Serikali imekosa mamilioni ya fedha za kodi, wasanii ndio kabisa! Wameendelea kudhulumiwa kwa kitendo hicho. Hivyo, kwanza, naomba itambulike kuwa Bodi ya sasa ni batili kwani uteuzi wake umekiukwa, pia naambiwa mimi ni mjumbe wa Bodi, sielewi niliteuliwa lini hata barua sina, niliitwa kwa simu kwenye kikao cha pili na kisha nikatumiwa taarifa ya kikao siku tatu kabla, yaani sielewi nini ni nini! Yaani unapigiwa kuulizwa lini utakuwa free ili tufanye kikao cha Bodi bila kujua kama wewe ni mjumbe, unasema okay, tufanye tarehe fulani, unapoondoka wanasema after 3 days uwe hapa mie sielewi jamani, sielewi tutafika kweli?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba mambo yafutayo:-

Kwanza, ili kuondoa tatizo la piracy, COSOTA ipewe nguvu za kushtaki kama iliyo TAKUKURU kwnai piracy ni tatizo sugu linaitia doa Serikali. Pia COSOTA inapokwenda kutetea wasanii, iache mambo ya kuwakingia kifua wahalifu.

Pili, CAG akague Account za COSOTA, nahisi kuna harufu ya ubadhirifu.

Tatu, TRA na TCRA waingilie kati kuweka mikakati ya namna ya uuzwaji wa kazi za sanaa na utumikaji kwenye vyombo vyote kama vile TV, RADIO, DJ’s na kadhalika. Japo TCRA wamejitahidi sana kusaidia hilo nawapongeza ni fedha tu hatujui zinaishia wapi.

Nne, Bodi iliyopo ivunjwe kwani ni batili! COSOTA iitishe mkutano wa wanachama ili wachague upya kama walivyofanya 2007 ama waliochaguliwa 2007 Waziri aidhinishe hao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba majibu na siungi mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuongezea jambo ambalo bado linanitatiza sana kwani mambo haya ya sanaa au kazi za wasanii yanakuwa njia panda, huwezi kujua jambo lipi nani anashughulikia na nani ana jambo lipi. Sasa niulize, je, COSOTA wana habari au wanahusika vipi juu ya Operation ya kamata kamata ya kazi za wizi wa sanaa nchini linaloendesha na Msama Promotion? Kwani amekamata kazi zilizorudufiwa kiharamu na si chini ya milioni moja na hamsini na kesi zingine ziko Mahakamani na zingine vituo vya Polisi na kadhalika. Naomba kujua hatma ya mambo hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba majibu na siungi mkono hoja.

MHE. LOLESIA J.M. BUKWIMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nitoe pongezi kwa hotuba nzuri inayolenga kuleta matumaini kwa wananchi. Tunapozungumzia suala la Viwanda na Biashara maana yake ni mpango wa kukuza uchumi na kuunguza umaskini. Kwa kuwa Serikali imeona umuhimu huu kwa kuangalia kuboresha sekta hii muhimu, nina uhakika kwa miaka mitano ijayo tutaweza kuona maendeleo dhahiri miongoni mwa Watanzania wa hali ya chini na walioko vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nikiangalia katika Mkoa mpya wa Geita tunazo rasilimali za kutosha na kama tukianzisha viwanda vidogo vidogo vya kuongeza thamani mazao yetu, nina uhakika tutanufaika zaidi. Wilayani Geita tuna kilimo cha matunda (mananasi), kupitia Wizara hii tunaomba tusaidiwe ili tuanzishe Kiwanda cha Kusindika Mananasi Geita. Kupitia kiwanda hiki watu wa Geita na wakulima katika maeneo ya Geita hasa wanaolima nanasi watapata soko la uhakika ambapo wakati wa mavuno mengi bado bei itakuwa ni nzuri kabisa. Kupitia kiwanda hiki pia tutaweza kuboresha maisha ya vijana walio wengi wasiokuwa na ajira kwa kuajiriwa kiwandani. Wilaya ya Geita pia imepakana na Ziwa Viktoria ambapo tuna uhakika wa samaki wa kutosha. Katika kuleta thamani kwa samaki wanaovuliwa katika mialo ya Nkome, Bukendo, Kasanghwa, Kageye na sehemu zingine ambazo sijazitaja tunaomba Wizara itusaidie kuanzisha Kiwanda cha Samaki. Ni kweli kuna viwanda vya samaki Mwanza lakini viwanda hivi havitoshelezi uhitaji wetu. Hivyo, tunahitaji msaada mkubwa Geita kwa kuzingatia kwamba Geita ni Mkoa mpya ambapo tunatakiwa tu-identity maeneo ya uwekezaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho naomba Wizara ianzishe soko kubwa la mazao ya nafaka Katoro. Mji wa Katoro ni mji wa kibiashara tukianzisha soko hili watu kutoka Uganda, Burundi, Rwanda, watapata bidhaa muhimu katika soko hili na tutainua hali ya kiuchumi katika ukanda huo wa Magharibi. Nimependekeza hivyo kutokana na hali halisi iliyopo katika mji huu kwa sasa. Zipo biashara za kila aina. Ili kuweza kupanua wigo wa kibiashara na kisoko, soko kubwa la nafaka litainua uchumi katika Kanda ya Magharibi. Bila kusahau Elimu ya ujasiriamali tunahitaji sana katika miji ya Katoro, Rwamgasa na Nyarugusu, hii itapanua wigo wa kibiashara. SIDO katika Jimbo la Busanda sijaona wala sijasikia kazi zake. Naomba SIDO ipanue shguhuli zake ifike Busanda na Geita kwa ujumla. Ni kweli kazi za SIDO ni nzuri sana zikipanuliwa hadi maeneo ya vijijini, wananchi watafaidika na watainuka kiuchumi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sina mengi ila nasisitiza tu kwamba Wizara ianzishe viwanda vya kusindika matunda Geita, Viwanda vya Samaki na soko kubwa la nafaka Katoro.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo, machache, naunga mkono hoja.

MHE. PINDI CHANA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashauri maeneo ya EPZ yatozwe kodi ndogo kwa ajili ya kulipa Serikali za mitaa, nini maoni ya Serikali kuhusiana na hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Ludewa Kata ya Mundindi wananchi wameambiwa wahame kuna uwekezaji, hivyo wananchi wapishe viwanda vya Liganga. Swali, ni lini wananchi hawa watalipwa fidia zao? Vile vile maeneo ya kuhamishiwa hayajaelekezwa vema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba TBS itoe elimu Ludewa na Makete juu ya utunzaji wa mazao yao ili kuongeza value ya bidhaa za viazi au ngano na bidhaa zote za kilimo. Je, linawezekana? Kama ndiyo lini?

MHE. ENG. ATHUMANI R. MFUTAKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Jimbo la Igalula linaomba SIDO iongezewe fedha Mkoani Tabora ili mikopo ya wajasiriamali wakopeshwe zaidi mabilioni ya JK.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda vidogo vidogo viongezwe na mafunzo ya kukamua asali na mafuta ya alizeti kuongeza kipato, ajira na uchumi wa wana Igalula.

MHE. REV. ISRAEL Y. NATSE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa maendeleo ya nchi yoyote ile, suala la uchumi wa viwanda ni muhimu sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ifanye juhudi za makusudi katika kufufua viwanda kwa mfano General Tyre East Africa, viwanda vya nguo, Urafiki, Mwatex na kadhalika, kiwanda cha magunia, ngozi na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nchi yetu ilishafika mahali fulani katika maendeleo ya kiviwanda kwa sababu ya kukosa umakini, uzalendo, viwanda hivyo vyote vimekufa na kama vipo basi vinasuasua. Ili nchi ipate maendeleo ya haraka basi Serikali ifufue viwanda hivyo na kuhakikisha kuwa tunalinda viwanda vyote vya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tusiuze raw material bali bidhaa za viwanda. Serikali kuwa mahiri katika ushindani wa bidhaa za viwandani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uingizwaji wa bidhaa feki nchini, hili ni tatizo kubwa sana. Udhibiti mkubwa unatakiwa kwa bidhaa zote zinazoingizwa nchini ili kulinda viwanda vya ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu masoko. Serikali iwahakikishie wakulima, wajasiriamali uhakika wa masoko kwa bidhaa au mazao yao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu viwanda vidogo vidogo. Serikali iwawezeshe wananchi katika vikundi kwa ku-support viwanda hivyo SIDO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu biashara. Serikali iwawezeshe wafanyabiashara wa Tanzania kufanya biashara kwa mafanikio na tija kwa kuwawekea mazingira mazuri ya ushindani kwa biashara zao.

MHE. PROF. KULIKOYELA K. KAHIGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nitachangia kwa kuuliza maswali machache yanayohitaji majibu:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, Sera ya Maendeleo endelevu vya viwanda Tanzania (2001) ilikamilisha mchakato wa kurasimisha ubinafsishaji wa viwanda na biashara nchini. Sera ya ubia baina ya sekta binafsi na Serikali ya hivi karibuni (Private Public Partnership) umeandaliwa ili kushughulikia miradi isiyowezekana kwa njia mbadala.

(a) Je, Serikali imejiandaaje kusimamia ubinafsishaji ili kudhibiti udanganyifu hasa kuhusiana na kiasi sahihi cha uzalishaji, kiasi sahihi cha uuzaji na kiasi sahihi cha pato?

(b) Kuna mafanikio gani tangu Sera hii ya viwanda (SIDP) ianzishwe, hasa kwa kuwa hadi sasa imeshindwa hata kufufua viwanda vilivyokuwepo kabla ya 1985?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, tatizo ambalo tumelishuhudia katika miaka ya hivi karibuni ni kushindwa kufanya uamuzi kuwekeza katika viwanda vya kimkakati kama vya chuma na makaa ya mawe. Tumeshuhudia Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC) likinyimwa fedha ya kutosha ili litekeleze majukumu yanayoelezwa katika sheria iliyounda Shirika hilo.

(a) Je, Serikali ina mipango gani ya uhakika ya kuanza kuwekeza katika viwanda vya kimkakati vitakavyoleta mabadiliko makubwa ya kiuchumi nchini?

(b) Je, Shirika la Maendeleo ya Taifa litapewa fedha ya kutosha kulingana na mahitaji ili litekeleze majukumu yake?

MHE. STEPHEN M. WASIRA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nichukue nafasi hii kumpongeza Waziri wa Viwanda na Biashara Mheshimiwa Dokta Cyril A. Chami na Naibu Waziri wa Wizara hii Mheshimiwa Lazaro S. Nyalandu, pamoja na watendaji wote wa Wizara kwa kuandaa bajeti ya mwaka 2011/2012 katika Wizara husika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuongelea suala la EPZA katika Kijiji cha Tairo kilichoko Wilayani Bunda hasa katika Jimbo langu la Bunda. Mpango wa EPZA umechukua ekari 3000 eneo ambalo ni makazi ya watu ambao wengi wao ni wafugaji. Wananchi wengi hawakutaka kuhama lakini baadaye wamekubali kwa misingi kuwa walipwe fidia halali. Tathmini iliyofanyika ilibainisha kuwa fidia kwa wakazi hao ni zaidi ya Sh. 2,000,000,000/= lakini hadi sasa ni kiasi cha Sh.1,000,000,000/= ambacho kimekwishalipwa. Naomba Waziri anijibu maswali yafuatayo:-

(a) Je, ni lini kiasi kilichobakia kitalipwa?

(b) Je, ikiwa kiasi kilichobakia hakitalipwa kwa muda mfupi ujao, itakuwa ni makosa kwa wananchi kuendeleza maeneo yao kwa kujenga majengo ya kudumu?

(c) Je, EPZA ikishakamilisha malipo ya fidia, Wizara itakuwa tayari kuendeleza eneo hilo kwa kuweka miundombinu ya kudumu ya barabara, maji na umeme?

(d) Kwa ujumla Wizara inasema nini juu ya uwekezaji huo wa EPZA katika maeneo mengine ya Tanzania?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba pia kukisema Kiwanda cha Nguo cha Mutex kilichoko Wilayani Musoma. Nahitaji majibu ya uhakika juu ya kiwanda hiki hasa:-

(a) Je, kimekwisha binafsishwa au kimeuzwa?

(b) Je, kinazalisha au hakizalishi?

(c) Je, Wizara ina mpango gani kuhusu kiwanda hiki?

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda pia kuuliza juu ya bidhaa zinazozalishwa hapa nchini:-

(a) Je, zina ubora kiasi gani?

(b) Zinaleta faida kiasi gani?

(c) Je, zinauzwa katika nchi zipi?

(d) Je, Wizara inawasaidiaje wazalishaji wa bidhaa zinazozalishwa hapa nchini na kuuzwa nje ya nchi?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba vilevile kufahamishwa ni namna gani Wizara imejipanga kuboresha masoko ya wakulima wa nchi yetu ya Tanzania. Pia napenda kufahamishwa ni kwa namna gani wizara hii imejipanga kuhakikisha kuwa inajenga masoko ya mpakani ili kuleta ufanisi wa biashara na wananchi wetu waweze kutumia fursa hizo kwa misingi ya kujipatia kipato.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. MODESTUS D. KILUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokuwa na Viwanda ndani ya nchi, kushindwa kuinua uchumi wa nchi pamoja na kuwanyima ajira Watanzania japo nchi hii ilikuwa na Viwanda vingi vya Nguo, vya Sementi, vya Zana za Kilimo, vya Mbolea na kadhalika vyote vilikufa, kama hiyo haitoshi nchi hii ilikuwa na Mashirika ya Umma ya kiuchumi kama vile NAFCO na Ranchi za Taifa kwa ajili ya ufugaji, sehemu kubwa vyote hivi navyo siyo endelevu. Leo tunasherehekea miaka 50 ya Uhuru tukiwa hatuna Viwanda na Mashirika ya Umma. Kubwa sana tulilolifanya ni kubinafsisha Viwanda na Mashirika ya Umma. Tumeingiliwa na maradhi gani Watanzania? Kama siyo tunaelekea utumwani ambako babu zetu walitoka? Inawezekanaje ubinafsishaji kila kitu cha thamani katika nchi hii?

Mheshimiwa Mwenyekiti,bajeti iliyopanga kwa wizara hii haitoshi, na hivyo sijaridhika na hatua ya wizara katika kuboresha sekta ya viwanda, naomba nijibiwe ni lini Serikali itaimarisha, fufua viwanda vyetu vilivyokuwepo ambavyo vilikufa katika mazingira yasiyo na mashiko katika kutoa ajira kwa watanzania lakini pia kwa uchumi wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, je Serikali ipo tayari sasa kuwataka wawekezaji upande wa viwanda waanzishe viwanda vipya badala ya kuwapa viwanda vyetu? Je, Serikali ipo tayari kutenga bajeti ya kutosha ili kuvifufua viwanda vyetu? Je, Serikali ipo tayari kuleta Muswada wa Sheria ambao utatoa adhabu kwa viongozi wote wanaoshindwa kusimamia viwanda vyetu, mashirika yetu na shughuli za umma badala yake kucheza mchezo mchafu wa kujinufaisha wao wenyewe? Kama itakubalika napendekeza adhabu ya kifungo cha maisha na kufilisiwa mali zao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuamue sasa kuchukua hatua kwa viongozi wasio waadilifu vinginevyo wimbo wa Tanzania yenye neema lakini wananchi wake maskini hautakwisha. Tuamue sasa tuokoe uchumi wa Taifa letu. Serikali isijitoe kabisa katika shughuli za kiuchumi na kukabidhi shughuli zote za kiuchumi kwa wawekezaji ambao wengi ni wageni wasio na uzalendo wa nchi yetu.

MHE. CHRISTOWAJA G. MTINDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika maeneo yafuatayo:-

Kwanza, suala la Kiwanda cha Matairi – Arusha (General Tyre East Africa Limited (GTEAL). Kiwanda cha GTEAL kilianzishwa mwaka 1969 kwa ubia wa Serikali ya Tanzania na General Tyre USA kwa lengo la kuzalisha na kuuza matairi kwa kuwa baadaye Kampuni ya General Tyre USA iliuzwa kwa kampuni ya Kijerumani ya kutengeneza matairi inayoitwa Continental AG ambapo Serikali ya Tanzania inamiliki hisa 74 na Continental AG inamiliki hisa 26. Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Kampuni hii ilikuwa ikiendeshwa kwa faida kubwa na pia kuzalisha matairi yenye ubora wa hali ya juu hadi kufikia 1997 ambapo kampuni ilianza kujiendesha kwa hasara na kulimbikiza madeni makubwa. Ni kwanini kampuni hii ilianza kupata hasara kwa kiasi hiki? Je, Menejimenti inajielezaje kwa Serikali kwa kulisababishia Taifa hasara kubwa kiasi hiki ilihali matairi yetu yalikuwa bado yanapendwa sana na Watanzania wote?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naitaka Serikali itoe maelezo juu ya mkopo ambao kampuni ilipewa na NSSF wa jumla ya dola za Kimarekani milioni kumi (10M. USD). Mkopo huu umetumikaje mpaka sasa maana hatujasikia lolote kuhusu kufufuliwa kwa kiwanda hicho. Je, Serikali imechukua hatua gani kwa Menejimenti kama mpaka sasa imeonekana fedha hizo zimefujwa na wachache?

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la Soko la Kariakoo. Kwa kuwa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Mashirika ya Umma haikuweza kupitia mahesabu ya Soko la Kariakoo kwa sababu kubwa ya msingi kwamba soko hilo halina Bodi iliyowekwa kwa uhalali. Hivi ni kwa sababu bodi iliyopo ilishamaliza muda wake zaidi ya miaka 10 iliyopita. Je, Serikali inalichukuaje suala hili la soko la Kariakoo ambalo ndilo kiini cha uchumi wa walaji na wafanyabiashara wadogo na wakubwa wa nchi hii? Ni kwa nini kumekuwa na kigugumizi cha kuteua Bodi mpya mpaka sasa ambapo soko limekuwa likijiendesha kwa hasara na pia maamuzi mengi yakifanywa na Bodi ambayo haipo halali kisheria? Naomba Wizara itolee tamko kuhusu suala hilo la Bodi ya Soko la Kariakoo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu uanzishwaji wa Viwanda vya Kusindika Mazao ya Mifugo. Kwa kuwa nchi yetu imejaliwa kuwa na mifugo mingi mfano ng’ombe, mbuzi, kondoo na punda na kwa kuwa wafugaji wamekuwa wakihangaika kuzunguka huku na huku pamoja na mifugo yao kutafuta maji na malisho, Serikali sasa inatakiwa kuwajengea wafugaji hawa viwanda vya kusindika mazao ya mifugo badala ya kuwajengea machinjio peke yake na kuyaita viwanda. Viwanda hivi vitawachochea wafugaji kufuga kwa kisasa na hivyo kuwa na idadi ndogo ya mifugo maana watakuwa na soko la kupeleka mifugo yao pamoja na mazao yake. Hii itasaidia kwa kiwango kikubwa kutunza mazingira na kuepusha ukame unaosababishwa na mifugo kula mimea na kuharibu ardhi kwa kuleta mmomonyoko wa ardhi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.

MHE. GAUDENCE C. KAYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuchangia katika maeneo yafuatayo:-

Kwanza, ni kuhusu udogo wa bajeti kwa Wizara hii. Wizara hii ni Wizara inayozalisha na Wizara kiongozi katika kufikia Dira ya Taifa 2025. Serikali iongeze fedha kwa muono huu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, ni structure ya Wizara Napendekeza kwamba NDC kwa shughuli na majukumu waliyonayo inabanwa sana na ceiling ya Wizara kwa vile majukumu yake pia ni crosscutting lakini pia naona kufuatia mgomo wa wafanyabiashara wa mafuta itabeba majukumu zaidi ya kuwekeza katika maeneo mbalimbali kwa niaba ya Serikali. Ni vema ikawa peke yake au sana kuwa chini ya Tume ya Mipango ili iwe ni mkono wa utekelezaji wa Tume ya Mipango kwenye maeneo ya Sekta ya Viwanda mama, Umeme na Kilimo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, Brela inayo fedha Sh. 3,000,000,000/=, hawana kiwanja. Napendekeza kuwa wajenge Dodoma au wakionana na DCA hapatakuwa na tatizo hilo. Lakini kama ni suala la biashara basi Manispaa ya Temeke wanayo maeneo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nne, ni Trekta (Carmatec). Naomba kujua ni lini tractor hili litazalishwa kibiashara ili litumike hapa nchini na litashindanaje na utitiri wa matrekta yanayoagizwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano, ni kuhusu SIDO. Fedha waliyotengewa haitawasaidia sana lakini ni kwa nini SIDO iliyoanzishwa 1973 iwe imefika mkoani na kubaki hapo. Ni vema tunaposherehekea miaka 50 ya Uhuru SIDO wafike Wilayani ndiko walipo wajasiriamali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tano ni kuhusu TEMDO. Napenda kumshukuru sana Mkurugenzi Mkuu kwa kutuma ujumbe Mbinga na kuonana na wajasiriamali wa Mbinga ambao walifurahi sana. Nategemea kwamba hatua thabiti zitachukuliwa ili kuwasaidia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sita, ni kuhusu EPZA. Ni vema Serikali sasa ifanye uamuzi wa kuendelea na dhana hii ili kuharakisha maendeleo au kuacha kabisa maana nchi za jirani na nchi nyingi duniani zinakwenda kwa kasi sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la saba, kwa vile ni wazi mradi wa Ngaka utaanza kazi, naiomba Serikali ifanye yafuatayo:-

Kwanza, uhamishaji wa wananchi. Jambo hili lifanywe kwa uangalifu mkubwa. Nataka mradi huo uwe wa kipekee na usio na malalamiko. Hatua ya kwanza iwe ni:-

- Kupima eneo la kuhamia watu ikiwa pamoja na miundo mbinu yake;

- Ni vema watu hawa wakajengewa nyumba au wale watakaotaka fedha wapewe mapema. Pawe na majadiliano na makubaliano;

- Pawe na eneo la mashamba pia tunataka kuwa na kijiji kilichopimwa; na

- Fidia iwe kikamilifu na izingatie hali ya uchumi ya sasa.

Pili, mipango ya kwanza ya TANCOAL kujenga Chuo cha Ufundi na nyumba za wafanyakazi ibaki vilevile.

Tatu, wananchi wapewe angalau umiliki wa asilimia tano. Sehemu nyingine duniani inafanyika.

MHE. VICKY P. KAMATA: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuipongeza Serikali kwa juhudi zake za kuendeleza biashara ya ndani ikiwa ni pamoja na kujenga dhana ya kutumia bidhaa zilizozalishwa ndani ya nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ombi langu kwa Serikali. Naomba tusaidiwe viwanda vya kusindika matunda kwani Geita ni Mkoa mpya ambao mbali na kilimo cha pamba na mazao mengine ya chakula, Geita inazalisha matunda kwa wingi hasa mananasi na maembe na yamekuwa yakioza bure bila kumnufaisha mkulima. Je, Serikali haioni sasa ni muda muafaka kuwasaidia wananchi wa Geita katika hilo?

Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru.

MHE. MAHMOUD H. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, naomba nichukue fursa hii kumpongeza sana Waziri na Naibu Waziri wa Wizara hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa masikitiko makubwa sana nashindwa kuelewa kwa nini Serikali haitaki kuiingiza Wizara hii kwenye Wizara za vipaumbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara hii ikiboreshwa kwa hakika tutakuwa tumeanza kupiga hatua ya maendeleo, hakuna nchi yoyote duniani iliyoendelea ambayo haijafanya Mapinduzi ya Viwanda. Naiomba Serikali yako Tukufu ikubaliane nami kuongeza pesa kwenye baadhi ya maeneo hasa NDC, SIDO, EPZA na CALMATEC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hakika kama lengo letu ni kutatua tatizo sugu la umeme, suluhisho la uhakika la umeme lipo hapa hasa katika maeneo ya Ngaka, Mchuchuma, Kiwira kwenye makaa ya mawe ya uhakika, pia kwenye eneo la Singida ambapo kunapatikana umeme wa upepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia naomba Serikali yetu, sikivu iongeze pesa kwenye maeneo ya SIDO, EPZA na CALMATEC hapa ndipo kwenye ajira ya uhakika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naunga mkono hoja.

MHE. FATUMA A. MIKIDADI: Mheshimiwa Mwenyekiti, hongera kwa bajeti nzuri yenye takwimu nyingi na za manufaa, hongera sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka nichangie mambo matano kama ifuatavyo:-

(a) Mheshimiwa Mwenyekiti, biashara ya Guest wanatozwa ushuru mwingi katika Miji, Majiji na Halmashauri nchini.

(b) T.B.S – Shirika la Viwango Tanzania T.B.S walivyoweza kudhibiti bidhaa toka nje na changamoto wanazozipata.

(c) Uhaba wa viwanda sehemu za ukanda wa kusini wakati fursa za kuwa na malighafi zipo, tatizo liko wapi?

(d) Bajeti ya SIDO ni ndogo waongezwe tena.

(e) Maendeleo ya Mtwara Corridor yakoje na changamoto zake na kwamba tangu ilipoanzishwa hadi leo inakuwaje?

Mheshimiwa Mwenyekiti,kuna kero moja ambayo inawapata wenye biashara ya Ma- Guest. Hapa nchini wenye Ma-Guest wote wanatozwa kodi nyingi kiasi kwamba wageni wanapoingia Guest kupanga, wenye ma-guest huwa hawawaandiki wageni. Wanawaficha ili wasitozwe ile kodi ya halmashauri ya miji, jiji, Halmashauri ya wilaya ya kukusanya 20% ya biashara iliyofanyika kwa mwezi, kodi iitwayo Hostel Levy. Kwa hiyo, wenye guests wanatozwa kodi aina tatu:-

(1) Kodi ya Mapato 10% yaani asilimia kumi kwa mwaka.

(2) T.R.A asilimia 10% kwa mwaka.

(3) Hostel Leavy asilimia 20% kwa mwezi bila kujali gharama za msingi (watumishi, sabuni) na kadhalika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba gharama za Hostel Leavy zipunguzwe kabisa iwe 5% badala ya 20% kwa usalama wa nchi, kwani wenye Guests wanavyowaficha wapangaji kwa kuogopa kodi ni hatari kwani wapangaji wengine ni wahalifu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunataka Sheria ya Business Activities Registration Act (BARA) katika vipengele vya Kodi ya biashara ya Guest iangaliwe upya ili kodi ipunguzwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu TBS. Nachukua nafasi hii kuwapongeza Shirika la TBS kwa kazi nzuri ya kudhibiti ubora wa bidhaa. Hivi karibuni wameweza kudhibiti bidhaa hafifu zilizoingizwa nchini, Mafuta ya Petrol Metric Tani 2,500 kutoka Bahrain, Uarabuni; mafuta ya kula kutoka China; viberiti vibovu kutoka China; majembe ya mkono kutoka China; pikipiki zisizo na ubora kutoka China, kwa kweli hongera sana. Lakini TBS inafanya kazi katika mazingira magumu sana kwa sababu ni vituo vitano vya mpakani vilivyofunguliwa na TBS wakati Tanzania kuna vijiji vingi mpakani zaidi ya 30 na vyenye ofisi ya TBS ni vitano tu, Tanga Mjini, Horohoro Tanga, Holili Kilimanjaro, Namanga Arusha, Sirari Mara. Bado kuna mipaka kadhaa ikiwemo Mtambaa Swala Mtwara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni afadhali bidhaa zikaguliwe kule kule zinakotoka kuliko kungojea bidhaa kukagua mpakani, mbona Serikali ilishasema kuwa bidhaa tukague kulekule inakotoka (Preshipment verification of comfomity to standards) Kenya wameanza 2005 na Uganda walishaanza 2010, ila Tanzania bado kwa nini? Wakati sheria ilishapitishwa na Bunge Sheria No.2 ya 2009, Sheria ya Viwango inawapa TBS mamlaka ya kukagua bidhaa zinakotoka hakikisheni mchakato huo unakwisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la tatu, viwanda hakuna katika Kanda ya Kusini hasa Mtwara na Lindi. Asilimia 60 ya vijana wanakwenda Dar es salaam kutafuta kazi na kuitwa Wamachinga. Mtwara na Lindi kuna fursa kubwa ya kuwa na malighafi ya kuendeleza viwanda kuna ufuta, korosho, karanga, mhogo, chumvi, samaki na nazi. Pia kuna gas, cypson, madini, Bahari kuu, chumvi na samaki wengi. Tunaomba viwanda Mtwara na Lindi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie Shirika la NDC hongera kwa kazi nzuri wanayoifanya, angalau sasa miradi ya Mtwara Corridor inaonekana. Lakini NDC iendelee kuhimiza miradi ya Chuma cha Liganga na makaa ya mawe Mchuchuma ili nchi iendelee mbele kwa suala la nishati, hatuna sababu ya kutokuwa na umeme kwani tuna vyanzo vya nishati vya mkaa na chuma, vipo nchini kwa nini tuwe na shida ya umeme.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, naunga mkono mia kwa mia.

MHE. SAIDI R. BWANAMDOGO: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na uwasilishaji mzuri wa bajeti ya Wizara ya Viwanda na Biashara ningependa maeneo yafuatayo yapewe kipaumbele:

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, fidia kwa wananchi waliochukuliwa maeneo yao kwa ajili ya kuanzisha maeneo maalum kama EPZ au SEZ, ni vema Wizara ilipe fidia mapema iwezekanavyo kwa watu wanaochukuliwa maeneo yao. Maeneo ya Bagamoyo yenye ujenzi wa EPZ bado kuna wananchi hadi leo hii hawajalipwa fidia. Ni kero kubwa, ni vizuri ikapatiwa ufumbuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, SIDO ipanuke zaidi. Ni vema Serikali ikaona haja ya kupanua SIDO kwenye maeneo mengi zaidi ili watu wengi waweze kujinufaisha hasa katika kipindi hiki ambacho ajira ni tatizo kubwa kwa vijana wengi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, mfumo wa stakabadhi za mazao ghalani, huu ni mfumo mzuri ingawa baadhi ya maeneo umeleta sintofahamu sana. Nashauri mfumo huu kabla ya kuanza kutumiwa na watu katika eneo husika ni vema wananchi wakashirikishwa na waelimishwe vya kutosha juu ya umuhimu wa jambo hilo.

MHE. ESTHER N. MATIKO: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia kwa kifupi sana kwenye Wizara hii ambapo nitazungumzia kuhusu eneo la uwekezaji lililotwaliwa na EPZ, ni vema sana kuwa na miradi kama hii katika nchi yetu na hasa kuona kuwa ipo kwenye Mkoa wetu wa Mara. Tatizo tulilonalo hapa ni fidia juu ya wananchi wale wanaotakiwa kuhama eneo lile, kwanza kuna malalamiko kuwa fidia ni finyu sana na kuna watu wengi hadi sasa hawajalipwa stahiki yao. Hii inapelekea kuwepo na chuki na jamii husika. Hivyo, naitaka Wizara au Serikali ichukue hatua juu ya kulipwa watu hao ili kuupisha mradi huu.

Pili, Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kuhusu uzalishaji ndani ya nchi ya bidhaa ambazo kwa mwaka wa 2010 kuna hizo bidhaa hazikuzalishwa kabisa. Mfano, ni uzalishaji wa Biskuti na Tambi, uzalishaji huu kwa mwaka 2009 ilikuwa tani 15,200, pia uzalishaji wa nyavu za uvuvi haukufanyika kabisa, vivyo hivyo mazulia, tabaka za mbao, dawa za pareto, mbolea na ni muhimu sana kuwa na uzalishaji wa mbolea kwa ndani na ukizingatia tuna maziwa ya chumvi lakini hatujengi viwanda ili tuweze kutengeneza mbolea za chumvi chumvi, maziwa haya yapo Hanang na kwingineko nchini, hii inatia fedheha sana. Naomba Serikali ichukulie hili kwa umakini wa hali ya juu na kuweka mkakati wa kutumia vyanzo hivi ambavyo ni malighafi ya asili. Vile vile hili jedwali namba 2 linaonyesha kutokuwepo kwa uzalishaji wa Aluminium ambapo mwaka wa jana yake kulikuwa na uzalishaji wa zaidi ya tani 58. Sasa najiuliza kutokuwepo na uzalishaji ni kuwa kiwanda kimefilisika au?

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwisho, ni kujaribu kutoa maoni na changamoto kwa Wizara kuwa wajitahidi kuvumbua sehemu zenye rasilimali ambazo zinahitaji viwanda vya kusindika na kuzalisha, mfano, maeneo yenye kuzalisha matunda na mboga mboga. Pia sehemu zenye kulima pamba, kahawa na hata chai kama Tarime wanalima chai lakini hamna kiwanda hata kimoja. Vile vile kwa maeneo yenye ufugaji kama Mkoa wa Mara na kwingineko tuweke viwanda vya kuvuna mazao ya mifugo hii. Mwisho, ni viwanda vya kusindika na ku-process samaki, jamani ni fedheha, Mara hatuna kiwanda ambacho ni prominent, no Kiwanda cha Maziwa, ile Mara Daily Milk vinakufa tu. Jamani hii ni aibu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vile vile suala la General tyre lipewe uharaka wa aina yake kwani mali za kiwanda kile zinauzwa kwa bei ya chini na zile asset zilizobaki zina depreciate kila kukicha. Serikali inabidi imtafute Mbia mwenza na kama hapatikani ichukue hatua mbadala kwa faida ya Taifa hili la Tanzania. Kiwanda kufunga kwa miaka yote hii sio tija bali linazidi kuleta loss of business na property pia. Hivyo, Serikali haina budi kuhakikisha kiwanda kile kinaanza uzalishaji kwa mwaka huu wa fedha. Ili tupate kuingiza fedha kwani product ya Tyres ndio inatumiwa kwa wingi sana hapa nchini na nje pia.

MHE. FAKHARIA S. KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa Wizara ya Viwanda na Biashara ndio kimbilio la Watanzania waliopo mjini na vijijini, hivi sasa Tanzania tayari inazalisha matunda mengi na ina malighafi mbalimbali tena ya kutosha. Mfano, inazalisha pamba, ngozi, matunda, mbogamboga pamoja na madini mbalimbali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara inahitaji kufufua viwanda vidogo vidogo ili kuweza kuzalisha ajira ya Watanzania. Vile vile Tanzania wapo wajasiriamali mjini na vijijini. Inawezekana ufufuaji wa viwanda vidogo vidogo pamoja na viwanda vikubwa ambavyo kwa pamoja vitazalisha na kuuza ndani na nje ya nchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Ukurasa wa 23 nampongeza Mheshimiwa Waziri kwa kuendeleza programu ya muunganisho wa wajasiriamali wa vijijini kwa kutoa ushauri, mafunzo, mitaji na huduma za kiufundi kwa wajasiriamali. Vile vile Wizara inatakiwa kuhamasisha Mikoa kwa Mikoa, Wilaya kwa Wilaya hadi Vijijini, hivi ni kuonekana kwa baadhi ya mikoa kuzalisha mazao mengi na baadhi kushindwa kutokana na hali ya hewa ya mikoa hiyo. Hivyo basi, Wizara izidi kutoa ujuzi kwa wajasiriamali kuweza kuzunguka katika mikoa mbalimbali ili kutoa mafunzo na kuonesha ujuzi wao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Sekta ya Biashara ili iweze kujipanua zaidi itabidi kuongeza maghala pamoja na masoko ya ndani na nje na hata ya Kimataifa. Tanzania inazalisha lakini hakuna kitengo cha ufuatiliaji masoko ya uzalishaji kwa Watanzania mfano, ziara ya Mheshimiwa Rais, Ushelisheli wana hamu ya kufanya biashara na Tanzania hasa ya mbogamboga, wao huwa wanaagiza India na wakati Tanzania inazalisha kwa wingi na hatuna soko. Je, Mheshimiwa Waziri, Wizara yako itasaidia nini ili Watanzania waondokane na ukosefu wa masoko ya Mikoa hadi Taifa?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. ANASTAZIA J. WAMBURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nampongeza Mheshimiwa Waziri na timu yake kwa maandalizi mazuri ya hotuba. Pili, naipongeza SIDO kwa kazi nzuri inayofanya ya kuwaelimisha wananchi elimu ya ujasiriamali na ujuzi wa viwanda vidogo pamoja na kutoa mikopo kwa wajasiriamali wadogo wadogo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na mazuri yote Serikali itatue changamoto zifuatazo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, wafaidikaji wa huduma za SIDO ni wananchi wa mijini. Sababu inayotolewa ni kwamba SIDO hawana uwezo kifedha wa kufika vijijini. Napenda kuishauri Serikali iwatendee haki wananchi wa vijijini kwa kuwawezesha wataalam wa SIDO kufika vijijini kwani Watanzania wote wanastahili kufaidika na kodi wanazolipa kwa kutumia fursa za SIDO.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, utekelezaji wa Sera ya Viwanda vidogo mara nyingi haukamiliki. Wananchi hupewa mafunzo ya ujuzi lakini wanapata ugumu wa kuanzisha viwanda vidogo kama utengenezaji sabuni kutokana na kukosa malighafi na kutojua mchakato wa kupata cheti cha TBS. SIDO ihakikishe inahusika na wajasiriamali wadogo tangu hatua za mwanzo hadi watakapoweza kusimama wenyewe kama wazalishaji.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, wagunduzi wa SIDO wawezeshwe kusambaza matokeo ya ugunduzi wao, yatumike vijijini. Nyenzo nyingi zinagundulika kwa ajili ya uzalishaji lakini usambazaji wake ni taratibu sana. Kwa mfano, mashine za kutotolea vifaranga na za kutengenezea sabuni zinasambaa kwa uchache sana. Mashine nyingi ni za umeme lakini umeme vijijini hakuna, kwa sababu hii wataalam wanaanza kurudi nyuma kubuni mashine zisizohitaji umeme. Je, ni kwa nini wale waliogundua mashine za kuzalisha umeme wa upepo wawezeshwe kuzalisha umeme vijijini ili vianzishwe viwanda vidogo vijijini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ili kuimarisha sekta ya viwanda nchini, naishauri Serikali iwape wajibu wafanyabiashara na makampuni kulingana na mahitaji ya Taifa kwani wanaweza.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

MHE. DKT. KEBWE S. KEBWE: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nipate maelezo juu ya viwanda vilivyobinafsishwa ni vingapi na ni vingapi vinafanya kazi na vingapi havifanyi kazi na kwa nini?

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wilaya ya Serengeti imepewa jukumu la kulima alizeti katika utaratibu wa One District One Product (ODOP). Ni maandalizi gani yamefanyika ili kusaidia Wilaya ya Serengeti juu ya kuanza kilimo cha alizeti? Wilaya tunao uwezo wa kuhamasisha wananchi kazi ambayo inaendelea vizuri hadi sasa na mwitikio wa wananchi ni mzuri sana.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Viwanda vya ndani viboreshwe hasa vya kutumia pamba ili isaidie kuimarisha soko la ndani la pamba na itasaidia kuondoa usumbufu ambao wakulima wanapata na mapunjo wanayopata hayatakuwepo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kiwanda cha UFI (Ubungo Farm Implements) kifufuliwe ili tupate plough ambazo zitasaidia kuinua kilimo kwa kasi zaidi. Pia itasaidia utekelezaji mzuri wa kilimo kwanza nchini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara ya Viwanda na Biashara isaidie Wilaya ya Serengeti Mitambo ya kuchuja mafuta ya alizeti ili iendane na uhamasishaji mzuri unaoendelea, sambamba na utayari mzuri wa wananchi wa Serengeti juu ya kulima alizeti na hali ya hewa inaruhusu sana.

MHE. DAVID E. SILINDE: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, ni ukosefu wa SIDO katika Jimbo la Mbozi Magharibi (Wilaya mpya ya Momba) kwa kipindi kirefu Wilaya mpya ya Momba haijawahi kabisa kuwa na viwanda vidogo vidogo (SIDO) ambavyo vingetumika katika kuwasaidia wananchi wa huko ambao ni maskini na hawana elimu mbadala itakayowawezesha kujikwamua na hali ngumu ya maisha, hivyo, naomba ufafanuzi katika hili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, uanzishwaji wa Kiwanda kikubwa cha Uzalishaji wa Mbolea, Jimbo la Mbozi Magharibi na Wilaya ya Mbozi. Wizara ya Mbozi ndio inayohusika zaidi na kilimo katika Mkoa wa Mbeya na Taifa kwa ujumla. Lakini cha kushangaza Wizara mpaka sasa haijawa na mkakati thabiti wa kujenga kiwanda kikubwa na cha kudumu kitakachosaidia kuzalisha mbolea itakayowasaidia wakulima na Taifa kwa ujumla, hivyo kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula na biashara kwa Watanzania. Naomba ufafanuzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuwasilisha.

MHE. DKT. ANTONY G. MBASSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote nashukuru kupata fursa hii kuchangia hoja hii iliyopo mbele yetu. Aidha, Wizara hii ni mojawapo ya Wizara Mtambuka kwani ni mojawapo ya nguzo kubwa katika kukuza ajira na kuinua uchumi wa nchi yetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, napenda kuchangia hoja yangu au kuelekeza maelezo yangu kwenye chombo kinachohusika na ubora wa bidhaa zetu au TBS. Chombo hiki kimekuwepo na mara nyingi hatuoni ni jitihada gani zinafanywa na mamlaka hii.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kumekuwepo na upotoshwaji wa makusudi kuhusiana na miradi inayofanyika hapa nchini. Mfano, kuna ujenzi wa nyumba nyingi ambazo mara nyingi zimekuwa zikiporomoka na kupoteza saa nyingine maisha ya watu. Ukifuatilia maelezo Wahandisi wanasema kuwa aidha, nondo na simenti vinatengenezwa chini ya ubora! Suala la kujiuliza mpaka bidhaa inazalishwa kiwandani na kupelekwa kwa watumiaji au walaji, mamlaka hizi zinakuwa wapi kuthibitisha ubora huu? Kama ndivyo je, kuna mkakati gani wa kuhakikisha ubora wa bidhaa zetu unalindwa. Hii ikumbukwe kuwa bidhaa tunazozalisha hapa nchini yawezekana tukaziuza hata nchi za nje!

Mheshimiwa Mwenyekiti, aidha, katika hali ya kawaida hatusikii taarifa ya kukanusha au kukubali kuwepo kwa uzalishaji wa bidhaa chini ya kiwango. Tumekuwa tukishuhudia bidhaa zinazotoka nje zikiteketezwa mara baada ya kugundulika! Sasa suala la kujiuliza je, mpaka bidhaa hizi zimeingizwa nchini chombo hiki kinakuwa wapi mpaka msako ufanyike madukani na wakati bidhaa hizo zimekwishauzwa kwa watumiaji?

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuishauri Serikali kulifanyia kazi suala hili ili kuondosha hasara kwa wananchi wetu na vile vile kuwalinda dhidi ya kupoteza maisha yao wakiwa kazini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nina imani kuwa viwanda vyetu vinaendeshwa na watu makini na wenye uchungu na nchi yao. Hivyo basi, namwomba Mheshimiwa Waziri mwenye dhamana alishughulikie suala hili kwa umakini mkubwa sana vinginevyo Tanzania tutajikuta kila siku tunakuwa wachuzi na si wafanyabiashara. Tutakuwa mstari wa mbele kuuza bidhaa ambazo zimetengenezwa na wengine na si bidhaa iliyotengenezwa na Mtanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba wakati wa hitimisho, Mheshimiwa Waziri anipe jibu juu ya suala muhimu la chombo hiki cha kuhakiki ubora, TBS.

MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nami napenda kuchangia hotuba hii ya Mheshimiwa Waziri kama ifuatavyo kuhusu EPZ na SEZ.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, kiasi cha kuwekeza katika Special economic zone ni kiwango kikubwa sana hasa kwa wawekezaji wa ndani, kiwango cha milioni mia moja ni kikubwa kwa kuanzia na ni kiwango cha kibaguzi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, Sheria hizi za SEZ zinalenga kukuza soko la nje na la ndani je, linatazamwa kwa jicho lipi, tunavyosema 80% ya bidhaa zote zitakazozalishwa ziuzwe nje ya nchi ni asilimia kubwa sana hasa kwa wawekezaji wa ndani na hata wa nje pia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kule Kigoma zimetengwa hekta takribani elfu 300 kwa ajili ya SEZ na miongoni mwa mambo yanayopelekea wawekezaji waje wawekeze ni pamoja na sekta ya miundombinu, pamoja na uhakika wa umeme. Cha ajabu Kigoma tunatumia generator, hali ambayo haimvutii Mwekezaji kuja kuweka kiwanda. Je, hii dhana ya kutenga maeneo ilihali tunajua hatuna umeme wa uhakika hatuoni kama ni kiini macho?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, kuna huu mkakati wa Wilaya moja, bidhaa moja, sidhani kama umefanyiwa promotion ya kutosha na ni wananchi wachache sana kwenye Wilaya zao wanalijua na kulifanyia kazi mkakati huu. Kwa mfano, Wilaya au Manispaa ya Kigoma-Ujiji imepangwa mawese, lakini zao la mawese linaweza kutoa bidhaa mbalimbali kama zifuatazo:-

Mawese, mafuta ya mise, chakula cha mifugo, zinatengeneza sabuni zijulikanazo kama Vifwebe, pia mafuta ya mawese yakiyeyushwa yanatoa Korie au mafuta safi ya kula. Je, Serikali ina mpango gani dhidi ya kufanya utafiti ili tuweze kupata mafuta safi ya kula. Lakini pia bado zao hilo linatoa majani ya kuezekea nyumba, mifagio na vijiti vya chostic, je, Serikali ina mikakati gani dhidi ya zao hili?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hayo machache, naomba kuwasilisha.

MHE. SALEH A. PAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja. Napenda kumpongeza Waziri pamoja na Naibu Waziri, Katibu Mkuu, Naibu Katibu Mkuu na Wafanyakazi wote wa Wizara kwa kazi nzuri mnayoifanya.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mpango wa Taifa wa Miaka Mitano umelenga kuifanya nchi yetu kuwa Middle Income Nation. Hilo litawezekana tu iwapo tutaendeleza viwanda vidogo, vya kati na vikubwa ndivyo vitakavyotupelekea huko. Bado hatujafanya vizuri katika viwanda vikubwa hasa vile vya Base Metals. Napongeza kwa hatua ya kuanza earnestly mradi wa Liganga na Mchuchuma. Kazi hii iende kwa haraka ili tusibakie na mazungumzo tu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali itenge fedha za kutosha kwa ajili ya kuendeleza viwanda vidogo vidogo. Nchi kama India na China wamepiga hatua sana kutokana na kuimarisha viwanda, hivyo SIDO iimarishwe kwa utaalam wa rasilimali fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunaipongeza Serikali kwa kuanzisha EPZ na SEZ takriban nchi nzima. Ili hizi EPZ na SEZ ziweze kufanya kazi tunatakiwa kuwa na jitihada za makusudi za kutangaza maeneo hayo ili kuwavutia wawekezaji. Aidha, tunatakiwa kuwa strategic ili tuweze kuwavutia wawekezaji hasa maeneo ya TEHAMA. Tukichagua eneo moja linaweza kuwa Silicon Valley ya Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu Viwanda vidogo na Jimbo la Pangani. Shughuli za Jimbo langu kiuchumi ni Uvuvi na Kilimo. Tunahitaji tupatiwe viwanda vidogo vya Fish Processing na Agro Processing kama vile uchakatuaji wa mihogo, nazi na korosho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu masoko. Mkoa wa Tanga unazalisha matunda na mbogamboga, Pangani ni wakulima wakubwa wa ndizi. Je, ule mpango wa kujenga Soko la Kimataifa la matunda na mbogamboga pale Segera limefikia wapi? Taarifa tulizonazo ni kwamba feasibility study imekamilika. Je, ni kweli feasibility study imekamilika?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusu masoko ya nje na packaging. Kuna masoko ya bidhaa za Tanzania katika nchi za falme za kiarabu, lakini tatizo kubwa ni jinsi tunavyofungasha mazao yetu. Je, ni kwa kiasi gani tumewafundisha wafanyabiashara wetu katika suala hili la packaging ili kuweza kufaidi soko kubwa la Falme za Kiarabu na Mashariki ya Kati.

MHE. MUHAMMAD IBRAHIM SANYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa moja ya tatizo kubwa la kutoendelea kwa sekta ya viwanda ni kukosekana kwa umeme wa kutosha na unaopatikana masaa 24 kwa siku kwa mwaka mzima na kwa kuwa kama jitihada za kutosha zitakuwepo, basi tatizo hili ama linaweza kupungua au hata kwisha kabisa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, inasemekana kwamba umeme wa makaa ya mawe huko Nyaka unao uwezo wa kutoa 400MW.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, vile vile umeme wa upepo huko Singida unao uwezo wa kutoa 300MV na muda wa kukamilisha miradi hii iwapo itachukuliwa kwa umuhimu wake unaweza kukamilika kwa kipindi cha si zaidi ya mwaka mmoja. Wadau wa shughuli hii ni pamoja na NDC, TANESCO na POWER POOL EAST AFRICA.

Fedha za miradi hii zimekuwa approved na Exim Bank ambazo ni kiasi cha dollar US 130 millions. Uchambuzi wa kina yaani Feasibility studies tayari umeshafanyika na kubaini kuwa umeme huu wa upepo unaweza kutoa umeme kwa kiasi cha senti 15 za Marekani je, ni kitu gani hata TANESCO kushindwa kutoa kibali yaani Power Purchase Agreement ( P.P.A)

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme wa upepo ni umeme rahisi ambao ni kuchomeka mitarimbo na kuanza kazi tena kwa senti 13 – 14. Umeme wa mawe hutoa umeme kwa gharama za sio zaidi ya senti 13 za Kimarekani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, umeme wa gesi huo hutoa umeme kwa gharama za senti 10 hadi 16. Tukumbuke kwamba inasemekana umeme wa IPTL ni kutoka senti 20 hadi 22 na Diesel hutoa umeme kwa gharama ya senti 30 hadi 33.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hivyo basi, kama ni kweli kilimo kwanza kiweze kuwa na tija na kupelekea kuwa na viwanda vinavyotokana na mazao mbalimbali kama vile pamba, matunda na hata viwanda vya kusindikia nyama havitafanya kazi iwapo hatutakuwa na vyanzo vipya ya kupata umeme wa uhakika.

Biashara ni suala lingine ambalo kwa asilimia kubwa limeathiriwa na kutokuwepo umeme wa uhakika. Hivyo, umeme ndiyo roho au moyo wa kuendesha mambo yote mawili yaani Biashara na Viwanda. Kama kweli hiyo miradi ya umeme wa nguvu za upepo na wa makaa ya mawe ambao ni rahisi kwa minajili ya gharama na upepo ni bure, wakati huo huo makaa ya mawe reserve yake inasemekana tunaweza kuyatumia kwa zaidi ya miaka 500. Kama hatutatumia nafasi hizi tutaonekana ni wachawi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka ufafanuzi kwa hili.

MHE. PUDENCIANA W. KIKWEMBE: Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuchangia hoja katika maeneo yafuatayo:-

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, pamoja na mipango mizuri ya Wizara hii ya kukuza na kuendeleza viwanda, je, Serikali ina mpango gani wa kuanzisha viwanda Mkoani Katavi au Mpanda hasa vya usindikaji kwa mfano matunda na mafuta?

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, kwa kuwa viwanda vingi hasa vya nguo vilikufa na kutelekezwa, je, Serikali imefanya utafiti na kubaini ni sababu zipi zilizopelekea viwanda hivyo kufa na kutelekezwa kabla ya kuvifungua?

Mheshimiwa Mwenyekiti, tatu, je, Serikali inaongea nini kuhusu ustawi wa SIDO, kwani imetengewa pesa kidogo wakati ukizingatia kwamba ina mchango mkubwa katika kukuza uchumi? Je, Serikali haioni kwamba kwa kuipatia SIDO fedha kidogo ni kuifanya SIDO kufanya kazi chini ya kiwango chake na kuiua SIDO?

Mheshimiwa Mwenyekiti, naunga mkono hoja.

(Saa 7.17 mchana Bunge lilisitishwa mpaka saa 10.00 jioni)

(Saa 10.00 jioni Bunge lilirudia)

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, kama nilivyosema wakati tukisitisha shughuli za Bunge mchana kwamba tukirudi jioni tunaanza majumuisho. Sasa nitamwita kwa kadri mlivyokubaliana muda ni saa moja, kwa hiyo, ataanza Naibu Waziri dakika 20, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mheshimiwa Lazaro S. Nyalandu!

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, awali ya yote, namshukuru sana Mwenyezi Mungu kwa afya na kwa uzima alionipa. Kwa mke wangu mpenzi Faraja, natuma salamu za kukupenda sana na kukupenda daima dumu. Pia kwa watoto wangu wawili Sarah Divine na Christopher Aman, ninyi kwangu na kwetu ni zawadi kutoka kwa Mungu. Kwa Baba na Mama yangu mzazi napenda niseme ahsanteni sana. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa Wanajimbo wa Singida Kaskazini, napenda kutumia neno moja kwamba mimi ni ninyi, nawashukuru sana kwa imani ambayo mmenipa mara ya tatu na kwa sababu hiyo, nchi itaiona siku njema.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa upande wa Madiwani kutoka Singida ambao wametutembelea leo hapa Bungeni, naomba kuwashukuru sana na nawashukuru kwa kuja kutembelea Bunge letu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, kipekeee, naomba nimshukuru sana Rais, Mheshimiwa Dkt. Jakaya M. Kikwete, kwa kuniteua kuwa Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara na naomba kumuahidi kwamba nitaifanya kazi hii aliyonituma kwa moyo mkunjufu na wa uhodari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimshukuru Waziri Mkuu Mheshimiwa , Mbunge. Mheshimiwa Waziri Mkuu namshukuru sana kwa uongozi wake, sisi Mawaziri na Manaibu Waziri wake, tuna imani kubwa sana naye na tunampenda sana. Kwa Mheshimiwa Waziri wangu Mheshimiwa Dkt. Cyril A. Chami, nakushukuru sana kwa nafasi ya kufanya kazi pamoja, najifunza mambo mengi sana kutoka kwako na uzoefu uliokuwa nao katika Wizara kama Naibu Waziri, umeendelea kunisaidia na mimi kusonga mbele.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pia namshukuru sana Katibu Mkuu, Ndugu Joyce Mapunjo pamoja na Naibu Katibu Mkuu Dkt. Shabaan. Nawashukuru watumishi wote katika Wizara yetu. Naomba nitoe shukrani zangu kwa mashujaa wa Wizara ambao ni watumishi wote wa Wizara ya Viwanda na Biashara popote mlipo na popote mnaponisikiliza. Naomba niwashukuru Wakuu wa Idara zote, Wakuu wa Mashirika yote ya Umma yaliyo chini ya Wizara, sisi sote Wizarani kwa kweli ningetumia neno la kigeni niseme we are proud of you! Kwa kweli tunawashukuru sana kwa kazi ambayo mnaifanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja hii. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kipekee niwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote kwa ujumla wenu na mmojammoja. Wale ambao mmechangia kwa maandishi, mimi na Mheshimiwa Waziri tumesoma andishi la kila aliyeandika, tumesoma kila pendekezo, tumesoma kila ushauri na tunawahakikishia kwamba kila mlichokisema, yote yatazingatiwa na Wizara yangu. Naomba nichukue nafasi hii kuwashukuru Wabunge wote ambao wamechangia kwa kuzungumza, tumeona imani waliyonayo katika Wizara yetu, tumeona mapendekezo mazuri waliyotupa na sisi kama Wizara tunayachukua na tutayafanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, wengi wamezungumzia hoja ya kuwa na mapinduzi ya viwanda Tanzania na kuifanya Tanzania iwe nchi ya viwanda vya kati kufikia mwaka 2025 kama ilivyo Dira ya Taifa. Serikali inakubaliana nao kabisa, ni azma ya Serikali hii kwa kupitia Wizara ya Viwanda na Biashara kuleta mapinduzi ya kweli ya viwanda, kuanzisha viwanda vidogovidogo vingi chini ya SIDO, kuanzisha viwanda vikubwa chini ya mfumo maalum ya EPZ na kuendelea kuwavutia wawekezaji wakubwa ambao wataleta mitaji yenye ushindani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Wizara kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa yaani NDC, imeazimia kujikita katika kuzalisha umeme kama sehemu ya kufanikisha azma ya mapinduzi ya viwanda kwa sababu wote tunafahamu pasipo umeme viwanda vyote vitafungwa na hakuna uzalishaji wowote utakaofanyika. Hadi sasa tunafahamu 41% ya nishati ya umeme duniani inatokana na makaa ya mawe. Nchi ya Afrika Kusini peke yake 93% ya umeme inaotumia ni wa makaa ya mawe, wakati nchi ya China ni takribani 80%. Mungu ametujalia Tanzania kuwa na hifadhi kubwa ya makaa ya mawe katika maeneo makubwa 17 na wataalam wanasema ujazo au wingi wa makaa ya mawe ya Tanzania yanakadiriwa kuwa tani bilioni moja na milioni laki mbili.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hadi sasa eneo la Mchuchuma, Katewanga, Sangwe, Kiwira na Ngaka ndiyo maeneo ambayo tayari yamefanyiwa uchunguzi na yanajulikana. Nishati ya makaa ya mawe ni bei nafuu sana kupita maji, ni bei nafuu sana kupita mitambo ya kufulia umeme, ni bei nafuu sana kupita nishati nyingine nyingi na NDC itaendeleza Mradi wa Makaa ya Mawe wa Ngaka, Mbinga. Inatarajiwa hivi karibuni kuanza kujenga Power Station ya megawatt 120 katika eneo la Ngaka. Tutatafuta dola za Kimarekani milioni 46 kwa ajili ya kujenga transmission line kutoka Songea mpaka Ngaka ili tuweze kuanza awamu ya kwanza mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, eneo la Mchuchuma na Linganga linakadiriwa kuzalisha megawatt 600 na Chuma cha Liganga kiweze kuleta mapinduzi makubwa ya viwanda mama katika eneo la uwekezaji la Corridor ya Mtwara. Mwekezaji ameteuliwa na Serikali kupitia NDC tayari wanaendelea kufanya mazungumzo ya mwisho kabla ya kusaini makubaliano ya mwisho.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Mungu amewajalia watu wa Singida kwa kitu kinachoitwa upepo mkali, kwa lugha ya Kingereza wanaita strong wind. Wale wanaochunga ng’ombe wanafahamu, unapochunga ng’ombe nguo yako inaweza ikapasuliwa na upepo mkali wa Singida. Shirika la Taifa la Maendeleo la NDC kwa kushirikiana na Power Pool East Africa ambayo ni kampuni ya wazawa, kwa kushirikiana na mbia mwingine ambaye anaitwa TANESCO, wameazimia kwa pamoja kuzalisha megawatt 300 za umeme Singida. Kwa kutumwa na Waziri wangu niliongoza mazungumzo kati ya NDC na Benki ya Exim ya China huko Beijing miezi ya hivi karibuni, tukafikia makuliano ya uwekezaji wa dola milioni 136 ambazo zitatumika kwa ajili ya mradi huu pale Singida. Kilichobaki ni jambo moja tu, PPA Term Sheet ya Power Purchase Agreement na hii iko mbele ya dawati na Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO na Serikali inasisitiza isainiwe haraka ili huu umeme ambao utagharimu senti 13 ambao ni wa bei rahisi na ni endelevu uweze kuanza mara moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hali kadhalika Waheshimiwa Wabunge wengi wamechangia juu ya ufinyu wa bajeti ya Wizara yetu, Ufinyu wa bajeti ya Taasisi zake kama vile SIDO na CAMATEC, maeneo ambayo lazima tuwalipe wananchi ya EPZ, FCC, TEMDO, TBS, BRELA na kadhalika. Nakubaliana na Waheshimiwa Wabunge hao na Wizara yangu inaona haja ya kuwashirikisha wafanyabishara wetu wote humu nchini katika suala zima la kupanua wigo wa mapato. Ni lazima na ni muhimu wafanyabiashara wote kama vile sisi, yaani kwa wale wanaokwenda Kanisani, kuna mtu alikwenda Kanisani akatoa senti moja kama sadaka na mwingine ambaye ni tajiri alikwenda akatoa asilimia yake kama sadaka na yule mkubwa aliyekuwa anaangalia akasema hakika yule aliyetoa kidogo alitoa kwa moyo mkubwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tunachotaka kusema hapa ni kwamba tutaijenga nchi yetu kwa sisi wote kuungana na kwa kila mtu kutekeleza wajibu wa kuwa sehemu ya maendeleo ya nchi hii. Kwa kipato chako unachokipata kila Mtanzania tukianza na wale ambao wamejaaliwa vingi kwao vingi vinahitajika na Wizara yetu itashirikiana na TRA na Wizara ya Fedha ili kuhakikisha kwamba wafanyabiashara wote ambao wana mpango wa aina yoyote ya kukwepa kodi ya Serikali hawataweza kufanya hivyo, watachukuliwa hatua za kisheria na tutahakikisha kwamba mapato ya Serikali yanalindwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Wizara yetu tumeangalia mpango unaoitwa SME Base Line Survey ambao ulifanywa kati ya Wizara ya Viwanda na Biashara wakishirikiana na Benki ya Dunia, mpango uliofadhiliwa na Benki ya Dunia ujulikanao kama Financial Deepening Trust, wakafanya tathmini. Jambo la kwanza walikuwa wanaangalia je, kuna enterprises ngapi Tanzania, SME ambazo zinafanya biashara zake za kila siku, ambazo zina ambazo zinalipa mishahara watu wao kila mwezi. Ili tuendelee kuwafahamu hao watu kwanza tuwasaidie, wasitukimbie. Wafanyabiashara wengine wakiona TRA wanakimbia lakini TRA iko hapa kukusaidia na hakika itakutaka na wewe ulipe kile ambacho ni cha Kaisari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika survey hii iliyofanyika ambayo itachapishwa na Wizara yetu muda si mrefu, katika nchi ya Tanzania kuna wajasiriamali wenye kazi zao na makampuni yao madogomadogo hapa nchini ambao wameajiri watu wanafanya kazi zao kila siku, wengine wako Tandahimba, Kilimanjaro, Maswa, Temeke na nchi nzima milioni 2.7, hizi ni SME zinazofanya kazi katika nchi ya Tanzania. Tathmini hii imeonyesha kuna SME zinazoongozwa na wanawake milioni 1.5, akina mama oyee! (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, milioni 1.2 zinaongozwa na wanaume na tulipofanya uchunguzi tumejua 53% ya biashara ndogondogo zote katika Tanzania zinajihusisha na masuala ya trade yaani kununua hapa na kuuza pale. 43% wanajihusisha na biashara mbalimbali zinazojulikana kama service industry yaani huduma mbalimbali. 4% wanajishughulisha na uzalishaji wa viwanda vidogovidogo, lakini cha muhimu jumla wameajiri watu milioni 4.5, watu hawa wameajiriwa moja kwa moja katika hizi shughuli ambazo zinasimamiwa na Idara ya Biashara Ndogondogo na Viwanda Vidogovidogo katika Wizara yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, ni lazima tuongeze idadi ya watu ambao wanashiriki katika kulipa kodi ijulikanayo kama Pay as you Earn ili pato la nchi liongezeke. Kuna mtu alizungumzia habari ya Sungura, tunataka kuhakikisha kwamba pato la Taifa kwa kupitia viwanda na biashara kwa kuhimiza watu wetu wanaofanyabiashara na wanaopata faida waweze kuchangia katika Mfuko Mkuu wa Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana nchi ya Tanzania ikiwa ni moja ya nchi zinazoongoza hapa Afrika, tuliweza kusajili watu wanaofikia milioni 20 wenye simu za mkononi ambao wanatumia fedha katika kuzungumza na kufanya biashara. Hadi kufikia mwaka huu, tumefikia watu millioni 41 ambao inakadiriwa kuwa idadi ya Watanzania. Tunaweza tukaongeza wigo wa kodi. Natoa wito kwa wafanyabiashara wote Tanzania tusikimbie TRA, tutahakikisha kwamba mkusanya kodi anakuwa rafiki wa yule anayetoa kodi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, vitabu viliandika na ni jambo ambalo naliangalia kila siku nikiamka. Watu wengi wanasema kwa sababu ya unyonge wangu na udhaifu wangu basi mimi nisitoe kodi kwa sababu biashara yangu imeajiri watu watano tu, basi isilipe kodi lakini tukaambiwa, yeye ambaye ni mnyonge na aseme mimi nina nguvu na yeye ambaye ni maskini na aseme mimi ni tajiri. Sisi kama Chama cha Mapinduzi mwaka 1977 tulianza kuimba wimbo unaosema ‘Mapinduzi ungali mtoto mdogo, nimepewa nikulinde upate makao’. Nchi yetu ya Tanzania imefikisha miaka 50 na naamini tutapiga hatua katika kuongeza Mapinduzi siyo tu ya viwanda vikubwavikubwa, siyo tu ya viwanda vya kati bali kuendeleza biashara ndogondogo, kuendeleza viwanda vidogovidogo na kuhakikisha sisi wote tunakuwa wazalendo, tunatoa kile ambacho ni cha Kaisari.

Mheshimiwa Mwenyekiti, uzalendo ni jambo la muhimu. Kama tutaendelea kuwaambia watoto wa Tanzania kwamba ninyi ni maskini watakua na watafikisha miaka 20 au 50 wakiamini kwamba bado wao ni maskini. Wizara yangu inaamini ni wakati wa kuhakikisha tunamwambia kila Mtanzania wewe unaweza na kumwambia kila mtoto kwamba wewe una nafasi ya kuijenga nchi hii na kuhakikisha inakua.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 1884, mtunzi maarufu anayekumbukwa na dunia nzima aliandika The Star Spangled Banner, wimbo ambao ulikuja kuchukuliwa kama wimbo wa Taifa la Marekani, anaitwa Bwana Francis Mchenry. Alifikiria maneno ya kutunga, akaiambia Marekani katika maneno aliyoyatunga akasema, ‘America the land of the free and the home of the brave’. Nchi hii ni nchi ya watu walio huru lakini pia naamini kwamba ni nchi ambayo ni ya watu wenye uwezo ndiyo maana Dar es Salaam ikajulikana kama Bongo Country yaani ni nchi ya watu wanaofikiri, ni nchi ambayo wamefanikiwa katika mambo mengi. Naamini na kila mtu na aseme mimi nina nguvu!

Mheshimiwa Mwenyekiti, kijiji kimoja katika Jimbo langu kinaitwa Msange waliniambia haiwezekani tena sisi Wanyaturu wa Msange tukajulikana kwamba tunakaa kwenye nyumba za Tembe, wakaanzisha ‘operation ondoa Tembe Singida’. Naweza nikakuhakikishia, vijana wengi kabla hawajaoa katika kijiji cha Msange na maeneo mengine ya Ilongero na Mtinko wameanza kujenga nyumba za bati kwa sababu wanaamini kwamba wanaweza. Kwa sababu wanaamini kwamba wanapozalisha wanajifunza kuweka akiba. Nchi hii itasogea mbele tutakapochukua wajibu sisi wenyewe kama wananchi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mambo mengi yamezungumzwa na mengi ni mazuri, niwahakikishie Waheshimiwa Wabunge na nimuhakikishie Mheshimiwa Martha Mlata alipozungumzia sana juu ya suala la COSOTA. Namwambia aunge mkono hoja kwa sababu Serikali na Wizara hii itahakikisha haki za wasanii zinalipwa sambamba na hizo haki kulipwa tutahakikisha kwamba kodi ya Serikali inalipwa katika hati miliki zote ambazo tutazisimamia. Tunaangalia uwezekano wa kuiboresha upya Bodi ya COSOTA na tutahakikisha kwamba katika yote yatakayofanyika tunamlinda msanii wa Tanzania afaidike na kazi ambayo tunaifanya na tunaangalia uwezekano wa kushirikiana na vyombo vingine vya dola ikiwepo TRA kuhakikisha kwamba siyo tu kwamba tutawalinda lakini kama nilivyosema hapo mwanzo na wao watachangia katika pato la Taifa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimalizie kwa kusema yafuatayo. Mambo mengi yamezungumzwa, katika Idara yetu ya Masoko kuanzia Mwenyekiti wa Kamati na Msemaji Mkuu wa Kambi ya Upinzani, tumesikiliza na tutatekeleza. SIDO kama nilivyosema hapo mwanzo imetengewa fedha ambazo na sisi tunaamini kwamba hazitoshi lakini napenda niseme kwamba licha ya quotation ambapo walisema SIDO imepewa shilingi bilioni 1.7 peke yake, naomba niseme kwamba zipo vilevile shilingi bilioni 4.5 ambazo ni kwa ajili ya Programu ya Uongezaji wa Thamani Mazao yaliyoteuliwa nchini chini ya Mradi wetu wa Wilaya moja Zao Moja.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tutaendelea katika mpango maalum wa kuhakikisha kwamba wawekezaji wa Economic Processing Zones (EPZ) wanapata nafasi ya kuwekeza na Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya kuhakikisha kwamba tunalipia maeneo ambayo tumeyahodhi katika Wilaya mbalimbali. Tumeona katika michango ya Waheshimiwa Wabunge wengi ambao wametuambia kwamba ni lazima yale maeneo yalipiwe. Nakubaliana na Waheshimiwa Wabunge na naomba niseme kwamba Serikali iko katika mkakati wa mwisho kabisa kuhakikisha tunapata fedha maalum kwa ajili ya kulipia madeni mengi sana ambayo yatatuwezesha kushika maeneo ya EPZs.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tulisema katika kusimamia vizuri bidhaa zinazoingia nchini, bidhaa ambazo tutahakikisha ubora wake chini ya Tanzania Bureau of Standards (TBS), tunaanzisha mpango maalum wa kuweza kuzikagua bidhaa hizi huko ziliko kabla hazijaja nchini kwetu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kuunga mkono hoja. Nawashukuru sana Waheshimiwa Wabunge na yale yaliyobaki naomba nimwachie Mheshimiwa Waziri wangu aendelee nayo. (Makofi)

MWENYEKITI: Ahsante sana, umemwachia mengi mno. Sasa nitamwita Mheshimiwa Waziri mtoa hoja ili aweze kufanya majumuisho. Mheshimiwa Waziri, Dkt. Cyril Chami. (Makofi)

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza kabisa, napenda kuchukua nafasi hii kutoa shukrani zangu za dhati kwako wewe binafsi na kwa Waheshimiwa Wabunge wote kwa kunisikiliza bila kuchoka wakati nilipokuwa nawasilisha makadirio ya Wizara yangu kwa mwaka wa 2011/2012. Aidha, napenda kuchukua fursa hii kuwapongeza Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwa njia ya maandishi na kwa kuzungumza katika Bunge lako Tukufu, kwa nia ya kuboresha utekelezaji wa malengo tuliyojiwekea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, pili, napenda kuchukua nafasi hii kuwashukuru Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa, Mbunge wa Mufindi Kaskazini, Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara; Mheshimiwa Eng. , Mbunge wa Viti Maalum (CCM), Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara na Wanakamati wote wa Kamati hii ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Biashara, kwa ushauri wao utakaosaidia kuendeleza sekta ya Viwanda na Biashara.

Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru pia Mheshimiwa Lucy Fidelis Owenya, Mbunge Viti Maalum (CHADEMA), Waziri Kivuli wa Viwanda na Biashara; kwa kutoa maoni mazuri yatakayosaidia kujenga Sekta ya Viwanda na Biashara. Vilevile namshukuru sana akiwa Msemaji wa Kambi ya Upinzani katika Wizara yangu kwa mawazo ya ufasaha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tumepokea pongezi nyingi za utendaji wa Wizara kutoka kwa Waheshimiwa Wabunge. Tunazipokea pongezi hizo kwa unyenyekevu na tunaahidi kwamba tutaendeleza mafanikio yaliyopatikana na ule upungufu uliojitokeza tutajitahidi kuurekebisha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, napenda kuwashukuru Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia hoja zinazohusu Wizara yangu kwa maandishi na kwa kauli wakati wakichangia katika hotuba za bajeti za Wizara mbalimbali. Michango yao itasaidia sana kuendeleza Wizara yangu. Michango ya Waheshimiwa Wabunge ni mingi na muhimu na hivyo inahitaji majibu ya kina. Kwa muda mfupi nilionao majibu yangu yataelekezwa katika maeneo makuu yaliyochangiwa kama nilivyoyataja hapo juu. Hata hivyo, nawahakikishia Waheshimiwa Wabunge wote waliochangia kwamba baadhi ya majibu yameelezwa kwa ufasaha katika vitabu vilivyosambazwa pamoja na hotuba ya bajeti ya Wizara. Vitabu hivyo ni pamoja na ‘Mkakati wa kuvikuza, kuviendeleza na kuvilinda Viwanda vya ndani vyenye uzalishaji mkubwa wa bidhaa’. Ukikiangalia utapata majibu mengi sana ya maswali ambayo Waheshimiwa Wabunge wanayo. Kitabu cha pili ni ‘Taarifa ya ufuatiliaji wa viwanda vilivyobinafsishwa ambavyo havijaendelezwa kwa mujibu wa mikataba ya mauzo’. Kitabu cha tatu ni ‘Mafanikio ya Sekta ya Viwanda na Biashara katika Utawala wa Serikali wa Awamu ya Nne na Kitabu cha Nne ni ‘Mpango wa Utekelezaji wa Kilimo Kwanza wa Wizara ya Viwanda na Biashara’.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nawasihi Waheshimiwa Wabunge wasome vitabu hivi ambavyo vitawapa maelezo ya kina kuhusu masuala hayo. Aidha, majibu ya kina yanayojibu kila hoja iliyotolewa yameandaliwa kwa maandishi na yatagawiwa kwa Waheshimiwa Wabunge wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja na michango iliyotolewa na Waheshimiwa Wabunge katika kujadili hotuba yangu inaonesha nia thabiti ya ushirikiano na Wizara yangu katika kuziendeleza Sekta za Viwanda na Biashara na kusukuma mbele gurudumu la maendeleo ya Taifa. Nimefarijika sana na mambo mawili. Jambo la kwanza ni kwamba Waheshimiwa Wabunge wote wamekubaliana na mimi kuhusu umuhimu wa Sekta hii ya Viwanda na Biashara. Michango mingi iliyotolewa kwa kweli ni kusema kwamba bila viwanda na biashara, nchi yetu haiwezi kupiga hatua na ndilo ambalo nilikuwa nasema katika bajeti yangu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, la pili, ni kutetea kwa nguvu zote maslahi ya Taifa na wananchi tunaowawakilisha hapa Bungeni. Hoja zote zinalenga katika kuboresha mambo ambayo kwa kweli yakiboreshwa basi tutakuwa tunainua maisha ya Watanzania wote.

Mheshimiwa Mwenyekiti, jumla ya Waheshimiwa Wabunge 161 walichangia hoja zinazohusu Wizara yangu wakati wakichangia hotuba ya bajeti ya Wizara hii. Aidha, jumla ya Waheshimiwa Wabunge 28 walichangia hotuba yangu kwa kauli na Waheshimiwa Wabunge 133 walichangia kwa maandishi.

Waheshimiwa Wabunge waliochangia hoja yangu kwa kauli ni Mheshimiwa Lazaro Samuel Nyalandu, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara; Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa, Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda na Biashara; Mheshimiwa Lucy Fidelis Owenya, Msemaji wa Kambi Rasmi ya Upinzani; halafu anafuata Mheshimiwa Hasnain Mohamed Murji, Mbunge wa Mtwara Mjini; Mheshimiwa Gaudence Cassian Kayombo; Mheshimiwa Maida Hamad Abdallah; Mheshimiwa Mch. Luckson Ndaga Mwanjale na Mheshimiwa Betty Eliezer Machangu. (Makofi)

Wengine ni Mheshimiwa Nyambari Chacha Mariba Nyangwine; Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina; Mheshimiwa Deogratias Aloyce Ntukamazina; Mheshimiwa Richard Mganga Ndassa; Mheshimiwa Naomi Amy Mwakyoma Kaihula; Mheshimiwa Ismail Aden Rage; Mheshimiwa Ahmed Ali Salum; Mheshimiwa Kapt. John Damian Komba; Mheshimiwa Hussein Nassor Amar; Mheshiwa Deo Haule Filikunjombe na Mheshimiwa Murtaza Ally Mangungu. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge waliochangia kwa maandishi ni hawa wafuatao. Mheshimiwa Pereira Ame Silima; Mheshimiwa Khatib Said Haji; Mheshimiwa Augustino Manyanda Maselle; Mheshimiwa Haji Khatib Kai; Mheshimiwa Amos Gabriel Makalla; Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu; Mheshimiwa Suleiman Nassib Omar; Mheshimiwa Abuu Hamoud Jumaa; Mheshimiwa Moshi Suleiman Kakoso; Mheshimiwa Mendrad Lutengano Kigola; Mheshimiwa Dkt. Abdallah Omar Kigoda; Mheshimiwa Hussein Nassor Amar; Mheshimiwa Martha Jachi Umbulla; Mheshimiwa Hawa Abdulrahman Ghasia; Mheshimiwa Godfrey Weston Zambi; Mheshimiwa Anne Kilango Malecela na Mheshimiwa Mhonga Said Ruhwanya. (Makofi)

Wengine ni Mheshimiwa Susan Limbweni Aloyce Kiwanga; Mheshimiwa Dkt. Mary Machuche Mwanjelwa; Mheshimiwa Said Amour Arfi; Mheshimiwa Herbert James Mtangi; Mheshimiwa AnnaMaryStella John Mallac; Mheshimiwa Ali Khamis Seif; Mheshimiwa Ritta Enespher Kabati; Mheshimiwa Eng. Ramo Matala Makani; Mheshimiwa Dkt. Fenella Ephraim Mukangara; Mheshimiwa Regia Estalatus Mtema; Mheshimiwa Rebecca Michael Mngodo; Mheshimiwa Kabwe Zubeir Zitto na Mheshimiwa Diana Mkumbo Chilolo. (Makofi)

Wengine ni Mheshimiwa Hamad Ali Amour; Mheshimiwa Victor Kilasile Mwambalaswa; Mheshimiwa Jasson Samson Rwekiza; Mheshimiwa Benedict Ngalama Ole- Nangoro; Mheshimiwa Mohamed Hamisi Missanga; Mheshimiwa Felister Aloyce Bura; Mheshimiwa Ignas Aloyce Malocha; Mheshimiwa Dkt. Maua Abeid Daftari; Mheshimiwa Mariam Reuben Kasembe; Mheshimiwa Stephen Hilary Ngonyani; Mheshimiwa Kapt. John Damiano Komba; Mheshimiwa Haji Juma Sereweji; Mheshimiwa Esther Amos Bulaya; Mheshimiwa Dkt. Charles John Tizeba; Mheshimiwa Slyvester Massele Mabumba; Mheshimiwa Mch. Israel Yohana Natse; Mheshimiwa Prof. Kulikoyela Kanalwanda Kahigi; Mheshimiwa Stephen Masatu Wasira; Mheshimiwa Modestus Dickson Kilufi; Mheshimiwa Christowaja Gerson Mtinda na Mheshimiwa Gaudence Cassian Kayombo. (Makofi)

Wengine ni Mheshimiwa Vick Paschal Kamata; Mheshimiwa Mahmoud Hassan Mgimwa; Mheshimiwa Fatuma Abdallah Mikidadi; Mheshimiwa Saidi Ramadhani Bwanamdogo; Mheshimiwa Esther Nicholas Matiko; Mheshimiwa Fakharia Khamis Shomar; Mheshimiwa Anastazia James Wambura; Mheshimiwa Dkt. Kebwe ; Mheshimiwa David Ernest Silinde; Mheshimiwa Anthony Gervase Mbassa; Mheshimiwa Sabreena Hamza Sungura; Mheshimiwa Saleh Ahmed Pamba na Mheshimiwa Muhammad Ibrahim Sanya. (Makofi)

Wengine ni Mheshimiwa Nyambari Chacha Mariba Nyangwine; Mheshimiwa Pudenciana Wilfred Kikwembe; Mheshimiwa ; Mheshimiwa Rajab Mbarouk Mohammed; Mheshimiwa Diana Mkumbo Chilolo; Mheshimiwa Agness Elias Hokororo; Mheshimiwa Dkt. Lucy Sawere Nkya; Mheshimiwa Rukia Kassim Ahmed; Mheshimiwa Eustace Osler Katagira; Mheshimiwa Kombo Khamis Kombo; Mheshimiwa Said Mussa Zubeir; Mheshimiwa Faida Mohammed Bakar; Mheshimiwa Abdul Jabiri Marombwa; Mheshimiwa Jenista Joakim Mhagama; Mheshimiwa Gosbert Begumisa Blandes; Mheshimiwa Philipo Augustino Mulugo; Mheshimiwa Balozi Seif Ali Idd; Mheshimiwa Selemani Saidi Jafo; Mheshimiwa Salome Daudi Mwambu; Mheshimiwa Yussuf Haji Khamis na Mheshimiwa Eugen Elishininga Mwaiposa. (Makofi)

Wengine ni pamoja na Mheshimiwa John John Mnyika; Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi; Mheshimiwa Azza Hillal Hamad; Mheshimiwa Juma Othman Ali; Mheshimiwa Mkiwa Adam Kimwanga; Mheshimiwa Amina Andrew Clement; Mheshimiwa Asha Mshimba Jecha; Mheshimiwa Abia Muhama Nyabakari; Mheshimiwa Susan Anselm Jerome Lyimo; Mheshimiwa Mussa Khamis Silima; Mheshimiwa Salim Hemed Khamis; Mheshimiwa Amina Mohamed Mwidau; Mheshimiwa Fatuma Abdallah Mikidadi; Mheshimiwa Luhaga Joelson Mpina; Mheshimiwa James Daudi Lembeli; Mheshimiwa Deogratias Aloyce Ntukamazina; Mheshimiwa Jitu Vrajilal Soni; Mheshimiwa Augustino Manyanda Massele; Mheshimiwa Mwanamrisho Taratibu Abama; Mheshimiwa Maryam Salum Msabaha; Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya; Mheshimiwa Ramadhani Haji Saleh; Mheshimiwa Mariam Salum Mfaki na Mheshimiwa Conchesta Leonce Rwamlaza. (Makofi)

Wengine ni Mheshimiwa Albert Obama Ntabaliba; Mheshimiwa John Paul Lwanji; Mheshimiwa Naomi Mwakyoma Kaihula; Mheshimiwa Haroub Muhammed Shamis; Mheshimiwa Elzabeth Nkunda Batenga; Mheshimiwa Shaffin Ahmedali Sumar; Mheshimiwa Salum Khalfan Barwany; Mheshimiwa Martha Moses Mlata; Mheshimiwa Zaynab Matitu Vullu; Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi; Mheshimiwa Mussa Hassan Mussa; Mheshimiwa Mary Pius Chatanda; Mheshimiwa Eng. Stella Martin Manyanya; Mheshimiwa Deo Haule Filikunjombe; Mheshimiwa Aliko Nikusuma Kibona na Mheshimiwa Hussein Mussa Mzee. (Makofi)

Wengine ni pamoja na Mheshimiwa Martha Moses Mlata, tena; Mheshimiwa Gregory George Teu; Mheshimiwa Moza Abedi Saidy; Mheshimiwa Lolesia Jeremiah Maselle Bukwimba; Mheshimiwa Magdalena Hamis Sakaya; Mheshimiwa Pindi Hazara Chana; Mheshimiwa Mariam Nasoro Kisangi; Mheshimiwa Dkt. Binilith Satano Mahenge; Mheshimiwa Dkt. William Augustino Mgimwa na Mheshimiwa Riziki Said Lulida ambaye kwa kweli alichangia kwa kuzungumza, namwomba radhi sana. (Makofi)

MWENYEKITI: Mheshimiwa Sylvester Maselle Mabumba naye alichangia kwa kusema.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti wa Bunge, nakuomba radhi, naona hapa nimekusahau lakini nakiri kwamba alichangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nianze kujibu. Kwanza ziko hoja za jumla ambazo zimesemwa hapa na Waheshimiwa Wabunge ambao walitaka napokuja kutoa majumuisho nitoe tamko. Tamko kubwa ambalo limesemwa na Waheshimiwa Wabunge wengi ni la bei ya Pamba. Waheshimiwa Wabunge wengi wanataka Waziri wa Viwanda anapozungumza hapa aseme kuhusu suala la bei ya Pamba.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Waziri, zile dakika zako sasa ndiyo zinaanzia hapo.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Naam?

MWENYEKITI: Dakika zako ndiyo zinaanzia hapo kwa sababu zile za kusoma majina hatuzihesabu.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili la bei ya Pamba kwanza niseme tu kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu alilitolea maelezo hapa wakati wa maswali ya papo kwa papo na alichosema ni kwamba bei ya Pamba inakuwa determined na bei katika soko la dunia. Hakuna mtu anapanga bei ya Pamba. Mara nyingi bei ya Pamba katika soko la dunia ikishaonesha kwamba imepanda na bei hapa inapanda, bei ikishuka katika soko la dunia na bei hapa inashuka. Sasa wadau wa Pamba walipokutana Mwanza siku za karibuni na wakaona bei ya Pamba duniani iko juu, walichofanya ni kwamba walitoa ile bei elekezi ya shilingi 1,100/= jambo ambalo lilikuwa ni uamuzi mzuri tu kutokana na bei ya Pamba ilivyokuwa wakati ule lakini mara baada ya tangazo lile walipotoka Mwanza sasa bei ya Pamba duniani ikashuka ghafla. Kwa hiyo, baada ya bei kushuka ghafla wale ambao wanafanya kazi ya kununua ile Pamba wakawa hawawezi kununua kwa ile bei elekezi kwa sababu wanajua wakija kuuza katika soko la dunia hawatapata bei ile ambayo walikuwa wanaifikiria mwanzoni. Kwa hiyo, kutokana na suala hilo imekuwa ni tatizo kubwa kweli.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka niungane na Waheshimiwa Wabunge wanaotoka maeneo yanayolima Pamba kusema kwamba kwa kweli ni tatizo kubwa katika maeneo yale. Mheshimiwa Waziri Mkuu, akatoa maelekezo kwa bodi ya Pamba na wadau wa Pamba kwamba wakutane mara moja waweze kuangalia suala hilo na waweze kutoa mapendekezo yao yaletwe Serikalini pamoja na mapendekezo ya mazao mengine ambayo yanapata matatizo kama hayo. Haikutosha, Mheshimiwa Waziri Mkuu ameunda tena Tume Maalum ya kushughulikia suala hilo. Hadi sasa hivi Tume ile iko kazini na hadi sasa sijapata majibu yake kwamba imepata nini.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nataka niwaombe subira wananchi wote wanaolima Pamba Tanzania kwamba Waheshimiwa Wabunge wao wameshafanya kazi ile ya kuleta kilio chao Serikalini na Serikali imekipokea ni kilio halali kwamba bei ya Pamba imeshuka kutoka shilingi 1,100/= mpaka shilingi 800/= kwa kilo. Japokuwa soko la dunia ndilo linafanya hivyo, ushauri wa Wabunge na kilio chao kwamba Serikali isiachie hali hiyo ikae hivyo kimepokelewa Serikalini na ndiyo maana Mheshimiwa Waziri Mkuu ameunda Tume. Nataka niwahakikishie kwamba Tume ile ikileta taarifa yake, Mheshimiwa Waziri Mkuu atawasiliana na wadau wote wa Pamba na atawaeleza tumefikia wapi. Mimi navyojua ni kwamba ushauri mwingi wa Waheshimiwa Wabunge ambao wanatoka katika maeneo yanayolima Pamba utazingatiwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna ushauri kwamba tutafute namna yoyote labda ya kuweka tuseme bima (insurance) ya aina fulani hivi ya kuwafanya wale wanaonunua Pamba kule waweze kuwa na amani wakijua kwamba wakinunua Pamba ile wanaweza wakaiuza baadaye kwa bei ambayo ni ya juu zaidi. Sasa huu ni ushauri ambao umetolewa, utafikiriwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Waheshimiwa Wabunge wametoa hata mapendekezo kwamba pengine benki fulani hivi zishauriwe kutoa fedha kwa ajili ya kununua Pamba hiyo kwa sababu ni aina fulani hivi kama ya stakabadhi ghalani. Ushauri huo utafuatiliwa. Sina hakika kama kwa kipindi cha muda mfupi linaweza likafanyiwa kazi, lakini ni ushauri mzuri ambao tumeupokea.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka niwaombe Waheshimiwa Wabunge wote wa maeneo ya Pamba waendelee kutoa ushauri wa aina mbalimbali, tutachanganya na ushauri wa Tume ambayo imeundwa na Mheshimiwa Waziri Mkuu ili baadaye Mheshimiwa Waziri Mkuu akija kutoa kauli hapa iwe ni kauli ambayo inatenda haki kwa watu wote; wakulima na wale ambao wananunua Pamba lakini vilevile na Serikali.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, nisingependa nitoe kauli hapa sasa hivi kwa ajili ya kuwatia moyo watu wanaolima Pamba wakati kuna Tume ambayo imeundwa ambayo pengine inaweza ikaja hapa ikatoa kauli nzuri zaidi. Tuwe na subira kidogo tu, Tume ya Waziri Mkuu ambayo imeundwa baada ya malalamiko ambayo yametolewa hapa, inafanya kazi, itakapokamilisha kazi yake tutaleta majibu yake hapa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala la pili lilikuwa kuhusu viwanda vilivyobinafsishwa. Waheshimiwa Wabunge wengi wamezungumzia suala hilo kwamba kwa nini viwanda vilivyobinafsishwa vingine havifanyi kazi hadi sasa hivi? Kwa nini Serikali inakaa kimya isichukue viwanda hivyo moja kwa moja na kuanza kuvitoa kwa watu wengine ambao wana nia ya kuwekeza?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme tu kwamba kati ya viwanda ambavyo vimefanyiwa (tunaita katika lugha yetu ya viwanda na biashara) ‘uperembaji’, yaani tathmini, viwanda vilivyo vingi vimefanya vizuri kuliko ambavyo vimefanya vibaya. Lakini imekuwa ni tendency ya watu kuona kitu ambacho kimekuwa kibaya ndiyo ambacho kinaangaliwa zaidi. Lakini hapa nilipo ninayo orodha ya viwanda 42 kati ya viwanda ambavyo vimebinafsishwa ambavyo vimefanya vizuri kuliko kile kiwango ambacho tumekubaliana, yaani Serikali ilipoingia mkataba na Mashirika haya na hao wenye viwanda tulikubaliana kwamba wazalishe kiasi fulani. Sasa kati ya hivi viwanda, 42 vimezalisha juu ya kile kiwango ambacho tulikuwa tumekubaliana nao.

Mheshimiwa Mwenyekiti, viwanda ambavyo havijafanya vizuri, kilichofanyika baada ya uperembaji mambo haya yote yamekabidhiwa kwa Consolidated Holdings Corporation. Kwa nini tumefanya vile? Viwanda hivi havikwenda tu hivi hivi au Mashirika haya hayakwenda hivi hivi kwa hao ambao wanaomiliki sasa hivi. Viwanda hivi vilitolewa kwa mikataba. Kila kiwanda kina mkataba wake na aliyesaini mkataba siyo Wizara ya Viwanda na Biashara. Aliyesaini mkataba ni PSRC. Sasa shughuli za PSRC zinafanywa na Consolidated Holdings Corporation ambayo Bunge lako Tukufu limeiongezea muda wake wa kufanya kazi. Kazi mojawapo ni kuingia katika mazungumzo na hao wenye viwanda ambavyo havijafanya vizuri kimoja kimoja na kuzingatia mkataba uliopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu Wizara yoyote ikiamua tu kuchukua viwanda vile bila kuzingatia mkataba, baada ya muda utasikia Serikali iko Mahakamani, inadaiwa shilingi bilioni 20 au shilingi bilioni 40 au shilingi bilioni 60. Sasa Waziri ambaye atakuwa amefanya hivyo, Bunge hili hili litamlaumu kwamba Waziri hakuwa makini kwa sababu kuna mikataba ambayo inapaswa kufuatiliwa.

Kwa hiyo, ninachoomba ni kwamba suala la uperembaji, Wizara ya Viwanda na Biashara inayo taarifa yote na kama hamjapata, itabidi tufanye utaratibu na Bunge muweze kupata taarifa yote ya viwanda vyote kwa sababu tunavyo ambavyo vimefanyiwa uperembaji na kila kiwanda status yake ipo. Lakini baada ya status ile, tumetoa na ushauri nini kifanyike. Ushauri huo tumeutoa kwa Consolidated Holdings Corporation. CHS ndio wataingia katika mazungumzo ya kuweza kujua kwamba kiwanda kipi kirudi na kiwanda kipi, kwa mfano nimepata taarifa kule Shinyanga kuna viwanda vingine ambavyo watu wanaambiwa kwamba mtaviacha viwanda hivi, lakini kumbe wenye viwanda wameshapata na fedha kabisa wanataka kuanza uzalishaji. Hii ameniambia Mheshimiwa Lembeli.

Sasa huwezi tu kutangaza kwenda kuchukua kiwanda. Unaweza ukachukua kiwanda ukakuta wawekezaji ndio wanaanza kuwekeza na wamepata fedha, ukawa umemtia hasara kubwa na Taifa likapata hasara vile vile. Kwa hiyo, lazima mikataba ile iingiwe mmoja mmoja na wale wote ambao hawawezi kuzalisha na kama wanaweza kuzalisha kitu kingine chenye faida kwa nchi na wakaji-commit, tutawaruhusu wazalishe. Wale ambao hawawezi kabisa, viwanda vitarudishwa na wale ambao wamefanya vizuri, viwanda hivi 42 hapa ambavyo siwezi kuvisoma kwa sababu ya muda tuwapongeze hawa kwamba wamefanya vizuri kuliko hata pale ambako walipaswa kufanya. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine ambayo imetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, imetolewa na Msemaji wa Kambi ya Upinzani, halafu Mheshimiwa Magdalena Sakaya, Mheshimiwa Betty Machangu, Mheshimiwa Ahmed Ali Salim, Mheshimiwa Deo Haule Filikunjombe, Mheshimiwa Kapteni John Damian Komba, Mheshimiwa Deogratias Aloyce Ntukamazina, Mheshimiwa Nyambari Chacha Mariba Nyangwine, Mheshimiwa Dkt. Mary Michael Nagu, Mheshimiwa Murtaza Ally Mangungu, Mheshimiwa Dkt. Mary Machuche Mwanjelwa na Mheshimiwa Mohamed Habib Mnyaa, ni hoja nzima ya suala zima la barcodes.

Waheshimiwa Wabunge wote hawa wamesifu kwamba Tanzania tumeweza kupata barcode, lakini wamesema kuna mashaka katika mchakato wa kupata barcode, kwamba kuna Kampuni inalalamika kwamba wameonewa, hiyo kazi walikuwa wapate wao, lakini wameonewa. Naomba tu kwa faida ya Bunge lako Tukufu na kwa faida ya Watanzania, nitoe maelezo machache kuhusu suala zima la barcode lilianzaje mpaka likafika hapa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, duniani katika biashara kuna kitu kinaitwa traceability ambako kwa Kiswahili ni mfumo wa ufuatiliaji. Mfumo wa kufuatilia bidhaa kutoka shambani au kiwandani mpaka mezani kwa mlaji. Mfumo huu umeanza Amerika na Ulaya walipoanza kuwa na mawazo ya kujali sana afya zao, wakawa wanasema vyakula tunavyokula, tunakaa navyo namna gani, hasa ambavyo vinatoka nje? Tutajuaje kama chakula ambacho tunakula hapa Amerika, ama hapa Ulaya, kimetoka labda Afrika au Asia ni chakula ambacho kina usalama? Kama kitaleta madhara, tutawezaje kukifuatilia chakula hicho mpaka shambani kwa yule mtu ambaye alikizalisha ili tuweze kumwajibisha yule mtu?

Kwa hiyo, mfumo huo ukapokelewa katika nchi za Ulaya na Amerika na wakati huo ndiyo kulikuwa na mambo ya GMO yameanza, kukawa na mambo mengi, watu wengi wanasema kuhusu GMO, wengine wanaunga mkono, wengine wanapinga.

Kwa hiyo, wale wote ambao walikuwa wanapinga mambo ya GMO na kadhalika wakaona ni muhimu kuwa na mfumo wa ufuatiliaji ili kujua kwamba chakula wanachokula ni kile ambacho wanakipenda, na siyo kile ambacho hawakipendi. Kitu ambacho kinaonyesha kwamba kitu fulani kimetoka sehemu fulani, kinaitwa barcode. Ndiyo ambacho ukiangalia kwenye chupa kama ya maji ya Kilimanjaro, kuna mistari michache iliyopo pale, hiyo ndiyo barcode yenyewe. Ukiingiza kwenye kompyuta ambayo imewezeshwa, utakuta pale maji haya yamezalishwa na Kampuni fulani tarehe fulani, expiring date, ndani yake kuna sodium kiasi fulani, kuna kila aina ya mineral ambayo iko ndani itakuonyesha hapa na bidhaa nyingine zinafanya hivyo.

Sasa kutokana na kwamba barcode imeanza kutumika duniani muda mrefu, wenzetu wa Afrika Kusini wametumia miaka 10 sasa, Kenya miaka saba. Wafanyabiashara wa Tanzania ambao wanataka kuuza bidhaa zao wakawa wanapata shida, hawawezi kuuza bidhaa kwa sababu wale watumiaji wa vile vyakula vinavyotoka katika Tanzania au bidhaa za viwanda hawawezi kuzikubali bidhaa hizi kwa sababu hawana uhakika zinatoka wapi. Ndiyo ikatokea sasa mfumo kama alivyosema Mheshimiwa Owenya kwenye hotuba yake, watu wanachukua Tanzanite wanapeleka Kenya pale inapata barcode inakwenda kuuzwa nje.

Watu wanachukua bidhaa Tanzania kama korosho inakwenda India wanaitengeneza pale wanaweka barcode inakwenda Amerika. Kwa mfano, AGOA pale Kenya wanauza dola milioni 200, Tanzania dola milioni 1.4 sababu kubwa nayo inayochangiwa ni kwamba hakuna barcode ya kutambulisha bidhaa kutoka Tanzania. Kwa hiyo, Serikali yetu ikaamua kwamba ni vizuri tukaanza mchakato wa kupata barcode Tanzania na Shirika ambalo tumelipa kazi hiyo ni Shirika la TIRDO (Tanzania Industrial Research Development Organisation) ambao kazi yao ni kufanya utafiti. Wakafanya utafiti na wakaona kwamba suala hili ni feasible kwa Tanzania, iko kada ya wafanyabiashara ambao watafurahi na wataweza kutumia barcodes.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka 2007 Wizara yangu ikaanza mchakato na mchakato tuliouanza tulichukua APEX bodies za sekta binafsi. Wizara yangu inafanya kazi na sekta binafsi. Kwa hiyo, tukakutana na sekta binafsi kwanza kuwapa taarifa kwamba kuna suala hilo, lakini pili, kuwahamasisha na tatu kuwafanya washiriki kwa sababu sheria ya kuwa na barcode katika nchi, inasema ni lazima wafanyabiashara wasiopungua 250 wakutane.

Wale wafanyabiashara 250 waunde Bodi yao, ile Bodi iunde Kampuni moja, ile Kampuni ndiyo ipewe franchise yaku-supply barcode kama huduma katika nchi yoyote. Sasa tulichofanya kwa kuangalia TCCIA, tukachukua Zanzibar Chamber of Commerce Industry and Agriculture kuzingatia pande mbili za Muungano, tukachukua Tanzania Women Chamber of Commerce Industry and Agriculture, tukachukua CTI (Conferedetaion of Tanzania Industries) tukawachukua TAHA (Tanzania Horticulture Association), tukachukua Tanzania Tea Association kwa sababu zao la chai ndio tulianza kulifanyia kama experiment na Mashirika mengine ya namna hiyo especially TPSF ambayo ndiyo umbrella board ya Sekta binafsi yote Tanzania nzima.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sasa wawakilishi wa sekta hizi zote, hizi umbrella bodies zote za Bara na Visiwani ndio wakawa wanakutana, mafunzo yametolewa kwa wajasiriamali 3,500 ya namna gani ya kutumia barcode katika nchi yetu. TIRDO wamefanya kazi hiyo, sasa mwaka huu ulikuwa ndiyo mwaka ambao tulikuwa tumedhamiria kupata barcode. Wakati Wizara inajiandaa ikishirikiana na sekta binafsi, kwa sababu ni suala kubwa, mimi nikapata malalamiko kutoka kwa mfanyabiashara mmoja mwenye Kampuni yake ya Bakery, akaja kwangu akaniambia kwamba, “Nimeunda Kampuni yangu ya kuwa Wakala wa barcode Tanzania, lakini nimehujumiwa na Katibu Mkuu wako na Watendaji wa Wizara yako wameamua kuunda Kampuni nyingine wakishirikiana na BRELA, ile Kampuni inataka kuchukua ile kazi yangu.” Mheshimiwa Mwenyekiti, alivyolieleza, kwa kweli utamwonea huruma na hata Waheshimiwa Wabunge waliopata documents zake hapa Bungeni wanafahamu zile documents, ukisoma kama hujapata upande mwingine, unaweza ukashangaa ukasema kwamba yule mtu ameonewa kweli kweli.

Basi mimi nafahamu kwamba BRELA inao uwezo wa kusajili Kampuni hata 10 na zikafanya shughuli moja na nafahamu BRELA inaweza ikasajili Kampuni 100 za ujenzi na zile 100 zikaenda kuomba kazi moja tu ikapata. Kwa hiyo, BRELA haizuiwi kusajili Kampuni zaidi ya moja au mbili. Lakini huyu bwana akasema kwamba yeye ndiye mwenye haki, yaani Kampuni yake ameshasajili BRELA, hawaruhusiwi kusajili ile Kampuni nyingine yoyote, kwa hiyo, BRELA imemwonea na Wizara imemwonea na hii Kampuni ambayo imeundwa na APEX Bodies akaniambia ni ya Katibu Mkuu, wala siyo ya APEX Bodies. Sasa mimi kama Waziri, nina Taasisi 17 ziko chini yangu. Waziri yeyote au Kiongozi yeyote ana wajibu wa ku-seek clarification, yaani kupata ushauri.

Mimi nikamwandikia Mkurugenzi wa BRELA, kwanza nikamwambia nimepata malalamiko na baada ya kumwambia malalamiko nikakariri kama yule bwana alivyosema shida atakazopata, gharama alizotumia na kwamba ameonewa. Lakini nikamwuliza mtu wa BRELA: Je, umefuata sheria? Maana yake mimi nafahamu BRELA anaweza akaandikisha hata Kampuni 10 au 100, lakini kwa hapo umefuata sheria? Pili, kama huyu bwana anasema ametumia gharama zake sana na kuna huu mchakato wa Wizara ambao unaendelea hapa: Je, kuna uwezekano wa kuwafanya wakafanya kazi pamoja?

Mheshimiwa Mwenyekiti, kabla sijapata majibu ya BRELA huyu bwana jina lake Jafferi Koimere, akaenda kwa Katibu Mkuu Kiongozi kwenda kuishtaki Wizara kwamba Wizara imemnyang’anya kazi yake. Katibu Mkuu Kiongozi akaita wataalam wa Wizara, akamwita yeye mwenyewe akaenda yeye na mwenzake anaitwa Bwana Kondo wamekaa pale, akaita na wawakilishi wa sekta binafsi ambao ndio wameunda hii Kampuni nyingine sasa, hii ambayo ni ya Kitaifa. Wamekaa pale, wameelezana, Katibu Mkuu Kiongozi akamwambia kwamba huwezi kupewa hii kazi wewe kwa sababu wewe ni Kampuni moja wakati hawa ni kampuni 255.

Hizi ni Kampuni ambazo zinawakilisha pande zote mbili za Muungano, ni Kampuni ambazo zinawakilisha wafanyabiashara na wenye viwanda. Kampuni hiyo moja inawakilisha wote hawa. Wewe ni Kampuni yako binafsi, haiwezikani ukapewa isipokuwa wewe sasa ungana na hawa kama nia yako ni kuleta barcode Tanzania, ungana na hawa katika mchakato, tuweze kuwa na barcode. Bwana Koimere hakufurahia kwa sababu yeye kwa mawazo yake ni kwamba anataka auze barcode, kumbe barcode zinakuwa supplied kama service.

Kwa hiyo, akaenda kwa Mheshimiwa Waziri Mkuu akaenda akashtaki vile vile, Mheshimiwa Waziri Mkuu akapata maelezo ya Wizara akaridhika kwamba Wizara imefanya sawa sawa. Lakini hapa Bungeni tumeona kwamba kumekuwa na maswali haya ambayo yanaulizwa. Kuna sifa mbili za Kampuni kupata barcode. Sifa ya kwanza ni kwamba lazima upate baraka za Wizara, kwa maana ya barua ya Katibu Mkuu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, huyu bwana amekuja Wizarani, ameshauriwa kwamba aungane na mchakato uliokuwepo, hajapenda. Amekwenda kwa Katibu Mkuu Kiongozi, ameshauriwa aungane na mchakato uliopo, hajapenda. Sasa ni Katibu Mkuu yupi ambaye ataandika barua ya kuunga mkono Kampuni moja, aache Kampuni ambayo inaundwa na APEX Bodies za Makampuni 255 Tanzania yote?

Kwa hiyo, Katibu Mkuu alifanya kile ambacho alipaswa kufanya na amefanya kizalendo. Sifa ya pili, ni lazima uwe na Makampuni 250 ambayo yameandika barua kusema kwamba Kampuni yako ndiyo inafaa na Makampuni hayo yapeleke barua Brussels kwenye Makao Makuu ya GS1 International ambayo ndiyo wanatoa franchise hiyo yaku-supply barcode hapa. Sasa ndugu yangu huyu Koimere hakufikisha haya Makampuni 250 na barua niliyonayo mimi inaonyesha kwamba hakutimiza viwango kule, Brussels inamwambia aache kutumia jina la GS.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo lingine nataka niliarifu Bunge lako Tukufu ni kwamba, mimi nina taarifa kwamba Bwana Koimere huyu huyu ni wakala wa barcode wa Kenya. Sasa hebu zingatia mtu ambaye hapendi kutoa ushirikiano na Wizara, hapendi kuwaeleza Wizara kwamba ana Makampuni mangapi yanamuunga mkono, anataka hii Kampuni ambayo inatoka pande zote za Muungano na inawakilisha wafanyabiashara wote na wenye viwanda wote inyang’anywe hiyo kazi apewe yeye. Lakini mtu huyu hana Makampuni ya kutosha. Ina maana kwamba, kama Katibu Mkuu angeandika barua kumuunga mkono, hata kule Brussels angekosa vile vile. Kwa hiyo, Tanzania yetu ingekosa tena barcode kwa kipindi cha miaka mitatu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nataka niseme kwenye magazeti, Wizara yangu imesemwa sana kwamba ni mafisadi, ni wezi na kadhalika. Lakini nataka niseme, Bunge hili na Watanzania wanasema Mawaziri fanyeni maamuzi magumu kwa maslahi ya Taifa. Uamuzi tulioufanya ni uamuzi mgumu kwa maslahi ya Taifa la Tanzania. Katika magazeti mtu ambaye ametajwa sana na kutukanwa sana kila mahali ni Katibu Mkuu, mpaka wanasema ile Kampuni iliyoundwa ni yake.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nimesimama hapa kwanza kusema kwamba ile Kampuni siyo ya Katibu Mkuu wala Katibu Mkuu hana maslahi yoyote katika mchakato mzima wa barcode Tanzania. Pili, nimesimama hapa kuliambia Bunge lako Tukufu kwamba huyu Katibu Mkuu wetu kwa kweli ni mzalendo, kwa sababu angekuwa legelege ina maana tusingekuwa na barcode leo Tanzania. Lakini leo hii ndani ya miezi mitatu mfanyabiashara wa Tanzania sasa hivi atakuwa anapata barcode hapa Tanzania na siyo kwa kuuziwa kama ambavyo wananunua Kenya na Afrika ya Kusini isipokuwa atakuwa anaipata kwa nomino fee na hiyo nomino fee inakuwa determined na wale wote ambao wameunda ile Kampuni. Walipounda wakati ule ilikuwa ni 255, leo hii wako 420. Mimi nataka niwaombe watendaji wote hapa Tanzania, kwa kweli wamuige Katibu Mkuu wangu kwa uzalendo wake na kusimama kidete kutetea maslahi ya Taifa. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, nina hakika wafanyabiashara watanufaika na nina hakika wale wote ambao walikuwa na mawazo labda kwamba kuna mashaka, nimeeleza hali yote halisi na kwa kweli tulichokifanya tumekifanya na tuna hakika kwamba ni kwa maslahi ya Taifa na huyu ndugu yangu ambaye anafikiri tunaweza kumpa kazi ya kuuza barcode ajue kwamba barcode haziuzwi, ni service na itatolewa na wale ambao wamepitishwa na niseme tu kwa furaha, tarehe 18 Mei, 2011 Tanzania ilipata barcode kama nilivyosema kwenye hotuba yangu na ndani ya miezi mitatu tutaanza kutoa barcode Tanzania.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya hapo, sasa nije kwenye hoja ambazo zimetolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge, Mheshimiwa . Amesema kwamba ili kukamilisha azma ya kilimo kwanza, kuna umuhimu mkubwa wa sekta ya viwanda kupewa kipaumbele na vile vile akasema Serikali ihamasishe wananchi wawekeze katika viwanda vya kusindika mazao ili kuongeza thamani ambayo kwa uhakika itaongeza bei ya bidhaa zetu na kuongeza pato la Taifa. Siyo tu yeye isipokuwa hata Mheshimiwa Abdallah Omar Kigoda - Mbunge wa Handeni naye ametoa ushauri huo.

Majibu yake hapa ni kwamba katika Mpango wa Maendeleo wa miaka mitano ambao Mheshimiwa Rais alizindua hivi karibuni Sekta ya Viwanda imepewa kipaumbele ambapo sekta hii sasa ni ya tatu kati ya sekta zilizopewa kipaumbele baada ya Sekta za Kilimo na miundombinu. Hii ni kutokana na umuhimu wa sekta hii katika uchumi na Waheshimiwa Wabunge wengi mmesema hapa jinsi ilivyo sekta mtambuka, inaingilia kila mahali na imeonekana sasa katika mpango wetu imepewa nafasi ya tatu. Pili, Serikali imekuwa ikihamasisha uwekezaji katika uongezaji thamani mazao ya kilimo kwa wawekezaji wa ndani na nje.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu Rais Kikwete achukue nchi hii miradi ya viwanda ambayo imepewa leseni ni miradi 522. Kati ya hii miradi 84 ni ya viwanda vya kuongeza thamani mazao ya kilimo. Kati ya miradi ambayo imepewa leseni, viwanda 168 vimeshajengwa na vinafanya kazi kabisa katika Tanzania. Hivi vingine vinavyobaki, tofauti kati ya 168 na 522 viko katika hatua mbalimbali za ujenzi. Kwa hiyo, mawazo ya Mwenyekiti na Mheshimiwa Kigoda kwa kweli yanafanyiwa kazi na Serikali.

Hoja nyingine, NDC itatoa suluhisho la tatizo la umeme kupitia utekelezaji wa miradi ya makaa ya Mchuchuma, Ngaka na Kiwira. Hilo limeshazungumziwa na Waheshimiwa Wabunge na hata Mheshimiwa Naibu Waziri katika kuchangia kwake hoja amelisema vizuri kama ambavyo limesemwa NDC, iko tayari tutakapoiwezesha, lakini hata kabla ya kuiwezesha kwa sababu inafanya kazi ya sekta binafsi, bado kuna miradi ambayo itaanza.

Mradi wa umeme wa upepo wa Singida, Mheshimiwa Naibu Waziri ameshautolea maelezo. Niseme tu kwamba Waheshimiwa Wabunge waliosema kwamba kuna ukiritimba, kuna mtu ambaye anazuia ile power purchasing agreement. Kamati yetu ya Viwanda na Biashara leo imemwita Mkurugenzi Mkuu wa TANESCO kuja kumwuliza kulikoni na kwa kweli yeye ndiye anapaswa kusaini ile power purchasing agreement. Kwa hiyo, imemwita na nina hakika watamalizana vizuri na wakimalizana vizuri, basi ikisainiwa ule umeme wa Singida utaanza mara moja kwa sababu siyo mradi unaohitaji uwekezaji wa miaka mingi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali izungumze na wahisani wa mradi wa Ngaka ili waharakishe ujenzi wa mradi huu. Mbia mwenza wa NDC katika utekelezaji wa mradi wa Ngaka wana nia ya kuhakikisha kwamba mradi huu unaanza ujenzi wa kituo cha kuzalisha umeme ambacho kitaanza 2014/2015. Hizi jitihada ni za kutia moyo na Serikali itatoa ushirikiano wa karibu ili jukumu hili litekelezwe. Niseme vilevile, kwa wale waliokuwa wanasema msongo kutoka Ngaka mpaka Mufindi, suala hilo vilevile tutajaribu kuongea na wenzetu wa Nishati na Madini kuona kwamba linafanywa ili umeme huu ukizalishwa pale, basi uweze kufika kwenye grid ya Taifa kupunguza tatizo lililopo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine iliyotolewa na Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda ni Serikali kwa ushirikiano na wadau, ijenge njia ya umeme kutoka Ngaka hadi Songea, nimeshalijibu. Maslahi ya wananchi watakaohitajika kupisha mradi, yaangaliwe kwa kuwalipa vizuri na kuwaandalia makazi ya kisasa zaidi. Utaratibu wa jinsi ya kuwahudumia wananchi watakaopisha utekelezaji wa mradi katika Wilaya ya Ludewa ulishaanza kwa kushirikisha Halmashauri ya Ludewa Mbunge wa kipindi kilichopita na nina hakika Mbunge wa sasa hivi atatoa ushirikiano mkubwa na wataalam wa ardhi wa Wilaya ya Ludewa waliweka mipaka ya eneo la NDC na kubainisha wananchi wanaoishi ndani ya eneo la mradi.

Aidha, maeneo mapya yamekwishatengwa na wananchi watakaohusika na kuhama walipewa fursa ya kuchagua sehemu watakayohamia. Utaratibu wa walipaji fidia na uwekaji huduma za kijamii katika maeneo mapya unaandaliwa kwa kushirikisha Halmashauri ya Ludewa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hoja nyingine inasema, EPZ-A ni muhimu lakini imetengewa fedha ambazo ni kidogo sana. Fedha hizi hazitatosha kuendeleza eneo la Bagamoyo na kulipa fidia maeneo hayo. Hoja hii imechangiwa siyo tu na Mwenyekiti wa Kamati ya Viwanda na Biashara, lakini vilevile Mheshimiwa Chacha Mariba Nyangwine, Mheshimiwa Felista Bura, Mheshimiwa Esther Bulaya naye kachangia hilo hilo hata Mheshimiwa Stephen Wassira, Mheshimiwa Said, Mheshimiwa Esther Matiko, Mheshimiwa Ahmed Ally Salum na Mheshimiwa Sylvester Masele Mabumba wote wamechangia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, tuseme tu kwamba tunakubaliana na ukweli kwamba tunahitaji raslimali hizi, niseme tu na hapa najibu kwa wale wote waliotoa hoja ya SIDO, hoja ya NDC na hoja ya EPZ kwamba Wizara hii iongezewe bajeti. Kwanza kabisa, tunaposema Serikali ni moja, maana yake nini? Maana yake ni kwamba kama fedha imekwenda miundombinu, barabara ikitengenezwa, watu wa kwanza wanaonufaika ni wadau wa Wizara yangu ambao ni wafanyabiashara ambao ni wenye viwanda na kadhalika. Kama bandari itatengenezwa vizuri, wanaopata faida, wa kwanza ni wadau wa Wizara yangu vilevile. Ndiyo maana wanapeleka vipaumbele viende kwenye maeneo hayo. Wizara yangu hatununi sana na tunajua kwamba tutakuwa beneficiaries.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na maeneo haya muhimu ambayo Waheshimiwa Wabunge wengi wameyasemea, kwa kweli Mheshimiwa Waziri Mkuu amesikia kilio chetu na nishukuru Kamati ya Viwanda na Biashara jinsi ambavyo imefanya kazi hii, imekwenda kwa Waziri Mkuu siyo chini ya mara mbili katika kumsisitizia umuhimu wa kuongeza Bajeti katika Wizara yetu na kwenye maeneo haya na Mheshimiwa Waziri Mkuu ameahidi kabisa kwamba kwenye mini review budget ya mwezi Desemba, taasisi hizi zitaongezewa fedha. Kwa sababu tutambue kwamba, kama kuna fedha kidogo itapatikana na leo ni mwezi wa Agosti, mwezi Desemba siyo mbali. Hii fedha kidogo itumike kwa miezi minne, halafu Mheshimiwa Waziri Mkuu atakuja kuongeza hizi fedha kuanzia mwezi Desemba zitumike mpaka mwezi Juni.

Kwa hiyo, naomba kwa kweli pamoja na nia nzuri iliyopo, tumwamini Mheshimiwa Waziri Mkuu kama alivyosema, fedha ile itakavyotoka itafanya kazi EPZ-A, NDC, SIDO na mengineyo wataweza kupata uwezeshaji wa kipindi ambacho kitakuwa kimebaki baada ya Desemba.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali ione uwezekano wa kusaidia wananchi ambao maeneo yao yametwaliwa na EPZ kwa kuwajengea nyumba. Ushauri huu umepokelewa na unafanyiwa kazi. Kule ambako tumeanza kuchukua maeneo wengine wamedai fidia na kadhalika. Lakini kama kuna maeneo ambako watu watadai kujengewa nyumba badala ya fidia EPZ-A itajaribu kuzingatia na kuona kama kuna haja ya kufanya zoezi hilo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna suala hili la Serikali iongeze ushuru wa ngozi ghafi kutoka asilimia 40 ya sasa hadi asilimia 90 ili kuzuia uuzwaji wa ngozi ghafi nje. Hii itasaidia viwanda vya usindikaji ngozi nchini kutumia uwezo wote. Jibu lake ni kwamba pamoja na changamoto kubwa ya viwanda vya kusindika ngozi nchini ni kukosekana au kupungua kwa kasi kwa ngozi ghafi, hali inayosababishwa na ushindani mkali wakati wa ununuzi wa ngozi ghafi kati ya wafanyabiashara wanaonunua na kuuza ngozi ghafi nje na wasindikaji wa ngozi wa ndani.

Mheshimiwa Mwenyekiti, athari za ushindani huo na matokeo kwa kukosekana au kupungua kwa malighafi hizo, imesababisha siyo tu viwanda vya ndani kutotumia uwezo wao wote kwa kukosa malighafi ya kutosha katika viwanda vyao, bali pia kufanya upanuzi na kuvutia wawekezaji. Lakini vilevile tumepata ushauri mzuri kwa Mheshimiwa Mpina kwamba ama viwanda vya ngozi viende kule Shinyanga kuliko na ngozi, lakini vilevile wenye viwanda vya ngozi wamesikia kwamba Shinyanga kuna ngozi, wakati tunafikiria kujenga viwanda kule nendeni Shinyanga, nendeni maeneo mengine kutafuta ngozi huko ambazo wanasema watu wanazilalia.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Kamati inashauri Wizara kuanza kazi ya kufufua kiwanda cha General Tyre kwa kuzingatia maoni ya Kamati ya Bunge iliyoundwa kuchunguza General Tyre. Niseme kwamba mchakato ule wa kuachana na mbia wa General Tyre ambaye tulikuwa naye na alikuwa hatusaidii, kwa kweli unakamilika sasa. Lakini hata kabla ya kuhitimisha, hata kabla ya kusaini mkataba wa kuachana, Mheshimiwa Rais ameshaelekeza na NDC imepewa kazi ya kufufua ile General Tyre na nafurahi kusema kwamba NSSF wameshaonyesha nia kwanza ya kuchukua zile share zao dola zao milioni kumi ziwe kama sehemu ya equity katika kile kiwanda na vilevile kuwa mbia moja kwa moja. Sasa NSSF na NDC watakaa kwa pamoja waone kama kuna haja ya kumtafuta mbia mwingine lakini kiwanda hiki kiko katika hatua za mwisho kufufuliwa.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali iruhusu waagizaji wa sukari mwaka mzima baada ya kufanya tathmini ya kweli na kujua mapungufu ambayo yatakuwepo katika mwaka husika badala ya kutoa leseni na vibali vya kuagiza sukari pale inapogundulika kuwa kuna upungufu.

Mheshimiwa Mwenyekiti, katika Afrika Mashariki, Sheria ya Sukari Na. 26 ya mwaka 2001 hapa kwetu pamoja na Sheria ya Ushuru wa Afrika Mashariki ya mwaka 2004, zote zinatamka kuwa bidhaa ya sukari imewekewa ulinzi wa ushuru wa asilimia mia moja na itaingizwa kwenye nchi za Jumuiya kwa utaratibu maalum. Nchi yoyote inapokuwa na upungufu wa sukari, huomba kibali maalum toka Jumuiya ya Afrika Mashariki ili kuingiza kiasi cha sukari na katika kipindi fulani na kibali hicho kinahusu pia kuingizwa bila ushuru.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kutokana na uwepo na utaratibu huu, Tanzania kila mwaka huomba kuingiza sukari ya kufidia upungufu katika vipindi ambavyo viwanda vya ndani havizalishi. Bodi ya Sukari huratibu zoezi hilo na waombaji hupewa vibali vya kuingiza sukari kulingana na utaratibu uliowekwa. Katika msimu wa mwaka 2010/2011 kiasi cha tani 60,000 kiliruhusiwa kuingizwa nchini katika utaratibu huo na kibali hicho kilikwisha tarehe 30 Juni.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba niingie kwenye Kambi ya Upinzani. Mheshimiwa Lucy Owenya - Msemaji wa Kambi ya Upinzani anataka tumweleze ni sababu gani zilifanya Continental, mbia huyu wa General Tyre hakutoa mtaji wowote. Niseme tu kwamba mbia huyu mwenza, yaani Continental AG hakuwahi kuonyesha nia ya kuwekeza mtaji katika kiwanda cha General Tyre. Yeye alichokuwa anasema, ni kwamba amewekeza pale, ni ile nembo yake tu na ndiyo maana alichukua asilimia 26 za share na Serikali asilimia 74, lakini hata pale alipokuja kuishiwa fedha kutokana na mismanagement alisema Serikali itoe fedha.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyosema, wachangiaji 161 kwa vyovyote hata ningetumia dakika moja moja kuwajibu wote nisingeweza, lakini kama nilivyosema, majibu yote tunayo na tutawapatia Waheshimiwa Wabunge kwa maandishi na kwa kweli nawashukuru kwamba michango yenu mingi inalenga kuboresha Wizara yetu na yote tumeipokea na tunaifanyia kazi.

Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kusema hayo, naomba kutoa hoja.

WAZIRI WA KATIBA NA SHERIA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.

(Hoja ilikubaliwa na Kuafikiwa)

KAMATI YA MATUMIZI

MATUMIZI YA KAWAIDA

Fungu 44 – Wizara ya Viwanda na Biashara

Kif. 1001 Administration and General ...... Sh. 6,824,830,300/= MWENYEKITI: Hapa leo tuna kazi, tuanze na Mheshimiwa Donald Max maana umesimama sana kwa haraka, tutumie vizuri muda wetu, wengi tuweze kutoa hoja kwa kifupi

MHE. DONALD K. MAX: Mheshimiwa Mwenyekiti, mimi nakushukuru wewe kwa kuniona. Lakini niwashukuru Waheshimiwa Wabunge waliochangia asubuhi kwa sababu wengine hatukupata nafasi hiyo, mimi ni ombi langu kwamba hii Wizara ndiyo inaweza kutukomboa sisi Watanzania, lakini nafikiri kilichasahaulika hapa lile suala la viwanda na ushirika. Ushirika bado viwanda vipo zaidi ya 20, lakini sikuona kitu gani tutafanya kufufua Vyama vya Ushirika ambavyo wengine wetu ndiyo vimetusomesha wakati wazazi wetu wakilima pamba na kuzalisha mle.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilipokuwa najibu kuhusu uperembaji au tathmini ambayo tumefanya, nilijaribu kwa ufupi tu kusema kwamba kuna viwanda vimefanya vizuri na vingine vimefanya vizuri sana na ambavyo vimefanya kwa wastani. Nikasema kwamba kwa vile ambavyo havijafanya vizuri, taarifa ambayo tumetayarisha vile ambavyo viko chini ya Wizara ya Viwanda na Biashara ni kuishauri Consolidated Holding Coorporation ili waweze kuingia nao katika mazungumzo kwa kuzingatia ile mikataba kwa kupewa vile viwanda au zile kampuni na yaliyofanyika katika Wizara ya Viwanda na Biashara, yanafanyika vilevile kwa Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika ambao ndiyo wasimamizi wa viwanda ambavyo viko chini ya Ushirika na wakimaliza kufanya uperembaji kama tulivyofanya sisi Wizara ya Viwanda, watapeleka huko huko CHC na CHC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, watakachofanya ni kuongea na hawa wenye viwanda kuona namna gani ya kuvianzisha tena upya au kama kuna haja ya kuwanyang’anya, wataangalia ile mikataba halafu wawanyang’anye halafu itarudishwa kwa Wizara husika na kutafutwa wawekezaji wengine. Kwa hiyo, nimweleze Mheshimiwa Max kwamba huo ndiyo utaratibu na tutashirikiana na wenzetu wa Kilimo kuhakikisha hilo linafanyika.

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, naomba hapa kwenye wakati wa Matumizi unahitaji kuomba jambo la ufafanuzi tu. Kwa hiyo, unauliza straight to the point na anayejibu ajibu straight to the point ili watu wengi zaidi waweze kupata nafasi. Kwa sababu sasa nina watu 48, kwa hakika sitajisikia vizuri kama sitafika hata 30. Kwa hiyo, nimwite sasa Mheshimiwa Mikidadi.

MHE. FATUMA A. MIKIDADI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kuniona. Katika mchango wangu wa maandishi, niliuliza kwamba, ile Sheria inayotathmini masuala ya biashara katika miji na vijiji, lini itafanyiwa kazi? Kwa sababu sehemu nyingi vitu ni ghali na sehemu za guest houses kodi ni kubwa. Kuna kodi ya mapato, kuna kodi ya TRA, kuna ya hostel levy. Kodi ni nyingi, hostel levy ni asilimia 20 kabla hujatoa sabuni, shuka, na kadhalika, asilimia 20. Lini itapunguzwa au lini itafanyiwa kazi ili mambo yaende vizuri?

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sheria ya Bara imeshakamilika na tunaanza utekelezaji wakati wowote kuanzia sasa hivi.

MWENYEKITI: Sheria inakuja. Nimwite Mheshimiwa Riziki.

MHE. RIZIKI S. LULIDA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana. Ningependa kumwuliza Waziri kuhusu uwekezaji na hasa katika viwanda vyetu Tanzania, ajira kubwa inakuwa kwa wageni, lakini katika majibu tunayoyapata humu ndani hayakinzani na hayalingani na takwimu zilizoko kule katika ajira. Je, ni lini Serikali itakuwa makini kuhakikisha ajira inawagusa Watanzania katika viwanda vyetu? Ahsante. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, sisi katika Wizara ya Viwanda na Biashara tunasisitiza kwamba waajiri wote wazingatie sheria za ajira. Sheria za ajira zinasema kwamba kazi ambazo zinaweza zikafanywa na Watanzania, wapewe Watanzania. Kazi ambazo zitafanywa na experts kutoka nje wapewe kwa kufuata na kwa kuzingatia ile sheria iliyopo.

MWENYEKITI: Nani ana-enforce? Nani anasimamia? Nadhani jibu lingesaidia sana. WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, anaye-enforce hiyo ni Wizara ya Kazi na Ajira.

MWENYEKITI: Ahsante kwa ufafanuzi. Tunaendelea. Mheshimiwa Kiwanga.

MHE. SUSAN L. A. KIWANGA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Moja kwa moja, katika mchango wangu wa maandishi nilipenda Waziri aniambie hatima ya wananchi wa Mkoa wa Morogoro na viwanda mbalimbali vilivyokuwa vinafanya kazi katika kipindi cha miaka ya 1980 na 1990. Lakini, mpaka leo kuna baadhi ya viwanda vingine pale Morogoro Mjini wanafugia Mbuzi: Je, hatima ya wananchi wa Morogoro ni nini? Naomba ufafanuzi. Kilosa, Kilombero, kuna viwanda vingi, vilikuwepo!

MWENYEKITI: Ahsante. Umeeleweka. Mheshimiwa Waziri ufafanuzi.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimeeleza vyema hapa kuhusu tathmini ambayo imefanyika ya viwanda na kwamba sasa hivi mchakato wote ni kuepeleka viwanda hivyo ambavyo havifanyi kazi vizuri kwa Consolidated Holdings Corporation ambao sasa ndiyo wataingia katika mazungumzo na hawa wenye kampuni hizo ili kuona kama kuna haja ya kuzirudisha kupata wawekezaji wengine, hilo lifanyike. Lakini la maana ni kwamba Wizara inaendelea kuhimiza uanzishwaji wa viwanda vipya katika Mkoa wa Morogoro na Mikoa mingine ili wananchi wa Morogoro waendelee kupata ajira.

MWENYEKITI: Nadhani Bunge tungeomba taarifa ya CHC, wapi hawafanyi vizuri na wapi wanafanya vizuri? Ingetusaidia kidogo. Nimwite Mheshimiwa Turky!

MHE. SALIM HASSAN ABDULLAH TURKY: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Swali langu linahusu upungufu wa sukari katika nchi yetu. Katika maandishi niliyoandika, sijapata majibu yake, na hivi sasa kuna upungufu mkubwa sana wa sukari nchini na SUDECO wameliona hili na wametoa vibali kwamba sukari iagizwe kutoka SADC Countries. SADC Countries wenyewe hakuna sukari. Mimi nahisi ukiritimba huu unatuumiza Watanzania. Upungufu kama huu ulikuwa kwenye saruji, saruji imeruhusiwa, inaagizwa huria sasa hivi. Kwa muda wa miaka mitatu sasa hivi bei ya saruji haijapanda nchini. Nafikiri wakati umefika sasa hivi tujipange vizuri na hii sukari tuitazame kwa sababu haiwezekani kila mwaka kiwanda kikifungwa, kikifunguliwa bei ya sukari inapanda kwa Sh. 10,000/= na wakulima mazao yao bei zao ziko pale pale. Sasa, hizi pesa zinakwenda wapi?

MWENYEKITI: Ahsante. Umeeleweka. Mheshimiwa Waziri, ufafanuzi.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nimjibu kwamba viwanda vingi vimeanza uzalishaji sasa hivi, na tunavyoongea sasa hivi angalau tani 28,000 ziko kwenye magodauni ya viwanda ambayo imezalishwa kwenye msimu huu. Lakini pili, pale ambapo tutakuwa na uhaba wa sukari, tutatumia taratibu zote za Afrika Mashariki na hasa za Kitaifa kuhakikisha kwamba tunaagiza sukari kutoka nje.

MWENYEKITI: Tunaendelea. Mheshimiwa Turky, wakati mwingine ni vizuri ku-declare interest. Hili jambo litakuja kuumiza mtu hapa halafu badaye tutalaumiana. Kama una interest na jambo, ni vizuri ku-declare interest.

MHE. SALIM HASSAN ABDULLAH TURKY: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba radhi, ni kutokujua. Nina-declare interest kwamba mimi mwenyewe ni mfanyabiashara, halafu ndiyo Mbunge. Ahsante sana. (Makofi/Kicheko)

MWENYEKITI: Ahsante. Ingawa hujasema mfanyabiashara wa nini, lakini tunajua hiyo hiyo. Tuendelee!

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante kwa kunipa nafasi. Nilikuwa naomba Serikali hii sikivu inisikie kama Mbunge wa Vijana Mkoa wa Mara na iwasikie wananchi wa Mara eneo la Tairo, Wilaya ya Bunda.

Mheshimiwa Mwenyekiti, inakuwaje Serikali inafanya tathmini zaidi ya miaka minne, halafu hawawalipi wananchi katika mradi wa EPZ? Kisheria, wanatakiwa wawalipe baada ya miezi sita. Tangu mwaka 2007 wamefanya tathmini, wananchi 228 Tairo hawajalipwa.

MWENYEKITI: Umeeleweka.

MHE. ESTER A. BULAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ninachotaka kusema, naomba unilinde, dakika zangu hazijakwisha. Nataka kujua Serikali itatumia utaratibu upi wa kuwalipa ili malipo yao yaendane na gharama husika za sasa? Tathmini imefanywa muda mrefu, tunajua thamani ya ardhi inapanda mara kwa mara. Naomba majibu.

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, tumpongeze sana Mheshimiwa Ester kwa jitihada za kulitetea hili suala la EPZA na malipo ambayo hayajafanyika.

Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali imesema katika majibu yetu ya awali na tutarudia tena. Mwezi Desemba katika Min-Budget, Wizara yetu itakuwa kipaumbele cha kuomba fedha maalum kwa ajili ya ku-compensate, kulipa watu katika maeneo mbalimbali ya EPZ, na tutahakikisha kwamba eneo hili alilolitaja la Bunda linakuwa kipaumbele. (Makofi)

MHE. DIANA M. CHILOLO: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Kupitia mchango wangu wa maandishi, nilimwomba Mheshimiwa Waziri ahadi ya Serikali toka wakati wa Mheshimiwa Mary Nagu akiwa Waziri kwamba ingepeleka mwekezaji kuweka kiwanda cha kusafisha mafuta Singida. Lakini mwekezaji aliyeweka mashine kule, inakamua tu, haisafishi, anapeleka Arusha kusafisha.

Sasa, kwa kuwa wako wafanyabiashara wazalendo wa Mkoa huo huo ambao wanakopesheka, Serikali kwa nini isiwe na Mfuko Maalum wa kuwakopesha kama inavyofanya kwenye pembejeo? Iwakopeshe wafanyabiashara waweze kuweka mashine ya kusafisha mafuta ili yapate soko la Kimataifa. (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru tena dada yangu, Mheshimiwa Chilolo kwa kulizungumzia hili suala. Ni kweli Serikali ilikuwa imeahidi kujenga kiwanda cha alizeti pale Singida. Ni kweli pia kwamba kiwanda hicho kimejengwa na kiwanda ambacho kimekamilika pale Singida kinaitwa Mount Meru Millers, kimegharimu shilingi bilioni 10 na azma ya mwekezaji (Mount Meru Millers) ni kuwekeza shilingi bilioni 16. Hajamalizia kuwekeza bilioni sita kutokana na tatizo tulilonalo sasa hivi la mgawo wa umeme. Lakini nimhakikishie Mheshimiwa Mbunge kwamba wawekezaji wote wa ndani ambao wangependa kuwekeza, Serikali inawakaribisha, tutaendelea kuwasaidia kwa kadri inavyowezekana.

MHE. STEPHEN H. NGONYANI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa kuniona. Pamoja na mchango wangu wa maandishi, nilikuwa nataka kujua kile kiwanda cha kule Mkumbala, Tembo Chipboard kitafunguliwa lini na wale wafanyakazi wake ambao hawajalipwa hela mpaka leo watalipwa lini?

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, CHC watakapomaliza mazungumzo na huyo mwenye kiwanda ambaye amefunga, Serikali itaweza kusema kwamba ni mtu gani atapewa. Huyo atakeyepewa baada ya kuingia mkataba, ndiyo tutaweza kujua kwamba ni lini kitafunguliwa. Kuhusu hili suala la kwamba kuna watu ambao wanadai malipo, naomba Mheshimiwa Mbunge tuwasiliane baadaye ili tuongee na wenzetu wa Wizara ya Kazi tuweze kufuatilia suala hili kama kuna malipo ambayo hayakulipwa, waweze kulipwa wafanyakazi.

MHE. GOSBERT B. BLANDES: Mheshimiwa Mwenyekiti, Watanzania wengi wamekuwa wakisikia biashara inayofanyika katika soko la AGOA – Marekani. Lakini Watanzania wengi wakiwemo wananchi wa Jimbo la Karagwe wameshindwa kufanya biashara huko Marekani kwa sababu kwanza, hawana elimu ya kutosha kuhusiana na soko hilo, na pia hawajui ni bidhaa gani ambazo zinatakiwa kupelekwa huko Marekani. Je, Serikali inatoa muda gani wa kuelimisha Watanzania ili na wenyewe waweze kushiriki katika soko hilo la AGOA – Marekani? WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati naeleza hapa kuhusu barcodes nilisema kwamba kukosekana barcodes Tanzania, kumechangia sana kuwafanya Watanzania wasiweze kuuza bidhaa zao Amerika. Sasa tumeshapata barcode, na katika mchakato mzima, ile kampuni na Wizara ya Viwanda na Biashara inatoa mafunzo nchi nzima namna gani ya kutumia barcode. Kwa hiyo, naomba watu wote wajiandae, watapata mafunzo waweze kutumia fursa hizo kupeleka bidhaa ambazo katika soko la AGOA ni bidhaa 5,000 wala siyo bidhaa tatu kama ambavyo tumezoea, ni bidhaa 5,000 ambazo ni nyingi sana.

MHE. SABREENA H. SUNGURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi nilikuwa nataka kumwuliza Mheshimiwa Waziri kwamba Wizara yake imekuwa ikikodi majengo kwa kutumia takribani milioni 26 kila mwaka. Je, Waziri haoni kwamba ni busara ya kawaida fedha hizi zijenge jengo lake yenyewe tena kwa kuanzia hapa Dodoma iweze kutafuta kiwanja?

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni ushauri mzuri, Wizara itazingatia.

MWENYEKITI: Ushauri huo kweli muuzingatie sana kama mnaleta Dodoma maneno hayo!

MHE. PROF. KULIKOYELA K. KAHIGI: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana kwa nafasi hii. Mimi swali langu linahusu soko la pamba. Soko la pamba siyo soko huria, ni soko finyu ambalo linahodhiwa na makampuni machache sana, makampuni yale yale ambayo baadhi ya hayo yalipata stimulus package ya trilioni 1.7 yalipodai kwamba yanapata hasara. Sasa, wakulima wa pamba, mimi nimetoka kule juzi, kule Bukombe, wanalia. Bei ya pamba ni Sh. 800/=, wanapata hasara sana. Sasa, Serikali iko tayari kuwafidia hawa wakulima kama ambavyo iliyafidia hayo makampuni kwa kupata hasara kama ambavyo sasa hivi wanapata hasara? (Makofi)

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama nilivyojibu wakati najibu hapa kuhusu suala zima la soko la pamba, nilitoa taarifa kwamba Mheshimiwa Waziri Mkuu ameunda Tume ambayo inafuatilia suala hili. Ile Tume mpaka wakati naongea hapa ilikuwa haijaleta taarifa, na nikaomba Waheshimiwa Wabunge wawe na subira mpaka taarifa ile ije. Taarifa ile sasa, kama itakuwa na mapendekezo ya compensation, kama itakuwa na mapendekezo ya aina yoyote ile, tutayapata wakati huo na nina uhakika wazo la Profesa pale nalo litazingatiwa wakati huo.

MHE. ALIKO N. KIBONA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru. Katika mchango wangu kwa maandishi nimetoa ushauri, lakini napenda kuuliza kwamba kwa kuwa wafanyakazi walioko katika makaa ya mawe kule Kiwira Coal Mine, wapo pale kwa muda mrefu, wamekaa pale, mitambo ipo, waya zipo za kusafirisha umeme na wanalipwa bila kufanya kazi yoyote. Je, siyo wakati muafaka Serikali kuchukua maamuzi magumu na kuhakikisha kwamba wanaipa NDC na vyombo vingine pesa kwa ajili ya kuzalisha umeme, tuondokane na giza kule Mbeya wakati kila kitu kiko tayari? (Makofi)

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nimshukuru Mheshimiwa Kibona kwa swali lake zuri. Kama tulivyosema kwenye jibu la msingi, Mradi wa Makaa ya Mawe wa Kiwira, sasa hivi NDC wanazungumza na STAMICO, wanazungumza na NSSF kuhakikisha kwamba uwekezaji unapatikana na kwamba tunaweza tukawekeza na mradi huu ukawa katika miradi ambayo ni ya quick win kwa ajili ya kunusuru Taifa kwenye janga la giza.

MHE. WILLIAM A. MGIMWA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru sana kwa kunipa nafasi hii niweze kusema. Imetolewa hoja asubuhi juu ya tatizo la bidhaa bandia, kwa mfano matairi na dawa ambazo zimesababisha hasara kubwa sana hapa nchini. Kwa mfano, matairi, accident nyingi sana zimetokea. Kwa mfano, hata kwa Mkoa wangu wa Iringa, ile Highway kutoka Dar es salaam kwenda Mbeya, watu wamepoteza maisha yao kwa sababu ya matairi bandia ambayo hayahimili barabara zetu. Mheshimiwa Waziri alipokuwa anawasilisha majibu, sikulisikia hili amelipa ufafanuzi gani. Kwa sababu tuna sheria ya mwaka 2009 ya udhibiti na inaonekana haijatumika vizuri. (Makofi)

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, nikubaliane na Mheshimiwa Mbunge kwamba hilo tatizo analosema lipo la matairi mengine ambayo ni hafifu na ambayo yanasababisha ajali. Sasa hivi TBS inachofanya, inakagua bidhaa zikishafika hapa nchini, na kwa sababu ya mipaka yetu kuwa mikubwa, Bahari kuwa pana nakadhalika, wengine wanatumia fursa hiyo kuingiza matairi hayo kwa njia ambazo siyo zile ambazo ni rasmi. Kwa hiyo, baada ya TBS kuona kwamba kudhibiti bidhaa zinazoingia hapa ina ugumu wake, ndiyo maana sasa hivi TBS wameanza mchakato wa kutafuta makampuni ya kufanya ukaguzi kule ambako bidhaa zinatoka. Eneo ambalo TBS wameliwekea mkazo, ni eneo hili la matairi kwa sababu matairi yale yasipokuwa imara, yakija hapa yanaleta ajali nyingi sana. Kwa hiyo, mchakato umeshaanza, tarehe 20 Septemba, kazi hiyo ya ukaguzi kutoka kule ambako matairi yanatoka inaanza na nina hakika hili litapunguza tatizo ambalo Mheshimiwa Mbunge analisema.

MHE. ABUU H. JUMAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika mchango wangu wa maandishi nilizungumzia suala la soko la Mlandizi na kiwanda kile. Kwa hiyo, nilikuwa naomba ufafanuzi na ukizingatia ahadi ile ilikuwa ya Mheshimiwa Rais…

MHENYEKITI: Soko la Mlandizi na…?

MHE. ABUU H. JUMAA: Kiwanda cha kusindika nyanya.

MWENYEKITI: Okay.

MHE. ABUU H. JUMAA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ukizingatia ahadi hii ni ya Mheshimiwa Rais, naomba ufafanuzi.

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza, tunazingatia ahadi ya Mheshimiwa Rais na Serikali imeziainisha ahadi zote ikiwa ni pamoja na hii ya Soko la Mlandizi katika utekelezaji wake katika kipindi hiki. Pili, nimhakikishie kwamba tutashirikiana siyo tu na Wizara yangu, lakini pamoja na Halmashauri yake kuangalia ni jinsi gani hiki kiwanda anachokisema kinaweza kikahuishwa na kikaweza kuwepo.

MWENYEKITI: Ahsante. Mheshimiwa Abuu, mimi nakupongeza kwa kuuliza vizuri. Hapa tunaomba ufafanuzi wa jambo ambalo ni la kisera linalohusiana na Wizara husika. Kwa hiyo, Waheshimiwa Wabunge, twende tuji-confine hapo. Nitamwita Mheshimiwa Mwaiposa.

MHE. EUGEN E. MWAIPOSA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nishukuru kupata nafasi. Mimi wakati nimechangia kwa maandishi, nilimwomba Waziri aeleze umma wa Watanzania kwamba ni lini kampuni ya BRELA itaweza kuwa na mtandao Tanzania nzima ili kuepusha usumbufu wa Watanzania kutoka katika Mikoa yote kwa ajili ya kufika Dar es salaam kuja kusajili kampuni kwa Sh. 6,000/=?

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika kitabu changu cha bajeti nimeeleza vizuri kwamba BRELA wameanza mchakato huo ambao Mheshimiwa Mbunge anasema. Sasa hivi tuko Wilaya 24 ambako tumeweka mtandao tayari. Katika Wilaya hizo walioko kule wanaweza wakaingia kwenye mtandao, waka-check majina, wakajaza form na BRELA ikawapostia leseni za makampuni yao ambayo wanataka kusajili. Mwaka unaokuja wa fedha tunataka kufika nchi nzima. Tumejipanga na bajeti ikipita ni kwamba mojawapo ya kazi ya BRELA ni kufika nchi nzima kuhakikisha kwamba Watanzania wote kila waliko wanaweza waka-check habari za BRELA kwa kutumia mtandao.

MHE. JOHN J. MNYIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Naomba kuuliza ufafanuzi kwa jambo la kisera ambalo linalenga kuongeza ajira kwa vijana wa Jimbo la Ubungo na Dar es salaam kwa ujumla, na linahusu viwanda vya Ubungo Garments, Ubungo Maziwa, Urafiki pamoja na UFI ambavyo vimebinafsishwa, vimedidimia na mikataba ya ubinafsishaji imekiukwa. Maelezo yaliyotolewa na Waziri ni kwamba Wizara imeshauri CHC kufanya mapitio, maelezo ambayo sikubaliani nayo kwa sababu tathmini ya Serikali ilifanyika mwaka 2007/2008, na hali halisi ya ukiukaji wa mikataba ikaonekana. Mwezi Julai, 2010 kwenye Bunge hili hili, Waziri wa Wizara hii hii, aliliahidi Bunge, kwamba ndani ya mwaka mmoja wa fedha hiyo, kazi ya ushauri CHC ingekuwa imekamilisha kazi yake na kadhalika, kwa mwaka mmoja baadaye. Ningeomba kauli thabiti ya kisera. Serikali hii ni moja, linalofanywa na Wizara ya Fedha linafanywa pia na Wizara ya Viwanda na Biashara. Nini hatma ya viwanda nilivyovitaja kwa lengo la kuongeza ajira kwa vijana wa Jimbo la Ubungo na Dar es Salaam kwa ujumla?

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namwonea Mheshimiwa Mnyika wivu kwamba viwanda karibu vyote vya EPZ na kadhalika vipo katika Jimbo la Ubungo. Kwa hiyo, ningetegemea kwanza aunge mkono bajeti. Lakini jambo la pili, niseme kwamba kuna kiwanda cha Urafiki ambacho amekitaja, hicho kiwanda Serikali ina share pale, na baada ya kuona kwamba kinasuasua, tumeshatafuta wabia ambao watakifufua kile kiwanda na ufufuaji wake utaanza wakati wowote. Hayo mengine anayosema kwamba CHC tulikubaliana wakati ule na ikafanyika, akumbuke kwamba muda wa CHC ulikuwa unakwisha, na Bunge letu ndiyo limeruhusu CHC ifanye kazi kwa muda wa miaka mitatu. Kwa hiyo unapokuwa unamaliza muda wako, wakati mwingine kuna kazi ambazo unaweza ukaziweka kando kama walivyofanya CHC.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa sababu tumeshawapa kazi naomba tu akubaliane na mimi kwamba tuwaache wafanye kazi yao ya kitalaamu ili tuweze kujua kwamba hatma ya viwanda hivyo anavyosema itakuwa wapi.

MHE. SUSAN A. J. LYIMO: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Nilikuwa naomba tu swali la ufafanuzi. Nataka kujua, Shirika la Viwango Tanzania TBS lina ubora gani wa vifaa vyake vya ukaguzi na wana wakaguzi kiasi gani? Kwa sababu ukienda katika maduka mengi hata ya spare parts watakuuliza unataka gunuine au unataka feki? Sasa nilitaka kujua ubora wa TBS ukoje?

NAIBU WAZIRI VIWANDA NA BIASHARA:Mheshimiwa Mwenyekiti, nimjibu tu Mheshimiwa Susan Lyimo na kumwondoa wasiwasi kwamba TBS siyo tu kwamba inajidhatiti sana katika kufikia ubora, lakini TBS sasa hivi imefikia mahali ambako inapewa hati ya ubora inayojulikana kama accredation na mashirika ya Kimataifa katika kaguzi zake. Hali kadhalika, TBS inaendelea kuongeza uwezo wake katika kukagua siyo tu vifaa kama magurudumu, lakini hata mashine kubwa, magari na kila aina ya vifaa ambavyo vinaingia nchini kuhakikisha kwamba havimdhuru mlaji na vina usalama wa kutosha. Tutaendelea katika kuomba na kuongeza bajeti ya TBS ili tuweze kupanua wigo wa kazi zake nchi nzima.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Naibu Waziri anasema, vifaa unakwenda dukani unaambiwa unataka original au feki, hii feki inatoka wapi kama TBS wapo? (Makofi)

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilitoa maelezo hapa nikasema kwamba pamoja na kwamba TBS wanafanya kazi nzuri, lakini wao wanakagua bidhaa zikiwa zimeshaingia Tanzania, na mipaka yetu ilivyo ni rahisi kwa mtu kuingiza bidhaa feki. Tukasema ili kupunguza hilo, maana yake TBS wanafanya ile pre-shipment inspection ndiyo maana tunasema Mwezi wa Tisa tarehe 20, hiyo kazi inaanza ya kukagua bidhaa kule ambako zinatoka ili kama ni feki zizuiliwe huko huko.

Sasa katika maeneo mengi, bidhaa nyingi ambazo zinaonekana kwamba unataka feki au genuine, hizo ndiyo zitalengwa na zitazuiliwa kuanzia kama ni China, Hongkong, au kama ni Uingereza tutazizuia huko huko ili zinaingia hapa kwetu zinakuwa zile ambazo ni bora tu? Kwa hiyo, ni mfumo ambayo TBS inajiboresha, inaongeza uwezo wake na nina hakika suala analosema Mheshimiwa Mbunge litakuwa linajitatua lenyewe kutokana na hizi hatua za TBS.

MHE. FELISTER A. BURA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kama tunavyofahamu kwamba Dodoma ndiyo Makao Makuu ya Serikali, na kwa sababu hiyo sisi wana Dodoma tulitegemea kwamba Serikali ingewekeza au ingetenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji, lakini kilichonisikitisha ni kwamba Serikali imetenga maeneo kwa ajili ya wawekezaji isipokuwa Dodoma na Tabora.

Mheshimiwa Mwenyekiti, sijui nilie, sijui tuandamane, ninaomba ufafanuzi kwanini Dodoma haipo kwenye maeneo yaliyotengwa na EPZA?

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, niseme kwamba hilo suala lipo kwa uongozi wa Mkoa zaidi. Mikoa aliyoisema ni miwili, lakini actually ni mitatu na Mkoa wa Rukwa nao ni mmojawapo. Tunahitaji kushirikiana na uongozi wa Mkoa tupate maeneo tuyatenge kwa ajili ya EPZ.

Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa hiyo, Mbunge ashirikiane na Mkuu wake wa Mkoa ili tuweze kupata maeneo hayo sisi kama EPZ tutakuwa very happy kuyapata hayo maeneo na tutayaendeleza.

MWENYEKITI: Wabunge wa Dodoma tukutane saa saba kesho. Tunaendelea Waziri kwa ufafanuzi.

WAZIRI WA NCHI OFISI YA WAZIRI MKUU SERA URATIBU NA BUNGE: Mheshimiwa Mwenyekiti, pamoja na maelezo ya Waziri, Waheshimiwa Wabunge wote wanajua kwamba Dodoma ni eneo maalum, kutokana na kuwa eneo maalum kwanza kuna tatizo la kisheria ambalo sasa tunalishughulikia, ili angalau uwekezaji uweze kufanyika. Kwa hiyo, kuna tatizo la kisheria la eneo la CDA, lakini la pili, hivi sasa ninavyozungumza na shahidi yangu ni Mhehsimiwa Mbunge wa Dodoma, kwamba Serikali inafanya mapitio upya ya master plan ya Dodoma ili hayo anayosema Mheshimiwa Bura yaweze kuwezekana.

Mheshimiwa Rais ameshaiona master plan na ameelekeza kwamba Dodoma haiwezi kukua bila kutenga maeneo ya uwekezaji na viwanda. Kwa hiyo, kwenye master plan hii sasa ambayo inakamilika kutokana na maagizo ya Rais tumeweka eneo maalum la viwanda na uwekezaji ili Dodoma kuweze kukua.

MWENYEKITI: Siyo lazima tubakie CDA siyo twende hata Kongwa tu? Kule CDA hawafiki, tuendelee. (Kicheko/Makofi)

MHE. PETER J. SERUKAMBA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mwaka jana viongozi wa EAC waliamua ku-hold on kusaini EPA na EU lakini negotiators wao wameendelea ku- negotiate. Lakini ukiangalia package yenyewe za EPA na EU bado ni problematic na kama tutaendelea kuzisaini tuta-jeopardize development ya EAC na potential ya kufanya biashara ya EAC na regional integration.

Mheshimiwa Mwenyekiti, nataka kuuliza swali bado EAC wanahitaji EPA, na kama wanahitaji EPA tunataka kujua Serikali ama EAC countries wamefanya cost benefit analysis kuona which way tuchukue kama nchi.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ni kweli analosema Mheshimiwa Serukamba kwamba tume-withhold kusaini mkataba na Eropean Union kama Afrika Mashariki kwa sababu masharti ambayo wenzetu wametupa ni masharti magumu ambayo hayana faida kwa Afrika Mashariki. Yapo mambo manne ambayo ningeweza nikayasema hapa, lakini kwa sababu ya muda, niseme tu kwamba wale wenzetu wanapaswa kutusaidia sisi tuweze kuwa at par tufanye nao biashara na tufungue milango yetu kama ambavyo wanataka, ndiyo tuweze kufanya nao biashara. Lakini maadamu wanakataa tunaendelea nao na mazungumzo, lakini mwisho wa yote ni kwamba Rais ameelekeza kwamba better no deal than a bad deal.

Mheshimiwa Mwenyekiti, hatutaingia mkataba na European Union kama tunaona kwamba hakuna maslahi yoyote kwa nchi yetu, tutaingia nao pale ambapo tu nao watakuwa wame-reciprocate wakaonyesha kwamba Afrika Mashariki nao wata-benefit kwa kuiingia mkataba huo.

MHE. SELEMAN S. JAFO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu wa maandishi nilizungumzia kiwanda cha STAMICO kilichopo Kisarawe. Kiwanda kile kilikuwa kinatoa ajira kwa vijana na akina mama, lakini mara baada ya kubinafsishwa kiwanda kile, sasa hivi kimekuwa sehemu ya popo, machaka yamejaa, ni wizi na ubadhirifu wa hali ya juu hata mitambo pale imeondolewa. Je, Serikali inasemaje na ina mkakati gani jinsi ya kufufua kiwanda hiki ili mradi vijana wa Kisarawe waweze kupata ajira?

NAIBU WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimjibu Mheshimiwa Jafo kuhusu kiwanda cha STAMICO pale Kisarawe. Kiwanda hiki cha STAMICO ni sawa sawa na viwanda vingine vingi ambavyo vilibinafsishwa, waliovichukua hawakuweza kuwekeza kama ambavyo walikubaliana katika mikataba, na sasa hivi kama alivyosema Waziri, Serikali inafanya mchakato wa mwisho kabisa kuhakikisha kwamba tunatolea maamuzi kwa kupitia Consolidated Holding na kuweza kuleta Mwekezaji mwingine ambaye atakuwa na tija.

MWENYEKITI: Ahsante sana. Mheshimiwa Zaynabu Vullu.

MHE. ZAYNABU M. VULLU: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante sana. Katika hotuba ya Waziri, alielezea juu ya mkakati wa utekelezaji wa kukuza uuzaji wa mazao nje, Mkoa wa Pwani ni Mkoa ambao unazalisha sana matunda, zikiwemo Wilaya za Bagamoyo, Rufiji na Kisarawe na hii ni sehemu ya ajira kwa wananchi. Je, Mkoa huo usimame katika nafasi ipi wakati wa utekelezaji wa awamu hii wa huo mradi?

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, swali linasema Mkoa usimamie wapi? Mkoa ukae vizuri tu kwa sababu mkakati tulionao ni kuhakikisha kwamba tunafanya agro-processing. Mkakati wa kwanza ambao tumesema ni kwamba tutawekeza zaidi katika kuongeza thamani ya bidhaa za mazao, na katika Wizara yangu sasa hivi SIDO ina ule mkakati wa ODOP, yaani One District, One Product.

Katika Mkoa wa Pwani anaposema Mheshimiwa Vullu, SIDO wameshaanza kwenda huko na naomba atoe ushirikiano, kila Wilaya ambayo ina zao fulani ambalo ni very common pale, SIDO inataka kuja kusaidia wananchi pale kuli-process na kuli-market. Kwa hiyo, tukifanya hivyo, itakuwa ni mwanzo mzuri kwa viwanda vidogo. Lakini tutaendelea kushirikiana naye Mbunge, tumeshirikiana naye hata kwa wawekezaji ambao wanatoka nje Algeria, wamekuja hapa, tulishirikiana naye kabisa katika kuongea nao, nina hakika na wao wakiwekeza kiwanda kimoja kikubwa na hivi vidogo vya SIDO, basi ule Mkoa utakuwa umesimama vizuri katika mahali pake, kwa sababu ni Mkoa ambao kwa kweli unazalisha matunda mengi sana.

MWENYEKITI: Waheshimiwa Wabunge, mtaona najitahidi hapa kujaribu kuwapa fursa wale ambao hawakusema kabisa. Kwa sababu kuna wengine walichangia, lakini pia hapa wanaleta vikaratasi ili waweze kuuliza. Kwa hiyo, nawaombeni sana, nitakwenda hivyo mpaka angalau wale wenzetu wapate nafasi. Mheshimiwa Makalla.

MHE. AMOS G. MAKALLA: Mheshimiwa Mwenyekiti ahsante, Serikali ilitoa kauli hapa wakati ikijibu swali langu kwamba sheria ya uanzishwaji wa viwanda vya sukari ni lazima kiwanda kianzishwe kilomita 80 kutoka kiwanda kingine. Katika mchango wangu wa maandishi nimesema kwamba sheria hiyo ni kandamizi, haitoi ushindani, na ni muda sasa kubadilishwa ili kuwa na kiwanda kingine cha sukari kule Mtibwa. Je, Waziri anatoa msimamo gani wa Serikali kuhusu hoja hiyo?

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mhehsimiwa Makalla, na niliongea naye wakati Fulani kuhusu suala hili. Ukweli ni kwamba, ile kilomita 80 ni kama malighafi ya pale haitoshi. Lakini kama malighafi inatosha, kama kuna miwa mingi sana unaweza ukawa na viwanda hata zaidi ya kimoja. Kwa hiyo, ile sheria ni kama tu mali ghafi haitoshi, kwa kuanzia. Hii sheria kama kuna mali ghafi ya kutosha pale sisi tunaruhusu kiwanda cha pili au kiwanda cha tatu kijengwe.

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini jambo la pili, mimi na Mheshimiwa Makalla katika maongezi yetu tuliongea uwezekano wa kujenga kiwanda kingine pale, tumeshampata Prospective Investor, tunamwahidi kwamba tutafanya naye kazi ili kuhakikisha kwamba tunajenga kiwanda kingine kama huyu Prospective Investor atakuwa fourthcoming na mimi na wewe tutaendelea kushirikiana katika kumfanya huyu mwekezaji awekeze kiwanda kingine pale Mvomero. MHE. JAMES D. LEMBELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika mchango wangu wa maandishi nilitaka kupata...

MWENYEKITI: Nimemwita Mheshimiwa Hemed, lakini endelea baada ya wewe tutaendelea na Mheshimiwa Hemed. Hapa umeingia kimjini mjini.

MHE. JAMES D. LEMBELI: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Niwie radhi. Katika mchango wangu wa maandishi, nilitaka ufafanuzi, ni sababu gani za msingi za CHC kuanza mchakato wa kutaka kukirejesha mkononi mwa Serikali kiwanda cha Nyama cha Shinyanga wakati Mkataba wa ununuzi bado upo hai, na walionunua kiwanda hicho wako katika hatua za mwisho za kuanza uzalishaji?

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati najibu hapa, nilimtaja Mheshimiwa Lembeli kwamba ni mfano wa wale waliochangia kwamba kuna maeneo mengine ambako watu wameshatafuta fedha, ziko njiani zinakaribia, wanataka kuanzisha kiwanda halafu anakuja mtu anaanza kuwatishia kwamba kile kiwanda kinaondoka. Nimhakikishie kwamba hili halitafanyika kwa sababu, kama kuna mtu mwenye fedha tayari, Wizara ya Viwanda na Biashara kazi yetu ni kumtia moyo ili awekeze na nina hakika CHC hawajaanza zoezi hilo. Kama kuna mtu anafanya hilo, ni mtu tu ambaye anafanya kwa maslahi binafsi, na sisi tutalifuatilia ili kuhakikisha kwamba hilo haliendelei. Ahsante sana.

MHE. SALIM HEMED KHAMIS: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru. Katika kitabu cha Waziri ukurasa wa 30, amezungumzia mafanikio ya soko la AGOA. Amesema mwaka 2009 mauzo yalikuwa dola milioni 1.8, mwaka 2010 zilikuwa dola milioni 2.1, tofauti hapa ni kama 0.3 ukipiga mahesabu ni kama dola laki tatu. Sasa hiyo ni kidogo sana, wakati sisi tumepewa fursa ya kupeleka bidhaa zetu Marekani, lakini hatuitumii. Kuna sababu gani za msingi nchi yetu haitumii vizuri fursa hizi za soko la AGOA?

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza tukiri hapa kwanza hatuwezi kujivunia perfomance yetu katika AGOA ukilinganisha na nchi jirani na nchi nyingine ndogo kama Lesotho, wamefanya vizuri kuliko hata sisi, lakini niseme kwamba ukiangalia nchi zote ambazo zimenufaika na AGOA ni zile nchi ambazo zime-develop EPZ zao zikawa na nguvu, yale maeneo ya uwekezaji hasa kwa ajili ya export yakiwa na nguvu ndipo wanakuja watu wengi wanawekeza viwanda ambavyo ni vya kimataifa, lakini vinazalisha kwa ajili ya export.

Mheshimiwa Mwenyekiti, EPZ yetu kama unavyoona ina miaka minne tu, na viwanda pale ndiyo vinaanza uzalishaji. Kwa hiyo, hilo limechangia sana tusiweze kufanikiwa. Wenzetu kwa mfano Kenya EPZ yao ina miaka 20 sasa, wameweza kuitumia vizuri wao wanauza dola milioni 200 kwa mwaka, sisi tunauza dola milioni moja. Hicho siyo kitu cha kujivunia!

Mheshimiwa Mwenyekiti, lakini vile vile nimesema hapa kuhusu suala la barcode, kama kuna bidhaa hasa za viwanda na hata kama ni bidhaa ambazo zina uasilia wa chakula, au vinywaji, ukipeleka kule kwenye soko la AGOA zinakataliwa kama hazina barcode. Tumeshapata barcode, imani yangu ni kwamba Tanzania tutanufaika zaidi na soko la AGOA sasa, lakini vile vile tukiwekeza zaidi kwenye EPZ tutakuwa na viwanda ambavyo vinazalisha kwa ajili ya ku-export duniani kote lakini hasa katika soko la AGOA.

MHE. JENISTA J. MHAGAMA: Mheshimiwa Mwenyekiti nakushukuru. Jimbo la Peramiho, Mkoa wa Ruvuma na Mikoa mingine ya kusini ndiyo wazalishaji wakubwa wa chakula kwa maana ya mahindi. Kwa kuwa, katika kufanya biashara ya kuuza mahindi, Serikali imekuwa ikiitaka mikoa hiyo kuuza chakula hicho kwenye hifadhi ya chakula ya Taifa na Serikali inatangaza bei, wakulima hawa wadogo wako-registered kwenye madaftari yao na wanajulikana, na hawatakiwi kwa mujibu wa sheria kulipa tozo ya asilimia mbili ili kuuza chakula hicho kwenye hifadhi ya chakula. Lakini mwaka huu toka bei imetangazwa ya Sh. 350/= kwa kilo, kwa wakulima hawa wa mahindi. Serikali ilitangaza, ni lazima walipe tozo ya asilimia mbili na hivyo ile bei ya Sh. 350/= imekuwa ikipungua.

Mheshimiwa Mwenyeiti, naomba kujua kauli ya Serikali kuhusu tatizo hilo, ni nini ili ununuzi wa mahindi uendelee vizuri na wale wakulima wapate haki yao ya kuuza mahindi ndani kama walivyoagizwa na Serikali?

WAZIRI WA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nakushukuru kwa kunipa nafasi hii niweze kutoa jibu la swali la Mheshimiwa .

Mheshimiwa Mwenyekiti, suala hili lilijitokeza mara tu tulipofungua masoko ya kununua mahindi katika Mkoa wa Rukwa, Mkoa wa Katavi, Mkoa wa Ruvuma, Mkoa wa Njombe na maeneo mengine ambapo wanunuzi katika kununua wakulima wametakiwa waonyeshe TIN numbers na walipe withholding tax ya asilimia 2.5. Nilichukua fursa hiyo kutafuta ushauri wa Commissioner General wa TRA, Ndugu Harry Kitilya na akatueleza kwamba kwanza, wakulima wadogo wanaouza chakula chao NFRA, hawatakiwi kulipa withholding tax na wala hawana sababu yoyote ya kuleya TIN wakati wa kuuza mahindi yao. (Makofi)

Mheshimiwa Mwenyekiti, hii ni tofauti na wafanyabiashara, wapo wafanyabiashara ambao pia wanauza mahindi yao NFRA, hawa ni lazima waoneshe TIN number na ni lazima walipe two and half percent with holding tax. Nashukuru.

MWENYEKITI: Ahsante kwa jibu la uhakika.

MHE. DKT. HAMIS A. KINGWANGWALA: Mheshimiwa Mwenyekiti, ahsante. Mimi naomba niseme kwamba hatutaweza kama Taifa ku-harnes opportunities hizi ambazo zinapatikana kwenye masoko ya AGOA, everything but arms projects led na mengineyo, kwa sababu nchi yetu haiwezi kuwekeza katika viwanda na imeshindwa kuhamasisha uwekezaji katika viwanda. Serikali leo hii inasema nini katika kutoa fursa za mikopo ambayo inalenga katika kuboresha industry moja specific ambayo pengine tunaweza tukajidai kwamba na sisi tuna viwanda pengine labda ni vya textile au ni viwanda vya electronics ili na sisi tujulikane katika ramani ya uwekezaji katika viwanda? Serikali inasema nini katika kuanzisha mfuko ambao utakuwa unatoa mikopo kwa wawekezaji kwenye viwanda vya value addition kwenye fani husika?

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba nimsihi Mheshimiwa Hamis Kigwangalla akubaliane na mimi kwamba Serikali inahamasisha wawekezaji kwenye viwanda tofauti na anavyosema kwamba hakuna kinachofanyika kwenye viwanda, nimesema hapa kwamba kwa miaka mitano viwanda ambavyo vimejengwa Tanzania, ni viwanda 168 na vimejengwa na sekta binafsi. Hii siyo namba ndogo kwa sababu ni viwanda vikubwa, viwanda vidogo ni kwa maelefu. Hilo la kwanza.

La pili, ni kwamba katika TIB kuna dirisha kwa ajili ya kusaidia wanaotaka kuwekeza kwenye viwanda, nikiri kwamba TIB haijawa na fedha za kutosha, lakini fedha zitakuwa zinaongezwa kutokana na uwezo wa Serikali, lakini wazo lake vile vile la kuanza mfuko mwingine kwa ajili ya viwanda tutalifanyia kazi tuone uwezekano wake.

MHE. MAGDALENA H. SAKAYA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwenye mchango wangu wa maandishi nilielezea hali halisi ya Mkoa wetu wa Tabora. Mkoa wa Tabora hauna kiwanda hata kimoja kinachofanya kazi, siyo kikubwa wala siyo kidogo na kwa kuwa kwa muda wa miaka mingi tumekuwa tunaomba angalau hata kiwanda cha juice kwa ajili ya matunda yanayooza au maziwa kwa ajili ya maziwa ambayo yanamwaga, sasa kwenye mpango wa Serikali kwenye huu upembuaji wa viwanda, Serikali imejiandaa kujenga kiwanda gani kuanzia nacho kwa Mkoa wa Tabora kwenye mwaka huu?

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimfahamishe dada yangu, Mheshimiwa Sakaya kwamba Serikali haijengi viwanda isipokuwa Serikali inajenga mazingira wezeshi kwa ajili ya ambao wanataka kujenga viwanda, wajenge viwanda. Kwa hiyo, naomba na yeye atumie uwezo wake na ushawishi wake katika kuwashawishi wawekezaji wengi waweze kupenda kujenga katika Mkoa wa Tabora.

Nataka nimwahidi kwamba hilo la kujenga mazingira na kushawishi tutaendelea kufanyia siyo tu kwa Tabora, lakini kwa nchi nzima. Lakini vile vile nataka nimwambie kwamba viko viwanda vingi vidogo hata kama wanasema hakuna vikubwa, lakini vikubwa tunafahamu viko vile vile lakini vidogo viko vingi ambavyo vinaendeshwa chini ya SIDO nafikiri tu ajaribu kufanya utafiti ataona na tutaendelea kuboresha mazingira kule, zao la asali na mazao mengine ambayo yanapatikana Tabora. SIDO imewekeza sana kule na tutaendelea kuwekeza zaidi na hivi vikubwa tutaendelea kuboresha mazingira ya wawekezaji.

MHE. MCH. LUCKSON N. MWANJALE: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu, nilikuwa nimeomba Serikali kusitisha mfumo wa lumbesa katika mazao, maana imekuwa ni kero ya wananchi wote wa Tanzania. Ahsante sana.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, mfumo wa lumbesa huu ambayo unafanya wakulima kwa kweli wanapunjwa. Kwanza, nikubaliane naye kwamba lumbesa imekuwa tatizo la muda mrefu hapa nchini na tumekuwa na wakala wa vipimo hapa Tanzania ambao kila mwaka unaongezeka na kwenye kitabu changu nimeeleza jinsi ambavyo mwaka huu tu wamekagua vipimo zaidi ya 800,040 ni pamoja na hayo magunia au vipimo ambavyo vinafanya watu wanaongeza mazao kwa hasara ya mkulima.

Vipimo wamefanya kazi hiyo lakini nataka niseme kwamba kwa sababu ya ukubwa wa nchi yetu, hawajaweza kufika kila mahali, kwa sababu biashara ni kati ya mtu na mtu, ni ngumu wakati mwingine Idara ya Vipimo kuweza kufahamu kwamba leo fulani kamwuzia mtu gunia Fulani, kampunja kilo 10 na kadhalika. Lakini kazi yetu kubwa tunayofanya kwa kweli ni kutoa elimu na kuliomba Bunge lako Tukufu lisaidiane na wananchi kwa kweli katika kutoa elimu ili watu wenyewe wakatae mfumo huo kutoka huko huko waliko kwa sababu mtu anayeongeza gunia anafahamika na wananchi wote. Sasa mkitoa taarifa kwa Wizara yetu au kwa vyombo vingine ambavyo ni law enforcers ikasaidia katika kuwasaidia katika kuwakamata hawa watu na tukiwakamata, basi itakuwa ni fundisho kwa watu wengine. Lakini tunaendelea na Wizara katika kudhibiti suala hilo.

MHE. HASNAIN MOHAMED MURJI: Mheshimiwa Mwenyekiti, wakati nachangia nilisha- declare interest. Mkoa wa Mtwara unazalisha sana chumvi na soko kuu la chumvi wakati huo ilikuwa katika kiwanda cha mgololo kule Iringa cha karatasi. Baada ya kubinafsishwa kile kiwanda sasa hivi soko limekufa kabisa la chumvi na inasemekana kwamba wale wenye kiwanda sasa hivi baada ya kubinafsishwa chumvi inatokea Kenya kuja pale. Sasa sijui kama Mheshimiwa Waziri anajua. Wanaingiza hiyo chumvi kama raw material kutoka Kenya kwa hiyo, hawataki kutumia chumvi ya hapa, wanatumia chumvi kutoka Kenya.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, hilo analosema Mheshimiwa Murji kama ni kweli ni changamoto kwa Wizara, tutafuatilia kwa kushirikiana naye kuhakikisha kwamba tunarekebisha hiyo hali.

MHE. NYAMBARI C. M. NYANGWINE: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wa maandishi pamoja na mchango wa kuzungumza niliongelea sana suala la Tume ya Bei. Ukiangalia katika nchi ya Tanzania bei zinapangwa kiholela. Nikatolea mfano, mtu anakwenda China ananunua simu kwa dola 20 akifika hapa Tanzania anauza zaidi ya Sh. 300,000/=, Je, Serikali inasema nini kuhusu kuwa na Tume ya Bei nchini Tanzania? (Makofi)

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, namshukuru Mheshimiwa Nyangwine. Kwanza Tume ya Bei ilikuwepo na tukiondoa wenyewe kwa sababu tuliingia mfumo wa soko huria, sasa tukisema tunarudisha Tume ya Bei ina maana tumerudi tena nyuma na kwa maana hiyo, tunafahamu sisi wenyewe kitakachotokea kwa maana ya kwamba tutakuwa tumegeuka. Lakini kitu ambacho ningependa nishauri mbadala ni kwamba labda tuwe na mamlaka za udhibiti kwa zile bidhaa ambazo tunaona kwamba kwa kweli ni muhimu kwa mlaji na ambazo tunaona kwamba bei zake inachezewa sana kama ilivyo kwa mafuta na usafiri, basi labda tungefikiria kuwa na chombo cha udhibiti kwa ajili ya bidhaa kama hizo ambazo Mheshimiwa Nyangwine alikuwa anazungumza kwenye maelezo yake. Lakini kurudisha Tume ya Bei, huo siyo uamuzi wa Serikali sasa hivi.

MHE. SILVESTRY F. KOKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa kuwa wananchi wa Kibaha Mjini kupitia Halmashauri yao wamekuwa katika mstari wa mbele kuenzi ahadi ya Mheshimiwa Rais ya kujenga viwanda mbalimbali katika mji wa Kibaha na hususan kwa kupima maeneo ya kata ya Misugusugu pamoja na kata ya Pangani kwa ajili ya viwanda mbalimbali: Je, Wizara sasa ina mpango gani wa kuhakikisha kwamba inaelekeza na kushawishi wawekezaji wa viwanda kuja na kujenga viwanda hivyo katika Jimbo la Mji wa Kibaha ili kupunguza msongamano na gharama kubwa za fidia katika Jiji la Dar es Salaam?

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nimweleze Mheshimiwa Mbunge kwamba ahadi ya Rais ni amri. Kama Rais ameshaahidi kitu ni kwamba Wizara lazima itekeleze. Lakini vile vile Mheshimiwa Rais ameahidi wakati wa kampeni, na mwaka haujakwisha na ahadi zake ni za miaka mitano. Nataka nimwahidi kwamba Wizara itashirikiana na Wizara husika hawa wanaopima maeneo Wizara ya Ardhi na wengineo kuhakikisha kwamba maeneo haya yanapimwa na tushirikiane naye katika kuhamasisha wawekezaji waje katika eneo la Kibaha kama anavyosema kwa ajili ya kuwa na hivi viwanda.

MHE. YUSUPH ABDALLAH NASSIR: Mheshimiwa Mwenyekiti, labda niseme kwamba nimekasirika kidogo na hotuba ya bajeti hii. Kuwepo kwa Bandari ya Tanga ni sababu tosha ya kuanzisha EPZ pale ili tuweze ku-export matunda yatakayozalishwa maeneo ya Korogwe, Muheza na maeneo mengine pamoja na mkonge tuliokuwa nao. Je, nini mkakati wa Wizara sasa kwa kutujengea EPZ Tanga ili tu-take advantage ya raslimali zilizokuwepo pamoja na ujirani tuliokuwa nao na wenzetu wa Kenya? Ahsante. (Makofi)

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza nakubaliana na Mheshimiwa Mbunge kwamba Tanga inahitaji kuwa na EPZ, lakini tunazo ekari 2,700 pale ambazo tumezitenga kwa ajili ya EPZ. Tuseme tu kwamba kwa sababu hatujapata fedha za kutosha kuzi- develop zote kwa wakati mmoja, nataka nimhakikishie kwamba fedha itakapopatikana, tukimaliza hapa tunapojenga sasa hivi, tutahamia Mikoa mingine na mmojawapo nafikiri Tanga nayo tutaipa kipaumbele.

MHE. MODESTUS D. KILUFI: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwa vile Watanzania wameshuhudia kuporomoka kwa viwanda vyao na mashirika ya umma na hakuna aliyechukuliwa hatua kwa kuporomosha na kuua mashirika ya umma: Je, sasa wakati si umefika Serikali kuleta Muswada wa Sheria ambayo itatoa adhabu ya kifungo cha maisha na kufilisiwa mali kwa yeyote ambaye atapelekea kufanya viwanda vyetu ambavyo sasa tunapigania vifufuke, viporomoke tena na hivyo kusababisha Watanzania wengi kukosa ajira kwa kutokuwa na viwanda katika nchi hii? Naomba nijibiwe.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, Serikali haitaweza kuleta Muswada wa namna hiyo kwa sababu viwanda vyote vinamilikiwa na sekta binafsi. Hata hivi ambavyo tunasema kwamba vimebinafsishwa na havijafanya kazi vizuri hata kama tutavirudisha, ina maana kwamba tunatafuta sekta binafsi waje wawekeze. Sasa kama mtu kawekeza kwenye kiwanda chake, halafu akapata hasara, ukimwekea tena sheria ya kufungwa maisha, ameshapata hasara, kiwanda kimekufa, halafu unamfunga maisha, nadhani kile kiwanda kitakuwa kimekufa kwa bahati mbaya na siyo kwa kusudi kama vile ambavyo vimekufa wakati ule vinamilikiwa na sekta ya umma.

MHE. MOSHI SELEMAN KAKOSO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu wa maandishi niliiomba Serikali itoe ufafanuzi juu ya ukosefu wa soko la tumbaku ambapo wakulima karibu zaidi ya 100,000 ambao wanazalisha zao hilo nchini wana matarajio ya kuzalisha kilo milioni 150, uwezo wa wanunuzi waliopo hapa nchini ni wa kununua kilo milioni 80. Je, Serikali imejipanga vipi kuwasaidia wakulima hao katika nchi hii? (Makofi)

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza namshukuru Mheshimiwa Rage alipokuwa anachangia alieleza jitihada ambazo zimefanyika katika kutafuta masoko haya ya tumbaku. Lakini niseme kwamba, soko la tumbaku ni soko ambalo liko kimkataba, siyo soko huria ni soko ambalo wenye makampuni wanaingia mkataba na wakulima na wakiingia mkataba na wakulima, basi wananunua kutokana na ile mikataba. Lakini inafika mahali uzalishaji unakuwa mkubwa kiasi kwamba hata wale ambao wananunua wanazidiwa. Ndivyo ilivyotokea mwaka huu, Mheshimiwa Rage amekuja, tumejitahidi karibu kutafuta soko China, Mheshimiwa Naibu Waziri amekwenda Iran na wote wameonyesha nia nzuri ya kuja kununua tumbaku ya Tanzania pamoja na hawa ambao wananunua sasa hivi lakini China na Iran wameshaonyesha nia ya kununua tumbaku zaidi. Kwa hiyo, nataka nimtie moyo na matumaini kwamba walime tu tumbaku hata kama ikiwa ni tani milioni moja na nusu sisi Wizara ya Viwanda na Biashara tutajitahidi kutafuta masoko ya nje ili kuchangia nguvu wale ambao wananunua hapa ndani kuhakikisha kwamba tumbaku ya mkulima haibaki bila kupata soko.

MHE. GAUDENCE C. KAYOMBO: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu nilizungumzia zaidi suala la umeme, lakini kwanza nianze kumshukuru Mheshimiwa Rais kwa kumwagiza Mtendaji wa NDC ahakikishe kwamba power station inajengwa katika eneo la mradi. Lakini pia nilitaka ufafanuzi wa Mheshimiwa Waziri kujua tatizo siyo wale kujenga, maana wawekezaji wako pale tayari na mitambo na kila kitu tatizo ni kuchukua ule umeme kuupeleka Songea na kuuingiza kwenye grid ya Taifa. Nilipendeza kwamba tuongeze capital structure kwa kuingiza mkono wa Serikali, aidha, kwa Serikali kuongea na NSSF au kwa kuiwezesha NDC iweze kukopa ili iweze kujenga hiyo transmission line, naomba ufafanuzi wa Mheshimiwa Waziri lakini wakati huo huo naunga mkono hoja.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, nashukuru kwa sababu Mheshimiwa Kayombo alikuwa amesema, asingeweza kuunga mkono hoja bila kupata maelezo haya. Kwanza nimtoe wasiwasi Mheshimiwa Kayombo kwamba eti ule mkaa utachukuliwa usafirishwe mpaka Dar es Salaam? Hicho kitu niseme tu kwamba hakipo kama alivyosema Mheshimiwa Rais, ni kwamba kiwanda kitajengwa pale pale cha kuzalisha huo umeme. Lakini pia mapendekezo yake aliyotoa ya NSSF na wengineo, sisi tumeyapokea.

Kama nilivyokuwa nachangia, nimesema kwamba tutafanya kazi na Wizara husika na sekta ya nishati ambayo kazi yake itakuwa ni kujenga msongo kutoka Ngaka mpaka eneo ambako linaweza likapokelewa kama Mufindi kwa ajili ya kuingia katika National Grid ili umeme huo wa MW 120 ambayo utakuja kuongezeka mpaka 600 uweze kupata mahali pa kuingilia katika National Grid na kutumika katika nchi nzima. Kwa hiyo, namhakikishia kwamba tutajitahidi na yeye mwenyewe kama Mjumbe active kwenye Kamati yetu tutashirikiana naye kuhakikisha kwamba hilo linafanikiwa.

MHE. RAJAB MBAROUK MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, katika mchango wangu wa maandishi, pamoja na mambo mengine, nilichangia kuhusiana na matumizi makubwa ambayo yanatia shaka katika Idara zetu. Kwa mfano, rental expenses ambazo zinatumika na Idara moja zinazofikia milioni 807 ambazo ni kodi ya nyumba nne za Dodoma na milioni 770 kwa ajili ya kodi ya Ofisi ya Dar es Salaam. Hata hivyo, nataka nimwombe Waziri anipe ufafanuzi katika item 23044 routine maintenance and repair of vehicle.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Mbunge, katika fungu hili ulipaswa kuuliza masuala ya kisera.

MHE RAJAB MBAROUK MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, ndiyo hilo.

MWENYEKITI: Hilo liko mbele.

MHE. RAJAB MBAROUK MOHAMED: No, ni hapo hapo.

MWENYEKITI: Tunaendelea, Mheshimiwa Mashishanga.

MHE. RACHEL M. ROBERT: Mheshimiwa Mwenyekiti, nilikuwa nataka ufafanuzi kutoka kwa Waziri. Waziri amesema wale wananchi waliochukua mashamba yao kwa ajili ya EPZ watalipwa kwenye mini budget. Nilikuwa nataka kujua, hiyo mini budget itatolewa lini na kama isipotosheleza kuwalipa wakulima: Je, Serikali itakuwa tayari kuwarejeshea mashamba yao ili waendelee na uzalishaji? (Makofi)

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kwanza niseme kwamba kwa Mkoa wowote eneo kutengwa kuwa EPZ ni faida kwa ule Mkoa, kwa kuanzia hapo. Lakini kuna wananchi wale ambao walikuwa wanaishi pale ambao huwezi kuwaacha hivi.

Kwa hiyo, nasema ni kwamba hii mini budget review inafanyika Desemba, leo tayari ni Agosti, kwa hiyo, ni miezi minne tu imebaki ifanyike review na kama Mheshimiwa Waziri Mkuu alichoahidi tutakachopata tutajaribu kugawa kwa namna ambavyo kwa kweli itapunguza machungu kwa hawa wananchi kama siyo kumaliza kabisa. Siwezi kuji-commit kwamba tutamaliza kuwalipa wote kwa sababu sijafahamu kwamba tutaweza kupata kiasi gani.

Mheshimiwa Waziri Mkuu ametoa ahadi nzuri, lakini huwezi kujua wakati huo kama itafikia hicho kiasi ambacho tungependa. Lakini kwa kadri inavyowezekana, tutajaribu kuhakikisha kwamba fedha itakayopatikana itatumika kuwalipa wale wote ambao wanadai fidia kwa sababu imekuwa kero kubwa, siyo tu kwa Mheshimiwa Mashishanga, lakini hata Mzee Wasira analalamika sana kule Bunda, anasema watu wake kwa kweli ni wakali.

MWENYEKITI: Mheshimiwa Rajab, umejipanga sasa katika hili?

MHE. RAJAB MBAROUK MOHAMED: Mheshimiwa Mwenyekiti, tangu pale mwanzo, lakini ulininyima nafasi. Sasa katika point zile mbili ambazo nimezitaja, item Na. 23 iko katika mshahara huu wa Waziri, item Na. 230400 na item 410800, hizi zote zinahusu masuala ya magari. Hii moja ni routine maintenance and repair of vehicle ambayo ina milioni 169 na hii nyingine ni rehabilitation of vehicle. Tafsiri halisi ya neno rehabilitation katika tafsiri za Kiswahili ni kukarabati upya na kutengeneza upya.

MWENYEKITI: Naomba ufafanuzi.

MHE. RAJAB MBAROUK MOHAMMED: Naomba Mheshimiwa Waziri anieleze hapa, ni namna gani ya ku-repair hizi gari na namna gani ya kutengeneza upya hizi gari au kaanzisha kiwanda ndani ya Wizara hii ya kutengeneza gari mpya?

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, kuna service ya kawaida ambayo lazima ifanyike kama ni baada ya miezi, kama ni baada ya minne lazima ifanyike.

MWENYEKITI: Inafanyika kwa kilometa.

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, baada ya kilometa Fulani, halafu kuna ile gari ambayo inapata ajali, gari linafika sehemu ambayo inatakiwa ufanye major repair. Lakini kifungu hiki lazima tutenganishe kwa sababu ukiweka mahali pamoja, kuna uwezekano mkubwa kujikuta umeacha kufanya service ya magari ukaleta hasara kubwa zaidi kwa Serikali.

MWENYEKITI: Nakushukuru kwa ufafanuzi. Waheshimiwa Wabunge, kwa hakika muda wetu umekwisha, na kwa namna yoyote lazima tuingie kwenye guillotine.

(Kifungu kilichotajwa hapo juu kilipitishwa na Kamati ya Matumizi bila mabadiliko yoyote)

Kif. 1002 – Finance and Accounts …..Tshs. 389,401,600/= Kif. 1003 – Policy and Planning ……...Tshs. 4,299,300,400/= Kif. 1004 – Information, Education & Comm. Unit ………….....Tshs. 154,802,800/= Kif. 1005 – Internal Audit Unit ..…… Tshs. 195,042,500/= Kif. 1006 – Legal Services Unit ………Tshs. 61,771,200/= Kif. 1007 – Management Information System…… Tshs. 142,586,900/= Kif. 1008 – Procurement Management Unit..……………Tshs. 170,632,000/= Kif. 2001 – Industry …..…………………Tshs. 3,713,518,300/= Kif. 2002 – Small and Medium Enterprises Division ...……Tshs. 5,064,069,200/= Kif. 3001 – Commerce ...... ………….Tshs. 1,653,501,700/= Kif. 4001 – Commodity Market Development .…………… Tshs. 7,383,132,100/= (Vifungu vilivyotajwa hapo juu vilipitishwa na Kamati ya Matumizi bila mabadiliko yoyote)

KITABU CHA NNE

MATUMIZI YA MAENDELEO

FUNGU 44 – WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA

Kif. 1003 – Policy and Planning…… Tshs. 16,727,859,000/= Kif. 2001 – Industry ….……………… Tshs. 271,323,600/= Kif. 2002 - Small and Medium Enterprises Division …….. Tshs. 4,786,320,000/= Kif. 3001 – Commerce ….…………..Tshs. 1,657,612,000/= Kif. 4002 – Commodity Market Development ……………..Tshs. 4,233,014,400/=

(Vifungu vilivyotajwa hapo juu vilipitishwa na Kamati ya Matumizi bila mabadiliko yoyote)

(Bunge lilirudia)

T A A R I F A

WAZIRI WA VIWANDA NA BIASHARA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa taarifa kuwa, Bunge lako Tukufu limekaa kama Kamati ya Matumizi na kuyapitia Makadirio ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2011/2012 kifungu kwa kifungu na kuyapitisha bila mabadiliko yote. Hivyo, naliomba Bunge lako Tukufu liyakubali makadirio hayo.

Mheshimiwa Mwenyekiti, naomba kutoa hoja.

WAZIRI WA KILIMO, CHAKULA NA USHIRIKA: Mheshimiwa Mwenyekiti, naafiki.

(Hoja ilitolewa iamuliwe) (Hoja iliamuliwa na kuafikiwa)

(Makadirio ya Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka 2011/2012 yalipitishwa na Bunge)

MWENYEKITI: Bajeti ya Viwanda na Biashara imepitishwa rasmi na Bunge hili leo tarehe 10 Agosti, 2011 nichukue nafasi hii kumpongeza sana Waziri na Naibu Waziri na Katibu Mkuu na Naibu Katibu Mkuu na Watumishi wote wa Wizara hii. Tuwatakie kila la heri katika shughuli hiyo, ahadi mmeahidi nyingi, lakini nina hakika Mungu atawasaidia mtazitekeleza. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, ninalo tangazo moja ambalo limetoka Kaimu Katibu wa Bunge - Ndugu John Joel. Anaomba niwatangazie Wabunge wote wanawake kuwa wanaalikwa na Mama Tunu Pinda kwenye futari siku ya Ijumaa tarehe 12 Agosti, 2011 katika Makazi ya Waziri Mkuu hapa Dodoma kuanzia saa 12.30 jioni. (Makofi)

Waheshimiwa Wabunge, baada ya maneno hayo, naahirisha Bunge hadi kesho saa tatu asubuhi.

(Saa 12. 25 jioni Bunge liliahirishwa hadi siku ya Alhamisi, Tarehe 11 Agosti, 2011 saa tatu asubuhi)